Yeremia

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24, 25, 26, 27, 28, 29, 30, 31, 32, 33, 34, 35, 36, 37, 38, 39, 40, 41, 42, 43, 44, 45, 46, 47, 48, 49, 50, 51, 52

Yeremia 1


1 Maneno ya Yeremia, mwana wa Hilkia, mmoja wa makuhani waliokuwa katika Anathothi, katika nchi ya Benyamini;
2 ambaye neno la Bwana lilimjia katika siku za Yosia, mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda, katika mwaka wa kumi na tatu wa kumiliki kwake.
3 Tena lilikuja siku za Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, hata mwisho wa mwaka wa kumi na mmoja wa Sedekia, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; hata wakati ulipochukuliwa mateka Yerusalemu, katika mwezi wa tano.
4 Neno la Bwana lilinijia, kusema,
5 Kabla sijakuumba katika tumbo nalikujua, na kabla hujatoka tumboni, nalikutakasa; nimekuweka kuwa nabii wa mataifa.
6 Ndipo niliposema, Aa, Bwana MUNGU! Tazama, siwezi kusema; maana mimi ni mtoto.
7 Lakini Bwana akaniambia, Usiseme, Mimi ni mtoto; maana utakwenda kwa kila mtu nitakayekutuma kwake, nawe utasema kila neno nitakalokuamuru.
8 Usiogope kwa sababu ya hao maana mimi nipo pamoja nawe nikuokoe, asema Bwana.
9 Ndipo Bwana akaunyosha mkono wake, akanigusa kinywa changu; Bwana akaniambia, Tazama, nimetia maneno yangu kinywani mwako;
10 angalia, nimekuweka leo juu ya mataifa na juu ya falme, ili kung'oa, na kubomoa, na kuharibu, na kuangamiza; ili kujenga na kupanda.
11 Tena neno la Bwana likanijia, kusema, Yeremia, waona nini? Nikasema, Naona ufito wa mlozi.
12 Ndipo Bwana akaniambia, Umeona vema, kwa maana ninaliangalia neno langu, ili nilitimize.
13 Neno la Bwana likanijia mara ya pili, kusema, Waona nini? Nikasema, Naona sufuria lenye maji yatokotayo, na mdomo wake unaelekea toka upande wa kaskazini.
14 Ndipo Bwana akaniambia, Toka kaskazini mabaya yatatokea, na kuwapata watu wote wakaao katika nchi hii.
15 Kwa kuwa, tazama, nitaziita jamaa zote za falme za kaskazini, asema Bwana; nao watakuja, na kuweka kila mtu kiti chake cha enzi mbele ya mahali pa kuingilia malango ya Yerusalemu, na kuzielekea kuta zake pande zote, na kuielekea miji yote ya Yuda.
16 Nami nitatamka hukumu zangu juu yao kwa habari ya uovu wao wote; kwa kuwa wameniacha mimi, wakaifukizia uvumba miungu mingine, wakaziabudu kazi za mikono yao wenyewe.
17 Haya basi, wewe jifunge viuno, ukaondoke ukawaambie maneno yote niliyokuamuru; usifadhaike kwa ajili yao, nisije nikakufadhaisha wewe mbele yao.
18 Maana, tazama, nimekufanya leo kuwa mji wenye boma, na nguzo ya chuma, na kuta za shaba, juu ya nchi yote; juu ya wafalme wa Yuda, na juu ya wakuu wake, na juu ya makuhani wake, na juu ya watu wa nchi hii.
19 Nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, asema Bwana, ili nikuokoe.

Yeremia 2


1 Neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Enenda ukalie masikioni mwa Yerusalemu, ukisema, Bwana asema hivi, Nakukumbuka, hisani ya ujana wako, upendo wa wakati wa uposo wako; Jinsi ulivyonifuata huko jangwani, katika nchi isiyopandwa mbegu.
3 Israeli walikuwa utakatifu kwa Bwana; malimbuko ya uzao wake; Wote watakaomla watakuwa na hatia; uovu utawajilia; asema Bwana.
4 Lisikieni neno la Bwana, ninyi nyumba ya Yakobo, na ninyi, jamaa zote za nyumba ya Israeli.
5 Bwana asema hivi, Baba zenu waliona dhuluma gani kwangu, hata wakafarakana nami, wakafuata ubatili, nao wakawa ubatili?
6 Wala hawakusema, Yuko wapi Bwana, aliyetutoa katika nchi ya Misri; akatuongoza jangwani, katika nchi ya ukame na mashimo, katika nchi ya kiu na ya kivuli cha mauti, katika nchi ambayo ndani yake hapiti mtu, wala haikukaliwa na watu?
7 Nami nikawatia katika nchi ya shibe, mpate kula matunda yake na mema yake; lakini ninyi mlipoingia katika nchi ile, mliitia unajisi nchi yangu, na urithi wangu mliufanya kuwa chukizo.
8 Makuhani hawakusema, Yuko wapi Bwana? Wala wana-sheria hawakunijua; wachungaji nao waliniasi, nao manabii walitoa unabii kwa Baali, wakafuata mambo yasiyofaidia kitu.
9 Basi, kwa ajili ya hayo nitateta nanyi, asema Bwana, nami nitateta na watoto wa watoto wenu.
10 Maana, vukeni mpaka visiwa vya Kitimu, mkaone; tumeni watu waende Kedari, mkafikiri sana; mkaone kwamba jambo kama hili limekuwa wakati wo wote.
11 Je! Taifa wamebadili miungu yao, ingawa siyo miungu? Lakini watu wangu wameubadili utukufu wao kwa ajili ya kitu kisichofaidia.
12 Enyi mbingu, staajabuni kwa ajili ya jambo hili, mkaogope sana, na kuwa ukiwa sana, asema Bwana.
13 Kwa maana watu wangu hawa wametenda maovu mawili; wameniacha mimi, niliye chemchemi ya maji ya uzima, wamejichimbia mabirika, mabirika yavujayo, yasiyoweza kuweka maji.
14 Je! Israeli ni mtumwa? Je! Ni mzalia? mbona amekuwa mateka?
15 Wana-simba wamenguruma juu yake, wametoa sana sauti zao; Nao wameifanya nchi yake kuwa ukiwa; miji yake imeteketea, haina watu.
16 Tena wana wa Nofu na Tahpanesi wamevunja utosi wa kichwa chako.
17 Je! Hukujipatia mambo haya mwenyewe, kwa kuwa umemwacha Bwana, Mungu wako, alipokuongoza njiani?
18 Na sasa una nini utakayotenda katika njia iendayo Misri, kunywa maji ya Shihori? Au una nini utakayotenda katika njia iendayo Ashuru, kunywa maji ya ule Mto?
19 Uovu wako mwenyewe utakurudi, maasi yako yatakukaripia; ujue, basi, ukaone, ya kuwa ni jambo baya sana na uchungu, kuwa umemwacha Bwana, Mungu wako, na ya kuwa moyoni mwako hamna kunihofu, asema Bwana, Bwana wa majeshi.
20 Kwa maana tangu zamani wewe umeivunja nira yako, na kuvipasua vifungo vyako; ukasema, Mimi sitatumika; kwa maana juu ya kila kilima kirefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi, umejiinamisha, ukafanya mambo ya ukahaba.
21 Nami nalikuwa nimekupanda, mzabibu mwema sana, mbegu nzuri kabisa; umegeukaje, basi, kuwa mche usiofaa wa mzabibu-mwitu machoni pangu?
22 Maana ujapojiosha kwa magadi, na kujipatia sabuni nyingi, lakini uovu wako umeandikwa mbele zangu, asema Bwana MUNGU.
23 Wawezaje kusema, Sikutiwa unajisi, sikuwafuata Mabaali? Itazame njia yako bondeni, ujue uliyoyatenda; wewe u ngamia mwepesi, apitaye katika njia zake;
24 punda wa mwitu aliyeizoelea nyika, avutaye pumzi za upepo katika tamaa yake; katika wakati wake ni nani awezaye kumgeuza? Wote wamtafutao hawatajichokesha nafsi zao; katika mwezi wake watamwona.
25 Zuia mguu wako usikose kiatu, na koo yako isiwe na kiu; lakini wewe ulisema, Hapana matumaini kabisa; la, maana nimewapenda wageni, nami nitawafuata.
26 Kama mwivi aonavyo haya akamatwapo, ndivyo waonavyo haya nyumba ya Israeli; wao, na wafalme wao, na wakuu wao, na makuhani wao, na manabii wao;
27 waliambiao gogo la mti, Wewe u baba yangu; na kuliambia jiwe, Ndiwe uliyenizaa; kwa maana wamenipa mimi visogo, wala hawakunielekezea nyuso zao; lakini wakati wa taabu watasema, Simama ukatuokoe.
28 Lakini wako wapi miungu yako ulioifanya? Na wasimame hao, kama wakiweza kukuokoa wakati wa taabu yako; kwa maana hesabu ya miungu yako ni sawasawa na hesabu ya miji yako, Ee Yuda.
29 Mbona mnataka kuteta nami? Ninyi nyote mmeniasi, asema Bwana.
30 Nimewapiga watoto wako bure; hawakukubali kurudiwa; upanga wenu wenyewe umewala manabii wako, kama simba aharibuye.
31 Ee kizazi litazameni neno la Bwana. Je! Nimekuwa jangwa kwa Israeli? Au nchi yenye giza kuu? Mbona watu wangu wanasema, Sisi tumetoroka, hatutaki kuja kwako tena?
32 Je! Mwanamwali aweza kusahau mapambo yake, au bibi arusi mavazi yake? Lakini watu wangu wamenisahau mimi kwa muda wa siku zisizo na hesabu.
33 Jinsi ulivyoitengeneza njia yako ili kutafuta mapenzi! Kwa sababu hiyo hata wanawake wabaya umewafundisha njia zako.
34 Tena katika pindo za nguo zako imeonekana damu ya roho zao maskini wasio na hatia; sikuiona penye mahali palipobomoka, lakini naliiona juu ya hawa wote.
35 Lakini ulisema, Sina hatia mimi; bila shaka hasira yake imegeuka na kuniacha. Tazama, nitaingia hukumuni pamoja nawe, kwa sababu unasema, Sikutenda dhambi mimi.
36 Mbona unatanga-tanga hivi upate kugeuza mwendo wako? Utaona haya kwa ajili ya Misri pia, kama ulivyoona haya kwa ajili ya Ashuru.
37 Hata kwake pia utatoka, na mikono yako juu ya kichwa chako; kwa maana Bwana amewakataa uliowakimbilia, wala hutafanikiwa katika hao.

Yeremia 3


1 Watu husema, Mtu akimwacha mkewe, naye akienda zake, akawa mke wa mtu mwingine, je! Mtu huyo atamrudia tena? Je! Nchi hiyo haitatiwa unajisi? Lakini wewe umefanya mambo ya ukahaba na wapenzi wengi; nawe, je! Utanirudia mimi? Asema Bwana.
2 Inua macho yako, ukavitazame vilele vya milima, ukaone; pa wapi mahali ambapo hawakulala nawe? Kando ya njia umeketi ili kuwangojea, kama vile Mwarabu jangwani; nawe umeitia nchi unajisi kwa ukahaba wako na uovu wako.
3 Kwa sababu hiyo manyunyu yamezuiliwa, wala hapakuwa na mvua ya vuli; hata hivyo ulikuwa na kipaji cha uso cha kahaba, ulikataa kutahayarika.
4 Je, tokea wakati huu hutanililia, Ee Baba yangu, wewe u kiongozi wa ujana wangu?
5 Je! Ataishika hasira yake hata milele? Ataishika hata mwisho? Tazama, umesema hivyo, bali umetenda mambo mabaya, umefuata njia yako mwenyewe.
6 Tena, Bwana akaniambia siku za mfalme Yosia, Je! Umeyaona aliyotenda Israeli mwenye kuasi? Amepanda juu ya kila mlima mrefu, akafanya huko mambo ya ukahaba, tena, chini ya kila mti wenye majani mabichi.
7 Nami nalisema baada ya yeye kuyatenda hayo yote, Atanirudia mimi, lakini hakurudi; na dada yake, Yuda mwenye hiana, akayaona hayo.
8 Nami nikaona, wakati nilipokuwa nimemwacha Israeli mwenye kuasi, nikampa hati ya talaka kwa sababu hiyo ya kuzini, dada yake, Yuda mwenye hiana, hakufanya hofu; bali yeye naye akaenda akafanya mambo ya ukahaba.
9 Hata ikawa, kwa sababu alikuwa mwepesi wa kufanya ukahaba, nchi ikatiwa unajisi, naye akazini na mawe na miti.
10 Na pamoja na hayo yote dada yake, Yuda mwenye hiana, hajanirudia mimi kwa moyo wake wote, bali kwa unafiki, asema Bwana.
11 Bwana, akaniambia, Israeli mwenye kuasi amejionyesha kuwa mwenye haki kuliko Yuda mwenye hiana.
12 Enenda, ukatangaze maneno haya kuelekea upande wa kaskazini, ukaseme, Rudi, Ee Israeli mwenye kuasi, asema Bwana; sitakutazama kwa hasira; maana mimi ni mwenye rehema, asema Bwana, sitashika hasira hata milele.
13 Ungama uovu wako tu; ya kwamba umemwasi Bwana, Mungu wako, na njia zako zimekuwa nyingi kuwaendea wageni chini ya kila mti wenye majani mabichi, wala hamkuitii sauti yangu, asema Bwana.
14 Rudini, enyi watoto wenye kuasi, asema Bwana; maana mimi ni mume wenu; nami nitatwaa mtu mmoja wa mji mmoja, na wawili wa jamaa moja, nami nitawaleta hata Sayuni;
15 nami nitawapa ninyi wachungaji wanipendezao moyo wangu, watakaowalisha kwa maarifa na fahamu.
16 Kisha itakuwa, mtakapoongezeka na kuwa wengi katika nchi hiyo, asema Bwana, siku zile hawatasema tena, Sanduku la agano la Bwana; wala halitaingia moyoni; wala hawatalikumbuka, wala hawatalizuru, wala hayatafanyika hayo tena.
17 Wakati ule watauita Yerusalemu kiti cha enzi cha Bwana; na mataifa yote watakusanyika huko Yerusalemu, kwa ajili ya jina la Bwana; wala hawatakwenda tena kwa ukaidi wa moyo wao mbaya.
18 Siku zile nyumba ya Yuda watakwenda pamoja na nyumba ya Israeli, nao watakuja pamoja, kutoka nchi ya kaskazini, mpaka nchi ile niliyowapa baba zenu iwe urithi wao.
19 Lakini mimi nalisema, Nitawezaje kukuweka pamoja na watoto, na kukupa nchi ipendezayo, urithi ulio mwema wa mataifa? Nami nikasema, Mtaniita, Baba yangu, wala hamtageuka na kuacha kunifuata.
20 Hakika kama vile mke amwachavyo mumewe kwa hiana, ndivyo mlivyonitenda mimi kwa hiana, Ee nyumba ya Israeli, asema Bwana.
21 Sauti inasikiwa juu ya vilele vya milima, ni kulia kwao na maombi yao wana wa Israeli; kwa kuwa wameipotosha njia yao, wamemsahau Bwana, Mungu wao.
22 Rudini, enyi watoto waasi, mimi nitaponya maasi yenu. Tazama, tumekuja kwako; maana wewe u Bwana, Mungu wetu.
23 Ni kweli, msaada haufai unaotazamiwa kutoka milimani, makutano yenye mshindo juu ya milima; ni kweli, wokovu wa Israeli ni katika Bwana, Mungu wetu.
24 Lakini kitu cha aibu kimeila kazi ya baba zetu tokea ujana wetu; makundi yao ya kondoo na ng'ombe, wana wao na binti zao.
25 Na tulale kwa aibu yetu, haya yetu na itufunike; kwa maana tumemwasi Bwana, Mungu wetu, sisi na baba zetu, tangu ujana wetu hata leo; wala hatukuitii sauti ya Bwana, Mungu wetu.

Yeremia 4


1 Kama ukitaka kurudi, Ee Israeli, asema Bwana, utanirudia mimi; na kama ukitaka kuyaondoa machukizo yako, yasiwe mbele ya macho yangu, ndipo hutaondolewa;
2 nawe utaapa hivi, Kama Bwana aishivyo, katika kweli, na katika hukumu, na katika haki ndipo mataifa watajibariki katika yeye, nao watajitukuza katika yeye.
3 Maana Bwana awaambia hivi watu wa Yuda na Yerusalemu Ulimeni udongo katika konde zenu, wala msipande mbegu kati ya miiba.
4 Jitahirini kwa Bwana, mkaziondoe govi za mioyo yenu, enyi watu wa Yuda na wenyeji wa Yerusalemu; ghadhabu yangu isije ikatoka kama moto, ikawaka hata mtu asiweze kuizima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu.
5 Tangazeni katika Yuda, hubirini katika Yerusalemu, na kusema, Pigeni baragumu katika nchi, pigeni kelele sana, na kusema, Jikusanyeni pamoja, tukaingie katika miji yenye boma.
6 Twekeni bendera kuelekea Sayuni; kimbieni mpate kuwa salama, msikawie; kwa maana nitaleta mabaya toka kaskazini, na maangamivu makuu.
7 Simba ametoka katika kichaka chake, ndiye aangamizaye mataifa; ameanza kushika njia, ametoka katika mahali pake; ili aifanye nchi yako kuwa ukiwa, miji yako ifanywe maganjo, asibaki mwenyeji ndani yake.
8 Kwa sababu hiyo jifungeni nguo za magunia; ombolezeni na kulia kwa uchungu; kwa maana hasira kali ya Bwana haikugeuka na kutuacha.
9 Na katika siku hiyo itakuwa, asema Bwana, moyo wa mfalme utapotea, na moyo wa wakuu wake; na makuhani watastaajabu, na manabii watashangaa.
10 Nami nikasema, Aa, Bwana MUNGU! Hakika umewadanganya sana watu hawa na Yerusalemu, ukisema, Mtakuwa na amani lakini upanga umeingia katika nafsi za watu.
11 Wakati ule watu hawa na Yerusalemu wataambiwa neno hili, Upepo wa moto utokao katika vilele vya nyikani visivyo na miti, ukimwelekea binti ya watu wangu, hauwi upepo wa kupepeta, wala upepo wa kutakasa;
12 ni upepo wa nguvu kuliko hizo utakaokuja kwa ajili yangu; sasa mimi nitatoa hukumu juu yao.
13 Tazama atapanda juu kama mawingu, na magari yake ya vita yatakuwa kama kisulisuli; farasi zake ni wepesi kuliko tai. Ole wetu, kwa sababu tumeharibika.
14 Ee Yerusalemu, jioshe moyo wako usiwe na uovu, upate kuokoka. Mawazo yako mabaya yatakaa ndani yako hata lini?
15 Maana sauti yatangaza habari toka Dani, yahubiri uovu toka vilima vya Efraimu;
16 Wapasheni mataifa habari; angalieni, hubirini juu ya Yerusalemu, ya kwamba walinzi wanatoka katika nchi ya mbali, wanatoa sauti yao juu ya miji ya Yuda.
17 Kama watu walindao shamba, wameuzunguka wauhusuru; kwa sababu ameniasi mimi, asema Bwana.
18 Njia yako na matendo yako yamekupatia haya; huu ndio uovu wako; kwa maana ni uchungu, hakika unafikilia hata moyo wako.
19 Mtima wangu, mtima wangu! Naumwa katika moyo wangu wa ndani; moyo wangu umefadhaika ndani yangu; siwezi kunyamaza; kwa sababu umesikia, Ee nafsi yangu, sauti ya tarumbeta, mshindo wa vita.
20 Uangamivu baada ya uangamivu umetangazwa; kwa maana nchi yote imeharibika; hema zangu zimetekwa nyara ghafula, na mapazia yangu katika dakika moja.
21 Niione bendera hata lini, na kuisikia sauti ya tarumbeta?
22 Kwa maana watu wangu ni wapumbavu, hawanijui; ni watoto waliopungukiwa na akili, wala hawana ufahamu; ni wenye akili katika kutenda mabaya, bali katika kutenda mema hawana maarifa.
23 Naliiangalia nchi, na tazama, ilikuwa ukiwa, haina watu; naliziangalia mbingu, nazo zilikuwa hazina nuru.
24 Naliiangalia milima, na tazama, ilitetemeka, na milima yote ilisogea huko na huko.
25 Nikaangalia, na tazama, hapakuwa na mtu hata mmoja, na ndege wote wa angani wamekwenda zao.
26 Nikaangalia, na tazama, shamba lililozaa sana limekuwa ukiwa, na miji yake yote ilikuwa imebomoka mbele za Bwana, na mbele za hasira yake kali.
27 Maana Bwana asema hivi, Nchi yote itakuwa ukiwa; lakini sitaikomesha kabisa.
28 Kwa ajili ya hayo nchi itaomboleza, na mbingu zitakuwa nyeusi; kwa sababu mimi nimeyanena haya, na kuyakusudia, wala sikujuta wala mimi sitarudi nyuma niyaache.
29 Mji mzima unakimbia, kwa sababu ya mshindo wa wapanda farasi na wenye pinde wanaingia vichakani, wanapanda juu ya majabali; kila mji umeachwa, hapana hata mtu mmoja akaaye ndani yake.
30 Na wewe, utakapotekwa, utafanyaje? Ujapojivika mavazi mekundu, ujapojipamba mapambo ya dhahabu, ujapojitia wanja machoni, unajifanya kuwa mzuri bure tu; wapenzi wako wanakudharau; wanakutafuta roho yako.
31 Kwa maana nimesikia sauti, kama sauti ya mwanamke wakati wa utungu wake, na sauti yake aumwaye, kama mwanamke azaaye mtoto wake wa kwanza, sauti ya binti Sayuni, atwetaye kupata pumzi, na kunyosha mikono yake, akisema, Ole wangu, sasa! Kwa maana roho yangu inazimia mbele ya wauaji.

Yeremia 5


1 Pigeni mbio huku na huku katika njia za Yerusalemu, mkaone sasa, na kujua, na kutafuta katika viwanja vyake, kwamba mwaweza kumpata mtu mmoja, kwamba yuko mtu mmoja awaye yote atendaye kwa haki, atafutaye uaminifu; nami nitausamehe mji huo.
2 Na wajaposema, Kama Bwana aishivyo, hakika waapa kwa uongo.
3 Ee Bwana, macho yako je! Hayaangalii uaminifu? Umewapiga, lakini hawakuhuzunika; umewakomesha, lakini wamekataa kurudiwa wamefanya nyuso zao kuwa ngumu kuliko mwamba wamekataa kurudi.
4 Ndipo nikasema, Hakika, hawa ni maskini; ni wajinga hawa; maana hawaijui njia ya Bwana, wala hukumu ya Mungu wao;
5 nitawaendea watu wakubwa, nami nitasema nao; kwa maana hao wanaijua njia ya Bwana, na hukumu ya Mungu wao. Bali hawa kwa nia moja wameivunja nira, na kuvikata vifungo.
6 Basi, kwa hiyo, simba atokaye mwituni atawaua, mbwa-mwitu wa jioni atawateka, chui ataivizia miji yao, kila mtu atokaye humo atararuliwa vipande vipande; kwa sababu makosa yao ni mengi, na kurudi nyuma kwao kumezidi.
7 Nawezaje kukusamehe? Watoto wako wameniacha mimi, na kuapa kwa hao ambao si miungu; nilipokuwa nimewashibisha chakula, walizini, wakakutana wengi pamoja katika nyumba za makahaba.
8 Walikuwa kama farasi walioshiba wakati wa asubuhi; kila mmoja akalia kwa kutamani mke wa mwenzake.
9 Je! Nisiwapatilize kwa sababu ya mambo hayo? Asema Bwana; na nafsi yangu, je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii?
10 Pandeni juu ya kuta zake mkaharibu, lakini msiharibu kabisa; ondoeni matawi yake; kwa maana si yake Bwana.
11 Maana nyumba ya Israeli na nyumba ya Yuda wamenitenda kwa hiana sana, asema Bwana.
12 Wamemkataa Bwana, na kusema, Si yeye; wala hayatatupata mabaya; wala hatutaona upanga wala njaa;
13 na manabii watakuwa upepo, wala neno lake halimo ndani yao; basi ndivyo watakavyotendwa.
14 Kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wa majeshi, asema hivi, Kwa sababu mnasema neno hili, tazama, nitafanya maneno yangu katika kinywa chako kuwa moto, na watu hawa kuwa kuni, nao moto utawala.
15 Angalia, nitaleta taifa juu yenu litokalo mbali sana, Ee nyumba ya Israeli, asema Bwana; ni taifa hodari, ni taifa la zamani sana, taifa ambalo hujui lugha yake, wala huyafahamu wasemayo.
16 Podo lao ni kaburi wazi, ni mashujaa wote pia.
17 Nao watakula mavuno yako, na mkate wako, ambao iliwapasa wana wako na binti zako kuula; watakula makundi yako ya kondoo na ya ng'ombe; watakula mizabibu yako na mitini yako; wataiharibu miji yako yenye boma, uliyokuwa ukiitumainia, naam, wataiharibu kwa upanga.
18 Lakini hata katika siku zile, asema Bwana, sitawakomesha ninyi kabisa.
19 Tena itakuwa mtakapouliza, Bwana ametutenda mambo hayo yote kwa sababu gani? Ndipo utakapowaambia, Vile vile kama ninyi mlivyoniacha mimi, na kuwatumikia miungu mingine katika nchi yenu wenyewe, ndivyo mtakavyowatumikia wageni katika nchi isiyo yenu.
20 Tangazeni neno hili katika nyumba ya Yakobo, litangazeni katika Yuda, kusema,
21 Sikilizeni neno hili, enyi watu wajinga msio na ufahamu; mlio na macho ila hamwoni; mlio na masikio ila hamsikii.
22 Je! Hamniogopi mimi? Asema Bwana; hamtatetemeka mbele za uso wangu; mimi niliyeweka mchanga kuwa mpaka wa bahari, kwa amri ya daima, isiweze kuupita? Mawimbi yake yajapoumuka-umuka, hayawezi kushinda nguvu; yajapovuma sana, hayawezi kuupita.
23 Lakini watu hawa wana moyo wa kuasi na ukaidi; wameasi, wamekwenda zao.
24 Wala hawasemi mioyoni mwao, Basi, na tumche Bwana, Mungu wetu, aletaye mvua, mvua ya mwaka, na mvua ya vuli, kwa wakati wake; na kutuwekea juma za mavuno zilizoamriwa.
25 Maovu yenu yameyageuza haya, na dhambi zenu zimewazuilia mema msiyapate.
26 Maana katika watu wangu wameonekana watu waovu; huotea kama vile watu wategao mitego; hutega mtego, na kunasa watu.
27 Kama tundu lijaavyo ndege, kadhalika nyumba zao zimejaa hila; kwa hiyo wamekuwa wakuu, wamepata mali.
28 Wamewanda sana, wang'aa; naam, wamepita kiasi kwa matendo maovu; hawatetei madai ya yatima, ili wapate kufanikiwa; wala hawaamui haki ya mhitaji.
29 Je! Nisiwapatilize kwa mambo hayo? Asema Bwana; na nafsi yangu, je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii?
30 Jambo la ajabu, la kuchukiza, limetokea katika nchi hii!
31 Manabii wanatabiri uongo, na makuhani wanatawala kwa msaada wa hao; na watu wangu wanapenda mambo yawe hivyo. Nanyi mtafanya nini mwisho wake?

Yeremia 6


1 Kimbieni mpate kuwa salama, enyi wana wa Benyamini; tokeni katika Yerusalemu, pigeni tarumbeta katika Tekoa, simamisheni ishara juu ya Beth-hakeremu; kwa maana mabaya yanachungulia toka kaskazini, na uharibifu mkuu.
2 Binti Sayuni aliye mzuri, mwororo, nitamkatilia mbali.
3 Wachungaji na makundi yao ya kondoo watamjilia; watapiga hema zao karibu naye pande zote; watalisha kila mmoja mahali pake.
4 Takaseni vita juu yake; inukeni, na tupande juu wakati wa adhuhuri. Ole wetu, kwa kuwa mchana umeanza kupungua, vivuli vya jioni vinazidi kuwa virefu.
5 Inukeni, na tupande juu wakati wa usiku, tukayaharibu majumba yake.
6 Maana Bwana wa majeshi asema hivi, Jikatieni miti, mfanyize boma juu ya Yerusalemu. Mji huu ni mji unaojiliwa; dhuluma tupu imo ndani yake.
7 Kama vile kisima kitoavyo maji yake, ndivyo utoavyo uovu wake; jeuri na kuharibu kwasikiwa ndani yake; ugonjwa na jeraha zi mbele zangu daima.
8 Uadhibishwe, Ee Yerusalemu, nafsi yangu, isije ikafarakana nawe; nisije nikakufanya ukiwa, nchi isiyokaliwa na watu.
9 Bwana wa majeshi asema hivi, Wataokota mabaki ya Israeli kama mzabibu; rudisha mkono wako ndani ya vikapu, kama mchuma zabibu.
10 Niseme na nani na kushuhudia, wapate kusikia? Tazama, sikio lao halikutahiriwa, wala hawawezi kusikiliza; tazama, neno la Bwana limekuwa matukano kwao; hawalifurahii.
11 Lakini nimejaa ghadhabu ya Bwana; nimechoka kwa kujizuia; imwageni juu ya watoto walio njiani, na juu ya kusanyiko la vijana pia; maana hata mume atatwaliwa pamoja na mkewe, mzee pamoja na yeye aliyetimiza siku zake.
12 Na nyumba zao zitakuwa mali za watu wengine, mashamba yao na wake zao pamoja; kwa kuwa nitaunyosha mkono wangu juu ya wenyeji wa nchi hii, asema Bwana.
13 Kwa maana, tangu aliye mdogo hata aliye mkubwa miongoni mwao, kila mmoja ni mtamanifu; na, tangu nabii hata kuhani, kila mmoja hutenda mambo ya udanganyifu.
14 Wameiponya jeraha ya watu wangu kwa juu juu tu, wakisema, Amani, Amani, wala hapana amani.
15 Je! Walitahayarika, walipokuwa wameunda machukizo? La, hawakutahayarika hata kidogo, wala hawakuweza kuona haya usoni; basi, wataanguka miongoni mwa hao waangukao; wakati nitakapowajilia wataangushwa chini, asema Bwana.
16 Bwana asema hivi, Simameni katika njia kuu, mkaone, mkaulize habari za mapito ya zamani, I wapi njia iliyo njema? Mkaende katika njia hiyo, nanyi mtajipatia raha katika nafsi zenu. Lakini walisema, Hatutaki kwenda katika njia hiyo.
17 Nami naliweka walinzi juu yenu, wakisema, Isikilizeni sauti ya tarumbeta; lakini walisema, Hatutaki kusikiliza.
18 Kwa sababu hiyo sikilizeni, enyi mataifa, mkajue, Ee kusanyiko, ni jambo gani litokealo kati yao.
19 Sikia, Ee nchi; tazama, nitaleta mabaya juu ya watu hawa, naam, matunda ya mawazo yao, kwa sababu hawakuyasikiliza maneno yangu; tena kwa habari ya sheria yangu, wameikataa.
20 Yafaa nini niletewe ubani kutoka Sheba, na uudi kutoka nchi iliyo mbali? Sadaka zenu za kuteketezwa hazikubaliwi, wala dhabihu zenu haziniridhii.
21 Basi, kwa hiyo, Bwana asema hivi, Tazama, nitaweka makwazo mbele ya watu hawa, na baba na wana wao watajikwaa pamoja; jirani ya mtu na rafiki yake watapotea.
22 Bwana asema hivi, Tazama, watu wanakuja, wakitoka katika nchi ya kaskazini; na taifa kubwa litaamshwa, litokalo katika pande za mwisho wa dunia.
23 Washika upinde na mkuki; ni wakatili, hawana huruma; sauti yao huvuma kama bahari, nao wamepanda farasi zao; kila mmoja kama mtu wa vita amejipanga juu yako, Ee binti Sayuni.
24 Tumesikia habari zake; mikono yetu inalegea; dhiki imetushika, na utungu kama wa mwanamke wakati wa kuzaa kwake.
25 Msitoke kwenda mashambani, wala msitembee njiani, kwa maana upanga wa adui uko huko; hofu ziko pande zote.
26 Ee binti wa watu wangu, ujivike nguo ya magunia, na kugaagaa katika majivu; fanya maombolezo, kama maombolezo kwa ajili ya mwana wa pekee, maombolezo ya uchungu mwingi; maana mwenye kuteka nyara atakuja juu yetu ghafula.
27 Nimekuweka uwe mnara na ngome kati ya watu wangu; upate kuijua njia yao na kuijaribu.
28 Ni waasi kupita kiasi wote pia, waendao huko na huko wakisingizia, ni shaba na chuma hao, hutenda dhuluma wote pia.
29 Mifuo inafukuta kwa nguvu; risasi tu inatoka katika moto huo; mfua fedha ameyeyusha bure tu; maana wabaya hawaondolewi mbali.
30 Watu watawaita taka za fedha, kwa sababu Bwana amewakataa.

