Waamuzi

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21

Waamuzi 1


1 Ikawa baada ya kufa kwake Yoshua, wana wa Israeli wakamwuliza Bwana, wakisema, Ni nani atakayekwea kwanza kwa ajili yetu juu ya Wakanaani, ili kupigana nao?
2 Bwana akasema, Yuda atakwea; tazama, nimeitia hiyo nchi mkononi mwake.
3 Ndipo Yuda akamwambia Simeoni ndugu yake, Kwea wewe pamoja nami katika kura yangu, ili tupate kupigana na Wakanaani; kisha mimi nami nitakwenda pamoja nawe katika kura yako. Basi Simeoni akaenda pamoja naye.
4 Yuda akakwea; naye Bwana akawatia Wakanaani na Waperizi mkononi mwao; nao wakawapiga huko Bezeki watu elfu kumi.
5 Wakampata huyo Adoni-bezeki huko Bezeki; wakapigana naye, nao wakawapiga Wakanaani na Waperizi.
6 Lakini Adoni-bezeki akakimbia; nao wakamwandamia na kumshika, wakamkata vyanda vyake vya gumba vya mikono na vya miguu.
7 Adoni-bezeki akasema, Wafalme sabini, waliokuwa wamekatwa vyanda vyao vya gumba vya mikono na vya miguu, waliokota chakula chao chini ya meza yangu; kama nilivyofanya mimi, Mungu amenilipa vivyo. Wakamleta Yerusalemu naye akafa kuko.
8 Kisha wana wa Yuda wakapigana na Yerusalemu, wakautwaa, wakaupiga kwa makali ya upanga, na kuupiga moto huo mji.
9 Baadaye wana wa Yuda wakatelemka ili wapigane na hao Wakanaani waliokaa katika nchi ya milimani, na nchi ya Negebu, na nchi ya Shefela.
10 Kisha Yuda akawafuatia hao Wakanaani waliokaa katika Hebroni; (jina la Hebroni hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Kiriath-arba;) nao wakamwua Sheshai, na Ahimani, na Talmai.
11 Kisha kutoka hapo akawafuatia wale wenye kukaa Debiri. (Jina la Debiri hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Kiriath-seferi.)
12 Huyo Kalebu alisema, Yeye atakayeupiga Kiriath-seferi na kuutwaa, nitamwoza mwanangu Aksa awe mkewe.
13 Naye Othnieli, mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa huyo Kalebu, aliutwaa; basi akamwoza mwanawe Aksa.
14 Ikawa hapo alipokwenda kukaa naye, huyo mwanamke akamtaka ili aombe shamba kwa baba yake; na huyo mwanamke akashuka katika punda wake; Kalebu akamwuliza, Una haja gani utakayo?
15 Mwanamke akasema, Nipe baraka; kwa kuwa wewe umeniweka katika nchi ya Negebu, basi unipe na vijito vya maji pia. Kalebu akampa vile vijito vya maji vya juu na vijito vya chini.
16 Hao wana wa Mkeni, huyo shemeji yake Musa, wakakwea juu kutoka katika huo mji wa mitende, pamoja na wana wa Yuda, na kuingia hiyo nyika ya Yuda, iliyo upande wa kusini wa Aradi; nao wakaenda na kukaa pamoja na watu hao.
17 Kisha Yuda akaenda pamoja na nduguye Simeoni, na wakawapiga Wakanaani waliokaa katika Sefathi, na kuuharibu mji kabisa. Na jina la mji huo ulikuwa ukiitwa Horma.
18 Pamoja na haya Yuda aliutwaa Gaza pamoja na mipaka yake, na Ashkeloni na mipaka yake, na Ekroni na mipaka yake.
19 Bwana alikuwa pamoja na Yuda; naye akawafukuza watu waliokaa katika nchi ya milimani; asiweze kuwafukuza hao waliokaa katika hilo bonde, kwa kuwa wao walikuwa na magari ya chuma.
20 Kisha wakampa huyo Kalebu Hebroni, kama alivyonena Musa naye akawafukuza wale wana watatu wa Anaki.
21 Lakini wana wa Benyamini hawakuwafukuza Wayebusi waliokaa mji wa Yerusalemu; bali Wayebusi walikaa pamoja na wana wa Benyamini ndani ya Yerusalemu hata hivi leo.
22 Nyumba ya Yusufu nayo, wao nao walikwea kwenda juu ya Betheli; naye Bwana alikuwa pamoja nao.
23 Kisha mbari ya Yusufu wakatuma watu waende kuupeleleza Betheli. (Jina la mji huo hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Luzu.)
24 Hao wapelelezi walimwona mtu atoka katika huo mji, wakamwambia, Tafadhali, utuonyeshe maingilio ya mji huu, nasi tutakutendea mema.
25 Basi akawaonyesha maingilio ya mji, nao wakaupiga huo mji kwa makali ya upanga; lakini huyo mtu walimwacha aende zake, na watu wote wa jamaa yake.
26 Huyo mtu akaenda katika nchi ya Wahiti, akajenga mji, akaliita jina la huo mji Luzu; nalo ndilo jina lake hata hivi leo.
27 Tena Manase hakuwatoa wenyeji wa Bethsheani na miji yake, wala hao waliokaa Taanaki na miji yake, wala hao waliokaa Dori na miji yake, wala hao waliokaa Ibleamu na miji yake, wala hao waliokaa Megido na miji yake; lakini hao Wakanaani walikuwa hawakukubali kuiacha nchi hiyo.
28 Kisha ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepata nguvu, ndipo walipowatia hao Wakanaani katika kazi ya shokoa, wala hawakuwafukuza kabisa.
29 Efraimu naye hakuwatoa Wakanaani waliokuwa wakikaa katika Gezeri; lakini Wakanaani walikaa ndani ya Gezeri kati yao.
30 Zabuloni naye hakuwatoa wenyeji wa Kitroni, wala hao waliokaa katika Nahalali; lakini Wakanaani walikaa kati yao, wakalazimishwa shokoa.
31 Asheri naye hakuwatoa wenyeji wa Aka, wala hao waliokaa Sidoni, wala hao wa Alabu, wala hao wa Akzibu, wala hao wa Helba, wala hao wa Afeka, wala hao wa Rehobu;
32 lakini Waasheri wakakaa kati ya Wakanaani, hao wenyeji wa nchi; kwa kuwa hawakuwafukuza.
33 Naftali naye hakuwatoa wenyeji wa Bethshemeshi, wala hao waliokaa Bethanathi; lakini alikaa kati ya Wakanaani, hao wenyeji wa nchi; pamoja na haya hao wenyeji wa Bethshemeshi, na wenyeji wa Bethanathi, wakawatumikia kazi ya shokoa.
34 Kisha Waamori waliwasukumiza wana wa Dani waende milimani; kwani hawakuwakubali kutelemkia bondeni;
35 lakini hao Waamori waliendelea kukaa katika kilima cha Heresi, na katika Aiyaloni, na katika Shaalbimu; pamoja na haya mkono wa hiyo nyumba ya Yusufu ulishinda, hata wakawalazimisha shokoa.
36 Mpaka wa Waamori ulikuwa tangu huko kupandia Akrabimu, tangu hilo jabali, na juu yake.

