2 WAKORINTHO

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13

2 WAKORINTHO 1


1 Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu; kwa kanisa la Mungu lililoko Korintho, pamoja na watakatifu wote walioko katika nchi yote ya Akaya.
2 Neema na iwe kwenu na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo.
3 Na ahimidiwe Mungu, Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote;
4 atufarijiye katika dhiki zetu zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo, tunazofarijiwa na Mungu.
5 Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo.
6 Lakini ikiwa sisi tu katika dhiki, ni kwa ajili ya faraja yenu na wokovu wenu; au ikiwa twafarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu; ambayo hutenda kazi yake kwa kustahimili mateso yale yale tuteswayo na sisi.
7 Na tumaini letu kwa ajili yenu ni imara, tukijua ya kuwa kama vile mlivyo washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo mmekuwa washiriki wa zile faraja.
8 Maana ndugu, hatupendi, msijue habari ya dhiki ile iliyotupata katika Asia, ya kwamba tulilemewa mno kuliko nguvu zetu, hata tukakata tamaa ya kuishi.
9 Naam, sisi wenyewe tulikuwa na hukumu ya mauti katika nafsi zetu ili tusijitumainie nafsi zetu, bali tumtumaini Mungu, awafufuaye wafu,
10 aliyetuokoa sisi katika mauti kuu namna ile; tena atatuokoa; ambaye tumemtumaini kwamba atazidi kutuokoa;
11 ninyi nanyi mkisaidiana nasi kwa ajili yetu katika kuomba, ili, kwa sababu ya ile karama tupewayo sisi kwa msaada wa watu wengi, watu wengi watoe shukrani kwa ajili yetu.
12 Kwa maana kujisifu kwetu ni huku, ushuhuda wa dhamiri yetu, ya kwamba kwa utakatifu na weupe wa moyo utokao kwa Mungu; si kwa hekima ya mwili, bali kwa neema ya Mungu; tulienenda katika dunia, na hasa kwenu ninyi.
13 Maana hatuwaandikii ninyi neno, ila yale msomayo, au kuyakiri; nami nataraji ya kuwa mtayakiri hayo hata mwisho;
14 vile vile kama mlivyotukiri kwa sehemu, ya kwamba sisi tu sababu ya kujisifu kwenu, kama ninyi mlivyo kwetu sisi, katika siku ile ya Bwana wetu Yesu.
15 Nami nikiwa na tumaini hilo nalitaka kufika kwenu hapo kwanza, ili mpate karama ya pili;
16 na kupita kwenu na kuendelea mpaka Makedonia; na tena toka Makedonia kurudi kwenu na kusafirishwa nanyi kwenda Uyahudi.
17 Basi, nilipokusudia hayo, je! Nalitumia kigeugeu? Au hayo niyakusudiayo, nayakusudia kwa jinsi ya mwili kwamba iwe hivi kwangu, kusema Ndiyo, ndiyo, na Siyo, siyo?
18 Lakini kama Mungu alivyo mwaminifu, neno letu kwenu si Ndiyo na siyo.
19 Maana Mwana wa Mungu, Kristo Yesu, aliyehubiriwa katikati yenu na sisi, yaani, mimi na Silwano na Timotheo, hakuwa Ndiyo na siyo; bali katika yeye ni Ndiyo.
20 Maana ahadi zote za Mungu zilizopo katika yeye ni Ndiyo; tena kwa hiyo katika yeye ni Amin; Mungu apate kutukuzwa kwa sisi.
21 Basi Yeye atufanyaye imara pamoja nanyi katika Kristo, na kututia mafuta, ni Mungu,
22 naye ndiye aliyetutia muhuri akatupa arabuni ya Roho mioyoni mwetu.
23 Lakini mimi namwita Mungu awe shahidi juu ya roho yangu, ya kwamba, kwa kuwahurumia sijafika Korintho.
24 Si kwamba tunatawala imani yenu; bali tu wasaidizi wa furaha yenu; maana kwa imani yenu mnasimama.