Yeremia 7


1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema,
2 Simama langoni pa nyumba ya Bwana, ukatangaze hapo neno hili, ukisema, Sikilizeni neno la Bwana, ninyi nyote wa Yuda, mnaoingia katika malango haya ili kumwabudu Bwana.
3 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, nami nitawakalisha ninyi mahali hapa.
4 Msitumainie maneno ya uongo, mkisema, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana, Hekalu la Bwana ndiyo haya.
5 Maana kama mkitengeneza kabisa njia zenu na matendo yenu; kama mkihukumu hukumu ya haki kati ya mtu na jirani yake;
6 kama hamwonei mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kumwaga damu isiyo na hatia mahali hapa, wala kuifuata miungu mingine kwa hasara yenu wenyewe;
7 ndipo nitakapowakalisha mahali hapa, katika nchi hii niliyowapa baba zenu, tokea zamani hata milele.
8 Angalieni, mnatumainia maneno ya uongo, yasiyoweza kufaidia.
9 Je! Mtaiba, na kuua, na kuzini, na kuapa kwa uongo, na kumfukizia Baali uvumba, na kuifuata miungu mingine ambayo hamkuijua;
10 kisha mtakuja na kusimama mbele zangu katika nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, na kusema, Tumepona; ili mpate kufanya machukizo hayo yote?
11 Je! Nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, imekuwa pango la wanyang'anyi machoni penu? Angalieni, mimi, naam, mimi, nimeliona jambo hili, asema Bwana.
12 Lakini enendeni sasa hata mahali pangu palipokuwapo katika Shilo, nilipolikalisha jina langu hapo kwanza, mkaone nilivyopatenda kwa sababu ya uovu wa watu wangu Israeli.
13 Na sasa, kwa sababu mmezifanya kazi hizi zote asema Bwana, nami nikasema nanyi, nikiamka mapema na kunena, lakini hamkusikia; nami nikawaita wala hamkuniitikia;
14 basi, nitaitenda nyumba hii, iitwayo kwa jina langu, mnayoitumainia, na mahali hapa nilipowapa ninyi na baba zenu, kama nilivyopatenda Shilo.
15 Nami nitawatupa ninyi mbali na macho yangu, kama nilivyowatupa ndugu zenu wote, yaani, wazao wote wa Efraimu.
16 Basi, wewe usiwaombee watu hawa, wala usiwapazie sauti yako, wala kuwaombea dua, wala usinisihi kwa ajili yao; kwa maana sitakusikiliza.
17 Je! Huoni wanavyotenda katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu?
18 Watoto huokota kuni, na baba zao huwasha moto, na wanawake hukanda unga, ili kumfanyizia mikate malkia wa mbinguni, na kuwamiminia miungu mingine sadaka za kinywaji, wapate kunikasirisha mimi.
19 Je! Watu hawa wanikasirisha mimi? Asema Bwana; hawajikasirishi nafsi zao, na kuzitia haya nyuso zao wenyewe?
20 Kwa hiyo, Bwana MUNGU asema hivi, Tazama, hasira yangu na ghadhabu yangu zitamwagwa juu ya mahali hapa, juu ya wanadamu, na juu ya wanyama, na juu ya miti ya mashamba, na juu ya mazao ya nchi; nayo itateketea, isizimike.
21 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tieni sadaka zenu za kuteketezwa pamoja na dhabihu zenu, mkale nyama.
22 Maana sikusema na baba zenu, wala sikuwaamuru kwa habari za sadaka za kuteketezwa na dhabihu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri;
23 lakini naliwaamuru neno hili, nikisema, Sikilizeni sauti yangu, nami nitakuwa Mungu wenu nanyi mtakuwa watu wangu; mkaende katika njia ile yote nitakayowaamuru mpate kufanikiwa.
24 Lakini hawakusikiliza, wala kutega sikio lao, bali walikwenda kwa mashauri yao wenyewe, na kwa ushupavu wa mioyo yao mibaya, wakaenda nyuma wala si mbele.
25 Tokea siku ile baba zenu walipotoka katika nchi ya Misri hata leo, nimewatuma watumishi wangu wote manabii kwenu ninyi, nikiamka mapema kila siku, na kuwatuma.
26 Lakini hawakunisikiliza, wala kutega sikio lao; bali walifanya shingo yao kuwa ngumu; walitenda mabaya kuliko baba zao.
27 Nawe utawaambia maneno hayo yote; lakini hawatakusikiliza, nawe utawaita; lakini hawatakuitikia.
28 Nawe utawaambia, Taifa hili ndilo lisilosikiliza sauti ya Bwana, Mungu wao, wala kupokea mafundisho; uaminifu umepotea, umekatiliwa mbali na vinywa vyao.
29 Zikate nywele zako, Ee Yerusalemu, uzitupe, Ukafanye maombolezo juu ya vilele vya milima; Kwa maana Bwana amekikataa na kukitupa Kizazi cha ghadhabu yake.
30 Maana wana wa Yuda wametenda yaliyo maovu machoni pangu, asema Bwana; wameweka machukizo yao ndani ya nyumba hiyo, iitwayo kwa jina langu, hata kuitia unajisi.
31 Nao wamepajenga mahali palipoinuka pa Tofethi, palipo katika bonde la mwana wa Hinomu, ili kuwateketeza wana wao na binti zao motoni; jambo ambalo mimi sikuliagiza, wala halikuingia moyoni mwangu.
32 Basi angalieni, siku zinakuja, asema Bwana, ambazo katika siku hizo halitaitwa tena Tofethi, wala Bonde la mwana wa Hinomu bali litaitwa, Bonde la Machinjo; maana watazika watu katika Tofethi, hata hapatakuwapo mahali pa kuzika tena.
33 Na mizoga ya watu hawa itakuwa chakula cha ndege wa angani, na cha wanyama wa nchi; wala hapana mtu atakayewafukuza.
34 Ndipo katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, nitaikomesha sauti ya kicheko na sauti ya furaha, sauti ya bwana arusi na sauti ya bibi arusi; kwa maana nchi hiyo itakuwa ukiwa.

Yeremia 8


1 Wakati ule, asema Bwana, watatoa mifupa ya wafalme wa Yuda, na mifupa ya wakuu wake, na mifupa ya makuhani, na mifupa ya manabii na mifupa ya wenyeji wa Yerusalemu, itoke makaburini mwao;
2 nao wataitawanya mbele ya jua, na mwezi, na jeshi lote la mbinguni, walivyovipenda, na kuvitumikia, na kuandamana navyo, na kuvitafuta, na kuviabudu haitakusanywa pamoja tena, wala kuzikwa; itakuwa ni samadi juu ya uso wa nchi.
3 Na kufa kutachaguliwa kuliko kuishi na mabaki yote waliosalia katika jamaa hii mbovu, waliosalia kila mahali nilikowafukuza, asema Bwana wa majeshi.
4 Tena utawaambia, Bwana asema hivi, Je! Watu wataanguka, wasisimame tena? Je! Mtu atageuka aende zake, asirudi tena?
5 Mbona, basi, watu hawa wa Yerusalemu wamegeuka waende nyuma, wasikome kugeuka hivyo? Hushika udanganyifu sana, hukataa kurudi.
6 Nalisikiliza nikasikia, lakini walisema yasiyo sawa; hapana mtu aliyetubia maovu yake, akisema, Nimefanya nini? Kila mtu hurudia mwendo wake mwenyewe, kama farasi aendavyo kasi vitani.
7 Naam, koikoi angani ajua nyakati zake zilizoamriwa; na hua na mbayuwayu na korongo huangalia wakati wa kuja kwao; bali watu wangu hawazijui amri za Bwana.
8 Mwasemaje, Sisi tuna akili, na torati ya Bwana tunayo pamoja nasi? Lakini, tazama, kalamu yenye uongo ya waandishi imeifanya kuwa uongo.
9 Wenye hekima wametahayari, wamefadhaika na kushikwa; tazama, wamelikataa neno la Bwana, wana akili gani ndani yao?
10 Basi, kwa hiyo nitawapa watu wengine wake zao na mashamba yao nitawapa wale watakaowamiliki; maana kila mmoja wao, tangu aliye mdogo hata aliye mkubwa, ni mtamanifu; tangu nabii hata kuhani, kila mmoja hutenda mambo ya udanganyifu.
11 Kwa maana wameiponya jeraha ya binti ya watu wangu kwa juu-juu tu, wakisema, Amani, Amani, wala hapana amani.
12 Je! Walitahayarika, walipokuwa wametenda machukizo? La! Hawakutahayarika, wala hawakuweza kuona haya usoni; basi wataanguka miongoni mwao waangukao; wakati wa kujiliwa kwao wataangushwa chini, asema Bwana.
13 Nitawaangamiza kabisa, asema Bwana; hapana zabibu katika mizabibu, wala tini katika mitini, hata jani lake litanyauka; na vitu vile nilivyowapa vitawapotea.
14 Mbona tunakaa kimya? Jikusanyeni, tukaingie ndani ya miji yenye maboma, tukanyamaze humo kwa maana Bwana, Mungu wetu, ametunyamazisha, naye ametupa maji yenye uchungu tunywe, kwa sababu tumemwasi Bwana.
15 Tulitazamia amani, lakini hayakuja mema yo yote; tulitazamia wakati wa kupona, na tazama, kufadhaika tu!
16 Kutoka Dani kumesikiwa mkoromo wa farasi zake; nchi yote pia inatetemeka kwa sauti ya mlio wa farasi zake za vita; maana wamekuja, wamekula nchi na vyote vilivyomo; huo mji na wote wakaao ndani yake.
17 Maana, tazama, nitatuma nyoka, naam, fira, kati yenu, wasioweza kutumbuizwa kwa uganga; nao watawauma, asema Bwana.
18 Laiti ningeweza kujifariji, nisione huzuni! Moyo wangu umezimia ndani yangu.
19 Tazama, sauti ya kilio cha binti ya watu wangu, itokayo katika nchi iliyo mbali sana; Je! Bwana hayumo katika Sayuni? Mfalme wake hayumo ndani yake? Mbona wamenikasirisha kwa sanamu zao walizochonga, na kwa ubatili wa kigeni?
20 Mavuno yamepita, wakati wa hari umekwisha, wala sisi hatukuokoka.
21 Kwa sababu ya maumivu ya binti ya watu wangu nimeumia mimi; nimevaa kaniki; ushangao umenishika.
22 Je! Hapana zeri katika Gileadi? Huko hakuna tabibu? Mbona, basi, haijarejea afya ya binti ya watu wangu?

Yeremia 9


1 Laiti kichwa changu kingekuwa maji, na macho yangu kuwa chemchemi ya machozi, ili nipate kulia mchana na usiku kwa ajili yao waliouawa wa binti ya watu wangu!
2 Laiti ningekuwa na mahali pa kukaa jangwani, kibanda cha wasafiri; nipate kuwaacha watu wangu, na kuondoka kwao! Maana wao ni wazinzi, wote pia, mkutano wa watu wenye hiana.
3 Huupinda ulimi wao, kana kwamba ni upinde, ili kusema uongo; nao wamepata nguvu katika nchi, lakini si katika uaminifu; maana huendelea toka ubaya hata ubaya, wala hawanijui mimi, asema Bwana.
4 Jihadharini, kila mtu na jirani yake, wala msimtumaini ndugu awaye yote; maana kila ndugu atachongea, na kila jirani atakwenda huko na huko na kusingizia.
5 Nao watadanganya kila mtu jirani yake, wala hawatasema kweli; wameuzoeza ulimi wao kusema uongo; hujidhoofisha ili kutenda uovu.
6 Makao yako ya katikati ya hadaa; kwa hadaa wanakataa kunijua mimi, asema Bwana.
7 Basi, kwa hiyo Bwana wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawayeyusha na kuwajaribu; maana nisipotenda hivi, nitende nini kwa ajili ya binti ya watu wangu?
8 Ulimi wao ni mshale ufishao; husema maneno ya hadaa; mtu mmoja husema maneno ya amani na mwenzake kwa kinywa chake, lakini moyoni mwake humwotea.
9 Je! Nisiwapatilize kwa mambo hayo? Asema Bwana; na nafsi yangu je! Nisijilipize kisasi juu ya taifa la namna hii?
10 Kwa milima nitalia na kulalama, Na kwa malisho ya nyikani nitafanya maombolezo; Kwa sababu yameteketea, hata hapana apitaye, Wala hapana awezaye kusikia sauti ya ng'ombe; Ndege wa angani, na wanyama wa mwituni, Wamekimbia, wamekwenda zao.
11 Nami nitafanya Yerusalemu kuwa magofu, Makao ya mbweha; Nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, Isikaliwe na mtu awaye yote.
12 Ni nani aliye na hekima, apate kuelewa na haya? Tena ni nani ambaye kinywa cha Bwana kimesema naye, apate kuyatangaza? Nayo ni nini maana yake nchi hii kuharibika, na kuteketea kama nyika, asipite mtu?
13 Naye Bwana asema, Ni kwa sababu wameiacha sheria yangu niliyoweka mbele yao, wala hawakuitii sauti yangu, wala kuenenda katika hiyo;
14 bali wameenenda katika ushupavu wa mioyo yao wenyewe, na kuandamana na Mabaali, kama walivyofundishwa na baba zao.
15 Basi, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitawalisha pakanga, naam, watu hawa, nami nitawapa maji ya uchungu wayanywe.
16 Nami nitawatawanya kati ya mataifa, ambao wao hawakuwajua; wala baba zao, nami nitatuma upanga nyuma yao, hata nitakapowaangamiza kabisa.
17 Bwana wa majeshi asema hivi, Fikirini ninyi, mkawaite wanawake waombolezao, ili waje; mkatume na kuwaita wanawake wenye ustadi, ili waje;
18 na wafanye haraka na kutuombolezea, ili macho yetu yachuruzike machozi, na kope zetu zibubujike maji.
19 Maana sauti ya maombolezo imesikiwa toka Sayuni, Jinsi tulivyotekwa! tulivyofadhaika sana! Kwa sababu tumeiacha nchi, kwa kuwa wameangusha makao yetu.
20 Lakini lisikieni neno la Bwana, enyi wanawake, Na masikio yenu yapokee neno la kinywa chake; Mkawafundishe binti zenu kuomboleza, Na kila mmoja jirani yake kulia.
21 Kwa maana mauti imepandia madirishani mwetu, imeingia majumbani mwetu; Ipate kuwakatilia mbali watoto walio nje, na vijana katika njia kuu.
22 Nena, Bwana asema hivi, Mizoga ya watu itaanguka kama samadi juu ya mashamba, Na kama konzi ya ngano nyuma yake avunaye, wala hapana mtu atakayeikusanya.
23 Bwana asema hivi, Mwenye hekima asijisifu kwa sababu ya hekima yake, wala mwenye nguvu asijisifu kwa sababu ya nguvu zake, wala tajiri asijisifu kwa sababu ya utajiri wake;
24 bali ajisifuye na ajisifu kwa sababu hii, ya kwamba ananifahamu mimi, na kunijua, ya kuwa mimi ni Bwana, nitendaye wema, na hukumu, na haki, katika nchi; maana mimi napendezwa na mambo hayo, asema Bwana,
25 Tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapowaadhibu wote waliotahiriwa katika hali yao ya kutokutahiriwa;
26 Misri, na Yuda, na Edomu, na wana wa Amoni, na Moabu, na wote wenye kunyoa denge, wakaao nyikani; maana mataifa hayo yote hawana tohara, wala nyumba yote ya Israeli hawakutahiriwa mioyo yao.

Yeremia 10


1 Enyi nyumba ya Israeli, lisikieni neno awaambialo Bwana;
2 Bwana asema hivi, Msijifunze njia ya mataifa, wala msishangae kwa sababu ya ishara za mbinguni; maana mataifa hushangaa kwa sababu ya ishara hizo.
3 Maana desturi za watu hao ni ubatili, maana mtu mmoja hukata mti mwituni, kazi ya mikono ya fundi na shoka.
4 Huupamba kwa fedha na dhahabu; huukaza kwa misumari na nyundo, usitikisike.
5 Mfano wao ni mfano wa mtende, kazi ya cherehani, hawasemi; hawana budi kuchukuliwa, kwa sababu hawawezi kwenda. Usiwaogope; kwa maana hawawezi kutenda uovu, wala hawana uwezo wa kutenda mema.
6 Hapana hata mmoja aliye kama wewe, Ee Bwana; wewe ndiwe uliye mkuu, na jina lako ni kuu katika uweza.
7 Ni nani asiyekucha wewe, Ee mfalme wa mataifa? Maana hii ni sifa yako wewe; kwa kuwa miongoni mwa wenye hekima wote wa mataifa, na katika hali yao ya enzi yote pia, hapana hata mmoja kama wewe.
8 Lakini wote pia huwa kama wanyama, ni wapumbavu. Haya ni maelezo ya sanamu, ni shina la mti tu.
9 Iko fedha iliyofuliwa ikawa mabamba, iliyoletwa kutoka Tarshishi, na dhahabu kutoka Ufazi, kazi ya stadi na ya mikono ya mfua dhahabu; mavazi yao ni rangi ya samawi na urujuani; hayo yote ni kazi ya mafundi yao.
10 Bali Bwana ndiye Mungu wa kweli; Ndiye Mungu aliye hai, Mfalme wa milele; Mbele za ghadhabu yake nchi yatetemeka, Wala mataifa hawawezi kustahimili hasira yake.
11 Mtawaambia hivi, Miungu hiyo isiyofanya mbingu na nchi, hiyo itaangamia katika nchi, nayo itatoweka chini ya mbingu.
12 Ameiumba dunia kwa uweza wake, Ameuthibitisha ulimwengu kwa hekima yake, Na kwa ufahamu wake amezitandika mbingu.
13 Atoapo sauti yake, pana mshindo wa maji mbinguni, Naye hupandisha mawingu toka ncha za nchi; Huifanyia mvua umeme, Huutoa upepo katika hazina zake.
14 Kila mtu amekuwa kama mnyama, hana maarifa; Kila mfua dhahabu amefedheheshwa na sanamu yake ya kuchonga; Maana sanamu yake ya kuyeyuka ni uongo, Wala hamna pumzi ndani yake.
15 Ni ubatili tu, ni kazi za udanganyifu; Wakati wa kujiliwa kwao watapotea.
16 Yeye, Fungu la Yakobo, siye kama hawa; Maana ndiye aliyeviumba vitu vyote; Na Israeli ni kabila ya urithi wake; Bwana wa majeshi ndilo jina lake.
17 Haya! Kusanya bidhaa yako katika nchi, wewe ukaaye katika mazingiwa.
18 Maana Bwana asema hivi, Tazama, wakati huu nitawatupa wenyeji wa nchi hii kama kwa kombeo, nitawataabisha, wapate kuona taabu.
19 Ole wangu, kwa sababu ya jeraha yangu! Pigo langu laumia; lakini nalisema, Kweli, ni huzuni yangu mimi, nami sina budi kuivumilia.
20 Hema yangu umetekwa nyara, kamba zangu zote zimekatika; watoto wangu wameniacha na kwenda zao, pia hawako. Hapana mtu atakayenitandikia tena hema yangu, na kuyatundika mapazia yangu.
21 Kwa sababu wachungaji wamekuwa kama wanyama, wala hawakuuliza kwa Bwana; basi hawakufanikiwa, na makundi yao yote yametawanyika.
22 Sauti imesikiwa, Tazama, inakuja; mshindo mkuu kutoka nchi ya kaskazini, ili kuifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, makao ya mbweha.
23 Ee Bwana, najua ya kuwa njia ya mwanadamu haimo katika nafsi yake; kuelekeza hatua zake si katika uwezo wa mwanadamu.
24 Ee Bwana, unirudi kwa haki; si kwa hasira yako, usije ukaniangamiza.
25 Hasira yako uwamwagie mataifa wasiokujua, na jamaa zao wasioliitia jina lako; kwa maana wamemla Yakobo, naam, wamemla kabisa na kumwangamiza, na kuyafanya makao yake kuwa ukiwa.

Yeremia 11


1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema,
2 Yasikieni maneno ya maagano haya; ukaseme na watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu;
3 ukawaambie, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Na alaaniwe mtu asiyeyasikia maneno ya maagano haya,
4 niliyowaamuru baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, katika tanuru ya chuma, nikisema, Itiini sauti yangu, mkafanye sawasawa na yote niwaagizayo ninyi; ndivyo mtakavyokuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu;
5 ili nipate kukitimiza kiapo nilichowaapia baba zenu, kuwapa nchi ijaayo maziwa na asali, kama ilivyo leo hivi. Ndipo nikajibu, nikasema, Amina, Ee Bwana.
6 Naye Bwana akaniambia, Hubiri maneno haya yote katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, ukisema, Yasikieni maneno ya maagano haya, mkayafanye.
7 Kwa maana naliwashuhudia sana baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, hata leo, nikiamka mapema na kuwashuhudia, nikisema, Itiini sauti yangu.
8 Lakini hawakutii, wala kutega masikio yao, bali walikwenda kila mtu katika ushupavu wa moyo wake mbaya; kwa hiyo nimeleta juu yao maneno yote ya maagano haya, niliyowaamuru wayafanye; lakini hawakuyafanya.
9 Naye Bwana akaniambia, Fitina imeonekana katika watu wa Yuda, na katika wenyeji wa Yerusalemu.
10 Wameyarudia maovu ya baba zao, waliokataa kusikia maneno yangu; wamewafuata miungu mingine na kuwatumikia; nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, wameyavunja maagano yangu niliyoyafanya na baba zao.
11 Basi, Bwana asema hivi, Tazama, nitaleta mabaya juu yao, ambayo hawataweza kuyakimbia; nao watanililia, walakini sitawasikiliza.
12 Ndipo miji ya Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, watakwenda na kuwalilia miungu wawafukiziao uvumba; lakini hawatawaokoa hata kidogo wakati wa taabu yao.
13 Maana hesabu ya miungu yako, Ee Yuda, ni sawasawa na hesabu ya miji yako; na kama ilivyo hesabu ya njia za Yerusalemu, ndivyo mlivyosimamisha madhabahu za kitu kile cha aibu, madhabahu za kumfukizia Baali uvumba.
14 Basi, usiwaombee watu hawa, wala usipaze sauti yako, wala kuwaombea dua watu hawa; maana sitawasikia wakati watakaponililia kwa ajili ya taabu yao.
15 Mpenzi wangu afanya nini nyumbani mwangu, ikiwa amefanya uasherati? Je! Nadhiri zako na nyama takatifu zitakuondolea hatia? Ufanyapo maovu, ndipo uonapo furaha.
16 Bwana alikuita jina lako, Mzeituni wenye majani mabichi, mzuri, wenye matunda mema; kwa kelele za mshindo mkuu amewasha moto juu yake, na matawi yake yamevunjika.
17 Kwa maana Bwana wa majeshi, aliyekupanda, ametamka mabaya juu yako, kwa sababu ya maovu ya nyumba ya Israeli, na ya nyumba ya Yuda, waliyoyatenda juu ya nafsi zao wenyewe kwa kunikasirisha, wakimfukizia Baali uvumba.
18 Tena Bwana akanijulisha haya, nami nikayajua; ndipo uliponionyesha matendo yao.
19 Lakini mimi nalikuwa kama mwana-kondoo mpole, achukuliwaye kwenda kuchinjwa; wala sikujua ya kuwa wamefanya mashauri kinyume changu, wakisema, Na tuuharibu mti pamoja na matunda yake, na tumkatilie mbali atoke katika nchi ya walio hai, ili jina lake lisikumbukwe tena.
20 Lakini, Ee Bwana wa majeshi, uhukumuye haki, ujaribuye viuno na moyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.
21 Basi, kwa hiyo, Bwana asema hivi, juu ya watu wa Anathothi, watakao uhai wako, wakisema, Hutafanya unabii kwa jina la Bwana, usije ukafa kwa mkono wetu.
22 Kwa sababu hiyo Bwana wa majeshi asema hivi, Tazama, nitawaadhibu watu hawa; vijana watakufa kwa upanga; wana wao na binti zao watakufa kwa njaa;
23 wala hapatakuwa na mtu atakayesalia kwao; maana nitaleta mabaya juu ya watu wa Anathothi, mwaka wa kujiliwa kwao.

Yeremia 12


1 Wewe u mwenye haki, Ee Bwana, nitetapo nawe, lakini nitasema nawe katika habari ya haki. Mbona njia ya wabaya inasitawi? Mbona wote watendao hila wanakaa salama?
2 Umewapanda, naam, wametia mizizi, wanakua, naam, wanazaa matunda; katika vinywa vyao u karibu, bali katika mioyo yao u mbali.
3 Lakini wewe, Bwana, wanijua; umeniona, umeujaribu moyo wangu, jinsi unavyokuelekea; uwakokote kama kondoo waendao kuchinjwa, ukawaweke tayari kwa siku ya kuchinjwa.
4 Hata lini itaomboleza nchi, na kukauka majani ya nchi yote? Kwa ajili ya mabaya yao wakaao ndani yake, wanyama wameangamia na ndege pia; kwa sababu walisema, Hatauona mwisho wetu.
5 Ikiwa umepiga mbio pamoja na hao waendao kwa miguu, nao wamekuchosha, basi wawezaje kushindana na farasi? Na ujapokuwa katika nchi ya amani u salama, lakini utafanyaje hapo katika kiburi cha Yordani?
6 Kwa maana hata ndugu zako, na nyumba ya baba yako, wamekutenda mambo ya hila; naam, wamepiga kelele nyuma yako; usiwasadiki, wajapokuambia maneno mazuri.
7 Nimeiacha nyumba yangu, nimeutupa urithi wangu; nimemtia mpenzi wangu katika mikono ya adui zake.
8 Urithi wangu umekuwa kwangu kama simba msituni; ameinua sauti yake juu yangu; kwa sababu hiyo nimemchukia.
9 Je! Urithi wangu umekuwa kwangu kama ndege mwenye madoadoa? Ndege wakali wanamtulia pande zote? Enendeni, wakusanyeni pamoja wanyama wote wa mwituni, waleteni ili wale.
10 Wachungaji wengi wameliharibu shamba langu la mizabibu, wamelikanyaga fungu langu chini ya miguu yao, wamefanya fungu langu zuri kuwa jangwa la ukiwa.
11 Wamelifanya kuwa ukiwa, na kwa kuwa ni ukiwa linanililia; nchi yote imefanywa kuwa ukiwa, kwa sababu hapana mtu aliyeweka haya moyoni mwake.
12 Watekao nyara wamepanda juu ya vilele vya milima katika nyika; kwa maana upanga wa Bwana utakula toka upande mmoja wa nchi hata upande wa pili wa nchi; hapana mwenye mwili atakayekuwa na amani.
13 Wamepanda ngano, lakini watavuna miiba; wamejiumiza nafsi zao, lakini hawatakuwa na faida; naam, tahayarini kwa ajili ya matunda yenu, kwa sababu ya hasira kali ya Bwana.
14 Bwana asema hivi juu ya jirani zangu wote walio wabaya, waugusao urithi wangu niliowarithisha watu wangu Israeli, Tazama, nitawang'oa katika nchi yao, nami nitaing'oa nyumba ya Yuda isiwe kati yao.
15 Tena itakuwa, baada ya kuwang'oa, nitarudi na kuwahurumia; nami nitawaleta tena, kila mtu aingie katika urithi wake, na kila mtu aingie katika nchi yake.
16 Kisha itakuwa, ikiwa watajifunza kwa bidii njia za watu wangu, kuapa kwa jina langu, Kama Bwana aishivyo, vile vile kama walivyowafundisha watu wangu kuapa kwa Baali, ndipo watakapojengwa kati ya watu wangu.
17 Bali, kama hawataki kusikia, kung'oa nitaling'oa taifa lile, na kuliangamiza kabisa, asema Bwana.

Yeremia 13


1 Bwana akaniambia hivi, Enenda, ukajinunulie mshipi wa kitani, ukajivike viuno, wala usiutie majini.
2 Basi nikanunua mshipi sawasawa na neno la Bwana, nikajivika viunoni.
3 Nalo neno la Bwana likanijia mara ya pili, kusema,
4 Twaa mshipi ule ulioununua, ulio viunoni mwako, kisha ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukaufiche huko katika pango la jabali.
5 Basi nikaenda, nikauficha karibu na mto Frati, kama Bwana alivyoniamuru.
6 Hata ikawa, baada ya siku nyingi, Bwana akaniambia, Ondoka, enenda mpaka mto Frati, ukautwae ule mshipi, niliokuamuru kuuficha huko.
7 Ndipo nikaenda mpaka mto Frati, nikachimba, nikautwaa ule mshipi katika mahali pale nilipouficha; na tazama, mshipi ulikuwa umeharibika, haukufaa tena kwa lo lote.
8 Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema,
9 Bwana asema hivi, Jinsi iyo hiyo nitakiharibu kiburi cha Yuda, na kiburi kikuu cha Yerusalemu.
10 Watu hawa waovu, wanaokataa kusikiliza maneno yangu, wanaokwenda kwa ushupavu wa mioyo yao, na kufuata miungu mingine ili kuitumikia na kuiabudu, watakuwa hali moja na mshipi huu, usiofaa kwa lo lote.
11 Maana kama vile mshipi unavyoshikamana na viuno vya mtu, ndivyo nilivyowashikamanisha nami nyumba yote ya Israeli; na nyumba yote ya Yuda, asema Bwana; wapate kuwa watu kwangu mimi, na jina, na sifa, na utukufu; lakini hawakutaka kusikia.
12 Basi utawaambia neno hili, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kila chupa itajazwa divai; nao watakuambia, Je, sisi hatujui ya kuwa kila chupa itajazwa divai?
13 Ndipo utakapowaambia, Bwana asema hivi, Tazama, nitawajaza ulevi wenyeji wote wa nchi hii, hata wafalme wanaoketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na makuhani, na manabii, na wenyeji wote wa Yerusalemu.
14 Nitawagonganisha, mtu na mwenzake, naam, baba za watu na watoto wao pamoja, asema Bwana; sitahurumia, wala sitaachilia, wala sitarehemu, hata nisiwaangamize.
15 Sikilizeni ninyi, kategeni masikio yenu; msifanye kiburi; maana Bwana amenena.
16 Mtukuzeni Bwana, Mungu wenu, kabla hajaleta giza, na kabla miguu yenu haijakwaa juu ya milima yenye giza; na wakati mnapoitazamia nuru, kabla hajaigeuza kuwa kivuli cha mauti, na giza nene.
17 Bali kama hamtaki kusikia, roho yangu italia kwa siri, kwa sababu ya kiburi chenu; na jicho langu litalia sana na kutoka machozi mengi, kwa kuwa kundi la Bwana limechukuliwa hali ya kufungwa.
18 Mwambie mfalme, na mama ya mfalme, Nyenyekeeni na kuketi chini; Kwa maana vilemba vyenu vimeshuka, naam, taji ya utukufu wenu.
19 Miji ya Negebu imefungwa malango yake, wala hapana mtu wa kuyafungua; Yuda amechukuliwa hali ya kufungwa; amechukuliwa kabisa hali ya kufungwa.
20 Inua macho yako, Ee Yerusalemu, ukawatazame hawa wanaokuja kutoka kaskazini; liko wapi kundi lako ulilopewa, kundi lile zuri?
21 Utasema nini wewe, atakapowaweka rafiki zako kuwa kichwa juu yako, ikiwa wewe mwenyewe umewafundisha kuwa juu yako? Je! Huzuni haitakushika, kama utungu wa mwanamke aliye katika kuzaa?
22 Nawe ukisema moyoni mwako, Mbona mambo haya yamenipata mimi? Ni kwa sababu ya wingi wa uovu wako, marinda yako yamefunuliwa, na visigino vya miguu yako vimeumia.
23 Je! Mkushi aweza kuibadili ngozi yake, au chui madoa-doa yake? Kama aweza, ndipo na ninyi mwaweza kutenda mema, ninyi mliozoea kutenda mabaya.
24 Kwa sababu hiyo nitawatawanya, kama makapi yapitayo, kwa upepo wa jangwani.
25 Hiyo ndiyo kura yako, fungu lako ulilopimiwa na mimi, asema Bwana; kwa kuwa umenisahau, na kuutumainia uongo.
26 Kwa ajili ya hayo, mimi nami nitayafunua marinda yako mbele ya uso wako, na aibu yako itaonekana.
27 Nimeona machukizo yako, naam, uzinifu wako, na ubembe wako, na uasherati wa ukahaba wako, juu ya milima katika mashamba. Ole wako, Ee Yerusalemu! Hutaki kutakaswa; mambo hayo yataendelea hata lini?

