Zekaria

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14

Zekaria 1


1 Katika mwezi wa nane, mwaka wa pili wa Dario, neno la Bwana lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema,
2 Bwana amewakasirikia sana baba zenu.
3 Basi, uwaambie, Bwana wa majeshi asema hivi, Nirudieni mimi, asema Bwana wa majeshi, nami nitawarudia ninyi, asema Bwana wa majeshi.
4 Msiwe ninyi kama baba zenu, ambao manabii wa zamani waliwalilia, wakisema, Bwana wa majeshi asema hivi, Rudini sasa, na kuziacha njia zenu mbovu, na matendo yenu maovu; lakini hawakusikia, wala kunisikiliza, asema Bwana.
5 Je! Baba zenu wako wapi? Nao manabii je! Waishi milele?
6 Lakini maneno yangu, na amri zangu nilizowaagiza hao manabii, watumishi wangu, je! Hazikuwapata baba zenu? Nao wakageuka na kusema, Vile vile kama Bwana wa majeshi alivyoazimia kututenda, sawasawa na njia zetu, na sawasawa na matendo yetu, ndivyo alivyotutenda.
7 Siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kumi na moja, yaani, mwezi uitwao Shebati, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la Bwana lilimjia Zekaria, mwana wa Berekia, mwana wa Ido, nabii, kusema,
8 Naliona wakati wa usiku, na tazama, mtu amepanda farasi mwekundu, akasimama kati ya mihadasi iliyokuwa mahali penye uvuli; na nyuma yake walikuwapo farasi wengine wekundu, na wa rangi ya kijivujivu, na weupe.
9 Ndipo nikasema, Ee Bwana wangu, ni nini hawa? Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Nitakuonyesha ni nini hawa.
10 Na yule mtu aliyesimama kati ya mihadasi akajibu, akasema, Hawa ndio Bwana aliowatuma, waende huko na huko duniani.
11 Nao wakamjibu yule malaika wa Bwana aliyesimama kati ya mihadasi, wakasema, Tumekwenda huko na huko duniani, na tazama, dunia yote inatulia, nayo imestarehe.
12 Ndipo yule malaika wa Bwana akajibu, akasema, Ee Bwana wa majeshi, hata lini utakataa kuurehemu Yerusalemu, na miji ya Yuda uliyoikasirikia miaka hii sabini?
13 Naye Bwana akamjibu yule malaika aliyesema nami kwa maneno mazuri, maneno yenye faraja.
14 Basi yule malaika aliyesema nami akaniambia, Haya, piga kelele na kusema, Bwana wa majeshi asema hivi, Naona wivu kwa ajili ya Yerusalemu, na kwa ajili ya Sayuni; naona wivu mkuu sana.
15 Nami ninawakasirikia sana mataifa wanaokaa hali ya raha; kwa maana mimi sikukasirika ila kidogo tu, na wao waliyahimiza mateso.
16 Kwa sababu hiyo Bwana asema hivi, Ninaurudia Yerusalemu kwa rehema nyingi; nyumba yangu itajengwa ndani yake, asema Bwana wa majeshi, na kamba itanyoshwa juu ya Yerusalemu.
17 Piga kelele tena, na kusema, Bwana wa majeshi asema hivi, Miji yangu kwa kufanikiwa itaenezwa huko na huko tena; naye Bwana ataufariji Sayuni tena, atauchagua Yerusalemu tena.
18 Nami nikainua macho yangu, nikaona, na tazama, pembe nne.
19 Nami nikamwuliza yule malaika aliyesema nami, Nini hizi? Naye akanijibu, Hizi ndizo pembe zilizowatawanya watu wa Yuda, na Israeli, na Yerusalemu.
20 Kisha Bwana akanionyesha wafua chuma wanne.
21 Ndipo nikauliza Hawa wanakuja kufanya nini? Akasema kwamba, Hizi ndizo pembe zilizowatawanya watu wa Yuda, hata ikawa hakuna mtu aliyeinua kichwa chake; lakini hawa wamekuja kuzifukuza, kuziangusha pembe za mataifa, walioinua pembe yao juu ya nchi ya Yuda, ili kuwatawanya watu wake.

Zekaria 2


1 Kisha nikainua macho yangu, nikaona, na tazama, mtu mwenye kamba ya kupimia mkononi mwake.
2 Ndipo nikasema, Unakwenda wapi? Akaniambia, Ninakwenda kuupima Yerusalemu, nione upana wake ulivyo na urefu wake ulivyo.
3 Na tazama, yule malaika aliyesema nami akasimama karibu, na malaika mwingine akatoka ili kuonana naye;
4 naye akamwambia, Piga mbio, kamwambie kijana huyu, na kusema, Yerusalemu utakaliwa na watu, kama vijiji visivyo na kuta, kwa sababu ya wingi wa watu na mifugo iliyomo ndani yake.
5 Kwa maana mimi, asema Bwana, nitakuwa ukuta wa moto kuuzunguka pande zote, nami nitakuwa huo utukufu ndani yake.
6 Haya! Haya! Ikimbieni nchi ya kaskazini, asema Bwana; kwa maana mimi nimewatawanya ninyi kama pepo nne za mbinguni, asema Bwana.
7 Haya! Ee Sayuni, jiponye, wewe ukaaye pamoja na binti Babeli.
8 Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Ili nitafute utukufu amenituma kwa mataifa wale waliowateka ninyi; maana yeye awagusaye ninyi aigusa mboni ya jicho lake.
9 Kwa maana, tazama, nitatikisa mkono wangu juu yao, nao watakuwa mateka ya hao waliowatumikia; nanyi mtajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma.
10 Imba, ufurahi, Ee binti Sayuni; maana, tazama, ninakuja, nami nitakaa kati yako, asema Bwana.
11 Na mataifa mengi watajiunga na Bwana katika siku ile, nao watakuwa watu wangu; nami nitakaa kati yako, nawe utajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwako.
12 Na Bwana atairithi Yuda, iwe sehemu yake katika nchi takatifu, naye atachagua Yerusalemu tena.
13 Nyamazeni, ninyi nyote wenye mwili, mbele za Bwana; kwa maana ameamka, na kutoka katika maskani yake takatifu.

