Habakuki

Sura: 1, 2, 3

Habakuki 1


1 Ufunuo aliouona nabii Habakuki.
2 Ee Bwana, nilie hata lini, wewe usitake kusikia? Nakulilia kwa sababu ya udhalimu, ila hutaki kuokoa.
3 Mbona wanionyesha uovu, na kunitazamisha ukaidi? Maana uharibifu na udhalimu u mbele yangu; kuna ugomvi, na mashindano yatokea.
4 Kwa sababu hiyo sheria imelegea, wala hukumu haipatikani; kwa maana watu wabaya huwazunguka wenye haki; kwa sababu hiyo hukumu ikipatikana imepotoka.
5 Angalieni, enyi mlio kati ya mataifa, katazameni, kastaajabuni sana; kwa maana mimi natenda tendo siku zenu, ambalo hamtaliamini hata mkiambiwa.
6 Kwa maana, angalieni, nawaondokesha Wakaldayo, taifa lile kali, lenye haraka kupita kiasi; wapitao katikati ya dunia, ili wayamiliki makao yasiyo yao.
7 Hao ni watu wa kutisha sana, wa kuogofya sana; hukumu yao na ukuu wao hutoka katika nafsi zao wenyewe.
8 Farasi zao ni wepesi kuliko chui, ni wakali kuliko mbwa-mwitu wa jioni; na wapanda farasi wao hujitapa naam, wapanda farasi wao watoka mbali sana; huruka kama tai afanyaye haraka ale.
9 Waja wote ili kufanya udhalimu; nyuso zao zimeelekezwa kwa bidii yao kama upepo wa mashariki, nao hukusanya mateka kama mchanga.
10 Naam, huwadhihaki wafalme, na wakuu ni kitu cha kudharauliwa kwake; huidharau kila ngome; kwa maana hufanya chungu ya mavumbi, na kuitwaa.
11 Kisha atapita kwa kasi, kama upepo, atapita na kuwa ana hatia; yeye ambaye nguvu zake ni mungu wake.
12 Ee Bwana, Mungu wangu, mtakatifu wangu, wewe si wa milele? Hatutakufa. Ee Bwana, umemwandikia hukumu, nawe, Ee Jabali, umemweka imara ili aadhibishwe.
13 Wewe uliye na macho safi hata usiweze kuangalia uovu, wewe usiyeweza kutazama ukaidi, mbona unawaangalia watendao kwa hila; na kunyamaza kimya, hapo mtu mwovu ammezapo mtu aliye mwenye haki kuliko yeye;
14 na kufanya wanadamu kuwa kama samaki wa baharini, kama vitu vitambaavyo, ambavyo havina mtawala?
15 Yeye huwatoa wote kwa ndoana yake, huwakamata katika wavu wake, na kuwakusanya katika juya lake; ndiyo sababu afurahi na kupendezwa.
16 Kwa sababu hiyo huutolea wavu wake sadaka, na kulifukizia uvumba juya lake; kwa sababu kwa vitu vile fungu lake limenona, na chakula chake kimekuwa tele.
17 Je! Atawatoa walio katika wavu wake, asiache kuwaua watu wa mataifa daima?

Habakuki 2


1 Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu.
2 Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji.
3 Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake, wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee; kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia.
4 Tazama, roho yake hujivuna, haina unyofu ndani yake; lakini mwenye haki ataishi kwa imani yake.
5 Naam, pamoja na hayo, divai ni mchumi mdanganyifu, mtu wa kiburi asiyekaa nyumbani mwake; huongeza tamaa yake kama kuzimu, naye huwa kama mauti, hawezi kushibishwa; bali hujikusanyia mataifa yote; hujiwekea kabila zote chungu chungu.
6 Je! Hawa wote hawatapiga mfano juu yake, na mithali ya kusimanga juu yake, wakisema, Ole wake yeye aongezaye kisicho mali yake! Hata lini? Na ole wake yeye ajitwikaye mzigo wa rehani!
7 Je! Hawatainuka ghafula wao watakaokuuma, hawataamka wao watakaokusumbua, nawe utakuwa mateka kwao?
8 Kwa sababu umeteka nyara mataifa mengi, mabaki yote ya kabila watakuteka wewe; kwa sababu ya damu ya watu, na kwa sababu ya udhalimu iliotendwa nchi hii, na mji huu, na watu wote wanaokaa ndani yake.
9 Ole wake yeye aipatiaye nyumba yake mapato mabaya, ili apate kukiweka kioto chake juu, apate kujiepusha na mkono wa uovu!
10 Wewe umeifanyia nyumba yako kusudi la aibu, kwa kukatilia mbali watu wengi, nawe umetenda dhambi juu ya roho yako.
11 Kwa maana jiwe litapiga kelele katika ukuta, nayo boriti katika miti italijibu.
12 Ole wake yeye ajengaye mji kwa damu, awekaye imara mji mkubwa kwa uovu!
13 Angalieni; je! Jambo hili halikutoka kwa Bwana wa majeshi, kwamba watu wajishughulikie moto, na mataifa wajisumbue kwa ajili ya ubatili?
14 Kwa maana dunia itajazwa maarifa ya utukufu wa Bwana, kama maji yaifunikavyo bahari.
15 Ole wake yeye ampaye jirani yake kileo, wewe utiaye sumu yako, na kumlevya pia, ili kuutazama uchi wao!
16 Umejaa aibu badala ya utukufu; unywe nawe, uwe kama mtu asiyetahiriwa; kikombe cha mkono wa kuume wa Bwana kitageuzwa ukipokee, na aibu kuu itakuwa juu ya utukufu wako.
17 Kwa maana udhalimu uliotendwa juu ya Lebanoni utakufunikiza, na kuangamizwa kwao wanyama kutakutia hofu; kwa sababu ya damu ya watu, na kwa sababu ya udhalimu iliotendwa nchi hii, na mji huu, na watu wote wanaokaa ndani yake.
18 Sanamu ya kuchora yafaa nini, hata yeye aliyeifanya ameichora? Sanamu ya kuyeyuka, nayo ni mwalimu wa uongo, yafaa nini, hata yeye aliyeifanya aiwekee tumaini lake, na kufanya sanamu zisizoweza kusema?
19 Ole wake yeye auambiaye mti, Amka; aliambiaye jiwe lisiloweza kusema, Ondoka! Je! Kitu hicho kitafundisha? Tazama, kimefunikwa kwa dhahabu na fedha, wala hamna pumzi ndani yake kabisa.
20 Lakini Bwana yumo ndani ya hekalu lake takatifu; dunia yote na inyamaze kimya mbele zake.