2 WAKORINTHO 2


1 Lakini nafsini mwangu nalikusudia hivi, nisije kwenu tena kwa huzuni.
2 Maana mimi nikiwatia huzuni, basi ni nani anifurahishaye mimi ila yeye ahuzunishwaye nami?
3 Nami naliwaandikia neno lilo hilo, ili nijapo nisitiwe huzuni na wale ambao ilinipasa kuwafurahia; nikiwatumaini ninyi nyote kwamba furaha yangu ni yenu nyote pia.
4 Maana katika dhiki nyingi na taabu ya moyo niliwaandikia na machozi mengi; si kwamba mhuzunishwe, bali mpate kujua upendo wangu nilio nao kwenu jinsi ulivyo mwingi.
5 Lakini iwapo mtu amehuzunisha, hakunihuzunisha mimi tu, bali kwa sehemu (nisije nikalemea mno), amewahuzunisha ninyi nyote.
6 Yamtosha mtu wa namna hii adhabu ile aliyopewa na walio wengi;
7 hata kinyume cha hayo, ni afadhali mmsamehe na kumfariji, mtu kama huyo asije akamezwa katika huzuni yake ipitayo kiasi.
8 Kwa hiyo nawasihi kumthibitishia upendo wenu.
9 Maana naliandika kwa sababu hii pia, ili nipate bayana kwenu kwamba mmekuwa wenye kutii katika mambo yote.
10 Lakini kama mkimsamehe mtu neno lo lote, nami nimemsamehe; kwa maana mimi nami, ikiwa nimemsamehe mtu neno lo lote, nimemsamehe kwa ajili yenu mbele za Kristo,
11 Shetani asije akapata kutushinda; kwa maana hatukosi kuzijua fikira zake.
12 Basi nilipofika Troa kwa ajili ya Injili ya Kristo, nikafunguliwa mlango katika Bwana,
13 sikuona raha nafsini mwangu, kwa sababu sikumwona Tito ndugu yangu, bali niliagana nao, nikaondoka kwenda Makedonia.
14 Ila Mungu ashukuriwe, anayetushangiliza daima katika Kristo, na kuidhihirisha harufu ya kumjua yeye kila mahali kwa kazi yetu.
15 Kwa maana sisi tu manukato ya Kristo, mbele za Mungu, katika wao wanaookolewa, na katika wao wanaopotea;
16 katika hao wa pili harufu ya mauti iletayo mauti; katika hao wa kwanza harufu ya uzima iletayo uzima. Naye ni nani atoshaye kwa mambo hayo?
17 Kwa maana sisi si kama walio wengi, walighoshio neno la Mungu; bali kama kwa weupe wa moyo, kama kutoka kwa Mungu, mbele za Mungu, twanena katika Kristo.

2 WAKORINTHO 3


1 Je! Tunaanza tena kujisifu wenyewe? Au tunahitaji, kama wengine, barua zenye sifa kuja kwenu, au kutoka kwenu?
2 Ninyi ndinyi barua yetu, iliyoandikwa mioyoni mwetu, inajulikana na kusomwa na watu wote;
3 mnadhihirishwa kwamba mmekuwa barua ya Kristo tuliyoikatibu, iliyoandikwa si kwa wino, bali kwa Roho wa Mungu aliye hai; si katika vibao vya mawe, ila katika vibao ambavyo ni mioyo ya nyama.
4 Na tumaini hilo tunalo mbele za Mungu kwa njia ya Kristo.
5 Si kwamba twatosha sisi wenyewe kufikiri neno lo lote kwamba ni letu wenyewe, bali utoshelevu wetu watoka kwa Mungu.
6 Naye ndiye aliyetutosheleza kuwa wahudumu wa agano jipya; si wa andiko, bali wa roho; kwa maana andiko huua, bali roho huhuisha.
7 Basi, ikiwa huduma ya mauti, iliyoandikwa na kuchorwa katika mawe, ilikuja katika utukufu, hata Waisraeli hawakuweza kuukazia macho uso wa Musa, kwa sababu ya utukufu wa uso wake; nao ni utukufu uliokuwa ukibatilika;
8 je! Huduma ya roho haitazidi kuwa katika utukufu?
9 Kwa maana ikiwa huduma ya adhabu ina utukufu, siuze huduma ya haki ina utukufu unaozidi.
10 Maana hata ile iliyotukuzwa haikuwa na utukufu hivi, kwa sababu ya utukufu uzidio sana.
11 Kwa maana, ikiwa ile inayobatilika ilikuwa na utukufu, zaidi sana ile ikaayo ina utukufu.
12 Basi, kwa kuwa mna taraja la namna hii, twatumia ujasiri mwingi;
13 nasi si kama Musa alivyotia utaji juu ya uso wake, ili kwamba Waisraeli wasitazame sana mwisho wa ile iliyokuwa ikibatilika;
14 ila fikira zao zilitiwa uzito. Kwa maana hata leo hivi, wakati lisomwapo Agano la Kale, utaji uo huo wakaa; yaani, haikufunuliwa kwamba huondolewa katika Kristo;
15 ila hata leo, torati ya Musa isomwapo, utaji huikalia mioyo yao.
16 Lakini wakati wo wote watakapomgeukia Bwana, ule utaji huondolewa.
17 Basi (Bwana) ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru.
18 Lakini sisi sote, kwa uso usiotiwa utaji, tukiurudisha utukufu wa Bwana, kama vile katika kioo, tunabadilishwa tufanane na mfano uo huo, toka utukufu hata utukufu, kama vile kwa utukufu utokao kwa Bwana, aliye Roho.

