WAFILIPI

Sura: 1, 2, 3, 4

WAFILIPI 1


1 Paulo na Timotheo, watumwa wa Kristo Yesu, kwa watakatifu wote katika Kristo Yesu, walioko Filipi, pamoja na maaskofu na mashemasi.
2 Neema na iwe kwenu na amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
3 Namshukuru Mungu wangu kila niwakumbukapo,
4 sikuzote kila niwaombeapo ninyi nyote nikisema sala zangu kwa furaha,
5 kwa sababu ya ushirika wenu katika kuieneza Injili, tangu siku ile ya kwanza hata leo hivi.
6 Nami niliaminilo ndilo hili, ya kwamba yeye aliyeanza kazi njema mioyoni mwenu ataimaliza hata siku ya Kristo Yesu;
7 vile vile kama ilivyo wajibu wangu kufikiri haya juu yenu nyote; kwa sababu ninyi mmo moyoni mwangu; kwa kuwa katika kufungwa kwangu na katika kazi ya kutetea Injili na kuithibitisha, ninyi nyote mmeshirikiana nami neema hii.
8 Maana Mungu ni shahidi wangu, jinsi ninavyowaonea shauku ninyi nyote katika moyo wake Kristo Yesu.
9 Na hii ndiyo dua yangu, kwamba pendo lenu lizidi kuwa jingi sana, katika hekima na ufahamu wote;
10 mpate kuyakubali yaliyo mema; ili mpate kuwa na mioyo safi, bila kosa, mpaka siku ya Kristo;
11 hali mmejazwa matunda ya haki, kwa njia ya Yesu Kristo, kwa utukufu na sifa ya Mungu.
12 Lakini, ndugu zangu, nataka mjue ya kuwa mambo yote yaliyonipata yametokea zaidi kwa kuieneza Injili;
13 hata vifungo vyangu vimekuwa dhahiri katika Kristo, miongoni mwa askari, na kwa wengine wote pia.
14 Na wengi wa hao ndugu walio katika Bwana, hali wakapata kuthibitika kwa ajili ya kufungwa kwangu, wamezidi sana kuthubutu kunena neno la Mungu pasipo hofu.
15 Wengine wanahubiri habari za Kristo kwa sababu ya husuda na fitina; na wengine kwa nia njema.
16 Hawa wanamhubiri kwa pendo, wakijua ya kuwa nimewekwa ili niitetee Injili;
17 bali wengine wanamhubiri Kristo kwa fitina, wala si kwa moyo mweupe, wakidhani kuongeza dhiki za kufungwa kwangu.
18 Yadhuru nini? Lakini kwa njia zote, ikiwa ni kwa hila, au ikiwa ni kwa kweli, Kristo anahubiriwa; na kwa hiyo nafurahi, naam, nami nitafurahi.
19 Maana najua ya kuwa haya yatanigeukia kuwa wokovu wangu, kwa sababu ya kuomba kwenu, na kuruzukiwa Roho wa Yesu Kristo;
20 kama vile nilivyotazamia sana, na kutumaini, kwamba sitaaibika kamwe, bali kwa uthabiti wote, kama sikuzote na sasa vivyo hivyo Kristo ataadhimishwa katika mwili wangu; ikiwa kwa maisha yangu, au ikiwa kwa mauti yangu.
21 Kwa maana kwangu mimi kuishi ni Kristo, na kufa ni faida.
22 Ila ikiwa kuishi katika mwili, kwangu mimi ni matunda ya kazi; basi nitakalolichagua silitambui.
23 Ninasongwa katikati ya mambo mawili; ninatamani kwenda zangu nikae na Kristo maana ni vizuri zaidi sana;
24 bali kudumu katika mwili kwahitajiwa zaidi kwa ajili yenu.
25 Nami nikitumaini hayo, najua ya kuwa nitakaa na kudumu pamoja nanyi, ili mpate kuendelea na kufurahi katika imani;
26 hata mzidi kuona fahari katika Kristo Yesu juu yangu kwa sababu ya kuwapo kwangu pamoja nanyi tena.
27 Lakini mwenendo wenu na uwe kama inavyoipasa Injili ya Kristo, ili, nikija na kuwaona ninyi, au nisipokuwapo, niyasikie mambo yenu, kama mnasimama imara katika roho moja, kwa moyo mmoja mkiishindania imani ya Injili;
28 wala hamwaogopi adui zenu, katika neno lo lote; kwao hao ni ishara mathubuti ya kupotea, bali kwenu ninyi ni ishara ya wokovu, huo utokao kwa Mungu.
29 Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;
30 mkiwa na mashindano yale yale mliyoyaona kwangu, na kusikia kwamba ninayo hata sasa.

