Esta

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10

Esta 1


1 Zamani za Ahasuero; naye huyu Ahasuero alimiliki toka Bara Hindi mpaka Kushi, juu ya majimbo mia na ishirini na saba;
2 siku zile mfalme Ahasuero alipoketi katika kiti cha enzi cha ufalme wake, huko Shushani ngomeni;
3 mwaka wa tatu wa kumiliki kwake, ikawa aliwafanyia karamu maakida wake wote na majumbe wake; wakuu wa Uajemi na Umedi, watu wenye cheo na maakida wa majimbo, wakihudhuria mbele zake.
4 Akawaonyesha utajiri wa ufalme wake mtukufu, na heshima ya enzi yake bora siku nyingi, maana siku mia na themanini.
5 Hata siku hizo zilipotimia, mfalme akawafanyia karamu watu wote waliokuwapo huko Shushani ngomeni, wakubwa kwa wadogo, muda wa siku saba, katika behewa la bustani ya ngome ya mfalme.
6 Palikuwa na mapazia ya bafta, nyeupe na samawi, yamefungiwa kamba za kitani safi za rangi ya zambarau kwa pete za fedha na nguzo za marumaru; pia na vitanda vilikuwa vya dhahabu na fedha juu ya sakafu ya marumaru, mawe mekundu, na meupe, na ya manjano, na meusi.
7 Wakawanywesha kileo katika vyombo vya dhahabu, na vile vyombo vilikuwa mbalimbali, na divai tele ya namna ya kifalme, sawasawa na ukarimu wa mfalme;
8 kunywa kulikuwa kama ilivyoamriwa, bila sharti; maana ndivyo mfalme alivyowaagiza watumishi-wa-nyumbani, kila mtu afanye apendavyo.
9 Tena Vashti, malkia, naye akawafanyia karamu wanawake ndani ya nyumba ya kifalme ya mfalme Ahasuero.
10 Hata siku ya saba, mfalme alipofurahiwa moyo wake kwa divai, aliwaamuru Mehumani, Biztha, Harbona, Bigtha, Abagtha, Zethari, na Karkasi, wale wasimamizi-wa-nyumba saba waliohudumu mbele za mfalme Ahasuero,
11 wamlete Vashti, malkia, mbele ya mfalme, amevaa taji ya kifalme; ili kuwaonyesha watu na maakida uzuri wake, maana alikuwa mzuri wa uso.
12 Bali Vashti, malkia, alikataa kuja kwa amri ya mfalme kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba; kwa hiyo mfalme akaghadhibika sana, na hasira yake ikawaka ndani yake.
13 Basi mfalme akawaambia wenye hekima, walio na elimu ya nyakati; maana ndivyo ilivyokuwa desturi ya mfalme kwa wote waliojua sheria na hukumu;
14 na karibu naye wameketi Karshena, Shethari, Admatha, Tarshishi, Meresi, Marsena, na Memukani, wale maakida saba wa Uajemi na Umedi, waliouona uso wa mfalme, na kuketi wa kwanza katika ufalme; akawauliza,
15 Tumfanyieje Vashti, malkia, kwa sheria, kwa sababu hakufanya kama vile alivyoamriwa na mfalme Ahasuero kwa mkono wa wasimamizi-wa-nyumba?
16 Basi Memukani akajibu mbele ya mfalme na maakida, Huyu Vashti, malkia, hakumkosa mfalme tu peke yake, ila na maakida wote, na watu wote pia walioko katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero.
17 Kwa maana tendo hilo la malkia litajulikana na wanawake wote, hata waume zao watadharauliwa machoni pao, itakaponenwa ya kuwa mfalme Ahasuero aliamuru Vashti, malkia, aletwe mbele yake, bali hakuja.
18 Hata na leo hivi mabibi wastahiki wa Uajemi na Umedi waliokwisha kuzisikia habari za tendo lake malkia watawaambia vivi hivi maakida wote wa mfalme. Hivyo kutatokea dharau nyingi na ghadhabu tele.
19 Basi mfalme akiona vema, na itoke kwake amri ya kifalme, nayo iandikwe katika sheria za Waajemi na Wamedi isitanguke, ya kwamba Vashti asifike tena mbele ya mfalme Ahasuero; na umalkia wake mfalme ampe mwingine aliye mwema kuliko yeye.
20 Basi mbiu ya mfalme atakayoipiga itakapotangazwa katika ufalme wake wote, nao ni mkubwa, wake wote watawaheshimu waume zao, wakubwa kwa wadogo.
21 Basi neno hili likawapendeza mfalme na maakida; naye mfalme akafanya sawasawa na neno lake Memukani.
22 Kwa maana alipeleka nyaraka katika majimbo yote ya mfalme, kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake, ya kwamba kila mwanamume atawale nyumbani mwake, na kuitangaza habari hii kwa lugha ya watu wake.