2 WAKORINTHO 4


1 Kwa sababu hiyo, kwa kuwa tuna huduma hii, kwa jinsi tulivyopata rehema, hatulegei;
2 lakini tumekataa mambo ya aibu yaliyositirika, wala hatuenendi kwa hila, wala kulichanganya neno la Mungu na uongo; bali kwa kuidhihirisha iliyo kweli twajionyesha kuwa na haki, dhamiri za watu zikitushuhudia mbele za Mungu.
3 Lakini ikiwa injili yetu imesitirika, imesitirika kwa hao wanaopotea;
4 ambao ndani yao mungu wa dunia hii amepofusha fikira zao wasioamini, isiwazukie nuru ya injili ya utukufu wake Kristo aliye sura yake Mungu.
5 Kwa maana hatujihubiri wenyewe, bali Kristo Yesu ya kuwa ni Bwana; na sisi wenyewe kuwa tu watumishi wenu kwa ajili ya Yesu.
6 Kwa kuwa Mungu, aliyesema, Nuru itang'aa toka gizani, ndiye aliyeng'aa mioyoni mwetu, atupe nuru ya elimu ya utukufu wa Mungu katika uso wa Yesu Kristo.
7 Lakini tuna hazina hii katika vyombo vya udongo, ili adhama kuu ya uwezo iwe ya Mungu, wala si kutoka kwetu.
8 Pande zote twadhikika, bali hatusongwi; twaona shaka, bali hatukati tamaa;
9 twaudhiwa, bali hatuachwi; twatupwa chini, bali hatuangamizwi;
10 siku zote twachukua katika mwili kuuawa kwake Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu.
11 Kwa maana sisi tulio hai, siku zote twatolewa tufe kwa ajili ya Yesu, ili uzima wa Yesu nao udhihirishwe katika miili yetu ipatikanayo na mauti.
12 Basi hapo mauti hufanya kazi ndani yetu, bali uzima ndani yenu.
13 Lakini kwa kuwa tuna roho ile ile ya imani; kama ilivyoandikwa, Naliamini, na kwa sababu hiyo nalinena; sisi nasi twaamini, na kwa sababu hiyo twanena;
14 tukijua ya kwamba yeye aliyemfufua Bwana Yesu atatufufua sisi nasi pamoja na Yesu, na kutuhudhurisha pamoja nanyi.
15 Kwa maana mambo yote ni kwa ajili yenu, ili neema hiyo ikiongezwa sana, kwa hao walio wengi shukrani izidishwe, na Mungu atukuzwe.
16 Kwa hiyo hatulegei; bali ijapokuwa utu wetu wa nje unachakaa, lakini utu wetu wa ndani unafanywa upya siku kwa siku.
17 Maana dhiki yetu nyepesi, iliyo ya muda wa kitambo tu, yatufanyia utukufu wa milele uzidio kuwa mwingi sana;
18 tusiviangalie vinavyoonekana, bali visivyoonekana. Kwa maana vinavyoonekana ni vya muda tu; bali visivyoonekana ni vya milele.

2 WAKORINTHO 5


1 Kwa maana twajua ya kuwa nyumba ya maskani yetu iliyo ya dunia hii ikiharibiwa, tunalo jengo litokalo kwa Mungu, nyumba isiyofanywa kwa mikono, iliyo ya milele mbinguni.
2 Maana katika nyumba hii twaugua, tukitamani sana kuvikwa kao letu litokalo mbinguni;
3 ikiwa tukiisha kuvikwa hatutaonekana tu uchi.
4 Kwa sababu sisi tulio katika maskani hii twaugua, tukilemewa; si kwamba twataka kuvuliwa, bali kuvikwa, ili kitu kile kipatikanacho na mauti kimezwe na uzima.
5 Basi yeye aliyetufanya kwa ajili ya neno lilo hilo ni Mungu, aliyetupa arabuni ya Roho.
6 Basi siku zote tuna moyo mkuu; tena twajua ya kuwa, wakati tuwapo hapa katika mwili, tunakaa mbali na Bwana.
7 (Maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona.)
8 Lakini tuna moyo mkuu; nasi tunaona ni afadhali kutokuwamo katika mwili na kukaa pamoja na Bwana.
9 Kwa hiyo, tena, ikiwa tupo hapa, au ikiwa hatupo hapa, twajitahidi kumpendeza yeye.
10 Kwa maana imetupasa sisi sote kudhihirishwa mbele ya kiti cha hukumu cha Kristo, ili kila mtu apokee ijara ya mambo aliyotenda kwa mwili, kadiri alivyotenda, kwamba ni mema au mabaya.
11 Basi tukiijua hofu ya Bwana, twawavuta wanadamu; lakini tumedhihirishwa mbele za Mungu. Nami natumaini ya kuwa tumedhihirishwa katika dhamiri zenu pia.
12 Maana hatujisifu wenyewe mbele yenu tena, bali tunawapa sababu ya kujisifu kwa ajili yetu, ili mpate kuwa nayo mbele yao wanaojisifu kwa mambo ya nje tu, wala si kwa mambo ya moyoni.
13 Maana ikiwa tumerukwa na akili zetu, ni kwa ajili ya Mungu; au ikiwa tunazo akili zetu timamu, ni kwa ajili yenu.
14 Maana, upendo wa Kristo watubidisha; maana tumehukumu hivi, ya kwamba mmoja alikufa kwa ajili ya wote, basi walikufa wote;
15 tena alikufa kwa ajili ya wote, ili walio hai wasiwe hai tena kwa ajili ya nafsi zao wenyewe, bali kwa ajili yake yeye aliyekufa akafufuka kwa ajili yao.
16 Hata imekuwa, sisi tangu sasa hatumjui mtu awaye yote kwa jinsi ya mwili. Ingawa sisi tumemtambua Kristo kwa jinsi ya mwili, lakini sasa hatumtambui hivi tena.
17 Hata imekuwa, mtu akiwa ndani ya Kristo amekuwa kiumbe kipya; ya kale yamepita tazama! Yamekuwa mapya.
18 Lakini vyote pia vyatokana na Mungu, aliyetupatanisha sisi na nafsi yake kwa Kristo, naye alitupa huduma ya upatanisho;
19 yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho.
20 Basi tu wajumbe kwa ajili ya Kristo, kana kwamba Mungu anasihi kwa vinywa vyetu; twawaomba ninyi kwa ajili ya Kristo mpatanishwe na Mungu.
21 Yeye asiyejua dhambi alimfanya kuwa dhambi kwa ajili yetu, ili sisi tupate kuwa haki ya Mungu katika Yeye.