Waamuzi 2


1 Kisha malaika wa Bwana alikwea juu kutoka Gilgali kwenda Bokimu. Akasema, Mimi nimewaleta ninyi mkwee juu kutoka nchi ya Misri, nami nimewaleta hata nchi niliyowaapia baba zenu; nami nilisema, Mimi milele sitalivunja hilo agano langu nililoagana nanyi;
2 nanyi msifanye agano lo lote na hawa wenyeji wa nchi hii; zipomosheni nchi madhabahu zao; lakini hamkuisikia sauti yangu; je! Mmefanya haya kwa sababu gani?
3 Basi kwa ajili ya hayo mimi nilisema zaidi, Mimi sitawafukuza watoke mbele zenu; lakini watakuwa kama miiba mbavuni mwenu, na miungu yao itakuwa ni tanzi kwenu.
4 Ikawa, hapo huyo malaika wa Bwana alipoyanena maneno haya, kuwaambia wana wa Israeli wote, ndipo hao watu wakainua sauti zao na kulia.
5 Nao wakaliita jina la mahali pale Bokimu; nao wakamchinjia Bwana sadaka huko.
6 Basi hapo Yoshua alipowapa watu ruhusa waende zao, wana wa Israeli wakaenda kila mtu kuuendea urithi wake, ili kuimiliki hiyo nchi.
7 Watu hao wakamtumikia Bwana siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioendelea siku zao baada ya Yoshua, hao waliokuwa wameiona hiyo kazi kubwa ya Bwana yote, aliyokuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli.
8 Kisha Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, akafa, naye alipata umri wa miaka mia na kumi.
9 Nao wakamzika katika mpaka wa urithi wake katika Timnath-heresi, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi.
10 Tena watu wote wa kizazi hicho nao walikusanywa waende kwa baba zao; kikainuka kizazi kingine nyuma yao, ambacho hakikumjua Bwana, wala hawakuijua hiyo kazi ambayo alikuwa ameitenda kwa ajili ya Israeli.
11 Wana wa Israeli walifanya yaliyokuwa ni maovu mbele za macho ya Bwana, nao wakawatumikia Mabaali.
12 Wakamwacha Bwana, Mungu wa baba zao, aliyewaleta kutoka katika nchi ya Misri, wakafuata miungu mingine, baadhi ya miungu ya watu wale waliokaa karibu nao pande zote, wakajiinamisha mbele yao; wakamkasirisha Bwana, akaghadhibika.
13 Wakamwacha Bwana, wakamtumikia Baali na Maashtorethi.
14 Hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, naye akawatia katika mikono ya watu waliowateka nyara, akawauza na kuwatia katika mikono ya adui zao pande zote; hata wasiweze tena kusimama mbele ya adui zao.
15 Kila walikokwenda mkono wa Bwana ulikuwa juu yao kuwatenda mabaya, kama Bwana alivyosema, na kama Bwana alivyowaapia; nao wakafadhaika sana.
16 Kisha Bwana akawainua waamuzi, waliowaokoa na mikono ya watu hao waliowateka nyara.
17 Lakini hawakuwasikiliza hao waamuzi wao, maana walifanya uasherati kwa kuifuata miungu mingine, wakajiinamisha mbele yao; wakageuka upesi, na kuiacha njia ile waliyoiendea baba zao, waliozitii amri za Bwana bali wao hawakufanya hivyo.
18 Na wakati Bwana alipowainulia waamuzi, ndipo Bwana alikuwa pamoja na mwamuzi huyo, akawaokoa na mikono ya adui zao siku zote za mwamuzi huyo; maana Bwana alighairi kwa ajili ya kuugua kwao kwa sababu ya watu wale waliowaonea na kuwasumbua.
19 Lakini ikawa, wakati alipokufa mwamuzi huyo, wakarudi nyuma wakafanya maovu kuliko baba zao, kwa kuifuata miungu mingine ili kuitumikia, na kuinama mbele yao; hawakuacha matendo yao, wala njia zao za ukaidi.
20 Basi hasira ya Bwana ikawaka juu ya Israeli, naye akasema, Kwa kuwa taifa hili wamelihalifu agano langu nililowaamuru baba zao, wala hawakuisikiliza sauti yangu;
21 mimi nami tokea sasa sitalifukuza taifa mojawapo la hayo aliyoyaacha Yoshua alipokufa;
22 ili kwa njia ya hayo nipate kuwajaribu Israeli, kwamba wataishika njia ya Bwana kwenda katika njia hiyo, au sivyo.
23 Basi Bwana akawaacha mataifa yale, wala hakuwafukuza kwa upesi, wala hakuwatia katika mikono ya Yoshua.