Yeremia 14


1 Neno la Bwana lililomjia Yeremia, katika habari ya ukosefu wa mvua.
2 Yuda huomboleza, Na malango yake yamelegea; Wameketi chini wamevaa kaniki; Na kilio cha Yerusalemu kimepaa juu.
3 Na wakuu wao huwatuma watoto wao kwenye maji; Nao hufika visimani wasione maji; Hurudi, na vyombo vyao ni vitupu; Wametahayarika na kufadhaika, Na kuvifunika vichwa vyao.
4 Kwa sababu ya nchi iliyopasuka, Kwa kuwa mvua haikunyesha katika nchi, Wenye kulima wametahayarika, Na kuvifunika vichwa vyao.
5 Naam, kulungu naye uwandani amezaa, Akamwacha mwanawe kwa kuwa hapana majani.
6 Na punda-mwitu husimama juu ya vilele vya milima, Hutwetea pumzi kama mbwa-mwitu; Macho yao hayaoni sawasawa, Kwa kuwa hapana majani.
7 Ijapokuwa maovu yetu yanatushuhudia, lakini utende wewe kwa ajili ya jina lako, Ee Bwana, maana kurudi nyuma kwetu ni kwingi; tumekutenda dhambi.
8 Wewe uliye tumaini la Israeli, wewe uliye Mwokozi wake wakati wa taabu, kwa nini wewe umekuwa kama mtu akaaye katika nchi, hali ya mgeni, na kama mtu mwenye kusafiri, ageukaye upande ili kukaa usiku mmoja tu?
9 Kwa nini wewe umekuwa kama mtu aliyesituka, kama shujaa asiyeweza kuokoa? Lakini wewe, Bwana, u katikati yetu, nasi tunaitwa kwa jina lako; usituache.
10 Bwana awaambia watu hawa hivi, Hivyo ndivyo walivyopenda kutanga-tanga; hawakuizuia miguu yao; basi, Bwana hawakubali; sasa ataukumbuka uovu wao, atawapatiliza dhambi zao.
11 Naye Bwana akaniambia, Usiwaombee watu hawa wapate heri.
12 Wafungapo, mimi sitasikia kilio chao; na watoapo sadaka za kuteketezwa na sadaka ya unga, sitazitakabali; bali nitawaangamiza kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni.
13 Ndipo nikasema, Aa, Bwana, MUNGU! Tazama, manabii huwaambia, Hamtauona upanga, wala hamtakuwa na njaa; bali nitawapa amani iliyo thabiti mahali hapa.
14 Ndipo Bwana akaniambia, Hao manabii wanatabiri uongo kwa jina langu mimi; mimi sikuwatuma, wala sikuwaamuru, wala sikusema nao; wanawapeni unabii wa maono ya uongo, na uaguzi, na neno la ubatili, na hadaa ya mioyo yao.
15 Basi, kwa hiyo Bwana asema hivi, Kwa habari za manabii wanaotabiri kwa jina langu, wala mimi sikuwatuma, lakini husema, Upanga na njaa havitaingia katika nchi hii; Kwa upanga na njaa manabii hao wataangamizwa.
16 Na watu hao, waliopewa unabii na wao, watatupwa nje katika njia kuu za Yerusalemu kwa sababu ya upanga na njaa; wala hawatakuwa na mtu wa kuwazika, wao na wake zao, na wana wao, na binti zao; maana nitamwaga uovu wao wenyewe juu yao.
17 Nawe utawaambia neno hili, Macho yangu na yatiririke machozi, usiku na mchana, wala yasikome; kwa maana bikira, binti ya watu wangu, amevunjika mavunjiko makuu, kwa jeraha isiyoponyeka.
18 Nikitoka kwenda shambani, tazama, wako huko waliouawa kwa upanga! Na nikiingia mjini, tazama, wamo humo wanaougua kwa sababu ya njaa! Maana nabii na kuhani, wote wawili, huenda huko na huko katika nchi, wala hawana maarifa.
19 Je! Umemkataa Yuda kabisa? Roho yako imeichukia Sayuni? Mbona umetupiga, tusiwe na dawa ya kutuponya? Tulitazamia amani, lakini hayakuja mema yo yote, tulitazamia wakati wa kupona, na tazama, kufadhaika tu!
20 Ee Bwana, tunakiri uovu wetu, na ubaya wa baba zetu; maana tumekutenda dhambi.
21 Usituchukie, kwa ajili ya jina lako; usikifedheheshe kiti cha enzi cha utukufu wako, kumbuka, usilivunje agano ulilofanya nasi.
22 Je! Katika vitu vya ubatili vya mataifa, kiko kitu kiwezacho kuleta mvua? Je! Mbingu zaweza kutoa manyunyu? Je! Si wewe, Ee Bwana, Mungu wetu? Kwa sababu hiyo tutakungoja; kwa kuwa wewe umevifanya vitu hivi vyote.

Yeremia 15


1 Ndipo Bwana akaniambia, Hata wangesimama mbele zangu Musa na Samweli, moyo wangu usingewaelekea watu hawa; watupe, watoke mbele za macho yangu, wakaende zao.
2 Kisha itakuwa, hapo watakapokuambia, Tutoke, tuende wapi? Utawaambia, Bwana asema hivi, Walioandikiwa kufa, watakwenda kufa; au kufa kwa upanga, watakufa kwa upanga; au kufa kwa njaa, watakufa kwa njaa, au kutekwa nyara, watakuwa mateka.
3 Nami nitaamrisha juu yao namna nne, asema Bwana; upanga uue, na mbwa wararue, na ndege wa angani, na wanyama wakali wa nchi, wale na kuangamiza.
4 Nami nitawafanya kuwa kitu cha kutisha katika falme zote za duniani, kwa sababu ya Manase, mwana wa Hezekia mfalme wa Yuda, kwa sababu ya mambo aliyoyatenda katika Yerusalemu.
5 Maana ni nani atakayekuhurumia, Ee Yerusalemu? Au ni nani atakayekulilia? Au ni nani atakayegeuka upande ili kuuliza habari za hali yako?
6 Umenikataa mimi, asema Bwana, umerudi nyuma; ndiyo maana nimenyosha mkono wangu juu yako, na kukuangamiza; nimechoka kwa kughairi.
7 Nami nimewapepea kwa kipepeo katika malango ya nchi nimewaondolea watoto wao, nimewaharibu watu wangu; hata hivyo hawakurudi na kuziacha njia zao.
8 Wajane wao wameongezeka kwangu kuliko mchanga wa bahari; nimeleta mwenye kuteka wakati wa adhuhuri juu ya mama wa vijana; nimeleta hamu na maogofyo yampate ghafula.
9 Mwanamke aliyezaa watoto saba anazimia; ametoa roho; jua lake limekuchwa, ungali ni wakati wa mchana; ametahayarika na kufedheheka; na mabaki yao nitawatoa kwa upanga mbele ya adui zao, asema Bwana.
10 Ole wangu, mama yangu, kwa kuwa umenizaa mtu wa kuteta, na mtu wa kushindana na dunia yote! Mimi sikukopesha kwa riba, wala watu hawakunikopesha kwa riba; lakini kila mmoja wao hunilaani.
11 Bwana akasema, Hakika nitakutia nguvu upate mema; hakika nitamlazimisha adui akusihi wakati wa uovu, na wakati wa taabu.
12 Je! Mtu aweza kuvunja chuma, naam, chuma kitokacho kaskazini, au shaba?
13 Mali yako na hazina zako nitazitoa kuwa nyara, bila kulipwa thamani yake; naam, kwa sababu ya dhambi zako zote, hata katika mipaka yako yote.
14 Nami nitakulazimisha kuwatumikia adui zako katika nchi usiyoijua; maana moto umewashwa katika hasira yangu, utakaowateketeza ninyi.
15 Ee Bwana, unajua wewe; unikumbuke, unijilie, ukanilipie kisasi juu yao wanaoniudhi; usiniondoe kwa uvumilivu wako; ujue ya kuwa ni kwa ajili yako nilivyopatikana na mashutumu.
16 Maneno yako yalionekana, nami nikayala; na maneno yako yalikuwa ni furaha kwangu, na shangwe ya moyo wangu; maana nimeitwa kwa jina lako, Ee Bwana, Mungu wa majeshi.
17 Sikuketi katika mkutano wao wanaojifurahisha, wala sikufurahi, naliketi peke yangu kwa sababu ya mkono wako; kwa maana umenijaza ghadhabu.
18 Mbona maumivu yangu ni ya daima, na jeraha yangu haina dawa, inakataa kuponywa? Je! Yamkini wewe utakuwa kwangu kama kijito kidanganyacho, na kama maji yasiyodumu?
19 Kwa sababu hiyo Bwana asema hivi, Ukirudi, ndipo mimi nitakapokurejeza, upate kusimama mbele zangu; nawe ukitoa kilicho cha thamani katika kilicho kibovu, utakuwa kama kinywa changu; nao watakurudia wewe, bali hutawarudia wao.
20 Nami nitakufanya kuwa kama ukuta wa boma la shaba juu ya watu hawa; nao watapigana nawe; lakini hawatakushinda; maana mimi nipo pamoja nawe, ili nikuokoe, na kukuponya, asema Bwana.
21 Nami nitakuokoa na mkono wa watu wabaya, nami nitakukomboa katika mkono wao wenye kutisha.

Yeremia 16


1 Tena neno la Bwana likanijia, kusema,
2 Wewe hutaoa mke, wala hutakuwa na wana wala binti mahali hapa.
3 Maana Bwana asema hivi, katika habari za wana, na katika habari za binti, wazaliwao mahali hapa, na katika habari za mama zao waliowazaa, na katika habari za baba zao waliowazaa, katika nchi hii;
4 watakufa kwa maradhi mabaya; hawataliliwa, wala hawatazikwa; watakuwa kama samadi juu ya uso wa nchi; nao wataangamizwa kwa upanga, na kwa njaa; na mizoga yao itakuwa chakula cha ndege wa angani, na cha wanyama wa nchi.
5 Maana Bwana asema hivi, Usiingie ndani ya nyumba yenye matanga, wala usiende kuwaombolezea, wala kuwalilia; maana nimewaondolea watu hawa amani yangu, asema Bwana, hata fadhili zangu na rehema zangu.
6 Wakubwa kwa wadogo wote pia watakufa katika nchi hii; hawatazikwa, wala watu hawatawalilia, wala kujikata-kata kwa ajili yao, wala kujinyoa kwa ajili yao;
7 wala watu hawatamega mkate kwa ajili yao, wakati wa kuomboleza, ili kuwafariji kwa ajili yao waliokufa; wala watu hawatawapa kikombe cha faraja, wanywe kwa ajili ya baba yao au mama yao.
8 Wala usiingie ndani katika nyumba yenye karamu, kuketi pamoja nao, na kula na kunywa.
9 Maana Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi, mbele ya macho yenu, na katika siku zenu, nitaikomesha sauti ya furaha, na sauti ya kicheko, mahali hapa; sauti ya bwana arusi, na sauti ya bibi arusi.
10 Tena itakuwa, utakapowaonyesha watu hawa maneno haya yote, nao wakakuambia, Mbona Bwana amenena juu yetu mabaya haya makuu? Uovu wetu ni uovu gani? Na dhambi yetu, tuliyomtenda Bwana, Mungu wetu, ni nini?
11 Ndipo utakapowaambia, Ni kwa sababu baba zenu wameniacha mimi, asema Bwana, na kuwafuata miungu mingine, na kuwatumikia, na kuwaabudu, wakaniacha mimi, wasiishike torati yangu;
12 na ninyi mmetenda mabaya kupita baba zenu; maana angalieni, mnaenenda kila mmoja wenu kwa ushupavu wa moyo wake mbaya, msinisikilize mimi;
13 basi, kwa sababu hiyo, nitawatoeni katika nchi hii, na kuwaingiza katika nchi ambayo hamkuijua, wala ninyi wala baba zenu; na huko mtawatumikia miungu mingine mchana na usiku; kwa maana mimi sitawapa fadhili zangu hata kidogo.
14 Kwa hiyo, angalia, siku zinakuja, asema Bwana, ambapo hawatasema tena, Aishivyo Bwana, aliyewaleta wana wa Israeli toka nchi ya Misri;
15 lakini, Aishivyo Bwana, aliyewaleta wana wa Israeli toka nchi ya kaskazini, na toka nchi zote alikowafukuza; nami nitawarudisha katika nchi yao wenyewe niliyowapa baba zao.
16 Tazama, asema Bwana, Nitatuma watu kuwaita wavuvi wengi, nao watawavua; na baada ya hayo nitatuma watu kuwaita wawindaji wengi, nao watawawinda, watoke katika kila mlima, na kila kilima, na pango za majabali.
17 Maana macho yangu yaziangalia njia zao zote, hawakufichwa uso wangu usiwaone, wala haukusitirika uovu wao macho yangu yasiuone.
18 Nami kwanza nitawalipa uovu wao na dhambi zao maradufu, kwa kuwa wameitia unajisi nchi yangu, kwa mizoga ya vitu vyao vichukizavyo, na kuujaza urithi wangu kwa machukizo yao.
19 Ee Bwana, nguvu zangu, ngome yangu, na kimbilio langu siku ya taabu, kwako wewe watakuja mataifa yote toka ncha za dunia, wakisema, Baba zenu hawakurithi kitu ila uongo, naam, ubatili na vitu visivyofaa.
20 Je! Mwanadamu ajifanyie miungu, wasio miungu?
21 Basi, tazama, nitawajulisha, mara moja hii nitawajulisha, mkono wangu, na nguvu zangu; nao watajua ya kuwa, jina langu ni YEHOVA.

Yeremia 17


1 Dhambi ya Yuda imeandikwa kwa kalamu ya chuma, na kwa ncha ya almasi; imechorwa katika kibao cha moyo wao, na katika pembe za madhabahu zenu;
2 na wakati huo watoto wao wazikumbuka madhabahu zao, na maashera yao, karibu na miti yenye majani mabichi juu ya milima mirefu.
3 Ee mlima wangu wa uwandani, nitatoa mali zako na hazina zako zote ziwe nyara, na mahali pako palipoinuka, kwa sababu ya dhambi, katika mipaka yako yote.
4 Nawe, naam, wewe nafsi yako, utaachana na urithi wako niliokupa; nami nitakulazimisha kuwatumikia adui zako katika nchi usiyoijua; maana umewasha moto katika hasira yangu, utakaowaka milele.
5 Bwana asema hivi, Amelaaniwa mtu yule amtegemeaye mwanadamu, Amfanyaye mwanadamu kuwa kinga yake Na moyoni mwake amemwacha Bwana.
6 Maana atakuwa kama fukara nyikani, Hataona yatakapotokea mema; Bali atakaa jangwani palipo ukame, Katika nchi ya chumvi isiyokaliwa na watu.
7 Amebarikiwa mtu yule anayemtegemea Bwana, Ambaye Bwana ni tumaini lake.
8 Maana atakuwa kama mti uliopandwa kando ya maji, Uenezao mizizi yake karibu na mto; Hautaona hofu wakati wa hari ujapo, Bali jani lake litakuwa bichi; Wala hautahangaika mwaka wa uchache wa mvua, Wala hautaacha kuzaa matunda.
9 Moyo huwa mdanganyifu kuliko vitu vyote, una ugonjwa wa kufisha; nani awezaye kuujua?
10 Mimi, Bwana, nauchunguza moyo, navijaribu viuno, hata kumpa kila mtu kiasi cha njia zake, kiasi cha matunda ya matendo yake.
11 Kama kware akusanyaye makinda asiyoyazaa, ndivyo alivyo mtu ajipatiaye mali, wala si kwa haki, katikati ya siku zake zitaachana naye, na mwisho wake atakuwa mpumbavu.
12 Kiti cha enzi, cha utukufu, kilichowekwa juu tangu mwanzo, ndicho mahali patakatifu petu.
13 Ee Bwana, tumaini la Israeli, wote wakuachao watatahayarika. Wao watakaojitenga nami wataandikwa katika mchanga, kwa sababu wamemwacha Bwana, kisima cha maji yaliyo hai.
14 Uniponye, Ee Bwana, nami nitaponyeka; uniokoe, nami nitaokoka; kwa maana wewe ndiwe uliye sifa zangu.
15 Tazama, wao waniambia, Neno la Bwana liko wapi? Na lije, basi.
16 Mimi hapa sikufanya haraka kuacha kuwa mchungaji nyuma yako; wala sikuitamani siku ya maradhi ya kufisha; wewe unajua; yaliyotoka midomoni mwangu yalikuwa mbele za uso wako.
17 Usiwe sababu ya hofu kuu kwangu mimi; wewe ndiwe uliye kimbilio langu siku ya uovu.
18 Na waaibike watu wanaoniudhi, lakini nisiaibike mimi; na waone hofu kuu, lakini mimi nisione hofu kuu; ulete juu yao siku ya uovu; uwaangamize maangamizo maradufu.
19 Bwana akaniambia hivi, Enenda ukasimame katika lango la wana wa watu hawa, waingiapo wafalme wa Yuda, na watokeapo, na katika malango yote ya Yerusalemu,
20 ukawaambie, Lisikieni neno la Bwana, enyi wafalme wa Yuda, na Yuda wote, nanyi wenyeji wote wa Yerusalemu, ninyi mwingiao kwa malango haya;
21 Bwana asema hivi, Jihadharini nafsi zenu, msichukue mzigo wo wote siku ya sabato, wala msiulete ndani kwa malango ya Yerusalemu;
22 wala msitoe mzigo katika nyumba zenu siku ya sabato, wala msifanye kazi yo yote; bali itakaseni siku ya sabato, kama nilivyowaamuru baba zenu;
23 lakini hawakusikiliza, wala hawakutega masikio yao, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, ili wasisikilize wala wasipokee mafundisho.
24 Na itakuwa, kama mkinisikiliza mimi kwa bidii, asema Bwana, msiingize mzigo wo wote kwa malango ya mji huu siku ya sabato, bali mkiitakasa siku ya sabato, bila kufanya kazi yo yote siku hiyo;
25 ndipo watakapoingia wafalme na wakuu kwa malango ya mji huu; wataketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kupanda magari na farasi, wao, na wakuu wao, watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu; na mji huu utakaa hata milele.
26 Nao watatoka miji ya Yuda, na mahali palipo pande zote za Yerusalemu, na nchi ya Benyamini, na Shefela, na milima,na upande wa Negebu,wakileta sadaka za kuteketezwa,na dhabihu,na sadaka za unga,na ubani,wakileta pia sadaka za shukurani,nyumbani kwa BWANA.
27 Lakini kama hamtaki kunisikiliza, kuitakasa siku ya sabato, kutokuchukua mzigo na kuingia kwa malango ya Yerusalemu siku ya sabato; basi, nitawasha moto malangoni mwake, nao utaziteketeza nyumba za enzi za Yerusalemu, wala hautazimika.

Yeremia 18


1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema,
2 Ondoka, ukashuke mpaka nyumba ya mfinyanzi, na huko nitakusikizisha maneno yangu.
3 Basi nikashuka mpaka nyumba ya mfinyanzi, na tazama, alikuwa akifanya kazi yake kwa magurudumu.
4 Na chombo kile, alichokuwa akikifinyanga, kilipoharibika mkononi mwake yule mfinyanzi, alikifanyiza tena kuwa chombo kingine, kama alivyoona vema yule mfinyanzi kukifanya.
5 Ndipo neno la Bwana likanijia, kusema,
6 Ee nyumba ya Israeli, je! Siwezi mimi kuwatendea ninyi vile vile kama mfinyanzi huyu alivyotenda? Asema Bwana. Angalieni, kama udongo ulivyo katika mkono wa mfinyanzi, ndivyo mlivyo ninyi katika mkono wangu, Ee nyumba ya Israeli.
7 Wakati wo wote nitakapotoa habari za taifa, na habari za ufalme, kuung'oa, na kuuvunja, na kuuangamiza;
8 ikiwa taifa lile nililolitaja litageuka, na kuacha maovu yake nitaghairi, nisitende mabaya yale niliyoazimia kuwatenda.
9 Na wakati wo wote nitakapotoa habari za taifa, na habari za ufalme, kuujenga na kuupanda,
10 ikiwa watatenda maovu mbele za macho yangu, wasiitii sauti yangu, basi nitaghairi, nisitende mema yale niliyoazimia kuwatendea.
11 Haya! Basi, ukawaambie watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, ukisema, Bwana asema hivi, Tazama, ninafinyanga mabaya juu yenu, na kuwaza mawazo juu yenu; rudini sasa, kila mmoja na aiache njia yake mbaya; zitengenezeni njia zenu, na matendo yenu.
12 Lakini wao wasema, Hapana tumaini lo lote; maana sisi tutafuata mawazo yetu wenyewe, nasi tutatenda kila mmoja wetu kwa kuufuata ushupavu wa moyo wake mbaya.
13 Basi, kwa ajili ya hayo, Bwana asema hivi, Ulizeni sasa katika mataifa, ni nani aliyesikia habari za mambo kama hayo; bikira wa Israeli ametenda tendo lichukizalo sana.
14 Je! Theluji ya Lebanoni itakoma katika jabali la kondeni? Au je! Maji ya baridi yashukayo toka mbali yatakauka?
15 Maana watu wangu wamenisahau, wameufukizia ubatili uvumba; nao wamewakaza katika njia zao, katika mapito ya zamani, ili wapite katika njia za kando, katika njia isiyotengenezwa;
16 ili kufanya nchi yao kuwa kitu cha kushangaza, na cha kuzomewa daima; kila mtu apitaye karibu nayo atashangaa, na kutikisa kichwa chake.
17 Nami nitawatawanya mbele ya adui, kama kwa upepo wa mashariki; nami nitaviangalia visogo vyao, wala si nyuso zao, siku ya msiba wao.
18 Hapo ndipo waliposema, Njoni na tufanye mashauri juu ya Yeremia; maana sheria haitampotea kuhani, wala shauri halitampotea mwenye hekima, wala neno halitampotea nabii. Njoni, na tumpige kwa ndimi zetu, wala tusiyaangalie maneno yake yo yote.
19 Niangalie, Ee Bwana, ukasikilize sauti ya wanaoshindana nami.
20 Je! Mabaya yalipwe badala ya mema? Maana wameichimbia nafsi yangu shimo. Kumbuka jinsi nilivyosimama mbele zako, ili niseme mema kwa ajili yao, nikaigeuze ghadhabu yako isiwapate.
21 Kwa sababu hiyo, uwatoe watoto wao waone njaa, uwatoe nguvu za upanga ziwapate; wake zao wafiwe na watoto wao, na kufiwa na waume zao; wanaume wao wauawe, na vijana wao wapigwe kwa upanga vitani.
22 Kilio na kisikiwe kitokacho katika nyumba zao, hapo utakapoleta kikosi juu yao kwa ghafula; kwa maana wamenichimbia shimo waninase, nao wameifichia miguu yangu mitego.
23 Lakini wewe, Bwana, unajua mashauri yao yote juu yangu, ya kuniua; usiwasamehe uovu wao, wala usifute dhambi yao mbele za macho yako; bali wakwazwe mbele zako; uwatende mambo wakati wa hasira yako.

Yeremia 19


1 Bwana akasema hivi, Enenda ukanunue gudulia la mfinyanzi, ukachukue pamoja nawe baadhi ya wazee wa watu, na baadhi ya wazee wa makuhani;
2 ukatoke uende mpaka bonde la mwana wa Hinomu lililo karibu na mahali pa kuingia kwa lango la vigae, ukahubiri huko maneno nitakayokuambia,
3 ukisema, Lisikieni neno la Bwana, enyi wafalme wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu; Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli asema hivi, Angalieni, nitaleta mabaya juu ya mahali hapa, ambayo mtu ye yote akisikia habari yake, masikio yake yatawaka.
4 Kwa sababu wameniacha mimi, nao wamepafanya mahali hapa kuwa mahali pageni, nao hapa wamewafukizia uvumba miungu mingine wasiowajua, wala wao, wala baba zao, wala wafalme wa Yuda; nao wamepajaza mahali hapa damu ya wasio na hatia;
5 nao wamemjengea Baali mahali pake palipo juu, ili kuwachoma moto wana wao, wawe sadaka za kuteketezwa kwa Baali; tendo nisiloliamuru mimi, wala kulinena, wala halikuingia moyoni mwangu;
6 basi, angalieni, siku zinakuja, asema Bwana, ambazo katika siku hizo mahali hapa hapataitwa tena Tofethi, wala Bonde la mwana wa Hinomu, bali, Bonde la Machinjo.
7 Nami nitalitangua shauri la Yuda na Yerusalemu mahali hapa; nami nitawaangusha kwa upanga mbele za adui zao, na kwa mkono wa watu watafutao roho zao; na mizoga yao nitawapa ndege wa angani na wanyama wakali wa nchi, iwe chakula chao.
8 Nami nitaufanya mji huu kuwa kitu cha kushangaza watu, na kuzomewa; kila mtu apitaye karibu nao atashangaa, na kuzomea kwa sababu ya mapigo yake.
9 Nami nitawalazimisha kula nyama ya wana wao, na nyama ya binti zao, nao watakula kila mmoja nyama ya rafiki yake, wakati wa mazingira na dhiki, ambayo adui zao, na watu wale watafutao roho zao, watawadhiikisha.
10 Ndipo hapo utalivunja gudulia lile, mbele ya macho ya watu wale waendao pamoja nawe,
11 na kuwaambia, Bwana wa majeshi asema hivi, Hivyo ndivyo nitakavyowavunja watu hawa, na mji huu, kama mtu avunjavyo chombo cha mfinyanzi, kisichoweza kutengenezwa tena na kuwa kizima; nao watazika watu katika Tofethi hata hapatabaki mahali pa kuzika.
12 Hivyo ndivyo nitakavyopatenda mahali hapa, asema Bwana, nao wakaao humo, hata kufanya mji huu kuwa kama Tofethi;
13 na nyumba za Yerusalemu, na nyumba za wafalme wa Yuda, zilizotiwa unajisi, zitakuwa kama mahali pa Tofethi; naam, nyumba zote ambazo juu ya dari zake wamelifukizia uvumba jeshi lote la mbinguni, na kuwamiminia miungu mingine sadaka za kunywewa.
14 Kisha Yeremia akatoka huko Tofethi, huko ambako Bwana alimtuma atoe unabii; naye akasimama katika ua wa nyumba ya Bwana, akawaambia watu wote,
15 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitaleta juu ya mji huu, na juu ya vijiji vyake vyote, mabaya yote niliyoyanena juu yake; kwa sababu wamefanya shingo zao kuwa ngumu, kusudi wasiyasikie maneno yangu.

Yeremia 20


1 Basi Pashuri, mwana wa Imeri, kuhani, aliyekuwa msimamizi mkuu katika nyumba ya Bwana, alimsikia Yeremia alipokuwa akitabiri maneno hayo.
2 Ndipo Pashuri akampiga Yeremia, nabii, akamtia katika mkatale, uliokuwa pale penye lango la juu la Benyamini, lililokuwa katika nyumba ya Bwana.
3 Hata ikawa, asubuhi, Pashuri huyo akamtoa Yeremia katika mkatale. Ndipo Yeremia akamwambia, Bwana hakukuita jina lako Pashuri, bali Magor-misabibu.
4 Maana Bwana asema hivi, Tazama, nitakufanya kuwa hofu kuu kwa nafsi yako, na kwa rafiki zako wote; nao wataanguka kwa upanga wa adui zao, na macho yako yataona hayo; nami nitatia Yuda yote katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atawachukua mateka mpaka Babeli, na kuwaua kwa upanga.
5 Tena mali zote za mji huu, na mapato yake yote, na vitu vyake vya thamani vyote pia, naam, hazina zote za wafalme wa Yuda, nitavitia katika mikono ya adui zao, watakaowateka nyara, na kuwakamata, na kuwachukua mpaka Babeli.
6 Na wewe, Pashuri, na watu wote wanaokaa katika nyumba yako, mtakwenda utumwani; nawe utafika Babeli, na huko utakufa, na huko utazikwa, wewe, na rafiki zako wote, uliowatabiria maneno ya uongo.
7 Ee Bwana, umenihadaa, nami nimehadaika; wewe una nguvu kuliko mimi, ukashinda; nimekuwa kitu cha kuchekesha, mchana kutwa; kila mtu hunidhihaki.
8 Maana kila ninenapo napiga kelele, nalia, Dhuluma na uharibifu! Kwa kuwa neno la Bwana limefanywa shutumu kwangu, na dhihaka, mchana kutwa.
9 Nami nikisema, Sitamtaja, wala sitasema tena kwa jina lake; basi, ndipo moyoni mwangu kumekuwamo kama moto uwakao, uliofungwa ndani ya mifupa yangu, nami nimechoka kwa kustahimili, wala siwezi kujizuia.
10 Maana nimesikia mashutumu ya watu wengi; hofu ziko pande zote. Rafiki zangu wote, wanaonivizia nisite, husema, Mshitaki, nasi tutamshitaki, huenda akahadaika, nasi tutamshinda, tutajilipiza kisasi kwake.
11 Lakini Bwana yu pamoja nami, mfano wa shujaa mwenye kutisha; kwa hiyo hao wanaonionea watajikwaa, wala hawatashinda; watatahayarika sana. Kwa sababu hawakutenda kwa akili, wataona aibu ya milele, ambayo haitasahauliwa kamwe.
12 Lakini, Ee Bwana wa majeshi, wewe wawajaribu wenye haki, waona viuno na mioyo, nijalie kuona kisasi chako juu yao; kwa maana nimekufunulia wewe neno langu.
13 Mwimbieni Bwana; msifuni Bwana; Kwa maana ameiponya roho ya mhitaji Katika mikono ya watu watendao maovu.
14 Na ilaaniwe siku niliyozaliwa, isibarikiwe siku ile aliyonizaa mama yangu.
15 Na alaaniwe mtu yule aliyemletea baba yangu habari, akisema, Umezaliwa mtoto mwanamume; akimfurahisha.
16 Mtu huyo na awe kama miji ile, ambayo Bwana aliiangamiza, asijute; na asikie kilio asubuhi, na kelele za fujo adhuhuri;
17 kwa sababu hakuniua nilipotoka tumboni, na hivyo mama yangu angekuwa kaburi langu, na mimba yake sikuzote nzito.
18 Nalitoka tumboni kwa sababu gani, kuona taabu na huzuni, hata siku zangu ziharibike katika aibu?

Yeremia 21


1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, hapo mfalme Sedekia alipompelekea Pashuri, mwana wa Malkiya, na Sefania, mwana wa Maaseya, kuhani, kusema,
2 Tafadhali utuulizie habari kwa Bwana; kwa maana Nebukadreza, mfalme wa Babeli, analeta vita juu yetu; labda Bwana atatutendea sawasawa na kazi zake zote za ajabu, ili aende zake akatuache.
3 Basi Yeremia akawaambia, Mwambieni Sedekia neno hili,
4 Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Angalieni, nitazigeuza nyuma silaha za vita zilizo mikononi mwenu, ambazo kwa hizo ninyi mnapigana na mfalme wa Babeli, na Wakaldayo, wanaowahusuru nje ya kuta zenu, nami nitazikusanya pamoja katikati ya mji huu.
5 Na mimi mwenyewe nitapigana nanyi, kwa mkono ulionyoshwa na kwa mkono hodari, naam, kwa hasira, na kwa ukali, na kwa ghadhabu nyingi.
6 Nami nitawapiga wenyeji wa mji huu, wanadamu na wanyama pia; watakufa kwa tauni kubwa.
7 Na baada ya hayo, asema Bwana, nitamtia Sedekia, mfalme wa Yuda, na watumishi wake, na watu wote waliosalia ndani ya mji huu, baada ya tauni ile, na upanga, na njaa, katika mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na katika mikono ya adui zao, na katika mikono ya watu wale wanaowatafuta roho zao; naye atawaua kwa ukali wa upanga; hatawaachilia, wala hatawahurumia, wala hatawarehemu.
8 Nawe waambie watu hawa, Bwana asema hivi, Tazama naweka mbele yenu njia ya uzima, na njia ya mauti.
9 Yeye atakayekaa katika mji huu atakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; bali yeye atakayetoka, na kujitia pamoja na Wakaldayo wanaowahusuru, yeye ataishi, na maisha yake yatakuwa nyara kwake.
10 Maana nimeweka uso wangu juu ya mji huu niuletee mabaya, wala nisiuletee mema, asema Bwana; utatiwa katika mkono wa mfalme wa Babeli, naye atauteketeza.
11 Na katika habari za nyumba ya mfalme wa Yuda, lisikieni neno la Bwana,
12 Ee nyumba ya Daudi, Bwana asema hivi, Hukumuni hukumu ya haki asubuhi, mkawaponye waliotekwa nyara na mkono wake aliyewadhulumu, ghadhabu yangu isije ikatoka kama moto, ikaunguza, asiweze mtu ye yote kuuzima, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu.
13 Tazama, mimi ni juu yako, Ewe ukaaye bondeni, na kwenye jabali la uwandani, asema Bwana ninyi mnaosema, Ni nani atakayeshuka apigane nasi? Au, Ni nani atakayeingia katika makao yetu?
14 Nami nitawaadhibu kwa kadiri ya matunda ya matendo yenu, asema Bwana; nami nitawasha moto katika msitu wake, nao utateketeza vitu vyote viuzungukavyo.