Esta 2


1 Baada ya hayo, hasira yake mfalme Ahasuero ilipotulia, alimkumbuka Vashti, na vile alivyotenda, na yale yaliyoamriwa juu yake.
2 Basi watumishi wa mfalme waliomhudumu walimwambia, Mfalme na atafutiwe mabikira vijana wazuri;
3 naye mfalme aweke wasimamizi katika majimbo yote ya ufalme wake, ili wakusanye pamoja mabikira vijana wazuri wote waende Shushani ngomeni, kwenye nyumba ya wanawake mikononi mwa Hegai, msimamizi-wa-nyumba wa mfalme, mwenye kuwalinda wanawake; tena wapewe vifaa vya utakaso.
4 Naye yule msichana atakayempendeza mfalme na awe malkia badala ya Vashti. Neno hilo likampendeza mfalme, naye akafanya hivyo.
5 Basi palikuwa na Myahudi mmoja huko Shushani ngomeni; jina lake Mordekai, bin Yairi, bin Shimei, bin Kishi, wa kabila ya Benyamini;
6 ambaye kwamba amechukuliwa mateka kutoka Yerusalemu miongoni mwa wafungwa waliochukuliwa pamoja na Yekonia, mfalme wa Yuda; ambaye Nebukadreza, mfalme wa Babeli,alimchukua.
7 Naye alikuwa amemlea Hadasa, yaani, Esta, binti wa mjomba wake, kwa kuwa hana baba wala mama. Naye msichana huyu alikuwa wa umbo mzuri na uso mwema; nao walipokufa baba yake na mama yake, yule Mordekai alimtwaa kuwa binti yake yeye.
8 Basi ikawa, wakati iliposikiwa amri ya mfalme na mbiu yake, wasichana wengi wakakusanyika huko Shushani ngomeni mikononi mwa Hegai; Esta naye aliingizwa katika nyumba ya mfalme, mikononi mwa Hegai mwenye kuwalinda wanawake.
9 Yule mwanamwali akampendeza, akapokea fadhili kwake; naye akampa upesi vifaa vya utakaso, pamoja na posho zake, na vijakazi saba walio haki yake, wa nyumbani mwa mfalme. Pia akamhamisha yeye na vijakazi wake akawaweka mahali pazuri katika nyumba ya wanawake.
10 Walakini Esta hakudhihirisha kabila yake wala jamaa yake, kwa maana ndivyo alivyomwagiza Mordekai asiwadhihirishe.
11 Na yule Mordekai akawa akitembea kila siku mbele ya ua wa nyumba ya wanawake, ili ajue hali yake Esta, na hayo yatakayompata.
12 Basi ilipowadia zamu yake mwanamwali mmojawapo aingie kwa mfalme Ahasuero, hali akiisha kufanyiwa sawasawa na sheria ya wanawake miezi kumi na miwili; yaani, ndivyo zilivyotimia siku zao za utakaso, miezi sita kwa mafuta ya manemane, na miezi sita kwa manukato na vifaa vya utakaso wa wanawake;
13 mwanamwali huingia hivyo kwa mfalme; kila akitakacho hupewa kwenda nacho kutoka katika nyumba ya wanawake ili kuingia katika nyumba ya mfalme.
14 Huenda jioni, na asubuhi hurudi nyumba ya pili ya wanawake, mikononi mwa Shaashgazi, msimamizi wake mfalme, mwenye kuwalinda masuria. Wala haingii tena kwa mfalme, isipokuwa amempendeza mfalme, naye akaitwa kwa jina.
15 Hata ilipowadia zamu yake Esta, binti Abihaili, mjomba wake Mordekai, ambaye alimtwaa kuwa binti yake, ili aingie kwa mfalme, yeye hakutaka kitu, ila vile vilivyoagizwa na Hegai, msimamizi wake mfalme, mwenye kuwalinda wanawake. Naye huyu Esta alikuwa amepata kibali machoni pa wote waliomwona.
16 Basi Esta alipelekwa kwa mfalme Ahasuero, katika nyumba ya kifalme, mwezi wa kumi, ndio mwezi wa Tebethi, mwaka wa saba wa kumiliki kwake.
17 Mfalme akampenda Esta kuliko wanawake wote, naye akapata neema na kibali machoni pake kuliko mabikira wote; basi akamtia taji ya kifalme kichwani pake, akamfanya awe malkia badala ya Vashti.
18 Ndipo mfalme alipowafanyia karamu kubwa maakida wake wote na watumishi wake, yaani, karamu yake Esta; akafanya msamaha katika majimbo yote, akatoa zawadi sawasawa na ukarimu wa mfalme.
19 Basi mabikira walipokusanyika mara ya pili, Mordekai alikuwa akiketi mlangoni pa mfalme.
20 Esta alikuwa hajadhihirisha jamaa yake wala kabila yake, kama vile Mordekai alivyomwagiza; kwa maana Esta alikuwa akiyashika maagizo ya Mordekai, vile vile kama wakati alipolelewa naye.
21 Ikawa siku zile, Mordekai alipokuwa akiketi mlangoni pa mfalme, wawili katika wasimamizi wake mfalme, Bigthana na Tereshi, wangoje mlango, walighadhibika, wakataka kumpelekea mikono mfalme Ahasuero.
22 Basi Mordekai akapata kulijua jambo hilo, naye akamjulisha Esta, malkia; naye Esta akamwambia mfalme habari hiyo kwa jina la Mordekai.
23 Na jambo hilo lilipochunguzwa, na hakika ikapatikana, hao wote wawili wakatundikwa juu ya mti. Hayo pia yakaandikwa katika kitabu cha taarifa mbele ya mfalme.