Waamuzi 3


1 Basi haya ndiyo mataifa ambao Bwana aliwaacha, ili awajaribu Israeli kwa hao, yaani, awajaribu hao wote ambao hawakuvijua vita vyote vya Kanaani;
2 ili kwamba vizazi vya wana wa Israeli wapate kujua ili kuwafundisha vita, hasa wao ambao hawakujua vita kabla ya wakati ule;
3 aliwaacha wakuu watano wa Wafilisti, na Wakanaani wote, na Wasidoni, na Wahivi waliokaa katika kilima cha Lebanoni, toka mlima wa Baal-hermoni mpaka kuingia Hamathi.
4 Naye aliwaacha ili awajaribu Israeli kwa hao, apate kujua kwamba watasikiliza amri za Bwana, alizowaamuru baba zao, kwa mkono wa Musa.
5 Basi wana wa Israeli wakaketi kati ya Wakanaani; hao Wahiti, na hao Waamori, na hao Waperizi, na hao Wahivi na hao Wayebusi;
6 wakawaoa binti zao, na binti zao wenyewe wakawaoza wana wao waume, na kuitumikia miungu yao.
7 Wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana, nao wakamsahau Bwana, Mungu wao, nao wakawatumikia Mabaali na Maashtorethi.
8 Kwa hiyo hasira za Bwana ziliwaka juu ya Israeli, naye akawauza na kuwatia mikononi mwa Kushan-rishathaimu mfalme wa Mesopotamia; na wana wa Israeli wakamtumikia huyo Kushan-rishathaimu muda wa miaka minane.
9 Kisha wana wa Israeli walipomlingana Bwana, Bwana akawainulia wana wa Israeli mwokozi, aliyewaokoa, yaani, Othnieli mwana wa Kenazi, ndugu mdogo wa Kalebu.
10 Roho ya Bwana ikamjilia juu yake, naye akawa mwamuzi wa Israeli; akatoka kwenenda vitani, naye Bwana akamtia huyo Kushan-rishathaimu, mfalme wa Mesopotamia, mkononi mwake; na mkono wake ukamshinda Kushan-rishathaimu.
11 Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka arobaini. Kisha Othnieli, mwana wa Kenazi, akafa.
12 Basi wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu tena mbele za Bwana; naye Bwana akamtia nguvu Egloni mfalme wa Moabu juu ya Israeli, kwa sababu walikuwa wameyafanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana.
13 Huyo Egloni akakutanisha kwake wana wa Amoni na Amaleki; akaenda na kuwapiga Israeli, nao wakauchukua huo mji wa mitende.
14 Wana wa Israeli walimtumikia Egloni mfalme wa Moabu muda wa miaka kumi na minane.
15 Lakini wana wa Israeli walipomlilia Bwana, Bwana akawainulia mwokozi, Ehudi, mwana wa Gera, Mbenyamini, mtu aliyekuwa mwenye shoto; nao wana wa Israeli walimpelekea Egloni mfalme wa Moabu tunu mkononi mwa huyo Ehudi.
16 Ehudi alijifanyia upanga uliokuwa na makali kuwili, urefu wake ulipata dhiraa moja; akaufunga huo upanga ndani ya nguo yake katika paja lake la mkono wa kuume.
17 Kisha akamsongezea Egloni, mfalme wa Moabu, hiyo tunu; basi Egloni alikuwa ni mtu aliyewanda sana.
18 Naye hapo alipokuwa amekwisha kuisongeza hiyo tunu, akawapa ruhusa watu hao walioichukua tunu, wakaenda zao.
19 Lakini yeye mwenyewe akageuka kutoka huko kwenye sanamu zilizokuwa karibu na Gilgali, akasema, Mimi nina ujumbe wa siri kwako wewe, Ee mfalme. Naye akasema, Nyamazeni kimya. Watu wote waliokuwa wanasimama karibu naye wakatoka na kumwacha.
20 Basi Ehudi akamwendea; naye alikuwa anaketi peke yake katika chumba chake cha baridi. Ehudi akasema, Mimi nina ujumbe utokao kwa Mungu kwako wewe. Basi akainuka katika kiti chake.
21 Ehudi akaunyosha mkono wake wa kushoto, akaushika huo upanga kuutoa hapo katika paja lake la kuume, akamtia tumboni mwake;
22 hicho kipini nacho kikaingia ndani pamoja na huo upanga wenyewe; nayo mafuta yakashikamana tena juu ya upanga, kwani hakuutoa tena upanga tumboni; nao ukatokea kwa nyuma.
23 Ndipo Ehudi akatoka nje barazani, akamfungia milango ya hicho chumba na kuifunga kwa ufunguo.
24 Basi alipokuwa amekwisha toka nje, hao watumishi wake wakaenda; wakaona, na tazama, hiyo milango ya chumba ilikuwa imefungwa kwa ufunguo; nao wakasema, Hapana budi amejifunika miguu yake ndani ya chumba cha baridi.
25 Wakangoja hata wakatahayari; na tazama, hakuifungua milango ya chumba; basi wakatwaa ufunguo, na kuifungua; na tazama, bwana wao alikuwa ameanguka nchi, naye amekufa.
26 Naye Ehudi alikimbia hapo walipokuwa wakingoja, akapita huko kwenye sanamu, na kukimbilia Seira.
27 Ikawa, hapo alipofika akapiga tarumbeta katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu, ndipo wana wa Israeli wakatelemka pamoja naye kutoka huko milimani, naye akawatangulia.
28 Akawaambia, Niandameni mimi; kwa kuwa Bwana amewatia adui zenu, Wamoabi, mikononi mwenu. Basi wakatelemka na kumfuata, wakavishika vivuko vya Yordani kinyume cha Wamoabi, wala hawakumwacha mtu kuvuka.
29 Wakati huo wakapiga katika Wamoabi watu waume wapata kama elfu kumi, ambao wote walikuwa wanene, na wote mashujaa; hakupona hata mtu mmoja.
30 Basi Moabu alishindwa siku hiyo chini ya mikono ya Israeli. Nayo nchi ikawa na amani muda wa miaka themanini
31 Tena baada yake huyo alikuwapo Shamgari mwana wa Anathi, aliyepiga katika Wafilisti watu mia sita kwa konzo la ng'ombe; yeye naye aliwaokoa Israeli.

