Nehemia

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13

Nehemia 1


1 Habari za Nehemia, mwana wa Hakalia. Ikawa katika mwezi wa Kisleu, mwaka wa ishirini, nilipokuwapo Shushani ngomeni,
2 Hanani, mmoja wa ndugu zangu, akanijia, yeye na watu wengine waliotoka Yuda; nami nikawauliza habari za Wayahudi waliopona, hao watu wa uhamisho waliosalia; na habari za Yerusalemu.
3 Wakaniambia, Watu wa uhamisho, waliosalia huko katika wilaya ile, wamo katika hali ya dhiki nyingi na mashutumu; tena ukuta wa Yerusalemu umebomolewa, na malango yake yameteketezwa kwa moto.
4 Hata ikawa niliposikia maneno hayo, nikaketi, nikalia, nikaomboleza siku kadha wa kadha; kisha nikafunga, nikaomba mbele za Mungu wa mbinguni;
5 nikasema, Nakusihi, Ee Bwana, Mungu wa mbinguni, Mungu mkuu, mwenye kuogofya, mwenye kutimiza agano lake na rehema zake kwa hao wampendao na kuzishika amri zake;
6 tega sikio lako, macho yako yakafumbuke, upate kuyasikiliza maombi ya mtumishi wako, ninayoomba mbele zako wakati huu, mchana na usiku, kwa ajili ya wana wa Israeli, watumishi wako; hapo ninapoziungama dhambi za wana wa Israeli, tulizozifanya juu yako; naam, mimi na nyumba ya baba yangu tumefanya dhambi.
7 Tumetenda maovu mengi juu yako, wala hatukuzishika amri, wala sheria, wala hukumu, ulizomwamuru Musa, mtumishi wako.
8 Nakuomba, likumbuke neno lile ulilomwamuru Musa, mtumishi wako, ukisema, Mkikosa, nitawatawanya kati ya mataifa;
9 bali mkinirudia mimi, na kuzishika amri zangu na kuzitenda, watu wako waliofukuzwa wajapokuwa katika pande za mwisho za mbingu, hata hivyo nitawakusanya kutoka huko, na kuwaleta mpaka mahali pale nilipopachagua ili kuliweka jina langu hapo.
10 Basi watu hao ni watumishi wako na watu wako, uliowakomboa kwa uweza wako mwingi, na kwa mkono wako hodari.
11 Ee Bwana, nakusihi, litege sikio lako, uyasikilize maombi ya mtumishi wako, na maombi ya watumishi wako, wanaofurahi kulicha jina lako; nakuomba sana; unifanikishe mimi, mtumishi wako, leo, ukanijalie rehema mbele ya mtu huyu. (Maana, nalikuwa mnyweshaji wa mfalme).

Nehemia 2


1 Ikawa katika mwezi wa Nisani, mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta, na divai imewekwa mbele yake, nikaishika ile divai, nikampa mfalme. Nami mpaka sasa sikuwa na huzuni mbele ya mfalme wakati wo wote.
2 Basi mfalme akaniambia, Mbona umesikitika uso wako, nawe huna ugonjwa? Nini hii, isipokuwa ni huzuni ya moyo? Ndipo nikaogopa sana.
3 Nikamwambia mfalme, Mfalme na aishi milele; kwani uso wangu usiwe na huzuni, iwapo mji, ulio mahali pa makaburi ya baba zangu, unakaa ukiwa, na malango yake yameteketezwa kwa moto?
4 Ndipo mfalme akaniambia, Una haja gani unayotaka kuniomba? Basi nikamwomba Mungu wa mbinguni.
5 Nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na ikiwa mimi, mtumishi wako, nimepata kibali machoni pako, tafadhali unipeleke mpaka Yuda, niuendee mji wa makaburi ya baba zangu, nipate kuujenga.
6 Mfalme akaniuliza, (malkia naye ameketi karibu naye), Safari yako itakuwa ya siku ngapi? Nawe utarudi lini? Hivyo mfalme akaona vema kunipeleka; nami nikampa muda.
7 Tena nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na nipewe nyaraka kwa maliwali walio ng'ambo ya Mto, ili waniache kupita mpaka nifike Yuda;
8 nipewe na waraka kwa Asafu, mwenye kuutunza mwitu wa mfalme, ili anipe miti ya kufanyizia boriti kwa malango ya ngome ya nyumba, na kwa ukuta wa mji; na kwa nyumba ile nitakayoingia mimi. Naye mfalme akanipa, kama mkono mwema wa Mungu wangu ulivyokuwa juu yangu.
9 Ndipo nikafika kwa maliwali walio ng'ambo ya Mto, nikawapa hizo nyaraka za mfalme. Naye mfalme alikuwa amepeleka maakida wa jeshi lake na wapanda farasi pamoja nami.
10 Hata Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, mtumishi wake, Mwamoni, waliposikia habari hizi, ziliwahuzunisha sana, kwa kuwa amekuja mtu kuwatakia heri wana wa Israeli.
11 Basi nikafika Yerusalemu, nikakaa huko muda wa siku tatu.
12 Kisha nikaondoka usiku, mimi na watu wachache pamoja nami; wala sikumwambia mtu neno hili alilolitia Mungu wangu moyoni mwangu, nilitende kwa ajili ya Yerusalemu; wala hapakuwa na mnyama pamoja nami, ila mnyama yule niliyempanda mwenyewe.
13 Nikatoka nje usiku, kwa njia ya lango la bondeni, nikashika njia iendayo kisima cha joka, na lango la jaa; nikazitazama kuta za Yerusalemu, zilizokuwa zimebomoka; na malango yake yameteketezwa kwa moto.
14 Kisha nikaendelea mpaka lango la chemchemi, na ziwa la mfalme; lakini hapakuwa na nafasi ya kupita kwa yule mnyama aliyekuwa chini yangu.
15 Kisha nikapanda usiku kando ya kijito, nikautazama ukuta; kisha nikarudi nyuma, nikaingia kwa lango la bondeni, nikarejea hivyo.
16 Wala mashehe hawakujua nilikokwenda, wala nilivyotenda; wala sijawaambia Wayahudi, wala makuhani, wala wakuu, wala mashehe, wala watu wengine waliokuwa wakiifanya kazi hiyo.
17 Kisha nikawaambia, Mnaona hali hii dhaifu tuliyo nayo, jinsi Yerusalemu ulivyo hali ya ukiwa, na malango yake yalivyoteketezwa kwa moto; haya! Na tuujenge tena ukuta wa Yerusalemu, ili tusiwe shutumu tena.
18 Nikawaeleza habari ya mkono wa Mungu wangu ulivyokuwa mwema juu yangu; pia na maneno ya mfalme aliyoniambia. Nao wakasema, Haya! Na tuondoke tukajenge. Basi wakaitia mikono yao nguvu kwa kazi hiyo njema.
19 Lakini waliposikia Sanbalati, Mhoroni, na Tobia, mtumishi wake, Mwamoni, na Geshemu, Mwarabu, walitucheka, wakatudharau, wakasema, Ni nini neno hili mnalofanya? Je! Mtaasi ninyi juu ya mfalme?
20 Ndipo nikawajibu, nikawaambia, Mungu wa mbinguni, yeye atatufanikisha; kwa hiyo sisi, watumishi wake, tutaondoka na kujenga; lakini ninyi hamna sehemu, wala haki, wala kumbukumbu, katika Yerusalemu.