WAFILIPI 2


1 Basi ikiwako faraja yo yote katika Kristo, yakiwako matulizo yo yote ya mapenzi, ukiwako ushirika wo wote wa Roho, ikiwako huruma yo yote na rehema,
2 ijalizeni furaha yangu, ili mwe na nia moja, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkinia mamoja.
3 Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.
4 Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.
5 Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;
6 ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;
7 bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;
8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba.
9 Kwa hiyo tena Mungu alimwadhimisha mno, akamkirimia Jina lile lipitalo kila jina;
10 ili kwa jina la Yesu kila goti lipigwe, la vitu vya mbinguni, na vya duniani, na vya chini ya nchi;
11 na kila ulimi ukiri ya kuwa YESU KRISTO NI Bwana, kwa utukufu wa Mungu Baba.
12 Basi, wapendwa wangu, kama vile mlivyotii sikuzote, si wakati mimi nilipokuwapo tu, bali sasa zaidi sana mimi nisipokuwapo, utimizeni wokovu wenu wenyewe kwa kuogopa na kutetemeka.
13 Kwa maana ndiye Mungu atendaye kazi ndani yenu, kutaka kwenu na kutenda kwenu, kwa kulitimiza kusudi lake jema.
14 Yatendeni mambo yote pasipo manung'uniko wala mashindano,
15 mpate kuwa wana wa Mungu wasio na lawama, wala udanganyifu, wasio na ila kati ya kizazi chenye ukaidi, kilichopotoka; ambao kati ya hao mnaonekana kuwa kama mianga katika ulimwengu,
16 mkishika neno la uzima; nipate sababu ya kuona fahari katika siku ya Kristo, ya kuwa sikupiga mbio bure wala sikujitaabisha bure.
17 Naam, hata nikimiminwa juu ya dhabihu na ibada ya imani yenu, nafurahi; tena nafurahi pamoja nanyi nyote.
18 Nanyi vivyo hivyo furahini, tena furahini pamoja nami.
19 Walakini natumaini katika Bwana Yesu kumtuma Timotheo afike kwenu karibu, nifarijiwe na mimi, nikiijua hali yenu.
20 Maana sina mtu mwingine mwenye nia moja nami, atakayeiangalia hali yenu kweli kweli.
21 Maana wote wanatafuta vyao wenyewe, sivyo vya Kristo Yesu.
22 Ila mwajua sifa yake, ya kuwa ametumika pamoja nami kwa ajili ya Injili, kama mwana na baba yake.
23 Basi, natumaini kumtuma huyo mara, hapo nitakapojua yatakayonipata.
24 Nami naamini katika Bwana ya kuwa nitakuja na mimi mwenyewe hivi karibu.
25 Lakini naliona imenilazimu kumtuma kwenu Epafrodito, ndugu yangu, mtenda kazi pamoja nami, askari pamoja nami; tena ni mtume wenu na mhudumu wa mahitaji yangu.
26 Kwa kuwa alikuwa na shauku kwenu ninyi nyote, akahuzunika sana, kwa sababu mlisikia ya kwamba alikuwa hawezi.
27 Kwa maana alikuwa hawezi kweli kweli, karibu na kufa; lakini Mungu alimhurumia; wala si yeye peke yake, ila na mimi pia; nisiwe na huzuni juu ya huzuni.
28 Kwa hiyo nimefanya bidii nyingi zaidi kumtuma, ili mtakapomwona tena mpate kufurahi, nami nipunguziwe huzuni yangu.
29 Mpokeeni, basi, katika Bwana, kwa furaha yote, mkawahesabu watu kama huyu kuwa watu wa kuheshimiwa.
30 Maana kwa ajili ya kazi ya Kristo alikaribia kufa akaponza roho yake; ili kusudi ayatimize yaliyopungua katika huduma yenu kwangu.