Waamuzi 4


1 Hata alipokufa Ehudi, wana wa Israeli wakafanya yaliyo maovu tena mbele za macho ya Bwana.
2 Bwana akawauza na kuwatia katika mkono wa Yabini, mfalme wa Kanaani, aliyetawala huko Hazori; na Sisera, aliyekaa katika Haroshethi wa Mataifa, alikuwa amiri wa jeshi lake.
3 Wana wa Israeli wakamlilia Bwana; kwa kuwa Sisera alikuwa na magari ya chuma mia kenda; naye akawaonea wana wa Israeli kwa nguvu muda wa miaka ishirini.
4 Basi Debora, nabii mke, mkewe Lapidothi, ndiye aliyekuwa mwamuzi wa Israeli wakati ule.
5 Naye alikaa chini ya mtende wa Debora, kati ya Rama na Betheli, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu; wana wa Israeli wakakwea kwake, awaamue.
6 Huyo akatuma mtu akamwita Baraka wa Abinoamu toka Kedesh-Naftali, akamwambia, Je! Bwana, Mungu wa Israeli, hakutoa amri, akisema, Enenda, ukawavute kwako, huko katika mlima wa Tabori, watu elfu kumi wa wana wa Naftali, na wa wana wa Zabuloni?
7 Nami nitakuvutia Sisera, amiri wa jeshi lake Yabini, hata mto wa Kishoni, pamoja na magari yake, na wingi wa watu wake; nami nitamtia mkononi mwako.
8 Baraka akamwambia, Kama utakwenda pamoja nami ndipo nitakwenda; bali kama huendi pamoja nami, mimi siendi.
9 Basi akasema, Hakika nitakwenda pamoja nawe, lakini safari utakayoiendea haitakupatia heshima wewe; maana Bwana atamwuza Sisera katika mkono wa mwanamke. Debora akainuka, akaenda pamoja na Baraka mpaka Kedeshi.
10 Baraka akawakutanisha Naftali na Zabuloni waende Kedeshi wakakwea watu elfu kumi wakimfuata; Debora naye akaenda pamoja naye.
11 Basi Heberi, Mkeni, alikuwa amejitenga na Wakeni, yaani na wana wa Hobabu, shemeji yake Musa, akaipiga hema yake mbali penye mwaloni ulioko Saanaimu, karibu na Kedeshi.
12 Watu wakamwambia Sisera ya kwamba Baraka, mwana wa Abinoamu amekwea kwenda mlima wa Tabori.
13 Sisera akayakusanya magari yake yote, naam, magari ya chuma mia kenda, na watu wote waliokuwa pamoja naye, toka Haroshethi wa Mataifa mpaka mto wa Kishoni.
14 Debora akamwambia Baraka, Haya! Inuka; maana siku hii ndiyo siku ambayo Bwana amemtia Sisera katika mkono wako. Je! Bwana hakutoka atangulie mbele yako? Basi Baraka akashuka katika mlima wa Tabori, na watu elfu kumi wakamfuata.
15 Bwana akamfadhaisha Sisera na magari yake yote, na jeshi lake lote, kwa makali ya upanga, mbele ya Baraka; basi Sisera akashuka katika gari lake, akakimbia kwa miguu.
16 Lakini Baraka akayafuatia magari, na jeshi, hata Haroshethi wa Mataifa; na hilo jeshi lote la Sisera likaanguka kwa makali ya upanga; hakusalia hata mtu mmoja.
17 Lakini Sisera akakimbia kwa miguu, akaifikilia hema ya Yaeli mkewe Heberi, Mkeni; kwa maana palikuwa na amani kati ya Yabini, mfalme wa Hazori, na nyumba ya Heberi, Mkeni.
18 Yaeli akatoka kwenda kumlaki Sisera, akamwambia, Karibu Bwana wangu, karibu kwangu; usiogope. Akakaribia kwake hemani, naye akamfunika kwa bushuti.
19 Akamwambia, Tafadhali nipe maji kidogo ninywe; maana nina kiu. Akafungua chupa ya maziwa, akampa kunywa, akamfunika.
20 Naye akamwambia, Simama mlangoni pa hema; kisha itakuwa mtu awaye yote akija na kukuuliza, akisema, Je! Yupo mtu hapa, basi, mjibu, La, hapana.
21 Ndipo Yaeli, mkewe Heberi, akatwaa kigingi cha hema, akashika nyundo mkononi mwake, akamwendea polepole, akamtia kile kigingi katika kipaji chake, nacho kikapenya, hata kuingia mchangani; kwa maana usingizi mzito ulikuwa umemshika; basi akazimia, akafa.
22 Na tazama, Baraka alipokuwa akimfuatia Sisera; Yaeli akatoka ili kumlaki, akamwambia, Njoo, nami nitakuonyesha yule mtu unayemtafuta. Basi akamwendea, na tazama, Sisera amelala humo, amekufa, na hicho kigingi kilikuwa kipajini mwake.
23 Basi hivyo Mungu akamshinda Yabini, mfalme wa Kanaani mbele ya wana wa Israeli siku hiyo.
24 Mkono wa wana wa Israeli ukazidi kupata nguvu juu ya Yabini, mfalme wa Kanaani, hata walipokuwa wamemwangamiza Yabini, mfalme wa Kanaani.