Nehemia 3


1 Ndipo akaondoka Eliashibu, kuhani mkuu, pamoja na nduguze makuhani, wakalijenga lango la kondoo; wakazitia boriti zake, wakaisimamisha milango yake; mpaka mnara wa Hamea wakalitakasa, mpaka mnara wa Hananeli.
2 Na baada yao wakajenga watu wa Yeriko. Na baada yao akajenga Zakuri, mwana wa Imri.
3 Na lango la samaki wakalijenga wana wa Senaa; wakazitia boriti zake, wakaisimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake.
4 Na baada yao akafanyiza Meremothi, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi. Na baada yao akafanyiza Meshulamu, mwana wa Berekia, mwana wa Meshezabeli. Na baada yao akafanyiza Sadoki, mwana wa Baana.
5 Na baada yao wakafanyiza Watekoi; lakini wakuu wao hawakutia shingo zao kazini mwa bwana wao.
6 Na lango la kale wakalifanyiza Yoyada, mwana wa Pasea, na Meshulamu, mwana wa Besodeya; wakazitia boriti zake, wakaisimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake.
7 Na baada yao wakafanyiza Melatia, Mgibeoni, na Yadoni, Mmeronothi, watu wa Gibeoni, na wa Mispa, raia wa kiti cha enzi cha liwali wa ng'ambo ya Mto.
8 Na baada yao akafanyiza Uzieli, mwana wa Harhaya, mmoja wa mafundi wa dhahabu. Na baada yake akafanyiza Hanania, mmoja wa mafundi wa manukato, nao wakaujengea Yerusalemu buruji mpaka ule ukuta mpana.
9 Na baada yao akafanyiza Refaya, mwana wa Huri, akida wa nusu ya Yerusalemu.
10 Na baada yao akafanyiza Yedaya, mwana wa Harumafu, kuielekea nyumba yake. Na baada yake akafanyiza Hatushi, mwana wa Hashabneya.
11 Malkiya, mwana wa Harimu, na Hashubu, mwana wa Pahath-moabu, wakafanyiza sehemu nyingine, na mnara wa tanuu.
12 Na baada yake akafanyiza Shalumu, mwana wa Haloheshi, akida wa nusu ya Yerusalemu, yeye na binti zake.
13 Lango la bondeni wakalifanyiza Hanuni, nao wakaao Zanoa; wakalijenga, wakaisimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake, na huo ukuta wa dhiraa elfu mpaka lango la jaa.
14 Na lango la jaa akalifanyiza Malkiya, mwana wa Rekabu, akida wa mtaa wa Beth-hakeremu; akalijenga, akaisimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake.
15 Na lango la chemchemi akalifanyiza Shalumu, mwana wa Kolhoze, akida wa mtaa wa Mispa; akalijenga na kulifunika, akaisimamisha milango yake, na vyuma vyake, na makomeo yake, na huo ukuu wa birika la Shiloa karibu na bustani ya mfalme, mpaka madaraja yashukayo kutoka mji wa Daudi.
16 Baada yake akafanyiza Nehemia, mwana wa Azbuki, akida wa nusu ya mtaa wa Beth-suri, mpaka mahali paelekeapo makaburi ya Daudi, na mpaka birika lililofanyizwa, na mpaka nyumba ya mashujaa.
17 Baada yake wakafanyiza Walawi, Rehumi, mwana wa Bani. Baada yake akafanyiza Hashabia, akida wa nusu ya mtaa wa Keila, kwa mtaa wake.
18 Baada yake wakafanyiza ndugu zao, Binui, mwana wa Henadadi, akida wa nusu ya mtaa wa Keila.
19 Na baada yake akafanyiza Ezeri, mwana wa Yeshua, akida wa Mispa, sehemu nyingine, kupaelekea penye kupanda kwa ghala ya silaha, ukuta ugeukapo.
20 Baada yake Baruki, mwana wa Zakai, akafanyiza kwa bidii sehemu nyingine, toka ugeukapo ukuta mpaka mlango wa nyumba ya Eliashibu, kuhani mkuu.
21 Baada yake akafanyiza Meremothi, mwana wa Uria, mwana wa Hakosi, sehemu nyingine, toka mlango wa nyumba ya Eliashibu mpaka mwisho wa nyumba ya Eliashibu.
22 Na baada yake wakafanyiza makuhani, watu wa Uwandani.
23 Baada yao wakafanyiza Benyamini na Hashubu, kuielekea nyumba yao. Baada yao akafanyiza Azaria, mwana wa Maaseya, mwana wa Anania, kando ya nyumba yake.
24 Baada yake akafanyiza Binui, mwana wa Henadadi, sehemu nyingine, toka nyumba ya Azaria mpaka ugeukapo ukuu, na mpaka pembeni.
25 Baada yake akafanyiza Palali, mwana wa Uzai, kuelekea ugeukapo ukuta, nao mnara utokezao penye nyumba ya juu ya kifalme, iliyopo karibu na uwanda wa walinzi. Baada yake akafanyiza Pedaya, mwana wa Paroshi,
26 (basi Wanethini hukaa Ofeli), mpaka mahali paelekeapo lango la maji kukabili mashariki, nao mnara utokezao.
27 Baada yake wakafanyiza Watekoi sehemu nyingine, kuuelekea mnara mkubwa utokezao, na mpaka ukuta wa Ofeli.
28 Juu ya lango la farasi wakafanyiza makuhani, kila mtu kuielekea nyumba yake. Baada yao akafanyiza Sadoki, mwana wa Imeri, kuielekea nyumba yake.
29 Na baada yake akafanyiza Shemaya, mwana wa Shekania, mlinzi wa lango la mashariki.
30 Baada yake wakafanyiza Hanania, mwana wa Shelemia, na Hanuni, mwana wa sita wa Salafu, sehemu nyingine. Baada yake akafanyiza Meshulamu, mwana wa Berekia, sehemu nyingine kuelekea chumba chake.
31 Baada yake akafanyiza Malkiya, mmoja wa mafundi wa dhahabu, mpaka nyumba ya Wanethini, na ya wafanya biashara, kulielekea lango la gereza, na mpaka chumba cha juu cha pembeni.
32 Na kati ya chumba cha juu cha pembeni na lango la kondoo wakafanyiza mafundi wa dhahabu na wafanya biashara.

Nehemia 4


1 Lakini ikawa, Sanbalati aliposikia ya kwamba tulikuwa tukiujenga ukuta, akaghadhibika, akaingiwa na uchungu sana, akawadhihaki Wayahudi.
2 Akanena mbele ya nduguze na mbele ya jeshi la Samaria, akisema, Wayahudi hawa wanyonge wanafanyaje? Je! Watajifanyizia boma? Watatoa dhabihu? Au watamaliza katika siku moja? Je! Watayafufua mawe katika chungu hizi za kifusi, nayo yameteketezwa kwa moto?
3 Basi Tobia, Mwamoni, alikuwa karibu naye, akasema, Hata hiki wanachokijenga, angepanda mbweha, angeubomoa ukuta wao wa mawe.
4 Sikia, Ee Mungu wetu; maana tunadharauliwa; ukawarudishie mashutumu yao juu ya vichwa vyao, ukawatoe watekwe katika nchi ya uhamisho;
5 wala usiusitiri uovu wao, wala isifutwe dhambi yao, mbele zako; kwa maana wamekukasirisha mbele ya hao wanaojenga.
6 Basi tukaujenga ukuta; nao ukuta wote ukaungamanishwa kiasi cha nusu ya kimo chake; maana watu walikuwa na moyo wa kufanya kazi.
7 Lakini ikawa, Sanbalati, na Tobia, na Waarabu, na Waamoni, na Waashdodi, waliposikia ya kuwa kazi ya kuzitengeneza kuta za Yerusalemu inaendelea, na ya kuwa mahali palipobomoka panaanza kuzibwa, basi wakaghadhibika mno;
8 wakafanya shauri wote pamoja kuja kupigana na Yerusalemu, na kufanya machafuko humo.
9 Bali sisi tulimwomba dua Mungu wetu, tena tukaweka walinzi, mchana na usiku, kwa sababu yao, ili kuwapinga.
10 Wakasema Yuda, Nguvu zao wachukuao mizigo zimedhoofika, na kifusi tele zipo; tusiweze kuujenga ukuta.
11 Nao adui zetu wakasema, Hawatajua wala kuona, hata tutakapokuja kati yao, na kuwaua, na kuikomesha kazi hiyo.
12 Kisha ikawa, Wayahudi walipokuja, wale waliokaa karibu nao, wakatuambia mara kumi, Kutoka kila mahali mtakaporejea watatushambulia.
13 Basi, nikaweka watu, mahali pa chini pa nafasi iliyokuwa nyuma ya ukuta, mahali palipokuwa wazi, kwa kadiri ya jamaa zao, nikawaweka wenye panga zao, na mikuki yao, na pinde zao.
14 Nikatazama, nikaondoka, nikawaambia wakuu, na mashehe, na watu wengine waliobaki, Msiwaogope; mkumbukeni Bwana, aliye mkuu mwenye kuogofya, mkawapiganie ndugu zenu, na wana wenu, na binti zenu, na wake zenu, na nyumba zenu.
15 Kisha ikawa, adui zetu waliposikia ya kuwa tumekwisha kupata habari, na ya kuwa Mungu amelibatilisha shauri lao, ndipo sisi sote tukarudi ukutani, kila mtu kwa kazi yake.
16 Ikawa tokea wakati huo, nusu ya watumishi wangu walitumika katika kazi hiyo, na nusu yao wakaishika mikuki, na ngao, na pinde, na darii; na maakida walikuwa nyuma ya nyumba yote ya Yuda.
17 Watu wale walioujenga ukuta, na wale waliochukua mizigo, walijitweka wenyewe, kila mtu alifanya kazi kwa mkono mmoja, na kwa mkono wake wa pili alishika silaha yake;
18 nao wajenzi, kila mtu alikuwa na upanga wake, umefungwa ubavuni mwake, ndivyo alivyojenga. Na yeye aliyepiga baragumu alikuwa karibu na mimi.
19 Nikawaambia wakuu, na mashehe na watu wengine; Kazi hii ni nyingi, tena kubwa, nasi tumetawanyika juu ya ukuta, kila mtu mbali na mwenzake;
20 basi mahali po pote mtakaposikia sauti ya baragumu, enendeni huko, mkatujie; Mungu wetu atatupigania.
21 Hivyo tukajitia katika kazi hiyo; na nusu yao waliishika mikuki, tangu alfajiri hata nyota zikatokea.
22 Kadhalika, wakati ule ule, nikawaambia watu, Kila mtu na akae ndani ya Yerusalemu pamoja na mtumishi wake, wapate kuwa walinzi wetu wakati wa usiku, na kufanya kazi wakati wa mchana.
23 Basi mimi, na ndugu zangu, na watumishi wangu, na watu wa ulinzi walionifuata, hatukuvua nguo zetu hata mmoja; kila mtu alikwenda kuteka maji akichukua silaha yake.