Zekaria 3


1 Kisha akanionyesha Yoshua, kuhani mkuu, amesimama mbele ya malaika wa Bwana, na Shetani amesimama mkono wake wa kuume ili kushindana naye.
2 Bwana akamwambia Shetani, Bwana na akukemee Ewe Shetani; naam, Bwana, aliyechagua Yerusalemu, na akukemee; je! Hiki si kinga kilichotolewa motoni?
3 Basi, Yoshua alikuwa amevaa nguo chafu sana, naye alikuwa akisimama mbele ya malaika.
4 Naye huyo akajibu, akawaambia wale waliosimama mbele yake, akisema, Mvueni nguo hizi zenye uchafu. Kisha akamwambia yeye, Tazama, nimekuondolea uovu wako, nami nitakuvika mavazi ya thamani nyingi.
5 Nikasema, Na wampige kilemba kizuri kichwani pake. Basi, wakampiga kilemba kizuri kichwani pake, wakamvika mavazi; naye malaika wa Bwana akasimama karibu.
6 Kisha malaika wa Bwana akamshuhudia Yoshua, akisema,
7 Bwana wa majeshi asema hivi, Kama ukienda katika njia zangu, na kama ukishika maagizo yangu, ndipo utakapoihukumu nyumba yangu, nawe utazilinda nyua zangu, nami nitakupa nafasi ya kunikaribia kati yao wasimamao karibu.
8 Sikiliza sasa, Ee Yoshua, kuhani mkuu, wewe na wenzako waketio mbele yako; maana hao ni watu walio ishara; kwa maana, tazama, ninamleta mtumishi wangu, aitwaye Chipukizi.
9 Maana, litazame jiwe hili nililoliweka mbele ya Yoshua; katika jiwe moja yako macho saba; tazama, nitachora machoro yake, asema Bwana wa majeshi, nami nitauondoa uovu wa nchi ile katika siku moja.
10 Katika siku ile, asema Bwana wa majeshi, ninyi mtamwalika kila mtu jirani yake chini ya mzabibu, na chini ya mtini.

Zekaria 4


1 Na yule malaika aliyesema nami akanijia mara ya pili, akaniamsha, kama mtu aamshwavyo katika usingizi wake.
2 Akaniuliza, Unaona nini? Nikasema, Nimeona, na tazama, kinara cha taa cha dhahabu tupu, nacho kina bakuli juu yake, na taa zake saba juu yake; tena iko mirija saba ya kuleta mafuta, kwa taa zote zilizo juu yake;
3 na mizeituni miwili karibu yake, mmoja upande wa kuume walile bakuli, na mmoja upande wake wa kushoto.
4 Nami nikajibu, nikamwambia yule malaika aliyesema nami, nikasema, Ee Bwana wangu, vitu hivi ni nini?
5 Ndipo malaika aliyesema nami akajibu, akaniambia, Hujui vitu hivi ni nini? Nikasema, La, Bwana wangu.
6 Akajibu akaniambia, akisema, Hili ndilo neno la Bwana kwa Zerubabeli, kusema, Si kwa uwezo, wala si kwa nguvu, bali ni kwa roho yangu, asema Bwana wa majeshi.
7 Nani wewe, Ee mlima mkubwa? Mbele ya Zerubabeli utakuwa nchi tambarare; naye atalileta lile jiwe la kuwekwa juu kabisa pamoja na vigelegele vya, Neema, neema, ilikalie.
8 Tena neno la Bwana likanijia, kusema,
9 Mikono yake Zerubabeli imeiweka misingi ya nyumba hii, na mikono yake ndiyo itakayoimaliza; nawe utajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwenu.
10 Maana ni nani aliyeidharau siku ya mambo madogo? Kwa kuwa watafurahi, nao wataiona timazi katika mkono wa Zerubabeli; naam, hizi saba ndizo macho ya Bwana; yapiga mbio huko na huko duniani mwote.
11 Ndipo nikajibu, nikamwambia, Ni nini mizeituni hii miwili iliyo upande wa kuume wa kinara cha taa kile na upande wake wa kushoto?
12 Nami nikajibu mara ya pili, nikamwuliza, Ni nini haya matawi mawili ya mizeituni, ambayo kwa njia ya ile mifereji miwili ya dhahabu hutoa mafuta yao?
13 Akanijibu, akasema, Hujui hivi ni nini? Nikasema, La, Bwana wangu.
14 Ndipo akasema, Hivi ni hao wana wawili wa mafuta, wasimamao karibu na Bwana wa dunia yote.