Esta 3


1 Baada ya hayo mfalme Ahasuero alimwongezea cheo Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, akampandisha, akamwekea kiti chake juu ya maakida wote waliokuwapo pamoja naye.
2 Nao watumishi wote wa mfalme, walioketi mlangoni pa mfalme, wakainama na kumsujudia Hamani, maana ndivyo alivyoamuru mfalme kwa habari zake. Bali Mordekai hakuinama, wala kumsujudia.
3 Basi watumishi wa mfalme walioketi mlangoni pa mfalme wakamwambia Mordekai, Mbona wewe waihalifu amri ya mfalme?
4 Ikawa, waliposema naye kila siku asiwasikilize, wakamwarifu Hamani, ili kuona kama mambo yake Mordekai yatasimama; maana alikuwa amewaambia ya kuwa yeye ni Myahudi.
5 Hata Hamani alipoona ya kwamba Mordekai hainami wala kumsujudia, alighadhibika sana.
6 Akaona si shani kumtia mikono Mordekai peke yake; maana wamemjulisha kabila yake Mordekai; kwa hiyo Hamani alitaka kuwaangamiza Wayahudi wote waliokuwa wakikaa katika ufalme wote mzima wa Ahasuero, yaani, watu wake Mordekai.
7 Basi mwezi wa kwanza, ndio mwezi wa Nisani, mwaka wa kumi na mbili wa mfalme Ahasuero, wakapiga Puri, yaani kura, mbele yake Hamani; siku kwa siku, na mwezi kwa mwezi, hata mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari.
8 Basi Hamani akamwambia mfalme Ahasuero, Kuna taifa moja waliotawanyika na kukaa mahali mahali katikati ya mataifa walioko katika majimbo yote ya ufalme wako. Nao sheria zao zimefarakana na sheria za kila taifa; wala hawazishiki amri za mfalme; kwa hiyo haimpasi mfalme kuchukuliana nao.
9 Basi, mfalme akiona vema, na iandikwe kwamba waangamizwe; nami nitalipa talanta kumi elfu za fedha mikononi mwao watakaosimamia shughuli hiyo, waziweke katika hazina ya mfalme.
10 Ndipo mfalme alipoivua pete yake mkononi, akampa Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi.
11 Kisha mfalme akamwambia Hamani, Hiyo fedha umepewa, na watu pia, fanya uonavyo vema.
12 Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kwanza; na barua zikaandikwa, kama vile Hamani alivyoagiza vyote, kwa maakida wa mfalme, na maliwali waliokuwa juu ya kila jimbo, na wakuu wa kila taifa; kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; zikaandikwa kwa jinsi la mfalme Ahasuero, na kutiwa muhuri kwa pete yake.
13 Barua zikapelekwa kwa mikono ya matarishi mpaka majimbo yote ya mfalme kuwaangamiza Wayahudi wote, na kuwaua, na kuwafisha, vijana kwa wazee, watoto wachanga na wanawake pia, siku moja, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili ndio mwezi wa Adari; na kuyachukua mali yao kuwa nyara.
14 Nakili ya andiko, ya kupigwa mbiu katika kila jimbo, ilitangazwa kwa mataifa yote wawe tayari siku ile ile.
15 Matarishi wakaondoka wakaenda haraka kwa amri ya mfalme; kukapigwa mbiu huko Shushani ngomeni. Mfalme na Hamani wakaketi ili kunywa divai; bali mji wa Shushani ukafadhaika.