Yeremia 22


1 Bwana akasema hivi, Shuka nyumbani kwa mfalme wa Yuda, ukaseme neno hili huko,
2 ya kwamba, Sikia neno la Bwana, Ee mfalme wa Yuda; wewe uketiye katika kiti cha enzi cha Daudi, wewe, na watumishi wako, na watu wako wote waingiao kwa malango haya;
3 Bwana asema hivi, Fanyeni hukumu na haki, mkamtoe yeye aliyetekwa katika mikono ya mdhalimu; wala msiwatende mabaya mgeni, wala yatima, wala mjane, wala kuwadhulumu, wala msimwage damu ya mtu asiye na hatia katika mahali hapa.
4 Kwa maana mkifanya haya kweli kweli, ndipo watakapoingia kwa malango ya nyumba hii wafalme wenye kuketi katika kiti cha enzi cha Daudi, wanakwenda kwa magari, na wamepanda farasi yeye, na watumishi wake, na watu wake.
5 Lakini kama hamtaki kusikia maneno haya, mimi naapa kwa nafsi yangu, asema Bwana, ya kuwa nyumba hii itakuwa ukiwa.
6 Kwa maana Bwana asema hivi, katika habari ya nyumba ya mfalme wa Yuda; Wewe u Gileadi kwangu, na kichwa cha Lebanoni; Ila hakika nitakufanya kuwa jangwa, na miji isiyokaliwa na watu.
7 Nami nitakufanyia tayari watu wenye kuharibu, kila mtu na silaha zake; Nao watakata mierezi miteule yako, na kuitupa motoni.
8 Na mataifa mengi watapita karibu na mji huu, nao watasema kila mtu na jirani yake, Nini maana yake Bwana kuutenda hivi mji huu mkubwa?
9 Ndipo watakapojibu, Ni kwa sababu waliliacha agano la Bwana, Mungu wao, wakaabudu miungu mingine, na kuitumikia.
10 Msimlilie aliyekufa, wala msimwombolezee, Bali mlilieni huyo aendaye zake mbali; Kwa maana yeye hatarudi tena, Wala hataiona nchi aliyozaliwa.
11 Maana Bwana asema hivi, katika habari za Shalumu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; aliyemiliki badala ya Yosia, baba yake, yeye aliyetoka mahali hapa; Hatarudi huku tena;
12 bali katika mahali pale walipomchukua mateka ndipo atakapokufa, wala hataiona nchi hii tena kamwe.
13 Ole wake aijengaye nyumba yake kwa uovu! Na vyumba vyake kwa udhalimu! Atumiaye utumishi wa mwenzake bila ujira, Wala hampi mshahara wake;
14 Asemaye, Nitajijengea nyumba pana na vyumba vipana; Naye hujikatia madirisha; Na kuta zake zimefunikwa kwa mierezi, Na kupakwa rangi nyekundu.
15 Je! Utatawala kwa sababu unashindana na watu kwa mierezi? Baba yako, je! Hakula na kunywa, na kufanya hukumu na haki? Hapo ndipo alipofanikiwa.
16 Alihukumu maneno ya maskini na mhitaji; hapo ndipo alipofanikiwa. Je! Huku siko kunijua, asema Bwana?
17 Bali macho yako na moyo wako hauna utakalo ila kutamani, na kumwaga damu isiyo na hatia, na kudhulumu, na kutenda jeuri.
18 Basi, Bwana asema hivi, katika habari ya Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda; Hawatamwombolezea, wakisema, Aa! Ndugu yangu; au, Aa! Dada yangu; wala hawatamlilia, wakisema, Aa! Bwana wangu; au, Aa! Utukufu wake.
19 Atazikwa maziko ya punda, akibururwa, na kutupwa nje ya malango ya Yerusalemu.
20 Haya panda Lebanoni, ukalie Upalize sauti yako katika Bashani; Ukalie kutoka Abarimu; Maana wapenzi wako wote wameangamia.
21 Mimi nalisema nawe wakati wa kufanikiwa kwako; lakini ulisema, Sitaki kusikia. Hii ndiyo iliyokuwa desturi yako tangu ujana wako, kutokuitii sauti yangu.
22 Upepo utawalisha wachungaji wako wote, na wapenzi wako watakwenda kufungwa; hakika wakati huo utatahayarika, na kufadhaika kwa sababu ya uovu wako wote.
23 Wewe ukaaye Lebanoni, Ufanyaye kioto chako katika mierezi, Utakuwa na hali ya kuhurumiwa sana, Upatapo utungu kama wa mwanamke azaaye.
24 Kama niishivyo mimi, asema Bwana, hata Konia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, angekuwa pete yenye muhuri katika mkono wangu wa kuume, ningekung'oa wewe hapo;
25 nami nitakutia katika mikono ya watu wale wakutafutao roho yako, na katika mikono yao unaowaogopa, naam, katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na katika mikono ya Wakaldayo.
26 Nami nitakutupa nje, wewe na mama yako aliyekuzaa, mwende nchi nyingine ambayo hamkuzaliwa huko, nanyi mtakufa huko.
27 Lakini nchi ile ambayo wanatamani kuirudia, hawatairudia kamwe.
28 Je! Mtu huyu, Konia, ni chombo kilichodharauliwa, na kuvunjika? Ni chombo kisichopendeza? Mbona wametupwa, yeye na wazao wake, na kutupwa katika nchi wasiyoijua?
29 Ee nchi, nchi, nchi, lisikie neno la Bwana.
30 Bwana asema hivi, Andikeni habari za mtu huyu kwamba hana watoto, kwamba mtu huyu hatafanikiwa siku zake zote; maana hapana mtu katika wazao wake atakayefanikiwa, akiketi katika kiti cha enzi cha Daudi, na kutawala tena katika Yuda.

Yeremia 23


1 Ole wao wachungaji, wanaoharibu kondoo za malisho yangu na kuwatawanya! Asema Bwana.
2 Kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, juu ya wachungaji wanaowalisha watu wangu, Mmetawanya kundi langu, na kuwafukuza, wala hamkwenda kuwatazama; angalieni, nitawapatiliza uovu wa matendo yenu, asema Bwana.
3 Nami nitakusanya mabaki ya kundi langu, katika nchi zile zote nilizowafukuza, nami nitawaleta tena mazizini mwao; nao watazaa na kuongezeka.
4 Nami nitaweka juu yao wachungaji watakaowalisha; wala hawataona hofu tena, wala kufadhaika, wala hatapotea hata mmoja wao, asema Bwana.
5 Tazama siku zinakuja, asema Bwana, nitakapomchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atamiliki mfalme, atatenda kwa hekima, naye atafanya hukumu na haki katika nchi.
6 Katika siku zake Yuda ataokolewa, na Israeli atakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu.
7 Kwa hiyo, angalia, siku zinakuja, asema Bwana, ambapo hawatasema tena, Aishivyo Bwana, aliyewatoa wana wa Israeli katika nchi ya Misri;
8 lakini, Aishivyo Bwana, aliyewapandisha na kuwaongoza wazao wa nyumba ya Israeli kutoka nchi ya kaskazini, na kutoka nchi zote nilikowafukuza; nao watakaa katika nchi yao wenyewe.
9 Katika habari za manabii. Moyo wangu ndani yangu umevunjika, Mifupa yangu yote inatikisika. Nimekuwa kama mtu aliye mlevi, Na kama mtu aliyeshindwa na divai;kwa ajili ya Bwana,na kwa ajili ya maneno yake matakatifu.
10 Maana nchi imejaa wazinzi; kwa sababu ya kuapa nchi inaomboleza; malisho ya nyikani yamekauka; mwenendo wao ni mbaya, na nguvu zao si za haki.
11 Maana nabii, na kuhani, wote wawili wanakufuru; naam, katika nyumba yangu nimeuona uovu wao, asema Bwana.
12 Kwa ajili ya hayo njia yao itakuwa kwao kama mahali pa kuteleza gizani; watatelemshwa na kuanguka hapo; kwa maana nitaleta uovu juu yao, naam, mwaka wa kujiliwa kwao, asema Bwana.
13 Nami nimeona upumbavu katika manabii wa Samaria; walitabiri kwa Baali, wakawakosesha watu wangu Israeli.
14 Katika manabii wa Yerusalemu nimeona neno linalochukiza sana; hufanya zinaa; huenenda katika maneno ya uongo, hutia nguvu mikono ya watendao maovu, hata ikawa hapana mtu arejeaye na kuuacha uovu wake; wote pia wamekuwa kama Sodoma kwangu, na wenyeji wake kama Gomora.
15 Basi Bwana wa majeshi asema hivi, katika habari ya manabii, Tazama, nitawalisha pakanga, nitawanywesha maji ya uchungu; kwa kuwa kutoka kwa manabii hao wa Yerusalemu kukufuru kumeingia katika nchi yote.
16 Bwana wa majeshi asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wakiwatabiria; huwafundisha ubatili; hunena maono ya mioyo yao wenyewe; hayakutoka katika kinywa cha Bwana.
17 Daima huwaambia wao wanaonidharau, Bwana amesema, Mtakuwa na amani; nao humwambia kila mtu aendaye kwa ukaidi wa moyo wake, Hamtapatwa na ubaya wo wote.
18 Maana, ni nani aliyesimama katika baraza la Bwana, hata akalifahamu neno lake na kulisikia? Ni nani aliyelitia moyoni neno langu, na kulisikia?
19 Tazama, tufani ya Bwana, yaani, ghadhabu yake, imetokea; ni dhoruba ya kisulisuli; itapasuka, na kuwaangukia waovu vichwani.
20 Hasira ya Bwana haitarudi, hata atakapokwisha kuyatimiza makusudi ya moyo wake; katika siku za mwisho mtalifahamu neno hili kabisa.
21 Mimi sikuwatuma manabii hao, lakini walikwenda mbio; sikusema nao, lakini walitabiri.
22 Lakini kama wangalisimama katika baraza yangu, ndipo wangaliwasikizisha watu wangu maneno yangu, na kuwageuza waziache njia zao mbaya, na uovu wa matendo yao.
23 Mimi ni Mungu aliye karibu, asema Bwana, mimi si Mungu aliye mbali.
24 Je, mtu ye yote aweza kujificha mahali pa siri, nisimwone? Asema Bwana. Je! Mbingu na nchi hazikujawa nami? Asema Bwana.
25 Nimesikia waliyoyasema manabii wanaotabiri uongo kwa jina langu, wakisema, Nimeota ndoto; nimeota ndoto.
26 Je! Mambo hayo yatakuwa katika mioyo ya manabii wanaotabiri uongo hata lini, manabii hao wenye udanganyifu katika mioyo yao wenyewe?
27 Wanaodhania ya kuwa watawasahaulisha watu wangu jina langu kwa ndoto zao, wanazomhadithia kila mtu jirani yake, kama vile baba zao walivyolisahau jina langu, kwa ajili ya Baali.
28 Nabii aliye na ndoto, na aseme ndoto yake; na yeye aliye na neno langu, na aseme neno langu kwa uaminifu. Makapi ni kitu gani kuliko ngano? Asema Bwana.
29 Je! Neno langu si kama moto? Asema Bwana; na kama nyundo ivunjayo mawe vipande vipande?
30 Basi kwa sababu hiyo mimi ni juu ya manabii hao, asema Bwana, wanaompokonya kila mtu jirani yake maneno yangu.
31 Tazama, mimi ni juu ya manabii, asema Bwana, wanaotumia ndimi zao na kusema, Yeye asema,
32 Tazama, mimi ni juu ya hao wanaotabiri ndoto za uongo, asema Bwana, na kuzisema, na kuwakosesha watu wangu kwa uongo wao, na kwa majivuno yao ya upuzi, lakini mimi sikuwatuma, wala sikuwapa amri; wala hawatawafaidia watu hawa hata kidogo, asema Bwana.
33 Na watu hawa, au nabii au kuhani, atakapokuuliza, akisema, Mzigo wa Bwana ni nini? Ndipo utawaambia, Mzigo gani? Bwana asema, Nitawatupilia mbali.
34 Na katika habari ya nabii, na kuhani, na watu, watakaosema, Mzigo wa Bwana, mimi nitamwadhibu mtu yule, na nyumba yake.
35 Mtasema hivi kila mtu na jirani yake, na kila mtu na ndugu yake, Bwana amejibu mtu? Na, Bwana amesemaje?
36 Na mzigo wa Bwana hamtautaja tena; maana neno la kila mtu ndilo litakalokuwa mzigo wake; maana ninyi mmeyapotosha maneno ya Mungu aliye hai, ya Bwana wa majeshi, Mungu wetu.
37 Nawe utamwambia nabii hivi, Bwana amekujibu nini? Na, Bwana amesemaje?
38 Lakini mkisema, Mzigo wa Bwana, basi, Bwana asema hivi, Kwa sababu mwasema neno hili, (Mzigo wa Bwana); nami nimemtuma mtu kwenu kusema, Msiseme, (Mzigo wa Bwana);
39 basi, kwa hiyo angalieni, nitawasahau ninyi kabisa, nami nitawatupilia mbali, pamoja na mji huu niliowapa ninyi na baba zenu, mtoke mbele za uso wangu;
40 nami nitaleta juu yenu aibu ya milele, na fedheha ya daima, ambayo haitasahauliwa.

Yeremia 24


1 Bwana akanionyesha, na tazama, vikapu viwili vya tini, vimewekwa mbele ya hekalu la Bwana, baada ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, kumchukua mateka Yekonia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, na wakuu wa Yuda, pamoja na mafundi na wafua chuma, kutoka Yerusalemu, kuwaleta Babeli.
2 Kikapu kimoja kilikuwa na tini nzuri sana, kama tini zilizotangulia kuiva; na kikapu cha pili kilikuwa na tini mbovu sana zisizoweza kuliwa, kwa kuwa zilikuwa mbovu sana.
3 Ndipo Bwana akaniambia, Unaona nini Yeremia? Nikasema, Naona tini; tini nzuri zilizo nzuri sana; na tini mbovu zilizo mbovu sana, zisizoweza kuliwa, kwa kuwa ni mbovu sana.
4 Kisha neno la Bwana likanijia, kusema,
5 Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama zilivyo tini hizi nzuri, ndivyo nitakavyowaangalia mateka wa Yuda, niliowatoa katika mahali hapa, waende mpaka nchi ya Wakaldayo, wapate mema.
6 Kwa maana nitawatulizia macho yangu, wapate mema, nami nitawaingiza katika nchi hii tena; nami nitawajenga, wala sitawabomoa; nitawapanda wala sitawang'oa.
7 Nami nitawapa moyo, wanijue ya kuwa mimi ni Bwana; nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao; kwa maana watanirudia kwa moyo wao wote.
8 Na habari za tini zile mbovu, zisizoweza kuliwa, kwa kuwa ni mbovu sana; hakika, asema, Bwana, ndivyo nitakavyomtoa Sedekia, mfalme wa Yuda, na wakuu wake, na mabaki ya Yerusalemu, waliosalia katika nchi hii, na hao wanaokaa katika nchi ya Misri.
9 Naam, nitawatoa watupwe huko na huko katika falme zote za dunia, wapate mabaya; wawe kitu cha kulaumiwa, na mithali, na dhihaka, na laana, katika mahali pote nitakapowafukuza.
10 Nami nitatuma upanga, na njaa, na tauni, kati yao, hata watakapopotelea mbali katika nchi niliyowapa, wao na baba zao.

Yeremia 25


1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, katika habari za watu wote wa Yuda; katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda mwaka ule ndio mwaka wa kwanza wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli;
2 ambalo Yeremia, nabii, aliwaambia watu wote wa Yuda, na wenyeji wote wa Yerusalemu, kusema,
3 Tangu mwaka wa kumi na tatu wa kutawala kwake Yosia, mwana wa Amoni, mfalme wa Yuda, hata siku hii ya leo, miaka hii ishirini na mitatu, neno la Bwana limenijia, nami nimesema nanyi, nikiamka mapema na kusema; lakini ninyi hamkusikiliza.
4 Naye Bwana ametuma kwenu watumishi wake wote, hao manabii, akiamka mapema na kuwatuma, lakini ninyi hamkusikiliza, wala hamkutega masikio yenu, msikilize.
5 Akasema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya; uacheni uovu wa matendo yenu, mkae katika nchi ambayo Bwana aliwapa, ninyi na baba zenu, tangu zamani za kale na hata milele;
6 wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia na kuwasujudia, wala msinikasirishe kwa kazi ya mikono yenu; basi, mimi sitawadhuru ninyi kwa dhara lo lote.
7 Lakini ninyi hamkunisikiliza, asema Bwana; ili mnikasirishe kwa kazi ya mikono yenu, na kujidhuru nafsi zenu.
8 Basi Bwana wa majeshi asema hivi, Kwa kuwa hamkuyasikiliza maneno yangu,
9 angalieni, nitapeleka watu na kuzitwaa jamaa zote za upande wa kaskazini, asema Bwana, nami nitatuma ujumbe kwa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu, nami nitawaleta juu ya nchi hii, na juu yao wakaao ndani yake, na juu ya mataifa haya yote yaliyopo pande zote; nami nitawaangamiza kabisa, na kuwafanya kitu cha kushangaza, na kitu cha kuzomewa, na ukiwa wa daima.
10 Tena, nitawaondolea sauti ya kicheko, na sauti ya furaha, sauti ya bwana arusi, na sauti ya bibi arusi, sauti ya mawe ya kusagia, na nuru ya mishumaa.
11 Na nchi hii yote pia itakuwa ukiwa, na kitu cha kushangaza; nayo mataifa haya watamtumikia mfalme wa Babeli miaka sabini.
12 Na itakuwa miaka hiyo sabini itakapotimia, nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na taifa lile, asema Bwana, kwa sababu ya uovu wao, nayo nchi ya Wakaldayo pia; nami nitaifanya kuwa ukiwa wa milele.
13 Nami nitaleta juu ya nchi ile maneno yangu yote niliyoyanena juu yake, naam, yote yaliyoandikwa ndani ya kitabu hiki, aliyotabiri Yeremia juu ya mataifa haya yote.
14 Kwa maana mataifa mengi na wafalme wakuu watawatumikisha; naam, hao pia; nami nitawalipa kwa kadiri ya matendo yao, na kwa kadiri ya kazi ya mikono yao.
15 Maana Bwana, Mungu wa Israeli, aniambia hivi, Pokea kikombe cha divai ya ghadhabu hii mkononi mwangu, ukawanyweshe mataifa yote, ambao nitakupeleka kwao;
16 nao watakunywa, na kulewalewa, na kufanya wazimu, kwa sababu ya upanga nitakaoupeleka kati yao.
17 Ndipo nikakipokea kikombe kile mkononi mwa Bwana, nikawanywesha mataifa yote, ambao Bwana alinipeleka kwao;
18 yaani, Yerusalemu, na miji ya Yuda, na wafalme wake, na wakuu wake, ili kuwafanya kuwa ukiwa, na ajabu, na mazomeo, na laana; vile vile kama ilivyo leo;
19 Farao, mfalme wa Misri, na watumishi wake na wakuu wake na watu wake wote;
20 na watu wote waliochanganyika pamoja, na wafalme wote wa nchi ya Uzi, na wafalme wote wa nchi ya Wafilisti, na Ashkeloni, na Gaza, na Ekroni, na mabaki ya Ashdodi;
21 Edomu, na Moabu, na wana wa Amoni;
22 na wafalme wote wa Tiro, na wafalme wote wa Sidoni, na wafalme wote wa kisiwa kilicho ng'ambo ya pili ya bahari;
23 Dedani, na Tema, na Buzi, na watu wote wakatao denge;
24 na wafalme wote wa Arabuni, na wafalme wote wa watu waliochanganyika wakaao jangwani;
25 na wafalme wote wa Zimri, na wafalme wote wa Elamu, na wafalme wote wa Wamedi;
26 na wafalme wote wa kaskazini, walio mbali na walio karibu, wote pamoja; na wafalme wote wa dunia, wakaao juu ya uso wa dunia; na mfalme wa Sheshaki atakunywa baada yao.
27 Nawe utawaambia hivi, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nyweni, na kulewa, na kutapika, na kuanguka msiinuke tena, kwa sababu ya upanga nitakaoupeleka kati yenu.
28 Tena itakuwa, kama wakikataa kukipokea kikombe kile mkononi mwako, wanywe, ndipo utakapowaambia, Bwana wa majeshi asema hivi, Lazima mtakunywa.
29 Maana angalieni, ninaanza kutenda mabaya katika mji uitwao kwa jina langu, je! Mtaachiliwa ninyi msiadhibiwe? Hamtaachiliwa msiadhibiwe; kwa maana nitauita upanga ule uwapige wote wakaao katika dunia, asema Bwana wa majeshi.
30 Basi, tabiri wewe maneno haya yote juu yao, na kuwaambia, Bwana atanguruma toka juu, Naye atatoa sauti yake toka patakatifu pake; Atanguruma sana juu ya zizi lake; Atapiga kelele kama mtu akanyagaye zabibu, Juu ya wenyeji wote wa dunia.
31 Mshindo utafika hata mwisho wa dunia; Maana Bwana ana mashindano na mataifa, Atateta na watu wote wenye mwili; Na waovu atawatoa wauawe kwa upanga; asema Bwana.
32 Bwana wa majeshi asema hivi, Tazama, uovu utatokea toka taifa hata taifa, na tufani kuu itainuliwa toka pande za mwisho wa dunia.
33 Na waliouawa na Bwana siku ile watakuwapo, toka upande mmoja wa dunia hata upande wa pili; hawataliliwa, wala kukusanywa, wala kuzikwa; watakuwa samadi juu ya uso wa nchi.
34 Pigeni yowe, enyi wachungaji, na kulia; na kugaagaa katika majivu, enyi mlio hodari katika kundi; maana siku za kuuawa kwenu zimetimia kabisa, nami nitawavunja vipande vipande, nanyi mtaanguka kama chombo cha anasa.
35 Nao wachungaji watakuwa hawana njia ya kukimbia, wala walio hodari katika kundi hawataokoka.
36 Sauti ya kilio cha wachungaji, na sauti ya kupiga yowe kwao walio hodari katika kundi, kwa maana Bwana anayaharibu malisho yao.
37 Na mazizi yenye amani yamenyamazishwa, kwa sababu ya hasira kali ya Bwana.
38 Ameacha mahali pake pa kujificha, kama simba; maana nchi yao imekuwa kitu cha kushangaza, kwa sababu ya ukali wa upanga uoneao, na kwa sababu ya hasira yake kali.

Yeremia 26


1 Mwanzo wa kumiliki kwake Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili lilitoka kwa Bwana, kusema,
2 Bwana asema hivi, Simama katika uwanja wa nyumba ya Bwana, useme na miji yote ya Yuda, wajao ili kuabudu katika nyumba ya Bwana; sema nao maneno yote ninayokuamuru kuwaambia, usizuie hata neno moja.
3 Labda watasikia, na kughairi na kuacha kila mtu njia yake mbaya; ili niyaghairi mabaya niliyokusudia kuwatenda, kwa sababu ya uovu wa matendo yao.
4 Nawe utawaambia, Bwana asema hivi, Kama hamtaki kunisikia, kwenda katika sheria yangu, niliyoiweka mbele yenu,
5 kuyasikiliza maneno ya watumishi wangu, manabii, ninaowatuma kwenu, naam, nikiondoka mapema na kuwatuma; lakini ninyi hamkuwasikiliza;
6 basi, nitafanya nyumba hii kuwa kama Shilo, na mji huu nitaufanya kuwa laana kwa taifa zote za dunia.
7 Na makuhani, na manabii, na watu wote, wakamsikia Yeremia, hapo aliposema maneno haya katika nyumba ya Bwana.
8 Ikawa, Yeremia alipokuwa amekwisha kusema maneno yote Bwana aliyomwamuru kuwaambia watu wote, ndipo hao makuhani, na manabii, na watu wote, wakamkamata, wakisema, Bila shaka utakufa.
9 Kwa nini umetabiri kwa jina la Bwana, ukisema, Nyumba hii itakuwa kama Shilo, na mji huu utakuwa ukiwa, hautakaliwa na mtu? Watu wote wakamkusanyikia Yeremia katika nyumba ya Bwana.
10 Na wakuu wa Yuda waliposikia habari za mambo haya, wakatoka katika nyumba ya mfalme, wakapanda juu mpaka nyumbani kwa Bwana; wakaketi, hapo watu waingiapo katika lango jipya la nyumba ya Bwana.
11 Ndipo hapo makuhani, na manabii, wakawaambia wakuu na watu wote, wakisema, Mtu huyu amestahili kufa, kwa sababu ametabiri juu ya mji huu, kama mlivyosikia kwa masikio yenu.
12 Ndipo Yeremia akawaambia wakuu wote na watu wote, akisema, Bwana ndiye aliyenituma kutabiri juu ya nyumba hii, na juu ya mji huu, maneno hayo yote mliyoyasikia.
13 Basi sasa, tengenezeni njia zenu, na matendo yenu, mkaisikilize sauti ya Bwana, Mungu wenu; naye Bwana atayaghairi mabaya aliyoyanena juu yenu.
14 Lakini kwangu mimi, tazama, mimi nipo hapa mikononi mwenu; nitendeni myaonayo kuwa mema na haki mbele ya macho yenu.
15 Lakini jueni yakini ya kuwa, mkiniua, mtajiletea juu yenu damu isiyo na hatia itakuwa juu yenu, na juu ya mji huu, na juu ya wenyeji wake; kwa maana ni kweli Bwana amenituma kwenu, kuwaambieni yote mliyoyasikia.
16 Ndipo wakuu na watu wote wakawaambia makuhani, na manabii, wakisema, Mtu huyu hastahili kuuawa; kwa maana amesema nasi katika jina la Bwana Mungu wetu.
17 Ndipo watu kadha wa kadha miongoni mwa wazee wa nchi wakaondoka, wakanena na mkutano wa watu, wakisema,
18 Mikaya Mmorashti, alitabiri katika siku za Hezekia, mfalme wa Yuda; akasema na watu wote wa Yuda, ya kwamba, Bwana wa majeshi asema hivi, Sayuni utalimwa kama shamba lilimwavyo, na Yerusalemu utakuwa magofu, na mlima wa nyumba utakuwa kama mahali palipoinuka msituni.
19 Je! Hezekia, mfalme wa Yuda, na watu wote wa Yuda, walimwua Mikaya? Je! Hakumcha Bwana, na kumwomba Bwana awafadhili; naye Bwana akaghairi, asiyatende mabaya yale aliyoyatamka juu yao? Na sisi tungetenda mabaya makuu juu ya roho zetu.
20 Tena, kulikuwa na mtu aliyetabiri katika jina la Bwana, Uria, mwana wa Shemaya, wa Kiriath-Yearimu; yeye naye alitabiri juu ya mji huu, na juu ya nchi hii, sawasawa na maneno yote ya Yeremia;
21 na Yehoyakimu, mfalme, na mashujaa wake wote, na wakuu wake wote, waliposikia maneno yake, mfalme akataka kumwua; lakini Uria alipopata habari, aliogopa, akakimbia akaenda Misri.
22 Basi, mfalme Yehoyakimu akatuma watu waende Misri, Elnathani, mwana wa Akbori, na watu wengine pamoja naye, kwenda Misri;
23 wakamtoa Uria katika Misri, wakamleta kwa Yehoyakimu, mfalme; naye akamwua kwa upanga, akamtupa yule maiti katika makaburi ya watu wasio na cheo.
24 Lakini mkono wa Ahikamu, mwana wa Shafani, alikuwa pamoja na Yeremia, wasimtie katika mikono ya watu auawe.

Yeremia 27


1 Mwanzo wa kumiliki kwake Sedekia, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili likamjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema,
2 Bwana ameniambia hivi, Jifanyizie vifungo na nira, ukajivike shingoni;
3 kisha uvipeleke kwa mfalme wa Edomu, na mfalme wa Moabu, na mfalme wa wana wa Amoni, na mfalme wa Tiro, na mfalme wa Sidoni, kwa mikono ya wajumbe watakaofika Yerusalemu kwa Sedekia, mfalme wa Yuda.
4 Uwaagize waende kwa bwana zao, na kuwaambia, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Mtawaambia bwana zenu maneno haya;
5 Mimi nimeiumba dunia hii, wanadamu na wanyama walio juu ya uso wa nchi, kwa uweza wangu mkuu, na kwa mkono wangu ulionyoshwa; nami nawapa watu kama inipendezavyo.
6 Na sasa nimetia nchi hizi zote katika mkono wa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu; na wanyama wa mwituni pia nimempa wamtumikie.
7 Na mataifa yote watamtumikia yeye, na mwanawe, na mwana wa mwanawe, hata utakapowadia wakati wa nchi yake mwenyewe, ndipo mataifa mengi na wafalme wakuu watamtumikisha yeye.
8 Na itakuwa, taifa lile na mfalme yule asiyetaka kumtumikia Nebukadreza, huyo mfalme wa Babeli, na kutia shingo zao katika nira ya mfalme wa Babeli, mimi nitaliadhibu taifa lile kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, asema Bwana, hata nitakapokuwa nimewaangamiza kwa mkono wake.
9 Lakini, katika habari zenu, msisikilize manabii wenu, wala wabashiri wenu, wala ndoto zenu, wala watambuzi wenu, wala waganga wenu, wanaowaambia, ya kwamba, Hamtamtumikia mfalme wa Babeli;
10 maana wanawatabiria uongo, ili kuwatoa ninyi mbali na nchi yenu; niwafukuze mkaangamie.
11 Bali taifa lile watakaotia shingo zao katika nira ya mfalme wa Babeli, na kumtumikia, taifa hilo nitawaacha wakae katika nchi yao wenyewe, asema Bwana; nao watailima, na kukaa ndani yake.
12 Nikamwambia Sedekia, mfalme wa Yuda, kwa mfano wa maneno hayo yote, nikisema, Tieni shingo zenu katika nira ya mfalme wa Babeli, mkamtumikie yeye na watu wake, mpate kuishi.
13 Mbona mnataka kufa, wewe na watu wako, kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, kama Bwana alivyosema katika habari ya taifa lile, lisilotaka kumtumikia mfalme wa Babeli?
14 Wala msisikilize maneno ya manabii wawaambiao ninyi, ya kwamba, Hamtamtumikia mfalme wa Babeli; maana wanawatabiria uongo.
15 Kwa maana mimi sikuwatuma, asema Bwana, bali wanatabiri uongo kwa jina langu; nipate kuwatoeni nje, mkaangamie, ninyi, na manabii hao wanaowatabiria.
16 Pia nalisema na makuhani, na watu wote, nikisema, Bwana asema hivi, Msisikilize maneno ya manabii wenu, wanaowatabiria, wakisema, Tazameni, vyombo vya nyumba ya Bwana, baada ya muda kidogo, vitaletwa tena toka Babeli; maana wanawatabiria uongo.
17 Msiwasikilize; mtumikieni mfalme wa Babeli, mkaishi; kwani mji huu kufanywa ukiwa?
18 Lakini ikiwa hao ni manabii, na ikiwa neno la Bwana liko kwao, basi na wamwombe Bwana wa majeshi, kwamba vyombo vile vilivyosalia katika nyumba ya Bwana, na katika nyumba ya mfalme wa Yuda, na hapa Yerusalemu, visiende Babeli.
19 Maana Bwana wa majeshi asema hivi, katika habari za nguzo, na katika habari za bahari, na katika habari za matako yake, na katika habari za mabaki ya vyombo vilivyoachwa katika mji huu,
20 ambavyo Nebukadreza, mfalme wa Babeli, hakuvichukua, hapo alipomchukua Yekonia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, toka Yerusalemu mpaka Babeli, pamoja na wakuu wote wa Yuda, na Yerusalemu;
21 naam, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, katika habari za vyombo vilivyobaki katika nyumba ya Bwana, na katika nyumba ya mfalme wa Yuda, na hapa Yerusalemu;
22 Vitachukuliwa mpaka Babeli, navyo vitakaa huko, hata siku ile nitakapovijilia, asema Bwana; hapo ndipo nitakapovileta tena, na kuvirudisha mahali hapa.

Yeremia 28


1 Ikawa, katika mwaka ule ule, mwanzo wa kutawala kwake Sedekia, mfalme wa Yuda, mwaka wa nne, mwezi wa tano, Hanania, mwana wa Azuri, nabii, wa Gibeoni, akasema nami ndani ya nyumba ya Bwana, mbele ya makuhani na watu wote, akisema,
2 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nimeivunja nira ya mfalme wa Babeli.
3 Kabla haujatimia muda wa miaka miwili mizima, nitavirudisha mahali hapa vyombo vyote vya nyumba ya Bwana, ambavyo Nebukadreza, mfalme wa Babeli, aliviondoa katika mahali hapa, akavichukua mpaka Babeli.
4 Nami nitamrudisha hapa Yekonia, mwana wa Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, pamoja na mateka wote wa Yuda, waliokwenda Babeli, asema Bwana; maana nitaivunja nira ya mfalme wa Babeli.
5 Ndipo nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, mbele ya makuhani, na mbele ya watu wote waliosimama ndani ya nyumba ya Bwana,
6 naam, nabii Yeremia akasema, Amina, Bwana na atende hivi; Bwana ayatimize maneno yako uliyotabiri, kuvirudisha hapa vyombo vya nyumba ya Bwana na watu wote waliofungwa, toka Babeli, hata mahali hapa.
7 Lakini lisikilize sasa neno hili nilisemalo, masikioni mwako, na masikioni mwa watu wote,
8 Manabii waliokuwako kabla ya zamani zangu, na zamani zako, walitabiri juu ya nchi nyingi, na juu ya falme kubwa, habari ya vita, na ya mabaya, na ya tauni.
9 Nabii atabiriye habari za amani, neno la nabii yule litakapotokea, ndipo nabii yule atakapojulikana, kuwa Bwana amemtuma kweli kweli.
10 Ndipo nabii Hanania akaitwaa hiyo nira iliyokuwa juu ya shingo ya Yeremia, akaivunja.
11 Naye Hanania akanena mbele ya watu wote, akisema, Bwana asema hivi, Hivyo ndivyo nitakavyoivunja nira ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, kabla haujatimia muda wa miaka miwili mizima, na kuiondoa shingoni mwa mataifa yote. Basi nabii Yeremia akaenda zake.
12 Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia, baada ya Hanania, nabii, kuivunja ile nira iliyokuwa juu ya shingo ya Yeremia, kusema,
13 Enenda ukamwambie Hanania, ukisema, Bwana asema hivi, Umezivunja nira za mti; lakini badala yake utafanya nira za chuma.
14 Maana Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nimetia nira ya chuma juu ya shingo ya mataifa haya yote, ili wamtumikie Nebukadreza, mfalme wa Babeli nao watamtumikia; nami nimempa wanyama wa nchi pia.
15 Kisha nabii Yeremia akamwambia nabii Hanania, Sikia sasa, Ee Hanania; Bwana hakukutuma; lakini unawatumainisha watu hawa maneno ya uongo.
16 Basi Bwana asema hivi, Tazama, nakutuma uende zako toka juu ya uso wa nchi; mwaka huu utakufa, kwa sababu umenena maneno ya uasi juu ya Bwana.
17 Basi nabii Hanania akafa, mwaka uo huo, mwezi wa saba.

