2 Walfame

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24, 25

2 Walfame 1


1 Ikawa, baada ya kufa kwake Ahabu, Moabu wakawaasi Israeli.
2 Na Ahazia akaanguka katika dirisha la chumba chake orofani, katika Samaria, akaugua; akatuma wajumbe, akawaambia, Enendeni mkaulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, kwamba nitapona ugonjwa huu.
3 Lakini malaika wa Bwana akamwambia Eliya Mtishbi, Ondoka, uende ukaonane na wale wajumbe wa mfalme wa Samaria, ukawaambie, Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni?
4 Basi sasa, Bwana asema hivi, Hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa. Eliya akaondoka.
5 Wale wajumbe wakarudi, na mfalme akawaambia, Mbona mmerudi?
6 Wakamwambia, Mtu alitokea, akaonana nasi, akatuambia, Enendeni, rudini kwa mfalme yule aliyewatuma, mkamwambie, Bwana asema hivi Je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, hata mnakwenda kuuliza kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni? Basi kwa ajili ya hayo hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa.
7 Akawaambia, Je! Mtu yule aliyetokea, akaonana nanyi, akawaambia maneno hayo, alikuwa mtu wa namna gani?
8 Wakamwambia, Alikuwa amevaa vazi la manyoya, tena amejifunga shuka ya ngozi kiunoni mwake. Naye akasema, Ndiye yule Eliya Mtishbi.
9 Ndipo mfalme akatuma akida wa askari hamsini pamoja na hamsini wake, wamwendee Eliya. Akamwendea, na tazama, ameketi juu ya kilima. Akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka.
10 Eliya akajibu, akamwambia yule akida wa hamsini, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto ukashuka, ukamteketeza, yeye na hamsini wake.
11 Akatuma tena akida wa hamsini mwingine pamoja na hamsini wake, wamwendee. Akajibu, akamwambia, Ewe mtu wa Mungu, mfalme asema, Shuka upesi.
12 Eliya akajibu, akamwambia, Ikiwa mimi ni mtu wa Mungu, na ushuke moto kutoka mbinguni, ukuteketeze wewe na hamsini wako. Moto wa Mungu ukashuka kutoka mbinguni, ukamteketeza, yeye na hamsini wake.
13 Tena akatuma akida wa hamsini wa tatu, pamoja na hamsini wake. Yule akida wa hamsini wa tatu akapanda, akaenda akapiga magoti mbele ya Eliya, akamsihi sana, akamwambia, Ee mtu wa Mungu, nakusihi, roho yangu, na roho za watumishi wako hawa hamsini, ziwe na thamani machoni pako.
14 Tazama, moto ulishuka kutoka mbinguni, ukawateketeza wale akida wa hamsini wawili wa kwanza pamoja na hamsini wao; laiti sasa roho yangu na iwe na thamani machoni pako.
15 Malaika wa Bwana akamwambia Eliya, Shuka pamoja naye; usimwogope. Akaondoka, akashuka pamoja naye hata kwa mfalme.
16 Akamwambia, Bwana asema hivi, Kwa kuwa umetuma wajumbe waulize kwa Baal-zebubu, mungu wa Ekroni, je! Ni kwa sababu hapana Mungu katika Israeli, uulize neno lake? Kwa hiyo hutashuka katika kile kitanda ulichokipanda, bali hakika utakufa.
17 Basi akafa, sawasawa na neno la Bwana alilolinena Eliya. Na Yoramu alianza kutawala mahali pake katika mwaka wa pili wa Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda; kwa kuwa yeye hakuwa na mwana.
18 Na mambo yote yaliyosalia aliyoyafanya Ahazia, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?

2 Walfame 2


1 Ikawa, hapo Bwana alipopenda kumpandisha Eliya mbinguni kwa upepo wa kisulisuli, Eliya alitoka Gilgali pamoja na Elisha.
2 Eliya akamwambia Elisha, Tafadhali, kaa hapa; maana Bwana amenituma niende mpaka Betheli.
3 Elisha akasema, Kama Bwana aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha, Basi wakashuka mpaka Betheli. Basi wana wa manabii, waliokuwako Betheli, wakatoka kuonana na Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa Bwana atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akasema, Naam, najua; nyamazeni.
4 Eliya akamwambia, Tafadhali, kaa hapa, Elisha; maana Bwana amenituma niende mpaka Yeriko. Akasema, Kama Bwana aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Nao wakafika Yeriko.
5 Basi wana wa manabii, waliokuwako Yeriko, wakamkaribia Elisha, wakamwambia, Je! Unajua ya kuwa Bwana atamwondoa bwana wako leo, asiwe mkubwa wako? Akajibu, Naam, najua, nyamazeni.
6 Eliya akamwambia, Tafadhali kaa hapa; maana Bwana amenituma niende mpaka Yordani. Akasema, Kama Bwana aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Wakaendelea mbele wote wawili.
7 Basi watu hamsini wa wale wana wa manabii wakaenda wakasimama, kuwakabili kwa mbali; na hao wawili wakasimama karibu na Yordani.
8 Eliya akalitwaa vazi lake la juu, akalikunja, akayapiga maji, yakagawanyika huku na huku, na hao wawili wakavuka pakavu.
9 Hata ikawa, walipokwisha kuvuka, Eliya akamwambia Elisha, Omba kwangu lo lote utakalo nikutendee, kabla sijaondolewa kwako. Elisha akasema, Nakuomba, sehemu maradufu ya roho yako na iwe juu yangu.
10 Akasema, Umeomba neno gumu; lakini, ukiniona nitakapoondolewa kwako, utalipata; la hukuniona, hulipati.
11 Ikawa, walipokuwa wakiendelea mbele na kuongea, tazama! Kukatokea gari la moto, na farasi wa moto, likawatenga wale wawili; naye Eliya akapanda mbinguni kwa upepo wa kisulisuli.
12 Naye Elisha akaona, akalia, Baba yangu, baba yangu, gari la Israeli na wapanda farasi wake! Asimwone tena kabisa; akashika mavazi yake mwenyewe, akayararua vipande viwili.
13 Kisha akaliokota lile vazi la Eliya lililomwangukia, akarudi, akasimama katika ukingo wa Yordani.
14 Akalitwaa lile vazi la Eliya lililomwangukia, akayapiga maji, akasema, Yuko wapi Bwana, Mungu wa Eliya? Naye alipoyapiga maji, yakagawanyika huku na huku, Elisha akavuka.
15 Na hao wana wa manabii, waliokuwako Yeriko wakimkabili, walipomwona, walisema, Roho ya Eliya inakaa juu ya Elisha. Wakaja kuonana naye, wakainama kifudifudi mbele yake.
16 Wakamwambia, Angalia, wako hapa pamoja nasi watumishi wako watu hamsini walio hodari; waende, twakuomba, wamtafute bwana wako; isiwe labda roho ya Bwana imemtwaa na kumtupa juu ya mlima mmoja, au katika bonde moja. Akasema, Msiwatume.
17 Wakamsisitiza hata akaona haya, akasema, Haya! Watumeni. Basi wakatuma watu hamsini; nao wakatafuta siku tatu, wasimwone.
18 Wakamrudia, alipokuwa anakawia Yeriko; akawaambia, Je! Mimi sikuwaambia, Msiende?
19 Watu wa mjini wakamwambia Elisha, Angalia, twakusihi, mahali pa mji huu ni pazuri, kama bwana wangu aonavyo; lakini maji yake hayafai, na nchi huzaa mapooza.
20 Akasema, Nileteeni chombo kipya, mtie chumvi ndani yake. Wakamletea.
21 Akatoka akaenda mpaka chemchemi ya maji, akatupa ile chumvi humo ndani, akasema, Bwana asema hivi, Nimeyaponya maji haya; hakutatoka huko tena kufa wala kuzaa mapooza.
22 Hivyo yale maji yakapona hata leo, sawasawa na neno la Elisha alilolinena.
23 Akakwea kutoka huko mpaka Betheli; naye alipokuwa akienda njiani, wakatoka vijana katika mji, wakamfanyizia mzaha, wakamwambia, Paa wewe mwenye upaa! Paa wewe mwenye upaa!
24 Akatazama nyuma akawaona, akawalaani kwa jina la Bwana. Wakatoka dubu wawili wa kike mwituni, wakawararua vijana arobaini na wawili miongoni mwao.
25 Akatoka huko akaenda mlima wa Karmeli, na toka huko akarudi mpaka Samaria.

2 Walfame 3


1 Basi Yoramu mwana wa Ahabu alianza kutawala juu ya Israeli huko Samaria katika mwaka wa kumi na nane wa Yehoshafati mfalme wa Yuda ,akatawala miaka kumi na miwili.
2 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana; ila si kama baba yake na kama mama yake; maana akaiondoa ile nguzo ya Baali aliyoifanya baba yake.
3 Pamoja na hayo alishikamana na dhambi za Yeroboamu mwana wa Nebati, ambazo kwa hizo aliwakosesha Israeli; wala hakuziacha.
4 Basi Mesha, mfalme wa Moabu, alikuwa mfuga kondoo; naye alikuwa akimlipa mfalme wa Israeli sufu ya wana-kondoo elfu mia, na ya kondoo waume elfu mia.
5 Lakini ikawa, Ahabu alipokufa, mfalme wa Moabu akamwasi mfalme wa Israeli.
6 Akatoka wakati ule ule mfalme Yoramu katika Samaria, akawahesabu Israeli wote.
7 Akaenda akatuma kwa Yehoshafati mfalme wa Yuda, akasema, Mfalme wa Moabu ameniasi; je! Utakwenda pamoja nami tupigane na Moabu? Akasema, Nitakwenda; mimi ni kama wewe, watu wangu ni kama watu wako, farasi zangu ni kama farasi zako.
8 Akauliza, Njia ipi tuiendee? Akajibu, Njia ya jangwa la Edomu.
9 Basi mfalme wa Israeli akaenda, na mfalme wa Yuda, na mfalme wa Edomu; wakazunguka mwendo wa siku saba; wala hapakuwa na maji kwa jeshi, wala kwa wanyama waliowafuata.
10 Mfalme wa Israeli akasema, Ole wetu! Kwani Bwana amewakutanisha hawa wafalme watatu, awaue mkononi mwa Moabu.
11 Lakini Yehoshafati akasema, Je! Hapana hapa nabii wa Bwana, ili tumwulize Bwana kwa yeye? Akajibu mtumishi mmoja wa mfalme wa Israeli, akasema, Yupo hapa Elisha mwana wa Shafati, aliyekuwa akimimina maji juu ya mikono yake Eliya.
12 Yehoshafati akasema, Neno la Bwana analo huyu. Basi mfalme wa Israeli, na Yehoshafati, na mfalme wa Edomu, wakamshukia.
13 Elisha akamwambia mfalme wa Israeli, Nina nini mimi nawe? Uende kwa manabii wa babayo, na manabii wa mamayo. Mfalme wa Israeli akamwambia, La, sivyo; kwa kuwa Bwana amewakutanisha hawa wafalme watatu, awaue mkononi mwa Moabu.
14 Elisha akasema, Kama Bwana wa majeshi aishivyo, ambaye nimesimama mbele zake, kama singemwangalia uso wake Yehoshafati mfalme wa Yuda, singekutazama, wala kuonana nawe.
15 Ila sasa niletee mpiga kinanda. Ikawa, mpiga kinanda alipokipiga, mkono wa Bwana ukamjia juu yake.
16 Akasema, Bwana asema hivi, Fanyeni bonde hili lijae mahandaki.
17 Kwa kuwa Bwana asema hivi, Hamutauona upepo, wala hamtaiona mvua, ila bonde hilo litajaa maji; nanyi mtakunywa, ninyi, na ng'ombe zenu, na wanyama wenu.
18 Na jambo hili ni jepesi machoni pa Bwana; pia atawatia Wamoabi mikononi mwenu.
19 Nanyi mtapiga kila mji wenye boma, na kila mji ulio mzuri, na kila mti mwema mtaukata, na chemchemi zote za maji mtaziziba, na kila mahali palipo pema mtapaharibu kwa mawe.
20 Ikawa asubuhi, wakati wa kutoa sadaka ya unga, tazama, maji yakaja kwa njia ya Edomu, hata nchi ikajaa maji.
21 Basi Wamoabi wote waliposikia ya kuwa wafalme hao wamekwea ili kupigana nao, walijikusanya pamoja, wote wawezao kuvaa silaha, na wenye umri zaidi, wakasimama mpakani.
22 Wakaamka asubuhi na mapema, na hilo jua likameta-meta juu ya maji, na Wamoabi wakayaona yale maji yaliyowaelekea kuwa ni mekundu kama damu.
23 Wakasema, Ndiyo damu hii; bila shaka hao wafalme wameharibika, wamepigana kila mtu na mwenziwe; basi sasa, enyi Wamoabi, nyara hizo!
24 Hata walipokuja matuoni kwa Israeli, Waisraeli wakainuka wakawapiga Wamoabi, hata wakakimbia mbele yao; wakaendelea wakiwapiga-piga Wamoabi hata kwao.
25 Wakaibomoa ile miji; wakatupa katika kila mahali palipo pema kila mtu jiwe lake, wakapajaza; wakaziziba chemchemi zote za maji, wakaikata miti yote iliyo mizuri; mpaka katika Kir-haresethi tu wakayasaza mawe yake; ila wenye kombeo wakauzunguka wakaupiga.
26 Naye mfalme wa Moabu alipoona ya kwamba ameshindwa vitani, alitwaa pamoja naye watu mia saba wenye kufuta panga ili wapenye hata kwa mfalme wa Edomu; wala hawakudiriki.
27 Ndipo akamtwaa mwanawe wa kwanza, yeye ambaye angetawala mahali pake, akamtoa awe sadaka ya kuteketezwa juu ya ukuta. Kukawa hasira kuu juu ya Israeli; basi wakatoka kwake, wakarudi kwenda nchi yao wenyewe.

2 Walfame 4


1 Basi, mwanamke mmoja miongoni mwa wake za wana wa manabii alimlilia Elisha, akasema, Mtumishi wako mume wangu amekufa; nawe unajua ya kuwa mtumishi wako alikuwa mcha Bwana; na aliyemwia amekuja ili ajitwalie wana wangu wawili kuwa watumwa.
2 Elisha akamwambia, Nikufanyie nini? Niambie; una kitu gani nyumbani? Akasema, Mimi mjakazi wako sina kitu nyumbani, ila chupa ya mafuta.
3 Akasema, Nenda, ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache.
4 Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge.
5 Basi akamwacha, akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, na yeye akamimina.
6 Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, Hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma.
7 Ndipo akaja akamwambia yule mtu wa Mungu. Naye akasema, Enenda ukayauze mafuta haya, uilipe deni yako; nayo yaliyosalia uyatumie wewe na watoto wako.
8 Hata ikawa siku moja, Elisha alikwenda Shunemu; na huko kulikuwa na mwanamke mmoja mwenye cheo; naye akamshurutisha aje ale chakula. Ikawa kila alipopita njia ile, huingia kula chakula.
9 Yule mwanamke akamwambia mumewe, Tazama, mimi naona ya kuwa mtu huyu apitaye kwetu mara kwa mara ni mtu mtakatifu wa Mungu.
10 Nakuomba, tumfanyie chumba kidogo ukutani; na ndani yake tumwekee kitanda, na meza, na kiti, na kinara cha taa; na itakuwa, atujiapo, ataingia humo.
11 Ikawa siku moja akafika huko, akaingia katika chumba kile akalala.
12 Akamwambia Gehazi mtumishi wake, Mwite yule Mshunami. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mbele yake.
13 Akamwambia, Sema naye sasa, Tazama, wewe umetutunza sana namna hii; utendewe nini basi? Je! Uombewe neno kwa mfalme, au kwa amiri wa jeshi? Yule mwanamke akamjibu, Mimi ninakaa katika watu wangu mwenyewe.
14 Akasema, Basi, atendewe nini? Gehazi akajibu, Hakika hana mwana, na mumewe ni mzee.
15 Akamwambia, Kamwite. Naye alipokwisha kuitwa, akasimama mlangoni.
16 Akasema, Panapo wakati huu mwakani, utamkumbatia mwana. Akasema, La! Bwana wangu, wewe mtu wa Mungu, usiniambie mimi mjakazi wako uongo.
17 Yule mwanamke akachukua mimba, akazaa mtoto mume wakati uo huo mwakani, kama Elisha alivyomwambia.
18 Hata yule mtoto alipokua, ikawa siku moja alitoka kwenda kwa baba yake kwenye wavunao.
19 Akamwambia baba yake, Kichwa changu! Kichwa changu! Naye akamwambia mtumishi wake, Mchukue kwa mama yake.
20 Akamchukua, akampeleka kwa mama yake, naye akakaa magotini mwake hata adhuhuri, kisha akafa.
21 Mamaye akapanda juu, akamlaza juu ya kitanda cha yule mtu wa Mungu, akamfungia mlango, akatoka.
22 Kisha akamwita mumewe, akasema, Tafadhali, uniletee mtu mmoja wa watumishi, na punda mmoja, ili nimwendee yule mtu wa Mungu kwa haraka, nikarudi tena.
23 Akasema, Kwa nini kumwendea leo? Sio mwandamo wa mwezi, wala sabato. Akasema, Si neno.
24 Akatandika punda, akamwambia mtumishi wake, Mwendeshe, twendelee mbele. Usinipunguzie mwendo, nisipokuambia.
25 Basi akaenda, akafika kwa yule mtu wa Mungu, katika mlima wa Karmeli. Ikawa, yule mtu wa Mungu alipomwona kwa mbali, akamwambia Gehazi mtumishi wake, Tazama, Mshunami yule kule.
26 Tafadhali piga mbio sasa kwenda kumlaki, ukamwambie, Hujambo? Mume wako hajambo? Mtoto hajambo? Akajibu, Hawajambo.
27 Naye alipofika kwa yule mtu wa Mungu kilimani, alimshika miguu. Gehazi akakaribia amwondoe; lakini mtu wa Mungu akamwambia, Mwache; maana roho yake ndani yake ina uchungu; na Bwana amenificha, wala hakuniambia.
28 Yule mwanamke akasema, Je! Naliomba mwana kwa bwana wangu? Mimi sikusema, Usinidanganye?
29 Ndipo Elisha akamwambia Gehazi, Jikaze viuno, ukachukue fimbo yangu mkononi mwako, ukaende zako; ukikutana na mtu, usimsalimu; na mtu akikusalimu, usimjibu; ukaweke fimbo yangu juu ya uso wa mtoto.
30 Na mama yake yule mtoto akasema, Kama Bwana aishivyo, na roho yako iishivyo, sitakuacha. Basi akaondoka, akamfuata.
31 Na Gehazi akawatangulia, akaiweka ile fimbo juu ya uso wa mtoto; lakini hapakuwa na sauti, wala majibu. Basi akarudi ili kumlaki, akamwambia, akisema, Mtoto hakuamka.
32 Basi Elisha alipofika nyumbani, tazama, mtoto amekwisha kufa, amelazwa kitandani pake.
33 Basi akaingia ndani, akajifungia mlango, yeye na yule mtoto wote wawili, akamwomba Bwana.
34 Akapanda juu ya kitanda, akajilaza juu ya mtoto, akaweka kinywa chake juu ya kinywa chake, na macho yake juu ya macho yake, na mikono yake juu ya mikono yake; akajinyosha juu yake; mwili wake yule mtoto ukaanza kupata moto.
35 Kisha akarudi, akatembea nyumbani, huko na huko mara moja; akapanda, akajinyosha juu yake; na yule mtoto akapiga chafya mara saba, na mtoto akafumbua macho yake.
36 Akamwita Gehazi, akasema, Mwite yule Mshunami. Basi akamwita. Na alipofika kwake, Elisha akasema, Haya! Mchukue mwanao.
37 Ndipo akaingia, akamwangukia miguu akainama mpaka nchi; kisha akamchukua mwanawe, akatoka.
38 Elisha akafika Gilgali tena; na kulikuwa na njaa katika nchi; na hao wana wa manabii walikuwa wakikaa mbele yake. Akamwambia mtumishi wake, Teleka sufuria kubwa, uwapikie wana wa manabii.
39 Na mmoja wao akaenda nje kondeni ili kuchuma mboga, akaona mtango-mwitu, akayachuma matango-mwitu, hata nguo yake ikawa imejaa, akaja akayapasua-pasua sufuriani; kwa maana hawakuyajua.
40 Basi wakawapakulia hao watu ili wale. Ikawa, walipokuwa katika kula chakula, wakapiga kelele, wakasema, Mauti imo sufuriani, Ee mtu wa Mungu. Wala hawakuweza kula.
41 Lakini yeye akasema, Leteni unga. Naye akautupa ndani ya sufuria; akasema, Wapakulie watu, ili wale. Wala hakikuwamo kitu kibaya sufuriani.
42 Tena, akaja mtu kutoka Baal-shalisha, akamletea mtu wa Mungu chakula cha malimbuko, mikate ishirini ya shayiri, na masuke mabichi ya ngano guniani. Akasema, Uwape watu, ili wale.
43 Na mtumishi wake akasema, Je! Niwaandikie hiki watu mia? Lakini akasema, Uwape watu, ili wale; kwa kuwa Bwana asema hivi, Watakula na kusaza.
44 Basi akawaandikia, nao wakala, wakasaza, sawasawa na neno la Bwana.