Waamuzi 5


1 Ndipo Debora, na Baraka mwana wa Abinoamu, wakaimba siku ile, wakisema;
2 Kwa sababu wakuu walitangulia katika Israeli, Kwa sababu watu walijitoa nafsi zao kwa hiari yao, Mhimidini Bwana.
3 Sikieni, enyi wafalme; tegeni masikio, enyi wakuu; Mimi, naam mimi, nitamwimbia Bwana; Nitamhimidi Bwana, Mungu wa Israeli.
4 Bwana, ulipotoka katika Seiri, Ulipokwenda vitani kutoka mashamba ya Edomu, Nchi ilitetema, mbingu nazo zikadondoza maji, Naam, mawingu yakadondoza maji.
5 Milima ikayeyuka mbele za uso wa Bwana, Naam hata Sinai ule mbele za uso wa Bwana, Mungu wa Israeli.
6 Katika siku za Shamgari, mwana wa Anathi, Siku za Yaeli, njia kuu zilikuwa hazina watu; Nao wenye kusafiri walipita kwa njia za kando.
7 Maliwali walikoma katika Israeli, walikoma, Hata mimi Debora nilipoinuka, Nilipoinuka mimi, mama katika Israeli.
8 Walichagua miungu mipya, Ndipo kulikuwa na vita malangoni; Je! Ilionekana ngao au mkuki Katika watu elfu arobaini wa Israeli?
9 Moyo wangu unawaelekea maliwali wa Israeli, Waliojitoa nafsi zao kwa hiari yao miongoni mwa watu; Mhimidini Bwana.
10 Itangazeni habari, ninyi mpandao punda weupe, Ninyi mketio juu ya mazulia ya thamani, Na ninyi mnaopita njiani kwa miguu.
11 Mbali na kelele za hao wapigao mishale, katika mahali pa kuteka maji, Hapo watatangaza matendo ya haki ya Bwana; Naam, matendo ya haki ya kutawala kwake katika Israeli. Ndipo watu wa Bwana waliposhuka malangoni.
12 Amka, amka, Debora; Amka, amka, imba wimbo. Inuka, Baraka, wachukue mateka wao Waliokuchukua mateka, Ee mwana wa Abinoamu.
13 Ndipo walitelemka mabaki ya waungwana na ya watu; Bwana alishuka kwa ajili yangu apigane na mashujaa.
14 Kutoka Efraimu walitelemka wao ambao shina lao ni katika Amaleki, Nyuma yako, Benyamini, kati ya watu wako. Kutoka Makiri walishuka maliwali, Na kutoka Zabuloni wao washikao fimbo ya mwandishi.
15 Na wakuu wa Isakari walikuwa pamoja na Debora. Kama alivyokuwa Isakari, ndivyo alivyokuwa Baraka. Waliingia bondeni kwa kasi miguuni pake. Kwenye vijito vya Reubeni Palikuwa na makusudi makuu mioyoni.
16 Mbona ulikaa katika mazizi ya kondoo, Kusikiliza filimbi zipigwazo ili kuita makundi? Kwenye vijito vya Reubeni Palikuwa na makusudi makuu mioyoni.
17 Gileadi alikaa ng'ambo ya Yordani, Na Dani, mbona alikaa katika merikebu? Asheri alikaa kimya penye bandari ya bahari, Alikaa katika hori zake.
18 Zabuloni ndio watu waliohatirisha roho zao hata kufa; Nao Naftali mahali palipoinuka kondeni.
19 Wafalme walikuja wakafanya vita, Ndipo wafalme wa Kanaani walifanya vita. Katika Taanaki, karibu na maji ya Megido; Hawakupata faida yo yote ya fedha.
20 Walipigana kutoka mbinguni, Nyota katika miendo yao zilipigana na Sisera.
21 Mto ule wa Kishoni uliwachukua, Ule mto wa zamani, mto wa Kishoni. Ee roho yangu, endelea mbele kwa nguvu.
22 Ndipo kwato za farasi zilikanyaga-kanyaga Kwa sababu ya kupara-para, Kupara-para kwao wenye nguvu.
23 Ulaanini Merozi, alisema malaika wa Bwana, Walaanini kwa uchungu wenyeji wake; Kwa maana hawakuja kumsaidia Bwana, Kumsaidia Bwana juu ya hao wenye nguvu.
24 Atabarikiwa Yaeli kuliko wanawake wote; Mkewe Heberi, Mkeni, Atabarikiwa kuliko wanawake wote hemani.
25 Aliomba maji, naye akampa maziwa. Akamletea siagi katika sahani ya heshima.
26 Akanyosha mkono wake akashika kigingi, Nao mkono wake wa kuume ukashika nyundo ya fundi; Akampiga Sisera kwa hiyo nyundo, akamtoboa kichwa chake. Naam, alimpiga akamtoboa kipaji chake.
27 Miguuni pake aliinama, akaanguka, akalala. Miguuni pake aliinama, akaanguka. Hapo alipoinama, ndipo alipoanguka amekufa.
28 Alichungulia dirishani, akalia, Mama yake Sisera alilia dirishani; Mbona gari lake linakawia kufika? Mbona gurudumu za gari lake zinakawia?
29 Mabibi yake wenye akili wakamjibu, Naam, alijipa nafsi yake jawabu.
30 Je! Hawakupata mateka na kuyagawanya, Kijakazi, vijakazi wawili, kwa kila mtu? Kwa Sisera nyara ya mavazi ya rangi mbali mbali, Nyara za mavazi ya rangi mbali mbali ya darizi; Ya rangi mbali mbali ya darizi, pande zote mbili, Juu ya shingo za hao mateka.
31 Na waangamie vivyo hivyo adui zako wote, Ee Bwana.