Esta 4


1 Basi Mordeikai alipojua mambo yote yaliyofanyika, alizirarua nguo zake, akajivika gunia pamoja na majivu, akatoka hata kufika katikati ya mji, akalia kwa sauti kuu ya uchungu.
2 Pia akafika hata mbele ya mlango wa mfalme; maana hakuna awezaye kuingia ndani ya mlango wa mfalme hali amevaa magunia.
3 Na katika kila jimbo, ambako amri ya mfalme na mbiu yake imewasili, palikuwako msiba mkuu kwa Wayahudi, na kufunga, na kulia, na kuomboleza; hata na wengi wakalala juu ya gunia na majivu.
4 Basi wajakazi wake Esta, na wasimamizi wake wa nyumba, wakamjia, wakampasha habari; naye malkia akahuzunika mno; akampelekea Mordekai mavazi, ili kumvika, na kumwondolea gunia lake; walakini yeye asikubali.
5 Kisha Esta akamwita Hathaki, msimamizi-wa-nyumba mmojawapo wa mfalme, aliyemwagiza amhudumu Esta, akamtuma kwa Mordekai, ili ajue mambo hayo, na maana yake ni nini.
6 Basi yule Hathaki akatoka nje kumwendea Mordekai kwenye uwanda wa mji ulipo mbele ya mlango wa mfalme.
7 Naye Mordekai akamweleza yote yaliyompata, na hesabu ya fedha Hamani aliyoahidi kulipa katika hazina ya mfalme, ili Wayahudi waangamizwe.
8 Pia akampa na nakili ya andiko la mbiu ya kuwaangamiza, iliyotangazwa Shushani, ili amwonyeshe Esta, na kumweleza; tena amwagize aingie kwa mfalme, kumsihi na kuwaombea watu wake.
9 Basi Hathaki akaja, akamwambia Esta maneno ya Mordekai.
10 Ndipo Esta akasema na Hathaki, akamtuma tena kwa Mordekai, kusema,
11 Watumwa wote wa mfalme wanajua sana, hata na watu wa majimbo ya mfalme, ya kwamba mtu ye yote, akiwa mwanamume au mwanamke, atakayemjia mfalme katika ua wa ndani, wala hakuitwa, kuna sheria moja kwake, ni kwamba auawe; isipokuwa yeye ambaye mfalme atamnyoshea fimbo ya dhahabu, ili aishi; wala mimi sikuitwa niingie kwa mfalme yapata siku thelathini.
12 Basi wakamwambia Mordekai maneno ya Esta.
13 Naye Mordekai akawaagiza wampelekee Esta jibu la kusema, Wewe usijidhanie kuwa wewe utaokoka nyumbani mwa mfalme, zaidi ya Wayahudi wote.
14 Kwa maana wewe ukinyamaza kabisa wakati huu, ndipo kutakapowatokea Wayahudi msaada na wokovu kwa njia nyingine; ila wewe utaangamia pamoja na mlango wote wa baba yako; walakini ni nani ajuaye kama wewe hukuujia ufalme kwa ajili ya wakati kama huo?
15 Basi Esta akawatuma ili wamjibu Mordekai,
16 Uende ukawakusanye Wayahudi wote waliopo hapa Shushani, mkafunge kwa ajili yangu; msile wala kunywa muda wa siku tatu, usiku wala mchana, nami na wajakazi wangu tutafunga vile vile; kisha nitaingia kwa mfalme, kinyume cha sheria; nami nikiangamia, na niangamie.
17 Basi Mordekai akaenda zake, akafanya yote kama vile Esta alivyomwagiza.

