Hagai

Sura: 1, 2

Hagai 1


1 Katika mwaka wa pili wa Dario mfalme, mwezi wa sita, siku ya kwanza ya mwezi, neno la Bwana lilimjia Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, kwa kinywa chake Hagai nabii, kusema,
2 Bwana wa majeshi asema hivi, ya kwamba, Watu hawa husema, Huu sio wakati utupasao kuja, huu sio wakati wa kujenga nyumba ya Bwana.
3 Ndipo neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha nabii Hagai, kusema,
4 Je! Huu ndio wakati wa ninyi kukaa katika nyumba zenye mapambo ya mbao, iwapo nyumba hii inakaa hali ya kuharibika?
5 Basi sasa, Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.
6 Mmepanda mbegu nyingi mkavuna kidogo; mnakula lakini hamshibi; mnakunywa lakini hamkujazwa na vinywaji; mnajivika nguo lakini hapana aonaye moto; na yeye apataye mshahara apata mshahara ili kuutia katika mfuko uliotoboka-toboka.
7 Bwana wa majeshi asema hivi, Zitafakarini njia zenu.
8 Pandeni milimani, mkalete miti, mkaijenge nyumba; nami nitaifurahia, nami nitatukuzwa, asema Bwana.
9 Mlitazamia vingi, kumbe vikatokea vichache; tena mlipovileta nyumbani nikavipeperusha. Ni kwa sababu gani? Asema Bwana wa majeshi. Ni kwa sababu ya nyumba yangu inayokaa hali ya kuharibika, wakati ambapo ninyi mnakimbilia kila mtu nyumbani kwake.
10 Basi, kwa ajili yenu mbingu zimezuiliwa zisitoe umande, nayo nchi imezuiliwa isitoe matunda yake.
11 Nami nikaita wakati wa joto uje juu ya nchi, na juu ya milima, na juu ya nafaka, na juu ya divai mpya, na juu ya mafuta, na juu ya kila kitu itoacho nchi, na juu ya wanadamu, na juu ya wanyama, na juu ya kazi zote za mikono.
12 Ndipo Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, pamoja na hayo mabaki yote ya watu, wakaitii sauti ya Bwana, Mungu wao, na maneno ya Hagai nabii, kama Bwana, Mungu wao, alivyomtuma; nao watu wakaogopa mbele za Bwana.
13 Ndipo Hagai mjumbe wa Bwana, katika ujumbe wa Bwana, akawaambia watu, akisema, Mimi nipo pamoja nanyi, asema Bwana.
14 Bwana akaiamsha roho ya Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na roho ya Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na roho zao mabaki ya watu; wakaenda, wakafanya kazi katika nyumba ya Bwana wa majeshi, Mungu wao;
15 katika siku ya ishirini na nne ya mwezi, katika mwezi wa sita, katika mwaka wa pili wa Dario mfalme.

Hagai 2


1 Katika mwezi wa saba, siku ya ishirini na moja ya mwezi, neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha Hagai nabii, kusema,
2 Sema sasa na Zerubabeli, mwana wa Shealtieli, liwali wa Yuda, na Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, na hayo mabaki ya watu, ukisema,
3 Miongoni mwenu amebaki nani aliyeiona nyumba hii katika utukufu wake wa kwanza? Nanyi mnaionaje sasa? Je! Mbele ya macho yenu, siyo kama si kitu?
4 Lakini sasa uwe hodari, Ee Zerubabeli, asema Bwana; nawe uwe hodari, Ee Yoshua, mwana wa Yehosadaki, kuhani mkuu, nanyi iweni hodari, enyi watu wote wa nchi hii, asema Bwana; mkafanye kazi, kwa kuwa mimi ni pamoja nanyi, asema Bwana wa majeshi;
5 kama neno lile nililoagana nanyi mlipotoka katika nchi ya Misri; na roho yangu inakaa kati yenu; msiogope.
6 Kwa maana Bwana wa majeshi asema hivi, Mara moja tena, ni kitambo kidogo tu, nami nitazitikisa hizo mbingu, na hii nchi, na bahari, na nchi kavu;
7 nami nitatikisa mataifa yote, na vitu vinavyotamaniwa na mataifa yote vitakuja; nami nitaijaza nyumba hii utukufu, asema Bwana wa majeshi.
8 Fedha ni mali yangu, na dhahabu ni mali yangu, asema Bwana wa majeshi.
9 Utukufu wa mwisho wa nyumba hii utakuwa mkuu kuliko utukufu wake wa kwanza, asema Bwana wa majeshi; na katika mahali hapa nitawapa amani, asema Bwana wa majeshi.
10 Siku ya ishirini na nne, ya mwezi wa kenda, katika mwaka wa pili wa Dario, neno la Bwana lilikuja kwa kinywa cha Hagai nabii, kusema,
11 Bwana wa majeshi asema hivi, Waulizeni sasa makuhani katika habari ya sheria, mkisema,
12 Mtu akichukua nyama takatifu katika upindo wa nguo yake, naye akagusa kwa upindo wake mkate, au ugali, au divai, au mafuta, au chakula cho chote, je! Kitu hicho kitakuwa kitakatifu? Makuhani wakajibu, wakasema, La.
13 Ndipo Hagai akasema, Kama mtu aliyetiwa unajisi kwa kugusa maiti, akigusa kimojawapo cha vitu hivi, je! Kitakuwa najisi? Makuhani wakajibu, wakasema, Kitakuwa najisi.
14 Ndipo Hagai akajibu, akasema, Hivyo ndivyo walivyo watu hawa, na hivyo ndivyo lilivyo taifa hili mbele zangu, asema Bwana; na hivyo ndivyo ilivyo kila kazi ya mikono yao; na kitu hicho wakitoacho sadaka huko ni najisi.
15 Na sasa nawaomba, tafakarini; tangu siku hii na siku zilizopita; kabla halijatiwa bado jiwe juu ya jiwe katika nyumba ya Bwana;
16 katika wakati huo wote, mtu alipofikia chungu ya vipimo ishirini, palikuwa na vipimo kumi tu; na mtu alipofikia shinikizo apate kuteka divai ya vyombo hamsini, palikuwa na divai ya vyombo ishirini tu.
17 Naliwapiga kwa ukavu, na ukungu, na mvua ya mawe, katika kazi zote za mikono yenu; lakini hamkunielekea mimi, asema Bwana.
18 Tafakarini, nawaomba; tangu siku hii ya leo na siku zijazo; tangu siku ya ishirini na nne ya mwezi wa kenda, naam, tangu siku hiyo ulipowekwa msingi wa hekalu la Bwana tafakarini haya.
19 Je! Mbegu ingali ghalani? Naam, huo mzabibu, wala mtini, wala mkomamanga, wala mzeituni, haikuzaa kitu; tangu siku hii ya leo nitawabariki.
20 Kisha neno la Bwana likamjia Hagai mara ya pili, siku ya ishirini na nne ya mwezi, kusema,
21 Sema na Zerubabeli, liwali wa Yuda, ukisema, Nitazitikisa mbingu na dunia;
22 nami nitakipindua kiti cha enzi cha falme, nami nitaziharibu nguvu za falme za mataifa; nami nitayapindua magari, na hao wapandao ndani yake; farasi na hao wawapandao wataanguka chini; kila mtu kwa upanga wa ndugu yake.
23 Katika siku ile, asema Bwana wa majeshi, nitakutwaa wewe, Ee Zerubabeli, mtumishi wangu, mwana wa Shealtieli, asema Bwana, nami nitakufanya kuwa kama pete yenye muhuri; kwa kuwa nimekuchagua, asema Bwana wa majeshi.