Nehemia 5


1 Ndipo kukatokea kilio kikuu cha watu, na wake zao, juu ya ndugu zao Wayahudi.
2 Maana, walikuwako watu waliosema, Sisi, na wana wetu na binti zetu, tu wengi; na tupate ngano, tule, tukaishi.
3 Tena walikuwako wengine waliosema, Tumeweka rehani mashamba yetu, na mizabibu yetu, na nyumba zetu; tupate ngano, kwa sababu ya njaa.
4 Tena walikuwako wengine waliosema, Tumekopa fedha ili kulipa kodi ya mfalme kwa kuweka rehani mashamba yetu, na mizabibu yetu.
5 Walakini miili yetu ni kama miili ya ndugu zetu, na watoto wetu kama watoto wao; kumbe! Mnawatia utumwani wana wetu na binti zetu kuwa watumishi, na baadhi ya binti zetu wamekwisha kutiwa utumwani; wala hatuwezi kujiepusha na hayo; maana watu wengine wana mashamba yetu na mizabibu yetu.
6 Nami nilikasirika sana, niliposikia kilio chao, na maneno hayo.
7 Ndipo nikafanya shauri na nafsi yangu, nikagombana na wakuu na mashehe, nikawaambia, Mnatoza watu riba, kila mtu ndugu yake. Nikakutanisha mkutano mkubwa ili kushindana nao.
8 Nikawaambia, Sisi kwa kadiri ya uwezo wetu tumewakomboa ndugu zetu Wayahudi, waliouzwa kwa makafiri; na ninyi mnataka kuwauza ndugu zenu, tena kuwauza ili sisi tuwanunue? Wakanyamaza kimya, wasiweze kusema neno lo lote.
9 Tena nalisema, Neno hili mnalolitenda si jema; je! Haiwapasi ninyi kwenda katika kicho cha Mungu wetu, kwa sababu ya mashutumu ya makafiri adui zetu?
10 Na mimi pia, na ndugu zangu, na watumishi wangu, twawakopesha fedha na ngano ili kupata faida? Tafadhali na tuliache jambo hili la riba.
11 Naomba, warudishieni leo hivi mashamba yao, na mashamba yao ya mizabibu, na mashamba yao ya mizeituni, na nyumba zao, na lile fungu la mia la fedha, na la ngano, na la divai, na la mafuta, mnalowatoza.
12 Ndipo wakasema, Tutawarudishia, wala hatutataka kitu kwao; tutafanya hivyo, kama ulivyosema. Kisha nikawaita makuhani, nikawaapisha, ya kwamba watafanya kama ahadi hiyo.
13 Tena nikakung'uta nguo yangu, nikasema, Mungu na amkung'ute vivyo hivyo kila mtu nyumbani mwake, na kazini mwake, asiyeitimiza ahadi hiyo; naam, na akung'utwe vivyo hivyo, na kuwa hana kitu. Mkutano wote wakasema, Amina; wakamhimidi Bwana. Nao watu wakafanya kama ahadi hiyo.
14 Tena tangu wakati huo nilipowekwa kuwa liwali wao katika nchi ya Yuda, tangu mwaka wa ishirini hata mwaka wa thelathini na mbili wa Artashasta mfalme, yaani, miaka kumi na miwili, mimi na ndugu zangu hatukula chakula cha liwali.
15 Lakini maliwali wa kwanza walionitangulia, wakawalemea watu, wakawatwalia chakula na mvinyo, zaidi ya shekeli arobaini za fedha; tena watumwa wao nao wakatawala juu ya watu; lakini mimi sikufanya hivyo, kwa kuwa nalimcha Mungu.
16 Naam, hata kazi ya ukuta huu tena nikaishika sana, wala hatukununua mashamba; na watumishi wangu wote wakakusanyika huko kazini.
17 Pamoja na hayo wakawako mezani pangu, katika Wayahudi na mashehe, watu mia na hamsini, zaidi ya wale waliotujia kutoka kwa makafiri waliotuzunguka.
18 Basi, maandalio yaliyoandaliwa kwa siku moja yalikuwa ng'ombe mmoja, na kondoo wazuri sita; tena nikaandaliwa kuku, na mara moja katika siku kumi akiba ya mvinyo ya namna zote; wala kwa hayo yote sikukidai chakula cha liwali, kwa kuwa utumwa ulikuwa mzito juu ya watu hao.
19 Unikumbukie, Ee Mungu wangu, kwa mema, yote niliyowafanyia watu hawa.

Nehemia 6


1 Basi ikawa, walipoarifiwa Sanbalati, na Tobia, na Geshemu, Mwarabu na adui zetu hao wengine, kwamba nimeujenga ukuta, wala hayakusalia mavunjiko ndani yake; (ijapokuwa hata wakati ule sijaisimamisha milango katika malango);
2 Sanbalati na Geshemu wakatuma wajumbe kwangu, wakasema, Njoo, tukutane huko vijijini katika nchi tambarare ya Ono. Walakini wakakusudi kunifanyia mabaya.
3 Na mimi nikatuma wajumbe kwao, nikasema, Hii ni kazi kubwa ninayoifanya mimi, hata nisiweze kushuka; mbona kazi ikome, hapo ninapoiacha, niwashukie?
4 Nao wakaniletea maneno kama hayo mara nne; nikawajibu maneno kama yale.
5 Ndipo Sanbalati akamtuma kwangu mtumwa wake vile vile mara ya tano, na barua wazi mkononi mwake;
6 nayo yakaandikwa humo, Habari imeenea katika mataifa, naye Geshemu asema neno lilo hilo, ya kwamba wewe na Wayahudi mwakusudi kuasi; ndiyo sababu waujenga huo ukuta; nawe wataka kuwamiliki, ndivyo wasemavyo.
7 Nawe umewaweka manabii ili wakuhubirie huko Yerusalemu, kusema, Yuko mfalme katika Yuda; basi sasa ataarifiwa mfalme sawasawa na maneno haya. Njoo sasa basi, na tufanye shauri pamoja.
8 Ndipo mimi nikatuma kwake wajumbe, kusema, Hakukufanyika mambo kama hayo uyasemayo, lakini kwa moyo wako wewe mwenyewe umeyabuni.
9 Kwani hao wote walitaka kutuogofisha, wakisema, Italegea mikono yao katika kazi, isifanyike. Lakini sasa nitaitia mikono yangu nguvu.
10 Nikaingia nyumbani kwa Shemaya, mwana wa Delaya, mwana wa Mehetabeli, aliyekuwa amefungwa; naye akasema, Tukutane nyumbani mwa Mungu, ndani ya hekalu, tukaifunge milango ya hekalu; kwa maana watakuja kukuua; naam, wakati wa usiku watakuja kukuua.
11 Nami nikasema, Je! Mtu kama mimi nikimbie? Naye ni nani, akiwa kama nilivyo mimi, atakayeingia hekaluni ili kuponya maisha yake? Sitaingia.
12 Nikatambua, na tazama, siye Mungu aliyemtuma; lakini amefanya unabii huu kinyume changu; nao Tobia na Sanbalati ndio waliomwajiri.
13 Kwa sababu hii aliajiriwa, ili mimi niogope, nikafanye hivyo na kutenda dhambi, kisha wao wawe nazo habari mbaya, ili wanishutumie.
14 Uwakumbuke, Ee Mungu wangu, Tobia na Sanbalati sawasawa na hayo matendo yao, na yule nabii mke Noadia, na hao manabii waliosalia, waliotaka kuniogofya.
15 Basi huo ukuta ukamalizika siku ya ishirini na tano ya mwezi wa Eluli, katika muda wa siku hamsini na mbili.
16 Ikawa adui zetu wote waliposikia, ndipo makafiri wote waliotuzunguka wakaogopa, nao wakakata tamaa sana machoni pao wenyewe; maana waliitambua kazi hiyo ilivyotendwa na Mungu wetu.
17 Tena siku zile wakuu wa Yuda walimletea Tobia nyaraka nyingi, nazo nyaraka za Tobia zikawafikilia.
18 Kwa maana walikuwa watu wengi katika Yuda waliomwapia, kwa sababu alikuwa mkwewe Shekania, mwana wa Ara; naye Yehohanani mwanawe amemwoa binti Meshulamu, mwana wa Berekia.
19 Tena waliyanena mema yake mbele yangu, nayo maneno yangu humwambia yeye. Tobia naye akaniletea mimi nyaraka za kuniogofisha.