Esta 5


1 Ikawa siku ya tatu Esta alijivika mavazi yake ya kifalme, akasimama katika ua wa ndani wa nyumba ya mfalme, kuielekea nyumba ya mfalme; naye mfalme akaketi juu ya kiti chake cha enzi katika nyumba ya mfalme, kuuelekea mlango wa nyumba.
2 Ikawa, mfalme alipomwona malkia Esta amesimama uani, yeye akapata kibali machoni pake; naye mfalme akamnyoshea Esta fimbo ya dhahabu aliyokuwa nayo mkononi. Basi Esta akakaribia, akaigusa ncha ya fimbo.
3 Mfalme akamwambia, Malkia Esta, wataka nini? Nayo ni haja gani uliyo nayo? Utapewa hata nusu ya ufalme.
4 Esta akasema, Mfalme akiona vema, na aje leo, mfalme na Hamani, kwenye karamu niliyomwandalia.
5 Basi mfalme akasema, Mhimize Hamani, ili ifanyike kama Esta alivyosema. Hivyo mfalme na Hamani wakafika katika karamu ile aliyoiandaa Esta.
6 Basi mfalme akamwambia Esta pale penye karamu ya divai, Dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utafanyiziwa.
7 Esta akajibu, na kusema, Dua yangu ni hii, na haja yangu ni hii,
8 Ikiwa nimepata kibali machoni pa mfalme, na mfalme akiona vema kunipa niombalo, na kunifanyizia haja yangu, na aje tena mfalme na Hamani kwenye karamu nitakayowaandalia, nami kesho nitafanya kama vile mfalme alivyosema.
9 Basi Hamani alitoka siku ile kwa furaha na ukunjufu wa moyo; lakini Hamani alipomwona Mordekai mlangoni pa mfalme, ya kwamba hasimami wala kutetemeka mbele yake, alijaa ghadhabu juu ya Mordekai.
10 Walakini Hamani akajizuia, akaenda zake nyumbani kwake; akatuma kuwaita rafiki zake na Zereshi mkewe.
11 Naye Hamani akawasimulia habari za fahari ya mali zake, na wingi wa watoto wake, nayo mambo yote pia ambayo mfalme amemfanikisha katika hayo, na jinsi alivyompandisha juu ya maakida na watumishi wa mfalme.
12 Zaidi ya hayo Hamani akasema, Naye malkia Esta hakumkaribisha mtu ye yote pamoja na mfalme katika karamu aliyoiandaa, ila mimi peke yangu; hata na kesho pia nimealikwa naye pamoja na mfalme.
13 Bali haya yote yanifaa nini, pindi nimwonapo yule Mordekai, Myahudi, ameketi mlangoni pa mfalme?
14 Basi Zereshi mkewe akamwambia, na rafiki zake wote, Na ufanyizwe mti wa mikono hamsini urefu wake, na kesho asubuhi useme na mfalme ili Mordekai atundikwe juu yake; ndipo utakapoingia kwa kicheko pamoja na mfalme karamuni. Basi neno likampendeza Hamani, akaufanyiza ule mti.

Esta 6


1 Usiku ule mfalme hakupata usingizi; akaamuru aletewe kitabu cha maandiko ya taarifa, nayo yakasomwa mbele ya mfalme.
2 Ikaonekana kuwa imeandikwa ya kwamba Mordekai aliwachongea Bigthana na Tereshi, wasimamizi wawili wa mfalme, katika hao waliolinda mlango, waliotaka kumtia mikono mfalme Ahasuero.
3 Mfalme akasema, Je! Ni heshima gani au jaha gani Mordekai aliyofanyiziwa kwa ajili ya hayo? Watumwa wa mfalme waliomhudumu wakamwambia, Hakuna alilofanyiziwa.
4 Mfalme akasema, Yupo nani behewani? Ikawa Hamani alikuwa ameingia katika ua wa nje wa nyumba ya mfalme, aseme na mfalme, ili kumtundika Mordekai juu ya mti ule aliomwekea tayari.
5 Basi watumwa wa mfalme wakamwambia, Tazama, Hamani yupo, amesimama behewani. Mfalme akasema, Na aingie.
6 Basi Hamani akaingia. Mfalme akamwambia, Afanyiziwe nini yule ambaye mfalme apenda kumheshimu? Hamani akasema moyoni mwake, Ni nani ambaye mfalme apenda kumheshimu kuliko mimi?
7 Basi Hamani akamwambia mfalme, Yule ambaye mfalme apenda kumheshimu,
8 na aletewe mavazi ya kifalme ambayo mfalme amezoea kuyavaa, na farasi ambaye mfalme humpanda mwenyewe, ambaye ametiwa taji ya kifalme kichwani;
9 na yale mavazi na yule farasi akabidhiwe mkononi mmojawapo wa maakida wa mfalme aliye mstahiki; ili makusudi amvike yule ambaye mfalme apenda kumheshimu, na kumrakibisha juu ya farasi kuipitia njia kuu ya mjini, na kupiga mbiu mbele yake, kusema, Hivyo ndivyo atakavyofanyiziwa mtu yule ambaye mfalme apenda kumheshimu.
10 Basi mfalme akamwambia Hamani, Hima! Twaa mavazi na farasi kama ulivyosema, ukamfanyizie vivyo hivyo Mordekai, Myahudi, aketiye mlangoni pa mfalme; lisipungue neno lo lote katika yote uliyoyasema.
11 Ndipo Hamani alipoyatwaa mavazi na farasi, akamvika Mordekai yale mavazi, akamrakibisha juu ya farasi kuipitia njia kuu ya mjini, akapiga mbiu mbele yake, Hivyo ndivyo atakavyofanyiziwa mtu yule ambaye mfalme apenda kumheshimu.
12 Kisha Mordekai akarudi kwenye mlango wa mfalme. Bali Hamani akaenda mbio nyumbani kwake, mwenye msiba, na kichwa chake kimefunikwa.
13 Basi Hamani akawasimulia Zereshi mkewe na rafiki zake wote kila neno lililompata. Kisha watu wake wenye hekima na Zereshi mkewe wakamwambia, Ikiwa huyu Mordekai, ambaye umeanza kuanguka mbele yake, ni wa uzao wa Wayahudi, wewe hutamweza, bali kuanguka utaanguka mbele yake.
14 Hata walipokuwa katika kusema naye, wasimamizi-wa-nyumba wa mfalme walifika, wakahimiza kumleta Hamani katika karamu ile aliyoiandaa Esta.

