2 WATHESALONIKE

Sura: 1, 2, 3

2 WATHESALONIKE 1


1 Paulo, na Silwano, na Timotheo, kwa kanisa la Wathesalonike, lililo katika Mungu Baba yetu, na Bwana Yesu Kristo.
2 Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba, na kwa Bwana Yesu Kristo.
3 Ndugu, imetupasa kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, kama ilivyo wajibu, kwa kuwa imani yenu inazidi sana, na upendo wa kila mtu kwenu kwa mwenzake umekuwa mwingi.
4 Hata na sisi wenyewe twaona fahari juu yenu katika makanisa ya Mungu kwa ajili ya saburi yenu, na imani mliyo nayo katika adha zenu zote na dhiki mnazostahimili.
5 Ndiyo ishara hasa ya hukumu iliyo haki ya Mungu, ili mhesabiwe kuwa mwastahili kuuingia ufalme wa Mungu, ambao kwa ajili yake mnateswa.
6 Kwa kuwa ni haki mbele za Mungu kuwalipa mateso wale wawatesao ninyi;
7 na kuwalipa ninyi mteswao raha pamoja na sisi; wakati wa kufunuliwa kwake Bwana Yesu kutoka mbinguni pamoja na malaika wa uweza wake
8 katika mwali wa moto; huku akiwalipiza kisasi wao wasiomjua Mungu, na wao wasioitii Injili ya Bwana wetu Yesu;
9 watakaoadhibiwa kwa maangamizi ya milele, kutengwa na uso wa Bwana na utukufu wa nguvu zake;
10 yeye atakapokuja ili kutukuzwa katika watakatifu wake, na kustaajabiwa katika wote waliosadiki katika siku ile, (kwa sababu ushuhuda wetu ulisadikiwa kwenu).
11 Kwa hiyo twawaombea ninyi sikuzote, ili Mungu wetu awahesabu kuwa mmekustahili kuitwa kwenu, akatimiza kila haja ya wema na kila kazi ya imani kwa nguvu;
12 jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo.

2 WATHESALONIKE 2


1 Basi, ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake,
2 kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe, kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo.
3 Mtu awaye yote asiwadanganye kwa njia yo yote; maana haiji, usipokuja kwanza ule ukengeufu; akafunuliwa yule mtu wa kuasi, mwana wa uharibifu;
4 yule mpingamizi, ajiinuaye nafsi yake juu ya kila kiitwacho Mungu ama kuabudiwa; hata yeye mwenyewe kuketi katika hekalu la Mungu, akijionyesha nafsi yake kana kwamba yeye ndiye Mungu.
5 Je! Hamkumbuki ya kuwa wakati nilipokuwapo pamoja nanyi naliwaambieni hayo?
6 Na sasa lizuialo mwalijua, yule apate kufunuliwa wakati wake.
7 Maana ile siri ya kuasi hivi sasa inatenda kazi; lakini yuko azuiaye sasa, hata atakapoondolewa.
8 Hapo ndipo atakapofunuliwa yule asi, ambaye Bwana Yesu atamwua kwa pumzi ya kinywa chake, na kumwangamiza kwa ufunuo wa kuwapo kwake;
9 yule ambaye kuja kwake ni kwa mfano wa kutenda kwake Shetani, kwa uwezo wote, na ishara na ajabu za uongo;
10 na katika madanganyo yote ya udhalimu kwa hao wanaopotea; kwa sababu hawakukubali kuipenda ile kweli, wapate kuokolewa.
11 Kwa hiyo Mungu awaletea nguvu ya upotevu, wauamini uongo;
12 ili wahukumiwe wote ambao hawakuiamini kweli, bali walikuwa wakijifurahisha katika udhalimu.
13 Lakini imetupasa sisi kumshukuru Mungu sikuzote kwa ajili yenu, ndugu mliopendwa na Bwana, kwa kuwa Mungu amewachagua tangu mwanzo mpate wokovu, katika kutakaswa na Roho, na kuiamini kweli;
14 aliyowaitia ninyi kwa injili yetu, ili kuupata utukufu wa Bwana wetu Yesu Kristo.
15 Basi, ndugu, simameni imara, mkayashike mapokeo mliyofundishwa, ama kwa maneno, ama kwa waraka wetu.
16 Na Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupa faraja ya milele na tumaini jema, katika neema,
17 awafariji mioyo yenu, na kuwafanya imara katika kila neno na tendo jema.

2 WATHESALONIKE 3


1 Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vile vile kama ilivyo kwenu;
2 tukaokolewe na watu wasio haki, wabaya; maana si wote walio na imani.
3 Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu.
4 Nasi tumemtumaini Bwana kwa mambo yenu, kwamba mnayafanya tulivyowaagiza, tena kwamba mtayafanya.
5 Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la Mungu, na saburi ya Kristo.
6 Ndugu, twawaagiza katika jina la Bwana Yesu Kristo, jitengeni nafsi zenu na kila ndugu aendaye bila utaratibu, wala si kwa kufuata mapokeo mliyoyapokea kwetu.
7 Mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu;
8 wala hatukula chakula kwa mtu ye yote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote.
9 Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate.
10 Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula.
11 Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine.
12 Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe.
13 Lakini ninyi, ndugu, msikate tamaa katika kutenda mema.
14 Na ikiwa mtu awaye yote halishiki neno letu la waraka huu, jihadharini na mtu huyo, wala msizungumze naye, apate kutahayari;
15 lakini msimhesabu kuwa adui, bali mwonyeni kama ndugu.
16 Sasa, Bwana wa amani mwenyewe na awape amani daima kwa njia zote. Bwana awe pamoja nanyi nyote.
17 Salamu zangu mimi Paulo, kwa mkono wangu mwenyewe. Hii ndiyo alama katika kila waraka, ndio mwandiko wangu.
18 Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo na iwe pamoja nanyi nyote.