Zekaria 5


1 Basi, nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, gombo la chuo lirukalo.
2 Akaniuliza, Unaona nini? Nikajibu, Naona gombo la chuo lirukalo; na urefu wake ni dhiraa ishirini, na upana wake dhiraa kumi.
3 Ndipo akaniambia, Hii ndiyo laana itokayo kwenda juu ya uso wa nchi yote; maana kwa hiyo kila aibaye atatolewa kama ilivyo upande mmoja, na kwa hiyo kila aapaye atatolewa kama ilivyo upande wa pili.
4 Nitaituma itokee, asema Bwana wa majeshi, nayo itaingia katika nyumba ya mwivi, na katika nyumba yake yeye aapaye kwa uongo kwa jina langu; nayo itakaa katikati ya nyumba yake, na kuiteketeza, pamoja na boriti zake na mawe yake.
5 Ndipo yule malaika aliyesema nami akatokea, akaniambia, Inua macho yako sasa, uone ni kitu gani kitokeacho.
6 Nikasema, Ni kitu gani? Akasema, Kitu hiki ni efa itokeayo. Tena akasema, Huu ndio uovu wao katika nchi hii yote;
7 na tazama, talanta ya risasi iliinuliwa; na tazama, mwanamke akaaye katikati ya hiyo efa.
8 Akasema, Huyu ni Uovu; akamtupa chini katikati ya ile efa; akalitupa lile jiwe la risasi juu ya mdomo wa ile efa.
9 Ndipo nikainua macho yangu, nikaona, na tazama, wanawake wawili walitokea, nao upepo ulikuwa katika mabawa yao; na mabawa yao yalikuwa kama mabawa ya korongo; wakaiinua ile efa kati ya dunia na mbingu.
10 Ndipo nikamwambia yule malaika aliyesema nami, Hawa wanaipeleka wapi efa hii?
11 Akaniambia, Wanakwenda kumjengea nyumba katika nchi ya Shinari; tena ikiisha kutengenezwa, atawekwa huko mahali pake mwenyewe.

Zekaria 6


1 Nikainua macho yangu tena, nikaona, na tazama, yanatokea magari ya vita manne, yanatoka kati ya milima miwili, na milima hiyo ilikuwa ni milima ya shaba.
2 Katika gari la kwanza walikuwa farasi wekundu; na katika gari la pili walikuwa farasi weusi;
3 na katika gari la tatu walikuwa farasi weupe; na katika gari la nne walikuwa farasi wa rangi ya kijivujivu.
4 Nikajibu, nikamwuliza yule malaika aliyesema nami, Hawa ni nini, Bwana wangu?
5 Malaika akajibu, akaniambia, Hawa ni pepo nne za mbinguni, zitokeazo baada ya kusimama mbele za Bwana wa dunia yote.
6 Gari lile lenye farasi weusi latoka kwenda hata nchi ya kaskazini; nao farasi weupe wakatoka wakafuata nyuma yao; na wale wa rangi ya kijivujivu wakatoka kwenda hata nchi ya kusini.
7 Na wale wekundu wakatoka, wakataka kwenda huko na huko katika dunia; naye akawaambia, Haya! Tokeni, mwende huko na huko katika dunia. Basi wakaenda huko na huko katika dunia.
8 Ndipo akaniita, akaniambia akisema, Tazama, wale waendao mpaka nchi ya kaskazini wameituliza roho yangu katika nchi ya kaskazini.
9 Neno la Bwana likanijia, kusema,
10 Pokea vitu mikononi mwa baadhi ya watu waliohamishwa, yaani, Heldai, na Tobia, na Yedaya; na siku iyo hiyo enenda ukaingie katika nyumba ya Yosia, mwana wa Sefania, waliyoifikia kutoka Babeli;
11 naam, pokea fedha na dhahabu, ukafanye taji, ukamvike kichwani Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu;
12 ukamwambie, ukisema, Bwana wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Tazama, mtu huyu ndiye ambaye jina lake ni Chipukizi; naye atakua katika mahali pake, naye atalijenga hekalu la Bwana.
13 Naam, yeye atalijenga hekalu la Bwana; naye atauchukua huo utukufu; ataketi akimiliki katika kiti chake cha enzi; na kutakuwa na kuhani katika kiti chake cha enzi; na shauri la amani litakuwa kati ya hao wawili.
14 Na hizo taji zitakuwa za Heldai, na Tobia, na Yedaya; na kwa fadhili za mwana wa Sefania; ziwe ukumbusho katika hekalu la Bwana.
15 Nao walio mbali watakuja na kujenga katika hekalu la Bwana, nanyi mtajua ya kuwa Bwana wa majeshi amenituma kwenu. Na haya yatatokea, kama mkijitahidi kuitii sauti ya Bwana, Mungu wenu.