Esta 7


1 Basi mfalme na Hamani walikuja kula karamu pamoja na malkia Esta.
2 Mfalme akamwambia Esta tena siku ya pili pale pale penye karamu ya divai, Malkia Esta, dua yako ni nini? Nawe utapewa; na haja yako ni nini? Hata nusu ya ufalme utafanyiziwa.
3 Ndipo malkia Esta alipojibu, akasema, Mfalme, ikiwa nimepata kibali machoni pako, na mfalme akiona vema, nipewe maisha yangu kuwa dua yangu, na watu wangu kuwa haja yangu.
4 Maana tumeuzwa, mimi na watu wangu, ili tuharibiwe, na kuuawa, na kuangamia. Kama tungaliuzwa kuwa watumwa na wajakazi, ningalinyamaza; ila hata hivyo msiba wetu haulinganishwi na hasara ya mfalme.
5 Ndipo mfalme Ahasuero aliponena, akamwambia malkia Esta, Ni nani huyu, tena yuko wapi, ambaye moyoni mwake alithubutu kufanya hivi?
6 Esta akasema, Ni mtesi, tena ni adui, ndiye huyu Hamani, mtu mbaya kabisa. Mara Hamani akaingiwa na hofu mbele ya mfalme na malkia.
7 Mfalme akaondoka katika ghadhabu yake kutoka kwenye karamu ya divai, akaingia bustani ya ngome. Hamani naye akasimama ili ajitakie maisha yake kwa malkia Esta; kwa kuwa aliona ya kwamba amekusudiwa madhara na mfalme.
8 Kisha mfalme akarudi kutoka katika bustani ya ngome hata mahali pa karamu ya divai. Ikawa Hamani amejitupa chini penye kitanda alipokuwapo Esta. Mfalme akasema, Namna gani! Je! Atamfanyia malkia jeuri hata machoni pangu nyumbani mwangu? Na neno lilipotoka kinywani mwa mfalme, wakamfunika uso Hamani.
9 Ndipo aliposema Harbona, msimamizi-wa-nyumba mmojawapo wa wale waliohudhuria mbele ya mfalme, Tazama, basi, mti wa mikono hamsini urefu wake, Hamani aliomwekea tayari Mordekai, ambaye alinena vema kwa ajili ya mfalme, upo umesimamishwa nyumbani kwa Hamani. Mfalme akasema, Mtundikeni juu yake.
10 Basi wakamtundika Hamani juu ya mti aliomwekea tayari Mordekai. Ghadhabu ya mfalme ikatulia.