Waamuzi 6


1 Kisha wana wa Israeli walifanya yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana; Bwana akawatia mikononi mwa Midiani muda wa miaka saba
2 Mkono wa Midiani ulikuwa na nguvu juu ya Israeli; tena kwa sababu ya Midiani wana wa Israeli walijifanyia hayo mashimo yaliyo milimani, na hayo mapango, na hizo ngome.
3 Basi ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamepanda mashamba, Wamidiani wakakwea, na Waamaleki, na hao wana wa mashariki; wakakwea juu yao;
4 wakapanga marago juu yao, na kuyaharibu hayo maongeo ya nchi, hata ufikapo Gaza, wala hawakuacha katika Israeli riziki ziwazo zote; kondoo, wala ng'ombe, wala punda.
5 Kwa maana walikwea na ng'ombe zao na hema zao, wakaja mfano wa nzige kwa wingi; wao na ngamia zao pia walikuwa hawana hesabu; nao waliingia katika hiyo nchi ili kuiharibu.
6 Israeli walitwezwa sana kwa sababu ya Wamidiani; nao wana wa Israeli wakamlilia Bwana.
7 Kisha ikawa, hapo wana wa Israeli walipomlilia Bwana kwa sababu ya Midiani,
8 Bwana akamtuma nabii aende kwa hao wana wa Israeli; naye akawaambia, Bwana, yeye Mungu wa Israeli, asema hivi, Mimi niliwaleta ninyi mkwee kutoka Misri, nikawatoa katika nyumba ya utumwa;
9 nami niliwaokoa na mikono ya Wamisri, na mikono ya wote waliokuwa wakiwaonea, nami niliwafukuza watoke mbele zenu, nami niliwapa ninyi nchi yao;
10 kisha niliwaambia, Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu; msiiche miungu ya Waamori, ambayo mwaketi katika nchi yao; lakini hamkuitii sauti yangu.
11 Malaika wa Bwana akaenda akaketi chini ya mwaloni uliokuwa katika Ofra, uliokuwa mali yake Yoashi, Mwabiezeri; na mwanawe Gideoni alikuwa akipepeta ngano ndani ya shinikizo, ili kuificha machoni pa Wamidiani.
12 Malaika wa Bwana akamtokea, akamwambia, Bwana yu pamoja nawe, Ee shujaa.
13 Gideoni akamwambia, Ee Bwana wangu, ikiwa Bwana yu pamoja nasi, mbona mambo haya yote yametupata? Yako wapi matendo yake ya ajabu, waliyotuhadithia baba zetu, wakisema, Je! Siye Bwana, aliyetuleta huku kutoka Misri? Ila sasa ametutupa, naye ametutia katika mikono ya Midiani.
14 Bwana akamtazama, akasema, Enenda kwa uwezo wako huu, ukawaokoe Israeli na mkono wa Midiani. Je! Si mimi ninayekutuma?
15 Akamwambia, Ee Bwana, nitawaokoa Israeli kwa jinsi gani? Tazama, jamaa zangu ndio walio maskini sana katika Manase, na mimi ndimi niliye mdogo katika nyumba ya baba yangu.
16 Bwana akamwambia, Hakika nitakuwa pamoja nawe, nawe utawapiga Wamidiani kama mtu mmoja.
17 Naye akamwambia, Kama nimepata kibali mbele za macho yako, basi unionyeshe ishara, ya kuwa ndiwe wewe unayesema nami.
18 Tafadhali, usiondoke hapa hata nikujie, nikatoe zawadi yangu, na kuiweka mbele zako. Akasema, Nitangoja hata utakaporudi.
19 Basi Gideoni akaingia ndani, akaandaa mwana-mbuzi, na mikate isiyotiwa chachu, ya efa ya unga; akaitia ile nyama katika kikapu, akautia mchuzi katika nyungu, akamletea hapo nje chini ya mwaloni, akampa.
20 Naye malaika wa Mungu akamwambia, Itwae nyama na mikate isiyotiwa chachu, uiweke juu ya mwamba huu, ukaumwage huu mchuzi. Akafanya hivyo.