Zekaria 7


1 Ikawa katika mwaka wa nne wa mfalme Dario, neno la Bwana lilimjia Zekaria, siku ya nne ya mwezi wa kenda, yaani, Kisleu.
2 Basi watu wa Betheli walikuwa wamewatuma Shareza na Regem-meleki, na watu wao, ili kuomba fadhili za Bwana,
3 na kusema na makuhani wa nyumba ya Bwana wa majeshi, na hao manabii, ya kwamba, Je! Yanipasa kulia katika mwezi wa tano, na kujitenga na watu, kama nilivyofanya miaka hii mingi iliyopita?
4 Ndipo neno la Bwana wa majeshi likanijia, kusema,
5 Waambie watu wote wa nchi, na hao makuhani, ukisema, Hapo mlipofunga na kuomboleza katika mwezi wa tano na mwezi wa saba, katika miaka hiyo sabini, je! Mlinifungia mimi kwa lo lote; mlinifungia mimi?
6 Na wakati mlapo chakula na kunywa, je! Hamli kwa ajili ya nafsi zenu, na kunywa kwa ajili ya nafsi zenu?
7 Je! Hayo siyo maneno aliyoyasema Bwana kwa vinywa vya manabii wa zamani, wakati Yerusalemu ulipokaliwa na watu na kufanikiwa, na miji yake iliyokuwa ikiuzunguka; na wakati ule ambao nchi ya Negebu na Shefela ilipokuwa ikikaliwa na watu?
8 Kisha neno la Bwana likamjia Zekaria, kusema,
9 Bwana wa majeshi amesema hivi, ya kwamba, Fanyeni hukumu za kweli, kila mtu na amwonee ndugu yake rehema na huruma;
10 tena msimdhulumu mjane, wala yatima, wala mgeni, wala maskini; wala mtu awaye yote miongoni mwenu asiwaze mabaya juu ya ndugu yake moyoni mwake.
11 Lakini hao walikataa kusikiliza, wakageuza bega lao, wakaziba masikio yao ili wasisikie.
12 Naam, walifanya mioyo yao kuwa kama jiwe gumu, wasije wakaisikia sheria na maneno ya Bwana wa majeshi, aliyoyapeleka kwa roho yake kwa mkono wa manabii wa kwanza; kwa sababu hiyo ghadhabu kuu ikatoka kwa Bwana wa majeshi.
13 Ikawa kwa sababu alilia, wao wasitake kusikiliza; basi, wao nao watalia, wala mimi sitasikiliza, asema Bwana wa majeshi.
14 Lakini nitawatawanya kwa upepo wa kisulisuli, katikati ya mataifa yote wasiowajua. Basi hivyo ndivyo ilivyokuwa ukiwa nchi baada yao, hata hapakuwa na mtu aliyepita kati yake, wala aliyerudi; maana waliifanya nchi iliyopendeza sana kuwa ukiwa.

Zekaria 8


1 Neno la Bwana wa majeshi likanijia, kusema,
2 Bwana wa majeshi asema hivi, Mimi nina wivu kwa ajili ya Sayuni, wivu mkuu, nami nina wivu kwa ajili yake kwa ghadhabu kuu.
3 Bwana asema hivi, Mimi nimerudi Sayuni, nami nitakaa katikati ya Yerusalemu; na Yerusalemu utaitwa, Mji wa kweli; na Mlima wa Bwana wa majeshi utaitwa, Mlima mtakatifu.
4 Bwana wa majeshi asema hivi, Wazee wanaume na wazee wanawake watakaa tena katika njia za Yerusalemu, kila mtu ana mkongojo wake mkononi, kwa kuwa ni mzee sana.
5 Na hizo njia za mji zitajaa wavulana, na wasichana, wakicheza katika njia zake.
6 Bwana wa majeshi asema hivi, Ingawa hili ni neno lililo gumu mbele ya macho ya mabaki ya watu hawa katika siku hizo, je! Liwe neno gumu mbele ya macho yangu? Asema Bwana wa majeshi.
7 Bwana wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawaokoa watu wangu toka nchi ya mashariki, na toka nchi ya magharibi;
8 nami nitawaleta, nao watakaa katikati ya Yerusalemu; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao, katika kweli na katika haki.
9 Bwana wa majeshi asema hivi, Mikono yenu na iwe hodari, ninyi mnaosikia siku hizi maneno haya kwa vinywa vya manabii, waliokuwapo siku hiyo ulipowekwa msingi wa nyumba ya Bwana wa majeshi; yaani, hekalu hilo; ili lijengwe.
10 Maana kabla ya siku zile hapakuwa na ijara kwa mwanadamu, wala hapakuwa na ijara kwa mnyama; wala hapakuwa na amani kwake yeye aliyetoka, wala kwake yeye aliyeingia, kwa sababu ya adui; nami nalimwacha kila mtu kugombana na jirani yake.
11 Lakini sasa sitakuwa kwa mabaki ya watu hawa kama nilivyokuwa siku zile za kwanza, asema Bwana wa majeshi.
12 Kwa maana itakuwako mbegu ya amani; mzabibu utatoa matunda yake, nayo ardhi itatoa mazao yake, na hizo mbingu zitatoa umande wake; nami nitawarithisha mabaki ya watu hawa vitu hivi vyote.
13 Kisha itakuwa, kama vile mlivyokuwa laana katika mataifa, Ee nyumba ya Yuda, na nyumba ya Israeli, ndivyo nitakavyowaokoa, nanyi mtakuwa baraka; msiogope, lakini mikono yenu na iwe hodari.
14 Maana Bwana wa majeshi asema hivi, Kama vile nilivyoazimia kuwatenda ninyi mabaya, baba zenu waliponikasirisha, asema Bwana wa majeshi, wala mimi sikujuta;
15 vivyo hivyo nimeazimia katika siku hizi kuutendea Yerusalemu mema, na nyumba ya Yuda pia; msiogope.
16 Haya ndiyo mtakayoyatenda; kila mtu na aseme kweli na jirani yake; hukumuni kweli na hukumu ya amani malangoni mwenu;
17 wala mtu wa kwenu asiwaze mabaya moyoni mwake juu ya jirani yake; wala msipende kiapo cha uongo; maana hayo yote ndiyo niyachukiayo, asema Bwana.
18 Tena neno la Bwana wa majeshi likanijia, kusema,
19 Bwana wa majeshi asema hivi, Saumu ya mwezi wa nne, na saumu ya mwezi wa tano, na saumu ya mwezi wa saba, na saumu ya mwezi wa kumi, zitakuwa furaha na shangwe, na sikukuu za kuchangamkia, kwa nyumba ya Yuda; basi zipendeni kweli na amani.
20 Bwana wa majeshi asema hivi, Itatokea halafu ya kwamba watakuja mataifa na wenyeji wa miji mingi;
21 wenyeji wa mji huu watauendea mji huu, wakisema, Haya! Twendeni zetu kwa haraka tuombe fadhili za Bwana, na kumtafuta Bwana wa majeshi; Mimi nami nitakwenda.
22 Naam, watu wa kabila nyingi na mataifa hodari watakuja Yerusalemu kumtafuta Bwana wa majeshi, na kuomba fadhili za Bwana.
23 Bwana wa majeshi asema hivi, Siku hizo watu kumi, wa lugha zote za mataifa, wataushika upindo wa nguo yake yeye aliye Myahudi; naam, wataushika wakisema, Tutakwenda pamoja nanyi, kwa maana tumesikia kwamba Mungu yu pamoja nanyi.