2 Walfame 5


1 Basi Naamani, jemadari wa jeshi la mfalme wa Shamu, alikuwa mtu mkubwa mbele ya bwana wake, na mwenye kuheshimiwa, kwa sababu kwa mkono wake Bwana alikuwa amewapa Washami kushinda; tena alikuwa mtu hodari wa vita; lakini alikuwa mwenye ukoma.
2 Na Washami walikuwa wametoka vikosi, wakachukua mfungwa mmoja kijana mwanamke kutoka nchi ya Israeli; naye akamhudumia mkewe Naamani.
3 Akamwambia bibi yake, Laiti bwana wangu angekuwa pamoja na yule nabii aliyeko Samaria! Maana angemponya ukoma wake.
4 Mtu mmoja akaingia, akamwambia bwana wake, akasema, Yule kijana mwanamke aliyetoka nchi ya Israeli asema hivi na hivi.
5 Mfalme wa Shamu akasema, Haya! Basi, mimi nitampelekea mfalme wa Israeli waraka. Basi akaenda zake, akachukua mikononi mwake talanta kumi za fedha, na vipande vya dhahabu elfu sita, na mavazi kumi.
6 Akampelekea mfalme wa Israeli waraka ule, kusema, Waraka huu utakapokuwasilia, tazama, nimemtuma mtumishi wangu Naamani kwako, ili upate kumponya ukoma wake.
7 Ikawa, mfalme wa Israeli alipousoma waraka, alirarua mavazi yake, akasema, Je! Mimi ni Mungu, niue na kuhuisha, hata mtu huyu akanipelekea mtu nimponye ukoma wake? Fahamuni, basi, nakusihini, mwone ya kuwa mtu huyu anataka kugombana nami.
8 Ikawa, Elisha, yule mtu wa Mungu, aliposikia kwamba mfalme wa Israeli ameyararua mavazi yake, ndipo akatuma mtu kwa mfalme, akisema, Mbona umeyararua mavazi yako? Na aje sasa kwangu mimi, naye atajua ya kuwa yuko nabii katika Israeli.
9 Basi Naamani akaja na farasi wake na magari yake, akasimama mlangoni pa nyumba ya Elisha.
10 Naye Elisha akampelekea mjumbe, akisema, Enenda ukaoge katika Yordani mara saba, na nyama ya mwili wako itakurudia, nawe utakuwa safi.
11 Lakini Naamani akakasirika, akaondoka, akasema, Tazama, nalidhania, Bila shaka atatoka kwangu, na kusimama, na kuomba kwa jina la Bwana, Mungu wake, na kupitisha mkono wake mahali penye ugonjwa, na kuniponya mimi mwenye ukoma.
12 Je! Abana na Farpari, mito ya Dameski, si bora kuliko maji yote ya Israeli? Je! Siwezi kujiosha ndani yake, na kuwa safi? Akageuka, akaondoka kwa hasira.
13 Watumishi wake wakamkaribia, wakamwambia, wakasema, Baba yangu, kama yule nabii angalikuambia kutenda jambo kubwa, usingalilitenda? Je! Si zaidi basi, akikuambia, Jioshe, uwe safi?
14 Ndipo akashuka, akajichovya mara saba katika Yordani, sawasawa na neno lake yule mtu wa Mungu; nayo nyama ya mwili wake ikarudi ikawa kama nyama ya mwili wa mtoto mchanga, akawa safi.
15 Akamrudia yule mtu wa Mungu, yeye na mafuatano yake yote. Akaja, akasimama mbele yake; akasema, Sasa tazama, najua ya kwamba hakuna Mungu duniani mwote, ila katika Israeli; basi nakuomba upokee mbaraka kwa mtumwa wako.
16 Lakini akasema, Kama Bwana aishivyo, ambaye nimesimama mbele yake, sipokei kitu. Akamshurutisha apokee; lakini akakataa.
17 Naamani akasema; Kama sivyo, lakini mtumwa wako na apewe mzigo wa udongo wa baghala wawili; kwa maana mtumwa wako hatatoa tena sadaka ya kuteketezwa wala dhabihu kwa miungu mingine, ila kwa Bwana.
18 Jambo hili Bwana amwachilie mtumwa wako; bwana wangu akiingia nyumbani mwa Rimoni ili aabudu humo, naye akitegemea mkononi mwangu, nami nikijiinama nyumbani mwa Rimoni, hapo ninapojiinama nyumbani mwa Rimoni, Bwana amwachilie mtumwa wako jambo hili.
19 Akamwambia, Enenda kwa amani Basi akamwondokea mbali kidogo.
20 Lakini Gehazi, mtumishi wa Elisha mtu wa Mungu, akasema, Tazama, bwana wangu amemwachilia huyo Naamani Mshami, asivipokee mikononi mwake vile vitu alivyovileta; kama Bwana aishivyo, mimi nitamfuata mbio, nipokee kitu kwake.
21 Basi Gehazi akamfuata Naamani. Naye Naamani, alipoona mtu apigaye mbio anakuja nyuma yake, alishuka garini amlaki, akasema, Je! Ni amani?
22 Akasema, Amani. Bwana wangu amenituma, kusema, Tazama, sasa hivi wamenijia kutoka milimani mwa Efraimu vijana wawili wa wana na manabii; uwape, nakuomba, talanta ya fedha, na mavazi mawili.
23 Naamani akasema, Uwe radhi, ukatwae talanta mbili. Akamshurutisha, akafunga talanta mbili za fedha ndani ya mifuko miwili, na mavazi mawili, akawatwika watumishi wake wawili; nao wakayachukua mbele yake.
24 Naye alipofika kilimani, alivitwaa mikononi mwao, akaviweka nyumbani; akawaacha wale watu kuondoka, nao wakaenda zao.
25 Lakini yeye akaingia, akasimama mbele ya bwana wake. Elisha akamwambia, Watoka wapi, Gehazi? Akanena, Mtumwa wako hakuenda mahali.
26 Akamwambia, Je! Moyo wangu haukuenda na wewe, hapo alipogeuka yule mtu katika gari ili akulaki? Je! Huu ndio wakati wa kupokea fedha, na kupokea mavazi, na mashamba ya mizeituni, na mizabibu, na kondoo, na ng'ombe, na watumwa, na wajakazi?
27 Basi ukoma wa Naamani utakushika wewe, na wazao wako hata milele. Naye akatoka usoni pake mwenye ukoma kama theluji.

2 Walfame 6


1 Kisha, wana wa manabii wakamwambia Elisha, Angalia basi, mahali tukaapo mbele yako ni padogo kwetu.
2 Basi twende mpaka Yordani, twakuomba, tutwae huko kila mtu mti mmoja, ili tujifanyie huko mahali pa kukaa. Akajibu, Haya! Nendeni.
3 Mmoja wao akasema, Uwe radhi, basi nakusihi, uende pamoja na watumishi wako. Akajibu, Nitakwenda.
4 Basi, akaenda pamoja nao. Nao walipofika Yordani, wakakata miti.
5 Lakini mmojawapo alipokuwa katika kukata boriti, chuma cha shoka kikaanguka majini; akalia, akasema, Ole wangu! Bwana wangu, kwani kiliazimiwa kile.
6 Mtu wa Mungu akasema, Kilianguka wapi? Akamwonyesha mahali. Akakata kijiti, akakitupa pale pale, chuma kikaelea.
7 Akasema, Kiokote. Basi akanyosha mkono, akakitwaa.
8 Basi, mfalme wa Shamu alikuwa akifanya vita na Israeli. Akafanya mashauri na watumishi wake, akasema, Kituo changu kitakuwapo mahali fulani.
9 Yule mtu wa Mungu akapeleka habari kwa mfalme wa Israeli, kusema, Jihadhari, usipite mahali fulani; kwa sababu ndiko wanakoshukia Washami.
10 Mfalme wa Israeli akapeleka watu mpaka mahali pale alipoambiwa na yule mtu wa Mungu, na kuhadharishwa; akajiokoa nafsi yake, si mara moja, wala si mara mbili.
11 Basi mfalme wa Shamu moyo wake ukamfadhaika sana kwa ajili ya jambo hili; akawaita watumishi wake, akawaambia, Je! Hamtanionyesha, ni mtu yupi miongoni mwenu aliye upande wa mfalme wa Israeli?
12 Mmojawapo wa watumishi wake akasema, La, bwana wangu, mfalme; lakini Elisha, yule nabii aliye katika Israeli, humwambia mfalme wa Israeli maneno uyanenayo katika chumba chako cha kulala.
13 Akasema, Enendeni, mkamwangalie aliko, nipate kupeleka watu kwenda kumchukua. Akaambiwa ya kwamba, Tazama, yuko Dothani.
14 Kwa hiyo akapeleka huko farasi, na magari, na jeshi kubwa; wakafika usiku, wakauzingira mji ule pande zote.
15 Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje?
16 Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.
17 Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote.
18 Na walipomtelemkia Elisha akamwomba Bwana, akasema, Uwapige, nakusihi, watu hawa kwa upofu. Akawapiga kwa upofu sawasawa na neno la Elisha.
19 Elisha akawaambia, Njia hii siyo, na mji huu sio, nifuateni mimi, nami nitawapeleka kwa mtu yule mnayemtafuta. Akawapeleka Samaria.
20 Hata walipokwisha kuingia Samaria, Elisha akasema, Bwana wafumbue macho watu hawa, wapate kuona. Bwana akawafumbua macho wakaona; kumbe! Walikuwa katikati ya Samaria.
21 Naye mfalme wa Israeli alipowaona, akamwambia Elisha, Ee baba yangu, niwapige? Niwapige?
22 Akamjibu, Usiwapige; je! Ungetaka kuwapiga watu ambao umewatwaa mateka kwa upanga wako na uta wako? Weka chakula na maji mbele yao, wapate kula na kunywa, na kwenda kwa bwana wao.
23 Basi akawaandalia chakula tele; nao walipokwisha kula na kunywa, akawaacha, wakaenda zao kwa bwana wao. Na vikosi vya Shamu havikuja tena katika nchi ya Israeli.
24 Ikawa baada ya hayo, Ben-hadadi mfalme wa Shamu akakusanya majeshi yake yote, akakwea akauhusuru Samaria.
25 Njaa ikawa kuu huko Samaria; na tazama, wakauhusuru, hata kichwa cha punda kikapata kuuzwa kwa vipande themanini vya fedha, na kibaba cha mavi ya njiwa kwa vipande vitano vya fedha.
26 Ikawa mfalme wa Israeli alipokuwa akipita ukutani, mwanamke mmoja akamwita akisema, Unisaidie, bwana wangu, mfalme.
27 Akasema, Bwana asipokusaidia, nikusaidieje mimi? Ya sakafuni, au ya shinikizoni?
28 Mfalme akamwambia, Una nini? Akajibu, Mwanamke huyu aliniambia, Mtoe mtoto wako, tumle leo, na mtoto wangu tutamla kesho.
29 Basi, tukamtokosa mtoto wangu, tukamla; nikamwambia siku ya pili, Mtoe mtoto wako, tumle; naye amemficha mtoto wake.
30 Ikawa, mfalme alipoyasikia maneno ya huyo mwanamke, aliyararua mavazi yake; (naye alikuwa akipita juu ya ukuta;) na watu wakaona, na tazama, alikuwa amevaa magunia ndani mwilini mwake.
31 Ndipo akasema, Mungu anifanyie hivyo, na kuzidi, kikimbakia kichwa Elisha mwana wa Shafati juu yake leo.
32 Lakini Elisha alikuwa akikaa nyumbani mwake, na wazee wakikaa pamoja naye; na mfalme akamtuma mtu wa mbele yake; lakini hata kabla ya kufika kwake yule aliyetumwa, akawaambia wazee, Je! Mwaona jinsi huyu mwana wa mwuaji alivyotuma aniondolee kichwa changu? Angalieni, huyo aliyetumwa akifika, fungeni mlango, mkamzuie mlangoni; je! Sauti ya miguu ya bwana wake haiko nyuma yake?
33 Hata alipokuwa katika kusema nao, tazama, yule aliyetumwa akamshukia; naye akasema, Angalia, mabaya haya yatoka kwa Bwana; kwani mimi kumngojea Bwana tena?

2 Walfame 7


1 Elisha akasema, Lisikieni neno la Bwana; Bwana asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria.
2 Basi yule akida, ambaye mfalme alikuwa akitegemea mkono wake, akamjibu yule mtu wa Mungu, akasema, Tazama, kama Bwana angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akamwambia, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula.
3 Basi walikuwapo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe?
4 Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo; nasi tukikaa hapa, tutakufa vile vile. Haya! Twende tukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai tutaishi; wakituua, tutakufa tu.
5 Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami; na walipofika mwanzo wa kimo cha Washami, kumbe! Hapana mtu.
6 Kwa maana Bwana alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa; wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi.
7 Kwa hiyo wakaondoka, wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na punda zao, na kimo chao vile vile kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kujiponya nafsi zao.
8 Basi wale wenye ukoma walipofika mwisho wa kituo, waliingia katika hema moja, wakala, na kunywa, wakachukua fedha, na dhahabu, na mavazi, wakaenda wakavificha; wakarudi, wakaingia katika hema ya pili, vile vile wakachukua vitu, wakaenda, wakavificha.
9 Ndipo wakaambiana, Mambo haya tufanyayo si mema; leo ni siku ya habari njema, na sisi tunanyamaza; mkingoja hata kutakapopambazuka, madhara yatatupata; basi twende tukawaambie watu wa nyumba ya mfalme.
10 Basi wakaenda, wakawaita mabawabu wa mji; wakawaambia, Tulifika kituo cha Washami, na tazama, hapana mtu ye yote huko, wala sauti ya mtu, ila farasi wamefungwa, na punda wamefungwa, na hema zao kama walivyoziacha.
11 Na mabawabu wakaita wakawaambia watu wa nyumba ya mfalme.
12 Mfalme akaondoka usiku, akawaambia watumishi wake, Sasa nitawaonyesha ninyi walivyotutendea Washami. Wanajua ya kuwa tuna njaa; basi wametoka kituoni, ili kujificha kondeni, wakisema Watakapotoka mjini, tutawakamata hai; tena tutapata kuingia mjini.
13 Na mmojawapo wa watumishi wake akajibu, akasema, Kunradhi; baadhi ya watu na watwae farasi watano katika hao waliosalia, waliobaki ndani ya mji (tazama wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli waliobaki ndani yake; tazama, wamekuwa kama mkutano wote wa Israeli walioangamia), tukawapeleke tukaone.
14 Basi wakatwaa magari mawili na farasi zake; mfalme akawatuma kuwafuata Washami, akasema, Enendeni, mkaangalie.
15 Wakawafuata mpaka Yordani; na kumbe! Njia yote ilikuwa imejaa mavazi na vyombo, walivyovitupa Washami, wapate kukimbia upesi. Watu wale waliotumwa wakarudi, wakamwambia mfalme.
16 Basi watu wakatoka, wakaziteka nyara hema za Washami. Ikawa kipimo cha unga mzuri kikauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, sawasawa na neno la Bwana.
17 Naye mfalme akamweka yule akida, ambaye alitegemea mkono wake, awasimamie watu langoni; na watu wakamkanyaga langoni, akafa; kama alivyosema yule mtu wa Mungu, aliyenena hapo mfalme alipomshukia.
18 Ikatukia kama vile yule mtu wa Mungu alivyomwambia mfalme, Vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, na kipimo cha unga mzuri kwa shekeli, ndivyo vitakavyokuwa kesho, panapo saa hii, katika lango la Samaria;
19 na yule akida akamjibu mtu wa Mungu, akasema, Sasa tazama, kama Bwana angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akasema, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula.
20 Ikampata vivyo hivyo, kwa kuwa watu wakamkanyaga langoni, akafa.