21 Ndipo malaika wa Bwana akanyosha ncha ya fimbo ile iliyokuwa mkononi mwake, akaigusa ile nyama na ile mikate; moto ukatoka mwambani, ukaiteketeza ile nyama na mikate; malaika wa Bwana akaondoka mbele ya macho yake.
22 Gideoni akaona ya kuwa ni malaika wa Bwana; Gideoni akasema, Ole wangu, Ee Bwana MUNGU! Kwa kuwa nimemwona Bwana uso kwa uso.
23 Bwana akamwambia Amani iwe pamoja nawe; usiogope; hutakufa.
24 Ndipo Gideoni akamjengea Bwana madhabahu hapo, akaiita jina lake, Yehova-Shalomu; hata hivi leo iko huko katika Ofra ya Waabiezeri.
25 Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Mtwae ng'ombe wa baba yako, yaani ng'ombe wa pili, wa miaka saba, ukaiangushe madhabahu ya Baali, aliyo nayo baba yako, ukaikate Ashera ile iliyo karibu nayo;
26 ukamjengee Bwana, Mungu wako, madhabahu juu ya ngome hii, kwa taratibu zake; ukamtwae yule ng'ombe wa pili na kumtoa awe sadaka ya kuteketezwa, kwa kuni za ile Ashera uliyoikata.
27 Ndipo Gideoni akatwaa watu kumi miongoni mwa watumishi wake, akafanya kama Bwana alivyomwambia; lakini ikawa kwa sababu aliwaogopa watu wa nyumba ya baba yake, na watu wa mji, hakuweza kuyatenda hayo wakati wa mchana, basi aliyatenda usiku.
28 Hata watu wa mji walipoondoka asubuhi na mapema, tazama, madhabahu ya Baali imebomolewa, na ile Ashera iliyokuwa karibu nayo imekatwa, na yule ng'ombe wa pili ametolewa sadaka juu ya ile madhabahu iliyojengwa.
29 Wakaambiana, Ni nani aliyetenda jambo hili? Hata walipotafuta habari na kuuliza, wakasema, Gideoni, mwana wa Yoashi, ndiye aliyetenda jambo hili.
30 Ndipo watu wa mji wakamwambia Yoashi Mlete mwanao, afe; kwa sababu ameibomoa madhabahu ya Baali na kwa sababu ameikata ile Ashera iliyokuwa karibu nayo.
31 Yoashi akawaambia watu wote waliokuwa wakishindana naye, Je! Mtamtetea Baali? Au mtamwokoa ninyi? Yeye atakayemtetea na auawe hivi asubuhi; kama yeye ni Mungu, na ajitetee nafsi yake, kwa sababu mtu mmoja ameibomoa madhabahu yake.
32 Basi akamwita Yerubaali siku hiyo, akisema, Baali na atete naye kwa ajili ya nafsi yake, kwa sababu ameibomoa madhabahu yake.
33 Wakati huo Wamidiani na Waamaleki, na hao wana wa mashariki walikutana pamoja; wakavuka na kupanga hema zao katika bonde la Yezreeli.
34 Lakini roho ya Bwana ikaja juu yake Gideoni; naye akapiga tarumbeta; na Abiezeri walikutanika na kumfuata.
35 Kisha akatuma wajumbe waende kati ya Manase yote; wao nao walikutana pamoja ili kumfuata; kisha akatuma wajumbe waende kwa Asheri, na kwa Zabuloni, na kwa Naftali; nao wakakwea ili kumlaki.
36 Gideoni akamwambia Mungu, Ikiwa wewe utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema,
37 tazama, nitaweka ngozi ya kondoo katika kiwanja cha kupuria; na kama ukiwapo umande juu ya ngozi tu, na nchi yote ikiwa kavu, basi, hapo ndipo nitakapojua ya kuwa utawaokoa Israeli kwa mkono wangu, kama ulivyosema.
38 Ikawa hivyo; kwa maana aliondoka asubuhi na mapema, akaikamua ile ngozi, akautoa ule umande katika ile ngozi, bakuli zima la maji.
39 Gideoni akamwambia Mungu, Hasira yako isiwake juu yangu, nami nitasema mara hii tu; nakuomba, nijaribu kwa ngozi hii mara hii tu; sasa ngozi tu na iwe kavu, na uwe umande juu ya nchi yote.
40 Mungu akafanya hivyo usiku ule; maana ile ngozi tu ilikuwa kavu, napo palikuwa na umande juu ya nchi yote.