2 WAKORINTHO 6


1 Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi msiipokee neema ya Mungu bure.
2 (Kwa maana asema, Wakati uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia;tazama,wakati uliokubalika ndiyo sasa; tazama siku ya wokovu ni sasa)
3 Tusiwe kwazo la namna yo yote katika jambo lo lote, ili utumishi wetu usilaumiwe;
4 bali katika kila neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa Mungu; katika saburi nyingi, katika dhiki, katika misiba, katika shida;
5 katika mapigo, katika vifungo, katika fitina, katika taabu, katika kukesha, katika kufunga;
6 katika kuwa safi, katika elimu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika Roho Mtakatifu, katika upendo usio unafiki;
7 katika neno la kweli, katika nguvu ya Mungu; kwa silaha za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto;
8 kwa utukufu na aibu; kwa kunenwa vibaya na kunenwa vema; kama wadanganyao, bali tu watu wa kweli;
9 kama wasiojulikana, bali wajulikanao sana; kama wanaokufa, kumbe tu hai; kama wanaorudiwa, bali wasiouawa;
10 kama wenye huzuni, bali siku zote tu wenye furaha; kama maskini, bali tukitajirisha wengi; kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu vyote.
11 Vinywa vyetu vimefumbuliwa kwenu, enyi Wakorintho; mioyo yetu imekunjuliwa.
12 Hamsongwi ndani yetu, bali mwasongwa katika mioyo yenu.
13 Basi, ili mlipe kadiri ile mliyopewa (nasema nanyi kama na watoto), nanyi pia mkunjuliwe mioyo.
14 Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza?
15 Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Au yeye aaminiye ana sehemu gani pamoja na yeye asiyeamini?
16 Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
17 Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha.
18 Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike,

2 WAKORINTHO 7


1 Basi, wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu katika kumcha Mungu.
2 Tupeni nafasi mioyoni mwenu. Hatukumdhulumu mtu ye yote, wala kumharibu mtu, wala kumkaramkia mtu.
3 Sisemi neno hilo ili niwahukumu ninyi kuwa na hatia; kwa maana nimetangulia kusema, ya kwamba ninyi mmo mioyoni mwetu hata kwa kufa pamoja, na kuishi pamoja.
4 Ninao ujasiri mwingi kwenu; naona fahari kuu juu yenu. Nimejaa faraja, katika dhiki yetu yote nimejaa furaha ya kupita kiasi.
5 Kwa maana hata tulipokuwa tumefika Makedonia miili yetu haikupata nafuu; bali tulidhikika kote kote; nje palikuwa na vita, ndani hofu.
6 Lakini Mungu, mwenye kuwafariji wanyonge, alitufariji kwa kuja kwake Tito.
7 Wala si kwa kuja kwake tu, bali kwa zile faraja nazo alizofarijiwa kwenu, akituarifu habari ya shauku yenu, na maombolezo yenu, na bidii yenu kwa ajili yangu, hata nikazidi kufurahi.
8 Kwa sababu, ijapokuwa naliwahuzunisha kwa waraka ule, sijuti; hata ikiwa nalijuta, naona ya kwamba waraka ule uliwahuzunisha, ingawa ni kwa kitambo tu.
9 Sasa nafurahi, si kwa sababu ya ninyi kuhuzunishwa, bali kwa sababu mlihuzunishwa, hata mkatubu. Maana mlihuzunishwa kwa jinsi ya Mungu, ili msipate hasara kwa tendo letu katika neno lo lote.
10 Maana huzuni iliyo kwa jinsi ya Mungu hufanya toba liletalo wokovu lisilo na majuto; bali huzuni ya dunia hufanya mauti.
11 Maana, angalieni, kuhuzunishwa kuko huko kwa jinsi ya Mungu kulitenda bidii kama nini ndani yenu; naam, na kujitetea, naam, na kukasirika, naam, na hofu, naam, na shauku, naam, na kujitahidi, naam, na kisasi! Kwa kila njia mmejionyesha wenyewe kuwa safi katika jambo hilo.
12 Basi, ijapokuwa naliwaandikia, sikuandika kwa ajili yake yeye aliyedhulumu, wala si kwa ajili yake yeye aliyedhulumiwa, bali bidii yenu kwa ajili yetu ipate kudhihirishwa kwenu mbele za Mungu.
13 Kwa hiyo tulifarijiwa. Tena katika kufarijiwa kwetu tulifurahi sana kupita kiasi kwa sababu ya furaha ya Tito; maana roho yake imeburudishwa na ninyi nyote.
14 Kwa maana, ikiwa nimejisifu mbele yake katika neno lo lote kwa ajili yenu, sikutahayarishwa; bali, kama tulivyowaambia mambo yote kwa kweli, vivyo hivyo na kujisifu kwetu kwa Tito kulikuwa kweli.
15 Na mapenzi yake kwenu yamekuwa mengi kupita kiasi, akumbukapo kutii kwenu ninyi nyote, jinsi mlivyomkaribisha kwa hofu na kutetemeka.
16 Nafurahi, kwa sababu katika kila neno nina moyo mkuu kwa ajili yenu.