Zekaria 9


1 Ufunuo wa neno la Bwana, lililosemwa juu ya nchi ya Hadraki, na Dameski itakuwa mahali pake pa kustarehe; kwa maana jicho la mwanadamu na la kabila zote za Israeli linamwelekea Bwana;
2 na Hamathi pia iliyo mpakani mwake; na Tiro, na Sidoni, kwa maana ana akili nyingi.
3 Na Tiro alijijengea ngome, akakusanya fedha kama mchanga, dhahabu safi kama matope ya njia kuu.
4 Tazama, Bwana atamwondolea mali zake, naye ataupiga uwezo wake alio nao baharini, naye mwenyewe atateketezwa kwa moto.
5 Ashkeloni ataona haya na kuogopa; Gaza pia, naye atafadhaika sana; na Ekroni, kwa maana taraja lake litatahayarika; na mfalme ataangamia toka Gaza, na Ashkeloni atakuwa hana watu.
6 Na mwana wa haramu atatawala huko Ashdodi, nami nitakatilia mbali kiburi cha Wafilisti.
7 Nami nitaondoa damu yake kinywani mwake, na machukizo yake nitayatoa katika meno yake; yeye naye atakuwa ni mabaki kwa Mungu wetu; naye atakuwa kama mtu mkuu katika Yuda, na Ekroni kama Myebusi.
8 Nami nitapiga kambi yangu pande zote za nyumba yangu ili kuwapinga adui, mtu awaye yote asipite ndani yake wala kurudi; wala mtu aoneaye hatapita tena kati yao; kwa maana sasa nimeona kwa macho yangu.
9 Furahi sana, Ee binti Sayuni; Piga kelele, Ee binti Yerusalemu; Tazama, mfalme wako anakuja kwako; Ni mwenye haki, naye ana wokovu; Ni mnyenyekevu, amepanda punda, Naam, mwana-punda, mtoto wa punda.
10 Na gari la vita nitaliondoa liwe mbali na Efraimu, na farasi awe mbali na Yerusalemu, na upinde wa vita utaondolewa mbali; naye atawahubiri mataifa yote habari za amani; na mamlaka yake yatakuwa toka bahari hata bahari, na toka Mto hata miisho ya dunia.
11 Na kwa habari zako wewe, kwa sababu ya damu ya agano lako, nimewatoa wafungwa wako katika shimo lile lisilo na maji.
12 Irudieni ngome, enyi wafungwa wa tumaini; hata hivi leo nasema ya kwamba nitakurudishia maradufu.
13 Maana nimejipindia Yuda, nimeujaza upinde wangu Efraimu; nami nitawaondokesha wana wako, Ee Sayuni, wapigane na wana wako, Ee Uyunani, nami nitakufanya wewe kuwa kama upanga wa shujaa.
14 Naye Bwana ataonekana juu yao, Na mshale wake utatoka kama umeme; Na Bwana MUNGU ataipiga tarumbeta, Naye atakwenda kwa pepo za kisulisuli za kusini.
15 Bwana wa majeshi atawalinda; Nao watakula na kuyakanyaga mawe ya teo; Nao watakunywa na kufanya kelele kama kwa divai; Nao watajazwa kama mabakuli, kama pembe za madhabahu.
16 Na Bwana, Mungu wao, atawaokoa siku hiyo, Kama kundi la watu wake; Kwa maana watakuwa kama vito vya taji, Vikimeta-meta juu ya nchi yake.
17 Maana wema wake, jinsi ulivyo mwingi! Na uzuri wake, jinsi ulivyo mwingi! Nafaka itawasitawisha vijana wanaume, Na divai mpya vijana wanawake.