Habakuki 3


1 Sala ya nabii Habakuki.
2 Ee Bwana, nimesikia habari zako, nami naogopa; Ee Bwana, fufua kazi yako katikati ya miaka; Katikati ya miaka tangaza habari yake; Katika ghadhabu kumbuka rehema.
3 Mungu alikuja kutoka Temani, Yeye aliye mtakatifu kutoka mlima Parani. Utukufu wake ukazifunika mbingu, Nayo dunia ikajaa sifa yake.
4 Mwangaza wake ulikuwa kama nuru; Alikuwa na mishale ya nuru ubavuni pake; Ndipo ulipofichwa uweza wake.
5 Mbele zake ilikwenda tauni, Na makaa ya moto yakatoka miguuni pake.
6 Akasimama, akaitetemesha dunia; Akatazama, akawasitusha mataifa; Na milima ya zamani ikatawanyika; Vilima vya kale vikainama; Miendo yake ilikuwa kama siku za kale.
7 Naliziona hema za Kushani katika taabu; Mapazia ya nchi ya Midiani yakatetemeka.
8 Je! Bwana aliikasirikia mito? Je! Hasira yako ilikuwa juu ya mito, Au ghadhabu yako juu ya bahari, Hata ukapanda farasi zako, Katika magari yako ya wokovu?
9 Uta wako ukafanywa wazi kabisa; Viapo walivyopewa kabila vilikuwa neno thabiti; Ukaipasua nchi kwa mito.
10 Milima ilikuona, ikaogopa; Gharika ya maji ikapita; Vilindi vikatoa sauti yake, Vikainua juu mikono yake.
11 Jua na mwezi vikasimama makaoni mwao; Mbele ya nuru ya mishale yako ilipotapakaa, Mbele ya mwangaza wa mkuki wako umeremetao.
12 Ulikwenda katikati ya nchi kwa ghadhabu; Ukawapura mataifa kwa hasira.
13 Ukatokea kwa ajili ya wokovu wa watu wako, Kwa ajili ya wokovu wa masihi wako; Ukakiponda kichwa cha nyumba ya waovu, Ukiuweka wazi msingi hata mwambani.
14 Ukakichoma kichwa cha mashujaa wake kwa fimbo zao wenyewe; Wakaja kama kisulisuli ili kunitawanya; Kama wakifurahi kuwameza maskini kwa siri.
15 Ukaikanyaga bahari kwa farasi zako, Chungu ya maji yenye nguvu.
16 Nikasikia, na tumbo langu likatetemeka, Midomo yangu ikatikisika kwa sauti ile; Ubovu ukaingia mifupani mwangu, Nikatetemeka katika mahali pangu; Ili nipate kuingoja ile siku ya dhiki, Kundi lao washambuliao wakweapo juu ya watu.
17 Maana mtini hautachanua maua, Wala mizabibuni hamtakuwa na matunda; Taabu ya mzeituni itakuwa bure, Na mashamba hayatatoa chakula; Zizini hamtakuwa na kundi, Wala vibandani hamtakuwa na kundi la ng'ombe;
18 Walakini nitamfurahia Bwana Nitamshangilia Mungu wa wokovu wangu.
19 YEHOVA, aliye Bwana, ni nguvu zangu, Yeye huifanya miguu yangu kuwa kama ya kulungu, Naye ataniendesha katika mahali pangu palipoinuka.