Nehemia 7


1 Ikawa, hapo ukuta ulipojengwa, na milango nimekwisha kuisimamisha, na mabawabu, na waimbaji, na Walawi, wamewekwa,
2 ndipo nilimwagiza ndugu yangu, Hanani, pamoja na yule Hanania, jemadari wa ngome, kuwa na amri juu ya Yerusalemu; kwa maana alikuwa mtu mwaminifu huyo, na mwenye kumcha Mungu kuliko wengi.
3 Nikawaambia, Yasifunguliwe malango ya Yerusalemu kabla halijachomoza jua; nao walinzi wangali wakisimama bado, waifunge milango, mkaikaze; kisha wekeni walinzi wa zamu wa hao wakaao Yerusalemu, kila mtu na zamu yake, na kila mtu kuielekea nyumba yake.
4 Basi mji ulikuwa wa nafasi nyingi, tena mkubwa; lakini watu waliomo walikuwa haba, wala nyumba hazijajengwa.
5 Mungu wangu akanitia moyoni mwangu, kwamba niwakusanye wakuu na mashehe, na watu, ili wahesabiwe kwa nasaba. Nikakiona kitabu cha vizazi vya hao waliokwea hapo kwanza, nikaona ya kwamba imeandikwa humo;
6 Hawa ndio wana wa wilaya, waliokwea kutoka katika ule uhamisho wa hao waliokuwa wamechukuliwa, ambao Nebukadreza, mfalme wa Babeli ,aliwachukua mateka,nao wakarudiYerusalemu na Yuda,kila mtu mjini kwake.
7 ndio hawa waliokuja pamoja na Zerubabeli, Yoshua, Nehemia, Seraya, Reelaya, Nahamani, Mordekai, Bilshani, Mispari, Bigwai, Rehumu, na Baana. Hii ndiyo hesabu ya wanaume wa watu wa Israeli;
8 Wana wa Paroshi, elfu mbili mia moja sabini na wawili.
9 Wana wa Shefatia, mia tatu sabini na wawili.
10 Wana wa Ara mia sita hamsini na wawili.
11 Wana wa Pahath-Moabu, wa wana wa Yeshua na Yoabu, elfu mbili mia nane na kumi na wanane.
12 Wana wa Elamu, elfu moja mia mbili hamsini na wanne.
13 Wana wa Zatu, mia nane arobaini na watano.
14 Wana wa Zakai, mia saba na sitini.
15 Wana wa Binui, mia sita arobaini na wanane.
16 Wana wa Bebai, mia sita ishirini na wanane.
17 Wana wa Azgadi, elfu mbili mia tatu ishirini na wawili.
18 Wana wa Adonikamu, mia sita sitini na saba.
19 Wana wa Bigwai, elfu mbili sitini na saba.
20 Wana wa Adini, mia sita hamsini na watano.
21 Wana wa Ateri, wa Hezekia, tisini na wanane.
22 Wana wa Hashumu, mia tatu ishirini na wanane.
23 Wana wa Besai, mia tatu ishirini na wanne.
24 Wana wa Harifu, mia moja na kumi na wawili.
25 Wana wa Gibeoni, tisini na watano.
26 Watu wa Bethlehemu na Netofa, mia na themanini na wanane.
27 Watu wa Anathothi, mia na ishirini na wanane.
28 Watu wa Beth-Azmawethi, arobaini na wawili.
29 Watu wa Kiriath-Yearimu, na Kefira, na Beerothi, mia saba arobaini na watatu.
30 Watu wa Rama na Geba, mia sita na ishirini na mmoja.
31 Watu wa Mikmashi, mia moja na ishirini na wawili.
32 Watu wa Betheli na Ai, mia moja ishirini na watatu.
33 Watu wa Nebo, hamsini na wawili.
34 Wana wa Elamu wa pili, elfu moja mia mbili hamsini na wanne.
35 Wana wa Harimu, mia tatu na ishirini.
36 Wana wa Yeriko, mia tatu arobaini na watano.
37 Wana wa Lodi, na Hadidi, na Ono, mia saba ishirini na mmoja.
38 Watu wa Senaa, elfu tatu mia kenda na thelathini.
39 Makuhani; Wana wa Yedaya, wa mbari ya Yeshua, mia kenda sabini na watatu.
40 Wana wa Imeri, elfu moja hamsini na wawili.
41 Wana wa Pashuri, elfu moja mia mbili arobaini na saba.
42 Wana wa Harimu, elfu moja na kumi na saba.
43 Walawi; Wana wa Yeshua, wa Kadmieli wa wana wa Hodavia, sabini na wanne.
44 Waimbaji; Wana wa Asafu, mia moja arobaini na wanane.
45 Mabawabu; Wana wa Shalumu, wana wa Ateri, wana wa Talmoni, wana wa Akubu, wana wa Hatita, wana wa Shobai, mia moja thelathini na wanane.
46 Wanethini; wana wa Siha, wana wa Hasufa, wana wa Tabaothi;
47 wana wa Kerosi, wana wa Siaha, wana wa Padoni;
48 wana wa Lebana, wana wa Hagaba, wana wa Salmai;
49 wana wa Hanani, wana wa Gideli, wana wa Gahari;
50 wana wa Reaya, wana wa Resini, wana wa Nekoda;
51 wana wa Gazamu, wana wa Uza, wana wa Pasea;
52 wana wa Besai wana wa Meunimu, wana wa Nefusimu;
53 wana wa Bakbuki, wana wa Hakufa, wana wa Harhuri;
54 wana wa Basluthi, wana wa Mehida, wana wa Harsha;
55 wana wa Barkosi, wana wa Sisera, wana wa Tema;
56 wana wa Nesia, wana wa Hatifa.
57 Akina watumwa wa Sulemani; Wana wa Sotai, wana wa Soferethi, wana wa Peruda;
58 wana wa Yaala, wana wa Darkoni, wana wa Gideli;
59 wana wa Shefatia, wana wa Hatili, wana wa Pokereth-Sebaimu, wana wa Amoni.
60 Wanethini wote, pamoja na akina watumwa wa Sulemani, walikuwa mia tatu tisini na wawili.
61 Na hawa ndio watu waliokwea kutoka Tel-mela, na Tel-harsha, na Kerubu, na Adani, na Imeri; walakini hawakuweza kuonyesha mbari za baba zao, wala kizazi chao, kwamba walikuwa wa Israeli;
62 Wana wa Delaya, wana wa Tobia, wana wa Nekoda, mia sita na arobaini na wawili.
63 Tena katika makuhani; Wana wa Habaya, wana wa Hakosi, wana wa Barzilai, yule aliyeoa mmojawapo binti Barzilai, Mgileadi, akaitwa kwa jina lao.
64 Hao waliitafuta orodha yao miongoni mwa wale waliohesabiwa kwa nasaba, wasionekane; kwa hiyo walihesabiwa kuwa na unajisi.
65 Na huyo Tirshatha akawaambia kwamba wasile katika vile vitu vitakatifu sana, hata atakaposimama kuhani mwenye Urimu na Thumimu.
66 Basi hilo kusanyiko lote zima, jumla yake ilikuwa watu arobaini na mbili elfu na mia tatu na sitini,
67 tena zaidi ya hao, kulikuwa na watumishi wao waume kwa wake, ambao walikuwa elfu saba na mia tatu na thelathini na saba; kisha walikuwa na waimbaji waume kwa wake mia mbili arobaini na watano.
68 Farasi zao walikuwa mia saba thelathini na sita; nyumbu zao, mia mbili arobaini na watano;
69 ngamia zao, mia nne thelathini na watano; punda zao, elfu sita na mia saba na ishirini.
70 Na baadhi ya wakuu wa mbari za mababa walitoa mali kwa ajili ya kazi hii. Yule Tirshatha akatoa kwa ajili ya hazina darkoni za dhahabu elfu moja ,na mabakuli hamsini , na mavazi ya makuhani mia tano na thelathini.
71 Na baadhi ya wakuu wa mbari za mababa wakatoa, na kutia katika hazina ya kazi hiyo, darkoni za dhahabu ishirini elfu, na mane za fedha elfu mbili na mia mbili.
72 Na mabaki ya watu wakatoa darkoni za dhahabu ishirini elfu, na mane za fedha elfu mbili, na mavazi ya makuhani sitini na saba.
73 Hivyo makuhani, na Walawi, na mabawabu, na waimbaji, na baadhi ya watu, na Wanethini, na Israeli wote, wakakaa mijini mwao. Hata ulipowadia mwezi wa saba, wana wa Islaeli walikuwa wakikaa katika miji yao.