2 Walfame 8


1 Basi Elisha alikuwa amemwambia yule mwanamke, ambaye alimfufulia mwanawe, akasema, Ondoka, ukaende wewe na jamaa yako, ukae hali ya kigeni utakakoweza kukaa; kwa sababu Bwana ameiita njaa; nayo itakuja juu ya nchi hii muda wa miaka saba.
2 Akaondoka yule mwanamke, akafanya kama alivyosema mtu wa Mungu; akaenda, yeye na jamaa yake, akakaa katika nchi ya Wafilisti miaka saba.
3 Ikawa miaka saba ilipoisha, yule mwanamke akarudi kutoka nchi ya Wafilisti; akatokea amlilie mfalme kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake.
4 Basi mfalme alikuwa akizungumza na Gehazi, mtumishi wa mtu wa Mungu, akinena, Uniambie, nakusihi, mambo makuu yote aliyoyafanya Elisha.
5 Ikawa, alipokuwa katika kumwambia mfalme jinsi alivyomfufua mtu aliyekufa, tazama, huyo mwanamke aliyemfufulia mwanawe, alimlilia mfalme kwa ajili ya nyumba yake na shamba lake. Gehazi akasema, Bwana wangu mfalme, huyu ndiye mwanamke, na huyu ndiye mwanawe, ambaye Elisha alimfufua.
6 Na mfalme alipomwuliza yule mwanamke, yeye akamweleza. Basi mfalme akamtolea akida, akasema, Mrudishie yote aliyokuwa nayo, na mapato yote ya shamba lake tangu siku aliposafiri, hata leo.
7 Kisha, Elisha akaenda Dameski; na Ben-hadadi, mfalme wa Shamu, alikuwa hawezi; akaambiwa ya kwamba, Yule mtu wa Mungu amefika hapa.
8 Mfalme akamwambia Hazaeli, Chukua zawadi mkononi mwako, ukaende ili kumlaki yule mtu wa Mungu, ukamwulize Bwana kwa kinywa chake, kusema, Je! Nitapona ugonjwa huu?
9 Basi Hazaeli akaenda kumlaki, akachukua zawadi mkononi mwake, za kila kitu chema kilichopatikana Dameski, kiasi cha mizigo ya ngamia arobaini, akaenda, akasimama mbele yake akasema, Mwana wako Ben-hadadi, mfalme wa Shamu, amenituma kwako, kusema, Je nitapona ugonjwa huu?
10 Elisha akamwambia, Enenda, ukamwambie, Bila shaka utapona; lakini Bwana amenionyesha ya kwamba bila shaka atakufa.
11 Akamkazia macho hata akatahayari; na yule mtu wa Mungu akalia machozi.
12 Hazaeli akasema, Bwana wangu analilia nini? Akajibu, Kwa sababu nayajua mabaya utakayowatenda wana wa Israeli; utazichoma moto ngome zao, utawaua vijana wao kwa upanga, utawaseta-seta watoto wao wachanga na wanawake wao wenye mimba utawapasua.
13 Hazaeli akasema, Lakini mimi mtumwa wako ni nani, mimi niliye mbwa tu, hata nifanye jambo hili kubwa? Elisha akajibu, Bwana amenionyesha ya kwamba wewe utakuwa mfalme juu ya Shamu.
14 Ndipo akamwacha Elisha, akarudi kwa bwana wake; naye akamwambia, Elisha alikuambiaje? Akajibu, Aliniambia ya kuwa bila shaka utapona.
15 Ikawa siku ya pili yake, akatwaa tandiko la kitanda, akalichovya katika maji, akalitandaza juu ya uso wake, hata akafa. Na Hazaeli akatawala badala yake.
16 Katika mwaka wa tano wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, [Yehoshafati alipokuwa mfalme wa Yuda], alianza kutawala Yehoramu mwana wa Yehoshafati mfalme wa Yuda.
17 Alikuwa na umri wa miaka thelathini na miwili alipoanza kutawala, akatawala miaka minane huko Yerusalemu.
18 Akaiendea njia ya wafalme wa Israeli kama walivyofanya nyumba ya Ahabu; kwa kuwa alikuwa amemwoa binti Ahabu; akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana.
19 Walakini Bwana hakupenda kuiharibu Yuda, kwa ajili ya Daudi mtumishi wake, kama alivyomwahidia akasema, kuwa atampa taa, yeye na wazao wake siku zote.
20 Zamani zake, Edomu wakaasi mkononi mwa Yuda, wakajifanyia mfalme.
21 Basi akaenda Yehoramu mpaka Sairi, na magari yake yote pamoja naye. Akaondoka usiku, akawapiga Waedomi waliomzunguka yeye na maakida wa magari; na watu wakakimbilia hemani kwao.
22 Hivyo Edomu wakaasi mkononi mwa Yuda hata leo. Na Libna wakaasi zamani zizo hizo.
23 Na mambo yote ya Yehoramu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
24 Akalala Yehoramu na baba zake, akazikwa pamoja na baba zake mjini mwa Daudi; na Ahazia mwanawe akatawala mahali pake.
25 Katika mwaka wa kumi na mbili wa Yoramu mwana wa Ahabu mfalme wa Israeli, Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda alianza kutawala.
26 Ahazia alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; akatawala mwaka mmoja huko Yerusalemu. Na jina la mamaye aliitwa Athalia binti Omri mfalme wa Israeli.
27 Akaiendea njia ya nyumba ya Ahabu, akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, kama walivyofanya nyumba ya Ahabu, kwa kuwa alikuwa mkwe wa jamaa ya Ahabu.
28 Akaenda pamoja na Yoramu mwana wa Ahabu ili kupigana na Hazaeli mfalme wa Shamu, huko Ramoth-gileadi; nao Washami wakamtia Yoramu jeraha.
29 Akarudi Yoramu mfalme, auguzwe katika Yezreeli jeraha walizotia Washami huko Rama alipopigana na Hazaeli mfalme wa Shamu. Naye Ahazia mwana wa Yehoramu mfalme wa Yuda akashuka amtazame Yoramu mwana wa Ahabu huko Yezreeli, kwa sababu alikuwa hawezi.

2 Walfame 9


1 Nabii Elisha akamwita mmojawapo wa wana wa manabii, akamwambia, Jikaze viuno, ukachukue chupa hii ya mafuta mkononi mwako, ukaende Ramoth-Gileadi.
2 Utakapofika huko, mtafute Yehu, mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, ukaingie, ukamtoe miongoni mwa ndugu zake, ukamchukue katika chumba cha ndani.
3 Kisha, ukatwae ile chupa ya mafuta, ukayamimine juu ya kichwa chake, ukaseme, Bwana asema hivi, Nimekutia mafuta uwe mfalme juu ya Israeli. Kisha ufungue mlango ukakimbie, wala usikawie.
4 Basi yule kijana, yule nabii kijana, akaenda Ramoth-Gileadi.
5 Naye alipofika, tazama, majemadari wa jeshi walikuwa wamekaa; naye akasema, Nimetumwa na neno kwako, Ee jemadari; Yehu akasema, Kwa yupi miongoni mwetu sote? Akasema, Kwako wewe, Ee jemadari.
6 Akainuka akaingia nyumbani; naye akayamimina yale mafuta kichwani mwake, akamwambia, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Nimekutia mafuta uwe mfalme juu ya watu wa Bwana, yaani, juu ya Israeli.
7 Nawe utawapiga nyumba ya Ahabu, bwana wako, ili nijilipize kisasi cha damu ya watumishi wangu manabii, na damu ya watumishi wote wa Bwana, mkononi mwa Yezebeli.
8 Kwa maana nyumba yote ya Ahabu wataangamia; nami nitamkatilia mbali kila mwanamume wa nyumba ya Ahabu, yeye aliyefungwa, na yeye asiyefungwa, katika Israeli.
9 Nami nitaifanya nyumba ya Ahabu kuwa kama nyumba ya Yeroboamu mwana wa Nebati, na kama nyumba ya Baasha mwana wa Ahiya.
10 Na mbwa watamla Yezebeli katika kiwanja cha Yezreeli, wala hapatakuwa na mtu wa kumzika. Akaufungua mlango, akakimbia.
11 Ndipo Yehu akatoka akawaendea watumishi wa bwana wake. Mmoja wao akamwuliza, Je! Ni amani? Huyu mwenye wazimu amekujia kwa nini? Akawaambia, Ninyi mnamjua mtu huyu na habari ya maneno yake.
12 Wakasema, Ni uongo; haya, tuambie. Akasema, Aliniambia haya na haya, akisema, Bwana asema hivi, Nimekutia mafuta, uwe mfalme juu ya Israeli.
13 Basi wakafanya haraka, kila mtu akalitwaa vazi lake, na kulitia chini yake juu ya madaraja, wakapiga baragumu wakasema, Yehu ni mfalme.
14 Hivyo Yehu, mwana wa Yehoshafati, mwana wa Nimshi, akafanya fitina juu ya Yoramu. Basi Yoramu alikuwa akiulinda Ramoth-Gileadi, yeye na Israeli wote, kwa sababu ya Hazaeli mfalme wa Shamu.
15 Lakini mfalme Yoramu mwenyewe alikuwa amerudi, apate kupona jeraha zake alizotiwa na Washami, alipokuwa akipigana na Hazaeli mfalme wa Shamu. Yehu akasema, Kama hii ndiyo nia yenu, basi, msimwache hata mtu mmoja atoke mjini, ili aende kupeleka habari Yezreeli.
16 Basi Yehu akapanda gari lake kwenda Yezreeli; kwa maana Yoramu alikuwa amelala huko; na Ahazia mfalme wa Yuda alikuwa ameshuka ili kumtazama Yoramu.
17 Basi mlinzi alikuwa anasimama juu ya mnara wa Yezreeli, akaliona lile kundi la watu wa Yehu, alipokuwa akija, akasema, Naona kundi la watu. Yoramu akasema, Haya! Mtwae mpanda farasi mmoja, ukampeleke aende kuwalaki, na kuwauliza, Je! Ni amani?
18 Basi mpanda farasi mmoja akatoka awalaki, akasema, Mfalme asema hivi, Je! Ni amani? Yehu akasema, Wewe una nini na amani? Geuka unifuate. Yule mlinzi akatoa habari, akasema, Yule mjumbe amewafikilia, lakini harudi tena.
19 Ndipo akapeleka mpanda farasi wa pili, naye akawafikilia, akasema, Mfalme asema hivi, Je! Ni amani? Yehu akasema, Wewe una nini na amani? Geuka unifuate.
20 Yule mlinzi akatoa habari, akasema, Amewafikilia wala harudi tena; na mwendo huu ni kama mwendo wa Yehu mwana wa Nimshi; maana analiendesha gari kwa kasi.
21 Yoramu akasema, Tandika gari. Wakalitandika gari lake. Yoramu mfalme wa Israeli akatoka, na Ahazia mfalme wa Yuda, kila mtu katika gari lake. Wakatoka ili kumlaki Yehu, wakamkuta katika kiwanja cha Nabothi, Myezreeli.
22 Ikawa, Yoramu alipomwona Yehu, akasema, Je! Ni amani, Yehu? Akajibu, Amani gani, maadamu uzinzi wa mama yako Yezebeli na uchawi wake ni mwingi?
23 Yoramu akageuza mikono yake, akakimbia, akamwambia Ahazia, Ni uhaini, Ahazia.
24 Yehu akavuta upinde wake kwa nguvu zake zote, akampiga Yoramu kati ya mikono yake, hata mshale ukamtoka penye moyo wake, akaanguka katika gari lake.
25 Ndipo Yehu akamwambia Bidkari, akida wake, Mtwae ukamtupe katika kiwanja cha Nabothi, Myezreeli; maana kumbuka, hapo mimi na wewe tulipokuwa tumepanda farasi zetu, na kumfuata Anabu baba yake, Bwana alimwekea mzigo huu, akasema;
26 Hakika, jana nimeiona damu ya Nabothi, na damu ya wanawe, asema Bwana; nami nitakulipa katika kiwanja hiki, asema Bwana. Basi sasa mtwae huyu ukamtupe katika kiwanja hicho, sawasawa na neno la Bwana.
27 Na Ahazia mfalme wa Yuda alipoona hayo, akakimbia kwa njia ya nyumba ya bustanini. Yehu akamfuatia, akasema, Mpigeni huyu naye katika gari lake; wakampiga hapo penye kupandia Guri, karibu na Ibleamu. Akakimbilia Megido, akafa huko.
28 Na watumishi wake wakamchukua garini mpaka Yerusalemu, wakamzika katika kaburi lake pamoja na baba zake katika mji wa Daudi.
29 Katika mwaka wa kumi na moja wa Yoramu mwana wa Ahabu, Ahazia alianza kutawala juu ya Yuda.
30 Hata Yehu alipofika Yezreeli, Yezebeli akapata habari; akatia uwanja machoni mwake, akapamba kichwa chake, akachungulia dirishani.
31 Hata Yehu alipoingia lango la mji, alisema, Je! Ni amani, Ewe Zimri, mwenye kumwua bwana wako?
32 Akainua uso wake kulielekea dirisha, akasema, Aliye upande wangu ni nani? Matowashi wawili watatu wakachungulia.
33 Akasema, Mtupeni chini. Basi wakamtupa chini; na damu yake ikamwagika nyingine juu ya ukuta, na nyingine juu ya farasi, naye akamkanyaga-kanyaga.
34 Alipoingia, akala, na kunywa; kisha akasema, Haya! Mwangalieni mwanamke huyu aliyelaaniwa, mkamzike; kwa maana ni binti mfalme.
35 Wakaenda ili kumzika; lakini hawakuona kitu ila kifuvu cha kichwa chake, na miguu yake, na vitanga vya mikono yake.
36 Basi wakarudi, wakampasha habari. Akasema, Hili ndilo neno la Bwana, alilolinena kwa kinywa cha mtumishi wake Eliya, Mtishbi, kusema, Katika kiwanja cha Yezreeli mbwa wataila nyama ya Yezebeli.
37 Na mzoga wa Yezebeli utakuwa kama mavi juu ya uso wa mashamba, katika kiwanja cha Yezreeli; hata wasipate kusema, Huyu ni Yezebeli.