2 WAKORINTHO 8


1 Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia;
2 maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na umaskini wao uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao.
3 Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao;
4 wakituomba sana pamoja na kutusihi kwa habari ya neema hii, na shirika hili la kuwahudumia watakatifu.
5 Tena walitenda hivi si kama tulivyotumaini tu, bali kwanza walijitoa nafsi zao kwa Bwana; na kwetu pia, kwa mapenzi ya Mungu.
6 Hata tukamwonya Tito kuwatimilizia neema hii kwenu kama vile yeye alivyotangulia kuianzisha.
7 Lakini kama mlivyo na wingi wa mambo yote; imani, na usemi, na elimu, na bidii yote, na upendo wenu kwetu sisi; basi vivyo hivyo mpate wingi wa neema hii pia.
8 Sineni ili kuwaamuru, bali kwa bidii ya watu wengine nijaribu unyofu wa upendo wenu.
9 Maana mmejua neema ya Bwana wetu Yesu Kristo, jinsi alivyokuwa maskini kwa ajili yenu, ingawa alikuwa tajiri, ili kwamba ninyi mpate kuwa matajiri kwa umaskini wake.
10 Nami katika neno hili natoa shauri langu; maana neno hili lawafaa ninyi mliotangulia, yapata mwaka, licha ya kutenda hata na kutaka pia.
11 Lakini sasa timizeni kule kutenda nako, ili kama vile mlivyokuwa tayari kutaka, vivyo hivyo mkawe tayari na kutimiza, kwa kadiri ya mlivyo navyo.
12 Maana, kama nia ipo, hukubaliwa kwa kadiri ya alivyo navyo mtu, si kwa kadiri ya asivyo navyo.
13 Maana sisemi hayo, ili wengine wapate raha nanyi mpate dhiki;
14 bali mambo yawe sawasawa; wakati huu wa sasa wingi wenu uwafae upungufu wao, ili na wingi wao uwafae ninyi mtakapopungukiwa; ili mambo yawe sawasawa.
15 Kama ilivyoandikwa, Aliyekusanya vingi, hakuzidi, wala yeye aliyekusanya vichache hakupungukiwa.
16 Lakini ahimidiwe Mungu atiaye bidii ile ile kwa ajili yenu katika moyo wa Tito.
17 Maana aliyapokea kweli yale maonyo; tena, huku akizidi kuwa na bidii, alisafiri kwenda kwenu kwa hiari yake mwenyewe.
18 Na pamoja naye tukamtuma ndugu yule ambaye sifa zake katika Injili zimeenea makanisani mwote.
19 Wala si hivyo tu, bali alichaguliwa na makanisa asafiri pamoja nasi katika jambo la neema hii, tunayoitumikia, ili Bwana atukuzwe, ukadhihirike utayari wetu.
20 Tukijiepusha na neno hili, mtu asije akatulaumu kwa habari ya karama hii tunayoitumikia;
21 tukitangulia kufikiri yaliyo mema, si mbele za Bwana tu, ila na mbele ya wanadamu.
22 Nasi pamoja nao tumemtuma ndugu yetu tuliyemwona mara nyingi katika mambo mengi kuwa ana bidii, na sasa ana bidii zaidi sana kwa sababu ya tumaini kuu alilo nalo kwenu.
23 Basi mtu akitaka habari za Tito, yeye ni mshirika wangu, na mtenda kazi pamoja nami kwa ajili yenu; tena akitaka habari za ndugu zetu, wao ni mitume wa makanisa, na utukufu wa Kristo.
24 Basi waonyesheni mbele ya makanisa hakika ya upendo wenu, na ya kujisifu kwetu kwa ajili yenu.