Nehemia 8


1 Na watu wote wakakusanyika kama mtu mmoja katika uwanja uliokuwa mbele ya lango la maji; wakamwambia Ezra, mwandishi, akilete kitabu cha torati ya Musa, Bwana aliyowaamuru Israeli.
2 Naye Ezra, kuhani, akaileta torati mbele ya kusanyiko, la wanaume na wanawake, na wote walioweza kusikia na kufahamu, siku ya kwanza na mwezi wa saba.
3 Akasoma humo mbele ya uwanja uliokuwa ukikabili lango la maji, tangu mapambazuko hata adhuhuri, mbele ya hao wanaume na wanawake, na wale walioweza kufahamu; na masikio ya watu wote yakasikiliza kitabu cha torati.
4 Naye Ezra, kuhani, akasimama juu ya mimbari ya mti, waliyokuwa wameifanya kwa kusudi hilo; na karibu naye wakasimama Matithia, na Shema, na Anaya, na Uria, na Hilkia, na Maaseya, mkono wake wa kuume; na mkono wake wa kushoto, Pedaya, na Misbaeli, na Malkiya, na Hashumu, na Hashbadani, na Zekaria, na Meshulamu.
5 Ezra akakifunua kitabu machoni pa watu wote; (maana alikuwa juu ya watu wote); na hapo alipokifungua, watu wote walisimama;
6 Ezra akamhimidi Bwana, Mungu Mkuu. Nao watu wote wakaitika, Amina, Amina, pamoja na kuinua mikono yao; kisha wakainama vichwa vyao, wakamsujudu Bwana kifudifudi.
7 Tena Yeshua, na Bani, na Sherebia, na Yamini, na Akubu, na Shabethai, na Hodai, na Maaseya, na Kelita, na Azaria, na Yozabadi, na Hanani, na Pelaya, nao ni Walawi, wakawafahamisha watu torati; na watu wakasimama mahali pao.
8 Nao wakasoma katika kitabu, katika torati ya Mungu, kwa sauti ya kusikilika; wakaeleza maana yake, hata wakayafahamu yaliyosomwa.
9 Naye Nehemia, ndiye aliyekuwa Tirshatha, na Ezra kuhani, mwandishi, na Walawi waliowafundisha watu, wakawaambia watu wote, Siku hii ni takatifu kwa Bwana, Mungu wenu; msiomboleze wala msilie. Maana watu wote walilia, walipoyasikia maneno ya torati.
10 Kisha akawaambia, Enendeni zenu, mle kilichonona, na kunywa kilicho kitamu, tena mpelekeeni sehemu yeye asiyewekewa kitu; maana siku hii ni takatifu kwa Bwana wetu; wala msihuzunike; kwa kuwa furaha ya Bwana ni nguvu zenu.
11 Hivyo Walawi wakawatuliza watu wote, wakasema, Nyamazeni, kwa maana siku hii ni takatifu; wala msihuzunike.
12 Na watu wote wakaenda zao kula na kunywa, na kuwapelekea watu sehemu, na kufanya furaha nyingi, kwa sababu walikuwa wameyafahamu maneno yale waliyohubiriwa.
13 Hata siku ya pili wakuu wa mbari za mababa za watu wote, na makuhani, na Walawi, wakamkusanyikia Ezra, mwandishi, ili wapate kuyasikiliza maneno ya torati.
14 Wakaona ya kuwa imeandikwa katika torati, jinsi Bwana alivyoamuru kwa mkono wa Musa, ya kwamba wana wa Israeli wakae katika vibanda, katika sikukuu ya mwezi wa saba;
15 na ya kwamba wahubiri na kutangaza katika miji yao yote, na katika Yerusalemu, kusema, Enendeni mlimani, mkalete matawi ya mzeituni, na matawi ya mzeituni-mwitu, na matawi ya mihadasi, na matawi ya mitende, na matawi ya miti minene, ili kufanya vibanda, kama ilivyoandikwa.
16 Basi watu wote wakatoka, wakayaleta, wakajifanyizia vibanda, kila mtu juu ya dari ya nyumba yake, na katika nyua zao, na katika nyua za nyumba ya Mungu, na katika uwanja wa lango la maji, na katika uwanja wa lango la Efraimu.
17 Na mkutano wote wa watu, waliorudi kutoka nchi ya uhamisho wao, wakafanyiza vibanda, wakakaa katika vibanda hivyo; maana tokea siku za Yoshua, mwana wa Nuni, hata siku ile, wana wa Israeli hawakufanya hivyo. Pakawa na furaha kubwa sana.
18 Tena siku baada ya siku, tangu siku ya kwanza hata siku ya mwisho, akasoma katika kitabu cha torati ya Mungu. Wakafanya sikukuu muda wa siku saba; na siku ya nane palikuwa na kusanyiko la makini, kama ilivyoagizwa.

Nehemia 9


1 Hata siku ya ishirini na nne ya mwezi huo wana wa Israeli wakawa wamekusanyika, wakifunga, wenye kuvaa magunia, na kujitia udongo vichwani.
2 Waliokuwa wa wazao wa Israeli wakajitenga na wageni wote, wakasimama, wakaziungama dhambi zao, na maovu ya baba zao.
3 Basi wakasimama mahali pao, wakasoma katika kitabu cha torati ya Bwana, Mungu wao, muda wa robo ya siku; na robo nyingine wakaungama, wakamwabudu Bwana, Mungu wao.
4 Ndipo wakasimama madarajani pa Walawi, Yeshua, na Bani, na Kadmieli, na Shebania, na Buni, na Sherebia, na Bani, na Kenani, wakamlilia Bwana, Mungu wao, kwa sauti kuu.
5 Ndipo Walawi, Yeshua na Kadmieli, na Bani, na Hashabneya, na Sherebia, na Hodia, na Shebania, na Pethahia, wakasema, Simameni, mkamhimidi Bwana, Mungu wenu, tangu milele na hata milele. Na lihimidiwe jina lako tukufu, lililotukuka kuliko baraka zote na sifa zote.
6 Ezra akasema, Wewe ndiwe Bwana, wewe peke yako; wewe ulifanya mbingu, mbingu za mbingu, pamoja na jeshi lake lote, dunia na vyote vilivyomo, bahari na vitu vyote vilivyomo, nawe unavihifadhi vitu hivi vyote; na jeshi la mbinguni lakusujudu wewe.
7 Wewe ndiwe Bwana, Mungu, uliyemchagua Abramu, na kumtoa katika Uri wa Wakaldayo, na kumpa jina la Ibrahimu;
8 nawe ukauona moyo wake kuwa mwaminifu mbele zako, ukafanya agano naye, kumpa nchi ya Mkanaani, na Mhiti, na Mwamori, na Mperizi, na Myebusi, na Mgirgashi, naam, kuwapa wazao wake; nawe umeyafikiliza maneno yako, kwa kuwa ndiwe mwenye haki.
9 Tena uliyaona mateso ya baba zetu katika Misri, ukakisikia kilio chao, huko kando ya bahari ya Shamu;
10 nawe ukaonyesha ishara nyingi na mambo ya ajabu juu ya Farao, na juu ya watumishi wake wote, na juu ya watu wote wa nchi yake; kwa maana ulijua ya kuwa waliwatenda kwa kutakabari; ukajipatia jina kama vile ilivyo leo.
11 Nawe uliipasua bahari mbele yao, hata wakapita katikati ya bahari katika nchi kavu; na wale waliokuwa wakiwafuatia ukawatupa vilindini, mfano wa jiwe katika maji makuu.
12 Zaidi ya hayo ukawaongoza kwa nguzo ya wingu mchana; na kwa nguzo ya moto usiku; ili kuwapa mwanga katika njia iliyowapasa kuiendea.
13 Tena ulishuka juu ya mlima Sinai, ukasema nao toka mbinguni, ukawapa hukumu za haki, na sheria za kweli, na amri nzuri na maagizo;
14 ukawajulisha sabato yako takatifu, na kuwaagiza maagizo, na amri, na sheria, kwa mkono wa mtumishi wako, Musa.
15 Ukawapa chakula toka mbinguni, kwa ajili ya njaa yao, na kwa ajili yao ukaleta maji kutoka mwambani, kwa sababu ya kiu yao, ukawaamuru kwamba waingie katika nchi na kuimiliki, ambayo umeinua mkono wako kuwapa.
16 Lakini wao na baba zetu wakatakabari, wakafanya shingo zao kuwa ngumu, wala hawakuzisikiliza amri zako,
17 ila wakakataa kutii, wala hawakuyakumbuka maajabu yako, uliyoyafanya kati yao; lakini wakafanya shingo zao kuwa ngumu, na katika kuasi kwao wakaweka jemadari, ili wairudie hali ya utumwa; lakini wewe u Mungu, uliye tayari kusamehe, mwenye neema, mwenye huruma nyingi, si mwepesi wa hasira, u mwingi wa rehema, basi hukuwaacha.
18 Naam, hata walipojifanyia ndama ya kusubu, na kusema, Huyu ndiye Mungu wako aliyekupandisha kutoka Misri, tena walipokuwa wamefanya machukizo makuu;
19 hata hivyo wewe kwa wingi wa rehema zako hukuwaacha jangwani; nguzo ya wingu haikuwaondokea wakati wa mchana, ili kuwaongoza njiani; wala nguzo ya moto haikuondoka wakati wa usiku, ili kuwapa mwanga na kuwaonyesha njia watakayoiendea.
20 Ukawapa na roho yako mwema ili kuwaelimisha, wala hukuwanyima mana vinywani mwao, tena ukawapa maji kwa ajili ya kiu yao.
21 Naam, muda wa miaka arobaini uliwaruzuku jangwani, wasihitaji kitu; nguo zao hazikuchakaa, wala miguu yao haikuvimba.
22 Pamoja na hayo ukawapa falme na taifa za watu, ulizowagawia sawasawa na mafungu yao; hivyo wakaimiliki nchi ya Sihoni, naam, nchi yake mfalme wa Heshboni, na nchi ya Ogu, mfalme wa Bashani.
23 Watoto wao nao uliwaongeza kama nyota za mbinguni, ukawaingiza katika nchi ile, uliyowaambia baba zao kuwa wataingia kuimiliki.
24 Basi wale watoto wakaingia wakaimiliki nchi, nawe ukawatiisha wenyeji wa nchi mbele yao, ndio Wakanaani, ukawatia mikononi mwao, pamoja na wafalme wao, na watu wa nchi, wawatende kama wapendavyo.
25 Wakaitwaa miji yenye boma, na nchi yenye neema, wakazitamalaki nyumba zilizojaa vitu vyema, birika zilizochimbwa, mizabibu, na mizeituni, na miti mingi yenye matunda; hivyo wakala, wakashiba, wakanenepa, wakajifurahisha katika wema wako mwingi.
26 Walakini hawakukutii, wakakuasi, wakaitupa sheria yako nyuma yao, wakawaua manabii wako walioshuhudu juu yao wapate kuwarejeza kwako; wakatenda machukizo makuu.
27 Kwa sababu hiyo ukawatia katika mikono ya adui zao, waliowasumbua; na wakati wa shida yao, walipokulilia, uliwasikia kutoka mbinguni; na kwa wingi wa rehema zako ukawapa waokozi waliowaokoa katika mikono ya adui zao.
28 Lakini walipokuwa wamekwisha kustarehe, walitenda mabaya tena mbele zako; kwa hiyo ukawaacha katika mikono ya adui zao, nao wakawatawala; hata hivyo waliporejea na kukulilia, uliwasikia toka mbinguni; ukawaokoa mara nyingi kwa rehema zako;
29 ukawashuhudia ili uwarudishe tena katika sheria yako; lakini walitakabari, wasizisikilize amri zako, bali wakazihalifu hukumu zako, (ambazo mtu akizitenda ataishi katika hizo), nao wakayaondoa mabega yao, wakafanya shingo zao kuwa ngumu, wasitake kusikiliza.
30 Lakini miaka mingi ukachukuliana nao, nawe ukawashuhudia kwa roho yako kwa vinywa vya manabii wako; wao wasitake kusikiliza; kwa hiyo ukawatia katika mikono ya watu wa nchi.
31 Ila kwa rehema zako nyingi hukuwakomesha kabisa, wala kuwaacha; kwa maana wewe u Mungu mwenye neema, mwenye rehema.
32 Basi sasa, Ee Mungu, mkuu, mwenye uweza, Mungu wa kuogofya, mwenye kushika maagano na rehema, mashaka yote yaliyotupata sisi, wafalme wetu, na wakuu wetu, na makuhani wetu, na manabii wetu, na baba zetu, na watu wako wote, tangu zamani za wafalme wa Ashuru hata leo, na yasihesabiwe kuwa ni madogo.
33 Lakini wewe u mwenye haki, katika hayo yote yaliyotupata; maana wewe umetenda yaliyo kweli, lakini sisi tumetenda yaliyo mabaya;
34 na wafalme wetu, na wakuu wetu, na makuhani wetu, na baba zetu, hawakuishika sheria yako, wala hawakuzisikiliza amri zako na shuhuda zako, ulizowashuhudia.
35 Kwa kuwa hawakukutumikia wewe katika ufalme wao, na katika wema wako mkuu uliowapa, na katika nchi ile kubwa yenye neema uliyowapa mbele yao, wala hawakughairi na kuyaacha mabaya yao.
36 Tazama, sisi hapa tu watumwa leo, na katika habari ya nchi hii uliyowapa baba zetu, wapate kula matunda yake na mema yake, tazama, sisi hapa tu watumwa ndani yake.
37 Nayo yawapatia faida nyingi wafalme uliowaweka juu yetu kwa sababu ya dhambi zetu; tena wana mamlaka juu ya miili yetu, na juu ya wanyama wetu, kadiri wapendavyo, nasi tu katika dhiki kuu.
38 Na kwa sababu ya hayo yote sisi twafanya agano la hakika, na kuliandika; na wakuu wetu, na Walawi wetu, na makuhani wetu, wanalitilia muhuri.