2 Walfame 10


1 Basi Ahabu alikuwa na wana sabini katika Samaria. Yehu akaandika barua, akazipeleka Samaria kwa wakuu wa Yezreeli, yaani, wazee na hao walezi wa wana wa Ahabu, kusema,
2 Barua hii mara ikiwawasilia, kwa kuwa mna wana wa bwana wenu pamoja nanyi, tena kwenu kuna magari na farasi, na mji wenye boma, na silaha;
3 basi mtazameni yeye aliye mwema na hodari miongoni mwa wana wa bwana wenu, mkamweke kitini mwa babaye, mkaipiganie nyumba ya bwana wenu.
4 Lakini wao wakaogopa mno, wakasema, Tazama, wafalme wawili hawakusimama mbele yake; tupateje sisi kusimama?
5 Kisha yeye aliyekuwa juu ya nyumba, na yeye aliyekuwa juu ya mji, na wazee, na walezi, wakatuma ujumbe kwa Yehu, wakisema, Sisi tu watumwa wako, kila neno utakalotuambia, tutalifanya; hatutamfanya mtu awaye yote kuwa mfalme; ufanye yaliyo mema machoni pako.
6 Ndipo akawaandikia barua ya pili, kusema, Mkiwa upande wangu, na sauti yangu mkiisikia, vitwaeni vichwa vyao hao watu, wana wa bwana wenu, mkanijie kama wakati huu kesho hapa Yezreeli. Na hao wana wa mfalme, watu sabini, walikuwako kwa wakuu wa mji waliowalea.
7 Ikawa, barua ilipowawasilia, waliwatwaa hao wana wa mfalme, wakawaua, watu sabini, wakatia vichwa vyao katika makapu, wakampelekea huko Yezreeli.
8 Akaja mjumbe, akamwambia, akasema, Wamevileta vile vichwa vya wana wa mfalme. Akasema, Viwekeni chungu mbili penye maingilio ya lango hata asubuhi.
9 Ikawa asubuhi, akatoka, akasimama, akawaambia watu wote, Ninyi ni wenye haki; tazameni, mimi nalifanya fitina juu ya bwana wangu, nikamwua; ila ni nani aliyewapiga hawa wote?
10 Jueni basi ya kwamba halianguki chini lo lote la neno la Bwana, alilolinena Bwana juu ya nyumba ya Ahabu; kwa maana Bwana ameyafanya hayo aliyoyanena kwa kinywa cha mtumishi wake Eliya.
11 Hivyo Yehu akawapiga wote waliosalia wa nyumba ya Ahabu katika Yezreeli, na hao wakuu wake wote, na rafiki zake, na makuhani wake, hata hakumwachia aliyesalia hata mmoja.
12 Akaondoka, akashika njia akaenda Samaria. Hata njiani karibu na nyumba ya kukatia manyoya kondoo, ya wachungaji.
13 Yehu akakutana na ndugu za Ahazia mfalme wa Yuda, akawauliza, Ni nani ninyi? Wakamjibu, Sisi tu ndugu zake Ahazia; tunashuka kuwasalimu wana wa mfalme na wana wa malkia.
14 Akasema, Wakamateni wa hai. Wakawakamata wa hai, wakawaua penye birika ya nyumba ya kukatia manyoya kondoo, watu arobaini na wawili; wala hakumsaza mtu wao awaye yote.
15 Alipotoka huko akamkuta Yehonadabu mwana wa Rekabu akija kumlaki; akamsalimu akamwambia, Je! Moyo wako umenyoka, kama moyo wangu ulivyo pamoja na moyo wako? Akajibu Yehonadabu, Ndio. Yehu akamwambia, Kama ndio, nipe mkono wako. Akampa mkono, akamkalisha pamoja naye garini.
16 Akasema, Fuatana nami, ukaone wivu wangu kwa Bwana. Wakampandisha garini mwake.
17 Naye alipofika Samaria, aliwapiga wote waliomsalia Ahabu katika Samaria, hata akamwangamiza, sawasawa na neno la Bwana alilomwambia Eliya.
18 Yehu akawakusanya watu wote, akawaambia, Ahabu alimtumikia Baali kidogo; bali Yehu atamtumikia sana.
19 Basi niitieni manabii wote wa Baali, wote wamwabuduo, na makuhani wake wote; mtu asikose kuwapo hata mmoja. Maana ninayo dhabihu kubwa ya kumtolea Baali; ye yote atakayekosa kuwapo hataishi. Lakini Yehu alifanya hayo kwa hila, ili awaharibu waliomwabudu Baali.
20 Yehu akasema, Takaseni kusanyiko la dini kwa Baali. Wakalitangaza.
21 Yehu akatuma wajumbe katika Israeli yote, nao wote waliomwabudu Baali wakaja, wala hakusalia mtu ye yote asiyekuja. Wakaingia nyumbani mwa Baali; ikajaa nyumba ya Baali tangu mlango hata mlango.
22 Akamwambia yule aliyekuwa juu ya hazina ya mavazi, Uwatolee mavazi wote wanaomwabudu Baali. Akawatolea mavazi.
23 Akaingia Yehu na Yehonadabu mwana wa Rekabu nyumbani mwa Baali, akawaambia waliomwabudu Baali, Tafuteni mkaangalie, asiwepo hapa pamoja nanyi mtu amtumikiaye Bwana, ila wamwabuduo Baali peke yao.
24 Wakaingia ili watoe dhabihu na sadaka za kuteketezwa. Basi Yehu alikuwa amejiwekea nje watu themanini, akasema, Mtu mmoja akiokoka wa watu niliowatia mikononi mwenu, amwachaye huyo, roho yake itakuwa badala ya roho yake.
25 Ikawa mara alipokwisha kutoa sadaka ya kuteketezwa, Yehu akawaambia walinzi na maakida, Ingieni mwapige; mtu awaye yote asitoke. Basi wakawapiga kwa makali ya upanga; walinzi na maakida wakawatupa nje, wakaenda mpaka mji wa nyumba ya Baali.
26 Wakazitoa nguzo zilizokuwamo nyumbani mwa Baali, wakaziteketeza.
27 Wakaibomoa nguzo ya Baali, na kuiangusha nyumba ya Baali, wakaifanya choo hata leo.
28 Ndivyo Yehu alivyomharibu Baali katika Israeli.
29 Walakini katika makosa yake Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli, Yehu hakutoka katika kuyafuata, yaani, ndama za dhahabu zilizokuwako katika Betheli na Dani.
30 Bwana akamwambia Yehu, Kwa kuwa umetenda vema kwa kufanya vilivyo haki machoni pangu, kuitendea nyumba ya Ahabu sawasawa na yote yaliyomo moyoni mwangu, wana wako wa kizazi cha nne watakaa kitini mwa Israeli.
31 Lakini Yehu hakuangalia, aende katika sheria ya Bwana, Mungu wa Israeli, kwa moyo wake wote; hakutoka katika makosa ya Yeroboamu, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.
32 Siku zile Bwana akaanza kupunguza Israeli. Hazaeli akawapiga mipakani mwote mwa Israeli;
33 kutoka Yordani upande wa mashariki, nchi yote ya Gileadi, na ya Wagadi, na Wareubeni, na Wamanase, kutoka Aroeri iliopo karibu na bonde la Arnoni, yaani, Gileadi, na Bashani.
34 Basi mambo yote ya Yehu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
35 Yehu akalala na babaze; wakamzika katika Samaria. Na Yehoahazi mwanawe akatawala mahali pake.
36 Na muda Yehu aliotawala juu ya Israeli katika Samaria ulikuwa miaka ishirini na minane.

2 Walfame 11


1 Na Athalia, mama yake Ahazia, alipoona ya kuwa mwanawe amekufa, akainuka, akawaharibu wazao wote wa kifalme.
2 Ila Yehosheba, binti wa mfalme Yehoramu, umbu lake Ahazia ,akamtwaa Yoashi mwana wa Ahazia ,akamwiba miongoni mwa hao wana wa mfalme waliouawa ,yeye na mlezi wake ,na kuwatia katika chumba cha kulala;wakamficha usoni pa Athalia,basi kwa hiyo hakuuawa.
3 Alikuwako pamoja naye, amefichwa nyumbani mwa Bwana, miaka sita. Naye Athalia akaitawala nchi.
4 Hata mwaka wa saba Yehoyada akatuma, na kuwaleta wakuu wa mamia, wa Wakari, na wa walinzi, akawaleta kwake ndani ya nyumba ya Bwana; akapatana nao, akawaapisha nyumbani mwa Bwana, akawaonyesha huyo mwana wa mfalme.
5 Akawaamuru, akasema, Hili ndilo neno mtakalolifanya; theluthi yenu, mtakaoingia siku ya sabato, mtayalinda malinzi ya nyumba ya mfalme;
6 na theluthi mtakuwapo mlangoni pa Suri; na theluthi langoni nyuma ya walinzi; hivyo mtayalinda malinzi ya nyumba, kuzuia watu wasiingie.
7 Na sehemu mbili zenu, yaani, wote watokao siku ya sabato, mtayalinda malinzi ya nyumba ya Bwana kumzunguka mfalme.
8 Mtamzunguka mfalme pande zote, kila mtu mwenye silaha zake mkononi; naye awaye yote aingiaye ndani ya safu auawe; mkafuatane na mfalme, akitoka na akiingia.
9 Nao wakuu wa mamia wakafanya sawasawa na yote aliyowaamuru Yehoyada kuhani; wakawatwaa kila mtu watu wake, hao watakaoingia sabato, nao watakaotoka sabato, wakaja kwa Yehoyada kuhani.
10 Naye yule kuhani akawapa wakuu wa mamia mikuki na ngao zilizokuwa za mfalme Daudi, zilizokuwamo nyumbani mwa Bwana.
11 Walinzi wakasimama, kila mtu na silaha zake mkononi, kutoka pembe ya kuume ya nyumba mpaka pembe ya kushoto ya nyumba, kando ya madhabahu na nyumba, wakimzunguka mfalme pande zote.
12 Ndipo akamleta nje mwana wa mfalme, akamvika taji, na kumpa ushuhuda; wakamfanya mfalme, wakamtia mafuta; wakapiga makofi, wakasema, mfalme na aishi.
13 Na Athalia alipoisikia sauti ya walinzi na ya watu, aliingia kwa watu nyumbani kwa Bwana;
14 akatazama, na tazama, mfalme amesimama karibu na nguzo kama ilivyokuwa desturi, nao wakuu na wapiga baragumu karibu na mfalme; na watu wote wa nchi wakafurahi, wakapiga baragumu. Ndipo Athalia akararua mavazi yake, akalia, Fitina! Fitina!
15 Naye Yehoyada kuhani akawaamuru wakuu wa mamia, majemadari wa jeshi, akawaambia, Mtoeni kati ya safu; naye ye yote amfuataye mwueni kwa upanga. Kwani kuhani akasema, Asiuawe nyumbani mwa Bwana.
16 Basi wakampisha njia; akaenda kwa njia ya kuingia kwa farasi nyumbani mwa mfalme; akauawa huko.
17 Kisha, Yehoyada akafanya mapatano kati ya Bwana na mfalme na watu, ili wawe watu wa Bwana; tena kati ya mfalme na watu.
18 Watu wote wa nchi wakaiendea nyumba ya Baali, wakaiangusha; madhabahu zake na sanamu zake wakazivunja-vunja kabisa, na Matani kuhani wa Baali wakamwua mbele ya madhabahu. Na Yehoyada kuhani akaweka maakida juu ya nyumba ya Bwana.
19 Akawatwaa wakuu wa mamia, na Wakari, na walinzi, na watu wote wa nchi; wakamleta mfalme kushuka nyumbani mwa Bwana, wakaja kwa njia ya mlango wa walinzi mpaka nyumba ya mfalme. Naye akakaa katika kiti cha enzi cha wafalme.
20 Basi watu wote wa nchi wakafurahi, na mji ukatulia. Naye Athalia wakamwua kwa upanga karibu na nyumba ya mfalme.
21 Yoashi alikuwa na umri wa miaka saba alipoanza kutawala.

2 Walfame 12


1 Katika mwaka wa saba wa Yehu, Yoashi alianza kutawala; akatawala miaka arobaini huko Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Sibia wa Beer-sheba.
2 Yoashi akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana siku zake zote Yehoyada kuhani alizomfundisha.
3 Ila mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu.
4 Yoashi akawaambia makuhani, Fedha yote ya vitu vitakatifu iliyoletwa nyumbani mwa Bwana, fedha ya matumizi, fedha ya watu kadiri alivyoandikiwa kila mtu, na fedha yote iliyoletwa kama mtu ye yote aonavyo moyoni mwake kuileta nyumbani mwa Bwana,
5 makuhani na waitwae, kila mtu kwa hao awajuao; nao watatengeneza palipobomoka nyumbani, kila mahali palipoonekana pamebomoka.
6 Lakini ikawa, mwaka wa ishirini na tatu wa mfalme Yoashi, makuhani walikuwa hawajatengeneza mabomoko ya nyumba.
7 Ndipo mfalme Yoashi akamwita Yehoyada kuhani, na makuhani wengine, akawauliza, Mbona hamtengenezi mabomoko ya nyumba? Basi sasa msipokee tena fedha kwa hao mwajuao, lakini itoeni kwa ajili ya mabomoko ya nyumba.
8 Nao makuhani wakakubali kwamba wasipokee fedha kwa watu, wala wasitengeneze mabomoko ya nyumba.
9 Lakini Yehoyada kuhani akatwaa kasha, akatoboa tundu katika kifuniko chake, akaliweka karibu na madhabahu, upande wa kuume mtu aingiapo nyumbani mwa Bwana; na makuhani, waliolinda mlangoni, wakatia ndani yake fedha yote iliyoletwa nyumbani mwa Bwana.
10 Ikawa, walipoona ya kuwa fedha nyingi imo kashani, karani wa mfalme akapanda na kuhani mkuu, wakaifunga mifukoni, wakaihesabu fedha iliyoonekana nyumbani mwa Bwana.
11 Na fedha iliyopimwa wakawapa mikononi wale waliofanya kazi, walioisimamia nyumba ya Bwana; na hao wakawatolea maseremala na wajenzi walioifanya kazi katika nyumba ya Bwana,
12 na hao waashi, na wakata mawe, tena kununua miti na mawe ya kuchongwa, ili kuyatengeneza mabomoko ya nyumba ya Bwana, tena kwa gharama zote za kuitengeneza nyumba.
13 Lakini havikufanywa kwa nyumba ya Bwana vikombe vya fedha, wala makasi, wala mabakuli, wala panda, wala vyombo vyo vyote vya dhahabu, wala vyombo vya fedha, kwa hiyo fedha iliyoletwa nyumbani mwa Bwana;
14 kwa sababu hiyo fedha waliwapa watenda kazi, wakaitengeneza kwayo nyumba ya Bwana.
15 Walakini hawakufanya hesabu na hao watu, waliokabidhiwa fedha hiyo ili wawape watenda kazi; kwa kuwa walitenda kwa uaminifu.
16 Lakini fedha ya matoleo ya kosa, na fedha ya matoleo ya dhambi, haikuletwa nyumbani mwa Bwana; hiyo ilikuwa ya makuhani wenyewe.
17 Ndipo akakwea Hazaeli mfalme wa Shamu akapigana na Gathi, akautwaa; Hazaeli akaelekeza uso ili akwee kwenda Yerusalemu.
18 Yoashi mfalme wa Yuda akavitwaa vyote alivyoviweka wakfu Yehoshafati, na Yehoramu, na Ahazia, baba zake, wafalme wa Yuda, navyo vyote alivyoweka wakfu mwenyewe, na dhahabu yote iliyoonekana katika hazina za nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme, akamletea Hazaeli mfalme wa Shamu; basi akaenda zake kutoka Yerusalemu.
19 Basi mambo yote ya Yoashi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
20 Nao watumishi wake wakaondoka, wakafanya fitina, wakamwua Yoashi katika nyumba ya Milo, hapo panaposhukia Sila.
21 Kwa maana Yozakari mwana wa Shimeathi, na Yehozabadi mwana wa Shomeri, watumishi wake, wakampiga, naye akafa; wakamzika pamoja na babaze mjini mwa Daudi. Na Amazia mwanawe akatawala mahali pake.

2 Walfame 13


1 Katika mwaka wa ishirini na tatu wa Yoashi mwana wa Ahazia, mfalme wa Yuda, Yehoahazi mwana wa Yehu alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka kumi na saba.
2 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, akayafuata makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; wala hakuyaacha.
3 Hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, akawatia mkononi mwa Hazaeli mfalme wa Shamu, na mkononi mwa Ben-hadadi mwana wa Hazaeli, siku zote.
4 Naye Yehoahazi akamsihi Bwana, Bwana akamsikiliza; kwa kuwa aliyaona mateso ya Israeli, jinsi mfalme wa Shamu alivyowatesa.
5 (Bwana akawapa Israeli mwokozi, nao wakatoka mikononi mwa Washami; wana wa Israeli wakakaa hemani mwao kama zamani za kwanza.
6 Lakini hawakuyaacha makosa ya nyumba ya Yeroboamu, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli, lakini wakaendelea katika hayo; nayo ile Ashera ikakaa vivyo katika Samaria).
7 Kwa kuwa hakumwachia Yehoahazi watu ila wapandao farasi hamsini, na magari kumi, na askari elfu kumi waendao kwa miguu; kwa kuwa mfalme wa Shamu aliwaharibu, akawaponda mfano wa mavumbi yaliyokanyagwa.
8 Basi mambo yote ya Yehoahazi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
9 Yehoahazi akalala na babaze; wakamzika katika Samaria. Na Yehoashi mwanawe akatawala mahali pake.
10 Katika mwaka wa thelathini na saba wa Yoashi mfalme wa Yuda, Yehoashi mwana wa Yehoahazi alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria, akatawala miaka kumi na sita.
11 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli; lakini akaendelea katika hayo.
12 Basi mambo yote ya Yehoashi yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake aliopigania na Amazia mfalme wa Yuda, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
13 Yehoashi akalala na babaze; na Yeroboamu akakaa katika kiti chake cha enzi; naye Yehoashi akazikwa huko Samaria, pamoja na wafalme wa Israeli.
14 Basi Elisha alikuwa ameshikwa na ugonjwa wake uliomwua; naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatelemka amtazame, akamlilia mbele yake, akasema, Baba yangu! Baba yangu! Gari la Israeli na wapanda farasi wake!
15 Elisha akamwambia, Twaa uta na mishale; naye akatwaa uta na mishale.
16 Akamwambia mfalme wa Israeli, Weka mkono wako katika uta; naye akaweka mkono wake juu yake. Elisha akaweka mikono yake juu ya mikono ya mfalme.
17 Akasema, Lifungue dirisha linaloelekea mashariki; akalifungua. Basi Elisha akasema, Piga; akapiga. Akasema, Mshale wa Bwana wa kushinda, naam, mshale wa kushinda Shamu, kwa maana utawapiga Washami katika Afeki hata utakapowaangamiza.
18 Akasema, Itwae mishale; akaitwaa. Akamwambia mfalme wa Israeli, Piga chini; akaipiga nchi mara tatu, akaacha.
19 Yule mtu wa Mungu akamkasirikia, akasema, Ingalikupasa kupiga mara tano au mara sita; ndipo ungaliipiga Shamu hata kuiangamiza; bali sasa utaipiga Shamu mara tatu tu.
20 Elisha akafa, nao wakamzika. Basi vikosi vya Wamoabi wakaingia katika nchi mwanzo wa mwaka.
21 Ikawa, walipokuwa wakimzika mtu, angalia, waliona kikosi; wakamtupa yule mtu kaburini mwa Elisha; mara yule maiti alipoigusa mifupa ya Elisha, alifufuka, akasimama kwa miguu.
22 Na Hazaeli mfalme wa Shamu akawaonea Israeli siku zote za Yehoahazi.
23 Lakini Bwana akawahurumia, akawasikitikia, na kuwaangalia, kwa ajili ya agano lake na Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo, wala hakutaka kuwaangamiza, wala hakuwatupa usoni pake bado.
24 Akafa Hazaeli mfalme wa Shamu, na Ben-hadadi mwanawe akatawala mahali pake.
25 Naye Yehoashi, mwana wa Yehoahazi, akaitwaa tena mkononi mwa Ben-hadadi mwana wa Hazaeli miji ile aliyoitwaa yeye mkononi mwa Yehoahazi baba yake vitani. Mara tatu Yehoashi akamshinda, akairudisha miji ya Israeli.