Yeremia 29


1 Maneno haya ndiyo maneno ya waraka, ambao nabii Yeremia aliupeleka toka Yerusalemu, kwa hao waliobaki wa wakuu waliochukuliwa mateka, na kwa makuhani, na kwa manabii, na kwa watu wote, ambao Nebukadreza aliwachukua mateka toka Yerusalemu hata Babeli;
2 (hapo walipokwisha kutoka Yerusalemu Yekonia mfalme, na mama yake mfalme, na matowashi, na wakuu wa Yuda na Yerusalemu, na mafundi, na wahunzi;)
3 kwa mkono wa Elasa, mwana wa Shafani, na Gemaria, mwana wa Hilkia, (ambao Sedekia, mfalme wa Yuda, aliwatuma hata Babeli, kwa Nebukadreza, mfalme wa Babeli), kusema,
4 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, awaambia hivi watu wote waliochukuliwa mateka, niliowafanya wachukuliwe toka Yerusalemu mpaka Babeli;
5 Jengeni nyumba, mkakae ndani yake, kapandeni bustani, mkale matunda yake;
6 oeni wake, mkazae wana na binti; kawaozeni wake wana wenu, mkawaoze waume binti zenu, wazae wana na binti; mkaongezeke huko wala msipungue.
7 Kautakieni amani mji ule, ambao nimewafanya mchukuliwe mateka, mkauombee kwa Bwana; kwa maana katika amani yake mji huo ninyi mtapata amani.
8 Maana Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Manabii walio kati yenu, na wabashiri wenu, wasiwadanganye ninyi, wala msisikilize ndoto zenu, mnazootesha.
9 Kwa maana kwa jina langu hutabiri maneno ya uongo kwenu; mimi sikuwatuma, asema Bwana.
10 Maana Bwana asema hivi, Babeli utakapotimiziwa miaka sabini, nitawajilia ninyi, na kulitimiza neno langu jema kwenu, kwa kuwarudisha mahali hapa.
11 Maana nayajua mawazo ninayowawazia ninyi, asema Bwana, ni mawazo ya amani wala si ya mabaya, kuwapa ninyi tumaini siku zenu za mwisho.
12 Nanyi mtaniita, mtakwenda na kuniomba, nami nitawasikiliza.
13 Nanyi mtanitafuta na kuniona, mtakaponitafuta kwa moyo wenu wote.
14 Nami nitaonekana kwenu, asema Bwana, nami nitawarudisha watu wenu waliofungwa, nami nitawakusanya ninyi, nikiwatoa katika mataifa yote, na katika mahali pote, nilikowafukuza, asema Bwana; nami nitawaleta tena, hata mahali ambapo kutoka hapo naliwafanya mchukuliwe mateka.
15 Maana mmesema, Bwana ametuinulia manabii huko Babeli.
16 Maana Bwana asema hivi, katika habari za mfalme aketiye katika kiti cha enzi cha Daudi, na katika habari za watu wote wakaao ndani ya mji huu, ndugu zenu wasiokwenda pamoja nanyi kufungwa;
17 Bwana wa majeshi asema hivi, Tazama, nitaleta juu yao upanga, na njaa, na tauni, nami nitawafanya kuwa kama tini mbovu, zisizoweza kuliwa, kwa kuwa ni mbovu sana.
18 Nami nitawafuatia kwa upanga, na njaa, na tauni, nami nitawatoa watupwe huko na huko katika falme zote za dunia, wawe kitu cha kulaaniwa, na cha kushangaza, na cha kuzomewa, na cha kulaumiwa, katika mataifa yote nilikowafukuza.
19 Kwa sababu hawakusikiliza maneno yangu, asema Bwana, ambayo naliwatuma watumishi wangu, hao manabii, nikiamka mapema, na kuwatuma; lakini hamkutaka kusikiliza, asema Bwana.
20 Basi, lisikieni neno la Bwana, ninyi nyote mliochukuliwa mateka, niliowapeleka toka Yerusalemu mpaka Babeli.
21 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, katika habari za Ahabu, mwana wa Kolaya, na katika habari za Sedekia, mwana wa Maaseya, wawatabiriao ninyi maneno ya uongo kwa jina langu; Tazama, nitawatia katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, naye atawaua mbele ya macho yenu.
22 Tena katika habari zao laana itatumiwa na wafungwa wote wa Yuda, walioko Babeli, kusema, Bwana akufanye uwe kama Sedekia, na kama Ahabu, ambao mfalme wa Babeli aliwaoka motoni;
23 kwa sababu wametenda upumbavu katika Israeli, nao wamezini na wake za jirani zao, nao wamenena maneno ya uongo kwa jina langu, nisiyowaamuru; nami ndimi nijuaye, nami ni shahidi, asema Bwana.
24 Na katika habari za Shemaya, Mnehelami, utanena, ukisema,
25 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, ya kwamba, Kwa kuwa kwa jina lako mwenyewe umewapelekea barua watu wote walioko Yerusalemu, na Sefania, mwana wa Maaseya, kuhani, na makuhani wote, kusema,
26 Bwana amekufanya kuhani badala ya Yehoyada, kuhani, ili mpate kuwa watumishi katika nyumba ya Bwana, kwa kila mtu aliye na wazimu, na kwa kila mtu ajifanyaye kuwa nabii, umtie katika mkatale na pingu.
27 Mbona, basi, hukumkemea Yeremia wa Anathothi, ajifanyaye kuwa nabii kwenu,
28 ambaye ametuma watu kwetu katika Babeli, kusema, Uhamisho huu ni wa siku nyingi; jengeni nyumba, mkakae ndani yake; pandeni bustani, mkale matunda yake.
29 Na Sefania, kuhani, akasoma barua hii masikioni mwa Yeremia nabii.
30 Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia, kusema,
31 Uwapelekee habari watu wote waliohamishwa, kusema, Bwana asema hivi, katika habari za Shemaya, Mnehelami; Kwa sababu Shemaya amewatabiria ninyi, lakini sikumtuma mimi, naye amewatumainisha neno la uongo;
32 basi, Bwana asema hivi, Tazama, nitamwadhibu Shemaya, Mnehelami, na wazao wake; hatakuwa na mtu atakayekaa katika watu hawa, wala hatayaona mema nitakayowatendea watu wangu, asema Bwana; kwa sababu amenena maneno ya uasi juu ya Bwana.

Yeremia 30


1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema,
2 Bwana Mungu wa Israeli, asema hivi, ya kwamba, Uyaandike kitabuni maneno hayo yote niliyokuambia.
3 Kwa maana, tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapowarejeza watu wangu wa Israeli na Yuda waliofungwa, asema Bwana; nami nitawarudisha hata nchi niliyowapa baba zao, nao wataimiliki.
4 Na haya ndiyo maneno aliyosema Bwana, katika habari za Israeli, na katika habari za Yuda.
5 Maana Bwana asema hivi, Tumesikia sauti ya tetemeko, na ya hofu, wala si ya amani.
6 Ulizeni sasa, mkaone kwamba mwanamume aona utungu wa uzazi; mbona, basi, ninaona kila mtu anaweka mikono yake viunoni, kama mwanamke aliye na utungu, na nyuso zote zimegeuka rangi.
7 Ole! Maana siku ile ni kuu, hata hapana inayofanana nayo, maana ni wakati wa taabu yake Yakobo; lakini ataokolewa nayo.
8 Na itakuwa katika siku ile, asema Bwana wa majeshi, nitaivunja nira yake itoke shingoni mwako, nami nitavipasua vifungo vyako; wala wageni hawatamtumikisha tena;
9 bali watamtumikia Bwana, Mungu wao, na Daudi, mfalme wao, nitakayemwinua kwa ajili yao.
10 Kwa sababu hiyo usiogope, Ee Yakobo, mtumishi wangu, asema Bwana; wala usifadhaike, Ee Israeli; kwa maana, tazama, nitakuokoa toka mbali, na wazao wako toka nchi ya uhamisho wao; na Yakobo atarudi, naye atatulia na kustarehe, wala hapana mtu atakayemtia hofu.
11 Maana mimi ni pamoja nawe, asema Bwana, nikuokoe; maana nitawakomesha kabisa mataifa yote huko nilikokutawanya, bali sitakukomesha wewe kabisa; lakini nitakurudi kwa hukumu, wala sitakuacha bila adhabu.
12 Maana Bwana asema hivi, Maumivu yako hayaponyekani, na jeraha yako ni kubwa.
13 Hapana mtu wa kukutetea; kwa jeraha yako huna dawa ziponyazo.
14 Wote wakupendao wamekusahau; hawakutafuti; maana nimekujeruhi kwa jeraha ya adui, kwa adhabu ya mtu mkatili; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi zako zilikuwa zimeongezeka.
15 Mbona unalilia maumivu yako? Hayaponyeki maumivu yako; kwa sababu ya ukubwa wa uovu wako, kwa sababu dhambi zako zimeongezeka, nimekutenda haya.
16 Basi, watu wote wakulao wataliwa; na adui zako wote watakwenda kufungwa; kila mmoja wao; na hao waliokuteka nyara watatekwa; na wote waliokuwinda nitawafanya kuwa mawindo.
17 Maana nitakurudishia afya, nami nitakuponya jeraha zako, asema Bwana, kwa sababu wamekuita, mwenye kutupwa, wakisema, Ni Sayuni, ambao hapana mtu autakaye.
18 Bwana asema hivi, Tazama, nitarudisha tena hema za Yakobo zilizohamishwa, na kuyahurumia makao yake; nao mji huo utajengwa juu ya magofu yake wenyewe, nalo jumba litakaliwa, kama ilivyokuwa desturi yake.
19 Tena kwao itasikiwa shukrani, na sauti yao wachangamkao; nami nitawazidisha, wala hawatakuwa wachache; tena nitawatukuza, wala hawatakuwa wanyonge.
20 Watoto wao nao watakuwa kama zamani, na kusanyiko lao litathibitika mbele zangu, nami nitawaadhibu wote wawaoneao.
21 Na mkuu wao atakuwa mtu wa kwao wenyewe, naye mwenye kuwatawala atakuwa mtu wa jamaa yao; nami nitamkaribisha, naye atanikaribia; maana ni nani aliye na moyo wa kuthubutu kunikaribia? Asema Bwana.
22 Nanyi mtakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wenu.
23 Tazama, tufani ya Bwana, yaani, ghadhabu yake, imetokea tufani ya kudumu; itawaangukia waovu vichwani.
24 Hasira kali ya Bwana haitarudi, hata atakapokwisha kutenda, hata atakapokwisha kuyatimiza makusudi ya moyo wake; katika siku za mwisho mtayafahamu haya.

Yeremia 31


1 Wakati huo, asema Bwana, nitakuwa Mungu wa jamaa zote za Israeli, nao watakuwa watu wangu.
2 Bwana asema hivi, Watu wale walioachwa na upanga walipata neema jangwani; yaani, Israeli, hapo nilipokwenda kumstarehesha.
3 Bwana alinitokea zamani, akisema, Naam nimekupenda kwa upendo wa milele, ndiyo maana nimekuvuta kwa fadhili zangu.
4 Mara ya pili nitakujenga, nawe utajengwa, Ee bikira wa Israeli mara ya pili utapambwa kwa matari yako, nawe utatokea katika michezo yao wanaofurahi.
5 Mara ya pili utapanda mizabibu juu ya milima ya Samaria; wapanzi watapanda, nao watayafurahia matunda yake.
6 Maana kutakuwa siku moja, ambayo walinzi watalia juu ya vilima vya Efraimu, Inukeni, tukaende Sayuni, kwa Bwana, Mungu wetu.
7 Maana Bwana asema hivi, Mwimbieni Yakobo kwa furaha, mkampigie kelele mkuu wa mataifa, tangazeni, sifuni, mkaseme, Ee Bwana, uwaokoe watu wako, mabaki ya Israeli.
8 Tazama, nitawaleta toka nchi ya kaskazini, na kuwakusanya katika miisho ya dunia, na pamoja nao watakuja walio vipofu, na hao wachechemeao, mwanamke mwenye mimba, na yeye pia aliye na utungu wa kuzaa; watarudi huko, jeshi kubwa.
9 Watakuja kwa kulia, na kwa maombi nitawaongoza; nitawaendesha penye mito ya maji, katika njia iliyonyoka; katika njia hiyo hawatajikwaa; maana mimi ni baba wa Israeli, na Efraimu ni mzaliwa wa kwanza wangu.
10 Lisikieni neno la Bwana, enyi mataifa, litangazeni visiwani mbali; mkaseme, Aliyemtawanya Israeli atamkusanya, na kumlinda, kama mchungaji alindavyo kundi lake.
11 Kwa maana Bwana amemweka huru Yakobo, amemkomboa mkononi mwake aliyekuwa hodari kuliko yeye.
12 Nao watakuja, na kuimba katika mlima Sayuni, wataukimbilia wema wa Bwana, nafaka, na divai, na mafuta, na wachanga wa kondoo na wa ng'ombe; na roho zao zitakuwa kama bustani iliyotiwa maji; wala hawatahuzunika tena kabisa.
13 Ndipo bikira atafurahi katika kucheza, na vijana na wazee pamoja; maana nitageuza masikitiko yao kuwa furaha, nami nitawafariji, na kuwafurahisha waache huzuni zao.
14 Nami nitaishibisha roho ya makuhani kwa unono, na watu wangu watashiba kwa wema wangu, asema Bwana
15 Bwana asema hivi, Sauti imesikiwa Rama, kilio, na maombolezo mengi, Raheli akiwalilia watoto wake; asikubali kufarijiwa kwa watoto wake, kwa kuwa hawako,
16 Bwana asema hivi, Zuia sauti yako, usilie, na macho yako yasitoke machozi; Maana kazi yako itapata thawabu, nao watakuja tena toka nchi ya adui; Ndivyo asemavyo Bwana.
17 Tena liko tumaini kwa siku zako za mwisho, asema Bwana; na watoto wako watarejea hata mpaka wao wenyewe.
18 Hakika nimemsikia Efraimu, akijililia hivi, Umeniadhibu, nami nikaadhibika, kama ndama asiyeizoelea nira; unigeuze, nami nitageuzwa; kwa maana wewe u Bwana, Mungu wangu.
19 Hakika baada ya kugeuzwa kwangu, nalitubu; na baada ya kufundishwa kwangu, nalijipiga pajani; nalitahayarika, naam, nalifadhaika, kwa sababu naliichukua aibu ya ujana wangu.
20 Je! Efraimu siye mwanangu mpendwa? Je! Siye mtoto apendezaye? Maana kila nisemapo neno juu yake, ningali nikimkumbuka sana; kwa sababu hiyo moyo wangu unataabika kwa ajili yake; bila shaka nitamrehemu, asema Bwana.
21 Jiwekee alama za njia; jifanyie miti ya kukuongoza; uuelekeze moyo wako kwenye njia kuu, njia ile ile uliyoiendea; rudi tena, Ee bikira wa Israeli, irudie hii miji yako.
22 Hata lini utatanga-tanga, Ee binti mwenye kuasi? Kwa maana Bwana ameumba jambo jipya duniani; mwanamke atamlinda mwanamume.
23 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Watatumia tena neno hili katika nchi ya Yuda, na katika miji yake, nitakapowarudisha mateka yao; Bwana na akubariki, Ee kao la haki, Ee mlima wa utakatifu.
24 Na Yuda, na miji yake yote, watakaa humo pamoja; wakulima, nao waendao huko na huko pamoja na makundi yao.
25 Kwa maana nimeishibisha roho yenye uchovu, nami nimeiridhisha kila roho yenye huzuni.
26 Basi, nikaamka, nikaangalia; na usingizi wangu ulikuwa mtamu kwangu.
27 Tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapoipanda nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda, mbegu ya mwanadamu na mbegu ya mnyama.
28 Tena itakuwa, kwa kadiri nilivyowaangalia, ili kung'oa, na kubomoa, na kuangusha, na kuangamiza, na kutesa; kwa kadiri iyo hiyo nitawaangalia, ili kujenga, na kupanda, asema Bwana.
29 Siku zile, hawatasema tena, Baba za watu wamekula zabibu kali, na meno ya watoto wao yametiwa ganzi.
30 Bali kila mtu atakufa kwa sababu ya uovu wake mwenyewe; kila mtu alaye zabibu kali, meno yake yatatiwa ganzi.
31 Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.
32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.
33 Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; Nitatia sheria yangu ndani yao, na katika mioyo yao nitaiandika; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
34 Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena.
35 Bwana asema hivi, awapaye watu jua, ili kuwa nuru wakati wa mchana, na amri za mwezi na nyota, ili kuwa nuru wakati wa usiku, aichafuaye bahari, hata mawimbi yake yakavuma; Bwana wa majeshi, ndilo jina lake;
36 Amri hizi zikiondoka, zisiwe mbele zangu, asema Bwana, ndipo wazao wa Israeli nao wataacha kuwa taifa mbele zangu milele.
37 Bwana asema hivi, Kama mbingu zikiweza kupimwa, na misingi ya dunia ikiweza kugunduliwa huko chini, ndipo wazao wa Israeli pia nitawatupilia mbali, kwa ajili ya hayo yote waliyoyatenda, asema Bwana.
38 Tazama, siku zinakuja, asema Bwana, mji huu utakapojengwa kwa ajili ya Bwana, toka buruji ya Hananeli hata lango la pembeni.
39 Na kamba ya kupimia itaendelea moja kwa moja hata mlima Garebu, tena itazunguka na kufika Goa.
40 Na bonde lote la mizoga, na majivu, na mashamba yote mpaka kijito Kidroni, mpaka pembe ya lango la farasi, upande wa mashariki, patakuwa patakatifu kwa Bwana; hapatang'olewa, wala hapatabomolewa, hata milele.

Yeremia 32


1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, katika mwaka wa kumi wa Sedekia, mfalme wa Yuda, nao ulikuwa mwaka wa kumi na nane wa Nebukadreza.
2 Basi, wakati huo jeshi la mfalme wa Babeli liliuzunguka Yerusalemu; na Yeremia, nabii, alikuwa amefungwa ndani ya uwanda wa walinzi, uliokuwa katika nyumba ya mfalme wa Yuda.
3 Kwa maana Sedekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amemfunga, akisema, Kwa nini unatabiri, na kusema, Bwana asema hivi, Angalia, nitatia mji huu katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atautwaa;
4 tena, Sedekia, mfalme wa Yuda, hatapona kutoka katika mikono ya Wakaldayo, lakini hakika yake atatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli, atanena naye mdomo kwa mdomo, na macho yake yatatazama macho yake;
5 naye atamchukua Sedekia mpaka Babeli, naye atakuwako huko hata nitakapomjilia, asema Bwana; mjapopigana na Wakaldayo hamtafanikiwa.
6 Yeremia akasema, Neno la Bwana limenijia, kusema,
7 Tazama, Hanameli, mwana wa Shalumu, mjomba wako, atakujia, akisema, Jinunulie shamba langu lililoko Anathothi; maana haki ya ukombozi ni yako, ulinunue.
8 Basi Hanameli, mwana wa mjomba wangu, akanijia ndani ya uwanda wa walinzi, sawasawa na lile neno la Bwana, akaniambia, Tafadhali, ulinunue shamba langu lililoko Anathothi, katika nchi ya Benyamini; maana haki ya urithi ni yako, na haki ya ukombozi ni yako; ujinunulie. Ndipo nikajua kama neno hili ni neno la Bwana.
9 Basi nikalinunua shamba lile lililoko Anathothi kwa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, nikampimia fedha yake, shekeli kumi na saba za fedha.
10 Nami nikaitia sahihi ile hati, na kuipiga muhuri, nikawaita mashahidi, nikampimia ile fedha katika mizani.
11 Nikaitwaa ile hati ya kununua, ile iliyopigwa muhuri kama ilivyo sheria na ada, na ile nayo iliyokuwa wazi;
12 na ile hati ya kununua nikampa Baruku, mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, mbele ya uso wa Hanameli, mwana wa mjomba wangu, na mbele ya mashahidi wale walioitia sahihi hati ya kununua, mbele ya Wayahudi wote walioketi katika uwanda wa walinzi.
13 Nami nikamwagiza Baruku mbele yao, nikisema,
14 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Twaa hati hizi, hati hii ya kununua, hati hii iliyopigwa muhuri, na hii iliyo wazi pia, ukazitie katika chombo cha udongo, zipate kukaa siku nyingi.
15 Maana Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nyumba na mashamba na mashamba ya mizabibu yatanunuliwa tena katika nchi hii.
16 Hata nikiisha kumpa Baruku, mwana wa Neria, hati ile ya kununua, nalimwomba Bwana, nikisema,
17 Aa! Bwana MUNGU, tazama, wewe umeziumba mbingu na nchi, kwa uweza wako mkuu na kwa mkono wako ulionyoshwa; hapana neno lililo gumu usiloliweza;
18 wewe uwarehemuye watu elfu nyingi, uwalipaye baba za watu uovu wao vifuani mwa watoto wao baada yao; Mungu aliye mkuu, aliye hodari, Bwana wa majeshi ndilo jina lake;
19 mkuu wa mashauri, mweza katika kutenda; ambaye macho yake yamefumbuka juu ya njia zote za wanadamu, kumpa kila mtu kwa kadiri ya njia zake, na kwa kadiri ya matunda ya matendo yake,
20 wewe uliyeweka ishara na ajabu katika nchi ya Misri hata siku hii ya leo, katika Israeli na kati ya watu wengine; na kujifanyia jina kama ilivyo leo;
21 ukawatoa watu wako, Israeli, katika nchi ya Misri, kwa ishara, na kwa ajabu, na kwa mkono hodari, na kwa mkono ulionyoshwa, na kwa utisho mkuu;
22 ukawapa nchi hii, uliyowaapia baba zao kwamba utawapa, nchi iliyojaa maziwa na asali;
23 nao wakaingia, wakaimiliki; lakini hawakuitii sauti yako, wala hawakuenda katika sheria yako; hawakutenda neno lo lote katika haya uliyowaagiza wayatende; basi, kwa sababu hii umeleta juu yao mabaya haya yote;
24 angalia maboma haya; wameujia mji huu ili kuutwaa; na mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo wanaopigana nao, kwa sababu ya upanga, na njaa, na tauni; na hayo uliyosema yamekuwa; na, tazama, wewe unayaona.
25 Nawe, Ee Bwana MUNGU, umeniambia, Jinunulie shamba lile kwa fedha, ukawaite mashahidi; iwapo mji huu umetiwa katika mikono ya Wakaldayo; je! Itakuwaje?
26 Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia, kusema,
27 Tazama, mimi ni Bwana, Mungu wa wote wenye mwili; je! Kuna neno gumu lo lote nisiloliweza?
28 Basi, Bwana asema hivi, Tazama, nitautia mji huu katika mikono ya Wakaldayo, na katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, naye atautwaa;
29 na Wakaldayo, wanaopigana na mji huu, watakuja, na kuutia moto mji huu, na kuuteketeza, pamoja na nyumba zake, ambazo juu ya dari zake wamemfukizia Baali uvumba, na kuwamiminia miungu mingine vinywaji, ili kunikasirisha.
30 Maana wana wa Israeli, na wana wa Yuda, wametenda yaliyo mabaya tu mbele za uso wangu, tangu ujana wao; maana wana wa Israeli wamenichokoza tu kwa matendo ya mikono yao, asema Bwana.
31 Kwa kuwa mji huu umekuwa sababu ya kunitia hasira, na sababu ya ghadhabu yangu, tangu siku ile walipoujenga hata siku hii ya leo; ili niuondoe usiwe mbele za uso wangu;
32 kwa sababu ya mabaya yote ya wana wa Israeli, na ya wana wa Yuda, waliyoyatenda ili kunitia hasira, wao, na wafalme wao, na wakuu wao, na makuhani wao, na manabii wao, na watu wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu.
33 Tena wamenigeuzia visogo vyao, wala si nyuso zao; ingawa naliwafundisha, niliondoka mapema na kuwafundisha, lakini hawakusikiliza ili wapate mafundisho.
34 Bali waliweka machukizo yao ndani ya nyumba iliyoitwa kwa jina langu, ili kuinajisi.
35 Tena walijenga mahali palipoinuka kwa Baali, palipo katika bonde la mwana wa Hinomu, ili kuwapitisha wana wao na binti zao katika moto kwa ajili ya Moleki, jambo nisilowaagiza; wala halikuingia moyoni mwangu kwamba walitende chukizo hilo; wapate kumkosesha Yuda.
36 Basi sasa, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, katika habari za mji huu, ambao ninyi mnasema juu yake maneno haya, Umetiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli, kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni;
37 Tazama, nitawakusanya, na kuwatoa katika nchi zote nilikowafukuza, katika hasira yangu, na uchungu wangu, na ghadhabu yangu nyingi; nami nitawaleta tena hata mahali hapa, nami nitawakalisha salama salimini;
38 nao watakuwa watu wangu, nami nitakuwa Mungu wao;
39 nami nitawapa moyo mmoja na njia moja, wapate kunicha sikuzote; kwa mema yao, na ya watoto wao baada yao;
40 nami nitafanya agano la milele pamoja nao, kwamba sitageuka wala kuwaacha, ili niwatendee mema; nami nitatia kicho changu mioyoni mwao, ili wasiniache.
41 Naam, nitafurahi juu yao niwatendee mema, nami nitawapanda katika nchi hii kweli kweli, kwa moyo wangu wote, na kwa roho yangu yote.
42 Maana Bwana asema hivi, Kama nilivyoleta mabaya makuu haya yote juu ya watu hawa, vivyo hivyo nitaleta juu yao mema hayo yote niliyowaahidia.
43 Na mashamba yatanunuliwa katika nchi hii, mnayoitaja, mkisema, Ni ukiwa, haina mwanadamu wala mnyama; imetiwa katika mikono ya Wakaldayo.
44 Watu watanunua mashamba kwa fedha, watazitia sahihi hati zake, na kuzipiga muhuri, na kuwaita mashahidi, katika nchi ya Benyamini, na katika mahali palipo pande zote za Yerusalemu, na katika miji ya Yuda, na katika miji ya nchi yenye vilima, na katika miji ya nchi tambarare, na katika miji ya Negebu; kwa maana nitawarudisha wafungwa wao, asema Bwana.

Yeremia 33


1 Tena, neno la Bwana likamjia Yeremia mara ya pili, hapo alipokuwa akali amefungwa katika uwanda wa walinzi, kusema,
2 Bwana alitendaye jambo hili, Bwana aliumbaye ili alithibitishe; Bwana ndilo jina lake; asema hivi,
3 Niite, nami nitakuitikia, nami nitakuonyesha mambo makubwa, magumu usiyoyajua.
4 Maana Bwana, Mungu wa Israeli asema hivi, katika habari za nyumba za mji huu, na katika habari za nyumba za wafalme wa Yuda, zilizobomolewa ili kuyapinga maboma na upanga;
5 Wanakuja kupigana na Wakaldayo, lakini ni kuzijaza kwa mizoga ya watu, niliowaua katika hasira yangu na ghadhabu yangu, ambao kwa ajili ya uovu wao wote nimeuficha mji huu uso wangu.
6 Tazama, nitauletea afya na kupona, nami nitawaponya; nami nitawafunulia wingi wa amani na kweli.
7 Nami nitawarudisha wafungwa wa Yuda, na wafungwa wa Israeli, na kuwajenga kama kwanza.
8 Nami nitawasafisha na uovu wao wote, ambao kwa huo wamenitenda dhambi; nami nitawasamehe maovu yao yote, ambayo kwayo wamenitenda dhambi, na kukosa juu yangu.
9 Na mji huu utakuwa kwangu jina la furaha, na sifa na utukufu, mbele ya mataifa yote ya dunia, watakaosikia habari ya mema yote niwatendeayo, nao wataogopa na kutetemeka, kwa sababu ya mema yote na amani nitakaoupatia mji huo.
10 Bwana asema hivi, katika mahali hapo ambapo mnasema kwamba ni ukiwa, hapana mwanadamu wala mnyama, naam, katika miji ya Yuda na katika njia za Yerusalemu, zilizo ukiwa, hazina mwanadamu wala mwenyeji wala mnyama,
11 itasikilikana tena sauti ya furaha na sauti ya shangwe, sauti ya bwana arusi na sauti ya bibi arusi, sauti yao wasemao Mshukuruni Bwana wa majeshi, maana Bwana ni mwema, rehema zake ni za milele; na sauti zao waletao sadaka za shukrani nyumbani kwa Bwana. Kwa kuwa nitawarudisha wafungwa wa nchi hii kama kwanza, asema Bwana.
12 Bwana wa majeshi asema hivi, Katika mahali hapa, palipo ukiwa, hapana mwanadamu wala mnyama, na katika miji yake yote, yatakuwapo makao ya wachungaji wakizilaza kondoo zao.
13 Katika miji ya nchi ya vilima, katika miji ya nchi tambarare, katika miji ya Negebu, na katika nchi ya Benyamini, na katika mahali palipo karibu na Yerusalemu, na katika miji ya Yuda, makundi ya kondoo yatapita tena chini ya mikono yake awahesabuye, asema Bwana.
14 Tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapolitimiza neno lile jema nililolinena, katika habari za nyumba ya Israeli, na katika habari za nyumba ya Yuda.
15 Katika siku zile, na wakati ule, nitamchipushia Daudi Chipukizi la haki; naye atafanya hukumu na haki katika nchi hii.
16 Katika siku zile Yuda ataokolewa, na Yerusalemu utakaa salama, na jina lake atakaloitwa ni hili, Bwana ni haki yetu.
17 Maana Bwana asema hivi, Daudi hatakosa kuwa na mtu wa kuketi katika kiti cha enzi cha nyumba ya Israeli;
18 wala makuhani Walawi hawatakosa kuwa na mtu wa kusimama mbele zangu, na kutoa sadaka za kuteketezwa, na kufukiza matoleo, na kufanya dhabihu daima.
19 Neno la Bwana likamjia Yeremia, kusema,
20 Bwana asema hivi, Kama mkiweza kulivunja agano langu la mchana, na agano langu la usiku, hata usiwepo tena mchana na usiku kwa wakati wake,
21 ndipo agano langu nililolifanya na Daudi, mtumishi wangu, laweza kuvunjika, hata asiwe na mwana wa kumiliki katika kiti chake cha enzi; tena agano langu nililofanya na Walawi makuhani, wahudumu wangu, laweza kuvunjika.
22 Kama vile jeshi la mbinguni haliwezi kuhesabiwa, wala mchanga wa bahari kupimwa; ndivyo nitakavyoongeza wazao wa Daudi, mtumishi wangu, na Walawi wanaonihudumia.
23 Kisha neno la Bwana likamjia Yeremia, kusema,
24 Je! Hufikiri neno hili walilolisema watu hawa, wakinena, Jamaa zile mbili alizozichagua Bwana amezitupilia mbali? Hivyo ndivyo wanavyowadharau watu wangu, ili wasiwe taifa tena mbele yao.
25 Bwana asema hivi, Ikiwa agano langu la mchana na usiku halikai imara, ikiwa mimi sikuziamuru kawaida za mbingu na dunia;
26 ndipo nitawatupilia mbali wazao wa Yakobo, na Daudi, mtumishi wangu, hata nisitwae wazao wake watawale juu ya wazao wa Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; kwa maana nitawarudisha wafungwa wao, nami nitawarehemu.

Yeremia 34


1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, hapo Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na jeshi lake lote, na falme zote za dunia zilizokuwa chini ya mamlaka yake, na kabila zote za watu, walipopigana na Yerusalemu, na miji yake yote, kusema,
2 Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Enenda ukaseme na Sedekia, mfalme wa Yuda, ukamwambie, Bwana asema hivi, Tazama, nitatia mji huu katika mikono ya mfalme wa Babeli, naye atauteketeza kwa moto;
3 tena wewe hutaokoka mkononi mwake, lakini utakamatwa kweli kweli, na kutiwa katika mikono yake; na macho yako yatayatazama macho ya mfalme wa Babeli, naye atasema nawe mdomo kwa mdomo, nawe utakwenda Babeli.
4 Hata hivyo lisikie neno la Bwana, Ee Sedekia, mfalme wa Yuda; Bwana asema hivi katika habari zako; hutakufa kwa upanga;
5 utakufa katika amani; na kwa mafukizo ya baba zako, wafalme wa zamani waliokutangulia, ndivyo watakavyokufukizia; nao watakulilia, Aa, Bwana! Kwa maana mimi nimelinena neno hili, asema Bwana.
6 Basi Yeremia, nabii, akamwambia Sedekia, mfalme wa Yuda, maneno hayo yote katika Yerusalemu,
7 wakati ule jeshi la Babeli walipopigana na Yerusalemu na miji yote ya Yuda iliyosalia, na Lakishi, na Azeka; kwa maana miji hiyo tu ndiyo iliyosalia katika miji ya Yuda yenye maboma.
8 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, baada ya wakati ule mfalme Sedekia alipofanya agano na watu wote waliokuwa katika Yerusalemu, kuwatangazia habari ya uhuru;
9 ya kwamba kila mtu amweke huru mtumwa wake, na kila mtu amweke huru mjakazi wake, ikiwa yule mwanamume au yule mwanamke ni Mwebrania; mtu ye yote asiwatumikishe, yaani, asimtumikishe Myahudi, nduguye;
10 na wakuu wote, na watu wote, wakati, waliofanya agano hilo, ya kwamba kila mtu amweke huru mtumwa wake na mjakazi wake, mtu ye yote asiwatumikishe tena; wakatii, wakawaacha.
11 Lakini baadaye wakaghairi, wakawarudisha watumwa wale, na wajakazi wale, ambao wamewaacha huru, nao wakawatia utumwani wawe watumwa na wajakazi wao.
12 Basi, neno la Bwana likamjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema,
13 Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nalifanya agano na baba zenu, siku ile nilipowatoa katika nchi ya Misri, katika nyumba ya utumwa, nikisema,
14 Mwisho wa kila mwaka wa saba kila mtu na amweke huru ndugu yake aliye Mwebrania, aliyeuzwa kwako na kukutumikia miaka sita utamwacha atoke kwako huru, lakini baba zenu hawakunisikiliza, wala hawakutega masikio yao.
15 Na ninyi mlikuwa mmegeuka, mkafanya yaliyo haki machoni pangu, kwa kumtangazia uhuru kila mtu ndugu yake; nanyi mlikuwa mmefanya agano mbele zangu, katika nyumba ile iitwayo kwa jina langu;
16 lakini mlighairi, na kulitukana jina langu; kila mtu akamrudisha mtumwa wake na mjakazi wake, ambao mmewaweka huru kama walivyopenda wenyewe, mkawatia utumwani tena, wawe watumwa wenu na wajakazi wenu.
17 Basi Bwana asema hivi, Hamkunisikiliza kumtangazia uhuru kila mtu ndugu yake, na kila mtu jirani yake; tazama, mimi nawatangazieni uhuru, asema Bwana, yaani, wa upanga, na njaa, na tauni; nami nitawatoa ninyi mtupwe huko na huko katika falme zote za dunia.
18 Na watu hao waliolivunja agano langu, wasioyatimiza maneno ya agano lile, walilolifanya mbele zangu, wakati ule walipomkata ndama vipande viwili, wakapita katikati ya vipande vile;
19 wakuu wa Yuda, na wakuu wa Yerusalemu, matowashi, na makuhani, na watu wote wa nchi, waliopita katikati ya vipande vile vya huyo ndama;
20 mimi nitawatia katika mikono ya adui zao, na katika mikono ya watu wale wanaowatafuta roho zao, na mizoga yao itakuwa ni chakula cha ndege za mbinguni, na cha wanyama wakali wa nchi.
21 Na Sedekia, mfalme wa Yuda, na wakuu wake nitawatia katika mikono ya adui zao, na katika mikono ya watu wale wanaowatafuta roho zao, na katika mikono ya jeshi la mfalme wa Babeli, waliokwenda zao na kuwaacheni.
22 Tazama, nitawapa amri yangu, asema Bwana, na kuwarejeza kwenye mji huu; nao watapigana nao, na kuutwaa, na kuuteketeza kwa moto; nami nitaifanya miji ya Yuda kuwa ukiwa, isikaliwe na mtu.