Nehemia 10


1 Basi hawa ndio waliotia muhuri; Nehemia, ndiye Tirshatha, mwana wa Hakalia, na Sedekia;
2 Seraya, Azaria, Yeremia;
3 Pashuri, Amaria, Malkiya;
4 Hamshi, Shekania, Maluki;
5 Harimu, Meremothi, Obadia;
6 Danieli, Ginethoni, Baruki;
7 Meshulamu, Abiya, Miyamini;
8 Maazia, Bilgai, Shemaya; hao ndio waliokuwa makuhani.
9 Na Walawi; ndio, Yeshua, mwana wa Azania, Binui wa wana wa Henadadi, Kadmieli;
10 na ndugu zao, Shebania, Hodia, Kelita, Pelaya, Hanani;
11 Mika, Rehobu, Hashabia;
12 Zakuri, Sherebia, Shebania;
13 Hodia, Bani, Beninu;
14 Na wakuu wa watu; Paroshi, Pahath-Moabu, Elamu, Zatu, Bani;
15 Buni, Azgadi, Bebai;
16 Adonikamu, Bigwai, Adini;
17 Ateri, Hezakia, Azuri;
18 Hodia, Hashumu, Besai;
19 Harifu, Anathothi, Nobai;
20 Magpiashi, Meshulamu, Heziri;
21 Meshezabeli, Sadoki, Yadua;
22 Pelatia, Hanani, Anaya;
23 Hoshea, Hanania, Hashubu;
24 Haloheshi, Pilha, Shobeki;
25 Rehumu, Hashabna, Maaseya;
26 Ahia, Hanani, Anani;
27 Maluki, Harimu, na Baana.
28 Na watu waliosalia, makuhani, Walawi, mabawabu, waimbaji, Wanethini, na hao wote waliojitenga katika watu wa nchi kwa torati ya Mungu; wake zao, na wana wao, na binti zao, kila mwenye maarifa na akili;
29 wakaambatana na ndugu zao, wakuu wao, nao wakaingia katika laana na kiapo, ya kuwa wataiendea torati ya Mungu, iliyotolewa kwa mkono wa Musa, mtumishi wa Mungu, na kuziangalia, na kuzitenda, amri zote za Bwana, Bwana wetu, na hukumu zake na sheria zake;
30 wala tusiwaoze watu wa nchi binti zetu, wala kuwatwalia wana wetu binti zao;
31 tena watu wa nchi wakitembeza biashara, au chakula cho chote, siku ya sabato, tusinunue kwao siku ya sabato, au siku takatifu; tena kwamba tuuache mwaka wa saba, na madai ya kila deni.
32 Tena tukajifanyia maagizo, kujitoza mwaka kwa mwaka theluthi ya shekeli kwa huduma ya nyumba ya Mungu wetu;
33 kwa mikate ya wonyesho, na kwa sadaka ya unga ya daima, na kwa sadaka ya kuteketezwa ya daima, ya sabato, na ya siku za mwezi mpya, na ya sikukuu, tena kwa vitu vile vitakatifu, na kwa sadaka za dhambi, za kuwafanyia Israeli upatanisho, na kwa ajili ya kazi yote ya nyumba ya Mungu wetu.
34 Kisha tukapiga kura, makuhani, na Walawi, na watu, juu ya matoleo ya kuni, ili kuzileta nyumbani kwa Mungu wetu, kwa kadiri ya mbari za baba zetu, kwa nyakati zilizoamriwa, mwaka kwa mwaka, kukoka moto madhabahuni mwa Bwana, Mungu wetu, kama ilivyoandikwa katika torati;
35 tena kuleta malimbuko ya ardhi yetu, na malimbuko ya matunda yote ya miti ya namna zote, mwaka kwa mwaka, nyumbani kwa Bwana;
36 tena wazaliwa wa kwanza wa wana wetu, na wa wanyama wetu, kama ilivyoandikwa katika torati, na wazaliwa wa kwanza wa ng'ombe zetu na kondoo zetu, ili kuwaleta nyumbani mwa Mungu wetu, kwa makuhani watumikao nyumbani mwa Mungu wetu;
37 tena tuyalete malimbuko ya unga wetu, na sadaka zetu za kuinuliwa, na matunda ya miti ya namna zote, mvinyo, na mafuta, kwa makuhani, hapo vyumbani kwa nyumba ya Mungu wetu; na zaka za ardhi yetu kwa Walawi; kwa kuwa hao Walawi wazitwaa zaka mijini mwote mwa kulima kwetu.
38 Naye kuhani, mwana wa Haruni, atakuwako pamoja na Walawi, watwaapo zaka Walawi; nao Walawi wataipandisha zaka ya hizo zaka nyumbani kwa Mungu wetu, vyumbani, katika nyumba ya hazina.
39 Kwa kuwa wana wa Israeli na wana wa Lawi wataleta sadaka ya kuinuliwa ya nafaka, na mvinyo, na mafuta, vyumbani, kwa kuwa ndimo vilimo vyombo vya patakatifu, na makuhani watumikao, na mabawabu, na waimbaji; wala sisi hatutaiacha nyumba ya Mungu wetu.