2 Walfame 14


1 Katika mwaka wa pili wa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda alianza kutawala.
2 Naye alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na kenda katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Yehoadani wa Yerusalemu.
3 Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana, ila si kama babaye Daudi; akafanya kama yote aliyoyafanya baba yake Yoashi.
4 Walakini mahali pa juu hapakuondolewa; watu wakaendelea kutoa dhabihu na kufukiza uvumba katika mahali pa juu.
5 Ikawa, mara ufalme ulipokuwa imara mkononi mwake, aliwaua watumishi wale waliomwua mfalme baba yake;
6 ila hakuwaua watoto wa hao wauaji; kama ilivyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, kama alivyoamuru Bwana, akisema, Mababa wasife kwa makosa ya wana, wala wana wasife kwa makosa ya mababa; lakini kila mtu atakufa kwa kosa lake mwenyewe.
7 Akawaua Waedomi katika Bonde la Chumvi watu elfu kumi; akautwaa Sela vitani, akauita jina lake Yoktheeli hata leo.
8 Ndipo Amazia akatuma wajumbe kwa Yehoashi mwana wa Yehoahazi mwana wa Yehu, mfalme wa Israeli, akisema, Njoo, tutazamane uso kwa uso.
9 Naye Yehoashi mfalme wa Israeli akatuma kwa Amazia mfalme wa Yuda, akisema, Mbaruti uliokuwako Lebanoni ulituma kwa mwerezi uliokuwako Lebanoni, kusema, Umwoze mwanangu binti yako; kukapita hayawani aliyekuwako Lebanoni, akaukanyaga ule mbaruti.
10 Kweli umepiga Edomu, na moyo wako umekutukuza; ujisifu basi, ukae nyumbani mwako. Mbona unataka kujitia bure katika madhara, hata uanguke, wewe na Yuda pamoja nawe?
11 Lakini Amazia hakutaka kusikia. Basi Yehoashi mfalme wa Israeli akakwea; wakatazamana uso kwa uso, yeye na Amazia mfalme wa Yuda, huko Beth-shemeshi ulio wa Yuda.
12 Yuda wakashindwa mbele ya Israeli; wakakimbia kila mtu hemani kwake.
13 Yehoashi mfalme wa Israeli akamtwaa Amazia mfalme wa Yuda, mwanawe Yoashi mwana wa Ahazia, huko Beth-shemeshi, akaja Yerusalemu, akauvunja ukuta wa Yerusalemu toka lango la Efraimu hata lango la pembeni, mikono mia nne.
14 Akaitwaa dhahabu yote na fedha, na vyombo vyote vilivyoonekana katika nyumba ya Bwana, na katika hazina za nyumba ya mfalme, tena watu, kuwa amana; akarudi Samaria.
15 Basi mambo yote ya Yehoashi yaliyosalia, aliyoyafanya, na ushujaa wake, na jinsi alivyopigana na Amazia mfalme wa Yuda, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
16 Yehoashi akalala na baba zake, akazikwa katika Samaria pamoja na wafalme wa Israeli; na Yeroboamu mwanawe akatawala mahali pake.
17 Naye Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda akaishi baada ya kufa kwake Yehoashi mwana wa Yehoahazi mfalme wa Israeli miaka kumi na mitano.
18 Basi mambo yote ya Amazia yaliyosalia, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
19 Wakafanya fitina juu yake katika Yerusalemu, naye akakimbia mpaka Lakishi, lakini wakatuma watu kumfuata mpaka Lakishi, wakamwua huko.
20 Wakamleta juu ya farasi; naye akazikwa huko Yerusalemu pamoja na babaze katika mji wa Daudi.
21 Na watu wote wa Yuda wakamtwaa Uzia aliyekuwa mwenye umri wa miaka kumi na sita,wakamfanya awe mfalme mahali pa baba yake Amazia.
22 Huyo akajenga Elathi, akaurudisha kwa Yuda, baada ya kulala mfalme pamoja na babaze.
23 Katika mwaka wa kumi na tano wa Amazia mwana wa Yoashi mfalme wa Yuda Yeroboamu mwana wa Yehoashi mfalme wa Israeli alianza kutawala katika Samaria; akatawala miaka arobaini na mmoja.
24 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana; wala hakuyaacha makosa yote ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.
25 Yeye akaurudisha mpaka wa Israeli toka kuingia kwa Hamathi hata bahari ya Araba, sawasawa na neno la Bwana, Mungu wa Israeli, alilolinena kwa mkono wa mtumishi wake Yona mwana wa Amitai, nabii, aliyekuwa wa Gath-heferi.
26 Kwani Bwana akayaona mateso ya Israeli, kwamba yalikuwa machungu sana; maana hakukuwa na mfungwa wala asiyefungwa, wala msaidizi kwa ajili ya Israeli.
27 Wala Bwana hakusema ya kwamba atalifuta jina la Israeli litoke chini ya mbingu; lakini akawaokoa kwa mkono wa Yeroboamu mwana wa Yehoashi.
28 Basi mambo yote ya Yeroboamu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na ushujaa wake, na jinsi aliyvopigana, akawapatia tena Israeli Dameski na Hamathi, iliyokuwa kwanza ya Yuda, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
29 Yeroboamu akalala na babaze, yaani, na wafalme wa Israeli. Na Zekaria mwanawe akatawala mahali pake.

2 Walfame 15


1 Katika mwaka wa ishirini na saba wa Yeroboamu mfalme wa Israeli Uzia mwana wa Amazia mfalme wa Yuda alianza kutawala.
2 Alikuwa na umri wa miaka kumi na sita alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na miwili huko Yerusalemu. Na jina la mamaye aliitwa Yekolia wa Yerusalemu.
3 Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana, kama yote aliyoyafanya babaye Amazia.
4 Ila mahali pa juu hapakuondolewa, nao watu wakaendelea kutoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu.
5 Bwana akampiga mfalme, akawa na ukoma hata siku ya kufa kwake, akakaa katika nyumba ya pekee. Na Yothamu mwana wa mfalme alikuwa juu ya nyumba, akiwahukumu watu wa nchi.
6 Basi mambo yote ya Uzia yaliyosalia, nayo yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
7 Uzia akalala na babaze; wakamzika pamoja na babaze mjini mwa Daudi; na Yothamu mwanawe akatawala mahali pake.
8 Katika mwaka wa thelathini na nane wa Uzia mfalme wa Yuda Zekaria mwana wa Yeroboamu akatawala juu ya Israeli katika Samaria miezi sita.
9 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana kama walivyofanya babaze; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.
10 Na Shalumu mwana wa Yabeshi akafanya fitina juu yake, akampiga mbele ya watu, akamwua, akatawala mahali pake.
11 Basi mambo yote ya Zekaria yaliyosalia, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli.
12 Hilo ndilo neno la Bwana alilomwambia Yehu, akisema, Wana wako watakaa kitini mwa Israeli hata kizazi cha nne. Ikawa vivyo hivyo.
13 Huyo Shalumu mwana wa Yabeshi alianza kutawala katika mwaka wa thelathini na kenda wa Uzia mfalme wa Yuda; akatawala muda wa mwezi mmoja katika Samaria.
14 Menahemu mwana wa Gadi akapanda kutoka Tirza, akaja Samaria, akampiga Shalumu mwana wa Yabeshi huko Samaria, akamwua, akatawala mahali pake.
15 Basi mambo yote ya Shalumu yaliyosalia, na fitina aliyoifanya, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli.
16 Ndipo Menahemu akapiga Tifsa, na wote waliokuwamo, na mipaka yake, toka Tirza; kwa sababu hawakumfungulia, kwa hiyo akaupiga; nao wanawake wote waliokuwamo wenye mimba akawapasua.
17 Katika mwaka wa thelathini na kenda wa Uzia mfalme wa Yuda Menahemu mwana wa Gadi alianza kutawala juu ya Israeli, akatawala miaka kumi katika Samaria.
18 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana; hakuyaacha siku zake zote makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.
19 Akaja Pulu mfalme wa Ashuru juu ya nchi; naye Menahemu akampa Pulu talanta elfu za fedha, ili kwamba mkono wake uwe pamoja naye, na ufalme uwe imara mkononi mwake.
20 Na Menahemu akawatoza Israeli fedha hiyo, yaani, wakuu wote wenye mali, kila mtu shekeli hamsini za fedha, ili ampe huyo mfalme wa Ashuru. Basi mfalme wa Ashuru akarejea, wala hakukaa huko katika nchi.
21 Basi mambo yote ya Menahemu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli?
22 Menahemu akalala na babaze; na Pekahia mwanawe akatawala mahali pake.
23 Katika mwaka wa hamsini wa Uzia mfalme wa Yuda Pekahia mwana wa Menahemu alianza kutawala juu ya Israeli hatika Samaria; akatawala miaka miwili.
24 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.
25 Na Peka mwana wa Remalia, jemadari wake, akamfanyia fitina, akampiga huko Samaria, katika ngome ya nyumba ya mfalme, pamoja na Argobu na Arie; na pamoja naye walikuwako watu hamsini wa Wagileadi. Akamwua, akatawala mahali pake.
26 Basi mambo yote ya Pekahia yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli.
27 Katika mwaka wa hamsini na mbili wa Uzia mfalme wa Yuda Peka mwana wa Remalia alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka ishirini.
28 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana; hakuyaacha makosa ya Yeroboamu mwana wa Nebati, ambayo kwa hayo aliwakosesha Israeli.
29 Katika siku za Peka mfalme wa Israeli akaja Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akatwaa Iyoni, na Abel-beth-maaka, na Yanoa, na Kedeshi, na Hazori, na Gileadi, na Galilaya, nchi yote ya Naftali; akawahamisha hao watu mpaka Ashuru.
30 Na Hoshea mwana wa Ela akafanya fitina juu ya Peka mwana wa Remalia, akampiga, akamwua, akatawala mahali pake, katika mwaka wa ishirini wa Yothamu mwana wa Uzia.
31 Basi mambo yote ya Peka yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, tazama, yameandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Israeli.
32 Katika mwaka wa pili wa Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli Yothamu mwana wa Uzia mfalme wa Yuda alianza kutawala.
33 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Yerusha binti Sadoki.
34 Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana; akafanya kama yote aliyoyafanya Uzia baba yake.
35 Ila mahali pa juu hapakuondolewa; watu walikuwa wakitoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu. Ndiye aliyelijenga lango la juu la nyumba ya Bwana.
36 Basi mambo yote ya Yothamu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
37 Zamani hizo akaanza Bwana kumtuma juu ya Yuda Resini mfalme wa Shamu, na Peka mwana wa Remalia.
38 Yothamu akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi baba yake. Na Ahazi mwanawe akatawala mahali pake.

2 Walfame 16


1 Katika mwaka wa kumi na saba wa Peka mwana wa Remalia Ahazi mwana wa Yothamu mfalme wa Yuda alianza kutawala.
2 Alikuwa na umri wa miaka ishirini alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na sita katika Yerusalemu; wala hakufanya mema machoni pa Bwana Mungu wake, kama Daudi babaye.
3 Lakini aliiendea njia ya wafalme wa Israeli, hata akampitisha mwanawe motoni, sawasawa na machukizo ya mataifa Bwana aliowafukuza mbele ya wana wa Israeli.
4 Kisha akatoa sadaka na kufukiza uvumba katika mahali pa juu, na juu ya vilima, na chini ya kila mti mbichi.
5 Hapo ndipo akakwea Resini mfalme wa Shamu pamoja na Peka mwana wa Remalia mfalme wa Israeli juu ya Yerusalemu ili wapigane; wakamhusuru Ahazi, ila hawakuweza kumshinda.
6 Wakati huo Resini mfalme wa Shamu akawarudishia Washami Elathi, akawafukuza Wayahudi kutoka Elathi; nao Washami wakaja Elathi, wakakaa humo hata leo.
7 Basi Ahazi akatuma wajumbe kwa Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akasema, Mimi ni mtumishi, tena mwana wako; kwea, ukaniokoe mkononi mwa mfalme wa Shamu, na mkononi mwa mfalme wa Israeli, walioniinukia.
8 Ahazi akatwaa fedha na dhahabu iliyoonekana katika nyumba ya Bwana, na katika hazina za nyumba ya mfalme, akazipeleka kwa mfalme wa Ashuru kuwa zawadi.
9 Na huyo mfalme wa Ashuru akamsikia; mfalme wa Ashuru akapanda juu ya Dameski, akautwaa, akawahamisha watu wake mateka mpaka Kiri, akamwua Resini.
10 Naye mfalme Ahazi akaenda Dameski ili aonane na Tiglath-pileseri mfalme wa Ashuru, akaiona ile madhabahu iliyokuwako Dameski. Mfalme Ahazi akamletea Uria kuhani namna yake ile madhabahu, na cheo chake, kama ilivyokuwa kazi yake yote.
11 Naye Uria kuhani akajenga madhabahu; sawasawa na yote aliyomletea mfalme Ahazi kutoka Dameski; ndivyo alivyoifanya Uria kuhani iwe tayari atakaporudi mfalme Ahazi kutoka Dameski.
12 Na mfalme aliporudi kutoka Dameski, mfalme akaiona ile madhabahu; mfalme akakaribia madhabahuni, na kutoa sadaka juu yake.
13 Akaiteketeza sadaka yake ya kuteketezwa, na sadaka yake ya unga, akamimina sadaka yake ya kinywaji, akanyunyiza damu ya sadaka zake za amani, juu ya madhabahu.
14 Na ile madhabahu ya shaba iliyokuwako mbele za Bwana, akaileta kutoka mbele ya nyumba, kutoka kati ya madhabahu yake mwenyewe na nyumba ya Bwana, akaiweka upande wa kaskazini wa madhabahu yake.
15 Mfalme Ahazi akamwamuru Uria kuhani, akisema, Juu ya madhabahu hiyo kubwa uiteketeze sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi, na sadaka ya unga ya jioni, na sadaka ya mfalme ya kuteketezwa, na sadaka yake ya unga, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya watu wote wa nchi, na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji; ukanyunyize juu yake damu yote ya sadaka ya kuteketezwa, na damu yote ya dhabihu; bali madhabahu ya shaba itakuwa kwangu mimi ili niiulizie.
16 Akafanya hivyo Uria kuhani, sawasawa na yote aliyoyaamuru mfalme Ahazi.
17 Mfalme Ahazi akakata papi za matako, akaliondoa lile birika juu yake; akaitelemsha ile bahari itoke juu ya ng'ombe za shaba zilizokuwa chini yake, akaiweka juu ya sakafu ya mawe.
18 Na ukumbi wa sabato walioujenga katika hiyo nyumba, na mahali pa kuingia pake mfalme palipokuwapo nje, akavigeuza kuikabili nyumba ya Bwana, kwa sababu ya mfalme wa Ashuru.
19 Basi mambo yote ya Ahazi yaliyosalia, aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
20 Ahazi akalala na babaze, akazikwa pamoja na babaze katika mji wa Daudi; na Hezekia mwanawe akatawala mahali pake.