Zekaria 10


1 Mwombeni Bwana mvua wakati wa masika, naam, Bwana afanyaye umeme, naye atawapa manyunyu ya mvua, kila mtu atapewa nyasi kondeni.
2 Kwa maana vinyago vimenena maneno ya ubatili, nao waaguzi wameona uongo; nao wameleta habari za ndoto za uongo, wafariji bure; kwa sababu hiyo waenda zao kama kondoo, wateswa, kwa sababu hapana mchungaji.
3 Hasira yangu imewaka juu ya wachungaji, nami nitawaadhibu mbuzi waume; kwa maana Bwana wa majeshi ameliangalia kundi lake, yaani, nyumba ya Yuda, naye atawafanya kuwa kama farasi wake mzuri vitani.
4 Kwake yeye litatoka lile jiwe la pembeni, kwake yeye utatoka msumari, kwake yeye utatoka upinde wa vita, kwake yeye atatoka kila mtawala pamoja.
5 Nao watakuwa kama mashujaa, wakanyagao adui zao katika matope ya njia vitani; nao watapiga vita, kwa sababu Bwana yu pamoja nao; na hao wapandao farasi watafadhaishwa.
6 Nami nitaitia nguvu nyumba ya Yuda, nami nitaiokoa nyumba ya Yusufu, nami nitawarudisha, kwa maana nawaonea rehema; nao watakuwa kana kwamba sikuwatupa; kwa maana mimi ni Bwana, Mungu wao, nami nitawasikia.
7 Na watu wa Efraimu watakuwa kama shujaa, na moyo wao utafurahi kana kwamba ni kwa divai; naam, watoto wao wataona mambo haya, na kufurahi; mioyo yao itamfurahia Bwana.
8 Nitawapigia kelele, na kuwakusanya pamoja; kwa maana nimewakomboa; nao wataongezeka kama walivyoongezeka.
9 Nami nitawapanda kama mbegu kati ya mataifa; nao watanikumbuka katika nchi zilizo mbali; nao watakaa pamoja na watoto wao; tena watarudi.
10 Tena nitawarudisha toka nchi ya Misri, nitawakusanya na kuwatoa katika Ashuru; nami nitawaingiza katika nchi ya Gileadi na Lebanoni; ila nafasi ya kuwatosha haitaonekana.
11 Naye atapita kati ya bahari ya mateso, na kuyapiga mawimbi ya bahari, na vilindi vyote vya mto wa Nile vitakauka; na kiburi cha Ashuru kitashushwa; na fimbo ya enzi ya Misri itatoweka.
12 Nami nitawatia nguvu katika Bwana; nao watatembea huko na huko katika jina lake, asema Bwana.

Zekaria 11


1 Ifungue milango yako, Ee Lebanoni, Ili moto uiteketeze mierezi yako.
2 Piga yowe, msunobari, maana mwerezi umeanguka, Kwa sababu miti iliyo mizuri imeharibika; Pigeni yowe, enyi mialoni ya Bashani, Kwa maana msitu wenye nguvu umeangamia.
3 Sauti ya wachungaji, ya uchungu mwingi! Kwa maana utukufu wao umeharibika; Sauti ya ngurumo ya wana-simba! Kwa maana kiburi cha Yordani kimeharibika.
4 Bwana, Mungu wangu, alisema hivi, Lilishe kundi la machinjo,
5 ambalo wenye kundi hilo huwachinja, kisha hujiona kuwa hawana hatia; na hao wawauzao husema, Na ahimidiwe Bwana, kwa maana mimi ni tajiri; na wachungaji wao wenyewe hawawahurumii.
6 Maana mimi sitawahurumia tena wenyeji wa nchi hii, asema Bwana; bali, tazama, nitawatia, kila mmoja wao, mikononi mwa mwenzake, na mikononi mwa mfalme; nao wataipiga hiyo nchi, wala mimi sitawaokoa mikononi mwao.
7 Basi nikalilisha kundi la machinjo, kweli kondoo waliokuwa wanyonge kabisa.
8 Nami nikawakatilia mbali wachungaji watatu katika mwezi mmoja; maana nafsi yangu ilikuwa imechoka kwa ajili yao, na nafsi zao pia walinichukia.
9 Ndipo nikasema, Sitawalisheni; afaye na afe; atakayekatiliwa mbali na akatiliwe mbali; nao waliosalia, kila mmoja na ale nyama ya mwili wa mwenziwe.
10 Nikaitwaa hiyo fimbo yangu, iitwayo Neema, nikaikata vipande viwili, ili nipate kulivunja agano langu nililolifanya na watu wa kabila zote.
11 Nayo ikavunjwa siku ile; na hivyo wale kondoo wanyonge walionisikiliza wakajua ya kuwa neno hili ndilo neno la Bwana.
12 Nikawaambia, Mkiona vema, nipeni ujira wangu; kama sivyo, msinipe. Basi wakanipimia vipande thelathini vya fedha, kuwa ndio ujira wangu.
13 Kisha Bwana akaniambia, Mtupie mfinyanzi kima kizuri, hicho nilichotiwa kima na watu hao. Basi nikavitwaa vile vipande thelathini vya fedha, nikamtupia huyo mfinyanzi ndani ya nyumba ya Bwana.
14 Ndipo nikaikata vipande viwili fimbo yangu ya pili, iitwayo Vifungo, ili nipate kuuvunja udugu uliokuwa kati ya Yuda na Israeli.
15 Bwana akaniambia, Jitwalie tena vyombo vya mchungaji mpumbavu.
16 Kwa maana, tazama, mimi nitainua katika nchi hii mchungaji, ambaye hatawaangalia waliopotea, wala hatawatafuta waliotawanyika, wala hatamganga aliyevunjika, wala hatamlisha aliye mzima; bali atakula nyama ya wanono, na kuzirarua-rarua kwato zao.
17 Ole wake mchungaji asiyefaa, aliachaye kundi! Upanga utakuwa juu ya mkono wake, na juu ya jicho lake la kuume; mkono wake utakuwa umekauka kabisa, na jicho lake la kuume litakuwa limepofuka.