Nehemia 11


1 Basi, wakuu wa watu walikuwa wakikaa Yerusalemu; nao watu waliosalia wakapiga kura, ili katika watu kumi kumleta mmoja akae ndani ya Yerusalemu mji mtakatifu, na wale kenda wakae mijini.
2 Na hao watu wakawabariki wote waliojitoa kwa hiari wakae Yerusalemu.
3 Basi hawa ndio wakuu wa jimbo waliokaa Yerusalemu; ila mijini mwa Yuda wakakaa kila mtu katika milki yake mijini mwao, yaani, Israeli, makuhani, na Walawi, na Wanethini, na akina watumwa wa Sulemani.
4 Tena wakakaa Yerusalemu wengine wa wana wa Yuda, na wengine wa wana wa Benyamini. Wa wana wa Yuda; Athaya, mwana wa Uzia, mwana wa Zekaria, mwana wa Amaria, mwana wa Shefatia, mwana wa Mahalaleli, wa wana wa Peresi;
5 na Maaseya, mwana wa Baruki, mwana wa Kolhoze, mwana wa Hazaya, mwana wa Adaya, mwana wa Yoyaribu, mwana wa Zekaria, Mshelani.
6 Wana wa Peresi wote waliokaa Yerusalemu walikuwa watu mia nne sitini na wanane, mashujaa.
7 Na wana wa Benyamini ndio hawa; Salu, mwana wa Meshulamu, mwana wa Yoedi, mwana wa Pedaya, mwana wa Kolaya, mwana wa Maaseva, mwana wa Ithieli, mwana wa Yeshaya.
8 Na baada yake Gabai, Salai, watu mia kenda ishirini na wanane.
9 Na Yoeli, mwana wa Zikri, alikuwa msimamizi wao; na Yuda, mwana wa Hasenua, alikuwa wa pili juu ya mji.
10 Wa makuhani; Yedaya, Yoyaribu, Yakini,
11 na Seraya, mwana wa Hilkia, mwana wa Meshulamu, mwana wa Sadoki, mwana wa Merayothi, mwana wa Ahitubu, msimamizi wa nyumba ya Mungu,
12 na ndugu zao waliofanya kazi ya nyumbani, watu mia nane ishirini na wawili; na Adaya, mwana wa Yerohamu, mwana wa Pelalia, mwana wa Amzi, mwana wa Zekaria, mwana wa Pashuri, mwana wa Malkiya,
13 na ndugu zake, wakuu wa mbari za mababa, watu mia mbili arobaini na wawili; na Maasai, mwana wa Azareli, mwana wa Azai, mwana wa Meshilemothi, mwana wa Imeri,
14 na ndugu zao, waume mashujaa, watu mia na ishirini na wanane; na msimamizi wao alikuwa Zabdieli, mmojawapo wa hao wakuu.
15 Na wa Walawi; Shemaya, mwana wa Hashubu, mwana wa Azrikamu, mwana wa Hashabia, mwana wa Buni;
16 na Shabethai na Yozabadi, wa wakuu wa Walawi, walioisimamia kazi ya nje ya nyumba ya Mungu;
17 na Matania, mwana wa Mika, mwana wa Zikri, mwana wa Asafu, mkuu mwenye kuanzisha shukrani katika sala, na Bakbukia, wa pili wake miongoni mwa nduguze; na Obadia, mwana wa Shemaya, mwana wa Galali, mwana wa Yeduthuni.
18 Walawi wote waliokaa katika mji mtakatifu walikuwa watu mia mbili themanini na wanne.
19 Pamoja na hao, mabawabu; Akubu, Talmoni, na ndugu zao waliolinda malangoni, walikuwa watu mia na sabini na wawili.
20 Na Israeli waliosalia, katika hao makuhani, na Walawi, walikuwamo mijini mwote mwa Yuda, kila mtu katika milki yake.
21 Lakini Wanethini walikuwa wakikaa Ofeli; na juu ya Wanethini walikuwa Siha na Gishpa.
22 Naye msimamizi wa Walawi huko Yerusalemu, ni Uzi, mwana wa Bani, mwana wa Hashabia, mwana wa Matania, mwana wa Mika, wa wana wa Asafu, hao waimbaji, alikuwa juu ya kazi ya nyumba ya Mungu.
23 Kwa kuwa palikuwa na amri ya mfalme juu yao, na agizo la hakika walilowekewa waimbaji, kama ilivyohusika na kila siku.
24 Na Pethahia, mwana wa Meshezabeli, wa wana wa Zera, mwana wa Yuda, alikuwa wakili wa mfalme kwa habari ya mambo yote ya watu.
25 Na katika habari za vijiji na mashamba yake; wengine wa wana wa Yuda walikuwa wakikaa Kiriath-arba na vijiji vyake, na katika Diboni na vijiji vyake, na Yekabzeeli na vijiji vyake;
26 na katika Yeshua, na Molada, na Beth-peleti;
27 na Hazar-shuali, na Beer-sheba na vijiji vyake;
28 na katika Siklagi, na Mekona na vijiji vyake;
29 na katika Enrimoni, na Sora, na Yarmuthi;
30 Zanoa, Adulamu na vijiji vyake, Lakishi na mashamba yake, Azeka na vijiji vyake. Hivyo wakatua toka Beer-sheba mpaka bonde la Hinomu.
31 Wana wa Benyamini nao walikuwa wakikaa Geba, na Mikmashi, na Aiya, na Beth-eli na vijiji vyake;
32 Anathothi, Nobu, Anania;
33 Hazori, Rama, Gitaimu;
34 Hadidi, Seboimu, Nebalati;
35 Lodi, na Ono, bonde la Wakarashi.
36 Na wa Walawi, wengine walikaa katika Yuda na wengine katika Benyamini.

Nehemia 12


1 Basi, hawa ndio makuhani na Walawi waliopanda na Zerubabeli, mwana wa Shealueli, na Yoshua; Seraya, Yeremia, Ezra;
2 Amaria, Maluki, Hatushi;
3 Shekania, Harimu, Meremothi;
4 Ido, Ginethoni, Abia;
5 Miyamini, Maazia, Bilgai;
6 Shemaya, Yoyaribu, Yedaya;
7 Salu, Amoki, Hilkia, Yedaya. Hawa walikuwa wakuu wa makuhani na ndugu zao siku za Yoshua.
8 Tena Walawi; Yeshua, Binui, Kadmieli, Sherebia, Yuda, na Matania, aliyekuwa juu ya shukrani, yeye na ndugu zake.
9 Tena Bakbukia na Uno, ndugu zao, kuwaelekea kwa zamu.
10 Naye Yoshua akamzaa Yoyakimu, Yoyakimu akamzaa Eliashibu, Eliashibu akamzaa Yoyada,
11 Yoyada akamzaa Yohana, Yohana akamzaa Yadua.
12 Na siku za Yoyakimu wakawako makuhani, wakuu wa mbari za mababa; wa Seraya, Meraya; wa Yeremia, Hanania;
13 wa Ezra, Meshulamu; wa Amaria, Yehohanani;
14 wa Maluki, Yonathani; wa Shekania, Yusufu;
15 wa Harimu, Adna; wa Meremothi, Helkai;
16 wa Ido, Zekaria; wa Ginethoni, Meshulamu;
17 wa Abia, Zikri; wa Miyamini; wa Maazia, Piltai;
18 wa Bilgai, Shamua; wa Shemaya, Yehonathani;
19 wa Yoyaribu, Matenai; wa Yedaya, Uzi;
20 wa Salu, Kalai; wa Amoki, Eberi;
21 wa Hilkia, Hashabia; wa Yedaya, Nethaneli.
22 Walawi siku za Eliashibu, na Yoyada, na Yohana, na Yadua, wameandikwa wakuu wa mbari za mababa; tena na makuhani; hata siku za kumiliki kwake Dario, Mwajemi.
23 Wana wa Lawi, wakuu wa mbari za mababa, wameandikwa katika kitabu cha tarehe, hata siku za Yohana mwana wa Eliashibu.
24 Nao wakuu wa Walawi; Hashabia, Sherebia, Yeshua, Binui, Kadmieli, na ndugu zao kuwaelekea, ili kusifu na kushukuru, kama amri ya Daudi, mtu wa Mungu, zamu kwa zamu.
25 Matania, Bakbukia, Obadia, Meshulamu, Talmoni, na Akubu, walikuwa mabawabu, wa kulinda nyumba za hazina penye malango.
26 Hao walikuwapo siku za Yoyakimu, mwana ya Yoshua, mwana wa Yosadaki, na siku za Nehemia, liwali, na Ezra, kuhani, mwandishi.
27 Basi, walipouweka wakfu ukuta wa Yerusalemu wakawatafuta Walawi katika mahali pao pote, ili kuwaleta Yerusalemu, wapate kufanya wakfu pamoja na furaha, na kwa shukrani, na kwa kuimba, kwa matoazi, vinanda na vinubi.
28 Waimbaji wakakusanyika kutoka uwanda na viunga vya Yerusalemu, na kutoka vijiji vya Wanetofathi;
29 tena toka Beth-gilgali, na toka mashamba ya Geba na Azmawethi; kwa maana waimbaji hao walikuwa wamejijengea vijiji katika viunga vya Yerusalemu.
30 Makuhani na Walawi wakajitakasa, nao wakawatakasa watu, na malango, na ukuta.
31 Ndipo nikawapandisha wakuu wa Yuda juu ya ukuta, nikawaagiza mikutano mikubwa miwili ya hao walioshukuru, na kuandamana; mmoja uende kwa kuume ukutani kuliendea lango la jaa;
32 na baada yao wakaenda Hoshaya, na nusu ya wakuu wa Yuda,
33 na Azaria, na Ezra, na Meshulamu,
34 na Yuda, na Benyamini, na Shemaya, na Yeremia,
35 na baadhi ya makuhani wenye baragumu; Zekaria, mwana wa Yonathani, mwana wa Shemaya, mwana wa Matania, mwana wa Mikaya, mwana wa Zakuri, mwana wa Asafu;
36 na ndugu zake, Shemaya, Azareli, Milalai, Gilalai, Maai, Nethaneli, Yuda, na Hanani, wenye vinanda vya Daudi mtu wa Mungu; Ezra, mwandishi, akawatangulia;
37 na kwa lango la chemchemi, wakienda moja kwa moja mbele yao, wakapanda madaraja ya mji wa Daudi, uinukapo ukuta, juu ya nyumba ya Daudi, mpaka lango la maji upande wa mashariki.
38 Na mkutano wa pili wao wenye kushukuru wakaenda kuwalaki, na mimi nikafuata nyuma yao, pamoja na nusu ya watu, ukutani juu ya mnara wa tanuu, mpaka ule ukuta mpana;
39 na juu ya lango la Efraimu, na kupita lango la kale, na lango la samaki, na mnara wa Hananeli, na mnara wa Hamea, mpaka lango la kondoo; nao wakasimama hapo langoni pa gereza.
40 Ndivyo walivyosimama mikutano miwili yao walioshukuru nyumbani mwa Mungu, na mimi, na nusu ya mashehe pamoja nami;
41 na makuhani, Eliakimu, Maaseya, Miyamini, Mikaya, Elioenai, Zekaria na Hanania, wenye baragumu;
42 na Maaseya, na Shemaya, na Eleazari, na Uzi, na Yehohanani, na Malkiya, na Elamu, na Ezeri. Waimbaji wakaimba kwa sauti kuu, wenye Yezrahia kuwa msimamizi wao.
43 Wakatoa dhabihu nyingi siku ile, wakafurahi; kwa kuwa Mungu amewafurahisha furaha kuu; na wanawake pia na watoto wakafurahi; hata ikasikiwa mbali sana furaha hiyo ya Yerusalemu.
44 Na siku hiyo watu wakaagizwa juu ya vyumba vya hazina, kwa sadaka za kuinuliwa, na kwa malimbuko, na kwa zaka, ili kuzikusanya, kwa kadiri ya mashamba ya miji, sehemu zilizoamriwa katika torati za makuhani, na Walawi; kwa maana Yuda waliwafurahia makuhani na Walawi waliotumika.
45 Wakauangalia ulinzi wa Mungu wao, na ulinzi wa kutakasika, na hao waimbaji na mabawabu vile vile, sawasawa na amri ya Daudi, na ya Sulemani mwanawe.
46 Kwa kuwa siku za Daudi zamani, Asafu alikuwa mkuu wa waimbaji, na juu ya nyimbo za sifa na shukrani kwa Mungu.
47 Na Israeli wote, siku za Zerubabeli, na siku za Nehemia, walitoa sehemu za waimbaji na mabawabu, kama ilivyohusika kila siku; nao wakawatakasia Walawi; na Walawi wakawatakasia wana wa Haruni.