Esta 8


1 Siku ile mfalme Ahasuero alimpa malkia Esta nyumba yake Hamani, yule adui ya Wayahudi. Mordekai naye akahudhuria mbele ya mfalme; kwa maana Esta alikuwa amedhihirisha alivyomhusu.
2 Basi mfalme akaivua pete yake, aliyompokonya Hamani, akampa Mordekai. Naye Esta akamweka Mordekai kuwa juu ya mlango wake Hamani.
3 Tena Esta akasema na mfalme mara ya pili, akaanguka miguuni pake, akamsihi kwa machozi ayaondoe madhara ya Hamani, Mwagagi, na shauri alilowafanyia Wayahudi.
4 Ndipo mfalme alipomnyoshea Esta fimbo yake ya dhahabu. Basi Esta akaondoka, akasimama mbele ya mfalme.
5 Akasema, Mfalme akiona vema, nami nikiwa nimepata kibali machoni pake, na neno likionekana jema mbele ya mfalme, nami nikimpendeza machoni pake, iandikwe kuzitangua barua za Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, alizotunga na kuziandika ili kuwaangamiza Wayahudi walioko katika majimbo yote ya mfalme.
6 Kwa maana niwezeje kuyaona mabaya yatakayowajia watu wangu? Au niwezeje kuyatazama maangamizo ya jamaa zangu?
7 Mfalme Ahasuero akawaambia malkia Esta na Mordekai, Myahudi, kusema, Tazama, nimekwisha kumpa Esta nyumba yake Hamani, naye mwenyewe wamekwisha kumtundika juu ya mti, kwa sababu aliwatia mikono Wayahudi.
8 Basi waandikieni Wayahudi pia vyo vyote mpendavyo, kwa jina la mfalme, mkatie muhuri kwa pete ya mfalme; kwa kuwa andiko lililoandikwa kwa jina la mfalme na kutiwa muhuri kwa pete ya mfalme hakuna awezaye kulitangua.
9 Basi, waandishi wa mfalme wakaitwa pale pale, siku ya ishirini na tatu ya mwezi wa tatu, ndio mwezi wa Siwani; na kama vile Mordekai alivyoamuru, Wayahudi wakaandikiwa, pamoja na maakida na maliwali, na wakuu wa majimbo toka Bara Hindi mpaka Kushi, majimbo mia na ishirini na saba, kila jimbo kwa mwandiko wake, na kila taifa kwa lugha yake; na Wayahudi kwa mwandiko wao na kwa lugha yao.
10 Akaandika kwa jina la mfalme Ahasuero, na kutia muhuri kwa pete ya mfalme, akazipeleka barua kwa matarishi, wamepanda farasi, wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, ndio waliozalishwa katika zizi la mfalme.
11 Katika barua hizo mfalme aliwaruhusu Wayahudi wakusanyike katika kila mji na kuzisimamia maisha zao, kuangamiza, na kuua, na kulifisha jeshi lote la watu na la jimbo watakaowaondokea, wao na wadogo wao na wanawake; na kuyachukua mali yao kuwa nyara;
12 siku moja, katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero, yaani, siku ya kumi na tatu ya mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari.
13 Nakili ya andiko, ya kupigwa mbiu katika kila jimbo, ilitangazwa kwa mataifa yote, na kwa Wayahudi, wawe tayari siku ile ile kujilipiza kisasi juu ya adui zao.
14 Matarishi wakaondoka, wamepanda wanyama wepesi sana waliotumika kwa huduma ya mfalme, huku wakihimizwa na kusukumizwa kwa amri ya mfalme; kukapigwa mbiu huko Shushani ngomeni.
15 Naye Mordekai akatoka usoni pa mfalme, amevaa mavazi ya kifalme, ya rangi ya samawi na nyeupe, mwenye taji kubwa ya dhahabu, na joho ya kitani safi na rangi ya zambarau. Mji wa Shushani wakapaza sauti, wakashangilia.
16 Ikawa nuru na furaha na shangwe na heshima kwa Wayahudi.
17 Na katika kila jimbo, na kila mji, po pote palipowasili amri ya mfalme na mbiu yake, Wayahudi wakapata furaha na shangwe, karamu na sikukuu. Hata wengi wa watu wa nchi wakajifanya Wayahudi, kwa kuwa hofu ya Wayahudi imewaangukia.