WAFILIPI 3


1 Hatimaye, ndugu zangu, furahini katika Bwana. Kuwaandikieni mambo yale yale hakuniudhi mimi, bali kutawafaa ninyi.
2 Jihadharini na mbwa, jihadharini na watendao mabaya, jihadharini na wajikatao.
3 Maana sisi tu tohara, tumwabuduo Mungu kwa Roho, na kuona fahari juu ya Kristo Yesu, wala hatuutumainii mwili.
4 Walakini mimi ningeweza kuutumainia mwili. Mtu ye yote akijiona kuwa anayo sababu ya kuutumainia mwili, mimi zaidi.
5 Nalitahiriwa siku ya nane, ni mtu wa taifa la Israeli, wa kabila ya Benyamini, Mwebrania wa Waebrania, kwa habari ya kuishika torati, ni Farisayo,
6 kwa habari ya juhudi, mwenye kuliudhi Kanisa, kwa habari ya haki ipatikanayo kwa sheria sikuwa na hatia.
7 Lakini mambo yale yaliyokuwa faida kwangu, naliyahesabu kuwa hasara kwa ajili ya Kristo.
8 Naam, zaidi ya hayo, nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nipate Kristo;
9 tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani;
10 ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake;
11 ili nipate kwa njia yo yote kuifikia kiyama ya wafu.
12 Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! Bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu.
13 Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele;
14 nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.
15 Basi sisi tulio wakamilifu na tuwaze hayo; na hata mkiwaza mengine katika jambo lo lote, Mungu atawafunulia hilo nalo.
16 Lakini, hapo tulipofika na tuenende katika lilo hilo.
17 Ndugu zangu, mnifuate mimi, mkawatazame wao waendao kwa kuufuata mfano tuliowapa ninyi.
18 Maana wengi huenenda, ambao nimewaambieni mara nyingi habari zao, na sasa nawaambia hata kwa machozi, kuwa ni adui za msalaba wa Kristo;
19 mwisho wao ni uharibifu, mungu wao ni tumbo, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani.
20 Kwa maana sisi, wenyeji wetu uko mbinguni; kutoka huko tena tunamtazamia Mwokozi, Bwana Yesu Kristo;
21 atakayeubadili mwili wetu wa unyonge, upate kufanana na mwili wake wa utukufu, kwa uweza ule ambao kwa huo aweza hata kuvitiisha vitu vyote viwe chini yake.

WAFILIPI 4


1 Basi, ndugu zangu, wapendwa wangu, ninaowaonea shauku, furaha yangu, na taji yangu, hivyo simameni imara katika Bwana, wapenzi wangu.
2 Namsihi Euodia, namsihi na Sintike, wawe na nia moja katika Bwana.
3 Naam, nataka na wewe pia, mjoli wa kweli, uwasaidie wanawake hao; kwa maana waliishindania Injili pamoja nami, na Klementi naye, na wale wengine waliotenda kazi pamoja nami, ambao majina yao yamo katika kitabu cha uzima.
4 Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema, Furahini.
5 Upole wenu na ujulikane na watu wote. Bwana yu karibu.
6 Msijisumbue kwa neno lo lote; bali katika kila neno kwa kusali na kuomba, pamoja na kushukuru, haja zenu na zijulikane na Mungu.
7 Na amani ya Mungu, ipitayo akili zote, itawahifadhi mioyo yenu na nia zenu katika Kristo Yesu.
8 Hatimaye, ndugu zangu, mambo yo yote yaliyo ya kweli, yo yote yaliyo ya staha, yo yote yaliyo ya haki, yo yote yaliyo safi, yo yote yenye kupendeza, yo yote yenye sifa njema; ukiwapo wema wo wote, ikiwapo sifa nzuri yo yote, yatafakarini hayo.
9 Mambo mliyojifunza kwangu na kuyapokea, na kuyasikia na kuyaona kwangu, yatendeni hayo; na Mungu wa amani atakuwa pamoja nanyi.
10 Nalifurahi sana katika Bwana, kwa kuwa sasa mwisho mmehuisha tena fikira zenu kwa ajili yangu, kama vile mlivyokuwa mkinifikiri hali yangu lakini hamkupata nafasi.
11 Si kwamba nasema haya kwa kuwa nina mahitaji; maana nimejifunza kuwa radhi na hali yo yote niliyo nayo.
12 Najua kudhiliwa, tena najua kufanikiwa; katika hali yo yote, na katika mambo yo yote, nimefundishwa kushiba na kuona njaa, kuwa na vingi na kupungukiwa.
13 Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.
14 Lakini mlifanya vema, mliposhiriki nami katika dhiki yangu.
15 Nanyi pia, ninyi wenyewe mnajua, enyi Wafilipi, ya kuwa katika mwanzo wa Injili, nilipotoka Makedonia, hakuna kanisa lingine lililoshirikiana nami katika habari hii ya kutoa na kupokea, ila ninyi peke yenu.
16 Kwa kuwa hata huko Thesalonike mliniletea msaada kwa mahitaji yangu, wala si mara moja.
17 Si kwamba nakitamani kile kipawa, bali nayatamani mazao yanayozidi kuwa mengi, katika hesabu yenu.
18 Lakini ninavyo vitu vyote na kuzidi, tena nimejaa tele; nimepokea kwa mkono wa Epafrodito vitu vile vilivyotoka kwenu, harufu ya manukato, sadaka yenye kibali, impendezayo Mungu.
19 Na Mungu wangu atawajazeni kila mnachokihitaji kwa kadiri ya utajiri wake, katika utukufu, ndani ya Kristo Yesu.
20 Sasa atukuzwe Mungu, Baba yetu, milele na milele. Amina.
21 Mnisalimie kila mtakatifu katika Kristo Yesu. Ndugu walio pamoja nami wawasalimu.
22 Watakatifu wote wawasalimu, hasa wao walio wa nyumbani mwa Kaisari.
23 Neema ya Bwana Yesu Kristo na iwe pamoja na roho zenu.