Zekaria 12


1 Ufunuo wa neno la Bwana juu ya Israeli. Haya ndiyo asemayo Bwana, azitandaye mbingu, auwekaye msingi wa dunia, aiumbaye roho ya mwanadamu ndani yake.
2 Angalia, mimi nitafanya Yerusalemu kuwa kikombe cha kuyumba-yumba kwa watu wa kabila zote, wazungukao pande zote; tena kitakuwa juu ya Yuda pia wakati wa kuhusuriwa Yerusalemu.
3 Tena itakuwa siku hiyo, nitafanya Yerusalemu kuwa jiwe la kuwalemea watu wa kabila zote; wote watakaojitwika jiwe hilo watapata jeraha nyingi; na mataifa yote ya dunia watakusanyika pamoja juu yake.
4 Katika siku hiyo, asema Bwana, nitamtia kila farasi ushangao, na yeye ampandaye nitamtia wazimu; nami nitaifunulia nyumba ya Yuda macho yangu, nami nitamtia upofu kila farasi wa hizo kabila za watu.
5 Na wakuu wa Yuda watasema mioyoni mwao, Wenyeji wa Yerusalemu ni nguvu zangu katika Bwana wa majeshi, Mungu wao.
6 Siku hiyo nitawafanya wakuu wa Yuda kuwa kama kigae chenye moto katika kuni, na kama kinga cha moto katika miganda; nao watateketeza watu wa kila kabila, wawazungukao pande zote, upande wa mkono wa kuume na upande wa mkono wa kushoto; na baada ya haya Yerusalemu utakaa mahali pake, naam, hapo Yerusalemu.
7 Naye Bwana ataziokoa hema za Yuda kwanza, ili utukufu wa nyumba ya Daudi, na utukufu wa wenyeji wa Yerusalemu, usipate kutukuzwa kuliko Yuda.
8 Katika siku hiyo Bwana atawalinda wenyeji wa Yerusalemu; na yeye aliye dhaifu miongoni mwao atakuwa kama Daudi siku hiyo; nayo nyumba ya Daudi itakuwa kama Mungu, kama malaika wa Bwana mbele yao.
9 Hata itakuwa siku hiyo, ya kwamba nitatafuta kuwaangamiza mataifa yote watakaokuja kupigana na Yerusalemu.
10 Nami nitawamwagia watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, roho ya neema na kuomba; nao watamtazama yeye ambaye walimchoma; nao watamwombolezea, kama vile mtu amwombolezeavyo mwanawe wa pekee; nao wataona uchungu kwa ajili yake, kama vile mtu aonavyo uchungu kwa ajili ya mzaliwa wake wa kwanza.
11 Siku hiyo kutakuwa na maombolezo makuu huko Yerusalemu, kama maombolezo ya Hadadrimoni katika bonde la Megido.
12 Nayo nchi itaomboleza, kila jamaa peke yake; jamaa ya nyumba ya Daudi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Nathani peke yao, na wake zao peke yao;
13 jamaa ya nyumba ya Lawi peke yao, na wake zao peke yao; jamaa ya nyumba ya Shimei peke yao, na wake zao peke yao.
14 Jamaa zote zilizosalia, kila jamaa peke yake, na wake zao peke yao.

Zekaria 13


1 Katika siku hiyo watu wa nyumba ya Daudi, na wenyeji wa Yerusalemu, watafunguliwa chemchemi kwa dhambi na kwa unajisi.
2 Kisha itakuwa katika siku hiyo, asema Bwana wa majeshi, nitakatilia mbali majina ya sanamu katika nchi, yasikumbukwe tena; pia nitawafukuza manabii, na roho ya uchafu, watoke katika nchi.
3 Tena itakuwa ya kwamba, mtu awaye yote atakapotoa unabii, basi baba yake na mama yake waliomzaa watamwambia, Hutaishi; kwa maana unanena maneno ya uongo kwa jina la Bwana; na baba yake na mama yake waliomzaa watamtumbua atoapo unabii.
4 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba manabii, kila mmoja wao, atayaonea haya maono yake atoapo unabii; wala hawatavaa joho ya nywele ili kudanganya watu;
5 bali atasema, Mimi si nabii kamwe; mimi ni mkulima wa nchi; kwa maana nalifanywa mtumwa tokea ujana wangu.
6 Na mtu atamwambia, Je! Jeraha hizi ulizo nazo kati ya mikono yako ni nini? Naye atajibu, Ni jeraha nilizotiwa katika nyumba ya rafiki zangu.
7 Amka, Ee upanga, juu ya mchungaji wangu, na juu ya mtu aliye mwenzangu, asema Bwana wa majeshi; mpige mchungaji, nao kondoo watatawanyika; nami nitaugeuza mkono wangu juu ya wadogo.
8 Hata itakuwa, ya kwamba katika nchi yote mafungu mawili yatakatiliwa mbali, nao watakufa, asema Bwana; lakini fungu la tatu litabaki humo.
9 Nami nitalileta fungu lile la tatu na kulipitisha kati ya moto, nami nitawasafisha kama fedha isafishwavyo, nami nitawajaribu kama dhahabu ijaribiwavyo; wataliitia jina langu, nami nitawasikia; mimi nitasema, Watu hawa ndio wangu; nao watasema, Bwana ndiye Mungu wangu.