2 WAKORINTHO 9


1 Kwa habari za kuwahudumia watakatifu sina haja ya kuwaandikia.
2 Maana najua utayari wenu, ninaojisifia kwa ajili yenu kwa Wamakedonia, kwamba Akaya ilikuwa tayari tangu mwaka mzima; na bidii yenu imewatia moyo wengi wao.
3 Lakini naliwatuma hao ndugu, ili kujisifu kwetu kwa ajili yenu kusibatilike katika jambo hili; mpate kuwa tayari, kama nilivyosema;
4 kusudi, wakija Wamakedonia pamoja nami, na kuwakuta hamjawa tayari, tusije tukatahayarika sisi, (tusiseme ninyi), katika hali hiyo ya kutumaini.
5 Basi naliona ya kuwa ni lazima niwaonye ndugu hawa watangulie kufika kwenu, na kutengeneza mapema karama yenu mliyoahidi tangu zamani, ili iwe tayari, na hivi iwe kama kipawa, wala si kama kitu kitolewacho kwa unyimivu.
6 Lakini nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu.
7 Kila mtu na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu.
8 Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema;
9 kama ilivyoandikwa, Ametapanya, amewapa maskini, Haki yake yakaa milele.
10 Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu;
11 mkitajirishwa katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu.
12 Maana utumishi wa huduma hii hauwatimizii watakatifu riziki walizopungukiwa tu, bali huzidi sana kuwa na faida kwa shukrani nyingi apewazo Mungu;
13 kwa kuwa mkijaribiwa kwa utumishi huo, wanamtukuza Mungu kwa ajili ya utii wenu katika kuikiri Injili ya Kristo, na kwa ajili ya ukarimu wenu mliowashirikisha wao na watu wote.
14 Nao wenyewe, wakiomba dua kwa ajili yenu, wawaonea shauku kwa sababu ya neema ya Mungu iliyozidi sana ndani yenu.
15 Mungu ashukuriwe kwa sababu ya kipawa chake, tusichoweza kukisifu kama ipasavyo.

2 WAKORINTHO 10


1 Basi, mimi Paulo mwenyewe nawasihi kwa upole na utaratibu wa Kristo; mimi niliye mnyenyekevu nikiwapo pamoja nanyi, bali nisipokuwapo ni mwenye ujasiri kwenu;
2 naam, naomba kwamba nikiwapo, nisiwe na ujasiri kwa uthabiti ambao nahesabu kuwa nao juu ya wale wanaodhania ya kuwa sisi tunaenenda kwa jinsi ya mwili.
3 Maana ingawa tunaenenda katika mwili, hatufanyi vita kwa jinsi ya mwili;
4 (maana silaha za vita vyetu si za mwili, bali zina uwezo katika Mungu hata kuangusha ngome;)
5 tukiangusha mawazo na kila kitu kilichoinuka, kijiinuacho juu ya elimu ya Mungu; na tukiteka nyara kila fikira ipate kumtii Kristo;
6 tena tukiwa tayari kupatiliza maasi yote, kutii kwenu kutakapotimia.
7 Yaangalieni yaliyo mbele ya macho yenu. Mtu akijitumainia mwenyewe ya kuwa ni mtu wa Kristo, na afikiri hivi pia nafsini mwake, ya kwamba kama yeye alivyo mtu wa Kristo, vivyo hivyo na sisi.
8 Maana, nijapojisifu zaidi kidogo kwa ajili ya mamlaka yetu, (tuliyopewa na Bwana, tupate kuwajenga wala si kuwaangusha), sitatahayarika;
9 nisije nikaonekana kana kwamba nataka kuwaogofya kwa nyaraka zangu.
10 Maana wasema, Nyaraka zake ni nzito, hodari; bali akiwapo mwenyewe mwilini ni dhaifu, na maneno yake si kitu.
11 Mtu kama huyo na afikiri hivi, ya kwamba jinsi tulivyo kwa maneno katika nyaraka tusipokuwapo, ndivyo tulivyo kwa matendo tukiwapo.
12 Kwa kuwa hatuthubutu kujihesabu pamoja na baadhi yao wanaojisifu wenyewe, wala kujilinganisha nao; bali wao wenyewe wakijipima nafsi zao na nafsi zao, na wakijilinganisha nafsi zao na nafsi zao, hawana akili.
13 Lakini sisi hatutajisifu zaidi ya kadiri yetu; bali kwa kadiri ya kipimo tulichopimiwa na Mungu, yaani, kadiri ya kufika hata kwenu.
14 Maana hatujitanui nafsi zetu kupita kadiri yetu, kana kwamba hatuwafikii ninyi; kwa sababu tulitangulia kufika mpaka kwenu katika injili ya Kristo;
15 wala hatujisifu zaidi ya kadiri yetu, yaani, katika taabu za watu wengine; bali tukiwa na tumaini ya kwamba, imani yenu ikuapo, tutakuzwa kwenu kwa kadiri ya kipimo chetu, na kupata ziada;
16 hata kuihubiri Injili katika nchi zilizo mbele kupita nchi zenu; tusijisifu katika kipimo cha mtu mwingine kwa mambo yaliyokwisha kutengenezwa.
17 Lakini, Yeye ajisifuye, na ajisifu katika Bwana.
18 Maana mtu mwenye kukubaliwa si yeye ajisifuye, bali yeye asifiwaye na Bwana.