Yeremia 35


1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, katika siku za Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, kusema,
2 Enenda nyumbani kwa Warekabi, ukanene nao, ukawalete nyumbani kwa Bwana, katika chumba kimoja, ukawape divai wanywe.
3 Basi nikamtwaa Yaazania, mwana wa Yeremia, mwana wa Habasinia, na ndugu zake, na wanawe wote, na nyumba yote ya Warekabi;
4 nikawaleta ndani ya nyumba ya Bwana, ndani ya chumba cha wana wa Hanani, mwana wa Igdalia, mtu wa Mungu, kilichokuwa karibu na chumba cha wakuu, nacho kilikuwa juu ya chumba cha Maaseya, mwana wa Shalumu, bawabu;
5 nikaweka mabakuli yaliyojaa divai, na vikombe, mbele ya wana wa nyumba ya Warekabi, nikawaambia, Nyweni divai.
6 Lakini wakasema, Hatutakunywa divai; kwa maana Yonadabu, mwana wa Rekabu, baba yetu, alituamuru, akisema, Msinywe divai, ninyi wala wana wenu, hata milele;
7 wala msijenge nyumba, wala msipande mbegu, wala msipande mizabibu, wala msiwe nayo; bali siku zenu zote mtakaa katika hema; mpate kuishi siku nyingi katika nchi ambayo mtakaa ndani yake hali ya wageni.
8 Nasi tumeitii sauti ya Yonadabu, mwana wa Rekabu, baba yetu, katika yote aliyotuamuru, kwamba tusinywe divai siku zetu zote, sisi, na wake zetu, na wana wetu, na binti zetu;
9 wala tusijijengee nyumba za kukaa; wala hatuna shamba la mizabibu, wala konde, wala mbegu;
10 bali tumekaa katika hema, nasi tumetii; tukafanya sawasawa na yote aliyotuamuru Yonadabu, baba yetu.
11 Lakini ikawa, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alipopanda akaingia nchi hii, ndipo tukasema, Haya! Twende Yerusalemu, tukiliogopa jeshi la Wakaldayo, na tukiliogopa jeshi la Washami; basi hivyo tunakaa Yerusalemu.
12 Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia, kusema,
13 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Enenda ukawaambie wana wa Yuda, na wenyeji wa Yerusalemu, Je! Hamtaki kupokea mafundisho, myasikilize maneno yangu? Asema Bwana.
14 Maneno ya Yonadabu, mwana wa Rekabu, aliyowaamuru wanawe, kwamba wasinywe divai, yametimizwa, na hata leo hawanywi; maana waitii hiyo amri ya baba yao; lakini mimi nimesema nanyi, nikiamka mapema na kunena, bali ninyi hamkunisikiliza mimi.
15 Pia naliwapeleka watumishi wangu wote, manabii, kwenu ninyi, nikiamka mapema na kuwapeleka, nikisema, Rudini sasa, kila mtu na aiache njia yake mbaya, mkatengeneze matendo yenu, wala msiwafuate miungu mingine, ili kuwatumikia, nanyi mtakaa katika nchi hii, niliyowapa ninyi na baba zenu; lakini hamkutega masikio yenu, wala hamkunisikiliza.
16 Basi, kwa kuwa wana wa Yonadabu, mwana wa Rekabu, wameitimiza amri ya baba yao aliyowaamuru, lakini watu hawa hawakunisikiliza mimi;
17 kwa sababu hiyo, asema Bwana, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli; Tazama nitaleta juu ya Yuda, na juu ya wenyeji wote wa Yerusalemu, mabaya yote niliyoyatamka juu yao; kwa sababu nimesema nao, wasinisikilize; nimewaita, wala hawakuniitikia.
18 Naye Yeremia akawaambia watu wa nyumba ya Warekabi, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa sababu mmeitii amri ya Yonadabu, baba yenu, na kuyashika maagizo yake yote, na kutenda sawasawa na yote aliyowaamuru;
19 basi, kwa sababu hiyo, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Yonadabu, mwana wa Rekabu, hatakosa kuwa na mtu wa kusimama mbele zangu hata milele.

Yeremia 36


1 Ikawa katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, neno hili likamjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, kusema,
2 Twaa gombo la chuo, ukaandike ndani yake maneno yote niliyokuambia juu ya Israeli, na juu ya Yuda, na juu ya mataifa yote, tangu siku ile niliponena nawe, tangu siku za Yosia, hata siku hii ya leo.
3 Huenda nyumba ya Yuda watasikia mabaya yote niliyokusudia kuwatenda; wapate kurudi, kila mtu akaiache njia yake mbaya; nami nikawasamehe uovu wao na dhambi yao.
4 Kisha Yeremia akamwita Baruku, mwana wa Neria; naye Baruku akaandika katika gombo la chuo maneno yote ya Bwana, yaliyotoka kinywani mwa Yeremia, ambayo Bwana amemwambia.
5 Yeremia akamwagiza Baruku, ya kwamba, Mimi nimefungwa, siwezi kuingia katika nyumba ya Bwana.
6 Basi, enenda wewe, ukasome katika gombo la chuo, ambacho umeandika ndani yake, maneno ya Bwana yaliyotoka kinywani mwangu, ukiyasoma katika masikio ya watu, ndani ya nyumba ya Bwana, siku ya kufunga; pia utayasoma masikioni mwa watu wote wa Yuda, watokao katika miji yao.
7 Labda wataomba dua zao mbele za Bwana, na kurudi, kila mtu akiiacha njia yake mbaya; kwa maana hasira na ghadhabu ni kuu sana, alizotamka Bwana juu ya watu hawa.
8 Basi, Baruku, mwana wa Neria, akafanya sawasawa na hayo yote, ambayo Yeremia, nabii, amemwagiza, akisoma katika chuo hicho, maneno ya Bwana, ndani ya nyumba ya Bwana.
9 Basi, ikawa katika mwaka wa tano wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kenda, watu wote waliokuwa katika Yerusalemu, na watu wote waliokuja Yerusalemu kutoka miji yote ya Yuda, wakapiga mbiu ya kufunga mbele za Bwana.
10 Basi, wakati huo Baruku akayasoma maneno ya Yeremia katika nyumba ya Bwana, katika chumba cha Gemaria, mwana wa Shafani, mwandishi, katika ua wa juu, mahali pa kuingilia kwa lango jipya la nyumba ya Bwana, akiyasoma katika masikio ya watu wote.
11 Basi, Mikaya, mwana wa Gemaria, mwana wa Shafani, aliposikia maneno yote ya Bwana yaliyokuwa katika chuo hicho,
12 akashuka, akaingia katika nyumba ya mfalme, katika chumba cha mwandishi, na, tazama, wakuu wote wameketi humo, nao ni hawa, Elishama, mwandishi, na Delaya, mwana wa Shemaya, na Elnathani, mwana wa Akbori, na Gemaria, mwana wa Shafani, na Sedekia, mwana wa Hanania, na wakuu wote.
13 Naye Mikaya akawaeleza maneno yote aliyoyasikia, hapo Baruku alipokuwa akikisoma kitabu masikioni mwa watu.
14 Basi, wakuu wote wakamtuma Yehudi, mwana wa Nethania, mwana wa Shelemia, mwana wa Kushi, aende kwa Baruku, kumwambia, Litwae mkononi mwako gombo lile ulilolisoma masikioni mwa watu, uje huku. Basi, Baruku, mwana wa Neria, akalitwaa gombo lile mkononi mwake, akaenda kwao.
15 Nao wakamwambia, Keti sasa, ukalisome masikioni mwetu. Basi, Baruku akalisoma masikioni mwao.
16 Ikawa, walipoyasikia maneno hayo yote, wakatazamana kwa hofu, wakamwambia Baruku, Hatuna budi kumwambia mfalme maneno haya yote.
17 Wakamwuliza Baruku, wakisema, Tuambie sasa; ulipataje kuyaandika maneno haya yote kinywani mwake?
18 Baruku akawajibu, Alinitamkia maneno haya yote kwa kinywa chake, nami nikayaandika kwa wino kitabuni.
19 Ndipo hao wakuu wakamwambia Baruku, Enenda ukajifiche, wewe na Yeremia, wala mtu asipajue mlipo.
20 Wakaenda kwa mfalme uwandani; lakini walikuwa wameliweka lile gombo katika chumba cha Elishama, mwandishi wakayanena maneno hayo yote masikioni mwa mfalme.
21 Basi, mfalme akamtuma Yehudi aende akalilete lile gombo; naye akalitoa katika chumba cha Elishama, mwandishi. Yehudi akalisoma masikioni mwa mfalme, na masikioni mwa wakuu waliosimama mbele ya mfalme.
22 Basi mfalme alikuwa ameketi katika nyumba iliyotumika wakati wa baridi, mwezi wa kenda; na pale palikuwa na moto wa makaa mbele yake.
23 Hata ikawa, Yehudi alipokuwa amekwisha kusoma kurasa tatu nne, mfalme akalikata kwa kijembe, akalitupa katika moto wa makaa, hata gombo lote likawa limekwisha kuteketea katika huo moto wa makaa.
24 Lakini hawakuogopa, wala hawakurarua mavazi yao, wala mfalme, wala watumishi wake hata mmoja waliosikia maneno hayo yote.
25 Hata hivyo Elnathani, na Delaya, na Gemaria, walikuwa wamemsihi mfalme asiliteketeze gombo lile, lakini hakukubali kuwasikia.
26 Mfalme akamwamuru Yerameeli, mwana wa mfalme, na Seraya, mwana wa Azrieli, na Shelemia, mwana wa Abdeeli, wamkamate Baruku, mwandishi, na Yeremia, nabii; lakini Bwana aliwaficha.
27 Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia, hapo mfalme alipokuwa amekwisha kuliteketeza gombo lile, na maneno yale aliyoyaandika Baruku, yaliyotoka katika kinywa cha Yeremia, kusema,
28 Haya! Twaa wewe gombo lingine, ukaandike ndani yake maneno yote ya kwanza, yaliyokuwa katika gombo la kwanza, ambalo Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, ameliteketeza.
29 Na katika habari za Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, utasema, Bwana asema hivi, Umeliteketeza gombo hili, ukisema, Mbona umeandika ndani yake, ukisema, Bila shaka mfalme wa Babeli atakuja, na kuiharibu nchi hii, na kukomesha mwanadamu na mnyama pia ndani yake?
30 Basi, Bwana aseme hivi, katika habari za Yehoyakimu, mfalme wa Yuda; Hatakuwa na mtu wa kukaa katika kiti cha enzi cha Daudi; na mzoga wake utatupwa nje wakati wa mchana upigwe kwa hari, na wakati wa usiku upigwe kwa baridi.
31 Nami nitamwadhibu yeye, na wazao wake, na watumishi wake, kwa sababu ya uovu wao, nami nitaleta juu yao, na juu ya wenyeji wa Yerusalemu, na juu ya watu wa Yuda, mabaya yote niliyoyatamka juu yao, lakini hawakukubali kusikiliza.
32 Ndipo Yeremia akatwaa gombo lingine, akampa Baruku, mwandishi, mwana wa Neria, naye akayaandika maneno yote yaliyotoka katika kinywa cha Yeremia, ya kitabu kile alichokiteketeza Yehoyakimu, mfalme wa Yuda, katika moto; tena maneno mengi zaidi kama yale yakatiwa ndani yake.

Yeremia 37


1 Na Sedekia, mwana wa Yosia, akamiliki badala ya Konia, mwana wa Yehoyakimu, ambaye Nebukadreza amemmilikisha katika nchi ya Yuda.
2 Lakini yeye, wala watumishi wake, wala watu wa nchi, hawakuyasikiliza maneno ya Bwana aliyonena kwa kinywa cha nabii Yeremia.
3 Sedekia, mfalme, akamtuma Yehukali, mwana wa Shelemia, na Sefania, mwana wa Maaseya, kuhani, kwa Yeremia, nabii, kusema, Utuombee sasa kwa Bwana, Mungu wetu.
4 Basi Yeremia alikuwa akiingia na kutoka kati ya watu; kwa maana walikuwa hawakumfunga gerezani.
5 Na jeshi la Farao lilikuwa limetoka nchi ya Misri; na Wakaldayo waliohusuru Yerusalemu, waliposikia habari zao, wakavunja kambi yao mbele ya Yerusalemu.
6 Ndipo neno la Bwana likamjia nabii Yeremia, kusema,
7 Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mtamwambia hivi mfalme wa Yuda, aliyewatuma kwangu kuniuliza; Angalieni, jeshi la Farao, ambalo linakuja kuwasaidia, litarudi Misri, nchi yao wenyewe.
8 Na Wakaldayo watakuja tena, na kupigana na mji huu; nao watautwaa, na kuuteketeza.
9 Bwana asema hivi, Msijidanganye mkisema, Bila shaka Wakaldayo watatuacha na kwenda zao; maana hawatawaacha.
10 Maana mngelipiga jeshi lote la Wakaldayo wanaopigana nanyi, wakabaki kati yao watu waliojeruhiwa tu, hata hivyo wangeondoka kila mtu katika hema yake, na kuuteketeza mji huu.
11 Hata ikawa, jeshi la Wakaldayo lilipokuwa limevunja kambi yao mbele ya Yerusalemu, kwa kuliogopa jeshi la Farao,
12 ndipo Yeremia akatoka Yerusalemu, ili aende mpaka nchi ya Benyamini, alipokee huko fungu lake kati ya watu.
13 Naye alipokuwa katika lango la Benyamini, akida wa walinzi alikuwapo, jina lake Iriya, mwana wa Shelemia, mwana wa Hanania; akamkamata Yeremia, nabii, akisema, Unakwenda kujiunga na Wakaldayo.
14 Ndipo Yeremia akasema, Ni uongo, siendi kujiunga na Wakaldayo; lakini yeye asimsadiki; basi Iriya akamkamata Yeremia, akamleta kwa wakuu.
15 Nao wakuu wakamkasirikia Yeremia, wakampiga, wakamtia gerezani katika nyumba ya Yonathani, mwandishi; kwa maana ndiyo waliyoifanya kuwa gereza.
16 Basi, Yeremia alipokuwa ameingia katika nyumba ya shimo, na katika vyumba vya ndani; na Yeremia alipokuwa amekaa humo siku nyingi;
17 ndipo Sedekia, mfalme, akatuma watu wamlete; naye mfalme akamwuliza kwa siri ndani ya nyumba yake, akasema, Je! Liko neno lililotoka kwa Bwana? Yeremia akasema, Liko. Akasema pia, Utatiwa katika mikono ya mfalme wa Babeli.
18 Pamoja na haya Yeremia akamwambia mfalme Sedekia, Nimefanya kosa gani juu yako, au juu ya watumishi wako, au juu ya watu hawa, hata mkanitia gerezani?
19 Wako wapi sasa manabii wenu waliowatabiria, wakisema, Mfalme wa Babeli hatakuja juu yenu, wala juu ya nchi hii?
20 Na sasa unisikilize, Ee bwana wangu mfalme; maombi yangu yakapate kibali mbele yako; usinirudishe nyumbani mwa Yonathani, mwandishi, nisije nikafa humo.
21 Ndipo Sedekia mfalme akatoa amri, wakamtia Yeremia katika uwanda wa walinzi; wakampa kila siku mkate mmoja uliotoka katika njia ya waokaji, hata mkate wote wa mji ulipokwisha. Basi Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi.

Yeremia 38


1 Na Shefatia, mwana wa Matani, na Gedalia, mwana wa Pashuri, na Yukali, mwana wa Shelemia, na Pashuri, mwana wa Malkiya, wakayasikia maneno ambayo Yeremia aliwaambia watu wote, kusema,
2 Bwana asema hivi, Akaaye ndani ya mji huu atakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; bali yeye atokaye kwenda kwa Wakaldayo ataishi, naye atapewa maisha yake yawe kama nyara, naye ataishi.
3 Bwana asema hivi, Bila shaka mji huu utatiwa katika mikono ya jeshi la mfalme wa Babeli, naye atautwaa.
4 Ndipo wakuu wakamwambia mfalme, Twakuomba, mtu huyu auawe, kwa kuwa aidhoofisha mikono ya watu wa vita, waliobaki katika mji huu, na mikono ya watu wote, kwa kuwaambia maneno kama hayo; maana mtu huyu hawatafutii watu hawa heri, bali shari.
5 Naye mfalme Sedekia akasema, Tazama, yu mikononi mwenu; maana mfalme siye awezaye kufanya neno lo lote kinyume chenu.
6 Basi wakamtwaa Yeremia, wakamtupa katika shimo la Malkiya, mwana wa mfalme, lililo katika uwanda wa walinzi; wakamshusha kwa kamba. Na mle shimoni hamkuwa na maji, ila matope tu; naye Yeremia akazama katika matope hayo.
7 Basi, Ebedmeleki, Mkushi, towashi, aliyekuwa katika nyumba ya mfalme, aliposikia kama wamemtia Yeremia shimoni; na wakati huo mfalme alikuwa amekaa katika lango la Benyamini;
8 Ebedmeleki akatoka nyumbani mwa mfalme, akamwambia mfalme, akisema,
9 Ee bwana wangu, mfalme, watu hawa wametenda mabaya katika mambo yote waliyomtenda Yeremia, nabii, ambaye wamemtupa shimoni; naye hakosi atakufa pale alipo, kwa sababu ya njaa; kwa kuwa hapana mkate kabisa katika mji.
10 Ndipo mfalme akamwamuru Ebedmeleki, Mkushi, akisema, Chukua pamoja nawe watu thelathini toka hapa, ukamtoe Yeremia shimoni, kabla hajafa.
11 Basi Ebedmeleki akawachukua watu hao pamoja naye, akaingia ndani ya nyumba ya mfalme chini ya ghala, akatoa mle nguo zilizotupwa, na vitambaa vikuukuu, akamtelemshia Yeremia shimoni kwa kamba.
12 Naye Ebedmeleki, Mkushi, akamwambia Yeremia, Tia nguo hizi zilizotupwa, na vitambaa hivi vikuukuu, chini ya kamba kwapani. Naye Yeremia akafanya hivyo.
13 Basi wakamwinua Yeremia kwa kamba hizo, wakamtoa shimoni; naye Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi.
14 Kisha mfalme Sedekia akatuma watu, akamleta nabii Yeremia kwake, ndani ya maingilio ya tatu ya nyumba ya Bwana; mfalme akamwambia Yeremia, Nataka kukuuliza neno, nawe usinifiche neno lo lote.
15 Basi Yeremia akamwambia Sedekia, Kama nikikufunulia neno hilo, je! Hutaniua wewe? Tena, mimi nikikupa shauri wewe hutanisikiliza.
16 Basi Sedekia mfalme akamwapia Yeremia kwa siri, akisema, Kama Bwana aishivyo, yeye aliyetufanyia roho zetu, sitakuua, wala sitakutia katika mikono ya watu hao wanaokutafuta wakuue.
17 Ndipo Yeremia akamwambia Sedekia, Bwana, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama ukitoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, basi nafsi yako utaishi, wala mji huu hautateketezwa; nawe utaishi na nyumba yako;
18 bali ukikataa kutoka kwenda kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, basi, mji huu utatiwa katika mikono ya Wakaldayo nao watauteketeza, hata na wewe hutajiepusha na mikono yao.
19 Mfalme Sedekia akamwambia Yeremia, Nawaogopa Wayahudi waliowakimbilia Wakaldayo, wasije wakanitia katika mikono yao, nao wakanidhihaki.
20 Lakini Yeremia akasema, La! Hawatakutoa. Nakusihi, uitii sauti ya Bwana katika hayo ninayokuambia; ndivyo itakavyokufaa, na nafsi yako utaishi.
21 Lakini kama ukikataa kutoka, hili ndilo neno ambalo Bwana amenionyesha;
22 Tazama, wanawake wote, walioachwa ndani ya nyumba ya mfalme wa Yuda, watatolewa na kuchukuliwa kwa wakuu wa mfalme wa Babeli, na wanawake hao watasema, Rafiki zako walio karibu wamekudanganya, nao wamekushinda; na kwa kuwa miguu yako imezama matopeni sasa, wamegeuka na kurudi nyuma.
23 Na watawatoa wake zako, na watoto wako wote, na kuwachukua kwa Wakaldayo; wala wewe hutapona na mikono yao, bali utakamatwa kwa mkono wa mfalme wa Babeli, nawe utakuwa sababu ya kuteketezwa mji huu.
24 Ndipo Sedekia akamwambia Yeremia, Mtu ye yote asipate habari ya maneno haya, nawe hutakufa.
25 Lakini kama wakuu wakisikia ya kuwa nimenena nawe, nao wakija kwako, na kukuambia, Tufunulie sasa uliyomwambia mfalme; usimfiche, nasi hatutakuua; na pia uliyoambiwa na mfalme;
26 basi, utawaambia, Nalimwomba mfalme asinirudishe nyumbani kwa Yonathani, nisije nikafa humo.
27 Ndipo wakuu wakamwendea Yeremia, wakamwuliza; naye akawaambia sawasawa na maneno aliyoamriwa na mfalme. Basi wakaacha kunena naye; maana neno lile halikujulikana.
28 Basi Yeremia akakaa katika uwanda wa walinzi hata siku ile Yerusalemu ulipotwaliwa.

Yeremia 39


1 Hata ikawa, Yerusalemu ulipotwaliwa, (katika mwaka wa kenda wa Sedekia, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kumi, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na jeshi lake lote, wakaja juu ya Yerusalemu, wakauhusuru;
2 katika mwaka wa kumi na mmoja wa Sedekia, mwezi wa nne, siku ya kenda ya mwezi, sehemu ya ukuta wa mji ilibomolewa;)
3 wakuu wote wa mfalme wa Babeli wakaingia, wakaketi katika lango la katikati, yaani, Nergal-Shareza, mnyweshaji, Nebu-Sarseki, mkuu wa matowashi, Nergal-Shareza, mkuu wa wanajimu, pamoja na wakuu wengine wote wa mfalme wa Babeli.
4 Ikawa Sedekia, mfalme wa Yuda, na watu wote wa vita walipowaona, ndipo wakakimbia, wakatoka mjini usiku, kwa njia ya bustani ya mfalme, kwa lango lililokuwa kati ya zile kuta mbili; naye akatoka kwa njia ya Araba.
5 Lakini jeshi la Wakaldayo wakawafuatia, wakampata Sedekia katika nchi tambarare ya Yeriko; nao walipomkamata, wakamleta kwa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, huko Ribla katika nchi ya Hamathi, naye akatoa hukumu juu yake.
6 Ndipo mfalme wa Babeli akawaua wana wa Sedekia huko Ribla mbele ya macho yake; pia mfalme wa Babeli akawaua wakuu wote wa Yuda.
7 Pamoja na hayo akampofusha macho Sedekia, akamfunga kwa pingu ili amchukue mpaka Babeli.
8 Nao Wakaldayo wakaiteketeza nyumba ya mfalme, na nyumba za watu kwa moto, wakazibomoa kuta za Yerusalemu.
9 Basi, Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawachukua mateka mabaki ya watu waliosalia katika mji mpaka Babeli, na hao pia waliouacha mji na kujiunga naye, na mabaki ya watu waliosalia.
10 Lakini Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawaacha baadhi ya maskini wa watu, waliokuwa hawana kitu, katika nchi ya Yuda, akawapa mashamba ya mizabibu na makonde wakati uo huo.
11 Basi Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akamwagiza Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, katika habari za Yeremia, akisema,
12 Mtwae, umtunze sana, wala usimtende neno baya lo lote; lakini umtendee kama atakavyokuambia.
13 Basi Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, na Nebu-Shazbani, mkuu wa matowashi, na Nergal-Shareza, mkuu wa wanajimu, na maakida wakuu wote wa mfalme wa Babeli.
14 wakatuma watu wakamwondoa Yeremia katika uwanda wa walinzi, wakamweka katika mikono ya Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, ili ampeleke nyumbani kwake; basi akakaa pamoja na hao watu.
15 Basi neno la Bwana likamjia Yeremia, wakati ule alipokuwa amefungwa katika uwanda wa walinzi, kusema,
16 Haya! Enenda ukaseme na Ebedmeleki, Mkushi, kusema, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitaupatiliza mji huu maneno yangu kwa mabaya, wala si kwa mema; nayo yatatimizwa mbele yako katika siku hiyo.
17 Lakini nitakuokoa wewe katika siku hiyo, asema Bwana; wala hutatiwa katika mikono ya watu wale unaowaogopa.
18 Kwa maana ni yakini, nitakuokoa, wala hutaanguka kwa upanga, lakini nafsi yako itakuwa kama nyara kwako; kwa kuwa ulinitumaini mimi, asema Bwana.

Yeremia 40


1 Neno hili ndilo lililomjia Yeremia, kutoka kwa Bwana, baada ya wakati ule Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, alipomwacha aende zake toka Rama, baada ya kumchukua hali ya kufungwa minyororo, pamoja na wafungwa wote wa Yerusalemu na Yuda, waliochukuliwa hali ya kufungwa mpaka Babeli.
2 Naye amiri wa askari walinzi akamtwaa Yeremia, akamwambia, Bwana, Mungu wako, alitamka mabaya haya juu ya mahali hapa;
3 naye Bwana ameyaleta, na kufanya kama alivyosema; kwa sababu mmemwasi Bwana, wala hamkuitii sauti yake; ndiyo maana neno hili limewajia ninyi.
4 Na sasa, tazama, nakufungulia leo minyororo hii iliyo mikononi mwako. Kama ukiona ni vema kwenda Babeli pamoja nami, haya! Njoo, nami nitakutunza sana; lakini kama ukiona ni vibaya kwenda Babeli pamoja nami, basi, acha; tazama, nchi yote i mbele yako; palipo pema machoni pako na pa kukufaa, enenda huko.
5 Alipokuwa bado hajaenda, akasema, Rudi sasa kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, ambaye mfalme wa Babeli amemweka kuwa liwali juu ya miji ya Yuda, ukakae pamoja naye kati ya watu; au enenda po pote utakapoona mwenyewe kuwa pakufaa. Basi, amiri wa askari walinzi akampa vyakula na zawadi, akamwacha aende zake.
6 Basi, Yeremia akaenda kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu, huko Mizpa, akakaa pamoja naye kati ya watu wale waliosalia katika nchi.
7 Kisha, wakuu wote wa majeshi waliokuwa katika bara, wao na watu wao, waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemweka Gedalia, mwana wa Ahikamu, kuwa liwali juu ya nchi, na kwamba amemkabidhi wanaume na wanawake na watoto, na baadhi ya maskini wa nchi wasiochukuliwa mateka Babeli;
8 ndipo wakamwendea Gedalia huko Mizpa; nao ni hawa, Ishmaeli, mwana wa Nethania, na Yohana na Yonathani, wana wa Karea, na Seraya, mwana wa Tanhumethi, na wana wa Efai, Mnetofa, na Yezania, mwana wa Mmaaka, wao na watu wao.
9 Na Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, akawaapia wao na watu wao, akisema, Msiogope kuwatumikia Wakaldayo; kaeni katika nchi, mkamtumikie mfalme wa Babeli; nayo itawafaa.
10 Na mimi, tazama, nitakaa Mizpa, ili nisimame mbele ya Wakaldayo watakaotujilia; lakini ninyi chumeni divai, na matunda ya wakati wa jua, na mafuta, mkaviweke vitu hivyo katika vyombo vyenu, mkakae katika miji yenu mliyoitwaa.
11 Kadhalika waliposikia Wayahudi wote, waliokuwa katika Moabu, na kati ya wana wa Amoni, na hao waliokuwa katika Edomu, na hao waliokuwa katika nchi zote, ya kuwa mfalme wa Babeli amewaachia Yuda mabaki, na ya kuwa amemweka Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, juu yao;
12 basi, Wayahudi wote wakarudi kutoka kila mahali walikofukuzwa wakaenda mpaka nchi ya Yuda, wakamwendea Gedalia huko Mizpa, wakakusanya divai, na matunda ya wakati wa jua mengi sana.
13 Tena Yohana, mwana wa Karea, na wakuu wote wa majeshi ya barani, wakamwendea Gedalia huko Mizpa,
14 wakamwambia, Je! Una habari wewe ya kuwa Baalisi, mfalme wa wana wa Amoni, amemtuma Ishmaeli mwana wa Nethania, akuue? Lakini Gedalia, mwana wa Ahikamu, hakusadiki neno hili.
15 Basi, Yohana, mwana wa Karea, akamwambia Gedalia huko Mizpa kwa siri, akisema, Niache niende nikampige Ishmaeli, mwana wa Nethania, wala hapana mtu atakayejua jambo hili; kwani akuue wewe, hata wakatawanyike Wayahudi waliokukusanyikia, na mabaki ya Yuda wakaangamie?
16 Lakini Gedalia, mwana wa Ahikamu, akamwambia Yohana, mwana wa Karea, Usilitende jambo hili, maana unamsingizia Ishmaeli.

Yeremia 41


1 Basi ikawa katika mwezi wa saba, Ishmaeli, mwana wa Nethania, mwana wa Elishama, mmoja wa wazao wa kifalme, tena ni mmoja wa majemadari wa mfalme, na watu kumi pamoja naye, wakamwendea Gedalia, mwana wa Ahikamu, huko Mizpa; nao walikula chakula pamoja huko Mizpa.
2 Akaondoka huyo Ishmaeli, mwana wa Nethania, na watu wale kumi waliokuwa pamoja naye, wakampiga Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, kwa upanga, wakamwua; yeye ambaye mfalme wa Babeli amemweka kuwa liwali wa nchi.
3 Tena Ishmaeli akawaua Wayahudi wote waliokuwa pamoja naye, yaani, pamoja na Gedalia, huko Mizpa, na hao Wakaldayo walioonekana huko, yaani, watu wa vita.
4 Ikawa siku ya pili baada ya kumwua Gedalia, wala hapakuwa na mtu aliyejua habari hii,
5 wakafika watu kadha wa kadha toka Shekemu, na toka Shilo, na toka Samaria, watu themanini, nao wamenyoa ndevu zao, na kurarua nguo zao, nao wamejikata-kata, wakichukua sadaka na ubani mikononi mwao, ili wazilete nyumbani kwa Bwana.
6 Na Ishmaeli, mwana wa Nethania, akatoka Mizpa kwenda kuwalaki, akilia alipokuwa akiendelea; ikawa alipokutana nao akawaambia, Njoni kwa Gedalia, mwana wa Ahikamu.
7 Basi ikawa walipokuwa katikati ya mji, Ishmaeli, mwana wa Nethania, akawaua, akawatupa katika shimo, yeye na watu wale waliokuwa pamoja naye.
8 Lakini watu kumi walionekana miongoni mwao, waliomwambia Ishmaeli, Usituue; kwa maana tuna akiba zetu zilizofichwa kondeni, za ngano, na shayiri, na mafuta, na asali. Basi, akawaacha, asiwaue watu hao pamoja na ndugu zao.
9 Basi, shimo lile, ambalo Ishmaeli ameitupa mizoga ya watu aliowaua, karibu na Gedalia, (ni lile lile alilolichimba Asa, mfalme, kwa kuwa alimwogopa Baasha, mfalme wa Israeli), Ishmaeli, mwana wa Nethania, akalijaza kwa watu wale aliowaua.
10 Kisha Ishmaeli akawachukua mateka watu wote waliosalia, waliokuwa huko Mizpa, yaani, binti za mfalme, na watu wote waliobaki Mizpa, ambao Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, alikuwa amemkabidhi Gedalia, mwana wa Ahikamu; Ishmaeli, mwana wa Nethania, akawachukua mateka. akaondoka, ili awaendee wana wa Amoni.
11 Lakini Yohana, mwana wa Karea, na maakida wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, waliposikia habari za hayo mabaya yote aliyoyatenda Ishmaeli, mwana wa Nethania,
12 wakawatwaa watu wote, wakaenda ili kupigana na Ishmaeli, mwana wa Nethania, nao wakampata karibu na maji makuu ya Gibeoni.
13 Basi, ikawa, watu wote waliokuwa pamoja na Ishmaeli, walipomwona Yohana, mwana wa Karea, na hao maakida wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, ndipo wakafurahi.
14 Basi, watu wote, ambao Ishmaeli amewachukua mateka kutoka Mizpa, wakazunguka, wakarudi, wakamwendea Yohana, mwana wa Karea.
15 Lakini Ishmaeli, mwana wa Nethania, akaokoka pamoja na watu wanane, Yohana asimpate, akawaendea wana wa Amoni.
16 Ndipo Yohana, mwana wa Karea, na maakida wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, wakawatwaa hao watu wote waliosalia, aliowapata tena katika mikono ya Ishmaeli, mwana wa Nethania, huko Mizpa, baada ya kumwua Gedalia, mwana wa Ahikamu, yaani, watu wa vita, na wanawake na watoto, na matowashi, aliowarudisha toka Gibeoni;
17 wakaenda zao, wakakaa katika Geruthi Kimhamu, ulio karibu na Bethlehemu, ili wapate kuingia Misri,
18 kwa sababu ya Wakaldayo; maana waliwaogopa, kwa sababu Ishmaeli, mwana wa Nethania, amemwua Gedalia, mwana wa Ahikamu, ambaye mfalme wa Babeli amemweka kuwa liwali juu ya nchi.