Nehemia 13


1 Siku hiyo walisoma katika kitabu cha Musa masikioni mwa watu; na ndani yake yalionekana maneno haya yameandikwa, ya kwamba Mwamoni na Mmoabi wasiingie katika kusanyiko la Mungu milele;
2 kwa sababu hawakuwalaki wana wa Israeli kwa chakula na maji, bali walimwajiri Balaamu juu yao ili awalaani; lakini Mungu aliigeuza ile laana kuwa baraka.
3 Ikawa walipoisikia torati, wakawatenga Israeli na umati wa watu waliochanganyika nao.
4 Na kabla ya hayo, Eliashibu, kuhani, aliyewekwa avisimamie vyumba vya nyumba ya Mungu wetu, kwa kuwa alikuwa karibu yake Tobia,
5 alikuwa amemtengenezea chumba kikubwa, hapo walipoweka zamani sadaka za unga, na ubani, na vyombo, na zaka za nafaka, na divai, na mafuta, walivyoamriwa kuwapa Walawi, na waimbaji, na mabawabu; tena sadaka za kuinuliwa zilizokuwa za makuhani.
6 Lakini wakati huo wote mimi sikuwako huko Yerusalemu; maana katika mwaka wa thelathini na mbili wa Artashasta, mfalme wa Babeli, nalimrudia mfalme; na baada ya siku kadha wa kadha nikaomba ruhusa tena kwa mfalme.
7 Nami nikaja Yerusalemu, nikafahamu yale mabaya, ambayo Eliashibu ameyatenda kwa ajili ya Tobia, kwa kumtengenezea chumba katika nyua za nyumba ya Mungu.
8 Nami nikasikitika sana; basi nikavitupa nje vyombo vyote vya Tobia vitoke humo chumbani.
9 Kisha nikatoa amri, nao wakavisafisha vyumba; nami nikavirudisha humo vyombo vya nyumba ya Mungu, pamoja na sadaka za unga na ubani.
10 Tena nikaona ya kwamba Walawi hawakupewa sehemu zao; basi wamekimbia Walawi na waimbaji, waliofanya kazi, kila mtu shambani kwake.
11 Ndipo nikagombana na mashehe, nikasema, Mbona nyumba ya Mungu imeachwa? Kisha nikawakusanya, nikawaweka mahali pao.
12 Ndipo Yuda wote walipoleta zaka za nafaka, na mvinyo, na mafuta, kwenye hazina.
13 Nami nikawaweka watunza hazina juu ya hazina, yaani, Shelemia kuhani, na Sadoki mwandishi, na wa Walawi, Pedaya; na wa pili wao alikuwa Hanani, mwana wa Zakuri, mwana wa Matania; kwani walihesabiwa kuwa waaminifu, na ilikuwa juu yao kuwagawia ndugu zao.
14 Unikumbukie hayo, Ee Mungu wangu, wala usifute fadhili zangu nilizozitenda kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu, na kwa taratibu zake.
15 Siku hizo naliona katika Yuda watu wengine waliokanyaga mashinikizo ya mvinyo siku ya sabato, na wengine waliochukua miganda, na kuwapakia punda zao; tena na mvinyo, na zabibu, na tini, na namna zote za mizigo, waliyoileta Yerusalemu, siku ya sabato; nami nikashuhudia juu yao siku ile waliyouza vyakula.
16 Tena wakakaa humo watu wa Tiro, walioleta samaki, na biashara za kila namna, wakawauzia wana wa Yuda siku ya sabato, na mumo humo Yerusalemu.
17 Ndipo nikagombana na wakuu wa Yuda, nikawaambia, Ni neno baya gani hili mnalofanya ninyi, na kuinajisi siku ya sabato?
18 Je! Sivyo hivyo walivyofanya baba zenu; na Mungu wetu, je! Hakuyaleta mabaya haya yote juu yetu, na juu ya mji huu? Nanyi hata hivyo mwazidi kuleta ghadhabu juu ya Israeli kwa kuinajisi sabato!
19 Ikawa malango ya Yerusalemu yalipoanza kuwa na giza kabla ya sabato, naliamuru milango ifungwe, nikaamuru isifunguliwe hata sabato iishe; na baadhi ya watumishi wangu nikawaweka juu ya malango, ili usiingizwe mzigo wo wote siku ya sabato.
20 Basi wenye biashara na wachuuzi wa bidhaa za kila namna wakalala nje ya Yerusalemu mara mbili tatu.
21 Ndipo nikawashuhudia, nikawaambia, Mbona mwalala mbele ya ukuta? Mkitenda hivi tena, nitawakamata. Tangu wakati ule hawakuja tena siku ya sabato.
22 Kisha nikawaamuru Walawi wajitakase, nao waje kuyalinda malango, ili kuitakasa siku ya sabato. Unikumbukie hayo nayo, Ee Mungu wangu, ukaniachilie sawasawa na wingi wa rehema zako.
23 Tena siku zizo hizo nikawaona wale Wayahudi waliokuwa wameoa wanawake wa Ashdodi, na Amoni, na Moabu;
24 na watoto wao wakanena nusu kwa lugha ya Ashdodi, wala hawakuweza kunena kwa Kiyahudi, bali kwa lugha ya watu hao mojawapo.
25 Nikagombana nao, nikawalaani, nikawapiga baadhi yao, na kuwang'oa nywele zao; nikawaapisha kwa Mungu, nikasema, Msiwaoze wana wao binti zenu, wala msiwatwae binti zao ili waolewe na wana wenu, wala na ninyi wenyewe.
26 Je! Sulemani, mwana wa Daudi, hakufanya dhambi kwa kutenda hayo? Lakini katika mataifa mengi hapakuwa na mfalme mwingine mfano wake. Tena alipendwa na Mungu wake, naye Mungu akamfanya mfalme juu ya Israeli; walakini wanawake wageni walimkosesha hata yeye.
27 Basi, na sisi, je! Tuwasikilize ninyi kutenda neno hili baya, hata kumhalifu Mungu wetu kwa kuwaoa wanawake wageni?
28 Na mwana mmoja wa Yoyada, mwana wa Eliashibu, kuhani mkuu, alikuwa mkwewe Sanbalati, Mhoroni, basi nikamfukuza kwangu.
29 Uwakumbuke, Ee Mungu wangu, jinsi walivyounajisi ukuhani, na agano la ukuhani na la Walawi.
30 Hivyo nikawatakasa na kila kitu kigeni, nami nikawaagizia zamu makuhani na Walawi, kila mtu kazini mwake;
31 na matoleo ya kuni nyakati zilizoamriwa, na malimbuko. Nikumbuke, Ee Mungu wangu, ili unitendee mema.