2 WAKORINTHO 11


1 Laiti mngechukuliana nami katika upumbavu wangu kidogo! Naam, mchukuliane nami.
2 Maana nawaonea wivu, wivu wa Mungu; kwa kuwa naliwaposea mume mmoja, ili nimletee Kristo bikira safi.
3 Lakini nachelea; kama yule nyoka alivyomdanganya Hawa kwa hila yake, asije akawaharibu fikira zenu, mkauacha unyofu na usafi kwa Kristo.
4 Maana yeye ajaye akihubiri Yesu mwingine ambaye sisi hatukumhubiri, au mkipokea roho nyingine msiyoipokea, au injili nyingine msiyoikubali, mnatenda vema kuvumiliana naye!
5 Maana nadhani ya kuwa mimi sikupungukiwa na kitu walicho nacho mitume walio wakuu.
6 Lakini nijapokuwa mimi ni mtu asiyejua kunena, hii si hali yangu katika elimu; ila katika kila neno tumedhihirishwa kwenu.
7 Je! Nalifanya dhambi kwa kunyenyekea ili ninyi mtukuzwe, kwa sababu naliwahubiri Injili ya Mungu bila ujira?
8 Naliwanyang'anya makanisa mengine mali yao, nikitwaa posho langu ili niwahudumie ninyi.
9 Nami nilipokuwa pamoja nanyi na kuhitaji sikumlemea mtu. Maana hao ndugu waliokuja kutoka Makedonia walinipa kadiri ya mahitaji yangu; nami katika mambo yote najilinda nafsi yangu nisiwalemee hata kidogo; tena najilinda.
10 Kama vile ile kweli ya Kristo ilivyo ndani yangu, hakuna mtu atakayenifumba kinywa katika kujisifu huku, katika mipaka ya Akaya.
11 Kwa nini? Je! Ni kwa sababu siwapendi ninyi? Mungu anajua.
12 Lakini nifanyalo nitalifanya, ili niwapinge hao watafutao nafasi wasipate nafasi; ili kwamba katika neno hilo wajisifialo waonekane kuwa kama sisi.
13 Maana watu kama hao ni mitume wa uongo, watendao kazi kwa hila, wanaojigeuza wawe mfano wa mitume wa Kristo.
14 Wala si ajabu. Maana Shetani mwenyewe hujigeuza awe mfano wa malaika wa nuru.
15 Basi si neno kubwa watumishi wake nao wakijigeuza wawe mfano wa watumishi wa haki, ambao mwisho wao utakuwa sawasawa na kazi zao.
16 Nasema tena, mtu asidhani ya kuwa mimi ni mpumbavu; lakini mjaponidhania hivi, mnikubali kama mpumbavu; ili mimi nami nipate kujisifu ngaa kidogo.
17 Ninenalo silineni agizo la Bwana, bali kama kwa upumbavu, katika ujasiri huu wa kujisifu.
18 Kwa sababu wengi wanajisifu kwa jinsi ya mwili, mimi nami nitajisifu.
19 Ninyi, kwa kuwa mna akili, mnachukuliana na wajinga kwa furaha.
20 Maana mwachukuliana na mtu akiwatia utumwani, akiwameza, akiwateka nyara, akijikuza, akiwapiga usoni.
21 Nanena kwa jinsi ya kujidhili kana kwamba sisi tulikuwa dhaifu. Walakini, akiwa mtu anao ujasiri kwa lo lote, (nanena kipuuzi), mimi nami ninao ujasiri.
22 Wao ni Waebrania? Na mimi pia. Wao ni Waisraeli? Na mimi pia. Wao ni uzao wa Ibrahimu? Na mimi pia.
23 Wao ni wahudumu wa Kristo? (Nanena kiwazimu), mimi ni zaidi; katika taabu kuzidi sana; katika vifungo kuzidi sana; katika mapigo kupita kiasi; katika mauti mara nyingi.
24 Kwa Wayahudi mara tano nalipata mapigo arobaini kasoro moja.
25 Mara tatu nalipigwa kwa bakora; mara moja nalipigwa kwa mawe; mara tatu nalivunjikiwa jahazi; kuchwa kucha nimepata kukaa kilindini;
26 katika kusafiri mara nyingi; hatari za mito; hatari za wanyang'anyi; hatari kwa taifa langu; hatari kwa mataifa mengine; hatari za mjini; hatari za jangwani; hatari za baharini; hatari kwa ndugu za uongo;
27 katika taabu na masumbufu; katika kukesha mara nyingi; katika njaa na kiu; katika kufunga mara nyingi; katika baridi na kuwa uchi.
28 Baghairi ya mambo ya nje, yako yanijiayo kila siku, ndiyo maangalizi ya makanisa yote.
29 Ni nani aliye dhaifu, nisiwe dhaifu nami? Ni nani aliyekwazwa nami nisichukiwe?
30 Ikinibidi kujisifu, nitajisifia mambo ya udhaifu wangu.
31 Mungu, Baba wa Bwana Yesu, aliye mtukufu hata milele, anajua ya kuwa sisemi uongo.
32 Huko Dameski liwali wa mfalme Areta alikuwa akiulinda mji wa Wadameski, ili kunikamata;
33 nami nikatelemshwa ndani ya kapu, katika dirisha la ukutani, nikaokoka katika mikono yake.