2 Walfame 17


1 Katika mwaka wa kumi na mbili wa Ahazi mfalme wa Yuda Hoshea mwana wa Ela alianza kutawala juu ya Israeli katika Samaria; akatawala miaka kenda.
2 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, ila si kama wafalme wa Israeli waliomtangulia.
3 Naye Shalmanesa mfalme wa Ashuru akakwea juu yake, Hoshea akawa mtumishi wake, akampa kodi.
4 Mfalme wa Ashuru akaona fitina katika huyo Hoshea; kwa maana alikuwa ametuma wajumbe kwa So, mfalme wa Misri, wala hakumletea kodi mfalme wa Ashuru, kama alivyofanya mwaka kwa mwaka; kwa hiyo mfalme wa Ashuru akamfunga, akamtia kifungoni.
5 Ndipo mfalme wa Ashuru akakwea katikati ya nchi yote, akaenda Samaria, akauhusuru miaka mitatu.
6 Katika mwaka wa kenda wa Hoshea, huyo mfalme wa Ashuru akautwaa Samaria, akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala na Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi.
7 Yalitukia hayo kwa sababu wana wa Israeli walikuwa wametenda dhambi juu ya Bwana, Mungu wao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri watoke chini ya mkono wa Farao mfalme wa Misri, wakawaacha miungu mingine.
8 Wakaziendea sheria za mataifa, ambao Bwana aliwafukuza mbele ya wana wa Israeli, na sheria za wafalme wa Israeli walizozifanya.
9 Tena, wana wa Israeli wakafanya kwa siri mambo yasiyokuwa mema juu ya Bwana, Mungu wao, wakajijengea mahali pa juu katika miji yao yote, kutoka mnara wa walinzi hata katika miji yenye boma.
10 Wakajisimamishia nguzo na maashera juu ya kila mlima mrefu, na chini ya kila mti wenye majani mabichi;
11 wakafukiza uvumba huko katika kila mahali pa juu, kama mataifa walivyofanya, ambao Bwana aliwafukuza mbele yao; wakaunda mambo mabaya, ili wamkasirishe Bwana;
12 wakatumikia sanamu, ambazo Bwana aliwakataza, akasema, Msitende jambo hili.
13 Pamoja na hayo Bwana aliwashuhudia Israeli, na Yuda, kwa kinywa cha kila nabii, na cha kila mwonaji, akisema, Geukeni, na kuziacha njia zenu mbaya, mkazishike amri zangu na hukumu zangu, sawasawa na ile sheria yote niliyowaamuru baba zenu, nikawapelekea kwa kinywa cha manabii watumishi wangu.
14 Walakini hawakutaka kusikia, bali walifanya shingo zao kuwa ngumu, kama shingo za baba zao, wasiomwamini Bwana, Mungu wao.
15 Wakazikataa sheria zake, na agano lake, alilolifanya na baba zao; na shuhuda zake alizowashuhudia; wakafuata ubatili, wakawa ubatili, nao wakaandamana na mataifa waliowazunguka, ambao Bwana alikuwa amewaagiza, wasitende kwa mfano wao.
16 Wakaziacha amri zote za Bwana, Mungu wao, wakajifanyizia sanamu za kusubu, yaani, ndama mbili, wakafanya na Ashera, wakaliabudu jeshi lote la mbinguni, wakamtumikia Baali.
17 Wakawapitisha watoto wao, waume na wake, motoni, wakapiga ramli, wakafanya uchawi, wakajiuza nafsi zao wapate kufanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, hata kumkasirisha.
18 Kwa hiyo Bwana akawaghadhibikia Israeli sana, akawahamisha mbali na uso wake; wala hapana aliyesalia ila kabila ya Yuda peke yake.
19 Hata na watu wa Yuda hawakuyashika maagizo ya Bwana, Mungu wao, lakini walikwenda katika amri za Israeli walizokuwa wamezifanya wenyewe.
20 Basi Bwana akakikataa kizazi chote cha Israeli, akawatesa, na kuwatia katika mikono ya watu wenye kuwateka nyara, hata alipokwisha kuwatupa, watoke machoni pake.
21 Maana aliwatenga mbali Israeli na nyumba ya Daudi; nao wakamfanya Yeroboamu mwana wa Nebati kuwa mfalme; Yeroboamu akawavuta Israeli wasimfuate Bwana, akawakosesha kosa kubwa.
22 Nao wana wa Israeli wakaendelea katika dhambi zote za Yeroboamu alizozifanya; hawakujiepusha nazo;
23 hata Bwana akawaondoa Waisraeli wasiwe mbele zake, kama vile alivyosema kwa kinywa cha watumishi wake wote, manabii. Basi Waisraeli walichukuliwa mateka kutoka nchi yao wenyewe, waende nchi ya Ashuru, hata leo.
24 Naye mfalme wa Ashuru akaleta watu kutoka Babeli, na Kutha, na Ava, na Hamathi, na Sefarvaimu, akawaweka katika miji ya Samaria badala ya wana wa Israeli; wakaumiliki Samaria, wakakaa katika miji yake.
25 Basi ikawa, wakati ule walipoanza kukaa huko, hawakumcha Bwana; kwa hiyo Bwana akapeleka simba kati yao, nao wakawaua baadhi yao.
26 Kwa hiyo wakamwambia mfalme wa Ashuru, wakasema, Wale wa mataifa uliowahamisha, na kuwaweka katika miji ya Samaria, hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi; kwa hiyo amepeleka simba kati yao, na tazama, wanawaua, kwa sababu hawaijui kawaida ya Mungu wa nchi.
27 Ndipo mfalme wa Ashuru akatoa amri, akasema, Mpelekeni mmojawapo wa makuhani, mliowachukua kutoka huko; aende akakae huko, akawafundishe kawaida ya Mungu wa nchi.
28 Basi mmoja wa makuhani waliochukuliwa kutoka Samaria akaenda akakaa katika Betheli, akawafundisha jinsi ilivyowapasa kumcha Bwana.
29 Lakini pamoja na hayo watu wa kila taifa wakajifanyia miungu yao wenyewe, wakaiweka katika nyumba za mahali pa juu, walipopafanya Wasamaria, kila taifa katika miji yao walimokaa.
30 Watu wa Babeli wakafanya Sukoth-benothi kuwa mungu wao, watu wa Kutha wakafanya Nergali, watu wa Hamathi wakafanya Ashima,
31 Waavi wakafanya Nibhazi na Tartaki; nao Wasefarvi wakawaunguza wana wao katika moto kwa Adrameleki na Anameleki, miungu ya Sefarvaimu.
32 Basi hivyo wakamcha Bwana, nao wakijifanyia wengine wao kuwa makuhani wa mahali pa juu, ambao waliwafanyia dhabihu katika nyumba za mahali pa juu.
33 Wakamcha Bwana, na kuitumikia miungu yao wenyewe, sawasawa na kawaida za mataifa ambao wao walihamishwa kutoka kwao.
34 Hata siku hii ya leo hufanya sawasawa na kawaida za kwanza; wala hawamwogopi Bwana, wala hawazifuati sheria zao, wala hukumu zao, wala ile torati, wala ile amri Bwana aliyowaamuru wana wa Yakobo, ambaye alimpa jina la Israeli;
35 hao ambao Bwana alifanya agano nao, akawaamuru, akasema, Msiche miungu mingine, wala kuisujudia, wala kuitumikia, wala kuitolea sadaka;
36 ila yeye Bwana, aliyewaleta kutoka nchi ya Misri kwa nguvu nyingi, na kwa mkono ulionyoshwa, yeye ndiye mtakayemcha, yeye ndiye mtakayemsujudia, yeye ndiye mtakayemtolea sadaka;
37 na sheria, na hukumu, na torati, na amri, alizowaandikia, hizo ndizo mtakazozishika na kuzifanya hata milele; wala msiche miungu mingine.
38 Na hilo agano nililofanya nanyi, msilisahau; wala msiche miungu mingine;
39 lakini Bwana, Mungu wenu, ndiye mtakayemcha; naye atawaokoa mikononi mwa adui zenu wote.
40 Walakini hawakusikia, bali wakafanya sawasawa na kawaida zao za kwanza.
41 Basi mataifa hawa wakamcha Bwana, tena wakaziabudu sanamu zao za kuchongwa; na wana wao vile vile, na wana wa wana wao; kama walivyofanya baba zao, wao nao hufanya vivyo hivyo hata leo.

2 Walfame 18


1 Ikawa katika mwaka wa tatu wa Hoshea, mwana wa Ela, mfalme wa Israeli, Hezekia, mwana wa Ahazi, mfalme wa Yuda, alianza kutawala.
2 Alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka ishirini na kenda katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Abiya, binti Zekaria.
3 Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana, mfano wa yote aliyoyafanya Daudi, baba yake.
4 Alipaondoa mahali pa juu, akazibomoa nguzo, akaikata hiyo Ashera; akaivunja vipande vipande ile nyoka ya shaba aliyoifanya Musa; maana hata siku zile wana wa Israeli walikuwa wakiifukizia uvumba; naye akaiita jina lake Nehushtani
5 Alimtumaini Bwana, Mungu wa Israeli; hata baada yake hapakuwa na mfano wake katika wafalme wote wa Yuda, wala katika hao waliomtangulia.
6 Maana alishikamana na Bwana, hakuacha kumfuata, bali alizishika amri zake Bwana alizomwamuru Musa.
7 Naye Bwana akawa pamoja naye, kila alikokwenda alifanikiwa; tena alimwasi mfalme wa Ashuru, wala hakumtumikia.
8 Akawapiga Wafilisti mpaka Gaza na mipaka yake, tangu mnara wa walinzi hata mji wenye boma.
9 Hata katika mwaka wa nne wa Hezekia, ndio mwaka wa saba wa Hoshea, mwana wa Ela, mfalme wa Israeli, Shalmanesa, mfalme wa Ashuru, akakwea ili kupigana na Samaria, akauhusuru.
10 Wakautwaa baada ya miaka mitatu; yaani, katika mwaka wa sita wa Hezekia, ndio mwaka wa kenda wa Hoshea, mfalme wa Israeli, ndipo Samaria ulipotwaliwa.
11 Mfalme wa Ashuru akawahamisha Israeli mpaka Ashuru, akawaweka katika Hala, na katika Habori, karibu na mto wa Gozani, na katika miji ya Wamedi;
12 kwa sababu hawakuitii sauti ya Bwana, Mungu wao, bali waliyahalifu maagano yake, mambo yote ambayo Musa mtumishi wa Bwana aliwaamuru, wasikubali kuyasikiliza, wala kuyatenda.
13 Ikawa katika mwaka wa kumi na nne wa kumiliki kwake mfalme Hezekia, Senakeribu, mfalme wa Ashuru, akapanda ili kupigana na miji yote ya Yuda yenye boma, akaitwaa.
14 Basi Hezekia, mfalme wa Yuda, akapeleka wajumbe waende Lakishi kwa mfalme wa Ashuru, kusema, Nimekosa; uniache ukarudi kwako; cho chote utakachoweka juu yangu, nitakichukua. Mfalme wa Ashuru akamtoza Hezekia, mfalme wa Yuda, talanta za fedha mia tatu, na talanta za dhahabu thelathini.
15 Hezekia akampa fedha yote iliyoonekana katika nyumba ya Bwana, na katika hazina za nyumba ya mfalme.
16 Wakati huo Hezekia aliiondoa dhahabu iliyokuwa juu ya milango ya hekalu la Bwana, na juu ya nguzo, ambazo Hezekia, mfalme wa Yuda, alikuwa amezitia dhahabu, akampa mfalme wa Ashuru.
17 Mfalme wa Ashuru akawatuma jemadari wake, na mkuu wa matowashi, na amiri wake toka Lakishi ,kwa mfalme Hezekia huko Yerusalemu, pamoja na jeshi kubwa. Nao wakakwea wakafika Yerusalemu. Na walipokwisha kufika , wakaja wakasimama karibu na mfereji wa birika la juu, lililo katika njia kuu ya kuuendea uwanda wa dobi.
18 Na walipokwisha kumwita mfalme, wakatokewa na Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe.
19 Yule amiri akawaambia ,haya mwambieni Hezekia,kusema ,Mfalme mkuu,mfalme wa Ashuru, asema hivi, Ni tumaini gani hili unalolitumainia?
20 Wewe wasema, lakini ni maneno yasiyo na maana, kwamba, Lipo shauri na zipo nguvu kwa vita hivi. Basi, unamtumaini nani hata ukaniasi mimi?
21 Sasa tazama, unaitumainia fimbo ya mwanzi huu uliopondeka, yaani, Misri, ambayo mtu akiitegemea, humwingia mkononi na kumchoma; ndivyo alivyo Farao, mfalme wa Misri, kwa wote wamtumainio.
22 Lakini mkiniambia, Tunamtumaini Bwana, Mungu wetu; je! Si yeye ambaye Hezekia ameondoa mahali pake pa juu, na madhabahu zake, akawaambia watu wa Yuda na Yerusalemu, Sujuduni mbele ya madhabahu hii hapa Yerusalemu?
23 Basi sasa, tafadhali mpe bwana wangu, mfalme wa Ashuru, dhamana, nami nitakupa farasi elfu mbili, ikiwa wewe kwa upande wako waweza kupandisha watu juu yao.
24 Wawezaje, basi, kurudisha nyuma uso wa akida mmoja wa watumishi walio wadogo wa bwana wangu, na kuitumainia Misri upewe magari na farasi?
25 Je! Nimepanda mimi, ili kupigana na mahali hapa na kupaangamiza, bila shauri la Bwana? Bwana ndiye aliyeniambia, Panda upigane na nchi hii na kuiangamiza.
26 Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, na Shebna, na Yoa, wakamwambia yule amiri, Tafadhali, sema na watumishi wako kwa lugha ya Kiashuri; maana tunaifahamu; wala usiseme nasi kwa lugha ya Kiyahudi, masikioni mwa hao watu walio ukutani.
27 Lakini yule amiri akawaambia, Je! Bwana wangu amenituma kwa bwana wako, na kwako wewe, niseme maneno haya? Je! Hakunituma kwa watu hawa walio ukutani, ili wale mavi yao wenyewe na kunywa mkojo wao pamoja nanyi?
28 Kisha yule amiri akasimama akalia kwa sauti kuu kwa lugha ya Kiyahudi, akasema, Lisikieni neno la mfalme mkuu, mfalme wa Ashuru.
29 Mfalme asema hivi, Hezekia asiwadanganye; kwa maana, hataweza kuwaokoa katika mkono wake.
30 Wala Hezekia asiwatumainishe katika Bwana, akisema, Hakika Bwana atatuokoa, wala mji huu hautatiwa mkononi mwa mfalme wa Ashuru.
31 Msimsikilize Hezekia; kwa sababu mfalme wa Ashuru asema hivi, Fanyeni suluhu na mimi, mkatoke mnijie; mkale kila mtu matunda ya mzabibu wake na matunda ya mtini wake, mkanywe kila mmoja maji ya birika lake mwenyewe;
32 hata nije nikawachukue mpaka nchi iliyo kama nchi yenu wenyewe, nchi ya nafaka na divai, nchi ya chakula na mashamba ya mizabibu, nchi ya mafuta ya mzeituni na asali, ili mpate kuishi, msife; wala msimsikilize Hezekia, awadanganyapo, akisema, Bwana atatuokoa.
33 Je! Yuko mungu mmoja wa mataifa aliyewaokoa watu wake wakati wo wote na mkono wa mfalme wa Ashuru?
34 Iko wapi miungu ya Hamathi, na ya Arpadi? Iko wapi miungu ya Sefarvaimu, na ya Hena, na ya Iva? Je! Imeuokoa Samaria na mkono wangu?
35 Katika miungu ya nchi hizi zote, ni miungu gani iliyookoa nchi yao na mkono wangu, hata Bwana auokoe Yerusalemu na mkono wangu?
36 Lakini hao watu wakanyamaza kimya; wala hawakumjibu hata neno moja; maana amri ya mfalme ilikuwa kwamba, Msimjibu neno.
37 Ndipo Eliakimu, mwana wa Hilkia, aliyekuwa msimamizi wa nyumba ya mfalme, na Shebna, mwandishi, na Yoa, mwana wa Asafu, mwenye kuandika tarehe, wakaenda kwa Hezekia, na nguo zao zimeraruliwa, wakamwambia maneno ya yule amiri.

2 Walfame 19


1 Ikawa mfalme Hezekia aliposikia hayo, alizirarua nguo zake, akajivika nguo za magunia, akaingia katika nyumba ya Bwana.
2 Akamtuma Eliakimu aliyekuwa msimamizi wa nyumba yake na Shebna, mwandishi, na wazee wa makuhani, wamevikwa nguo za magunia, waende kwa Isaya nabii, mwana wa Amozi.
3 Wakamwambia, Hezekia asema hivi, Siku hii ni siku ya dhiki, na aibu, na matukano; maana watoto wa tayari kuzaliwa, wala hapana nguvu za kuwazaa.
4 Yamkini Bwana, Mungu wako, atayasikia maneno yote ya amiri huyu, ambaye mfalme wa Ashuru ,bwana wake,amemtuma ili amtukane Mungu aliye hai,naye atayakemea hayo maneno aliyoyasikia BWANA ,Mungu wako;kwa sababu hii inua dua yako kwa ajili ya mabaki yaliyobakia.
5 Basi watumishi wa mfalme Hezekia wakamwendea Isaya.
6 Isaya akawaambia, Mwambieni bwana wenu maneno haya; Bwana asema hivi, Usiyaogope maneno hayo uliyoyasikia, ambayo watumishi wa mfalme wa Ashuru wamenitukana.
7 Tazama, nitatia roho ya hofu ndani yake, naye atasikia kivumi, na kuirudia nchi yake mwenyewe; nami nitamwangusha kwa upanga katika nchi yake mwenyewe.
8 Basi yule amiri akarudi, akamkuta mfalme wa Ashuru, anapigana na Libna; maana alikuwa amesikia ya kwamba ameondoka, akaacha Lakishi.
9 Na aliposikia habari ya Tirhaka mfalme wa Kushi, ya kwamba, Tazama, ametoka ili kupigana nawe; alituma wajumbe kwa Hezekia mara ya pili, kusema,
10 Mwambieni Hezekia, mfalme wa Yuda, maneno haya, mkisema, Asikudanganye Mungu wako unayemtumaini, akisema, Yerusalemu hautatiwa katika mikono ya mfalme wa Ashuru.
11 Tazama, umesikia ni mambo gani wafalme wa Ashuru waliyozitenda nchi zote, kwa kuziangamiza kabisa; je! Utaokoka wewe?
12 Je! Miungu ya mataifa wale, ambao baba zangu waliwaangamiza, imewaokoa? Yaani, Gozani, na Harani, na Resefu, na wana wa Adini waliokuwa katika Telasari?
13 Yuko wapi mfalme wa Hamathi, na mfalme wa Arpadi, na mfalme wa mji wa Sefarvaimu, na wa Hena, na wa Iva?
14 Basi Hezekia akaupokea waraka katika mikono ya wale wajumbe, akausoma; kisha Hezekia akapanda, akaingia katika nyumba ya Bwana, akaukunjua mbele za Bwana.
15 Naye Hezekia akaomba mbele za Bwana, akasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, ukaaye juu ya makerubi, wewe, naam, wewe peke yako, ndiwe Mungu wa falme zote za dunia; wewe ndiwe uliyeziumba mbingu na nchi.
16 Tega sikio lako, Ee Bwana, usikie; fumbua macho yako, Ee Bwana, uone; uyasikie maneno ya Senakeribu, ambayo amemtuma mtu aje nayo ili kumtukana Mungu aliye hai.
17 Ni kweli, Bwana, wafalme wa Ashuru wamewaharibu mataifa na nchi zao,
18 na kuitupa miungu yao motoni; kwa maana haikuwa miungu, bali ni kazi ya mikono ya wanadamu; ilikuwa miti na mawe tu, ndiyo sababu wakaiharibu.
19 Basi sasa, Ee Bwana, Mungu wetu, utuokoe na mkono wake, nakusihi, ili kwamba falme zote za dunia zipate kujua ya kuwa wewe ndiwe Bwana Mungu, wewe peke yako.
20 Ndipo Isaya, mwana wa Amozi, akapeleka ujumbe kwa Hezekia, akisema, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa kuwa umeniomba juu ya Senakeribu, mfalme wa Ashuru, mimi nimekusikia.
21 Tamko alilolitamka Bwana katika habari zake ndilo hili, Bikira, binti Sayuni, amekudharau, na kukudhihaki sana; binti Yerusalemu ametikisa kichwa chake juu yako.
22 Ni nani uliyemshutumu na kumtukana? Umeinua sauti yako juu ya nani, na kuinua macho yako juu? Juu ya Mtakatifu wa Israeli.
23 Kwa vinywa vya wajumbe wako umemshutumu Bwana, ukasema, Kwa wingi wa magari yangu nimepanda juu ya vilele vya milima, mpaka mahali pa ndani pa Lebanoni. Nami nitaikata mierezi yake mirefu, na misunobari yake mizuri; nami nitaingia ndani ya makazi yake yaliyo mbali sana, na msitu wa shamba lake lizaalo sana.
24 Nimechimba na kunywa maji mageni, na kwa nyayo za miguu yangu nitaikausha mito yote ya Misri.
25 Je! Hukusikia wewe ya kuwa mimi ndimi niliyeyatenda hayo tokea zamani, na kuyafanya tokea siku za kale? Sasa mimi nimelitimiza jambo hili, iwe kazi yako kuangamiza miji yenye boma, hata ikawe chungu na magofu.
26 Ndiyo sababu wenyeji wao walikuwa na nguvu chache, wakafadhaika, na kuhangaika; wakawa kama majani ya mashamba, kama miche mibichi, kama majani juu ya dari, na kama ngano iliyokaushwa kabla haijaiva.
27 Lakini nakujua, kuketi kwako, na kutoka kwako, na kuingia kwako; na ghadhabu yako unayonighadhibikia.
28 Kwa sababu ya kunighadhibikia kwako, na kwa sababu kutakabari kwako kumefika masikioni mwangu; kwa sababu hiyo nitatia kulabu yangu puani mwako, na hatamu yangu midomoni mwako, nami nitakurudisha nyuma kwa njia ile ile uliyoijia.
29 Na kwako wewe hii ndiyo dalili; mwaka huu mtakula vitu viotavyo vyenyewe; na mwaka wa pili mtakula mazao ya vitu hivyo; na mwaka wa tatu pandeni mbegu, kavuneni; mkapande mashamba ya mizabibu, mkale matunda yake.
30 Na mabaki yaliyookoka ya nyumba ya Yuda yatatia mizizi chini, na kuzaa matunda juu.
31 Maana mabaki yatatoka katika Yerusalemu, na wao watakaookoka katika mlima wa Sayuni wivu wa Bwana utatimiza jambo hilo.
32 Basi Bwana asema hivi katika habari za mfalme wa Ashuru, Yeye hatauingia mji huu, wala hatapiga mshale hapa, wala hatakuja mbele yake kwa ngao, wala hatajenga boma juu yake.
33 Njia ile ile aliyojia, kwa njia iyo hiyo atarudi zake, wala hataingia ndani ya mji huu, asema Bwana.
34 Maana nitaulinda mji huu, niuokoe, kwa ajili yangu mwenyewe, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu.
35 Ikawa usiku uo huo malaika wa Bwana alitoka, akakiingia kituo cha Waashuri, akawapiga watu mia na themanini na tano elfu. Na watu walipoondoka asubuhi na mapema, kumbe! Hao walikuwa maiti wote pia.
36 Basi Senakeribu mfalme wa Ashuru akaondoka, akaenda zake, akarudi akakaa Ninawi.
37 Ikawa, alipokuwa akiabudu nyumbani mwa Nisroki, mungu wake, Adrameleki na Shareza wakampiga kwa upanga; wakaikimbilia nchi ya Ararati. Na Esar-hadoni mwanawe akatawala mahali pake.