Zekaria 14


1 Tazama, siku moja ya Bwana inakuja, ambayo mateka yatagawanyika kati yako.
2 Kwa maana nitawakusanya mataifa yote walete vita juu ya Yerusalemu; na huo mji utapigwa, nazo nyumba zitatekwa, nao wanawake watatendwa jeuri; na nusu ya watu wa mji watatoka kwenda utumwani; ila mabaki ya watu wa mji hawatakatiliwa mbali.
3 Hapo ndipo atakapotokea Bwana, naye atapigana na mataifa hayo, kama vile alipopigana zamani siku ya vita.
4 Na siku hiyo miguu yake itasimama juu ya mlima wa Mizeituni, unaoelekea Yerusalemu upande wa mashariki, nao mlima wa Mizeituni utapasuka katikati yake, upande wa mashariki na upande wa magharibi; litakuwako huko bonde kubwa sana; na nusu ya mlima ule utaondoka kwenda upande wa kaskazini, na nusu yake itaondoka kwenda upande wa kusini.
5 Nanyi mtakimbia kwa njia ya bonde la milima yangu; kwa maana bonde lile la milima litaenea hata Aseli; naam, mtakimbia, kama vile mlivyokimbia mbele ya tetemeko la nchi, siku za Uzia, mfalme wa Yuda; na Bwana, Mungu wangu, atakuja, na watakatifu wote pamoja naye.
6 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba nuru yake haitakuwa na mwangaza na kiwi;
7 lakini itakuwa siku moja, iliyojulikana na Bwana; si mchana, wala si usiku; lakini itakuwa, ya kwamba wakati wa jioni kutakuwako nuru.
8 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba maji yaliyo hai yatatoka katika Yerusalemu; nusu yake itakwenda upande wa bahari ya mashariki, na nusu yake upande wa bahari ya magharibi; wakati wa hari na wakati wa baridi itakuwa hivi.
9 Naye Bwana atakuwa Mfalme juu ya nchi yote; siku hiyo Bwana atakuwa mmoja, na jina lake moja.
10 Nchi yote itageuzwa kuwa kama Araba, toka Geba mpaka Rimoni upande wa kusini wa Yerusalemu; naye atainuliwa juu, atakaa mahali pake mwenyewe, toka lango la Benyamini mpaka mahali pa lango la kwanza, mpaka lango la pembeni; tena toka mnara wa Hananeli mpaka mashinikizo ya mfalme.
11 Na watu watakaa ndani yake, wala hakutakuwako laana tena; lakini Yerusalemu utakaa salama.
12 Na hii ndiyo tauni, ambayo Bwana atawapiga watu wote waliofanya vita juu ya Yerusalemu; nyama ya mwili wao itaharibika, wasimamapo juu ya miguu yao, na macho yao yataharibika ndani ya vichwa vyao, na ndimi zao zitaharibika vinywani mwao.
13 Tena itakuwa siku hiyo, ya kwamba mashaka makubwa yatokayo kwa Bwana yatakuwa kati yao; na kila mmoja wao atakamata mkono wa jirani yake, na mkono wake utainuliwa ili kushindana na mkono wa jirani yake.
14 Yuda naye atafanya vita juu ya Yerusalemu; na huo utajiri wa mataifa wa pande zote utakusanyika, dhahabu, na fedha, na mavazi; vitu vingi sana.
15 Na hivyo ndivyo itakavyokuwa tauni ya farasi, na nyumbu, na ngamia, na punda, na ya hao wanyama wote watakaokuwamo matuoni mle, kama tauni hiyo.
16 Hata itakuwa, ya kwamba kila mtu aliyesalia wa mataifa yote, waliokuja kupigana na Yerusalemu, atakwea mwaka baada ya mwaka ili kumwabudu Mfalme, Bwana wa majeshi, na kuishika sikukuu ya Vibanda.
17 Tena itakuwa, ya kwamba mtu awaye yote wa jamaa zote zilizomo duniani, asiyekwea kwenda Yerusalemu ili kumwabudu Mfalme, Bwana wa majeshi, mvua haitanyesha kwao.
18 Na kama jamaa ya Misri hawakwei, wala hawaji, pia haitanyesha kwao; itakuwako tauni, ambayo Bwana atawapiga mataifa, wasiokwea ili kushika sikukuu ya Vibanda.
19 Hii ndiyo adhabu ya Misri, na adhabu ya mataifa yote, wasiokwea ili kushika sikukuu ya Vibanda.
20 Siku hiyo katika njuga za farasi yataandikwa maneno haya, WATAKATIFU KWA Bwana; navyo vyombo vilivyomo ndani ya nyumba ya Bwana vitakuwa kama mabakuli yaliyoko mbele ya madhabahu.
21 Naam, kila chombo katika Yerusalemu, na katika Yuda, kitakuwa kitakatifu kwa Bwana wa majeshi; nao wote watoao dhabihu watakuja kuvitwaa vile vyombo, na kutokosa nyama ndani yake; wala siku hiyo hatakuwamo tena mfanya biashara ndani ya nyumba ya Bwana wa majeshi.