2 WAKORINTHO 12


1 Sina budi kujisifu, ijapokuwa haipendezi; lakini nitafikilia maono na mafunuo ya Bwana.
2 Namjua mtu mmoja katika Kristo, yapata sasa miaka kumi na minne, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua). Mtu huyo alinyakuliwa juu mpaka mbingu ya tatu.
3 Nami namjua mtu huyo, (kwamba alikuwa katika mwili sijui; kwamba alikuwa nje ya mwili sijui; Mungu ajua);
4 ya kuwa alinyakuliwa mpaka Peponi, akasikia maneno yasiyotamkika, ambayo haijuzu mwanadamu ayanene.
5 Kwa habari za mtu kama huyo nitajisifu; lakini kwa ajili ya nafsi yangu sitajisifu, isipokuwa katika habari ya udhaifu wangu.
6 Maana kama ningetaka kujisifu singekuwa mpumbavu, kwa sababu nitasema kweli. Lakini najizuia, ili mtu asinihesabie zaidi ya hayo ayaonayo kwangu au kuyasikia kwangu.
7 Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi.
8 Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke.
9 Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.
10 Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.
11 Nimekuwa mpumbavu, ninyi mmenilazimisha. Maana ilinipasa nisifiwe na ninyi; kwa sababu sikuwa duni ya mitume walio wakuu kwa lo lote, nijapokuwa si kitu.
12 Kweli ishara za mtume zilitendwa katikati yenu katika saburi yote, kwa ishara na maajabu na miujiza.
13 Maana ni kitu gani mlichopungukiwa kuliko makanisa mengine, ila kwa kuwa mimi sikuwalemea? Mnisamehe udhalimu huu.
14 Tazama, hii ni mara ya tatu ya mimi kuwa tayari kuja kwenu, wala sitawalemea. Maana sivitafuti vitu vyenu, bali nawatafuta ninyi; maana haiwapasi watoto kuweka akiba kwa wazazi, bali wazazi kwa watoto.
15 Nami kwa furaha nyingi nitatapanya, tena nitatapanywa kwa ajili ya roho zenu. Je! Kadiri nizidivyo kuwapenda sana, ninapungukiwa kupendwa?
16 Lakini na iwe hivyo, mimi sikuwalemea; bali kwa kuwa mwerevu naliwapata kwa hila.
17 Je! Mtu ye yote niliyemtuma kwenu, kwa mtu huyo naliwatoza kitu?
18 Nalimwonya Tito, nikamtuma ndugu yule pamoja naye. Je! Tito aliwatoza kitu? Je! Hatukuenenda kwa Roho yeye yule na katika nyayo zile zile?
19 Mwadhani hata sasa ya kuwa najidhuru kwenu! Mbele za Mungu twanena katika Kristo. Na hayo yote, wapenzi, ni kwa ajili ya kuwajenga ninyi.
20 Maana nachelea, nisije nikawakuta si kama vile nitakavyo kuwakuta, nikaonekana kwenu si kama vile mtakavyo; nisije nikakuta labda fitina na wivu, na ghadhabu, na ugomvi, na masingizio, na manong'onezo, na majivuno, na ghasia;
21 nami nitakapokuja tena, Mungu wangu asije akanidhili kwenu, nami nikawasikitikia wengi waliokosa tangu hapo, wasiutubie uchafu, na uasherati, na ufisadi walioufanya.

2 WAKORINTHO 13


1 Hii ndiyo mara ya tatu ya mimi kuja kwenu. Kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno litathibitishwa.
2 Nimetangulia kuwaambia; na, kama vile nilipokuwapo mara ya pili, vivyo hivyo sasa nisipokuwapo, nawaambia wazi wao waliotenda dhambi tangu hapo, na wengine wote, ya kwamba, nikija, sitahurumia;
3 kwa kuwa mnatafuta dalili ya Kristo, asemaye ndani yangu, ambaye si dhaifu kwenu, bali ana uweza ndani yenu.
4 Maana, alisulibiwa katika udhaifu, lakini anaishi kwa nguvu za Mungu. Maana sisi nasi tu dhaifu katika yeye; lakini tutaishi pamoja naye kwa uweza wa Mungu ulio kwenu.
5 Jijaribuni wenyewe kwamba mmekuwa katika imani; jithibitisheni wenyewe. Au hamjijui wenyewe, kwamba Yesu Kristo yu ndani yenu? Isipokuwa mmekataliwa.
6 Lakini natumaini kama mtajua ya kuwa sisi hatukukataliwa.
7 Nasi twamwomba Mungu, msifanye lo lote lililo baya; si kwamba sisi tuonekane tumekubaliwa, lakini ninyi mfanye lile lililo jema, tujapokuwa sisi tu kama waliokataliwa.
8 Maana hatuwezi kutenda neno lo lote kinyume cha kweli, bali kwa ajili ya kweli.
9 Maana twafurahi, iwapo sisi tu dhaifu, nanyi mmekuwa hodari. Tena twaomba hili nalo, kutimilika kwenu.
10 Kwa sababu hiyo, naandika haya nisipokuwapo, ili, nikiwapo, nisiutumie ukali kwa kadiri ya uwezo ule niliopewa na Bwana, kwa kujenga wala si kwa kubomoa.
11 Hatimaye, ndugu, kwaherini; mtimilike, mfarijike, nieni mamoja, mkae katika amani; na Mungu wa upendo na amani atakuwa pamoja nanyi.
12 Salimianeni kwa busu takatifu.
13 Watakatifu wote wawasalimu.
14 Neema ya Bwana Yesu Kristo, na pendo la Mungu, na ushirika wa Roho Mtakatifu ukae nanyi nyote.