2 Walfame 20


1 Siku hizo Hezekia akaugua, akawa katika hatari ya kufa. Isaya, nabii, mwana wa Amozi, akamjia akamwambia, Bwana asema hivi, Tengeza mambo ya nyumba yako; maana utakufa, wala hutapona.
2 Basi Hezekia akajigeuza, akaelekeza uso wake ukutani, akamwomba Bwana akasema,
3 Nakusihi, Bwana, ukumbuke sasa, jinsi nilivyokwenda mbele zako katika kweli na kwa moyo mkamilifu, na kutenda yaliyo mema machoni pako. Hezekia akalia sana sana.
4 Ikawa, kabla Isaya hajatoka katika mji wa kati, neno la Bwana likamjia, kusema,
5 Rudi, ukamwambie Hezekia, mkuu wa watu wangu, Bwana, Mungu wa Daudi baba yako asema hivi, Nimeyasikia maombi yako, na kuyaona machozi yako; tazama, nitakuponya; siku ya tatu utapanda nyumbani kwa Bwana.
6 Tena, nitazizidisha siku zako, kiasi cha miaka kumi na mitano, nami nitakuokoa wewe, na mji huu, na mkono wa mfalme wa Ashuru, nami nitaulinda mji huu kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Daudi, mtumishi wangu.
7 Naye Isaya akasema, Twaeni mkate wa tini. Wakautwaa, wakauweka juu ya jipu, naye akapona.
8 Hezekia akamwambia Isaya, Je! Kutakuwa na ishara gani ya kwamba Bwana ataniponya, nami siku ya tatu nitapanda nyumbani kwa Bwana.
9 Isaya akamwambia, Jambo hili litakuwa ishara kwako, itokayo kwa Bwana, ya kwamba Bwana atalifanya neno hilo alilolinena; je! Kivuli kiendelee madaraja kumi, au kirudi nyuma madaraja kumi?
10 Hezekia akajibu, Ni jambo jepesi kivuli kuendelea madaraja kumi; la, hicho kivuli na kirudi nyuma madaraja kumi.
11 Isaya nabii akamlilia Bwana; akakirudisha nyuma kile kivuli madaraja kumi, ambayo kilikuwa kimeshuka katika madaraja ya Ahazi.
12 Wakati huo Merodak-baladani mwana wa Baladani, Mfalme wa Babeli, alipeleka barua na zawadi kwa Hezekia; kwa maana alipata habari kwamba Hezekia ameugua.
13 Hezekia akawasikiliza, akawaonyesha nyumba yote yenye vitu vyake vya thamani, fedha, na dhahabu, na manukato, na marhamu ya thamani, na nyumba yenye silaha zake, na vitu vyote vilivyoonekana katika hazina zake. Wala hapakuwa na kitu asichowaonyesha Hezekia, katika nyumba yake, wala katika ufalme wake wote.
14 Ndipo Isaya nabii akamwendea mfalme Hezekia, akamwambia, Wasemaje watu hawa? Nao wametoka wapi kuja kwako? Hezekia akasema, Wametoka katika nchi iliyo mbali, yaani Babeli.
15 Ndipo akasema, Wameona nini nyumbani mwako? Hezekia akajibu, Vitu vyote vilivyomo nyumbani mwangu wameviona; hapana kitu nisichowaonyesha katika hazina zangu.
16 Isaya akamwambia Hezekia, Basi, lisikie neno la Bwana,
17 Angalia, siku zinakuja, ambazo vitu vyote vilivyomo nyumbani mwako, na hivyo vilivyowekwa akiba na baba zako hata leo, vitachukuliwa mpaka Babeli; hakitasalia kitu, asema Bwana.
18 Na baadhi ya wanao watakaotoka kwako, utakaowazaa, watawachukulia mbali; nao watakuwa matowashi jumbani mwake mfalme wa Babeli.
19 Ndipo Hezekia akamwambia Isaya, Neno la Bwana ulilolinena ni jema. Tena akasema, Je! Sivyo, ikiwapo amani na kweli katika siku zangu?
20 Basi mambo yote ya Hezekia yaliyosalia, na ushujaa wake wote, tena alivyolifanya birika na mfereji, akaleta maji ndani ya mji, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
21 Hezekia akalala na baba zake; na Manase mwanawe akatawala mahali pake.

2 Walfame 21


1 Manase alikuwa na umri wa miaka kumi na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka hamsini na mitano katika Yerusalemu, na jina la mamaye aliitwa Hefziba.
2 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na machukizo ya mataifa, aliowafukuza Bwana mbele ya wana wa Israeli.
3 Kwa maana akapajenga tena mahali pa juu alipopaharibu Hezekia baba yake; akamjengea Baali madhabahu, akafanya Ashera kama alivyofanya Ahabu mfalme wa Israeli. Akajiinama mbele ya jeshi lote la mbinguni na kulitumikia.
4 Akazijenga madhabahu ndani ya nyumba ya Bwana, napo ndipo alipopanena Bwana, Katika Yerusalemu nitaliweka jina langu.
5 Akajenga madhabahu kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni katika behewa mbili za nyumba ya Bwana.
6 Akampitisha mwanawe motoni, akatazama bao, akafanya uganga, akajishughulisha na hao wenye pepo wa utambuzi, na wachawi; akafanya mabaya mengi machoni pa Bwana, hata kumkasirisha.
7 Akaiweka sanamu ya kuchongwa ya Ashera aliyoifanya ndani ya nyumba, ambayo Bwana alimwambia Daudi, na Sulemani mwanawe, Katika nyumba hii, na katika Yerusalemu, niliouchagua miongoni mwa kabila zote za Israeli, nitaliweka jina langu milele;
8 wala sitawapotosha Israeli miguu watoke katika nchi niliyowapa baba zao; wakiangalia tu na kufanya sawasawa na yote niliyowaamuru, na kwa kuishika torati yote aliyowaamuru mtumishi wangu Musa.
9 Walakini hawakusikia; naye Manase akawakosesha wafanye mabaya, kuliko mataifa Bwana aliowaharibu mbele za wana wa Israeli.
10 Bwana akanena kwa watumishi wake manabii, akisema,
11 Kwa sababu Manase mfalme wa Yuda amefanya machukizo haya, na kutenda vibaya kuliko yote waliyoyatenda Waamori, waliokuwa kabla yake, naye akawakosesha Yuda kwa sanamu zake;
12 kwa sababu hiyo Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Angalia, naleta mabaya juu ya Yerusalemu na juu ya Yuda, hata kila mtu asikiaye, masikio yake yatawasha yote mawili.
13 Nami nitanyosha juu ya Yerusalemu kamba ya Samaria, na timazi ya nyumba ya Ahabu; nami nitaifuta Yerusalemu, kama mtu afutavyo sahani, kuifuta na kuifudikiza.
14 Nami nitawatupa mabaki ya urithi wangu, na kuwatia mikononi mwa adui zao; nao watakuwa nyara na mateka kwa adui zao wote;
15 kwa sababu wametenda yaliyo mabaya machoni pangu, na kunikasirisha, tangu siku ile walipotoka baba zao katika Misri, hata leo hivi.
16 Na Manase akazimwaga damu zisizo na hatia, nyingi sana, hata alipokuwa ameijaza Yerusalemu tangu upande huu hata upande huu; zaidi ya kosa lake alilowakosesha Yuda, kutenda yaliyo mabaya machoni pa Bwana.
17 Basi mambo yote ya Manase yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, na kosa lake alilolikosa, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
18 Manase akalala na babaze, akazikwa katika bustani ya nyumba yake mwenyewe, yaani, bustani ya Uza. Na Amoni mwanawe akatawala mahali pake.
19 Amoni alikuwa na umri wa miaka ishirini na miwili alipoanza kutawala; akatawala miaka miwili huko Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Meshulemethi, binti Haruzi wa Yotba.
20 Akafanya yaliyo maovu machoni pa Bwana, kama Manase babaye alivyofanya.
21 Akaiendea njia yote aliyoiendea baba yake, akazitumikia sanamu alizozitumikia baba yake, akaziabudu.
22 Akamwacha Bwana, Mungu wa babaze, wala hakuiendea njia ya Bwana.
23 Nao watumishi wa Amoni wakafanya fitina juu yake, wakamwua mfalme ndani ya nyumba yake mwenyewe.
24 Lakini watu wa nchi wakawaua wote waliofanya fitina juu yake mfalme Amoni, watu wa nchi wakamfanya Yosia mwanawe awe mfalme mahali pake.
25 Basi mambo yote ya Amoni yaliyosalia, aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
26 Akazikwa kaburini mwake katika bustani ya Uza. Na Yosia mwanawe akatawala mahali pake.

2 Walfame 22


1 Yosia alikuwa na umri wa miaka minane alipoanza kutawala; akatawala miaka thelathini na mmoja katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Yedida, binti Adaya wa Bozkathi.
2 Akafanya yaliyo mema machoni pa Bwana, akaenda katika njia yote ya Daudi baba yake, wala hakugeuka upande wa kuume wala wa kushoto.
3 Ikawa, katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia, mfalme akamtuma Shafani, mwana wa Azalia, mwana wa Meshulamu, mwandishi, nyumbani kwa Bwana, akisema,
4 Enenda kwa Hilkia, kuhani mkuu, ili aihesabu fedha yote inayoletwa nyumbani mwa Bwana, ambayo mabawabu wameipokea kwa watu;
5 tena waitie ile fedha katika mikono ya wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya Bwana; wakapewe wafanya kazi waliomo ndani ya nyumba ya Bwana, ili wapate kupatengeneza mahali palipobomoka ndani ya nyumba;
6 wapewe maseremala, na wajenzi, na waashi; ili kununua miti na mawe yaliyochongwa wapate kuitengeneza nyumba.
7 Lakini hawakuulizwa habari za ile fedha waliyokabidhiwa; maana walitenda kazi kwa uaminifu.
8 Naye Hilkia, kuhani mkuu, akamwambia Shafani, mwandishi, Nimekiona kitabu cha torati katika nyumba ya Bwana. Hilkia akampa Shafani kile kitabu, naye akakisoma.
9 Shafani mwandishi akamwendea mfalme, akamletea mfalme habari tena, akasema, Watumishi wako wamezitoa zile fedha zilizoonekana ndani ya nyumba, nao wamewakabidhi wafanya kazi wanaoisimamia nyumba ya Bwana.
10 Kisha Shafani mwandishi akamwambia mfalme, akasema, Hilkia kuhani amenipa kitabu. Shafani akakisoma mbele ya mfalme.
11 Ikawa, mfalme alipokwisha kuyasikia maneno ya kitabu hicho cha torati, alirarua nguo zake.
12 Mfalme akamwamuru Hilkia kuhani, na Ahikamu, mwana wa Shafani, na Akbori, mwana wa Mikaya, na Shafani mwandishi, na Asaya, mtumishi wa mfalme akasema,
13 Enendeni, mkamwulize Bwana kwa ajili yangu, na kwa ajili ya watu hawa, na kwa ajili ya Yuda yote, katika habari za maneno ya kitabu hiki kilichoonekana; kwa kuwa hasira ya Bwana ni kubwa aliyotukasirikia, kwa sababu baba zetu hawakuyaangalia maneno ya kitabu hiki, kufanya kama hayo yote tuliyoandikiwa.
14 Basi Hilkia kuhani, na Ahikamu, na Akbori, na Shafani, na Asaya, wakamwendea Hulda, nabii mke, mkewe Shalumu, mwana wa Tikva, mwana wa Harhasi, mtunza mavazi ya mfalme; (naye alikaa Yerusalemu katika mtaa wa pili;) wakasema naye.
15 Akawaambia, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi; Mwambieni mtu yule aliyewatuma ninyi kwangu,
16 Bwana asema hivi, Tazama, mimi nitaleta uovu juu ya mahali hapa, na juu yao wakaao hapa, naam, maneno yote ya kitabu alichokisoma mfalme wa Yuda;
17 kwa sababu wameniacha mimi, wameifukizia uvumba miungu mingine, ili wapate kunikasirisha kwa kazi yote ya mikono yao; kwa hiyo hasira yangu itawaka juu ya mahali hapa, isizimike.
18 Lakini yule mfalme wa Yuda, aliyewatuma ninyi kumwuliza Bwana, mtamwambia hivi, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Kwa habari ya maneno yale uliyoyasikia,
19 kwa kuwa moyo wako ulikuwa mwororo, nawe ukajinyenyekesha mbele za Bwana, hapo ulipoyasikia maneno niliyoyanena juu ya mahali hapa, na juu ya wenyeji wake, ya kwamba watakuwa ukiwa na laana, nawe ulizirarua nguo zako, ukalia mbele zangu; basi, mimi nami nimekusikia wewe, asema Bwana.
20 Kwa hiyo tazama, nitakukusanya pamoja na baba zako, nawe utawekwa kaburini mwako kwa amani; wala macho yako hayatauona uovu huo wote nitakaouleta juu ya mahali hapa. Basi wakamletea mfalme habari tena.