Yeremia 42


1 Ndipo maakida wote wa majeshi, na Yohana, mwana wa Karea, na Yezania, mwana wa Hoshaya, na watu wote tangu wadogo hata wakubwa, wakakaribia,
2 wakamwambia Yeremia, nabii, Twakusihi, maombi yetu yakubaliwe mbele yako, ukatuombee kwa Bwana, Mungu wako, yaani, watu hawa wote waliosalia; maana tumesalia wachache tu katika watu wengi, kama macho yako yatuonavyo;
3 ili kwamba Bwana, Mungu wako, atuonyeshe njia ambayo yatupasa tuiendee, na jambo litupasalo tulitende.
4 Ndipo Yeremia, nabii, akawaambia, Nimewasikia; tazama, nitamwomba Bwana, Mungu wenu, sawasawa na maneno yenu; tena itakuwa, neno lo lote ambalo Bwana atawajibu, nitawaambia; sitawazuilia neno liwalo lote.
5 Wakamwambia Yeremia, Bwana na awe shahidi wa kweli na uaminifu kati yetu; ikiwa hatufanyi sawasawa na neno lile, ambalo Bwana, Mungu wako, atakutuma utuletee.
6 Likiwa jema, au likiwa baya, sisi tutaitii sauti ya Bwana, Mungu wetu, ambaye tunakutuma kwake; ipate kuwa faida yetu, tunapoitii sauti ya Bwana, Mungu wetu.
7 Ikawa, baada ya siku kumi, neno la Bwana likamjia Yeremia.
8 Ndipo akamwita Yohana, mwana wa Karea, na maakida wote wa majeshi waliokuwa pamoja naye, na watu wote tangu wadogo hata wakubwa,
9 akawaambia, Bwana, Mungu wa Israeli, ambaye mlinituma kwake, ili niyaweke maombi yenu mbele yake, asema hivi;
10 Ikiwa mtakaa bado katika nchi hii, ndipo nitawajenga, wala sitawabomoa, nami nitawapanda, wala sitawang'oa; kwa maana nayajutia mabaya niliyowatenda.
11 Msimwogope mfalme wa Babeli, mnayemwogopa; msimwogope, asema Bwana; maana mimi ni pamoja nanyi, niwaokoe, na kuwaponya na mkono wake.
12 Nami nitawapa rehema, kwamba awarehemu ninyi, na kuwarudisha mkae katika nchi yenu wenyewe.
13 Lakini mkisema, Hatutaki kukaa katika nchi hii; msiitii sauti ya Bwana, Mungu wenu;
14 mkisema, La! Lakini tutakwenda nchi ya Misri, ambayo hatutaona vita, wala kuisikia sauti ya tarumbeta, wala kuona njaa kwa kukosa chakula; nasi tutakaa huko;
15 basi, lisikieni neno la Bwana, enyi mabaki ya Yuda; Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ikiwa mwakaza nyuso zenu kuingia Misri, na kwenda kukaa huko;
16 basi, itakuwa, upanga mnaouogopa utawapata huko, katika nchi ya Misri, nayo njaa mnayoiogopa itawafuatia mbio huko Misri, nanyi mtakufa huko.
17 Haya ndiyo yatakayowapata watu wote waelekezao nyuso zao kwenda Misri, na kukaa huko; watakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesalia, au kuokoka katika mabaya nitakayoyaleta juu yao.
18 Maana Bwana wa majeshi Mungu wa Israeli, asema hivi, Kama hasira yangu, na ghadhabu yangu, ilivyomwagwa juu ya hao wakaao Yerusalemu, ndivyo ghadhabu yangu itakavyomwagwa juu yenu, mtakapoingia Misri; nanyi mtakuwa apizo, na ajabu, na laana, na aibu; wala hamtapaona mahali hapa tena.
19 Bwana asema katika habari zenu, enyi mabaki ya Yuda, Msiingie Misri; jueni sana ya kuwa nimewashuhudia hivi leo.
20 Maana mmetenda kwa hila juu ya nafsi zenu wenyewe; kwa kuwa mmenituma kwa Bwana, Mungu wenu, mkisema, Utuombee kwa Bwana, Mungu wetu, ukatufunulie sawasawa na yote atakayoyanena Bwana, Mungu wetu, nasi tutayatenda;
21 nami nimewafunulia haya leo; lakini ninyi hamkuitii sauti ya Bwana, Mungu wenu, katika neno lo lote ambalo amenituma kwenu.
22 Basi, sasa jueni sana ya kuwa mtakufa kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni, katika mahali pale mnapopatamani kwenda na kukaa.

Yeremia 43


1 Ikawa Yeremia alipokwisha kuwaambia watu wote maneno yote ya Bwana, Mungu wao, ambayo Bwana, Mungu wao, amemtuma kwao, yaani, maneno hayo yote,
2 ndipo Azaria, mwana wa Hoshaya, na Yohana mwana wa Karea, na watu wote wenye kiburi wakanena, wakimwambia Yeremia, Unasema uongo; Bwana, Mungu wetu, hakukutuma useme, Msiende Misri kukaa huko;
3 bali Baruku, mwana wa Neria, akushawishi kinyume chetu, ili kututia katika mikono ya Wakaldayo, ili watuue, na kutuchukua mateka mpaka Babeli.
4 Basi Yohana, mwana wa Karea, na wakuu wote wa majeshi, na watu wote hawakuitii sauti ya Bwana, kwamba wakae katika nchi ya Yuda.
5 Lakini Yohana, mwana wa Karea, na wakuu wote wa majeshi, wakawatwaa wote waliosalia wa Yuda, waliokuwa wamerudi kutoka taifa zote walikofukuzwa, wakae katika Yuda;
6 wanaume, na wanawake, na watoto, na binti za mfalme, na kila mtu ambaye Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, amemwacha pamoja na Gedalia, mwana wa Ahikamu, mwana wa Shafani, pia na Yeremia, nabii, na Baruku, mwana wa Neria;
7 wakaingia nchi ya Misri; maana hawakuitii sauti ya Bwana; wakafika hata Tahpanesi.
8 Ndipo neno la Bwana likamjia Yeremia huko Tahpenesi, kusema,
9 Twaa mawe makubwa mikononi mwako, ukayafiche ndani ya chokaa ya kazi ya matofali, penye maingilio ya nyumba ya Farao huko Tahpanesi, machoni pa watu wa Yuda;
10 ukawaambie, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitatuma na kumtwaa Nebukadreza, mfalme wa Babeli, mtumishi wangu, nami nitaweka kiti chake cha enzi juu ya mawe haya niliyoyaficha; naye atatandaza hema yake ya fahari juu yake.
11 Naye atakuja, na kuipiga nchi ya Misri; watu walioandikiwa kufa watakufa, nao walioandikiwa kuwa mateka watakuwa mateka, nao walioandikiwa kupigwa kwa upanga watapigwa kwa upanga.
12 Nami nitawasha moto katika nyumba za miungu ya Misri, na kuziteketeza, na kuwachukua mateka; naye atajipamba kwa nchi ya Misri, kama vile mchungaji avaavyo nguo zake; naye atatoka huko na amani.
13 Naye atazivunja nguzo za Bethshemeshi, iliyoko huko katika nchi ya Misri, na nyumba za miungu ya Misri ataziteketeza.

Yeremia 44


1 Neno lililomjia Yeremia, katika habari za Wayahudi wote waliokaa katika nchi ya Misri, waliokaa Migdoli, na Tahpanesi, na Nofu, na katika nchi ya Pathrosi, kusema,
2 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ninyi mmeona mabaya yote niliyoleta juu ya Yerusalemu, na juu ya miji yote ya Yuda; na, tazama, ni ukiwa leo, wala hapana mtu akaaye ndani yake;
3 kwa sababu ya uovu wao, waliotenda ili kunikasirisha, kwa kuwa walikwenda kufukiza uvumba, na kuwatumikia miungu mingine, ambao hawakuwajua, wao, wala ninyi, wala baba zenu.
4 Tena nalituma kwenu watumishi wangu wote, manabii, nikiamka mapema na kuwatuma, nikisema, Basi ninyi; msilifanye chukizo hili linichukizalo.
5 Lakini hawakusikiliza, wala hawakutega masikio yao, ili wageuke na kuacha uovu wao, wasifukizie uvumba miungu mingine.
6 Kwa sababu hiyo ghadhabu yangu, na hasira yangu, zilimwagika, nazo ziliwaka katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, na miji hiyo imeachwa ukiwa, na kuharibika, kama ilivyo leo.
7 Basi, sasa, Bwana, Mungu wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa nini mnafanya uovu huu mkubwa juu ya nafsi zenu wenyewe, kujikatilia mbali mwanamume na mwanamke, mtoto mchanga na anyonyaye, mtoke kati ya Yuda, msijiachie mtu abakiye;
8 kwa kuwa mnanikasirisha kwa matendo ya mikono yenu, mkifukizia uvumba miungu mingine katika nchi ya Misri, mlikokwenda kukaa ugenini; mpate kukatiliwa mbali, na kuwa laana, na aibu, katika mataifa yote ya dunia?
9 Je! Mmeusahau uovu wa baba zenu, na uovu wa wafalme wa Yuda, na uovu wa wake zao, na uovu wenu wenyewe, na uovu wa wake zenu, walioutenda katika nchi ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu?
10 Hawajanyenyekea hata leo, wala hawakuogopa, wala hawakuenenda katika sheria yangu, wala katika amri zangu, nilizoweka mbele yenu, na mbele ya baba zenu.
11 Basi, kwa sababu hiyo Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitaelekeza uso wangu juu yenu, ili niwaletee mabaya, hata kukatilia mbali Yuda yote.
12 Nami nitawatwaa mabaki ya Yuda, walioelekeza nyuso zao kuiingia nchi ya Misri, wakae huko, nao wataangamia wote pia; wataanguka katika nchi ya Misri; wataangamia kwa upanga, na kwa njaa; watakufa, tangu wadogo hata wakubwa, kwa upanga, na kwa njaa; nao watakuwa apizo, na ajabu, na laana, na aibu.
13 Kwa maana nitawaadhibu wakaao katika nchi ya Misri, kama nilivyouadhibu Yerusalemu, kwa upanga, na kwa njaa, na kwa tauni;
14 hata katika watu wale wa Yuda waliosalia, waliokwenda nchi ya Misri ili wakae huko, hapatakuwa na mtu ye yote atakayepona, wala atakayesalia, na kupata kurudi nchi ya Yuda, ambayo wanatamani kurudi ili kukaa huko; maana hapana atakayerudi, ila wao watakaopona.
15 Ndipo watu wote waliojua ya kuwa wake zao waliwafukizia uvumba miungu mingine, na wanawake wote waliosimama karibu, mkutano mkubwa, yaani, watu wote waliokaa katika nchi ya Misri, katika Pathrosi, wakamjibu Yeremia, wakisema,
16 Neno lile ulilotuambia kwa jina la Bwana, sisi hatutakusikiliza.
17 Lakini bila shaka tutalitimiza kila neno lililotoka katika vinywa vyetu, kumfukizia uvumba malkia wa mbinguni, na kummiminia sadaka za kinywaji, kama tulivyotenda sisi, na baba zetu, na wafalme wetu, na wakuu wetu, katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu; maana wakati huo tulikuwa na chakula tele, na kufanikiwa, wala hatukuona mabaya.
18 Lakini tulipoacha kumfukizia uvumba malkia wa mbinguni, na kummiminia sadaka za kinywaji, tumepungukiwa na vitu vyote; na kuangamizwa kwa upanga, na kwa njaa.
19 Nasi tulipomfukizia uvumba malkia wa mbinguni, na kummiminia sadaka za kinywaji, je! Tulimfanyizia mikate, ili kumwabudu, na kummiminia mamiminiko, waume zetu wasipokuwapo?
20 Ndipo Yeremia akawaambia watu wote, wanaume na wanawake, yaani, watu wote waliompa jibu lile, akisema,
21 Uvumba mliofukiza katika miji ya Yuda, na katika njia kuu za Yerusalemu, ninyi, na baba zenu, wafalme wenu, na wakuu wenu, na watu wa nchi, je! Bwana hakuwakumbuka watu hao? Je! Jambo hili halikuingia moyoni mwake?
22 Hata Bwana asiweze kuvumilia tena, kwa sababu ya uovu wa matendo yenu, na kwa sababu ya machukizo mliyoyafanya; kwa sababu hiyo nchi yenu imekuwa ukiwa, na ajabu, na laana, isikaliwe na mtu kama ilivyo leo.
23 Kwa sababu mmefukiza uvumba, na kwa sababu mmetenda dhambi juu ya Bwana, wala hamkuitii sauti ya Bwana, wala hamkwenda katika torati yake, wala katika amri zake, wala katika shuhuda yake; ndiyo maana mabaya haya yamewapata kama ilivyo leo.
24 Tena Yeremia akawaambia watu wote, na wanawake wote, Lisikieni neno hili la Bwana, ninyi nyote wa Yuda, mliopo hapa katika nchi ya Misri;
25 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ninyi na wake zenu mmenena kwa vinywa vyenu, na kutimiza kwa mikono yenu, mkisema, Bila shaka tutazitimiza nadhiri zetu tulizoziweka, na kumfukizia uvumba malkia wa mbinguni, na kummiminia sadaka za kinywaji; basi, zithibitisheni nadhiri zenu, zitimizeni nadhiri zenu.
26 Basi, kwa sababu hiyo lisikieni neno la Bwana, ninyi nyote wa Yuda, mnaokaa katika nchi ya Misri, Tazama, nimeapa kwa jina langu kuu, asema Bwana, ya kwamba jina langu halitatajwa tena katika kinywa cha mtu awaye yote wa Yuda, katika nchi yote ya Misri, akisema, Kama Bwana MUNGU aishivyo!
27 Tazama, nawaangalia niwaletee mabaya, wala si mema; nao watu wote wa Yuda, waliopo hapa katika nchi ya Misri, wataangamizwa kwa upanga, na kwa njaa, hata wakomeshwe kabisa.
28 Nao watakaoukimbia upanga, watatoka katika nchi ya Misri, na kuiingia nchi ya Yuda, watu wachache sana; na wote wa Yuda waliosalia, waliokwenda nchi ya Misri ili kukaa huko, watajua ni neno la nani litakalosimama, neno langu, au neno lao.
29 Na hii ndiyo itakayokuwa ishara kwenu, asema Bwana, kwamba mimi nitawaadhibu ninyi mahali hapa, mpate kujua ya kuwa maneno yangu yatasimama juu yenu, kuwaletea mabaya bila shaka;
30 Bwana asema hivi, Tazama, nitamtia Farao Hofra, mfalme wa Misri, katika mikono ya adui zake, na katika mikono yao wamtafutao roho yake; kama vile nilivyomtia Sedekia, mfalme wa Yuda, katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, adui yake aliyemtafuta roho yake.

Yeremia 45


1 Neno hili ndilo ambalo Yeremia, nabii, alimwambia Baruku, mwana wa Neria, alipoyaandika maneno haya katika kitabu kwa kinywa cha Yeremia, mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda, kusema,
2 Bwana, Mungu wa Israeli, akuambia wewe Ee Baruku;
3 Ulisema, Ole wangu! Kwa maana Bwana ameongeza huzuni pamoja na maumivu yangu. Nimechoka kwa ajili ya kuugua kwangu, wala sioni raha.
4 Basi, mwambie hivi, Bwana asema hivi, Tazama, niliyoyajenga nitayabomoa, na niliyoyapanda nitayang'oa; na haya yatakuwa katika nchi yote.
5 Je! Unajitafutia mambo makuu? Usiyatafute; kwa maana tazama, nitaleta mabaya juu ya wote wenye mwili, asema Bwana; lakini roho yako nitakupa iwe nyara, katika mahali pote utakapokwenda.

Yeremia 46


1 Neno la Bwana lililomjia Yeremia, nabii, katika habari za mataifa.
2 Katika habari za Misri; habari za jeshi la Farao Neko, mfalme wa Misri, lililokuwa karibu na mto Frati katika Karkemishi, ambalo Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alilipiga katika mwaka wa nne wa Yehoyakimu, mwana wa Yosia, mfalme wa Yuda.
3 Tengenezeni kigao na ngao, mkakaribie ili kupigana.
4 Watandikeni farasi; pandeni, enyi mpandao farasi; simameni na chapeo zenu, isugueni mikuki; zivaeni dirii.
5 Nimeyaona haya kwa sababu gani? Wamefadhaika, wamerudi nyuma; mashujaa wao wamevunjika-vunjika; wanakimbia upesi sana, hawatazami nyuma; hofu ziko pande zote; asema Bwana.
6 Mtu mwepesi asikimbie, wala shujaa asiokoke; pande za kaskazini karibu na mto Frati wamejikwaa na kuanguka.
7 Nani huyu ajiinuaye kama mto Nile, Ambaye maji yake yanajirusha kama mito?
8 Misri anajiinua kama mto Nile, Na maji yake yanajirusha kama mito; Asema, Nitajiinua, nitaifunikiza nchi; Nitauharibu mji na hao wakaao ndani yake.
9 Haya! Pandeni, enyi farasi; Jihimizeni, enyi magari ya vita; Mashujaa nao na watoke nje Kushi na Puti, watumiao ngao; Nao Waludi, washikao uta na kuupeta.
10 Maana hiyo ni siku ya Bwana, Bwana wa majeshi, Siku ya kisasi, ili ajilipize kisasi juu ya adui zake; Nao upanga utakula na kushiba, Utakunywa damu yao hata kukinai; Maana Bwana, Bwana wa majeshi, ana sadaka yake Katika nchi ya kaskazini karibu na mto Frati.
11 Panda uende Gileadi, ukatwae zeri, Ee binti, bikira wa Misri; unatumia dawa nyingi bure tu; hupati kupona kamwe.
12 Mataifa wamesikia habari za aibu yako, nayo dunia imejaa kilio chako; maana shujaa amejikwaa juu ya shujaa mwenzake, wameanguka wote wawili pamoja.
13 Neno hili ndilo ambalo Bwana alimwambia Yeremia, nabii, kueleza jinsi Nebukadreza, mfalme wa Babeli, atakavyokuja na kuipiga nchi ya Misri.
14 Tangazeni habari hii katika Misri, mkaihubiri katika Migdoli, na kuihubiri katika Nofu, na Tahpanesi; semeni, Simama, ujifanye tayari kwa maana upanga umekula pande zako zote.
15 Mbona mashujaa wako wamechukuliwa mbali? Hawakusimama kwa sababu Bwana aliwafukuza.
16 Aliwakwaza wengi, naam, wakaangukiana wao kwa wao; wakasema, Haya! Na tuondoke, tukarudi kwa watu wetu wenyewe, hata nchi tuliyozaliwa, tuukimbie upanga unaotuonea.
17 Wakalia huko, Farao, mfalme wa Misri, ni kishindo tu; muhula alioandikiwa ameuacha upite.
18 Kama mimi niishivyo, asema Mfalme, ambaye jina lake ni Bwana wa majeshi, hakika yake, kama Tabori katika milima, na kama Karmeli karibu na bahari, ndivyo atakavyokuja.
19 Ee binti ukaaye katika Misri, Ujiweke tayari kwenda zako hali ya kufungwa; Kwa maana Nofu utakuwa ukiwa, Utateketezwa, usikaliwe na watu.
20 Misri ni mtamba mzuri sana, lakini uharibifu umekuja, Umekuja utokao pande za kaskazini.
21 Na watu wake waliojiwa, walio kati yake, Ni kama ndama waliowanda malishoni; Maana wao nao wamerudi nyuma, Wamekimbia wote pamoja, wasisimame; Maana siku ya msiba wao imewafikilia, Wakati wa kujiliwa kwao.
22 Sauti yake ni kama nyoka, wajapo kwa nguvu, Watamjia na mashoka, kama wachanja kuni.
23 Wataukata msitu wake, asema Bwana, ingawa haupenyeki; Kwa maana ni wengi kuliko nzige, hawahesabiki.
24 Binti ya Misri ataaibishwa; Atatiwa mikononi mwa watu wa kaskazini.
25 Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, nitamwadhibu Amoni wa No, na Farao, na Misri, pamoja na miungu yake, na wafalme wake, naam, Farao, na hao wanaomtumainia;
26 nami nitawatia katika mikono ya hao wanaowatafuta roho zao, na katika mikono ya Nebukadreza, mfalme wa Babeli, na katika mikono ya watumishi wake; na baada ya hayo itakaliwa na watu, kama katika siku za kale, asema Bwana.
27 Lakini usiogope wewe, Ee Yakobo, mtumishi wangu; wala usifadhaike, Ee Israeli; kwa maana, tazama, nitakuokoa toka mbali, na wazao wako toka nchi ya uhamisho wao; na Yakobo atarudi, naye atatulia na kustarehe, wala hapana mtu atakayemtia hofu.
28 Usiogope wewe, Ee Yakobo, mtumishi wangu, asema Bwana; kwa maana mimi ni pamoja nawe; maana nitawakomesha kabisa mataifa yote huko nilikokufukuza, bali sitakukomesha wewe kabisa; lakini nitakurudi kwa hukumu, wala sitakuacha bila adhabu.

Yeremia 47


1 Neno la Bwana lililomjia Yeremia, nabii, katika habari za Wafilisti, kabla Farao hajapiga Gaza.
2 Bwana asema hivi, Tazama, maji yanatokea katika pande za kaskazini, nayo yatakuwa mto ufurikao, nayo yataifunika nchi, na kila kitu kilichomo, huo mji na wote wakaao ndani yake; nao watu watalia na watu wote wakaao katika nchi watapiga yowe.
3 Kwa sababu ya mshindo wa kukanyaga kwato za farasi wake walio hodari, kwa sababu ya mwendo wa mbiombio wa magari yake ya vita; kwa sababu ya ngurumo ya magurudumu yake, hao akina baba hawatazami nyuma ili kuwaangalia watoto wao, kwa kuwa mikono yao ni dhaifu;
4 kwa sababu ya siku ijayo kuwaangamiza Wafilisti wote, kukatilia mbali kila msaidizi wa Tiro na Sidoni asaliaye; maana Bwana atawaharibu Wafilisti, mabaki ya kisiwa cha Kaftori.
5 Upaa umeupata Gaza; Ashkeloni umenyamazishwa Mabaki ya bonde lao; Hata lini utajikata-kata?
6 Ee upanga wa Bwana, Siku ngapi zitapita kabla hujatulia? Ujitie katika ala yako; Pumzika, utulie.
7 Utawezaje kutulia, Ikiwa Bwana amekupa agizo? Juu ya Ashkeloni na juu ya pwani, Ndipo alipoyaamuru hayo.

Yeremia 48


1 Habari za Moabu. Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Ole wake Nebo! Kwa maana umeharibika; Kiriathaimu umeaibishwa, umetwaliwa; Misgabu umeaibishwa, nao umebomolewa.
2 Sifa za Moabu haziko tena; katika Heshboni wameazimia mabaya juu yake, Haya! Njoni, na tumkatilie mbali asiwe taifa. Wewe nawe, Ee Madmena, utanyamazishwa; upanga utakufuatia.
3 Sauti ya kilio toka Horonaimu, Ya kutekwa na uharibifu mkuu.
4 Moabu umeharibika; Wadogo wake wamewasikiza watu kilio.
5 Kwa maana watu wapandapo huko Luhithi Watapanda wasiache kulia; Nao watu watelemkapo huko Horonaimu Wameisikia huzuni ya kilio cha uharibifu.
6 Haya! Kimbieni! Jiokoeni nafsi zenu! Mkawe kama mtu aliye mkiwa.
7 Maana, kwa kuwa umeyatumainia matendo yako, na hazina zako, wewe nawe utatwaliwa; na Kemoshi atatoka aende katika uhamisho, makuhani wake na wakuu wake pamoja.
8 Naye mwenye kuteka nyara atakuja juu ya kila mji, wala hapana mji utakaookoka; bonde nalo litaangamia, nayo nchi tambarare itaharibiwa; kama Bwana alivyosema.
9 Mpe Moabu mabawa, apate kuruka na kwenda zake; na miji yake itakuwa ukiwa, isiwe na mtu wa kukaa ndani yake.
10 Na alaaniwe mtu afanyaye kazi ya Bwana kwa ulegevu; na alaaniwe auzuiaye upanga wake usimwage damu.
11 Moabu amestarehe tangu ujana wake, naye ametulia juu ya sira zake, wala hakumiminwa kutoka chombo kimoja kutiwa chombo kingine, wala hakwenda kufungwa; kwa hiyo ladha yake anakaa nayo, wala harufu yake haikubadilika.
12 Basi, tazama, siku zinakuja, asema Bwana, ambazo nitampelekea wamiminao, nao watammimina, nao watamwaga vyote vilivyomo vyomboni mwake, na kuzivunja chupa zake vipande vipande.
13 Na Moabu ataona haya kwa ajili ya Kemoshi, kama nyumba ya Israeli ilivyoona haya kwa ajili ya Betheli, matumaini yao.
14 Mwasemaje ninyi, Sisi tu mashujaa, watu hodari wa vita.
15 Moabu ameharibika, na moshi wa miji yake umepanda; na vijana wake wateule wametelemka kwenda kuchinjwa, asema Mfalme, ambaye jina lake ni Bwana wa majeshi.
16 Msiba wa Moabu umefika karibu, Na mateso yake yanafanya haraka.
17 Ninyi nyote mnaomzunguka, mlilieni, Nanyi nyote mlijuao jina lake, semeni, Jinsi ilivyovunjika fimbo ya enzi, Fimbo ile iliyokuwa nzuri!
18 Ee binti ukaaye Diboni, Shuka toka utukufu wako, ukae katika kiu; Maana atekaye Moabu amepanda juu yako, Ameziharibu ngome zako.
19 Wewe ukaaye Aroeri, Simama kando ya njia upeleleze; Mwulize mwanamume akimbiaye na mwanamke atorokaye, Sema, Imetendeka nini?
20 Moabu ameaibishwa, kwa maana amevunjika; Pigeni yowe na kulia; Tangazeni habari hii katika Arnoni, Ya kuwa Moabu ameharibika.
21 Na hukumu imeifikilia nchi tambarare; juu ya Holoni, na juu ya Yasa, na juu ya Mefaathi;
22 na juu ya Diboni, na juu ya Nebo, na juu ya Beth-diblathaimu;
23 na juu ya Kiriathaimu, na juu ya Beth-gamuli, na juu ya Beth-meoni;
24 na juu ya Keriothi, na juu ya Bozra, na juu ya miji yote ya nchi ya Moabu, iliyo mbali na iliyo karibu.
25 Pembe ya Moabu imekatika, na mkono wake umevunjika, asema Bwana. Mlevyeni; kwa maana alijitukuza juu ya Bwana
26 na Moabu atagaa-gaa katika matapiko yake, naye atadhihakiwa. Kwa maana Israeli, je! Hakuwa dhihaka kwako?
27 Alionekana kati ya wevi? Maana kila umtajapo watikisa kichwa chako.
28 Enyi mkaao Moabu, iacheni miji, Enendeni kukaa majabalini; Mkawe kama njiwa afanyaye kioto chake Katika ubavu wa mdomo wa shimo.
29 Tumesikia habari za kiburi cha Moabu; Ya kuwa ana kiburi kingi; Jeuri yake, na kiburi chake, na majivuno yake, Na jinsi alivyotakabari moyoni mwake.
30 Najua ghadhabu yake, asema Bwana, ya kuwa si kitu; majisifu yake hayakutenda neno lo lote.
31 Kwa sababu hiyo nitampigia yowe Moabu, naam, nitapiga kelele kwa ajili ya Moabu yote; nitawaombolezea watu wa Kir-heresi.
32 Nitakulilia, Ee mzabibu wa Sibma, kwa vilio vipitavyo vilio vya Yazeri; matawi yako yalipita juu ya bahari, yalifika hata bahari ya Yazeri; atekaye nyara ameyaangukia matunda yako ya wakati wa jua, na mavuno yako ya zabibu.
33 Furaha na shangwe zimeondoshwa, katika shamba lizaalo sana, na katika nchi ya Moabu; nami nimeikomesha divai katika mashinikizo; hapana mtu atakayekanyaga zabibu kwa shangwe; shangwe ile itakuwa si shangwe.
34 Toka kilio cha Heshboni mpaka Eleale, naam, mpaka Yahasa, wametoa sauti zao, toka Soari mpaka Horonaimu, hata Eglath-shelishia; maana maji ya Nimrimu nayo yatakuwa ukiwa.
35 Pamoja na hayo, asema Bwana, nitamkomesha katika Moabu mtu atoaye sadaka katika mahali pa juu, naye awafukiziaye uvumba miungu yake.
36 Kwa sababu hiyo moyo wangu watoa sauti kama filimbi kwa ajili ya Moabu, na kwa ajili ya watu wa Kir-heresi, moyo wangu watoa sauti kama filimbi; kwa kuwa wingi aliojipatia umepotea.
37 Maana kila kichwa kina upaa, na ndevu zote zimenyolewa; mikono yote ina alama za chale, na viuno vyote vimevikwa nguo za magunia.
38 Juu ya dari zote za nyumba za Moabu, na katika njia kuu zake, pana maombolezo, kila mahali; kwa maana nimevunja Moabu kama chombo kisichopendeza, asema Bwana.
39 Jinsi alivyovunjika! Pigeni yowe! Jinsi Moabu alivyogeuza kisogo kwa haya! Hivyo ndivyo Moabu atakavyokuwa dhihaka, na sababu ya kuwashangaza watu wote wamzungukao.
40 Maana Bwana asema hivi, Tazama, ataruka kama tai, na kutandaza mabawa yake juu ya Moabu.
41 Miji imetwaliwa, ngome zimeshambuliwa, na mioyo ya mashujaa wa Moabu siku hiyo itakuwa kama moyo wa mwanamke katika utungu wake.
42 Na Moabu ataangamizwa, asiwe taifa tena, kwa sababu alijitukuza juu ya Bwana.
43 Hofu, na shimo, na mtego, zaja juu yako, Ee mwenyeji wa Moabu, asema Bwana.
44 Aikimbiaye hofu ataanguka shimoni; na yeye atokaye shimoni atanaswa kwa mtego; maana nitaleta juu yake, yaani, juu ya Moabu, mwaka wa kujiliwa kwake, asema Bwana.
45 Wamekimbia, wasio na nguvu Wanasimama chini ya kivuli cha Heshboni; Ila moto umetoka katika Heshboni, Na mwali wa moto toka kati ya Sihoni Nao umekula pembe ya Moabu, Na utosi wa kichwa wa watu wapigao kelele.
46 Ole wako! Ee Moabu, Watu wa Kemoshi wamepotea; Maana wana wako wamechukuliwa mateka, Na binti zako wamekwenda utumwani.
47 Lakini nitawarudisha watu wa Moabu walio utumwani, siku za mwisho, asema Bwana. Hukumu ya Moabu imefikilia hapa.