Esta 9


1 Hata ulipofika mwezi wa kumi na mbili, ndio mwezi wa Adari, siku yake ya kumi na tatu, amri ya mfalme na mbiu yake ilipowadia kutekelezwa; ambayo siku ile adui za Wayahudi walitumaini kuwatawala, bali kumebadilika kinyume, hata Wayahudi waliwatawala wale waliowachukia;
2 siku ile ile Wayahudi wakakusanyika mijini mwao katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero ili kuwatia mikono wale watu waliowatakia hasara; wala asiweze mtu kuwazuia, kwa kuwa hofu yao imewaangukia watu wote.
3 Nao maakida wa majimbo, na majumbe, na maliwali, na wale waliofanya shughuli ya mfalme, waliwasaidia Wayahudi; kwa sababu hofu ya Mordekai imewaangukia.
4 Maana Mordekai alikuwa mkuu nyumbani mwa mfalme, na sifa yake imevuma katika majimbo yote, kwa kuwa huyo Mordekai amezidi kukuzwa.
5 Basi Wayahudi wakawapiga adui zao wote mapigo ya upanga, na machinjo, na maangamizo, wakawatenda kama wapendavyo wale waliowachukia.
6 Hata huko Shushani ngomeni Wayahudi wakawaua watu mia tano, na kuwaangamiza.
7 Wakawaua na Parshandatha, na Dalfoni, na Aspatha,
8 na Poratha, na Adalia, na Aridatha,
9 na Parmashta, na Arisai, na Aridai, na Waizatha,
10 wana kumi wa Hamani bin Hamedatha, adui ya Wayahudi; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono.
11 Siku ile mfalme akaletewa hesabu ya hao waliouawa huko Shushani ngomeni.
12 Mfalme akamwambia malkia Esta, Wayahudi wamewaua watu mia tano hapa Shushani ngomeni na kuwaangamiza, pamoja na wana kumi wa Hamani, je! Wamefanyaje basi katika majimbo ya mfalme yaliyosalia! Basi, una nini uombalo? Nawe utapewa; ama unayo haja gani tena? Nayo itatimizwa.
13 Ndipo Esta aliposema, Mfalme akiona vema, Wayahudi walioko Shushani na wapewe ruhusa kufanya tena kesho sawasawa na mbiu ya leo, na hao wana kumi wa Hamani watundikwe juu ya mti ule.
14 Mfalme akaamuru vifanyike vivyo hivyo, mbiu ikapigwa huko Shushani, wakawatundika wale wana kumi wa Hamani.
15 Basi Wayahudi wa Shushani wakakusanyika tena siku ya kumi na nne pia ya mwezi wa Adari, wakawaua watu mia tatu huko Shushani; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono.
16 Nao Wayahudi wengine waliokaa katika majimbo ya mfalme walikusanyika, wakazishindania maisha zao, wakajipatia raha mbele ya adui zao, wakawaua waliowachukia, watu sabini na tano elfu; walakini juu ya nyara hawakuweka mikono.
17 Hii ndiyo siku ya kumi na tatu ya mwezi wa Adari; na siku ya kumi na nne ya mwezi huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha.
18 Lakini Wayahudi wa Shushani walikusanyika siku ya kumi na tatu ya mwezi huo, na siku ya kumi na nne pia; na siku ya kumi na tano ya mwezi uo huo wakapumzika, wakaifanya kuwa siku ya karamu na furaha.
19 Kwa sababu hii Wayahudi wa vijijini, wakaao katika miji isiyo na boma, huishika siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, kuwa siku ya furaha na karamu, sikukuu ya kupelekeana zawadi.
20 Basi Mordekai aliyaandika mambo hayo; naye akapeleka barua kwa Wayahudi wote waliokaa katika majimbo yote ya mfalme Ahasuero, waliokuwa karibu na waliokuwa mbali,
21 kuwaonya wazishike siku ya kumi na nne ya mwezi wa Adari, na siku ya kumi na tano yake, mwaka kwa mwaka,
22 ambazo ni siku Wayahudi walipojipatia raha mbele ya adui zao, na mwezi uliogeuzwa kwao kuwa furaha badala ya huzuni, na kuwa sikukuu badala ya kilio; wazifanye siku hizo ziwe za karamu na furaha, za kupeana zawadi na za kuwapa maskini vipawa.
23 Nao Wayahudi wakakubali kufanya kama walivyoanza, na kama Mordekai alivyowaandikia;
24 kwa sababu Hamani bin Hamedatha, Mwagagi, adui ya Wayahudi wote, alikuwa amefanya shauri juu ya Wayahudi ili kuwaangamiza, akapiga Puri, yaani kura, ili kuwakomesha na kuwaangamiza pia;
25 bali mfalme alipoarifiwa, aliamuru kwa barua ya kwamba hilo shauri baya alilolifanya juu ya Wayahudi limrudie kichwani pake mwenyewe; na ya kwamba yeye na wanawe watundikwe juu ya mti.
26 Hivyo wakaziita siku hizo Purimu, kwa jina la Puri. Basi, kwa ajili ya maneno yote ya barua hiyo, na kwa yale waliyoyaona wenyewe juu ya jambo hilo, na mambo yenyewe yaliyowajia,
27 Wayahudi wakaagiza na kutadariki juu yao wenyewe, na juu ya wazao wao, na juu ya wote watakaojiunga nao, isikome, ya kwamba watazishika siku hizo mbili sawasawa na andiko lile, na kwa majira yake kila mwaka;
28 siku hizo zikumbukwe na kushikwa kwa vizazi vyote na kila jamaa, katika kila jimbo na kila mji; wala siku hizo za Purimu zisikome katikati ya Wayahudi, wala kumbukumbu lake lisiishe kwa wazao wao.
29 Ndipo malkia Esta, binti Abihaili, pamoja na Mordekai Myahudi, alipoandika kwa mamlaka yote kuithibitisha barua hii ya pili ya Purimu.
30 Akapeleka barua kwa Wayahudi wote katika majimbo yote mia na ishirini na saba ya ufalme wake Ahasuero, maneno ya amani na kweli,
31 ili kuzithibitisha siku hizo za Purimu kwa majira yake, kama Mordekai Myahudi na malkia Esta walivyoamuru, na kama walivyojiagizia juu yao wenyewe, na juu ya wazao wao, kwa habari ya kufunga na kilio.
32 Amri yake Esta ikayathibitisha mambo hayo ya Purimu; ikaandikwa katika kitabu.

Esta 10


1 Basi mfalme Ahasuero alitoza kodi katika nchi na katika visiwa vya bahari.
2 Na matendo yake yote yenye nguvu na ya ushujaa, na habari zote za ukuu wake Mordekai ambao alipewa na mfalme, hazikuandikwa katika kitabu-cha-taarifa cha wafalme wa Umedi na Uajemi?
3 Kwa maana Mordekai Myahudi akawa wa pili wake mfalme Ahasuero, na mkuu wa Wayahudi, amependeza mbele ya jamii ya ndugu zake; ambaye aliwatafuta watu wake wema, na kuiangalia hali njema ya wazao wao wote.