2 Walfame 23


1 Kisha, mfalme akatuma wajumbe, nao wakamkusanyia wazee wote wa Yuda na wa Yerusalemu.
2 Mfalme akapanda kwenda nyumbani kwa Bwana, na watu wote wa Yuda, nao wote waliokaa Yerusalemu, pamoja naye, na makuhani, na manabii, na watu wote, wadogo kwa wakubwa; akasoma masikioni mwao maneno yote ya kitabu cha agano kilichoonekana katika nyumba ya Bwana.
3 Mfalme akasimama karibu na nguzo, akafanya agano mbele za Bwana, kumfuata Bwana, na kuyashika maagizo yake, na shuhuda zake, na amri zake, kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kuyathibitisha maneno ya agano hilo yaliyoandikwa katika kitabu hicho; nao watu wote wakalikubali agano lile.
4 Kisha, mfalme akamwamuru Hilkia, kuhani mkuu, na makuhani wa daraja ya pili, na walinzi wa mlango, kwamba watoe katika hekalu la Bwana vyombo vyote vilivyofanywa kwa ajili ya Baali, na kwa ajili ya Ashera, na kwa ajili ya jeshi lote la mbinguni; akavipiga moto nje ya Yerusalemu, katika mashamba ya Ridroni, akayachukua majivu yake mpaka Betheli.
5 Akawaondosha wale makuhuni walioabudu sanamu, ambao wafalme wa Yuda waliwaweka ili kufukiza uvumba katika mahali pa juu, ndani ya miji ya Yuda, na katika kila mahali, pande zote za Yerusalemu; na hao pia waliomfukizia uvumba Baali, na jua, na mwezi, na sayari, na jeshi lote la mbinguni.
6 Naye akaiondoa Ashera katika nyumba ya Bwana, nje ya Yerusalemu, mpaka Kidroni, akaipiga moto penye kijito cha Kidroni, na kuiponda-ponda iwe mavumbi, akayatupa mavumbi yake juu ya makaburi ya watu.
7 Akaziangusha nyumba za mahanithi, waliokuwamo nyumbani mwa Bwana, wanawake walipofuma mapazia ya Ashera.
8 Akawatoa makuhani wote katika miji ya Yuda, akapanajisi mahali pa juu, makuhani walipokuwa wamefukiza uvumba, tangu Geba hata Beer-sheba; akapavunja mahali pa juu pa malango, palipokuwapo penye kuingia lango la Yoshua, liwali wa mji, palipokuwa upande wa kushoto wa mtu langoni pa mji.
9 Walakini hao makuhani wa mahali pa juu hawakupanda madhabahuni kwa Bwana katika Yerusalemu, bali wakala mikate isiyo na chachu katikati ya ndugu zao.
10 Naye akainajisi Tofethi, iliyomo katika bonde la wana wa Hinomu, ili mtu asipitishe mwana wake au binti yake motoni kwa Moleki.
11 Akawaondoa farasi ambao wafalme wa Yuda waliwatoa kwa jua, hapo pa kuingia nyumbani mwa Bwana, karibu na chumba cha Nathan-Meleki, towashi, kilichohuwako kiungani; akayapiga moto magari ya jua.
12 Nazo madhabahu zilizokuwako darini juu ya chumba cha juu cha Ahazi, wafalme wa Yuda walizozifanya, nazo madhabahu alizozifanya Manase katika behewa mbili za nyumba ya Bwana, mfalme akazivunja, akazitelemsha huko nje, na kuyatupa mavumbi yake katika kijito cha Kidroni.
13 Na mahali pa juu palipokuwapo mbele ya Yerusalemu, palipokuwa upande wa kuume wa mlima wa uharibifu, alipopajenga Sulemani, mfalme wa Israeli, kwa Ashtorethi, chukizo la Wasidoni, na Kemoshi, chukizo la Moabu, na Milkomu, chukizo la wana wa Amoni, mfalme akapanajisi.
14 Akazivunja-vunja nguzo, akayakata-kata maashera, akapajaza mahali pake mifupa ya watu.
15 Tena zaidi ya hayo, ile madhabahu iliyokuwako Betheli, na mahali pa juu alipopafanya Yeroboamu, mwana wa Nebati, aliyewakosesha Israeli, madhabahu hiyo aliibomoa; na mahali pa juu alipateketeza, akapaponda-ponda hata pakawa mavumbi, akaiteketeza ile Ashera.
16 Naye Yosia alipogeuka, aliyaona makaburi yale yaliyokuwako huko, juu ya mlima; akatuma watu, akaitoa ile mifupa katika yale makaburi, akaiteketeza juu ya madhabahu, akainajisi, sawasawa na lile neno la Bwana, alilolinena yule mtu wa Mungu, aliyetamka mambo hayo.
17 Kisha akasema, Ni kumbukumbu la nani, hili ninaloliona? Na watu wa mji wakamwambia, Ni kaburi la yule mtu wa Mungu, aliyetoka Yuda, akayanena mambo hayo uliyoyatenda wewe juu ya madhabahu ya Betheli.
18 Akasema, Mwacheni; mtu awaye yote asiiondoe mifupa yake. Basi wakaiacha mifupa yake, pamoja na mifupa ya yule nabii aliyetoka Samaria.
19 Na nyumba zote pia za mahali pa juu palipokuwa katika miji ya Samaria, wafalme wa Israeli walizozifanya, ili kumkasirisha Bwana, Yosia aliziondoa, akazitenda kwa mfano wa mambo yote aliyoyatenda katika Betheli.
20 Akawaua na makuhani wote wa mahali pa juu waliokuwako huko, juu ya madhabahu, akateketeza mifupa ya watu juu yake; kisha akarejea Yerusalemu.
21 Naye mfalme akawaamuru watu wote, akasema, Mfanyieni Bwana, Mungu wenu, pasaka, kama ilivyoandikwa katika kitabu hiki cha agano.
22 Hakika yake haikufanyika pasaka kama hiyo, tangu zamani za waamuzi waliowaamua Israeli, wala katika zamani za wafalme wa Israeli, wala za wafalme wa Yuda.
23 Bali katika mwaka wa kumi na nane wa mfalme Yosia ilifanyika pasaka hii kwa Bwana ndani ya Yerusalemu.
24 Tena wenye pepo wa utambuzi, na wachawi, na vinyago, na sanamu, na machukizo yote yaliyoonekana katika nchi ya Yuda na katika Yerusalemu, Yosia akayaondoa yote, ili apate kuyathibitisha maneno ya torati yaliyoandikwa katika kile kitabu alichokiona Hilkia kuhani ndani ya nyumba ya Bwana.
25 Kabla ya huyo hapakuwa na mfalme mfano wake, aliyemwelekea Bwana kwa moyo wake wote, na kwa roho yake yote, na kwa nguvu zake zote, sawasawa na sheria zote za Musa; wala baada yake hakuinuka mmoja mfano wake yeye.
26 Walakini Bwana hakuuacha ukali wa ghadhabu yake nyingi, ambayo kwayo hasira yake iliwaka juu ya Yuda, kwa sababu ya machukizo yote ambayo Manase amemchukiza.
27 Bwana akasema Nitawahamisha Yuda pia mbali nami, kama nilivyowahamisha Israeli, nami nitautupa mji huu niliouchagua, naam, Yerusalemu, na nyumba ile niliyoinena, Jina langu litakuwa humo.
28 Basi mambo yote ya Yosia yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
29 Katika siku zake, Farao-neko, mfalme wa Misri, akakwea ili kupigana na mfalme wa Ashuru, akafika mto Frati; naye mfalme Yosia akaenda kupigana naye; naye mfalme wa Misri akamwua huko Megido, hapo alipoonana naye.
30 Watumishi wake wakamchukua garini, amekwisha kufa, kutoka Megido, wakamleta Yerusalemu, wakamzika katika kaburi lake mwenyewe. Watu wa nchi wakamtwaa Yehoahazi mwana wa Yosia, wakamtia mafuta, wakamtawaza awe mfalme badala ya baba yake.
31 Yehoahazi alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitatu alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Hamutali binti Yeremia wa Libna.
32 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na yote waliyoyafanya baba zake.
33 Naye Farao-neko akamfunga huko Ribla, katika nchi ya Hamathi, ili asitawale huko Yerusalemu. Akaitoza nchi kodi talanta mia za fedha na talanta ya dhahabu.
34 Farao-neko akamfanya Eliakimu mwana wa Yosia awe mfalme mahali pa Yosia babaye, akambadilisha jina lake kuwa Yehoyakimu, lakini akamwondoa Yehoahazi; akaenda naye Misri, naye akafa huko.
35 Na Yehoyakimu akampa Farao dhahabu na fedha; lakini akaitoza nchi kodi, ili apate kutoa zile fedha kwa amri yake Farao; akawatoza fedha na dhahabu watu wa nchi, kila mtu kwa kodi yake, ili ampe Farao-neko.
36 Yehoyakimu alikuwa na umri wa miaka ishirini na mitano alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na mmoja huko Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Zebida binti Pedaya wa Ruma.
37 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na yote waliyoyafanya baba zake.

2 Walfame 24


1 Katika siku zake akakwea Nebukadreza, mfalme wa Babeli na Yehoyakimu akawa mtumishi wake muda wa miaka mitatu;kisha ,akageuka,akamwasi.
2 Naye Bwana akatuma juu yake vikosi vya Wakaldayo, na vikosi vya Washami, na vikosi vya Wamoabi, na vikosi vya wana wa Amoni, akawatuma juu ya Yuda ili kuiharibu, sawasawa na neno la Bwana alilolinena kwa mkono wa watumishi wake manabii.
3 Hakika kwa amri ya Bwana mambo hayo yalimpata Yuda, ili waondoshwe kutoka machoni pake, kwa sababu ya dhambi zake Manase, kadiri ya yote aliyoyafanya;
4 tena kwa ajili ya damu zisizo na hatia alizozimwaga; kwani aliujaza Yerusalemu damu zisizo na hatia; wala Bwana hakukubali kusamehe.
5 Basi mambo yote ya Yehoyakimu yaliyosalia, na yote aliyoyafanya, je! Hayakuandikwa katika kitabu-cha-tarehe cha wafalme wa Yuda?
6 Yehoyakimu akalala na babaze; na mwanawe Yekonia akatawala mahali pake.
7 Basi mfalme wa Misri hakuja tena kutoka nchi yake; kwa kuwa mfalme wa Babeli alikuwa amemnyang'anya nchi, tangu kijito cha Misri mpaka mto wa Frati, yote aliyokuwa nayo mfalme wa Misri.
8 Yekonia alikuwa na umri wa miaka kumi na minane alipoanza kutawala; akatawala miezi mitatu katika Yerusalemu; na jina la mama yake aliitwa Nehushta binti Elnathani wa Yerusalemu.
9 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, mfano wa yote aliyoyafanya baba yake.
10 Wakati ule watumishi wa Nebukadreza mfalme wa Babeli wakakwea kwenda Yerusalemu, na mji ukahusuriwa.
11 Na Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akaufikilia huo mji, hapo watumishi wake walipokuwa wakiuhusuru.
12 Na Yekonia, mfalme wa Yuda, akatoka akamwendea mfalme wa Babeli, yeye na mama yake, na watumishi wake, na wakuu wa watu wake, na maakida wake; mfalme wa Babeli akamchukua mateka katika mwaka wa nane wa kutawala kwake.
13 Akatoa huko hazina zote za nyumba ya Bwana, na hazina za nyumba ya mfalme, akavikata-kata vyombo vyote vya dhahabu ambavyo Sulemani, mfalme wa Israeli, alivifanya katika hekalu la Bwana, kama Bwana alivyosema.
14 Akawachukua mateka watu wa Yerusalemu wote pia, na wakuu wote, na mashujaa wote, watu elfu kumi; na mafundi wote, na wafua chuma wote; hapana mtu aliyebaki, ila waliokuwa wanyonge wa watu wa nchi.
15 Akamchukua Yekonia mpaka Babeli; na mama yake mfalme, na wake zake mfalme, na maakida wake, na wakuu wa nchi, aliwachukua mateka toka Yerusalemu mpaka Babeli.
16 Na mashujaa wote, watu elfu saba, na mafundi na wafua chuma elfu moja, wote pia wenye nguvu, tayari kwa vita, hao wote mfalme wa Babeli aliwachukua mateka mpaka Babeli.
17 Mfalme wa Babeli akamtawaza Matania, ndugu ya baba yake, awe mfalme badala yake, akalibadili jina lake, akamwita Sedekia.
18 Sedekia alikuwa na umri wa miaka ishirini na mmoja alipoanza kutawala; akatawala miaka kumi na mmoja katika Yerusalemu; na jina la mamaye aliitwa Hamutali, binti Yeremia wa Libna.
19 Akafanya yaliyo mabaya machoni pa Bwana, sawasawa na yote aliyoyafanya Yehoyakimu.
20 Maana kwa sababu ya hasira ya Bwana mambo hayo yalitokea katika Yerusalemu na katika Yuda, hata alipokuwa amewaondosha wasiwe mbele ya uso wake; naye Sedekia akamwasi mfalme wa Babeli.

2 Walfame 25


1 Ikawa katika mwaka wa kenda wa kutawala kwake, katika mwezi wa kumi, na siku ya kumi ya mwezi huo, Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akaja, yeye na jeshi lake lote, kupigana na Yerusalemu, akapanga hema zake kuukabili; nao wakajenga ngome juu yake pande zote.
2 Basi mji huo ulihusuriwa hata mwaka wa kumi na moja wa mfalme Sedekia.
3 Siku ya kenda ya mwezi wa nne njaa ilikuwa nzito ndani ya mji, hata hapakuwa na chakula kwa watu wa nchi.
4 Ndipo mahali pakabomolewa katika ukuta wa mji, watu wote wa vita wakakimbia usiku kwa njia ya lango lililokuwa kati ya zile kuta mbili, karibu na bustani ya mfalme; (basi wale Wakaldayo walikuwa wakiuzuia mji pande zote;) mfalme akaenda kwa njia ya Araba.
5 Lakini jeshi la Wakaldayo wakamfuatia mfalme, wakampata katika nchi tambarare ya Yeriko; na jeshi lake lote walikuwa wametawanyika na kumwacha.
6 Ndipo wakamkamata mfalme, wakamchukua kwa mfalme wa Babeli huko Ribla; wakatoa hukumu juu yake.
7 Wakawaua wana wa Sedekia mbele ya macho yake, wakampofusha macho Sedekia, wakamfunga kwa pingu, wakamchukua mpaka Babeli.
8 Hata mwezi wa tano, siku ya saba ya mwezi, ndio mwaka wa kumi na kenda wa mfalme Nebukadreza, mfalme wa Babeli, Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, mtumishi wa mfalme wa Babeli, akaingia Yerusalemu.
9 Akaiteketeza nyumba ya Bwana, na nyumba ya mfalme; na nyumba zote za Yerusalemu, naam, kila nyumba kubwa aliiteketeza kwa moto.
10 Na jeshi lote la Wakaldayo, waliokuwa pamoja na huyo amiri wa askari walinzi, wakazibomoa kuta za Yerusalemu pande zote.
11 Na mabaki ya watu waliosalia katika mji, nao wale walioasi, na kumkimbilia mfalme wa Babeli, na mabaki ya watu wote wengine, watu hao Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawachukua mateka.
12 Lakini huyo amiri wa askari walinzi akawaacha watu walio maskini ili wawe watunza mizabibu na wakulima.
13 Na zile nguzo za shaba zilizokuwako nyumbani mwa Bwana, na matako, na ile bahari ya shaba, iliyokuwamo nyumbani mwa Bwana, Wakaldayo wakavivunja vipande vipande, wakaichukua shaba yake yote mpaka Babeli.
14 Nayo masufuria, na majembe, na makasi, na miiko, na vyombo vyote vya shaba walivyokuwa wakivitumia, wakavichukua vyote.
15 Na vyetezo, na mabakuli; vilivyokuwa vya dhahabu katika dhahabu, na vilivyokuwa vya fedha katika fedha, amiri wa askari walinzi akavichukua.
16 Zile nguzo mbili, na ile bahari moja, na yale matako, Sulemani alivyoifanyia nyumba ya Bwana; shaba ya vyombo hivyo vyote haikuwa na uzani.
17 Urefu wa nguzo moja ulikuwa dhiraa kumi na nane, na kichwa cha shaba kilikuwa juu yake; na urefu wa kichwa ulikuwa dhiraa tatu; na mapambo ya wavu na makomamanga juu ya kichwa hicho kote kote, yote yalikuwa ya shaba. Nayo nguzo ya pili ilikuwa vivyo hivyo, pamoja na ule wavu.
18 Na amiri wa askari walinzi akamtwaa Seraya, kuhani mkuu, na Sefania, kuhani wa pili, na wale walinzi watu wa mlango;
19 na katika mji akamtwaa towashi mmoja, aliyewasimamia watu wa vita; na watu watano katika wale waliosimama mbele ya mfalme, walioonekana mjini; na katibu wa jemadari wa jeshi, aliyewaandika watu wa nchi; na watu sitini katika watu wa nchi, walioonekana mjini.
20 Kisha Nebuzaradani, amiri wa askari walinzi, akawatwaa hao, akawaleta kwa mfalme wa Babeli huko Ribla.
21 Naye mfalme wa Babeli akawapiga, na kuwaua huko Ribla katika nchi ya Hamathi. Hivyo Yuda wakachukuliwa utumwani kutoka nchi yao.
22 Na kwa habari ya watu waliosalia katika nchi ya Yuda, aliowasaza Nebukadreza, mfalme wa Babeli, akamweka Gedalia mwana wa Ahikamu mwana wa Shafani awe liwali juu yao.
23 Kisha, wakuu wote wa majeshi, wao na watu wao, waliposikia kwamba mfalme wa Babeli amemweka Gedalia kuwa liwali, wakamwendea Gedalia huko Mispa; nao ni hawa, Ishmaeli mwana wa Nethania, na Yohana mwana wa Karea, na Seraya mwana wa Tanhumethi Mnetofa, na Yezania mwana wa Mmaaka, wao na watu wao.
24 Na Gedalia akawaapia wao na watu wao, akawaambia, Msiogope kwa ajili ya watumishi wa Wakaldayo; kaeni katika nchi; mkamtumikie mfalme wa Babeli; itakuwa vyema kwenu.
25 Lakini ikawa katika mwezi wa saba Ishmaeli mwana wa Nethania, mwana wa Elishama, mmoja wa wazao wa kifalme, na watu kumi pamoja naye, wakamwendea Gedalia, wakampiga hata akafa, na hao Wayahudi na Wakaldayo waliokuwa pamoja naye huko Mispa.
26 Wakaondoka watu wote, wadogo kwa wakubwa, pamoja na wakuu wa majeshi, wakainuka kwenda Misri; kwa kuwa waliwaogopa Wakaldayo.
27 Ikawa katika mwaka wa thelathini na saba wa kuhamishwa kwake Yekonia mfalme wa Yuda ,katika mwezi wa kumi na mbili ,siku ya ishirini na saba ya mwezi ,Evil-merodaki,mfalme wa Babeli ,katika mwaka wa kwanza wa kutawala kwake,akamwinua kichwa Yekonia,mfalme wa Yuda,akamtoa gerezani.
28 Akasema naye maneno mazuri, akaweka kiti chake cha enzi juu ya viti vya enzi vya wafalme waliokuwa pamoja naye huko Babeli;
29 naye akambadilishia mavazi yake ya gerezani, akala chakula mbele yake daima, siku zote za maisha yake.
30 Na kwa posho yake, alipewa posho ya daima na mfalme, siku kwa siku sehemu, siku zote za maisha yake.