Yeremia 49


1 Habari za wana wa Amoni. Bwana asema hivi, Je, Israeli hana wana? Je! Hana mrithi? Basi, mbona Malkamu anamiliki Gadi, na watu wake wanakaa katika miji yake?
2 Basi, kwa sababu hiyo, tazama, siku zinakuja, asema Bwana, nitakaposikizisha mshindo wa vita juu ya Raba, mji wa Amoni, nao utakuwa magofu ya ukiwa, na binti zake watateketezwa kwa moto; ndipo Israeli watawamiliki wao waliokuwa wakimmiliki, asema Bwana.
3 Piga yowe, Ee Heshboni, Kwa maana Ai umeangamizwa; Lieni, enyi binti za Raba, Mjivike nguo za magunia; Ombolezeni, mkipiga mbio Huko na huko kati ya maboma; Maana Malkamu atakwenda kuhamishwa, Makuhani wake na wakuu wake pamoja.
4 Mbona unajisifu kwa sababu ya mabonde, bonde lako litiririkalo, Ee binti mwenye kuasi? Utumainiaye hazina zako, ukisema, Ni nani atakayenijilia?
5 Tazama, nitaleta hofu juu yako, asema Bwana, Bwana wa majeshi, itakayotoka kwa wote wakuzungukao; nanyi mtafukuzwa nje, kila mtu mbali kabisa, wala hapana mtu wa kuwakusanya wapoteao.
6 Lakini baada ya hayo nitawarudisha wana wa Amoni walio utumwani, asema Bwana.
7 Habari za Edomu. Bwana wa majeshi asema hivi, Je! Hapana tena hekima katika Temani? Mashauri yamewapotea wenye busara? Je! Imetoweka hekima yao?
8 Kimbieni, rudini nyuma, kaeni chini sana, enyi mnaokaa Dedani; maana nitaleta msiba wa Esau juu yake, wakati nitakapomwangalia.
9 Je! Kama wachuma zabibu wangekujia, wasingeacha zabibu ziokotwe? Kama wangekujia wevi usiku, wasingeharibu hata watakapopata vya kutosha?
10 Lakini nimemwacha Esau hana kitu, nimepafunua mahali pake pa siri, wala hataweza kujificha; kizazi chake kimeangamizwa, na ndugu zake, na jirani zake, naye mwenyewe hayuko.
11 Waache watoto wako wasio na baba, mimi nitawahifadhi hai, na wajane wako na wanitumaini mimi.
12 Maana Bwana asema hivi, Tazama, wale wasioandikiwa kunywea kikombe, watakinywea, ni hakika; na wewe je! U mtu ambaye hataadhibiwa kabisa? Hukosi utaadhibiwa, naam, kunywa utakunywa.
13 Kwa maana nimeapa kwa nafsi yangu, asema Bwana, kwamba Bozra utakuwa ajabu, na aibu, na ukiwa, na laana; na miji yake yote itakuwa ukiwa wa daima.
14 Nimepata habari kwa Bwana, Na mjumbe ametumwa kati ya mataifa, Akisema, Jikusanyeni, mkaujie, Mkainuke kwenda vitani.
15 Maana nimekufanya mdogo kati ya mataifa, Na kudharauliwa katika watu.
16 Katika habari za kuogofya kwako, Kiburi cha moyo wako kimekudanganya, Wewe ukaaye katika pango za majabali, Ushikaye kilele cha milima; Ujapofanya kioto chako juu sana kama tai, Nitakushusha kutoka huko; asema Bwana.
17 Na Edomu atakuwa ajabu; kila mtu apitaye atashangaa, na kuzomea, kwa sababu ya mapigo yake yote.
18 Kama vile vilivyotokea wakati wa kuangushwa Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa karibu nayo, asema Bwana; hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo.
19 Angalia, atapanda kama simba toka kiburi cha Yordani juu ya malisho yasiyonyauka; lakini nitamkimbiza ghafula ayaache; na yeye aliye mteule nitamweka juu yake; maana ni nani aliye kama mimi? Tena ni nani atakayeniandikia muda? Tena ni mchungaji yupi atakayesimama mbele zangu?
20 Basi, lisikieni shauri la Bwana; Alilolifanya juu ya Edomu; Na makusudi yake aliyoyakusudia Juu yao wakaao Temani; Hakika watawaburura, naam, wadogo wa kundi; Hakika malisho yao yatafadhaika kwa ajili yao.
21 Nchi yatetemeka kwa sauti ya kuanguka kwao; Kuna kilio, sauti yake yasikiwa katika Bahari ya Shamu.
22 Tazama, atapanda na kuruka kama tai, na kutandaza mabawa yake juu ya Bozra; na mioyo ya mashujaa wa Edomu siku hiyo itakuwa kama moyo wa mwanamke katika utungu wake.
23 Habari za Dameski. Hamathi umetahayarika, na Arpadi pia; Maana wamesikia habari mbaya; Wameyeyuka kabisa; Huzuni iko baharini, haiwezi kutulia.
24 Dameski umedhoofika; Umejigeuza kukimbia; tetemko limeushika; Dhiki na huzuni zimeupata, Kama za mwanamke katika utungu wake.
25 Imekuwaje mji wa sifa haukuachwa, mji wa furaha yangu?
26 Kwa hiyo vijana wake wataanguka katika njia kuu zake, na watu wote wa vita watanyamazishwa katika siku hiyo, asema Bwana wa majeshi.
27 Nami nitawasha moto katika ukuta wa Dameski, nao utayateketeza majumba ya Ben-hadadi.
28 Habari za Kedari, na za falme za Hazori, ambazo Nebukadreza, mfalme wa Babeli, alizipiga. Bwana asema hivi, Ondokeni, pandeni hata Kedari, mkawateke nyara wana wa mashariki.
29 Hema zao na makundi yao watayatwaa; watachukulia mbali mapazia yao kwa faida yao wenyewe, na vyombo vyao vyote, na ngamia zao; nao watawapigia kelele wakisema, Hofu ziko pande zote.
30 Kimbieni ninyi, enendeni mbali mkitanga-tanga, kaeni chini sana, enyi mkaao Hazori, asema Bwana; maana Nebukadreza, mfalme wa Babeli, amefanya shauri juu yenu, naye amekusudia neno juu yenu.
31 Ondokeni, pandeni hata taifa lililo katika hali ya raha, likaalo bila kuhangaika, asema Bwana; wasio na malango wala makomeo, wakaao peke yao.
32 Na ngamia zao watakuwa mateka, na wingi wa makundi yao utakuwa nyara; nami nitawatawanya hata pepo zote watu wale wanyoao denge; nami nitaleta msiba wao toka pande zao zote, asema Bwana.
33 Na Hazori utakuwa kao la mbwa-mwitu; ukiwa milele; hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama mgeni akaavyo.
34 Neno la Bwana lililomjia Yeremia, nabii, juu ya Elamu, mwanzo wa kumiliki kwake Sedekia, mfalme wa Yuda, kusema,
35 Bwana wa majeshi asema hivi, Tazama nitauvunja upinde wa Elamu, ulio mkuu katika nguvu zao.
36 Na juu ya Elamu nitazileta pepo nne, toka pembe nne za mbinguni, nami nitawatawanya hata pepo nne zote, wala hapana taifa ambalo hawatalifikilia watu wa Elamu waliofukuzwa.
37 Nami nitawafadhaisha watu wa Elamu mbele ya adui zao, na mbele ya hao wanaowatafuta roho zao; nami nitawaletea mabaya, naam, hasira yangu kali, asema Bwana; nami nitautuma upanga uwafuatie, hata nitakapowaangamiza;
38 nami nitaweka kiti changu cha enzi huko Elamu, nami nitawaharibu, mfalme na wakuu, watoke huko, asema Bwana.
39 Lakini itakuwa, katika siku za mwisho, nitawarudisha wafungwa wa Elamu, asema Bwana.

Yeremia 50


1 Neno hili ndilo alilosema Bwana, katika habari za Babeli, na katika habari za Wakaldayo, kwa kinywa cha Yeremia, nabii.
2 Tangazeni katika mataifa, Mkahubiri na kutweka bendera; Hubirini, msifiche, semeni, Babeli umetwaliwa! Beli amefedheheka; Merodaki amefadhaika; Sanamu zake zimeaibishwa, Vinyago vyake vimefadhaika.
3 Maana toka kaskazini taifa linakuja juu yake, litakaloifanya nchi yake kuwa ukiwa; wala hapana mtu atakayekaa humo; wamekimbia, wamekwenda zao, mwanadamu na mnyama pia.
4 Katika siku hizo, na wakati huo, asema Bwana, wana wa Israeli watakuja, wao na wana wa Yuda pamoja; Wataendelea njiani mwao wakilia, nao watamtafuta Bwana, Mungu wao.
5 Watauliza habari za Sayuni, na nyuso zao zitaelekea huko, wakisema, Njoni ninyi, mjiunge na Bwana, kwa agano la milele ambalo halitasahauliwa.
6 Watu wangu wamekuwa kondoo waliopotea, wachungaji wao wamewapoteza; wamewapotosha milimani; wamekwenda toka mlima hata kilima, wamesahau mahali pao pa kupumzika.
7 Watu wote waliowaona wamewala; na adui zao walisema, Sisi hatuna hatia, kwa kuwa hao wametenda dhambi juu ya Bwana, aliye kao la haki, yaani, Bwana, tumaini la baba zao.
8 Kimbieni kutoka kati ya Babeli, mkatoke katika nchi ya Wakaldayo, mkawe kama mabeberu mbele ya makundi.
9 Kwa maana juu ya Babeli nitaamsha na kuleta kusanyiko la mataifa makubwa, toka nchi ya kaskazini; nao watajipanga juu yake; kutoka huko atatwaliwa; mishale yao itakuwa kama ya mtu shujaa aliye stadi; hapana hata mmoja utakaorudi bure.
10 Nao Ukaldayo utakuwa mateka; wote wautekao watashiba, asema Bwana.
11 Kwa sababu mnafurahi, kwa sababu mnashangilia, enyi mnaouteka urithi wangu, kwa sababu mmewanda kama mtamba akanyagaye nafaka, nanyi mnalia kama farasi wenye nguvu;
12 mama yenu atatahayarika sana; yeye aliyewazaa atafadhaika; tazama, atakuwa taifa lililo nyuma katika mataifa yote, atakuwa jangwa, nchi ya ukame, na nyika.
13 Kwa sababu ya ghadhabu ya Bwana haitakaliwa na mtu, bali itakuwa ukiwa mtupu; kila mtu apitaye karibu na Babeli atashangaa, atazomea kwa sababu ya mapigo yake yote.
14 Jipangeni juu ya Babeli pande zote, Ninyi nyote mpindao upinde; Mpigeni, msiuzuie hata mshale mmoja; Kwa maana amemtenda Bwana dhambi.
15 Mpigieni kelele pande zote; amejitoa; Maboma yake yameanguka, kuta zake zimebomolewa; Kwa maana ni kisasi cha Bwana; mlipizeni kisasi; Kama yeye alivyotenda, mtendeni yeye.
16 Mpanzi mkatilie mbali na Babeli, Naye ashikaye mundu wakati wa mavuno; Kwa sababu ya kuuogopa upanga uoneao, Watageuka kila mtu kwa watu wake, Nao wataikimbilia kila mmoja nchi yake.
17 Israeli ni kondoo aliyetawanywa; simba wamemfukuzia mbali; kwanza mfalme wa Ashuru amemla, na mwisho Nebukadreza huyu, mfalme wa Babeli, amemvunja mifupa yake.
18 Basi, Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi, Tazama, mimi nitamwadhibu mfalme wa Babeli, na nchi yake, kama nilivyomwadhibu mfalme wa Ashuru.
19 Nami nitamleta Israeli tena malishoni kwake, naye atalisha juu ya Karmeli, na Bashani, na nafsi yake itashiba juu ya milima ya Efraimu, na katika Gileadi.
20 Katika siku hizo na wakati huo, asema Bwana, uovu wa Israeli utatafutwa, wala uovu hapana; na dhambi za Yuda zitatafutwa, wala hazitaonekana; maana nitawasamehe wale niwaachao kuwa mabaki.
21 Panda juu ya nchi ya Merathaimu, naam, juu yake, na juu yao wakaao Pekodi; ua, ukaangamize nyuma yao, asema Bwana, ukatende kama nilivyokuagiza, yote pia.
22 Pana mshindo wa vita katika nchi, Mshindo wa uharibifu mkuu.
23 Imekuwaje nyundo ya dunia yote Kukatiliwa mbali na kuvunjwa? Imekuwaje Babeli kuwa ukiwa Katikati ya mataifa?
24 Nimekutegea mtego, Ee Babeli, nawe ukanaswa, nawe ulikuwa huna habari; umeonekana, ukakamatwa, kwa sababu ulishindana na Bwana.
25 Bwana amefungua akiba yake ya silaha, naye amezitoa silaha za ghadhabu yake; maana Bwana, Bwana wa majeshi, ana kazi atakayofanya katika nchi ya Wakaldayo.
26 Njoni juu yake toka mpaka ulio mbali; Zifungueni ghala zake; Mfanyeni kuwa magofu na kumharibu kabisa; Msimsazie kitu cho chote.
27 Wachinjeni mafahali wake wote; Na watelemkie machinjoni; Ole wao! Maana siku yao imewadia, Wakati wa kujiliwa kwao.
28 Sauti yao wakimbiao na kuokoka, Kutoka katika nchi ya Babeli, Ili kutangaza Sayuni kisasi cha Bwana, Mungu wetu, Kisasi cha hekalu lake.
29 Waiteni wapiga mishale juu ya Babeli, Naam, wote waupindao upinde; Pangeni hema kumzunguka pande zote; Ili asiokoke hata mtu mmoja wao; Mlipeni kwa kadiri ya kazi yake; Mtendeni sawasawa na yote aliyoyatenda; Kwa sababu amefanya kiburi juu ya Bwana, Juu yake aliye Mtakatifu wa Israeli.
30 Kwa sababu hiyo vijana wake wataanguka katika njia kuu zake, na watu wake wa vita, wote pia, watanyamazishwa katika siku hiyo, asema Bwana.
31 Tazama, mimi ni juu yako, Ewe mwenye kiburi, asema Bwana, Bwana wa majeshi; maana siku yako imewadia, wakati nitakapokujilia.
32 Na mwenye kiburi atajikwaa, na kuanguka, wala hapana atakayemwinua; nami nitawasha moto katika miji yake, nao utawala wote wamzungukao pande zote.
33 Bwana wa majeshi asema hivi, Wana wa Israeli, na wana wa Yuda, wameonewa pamoja; na wote waliowachukua mateka wanawashika sana; wanakataa kuwaacha.
34 Mkombozi wao ni hodari; Bwana wa majeshi ndilo jina lake; yeye atawatetea kwa bidii, apate kuistarehesha nchi, na kuwasumbua wakaao katika Babeli.
35 Upanga u juu ya Wakaldayo, asema Bwana, na juu yao wakaao Babeli, na juu ya wakuu wake, na juu ya watu wake wenye hekima.
36 Upanga u juu ya hao wajisifuo, nao watapumbazika; upanga u juu ya mashujaa wake, nao watafadhaika.
37 Upanga u juu ya farasi zao, na juu ya magari yao ya vita; na juu ya watu wote waliochanganyika ndani yake, nao watakuwa kama wanawake; upanga u juu ya hazina zake, nazo zitaibwa.
38 Ukosefu wa mvua u juu ya maji yake, nayo yatakaushwa; maana ni nchi ya sanamu za kuchongwa, nao wameingiwa na wazimu kwa ajili ya sanamu.
39 Basi, wanyama wakali wa jangwani, pamoja na mbwa-mwitu, watakaa huko, na mbuni watakaa ndani yake; wala haitakaliwa na watu milele; wala hapana mtu atakayekaa huko tangu kizazi hata kizazi.
40 Kama vile vilivyotokea Mungu alipoangusha Sodoma na Gomora, na miji iliyokuwa karibu nayo, asema Bwana; kadhalika hapana mtu atakayekaa huko, wala hapana mwanadamu atakayekaa huko kama wageni wakaavyo.
41 Angalia, watu wanakuja watokao kaskazini; na taifa kubwa, na wafalme wengi wataamshwa toka pande za mwisho za dunia.
42 Wanashika upinde na mkuki; Ni wakatili, hawana huruma; Sauti yao inanguruma kama bahari, Nao wamepanda farasi; Kila mmoja amejipanga kama aendaye vitani, Juu yako, Ee binti Babeli.
43 Mfalme wa Babeli amesikia habari zao, Na mikono yake imekuwa dhaifu; Dhiki imemshika, na maumivu, Kama ya mwanamke katika utungu wake.
44 Angalia, atapanda kama simba toka kiburi cha Yordani juu ya malisho yasiyonyauka; lakini nitamkimbiza ghafula ayaache; na yeye aliye mteule nitamweka juu yake; maana ni nani aliye kama mimi? Tena ni nani atakayeniandikia muda? Tena ni mchungaji yupi atakayesimama mbele zangu?
45 Basi, lisikieni shauri la Bwana, Alilolifanya juu ya Babeli; Na makusudi yake aliyoyakusudia Juu ya nchi ya Wakaldayo. Hakika watawaburura, naam, wadogo wa kundi; Hakika malisho yao yatafadhaika kwa ajili yao.
46 Kwa mshindo wa kutwaliwa Babeli nchi yatetemeka, Na kilio chake chasikiwa katika mataifa.

Yeremia 51


1 Bwana asema hivi, Angalia, nitaamsha juu ya Babeli, na juu yao wakaao Leb-kamai upepo uharibuo.
2 Nami nitapeleka wageni mpaka Babeli, watakaompepea; nao wataifanya nchi yake kuwa tupu; kwa kuwa katika siku ya taabu watakuwa juu yake pande zote.
3 Juu yake apindaye upinde, mwenye upinde na apinde upinde wake, na juu yake ajiinuaye katika dirii yake; msiwaachilie vijana wake; liangamizeni jeshi lake lote.
4 Nao wataanguka, hali ya kuuawa, katika nchi ya Wakaldayo, hali ya kutumbuliwa katika njia kuu zake.
5 Kwa maana Israeli, wala Yuda, hakuachwa na Mungu wake, Bwana wa majeshi; ijapokuwa nchi yao imejaa hatia juu yake aliye Mtakatifu wa Israeli.
6 Kimbieni kutoka kati ya Babeli, kila mtu na ajiokoe nafsi yake; msikatiliwe mbali katika uovu wake; maana ni wakati wa kisasi cha Bwana, atamlipa malipo.
7 Babeli umekuwa kikombe cha dhahabu mkononi mwa Bwana; kilicholevya dunia yote; mataifa wamekunywa mvinyo wake; kwa sababu hiyo mataifa wameingiwa na wazimu.
8 Babeli umeanguka na kuangamia ghafula; mpigieni yowe; twaeni zeri kwa maumivu yake; ili labda apate kuponywa.
9 Tungependa kuuponya Babeli, Lakini haukuponyeka; Mwacheni, nasi twendeni zetu, Kila mtu hata nchi yake mwenyewe; Maana hukumu yake inafika hata mbinguni, Nayo imeinuliwa kufikilia mawinguni.
10 Bwana ameitokeza haki yetu; Njoni, tutangaze katika Sayuni Habari za kazi ya Bwana, Mungu wetu.
11 Inoeni hiyo mishale; zishikeni ngao kwa nguvu; Bwana ameziamsha roho za wafalme wa Wamedi; kwa sababu shauri lake ni juu ya Babeli auangamize; maana ni kisasi cha Bwana, kisasi cha hekalu lake.
12 Twekeni bendera juu ya kuta za Babeli, yatieni malindo nguvu, wawekeni walinzi, tengenezeni waviziao; kwa maana Bwana ameazimia na kutenda yote aliyoyasema juu yao wakaao Babeli.
13 Ewe ukaaye juu ya maji mengi, uliye na hazina nyingi, mwisho wako umewadia, kadiri ya tamaa zako.
14 Bwana wa majeshi ameapa kwa nafsi yake, akisema, Hakika nitakujaza watu, kama nzige, nao watapiga kelele juu yako.
15 Ameiumba dunia kwa uweza wake, Ameuthibitisha ulimwengu kwa hekima yake, Na kwa ufahamu wake amezitandika mbingu.
16 Atoapo sauti yake pana mshindo wa maji mbinguni, Naye hupandisha mawingu toka ncha za nchi; Huifanyia mvua umeme, Huutoa upepo katika hazina zake.
17 Kila mtu amekuwa kama mnyama, hana maarifa; Kila mfua dhahabu amefedheheshwa na sanamu yake ya kuchonga; Maana sanamu yake ya kuyeyuka ni uongo, Wala hamna pumzi ndani yake.
18 Ni ubatili tu, ni kazi za udanganyifu; Wakati wa kujiliwa kwao watapotea.
19 Yeye, Fungu la Yakobo, siye kama hawa; Maana ndiye aliyeviumba vitu vyote; Na Israeli ni kabila ya urithi wake; Bwana wa majeshi ndilo jina lake.
20 Wewe u rungu langu na silaha zangu za vita; kwa wewe nitawavunja-vunja mataifa; na kwa wewe nitaharibu falme;
21 na kwa wewe nitamvunja-vunja farasi, na yeye ampandaye; na kwa wewe nitalivunja-vunja gari la vita, na yeye achukuliwaye ndani yake;
22 na kwa wewe nitawavunja-vunja mwanamume na mwanamke; na kwa wewe nitawavunja-vunja mzee na mtoto; na kwa wewe nitawavunja-vunja kijana mwanamume na kijana mwanamke;
23 na kwa wewe nitamvunja-vunja mchungaji na kundi lake; na kwa wewe nitamvunja-vunja mkulima na jozi yake ya ng'ombe; na kwa wewe nitawavunja-vunja maliwali na maakida.
24 Nami nitamlipa Babeli, na wote wakaao ndani ya Ukaldayo, mabaya yao yote, waliyoyatenda katika Sayuni mbele ya macho yenu, asema Bwana.
25 Tazama, mimi ni juu yako, Ee mlima uharibuo, asema Bwana; wewe uiharibuye dunia nzima; nami nitaunyosha mkono wangu juu yako, na kukufingirisha chini toka majabalini; nami nitakufanya kuwa mlima ulioteketezwa.
26 Wala hawatatwaa kwako jiwe moja liwe la pembeni, wala jiwe moja liwe msingi; bali wewe utakuwa ukiwa daima, asema Bwana.
27 Itwekeni bendera katika nchi, pigeni tarumbeta kati ya mataifa, yawekeni mataifa tayari juu yake; ziiteni juu yake falme za Ararati, na Mini, na Ashkenazi; agizeni jemadari juu yake; wapandisheni farasi, kama tunutu.
28 Wekeni mataifa tayari juu yake, wafalme wa Wamedi, na maliwali wake, na maakida wake, na nchi yote ya mamlaka yake.
29 Nayo nchi yatetemeka, nayo ina utungu; maana makusudi ya Bwana juu ya Babeli yasimama, kuifanya nchi ya Babeli ukiwa, isikaliwe na mtu.
30 Mashujaa wa Babeli wameacha kupigana; Wanakaa katika ngome zao; Ushujaa wao umewapungukia; Wamekuwa kama wanawake; Makao yake yameteketea; Makomeo yake yamevunjika.
31 Tarishi mmoja atapiga mbio kumlaki mwingine, Na mjumbe mmoja atapiga mbio kumlaki mwenziwe, Ili kumpasha habari mfalme wa Babeli, Ya kuwa mji wake umetwaliwa kila upande.
32 Navyo vivuko vimeshambuliwa, Nayo makangaga wameyatia moto, Nao watu wa vita wameingiwa na hofu.
33 Kwa maana Bwana wa majeshi, Mungu wa Israeli, asema hivi; Binti Babeli amekuwa kama sakafu ya kufikichia wakati wa kukanyagwa kwake; bado kitambo kidogo na wakati wa mavuno utafika kwake.
34 Nebukadreza, mfalme wa Babeli, amenila, ameniseta, amenifanya kuwa chombo kitupu; amenimeza kama joka, amelijaza tumbo lake vitu vyangu vya anasa; amenitupa
35 Udhalimu niliotendwa mimi, na uliotendwa mwili wangu, umpate Babeli; ndivyo atakavyosema yeye akaaye Sayuni; na Yerusalemu atasema, Damu yangu na iwe juu yao wakaao katika Ukaldayo.
36 Basi, Bwana asema hivi, Tazama, nitakutetea, nami nitatwaa kisasi kwa ajili yako; nami nitaikausha bahari yake, nitaifanya chemchemi yake kuwa pakavu.
37 Na Babeli utakuwa magofu, makao ya mbwa-mwitu, ajabu, na mazomeo, pasipo mtu wa kukaa huko.
38 Watanguruma pamoja kama wana-simba; watanguruma kama simba wachanga.
39 Wakiingiwa na ukali, nitawafanyizia karamu yao, nami nitawalevya, wapate kufurahi, na kulala usingizi wa milele, wasiamke tena, asema Bwana.
40 Nitawatelemsha kama wana-kondoo machinjoni, kama kondoo waume pamoja na mabeberu.
41 Jinsi Sheshaki alivyotwaliwa! Naye sifa ya dunia yote alivyoshambuliwa! Jinsi Babeli alivyokuwa ukiwa katikati ya mataifa.
42 Bahari imefika juu ya Babeli, Umefunikwa kwa wingi wa mawimbi yake.
43 Miji yake imekuwa maganjo; Nchi ya ukame, na jangwa; Nchi asimokaa mtu ye yote, Wala hapiti mwanadamu huko.
44 Nami nitafanya hukumu juu ya Beli katika Babeli, nami nitavitoa katika kinywa chake alivyovimeza; wala mataifa hawatamwendea tena; naam, ukuta wa Babeli utaanguka.
45 Enyi watu wangu; tokeni katikati yake, mkajiokoe nafsi zenu na hasira kali ya Bwana, kila mmoja wenu.
46 Wala isizimie mioyo yenu, wala msiiogope habari itakayosikiwa katika nchi; maana habari itakuja mwaka mmoja, na baadaye mwaka wa pili habari itakuja, na udhalimu katika nchi, mwenye kutawala akishindana na mwenye kutawala.
47 Basi angalia, siku zitakuja, ambazo katika siku hizo, nitafanya hukumu juu ya sanamu za Babeli, na nchi yake yote itatahayarika; na watu wake wote waliouawa wataanguka katikati yake.
48 Ndipo mbingu, na nchi, na vitu vyote vilivyomo, vitaimba kwa furaha juu ya Babeli; kwa maana watu waangamizao watamjilia kutoka kaskazini, asema Bwana.
49 Kama vile Babeli alivyowaangusha watu wa Israeli waliouawa, ndivyo watakavyoanguka katika Babeli watu wa nchi yake nzima waliouawa.
50 Ninyi mliojiepusha na upanga, Enendeni zenu, msisimame; Mkumbukeni Bwana tokea mbali, Na Yerusalemu ukatiwe mioyoni mwenu.
51 Twaona haya kwa kuwa tumesikia mashutumu; Fedheha imetufunikiza nyuso zetu; Kwa sababu wageni wamepaingia Patakatifu pa nyumba ya Bwana.
52 Kwa sababu hiyo siku zinakuja, asema Bwana, nitakapozihukumu sanamu zake; na katika nchi yake yote waliojeruhiwa wataugua.
53 Babeli ujapopanda mbinguni, na ujapopafanya mahali pa juu penye nguvu zake kuwa ngome, hata hivyo toka kwangu wenye kuangamiza watamwendea, asema Bwana.
54 Sauti ya kilio kutoka Babeli, Na ya uangamivu mkuu toka nchi ya Wakaldayo!
55 Maana Bwana amwangamiza Babeli, Na kuikomesha sauti kuu ndani yake; Na mawimbi yake yavuma kama maji mengi, Mshindo wa sauti zao wafanya makelele;
56 Kwa maana mwenye kuangamiza amefika kwake; Naam, amefika Babeli; Na mashujaa wake wametwaliwa; Pinde zao zimevunjika kabisa; Maana Bwana ni Mungu wa kisasi; Hakika yake yeye atalipa.
57 Nami nitawalevya wakuu wake, na watu wake wenye hekima, maliwali wake, na maakida wake, na mashujaa wake; nao watalala usingizi wa milele, wasiamke, asema Mfalme, Bwana wa majeshi, ambaye jina lake ni Bwana.
58 Bwana wa majeshi asema hivi, Kuta pana za Babeli zitabomolewa kabisa, na malango yake marefu yatateketezwa; nao watu watajitaabisha kwa ubatili, na mataifa kwa moto; nao watachoka.
59 Neno ambalo Yeremia, nabii, alimwamuru Seraya, mwana wa Neria, mwana wa Maaseya, alipokwenda Babeli pamoja na Sedekia, mfalme wa Yuda, katika mwaka wa nne wa kumiliki kwake. Basi Seraya alikuwa msimamizi mkuu wa nyumba ya mfalme.
60 Naye Yeremia akaandika katika kitabu habari ya mabaya yote yatakayoupata Babeli, maneno hayo yote yaliyoandikwa juu ya Babeli.
61 Naye Yeremia akamwambia Seraya, Utakapofika Babeli, basi angalia uyasome maneno haya yote,
62 ukaseme, Ee Bwana, umenena habari za mji huu kwamba utakatiliwa mbali, usikaliwe na awaye yote, wala wanadamu wala wanyama, lakini uwe ukiwa hata milele.
63 Tena itakuwa utakapokwisha kukisoma kitabu hicho, utakifungia jiwe, na kukitupa katika mto Frati;
64 nawe utasema, Hivyo ndivyo utakavyozama Babeli, wala hautazuka tena, kwa sababu ya mabaya yote nitakayoleta juu yake; nao watachoka. Maneno ya Yeremia yamefika hata hapa.

Yeremia 52


1 Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja hapo alipoanza kumiliki; naye akamiliki miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Hamutali, binti Yeremia wa Libna.
2 Naye alitenda yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na yote aliyoyatenda Yehoyakimu.
3 Maana, kwa sababu ya hasira ya Bwana, mambo haya yalitokea katika Yerusalemu na katika Yuda, hata akawaondosha wasiwe mbele za uso wake, naye Sedekia akamwasi mfalme wa Babeli.
4 Ikawa, katika mwaka wa kenda wa kumiliki kwake, katika mwezi wa kumi, na siku ya kumi ya mwezi huo, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akaja, yeye na jeshi lake lote, juu ya Yerusalemu, akapanga hema zake juu yake; nao wakajenga ngome juu yake pande zote.
5 Basi mji huo ulihusuriwa hata mwaka wa kumi na mmoja wa mfalme Sedekia.
6 Katika mwezi wa nne, siku ya kenda ya mwezi, njaa ilizidi sana ndani ya mji, hata hapakuwa na chakula kwa watu wa nchi.
7 Ukuta wa mji ukabomolewa, watu wote wa vita wakakimbia, wakatoka mjini usiku, kwa njia ya lango lililokuwa kati ya zile kuta mbili, karibu na bustani ya mfalme; (basi wale Wakaldayo walikuwa wameuzunguka mji pande zote;) wakaenda zao kwa njia ya Araba.
8 Lakini jeshi la Wakaldayo wakamfuatia mfalme, wakampata Sedekia katika nchi tambarare ya Yeriko, na jeshi lake lote walikuwa wametawanyika na kumwacha.
9 Nao wakamshika mfalme, wakamchukua kwa mfalme wa Babeli, aliyekuwa huko Ribla katika nchi ya Hamathi, naye akatoa hukumu juu yake.
10 Ndipo mfalme wa Babeli akawaua wana wa Sedekia mbele ya macho yake; pia akawaua wakuu wote wa Yuda huko Ribla.
11 Akampofusha macho Sedekia; tena mfalme wa Babeli akamfunga kwa pingu, akamchukua mpaka Babeli, akamtia gerezani hata siku ya kufa kwake.
12 Basi katika mwezi wa tano, siku ya kumi ya mwezi, ndio mwaka wa kumi na kenda wa mfalme Nebukadreza, mfalme wa Babeli; Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, aliyesimama mbele ya mfalme wa Babeli, aliingia Yerusalemu.
13 Akaiteketeza nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme; na nyumba zote za Yerusalemu, naam, kila nyumba kubwa aliiteketeza kwa moto.
14 Na jeshi lote la Wakaldayo, waliokuwa pamoja na huyo amiri wa askari walinzi, wakazibomoa kuta zote za Yerusalemu pande zote.
15 Kisha Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawachukua wafungwa baadhi ya watu waliokuwa maskini, na mabaki ya watu walioachwa katika mji, nao wale walioasi na kumkimbilia mfalme wa Babeli, nao mabaki ya vibarua.
16 Lakini Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawaacha watu walio maskini kabisa ili wawe watunza mizabibu na wakulima.
17 Na nguzo za shaba zilizokuwa katika nyumba ya Bwana, na matako ya bahari ya shaba iliyokuwa katika nyumba ya Bwana, Wakaldayo walivivunja vipande vipande, wakaichukua shaba yake yote mpaka Babeli.
18 Nayo masufuria, na majembe, na makasi, na mabakuli, na miiko, na vyombo vyote vya shaba walivyokuwa wakivitumia, wakavichukua vyote.
19 Navyo vikombe, na vyombo vya kutolea majivu, na mabakuli, na masufuria, na vinara, na miiko, na vyetezo, vilivyokuwa vya dhahabu katika dhahabu, na vilivyokuwa vya fedha katika fedha, amiri wa askari walinzi akavichukua.
20 Nguzo mbili, bahari moja, na ng'ombe kumi na mbili za shaba zilizokuwa chini ya matako yake, ambavyo mfalme Sulemani aliifanyia nyumba ya Bwana; shaba ya vitu hivyo vyote ilikuwa haiwezi kupimwa kwa kuwa nyingi sana.
21 Na nguzo hizo, urefu wa nguzo moja ulikuwa dhiraa kumi na nane, na uzi wa dhiraa kumi na mbili ungeweza kuizunguka; na unene wake ulikuwa nyanda nne; nayo ilikuwa ya uvungu.
22 Nayo ilikuwa na kichwa cha shaba juu yake; na urefu wa kichwa kimoja ulikuwa dhiraa tano; palikuwa na mapambo ya wavu na makomamanga juu ya kichwa hicho pande zote; vyote vilikuwa vya shaba; nayo nguzo ya pili ilikuwa na mapambo kama hayo, na makomamanga.
23 Palikuwa na makomamanga tisini na sita katika pande zake; makomamanga; yote yalikuwa mia juu ya wavu huo pande zote.
24 Naye amiri wa askari walinzi akamtwaa Seraya, kuhani mkuu, na Sefania, kuhani wa pili, na wale walinzi watatu wa mlango;
25 na katika mji akatwaa towashi mmoja aliyewasimamia watu wa vita; na watu saba katika wale waliouona uso wa mfalme, walioonekana katika mji; na karani wa jemadari wa jeshi, aliyewaandika watu wa nchi; na watu sitini katika watu wa nchi, walioonekana ndani ya mji.
26 Na Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawatwaa, akawaleta kwa mfalme wa Babeli huko Ribla.
27 Naye mfalme wa Babeli akawapiga na kuwaua huko Ribla katika nchi ya Hamathi. Ndivyo Yuda alivyochukuliwa utumwani, akatolewa katika nchi yake.
28 Watu hawa ndio wale ambao Nebukadreza aliwachukua mateka; katika mwaka wa saba, Wayahudi elfu tatu na ishirini na watatu;
29 katika mwaka wa kumi na nane wa Nebukadreza aliwachukua toka Yerusalemu watu mia nane na thelathini na wawili;
30 katika mwaka wa ishirini na tatu wa Nebukadreza, Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawachukua mateka katika Wayahudi watu mia saba na arobaini na watano; jumla ya watu hao wote ni watu elfu nne na mia sita.
31 Hata ikawa, katika mwaka wa thelathini na saba wa kuhamishwa kwake Yehoyakini, mfalme wa Yuda, katika mwezi wa kumi na mbili, siku ya ishirini na tano ya mwezi, Evil-merodaki, mfalme wa Babeli, katika mwaka wa kwanza wa kumiliki kwake, akamwinua kichwa chake Yehoyakini, mfalme wa Yuda, akamtoa gerezani.
32 Akasema naye maneno mazuri, akaweka kiti chake juu ya viti vya wafalme waliokuwa pamoja naye huko Babeli.
33 Naye akabadili mavazi yake ya gerezani, akala chakula mbele yake daima, siku zote za maisha yake.
34 Na kwa posho yake, alipewa posho ya daima na mfalme wa Babeli; kila siku alipewa posho hata siku ya kufa kwake, siku zote za maisha yake.