Waamuzi 7


1 Kisha Yerubaali, yaani Gideoni, na watu wote waliokuwa pamoja naye wakaondoka na mapema, wakapiga kambi yao karibu na kijito cha Harodi; na kambi ya Midiani ilikuwa upande wao wa kaskazini, karibu na mlima wa More, bondeni.
2 Bwana akamwambia Gideoni, Watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno hata nikawatie Wamidiani katika mikono yao, wasije Israeli wakajivuna juu yangu wakisema, Mkono wangu mwenyewe ndio ulioniokoa.
3 Basi sasa enda, tangaza habari masikioni mwa watu hawa, na kusema, Mtu awaye yote anayeogopa na kutetemeka, na arudi aondoke katika mlima wa Gileadi. Ndipo watu ishirini na mbili elfu wakarudi katika watu hao, wakabaki watu elfu kumi.
4 Bwana akamwambia Gideoni; Hata sasa watu hawa ni wengi mno; uwalete chini majini, nami nitawajaribu huko kwa ajili yako; kisha itakuwa ya kwamba yule nitakayekuambia, Huyu atakwenda pamoja nawe, ndiye atakayekwenda pamoja nawe; na mtu yule nitakayekuambia, Huyu hatakwenda pamoja nawe, basi mtu huyo hatakwenda.
5 Basi akawaleta watu chini majini. Bwana akamwambia Gideoni, Kila mtu atakayeyaramba maji kwa ulimi wake, kama vile arambavyo mbwa, huyo utamweka kando; kadhalika kila mtu apigaye magoti kunywa.
6 Na hesabu ya hao waliokunywa kwa kuramba-ramba, wakipeleka mkono kinywani, ilikuwa watu mia tatu; bali watu wengine wote walipiga magoti kunywa maji.
7 Bwana akamwambia Gideoni, Kwa watu hawa mia tatu walioyaramba maji nitawaokoa, nami nitawatia Wamidiani katika mikono yako; lakini watu hawa wote wengine na waende zao, kila mtu mahali pake.
8 Basi wale watu wakachukua vyakula vyao mikononi mwao, na tarumbeta zao; naye akawapeleka watu wote wa Israeli, kila mtu hemani kwake; bali aliwazuia wale watu mia tatu; na kambi ya Wamidiani ilikuwa chini yake, bondeni.
9 Ikawa usiku uo huo Bwana akamwambia, Ondoka, shuka kambini; maana nimeitia katika mikono yako.
10 Lakini, ukiogopa kushuka, shuka pamoja na Pura mtumishi wako kambini;
11 nawe utasikia wanayoyasema, na baada ya haya mikono yako itatiwa nguvu; ushuke kambini. Ndipo akashuka pamoja na Pura mtumishi wake hata kufikilia mwisho wa watu wenye silaha waliokuwa kambini.
12 Nao Wamidiani na Waamaleki na, hao wana wa mashariki walikuwa wametua bondeni, mfano wa nzige kwa wingi; na ngamia zao walikuwa hawana hesabu; mfano wa mchanga wa ufuoni, kwa wingi.
13 Hata Gideoni alipofika, tazama, palikuwa na mtu mmoja aliyekuwa akimhadithia mwenziwe ndoto, akasema, Tazama, naliota ndoto, na tazama, mkate wa shayiri ulianguka katika kambi ya Wamidiani, ukafika hata hema moja, ukaipiga hata ikaanguka, nao ukaipindua, hata ikalala chini.
14 Mwenzake akamjibu akasema, Habari hii haikosi kuwa upanga wa Gideoni, mwana wa Yoashi, mtu wa Israeli. Mungu amewatia Wamidiani na jeshi lote katika mkono wake.
15 Ikawa, aliposikia habari ya ile ndoto, na kufasiriwa kwake, akasujudu; akarudi katika jeshi la Israeli akasema, Inukeni, kwa maana Bwana amelitia jeshi la Midiani mikononi mwenu.
16 Kisha akawapanga wale watu mia tatu wawe vikosi vitatu, akatia tarumbeta katika mikono ya watu wote, na mitungi isiyo maji, na mienge ndani ya hiyo mitungi.
17 Akawaambia, Nitazameni, mkafanye kama nifanyavyo mimi; angalieni, nitakapofika mwisho wa kambi, itakuwa, nifanyavyo mimi nanyi fanyeni kadhalika.
18 Nitakapopiga tarumbeta, mimi na wote walio pamoja nami, basi ninyi nanyi zipigeni tarumbeta pande zote za kambi, mkaseme, Kwa Bwana, na kwa Gideoni.
19 Basi Gideoni, na wale watu mia waliokuwa pamoja naye, wakafika mwisho wa kambi, mwanzo wa zamu ya kati, wakati walipokuwa wamebadili wenye zamu; wakazipiga hizo tarumbeta, wakaivunja vipande vipande ile mitungi iliyokuwa mikononi mwao.
20 Vile vikosi vitatu wakapiga tarumbeta, wakaivunja mitungi, wakaishika mienge kwa mikono yao ya kushoto, na zile tarumbeta katika mikono yao ya kuume ili kuzipiga; wakapiga kelele, Upanga wa Bwana na wa Gideoni.
21 Wakasimama kila mtu mahali pake kuizunguka kambi pande zote; jeshi lote wakakimbia; nao wakapiga kelele, wakawakimbiza.
22 Wakazipiga zile tarumbeta mia tatu, naye Bwana akaufanya upanga wa kila mtu uwe juu ya mwenziwe, na juu ya jeshi lote, jeshi likakimbia mpaka Bethshita, kuendelea Serera, hata mpaka wa Abel-Mehola, karibu na Tabathi.
23 Wanaume wa Israeli walikuwa wamekusanyika kutoka Naftali, na kutoka Asheri, na kutoka Manase yote, wakawafuata Midiani.
24 Kisha Gideoni akapeleka wajumbe katika nchi yote ya vilima vilima ya Efraimu, akisema, Haya, telemkeni juu ya Midiani, na kuyashika hayo maji mbele yao, mpaka Bethbara, maana, huo mto wa Yordani. Basi watu waume wote wa Efraimu walikutana pamoja, wakayashika maji mpaka Bethbara, maana, huo mto wa Yordani.
25 Wakawashika hao wakuu wawili wa Midiani, Orebu na Zeebu; wakamwua huyo Orebu pale penye jabali la Orebu, na huyo Zeebu wakamwua hapo penye shinikizo la divai la Zeebu, kisha wakawaandamia Wamidiani; vichwa vya Orebu na Zeebu wakamletea Gideoni huko ng'ambo ya pili ya Yordani.

Waamuzi 8


1 Basi watu wa Efraimu wakamwambia, Kwa nini wewe kututendea sisi kama haya? Hata usituite, hapo ulipokwenda kupigana na Midiani? Nao wakateta naye sana.
2 Lakini akawaambia, Je! Mimi nimefanya nini sasa kama mlivyofanya ninyi? Hayo masazo ya zabibu za Efraimu si mema kuliko mavuno ya Abiezeri?
3 Mungu amewatia hao wakuu wa Midiani, Orebu na Zeebu, mikononi mwenu; na mimi nilipata kufanya nini kama mlivyofanya ninyi? Ndipo hasira zao walizokuwa nazo juu yake zikatulia aliposema maneno hayo.
4 Basi Gideoni akafika Yordani, akauvuka, yeye na hao watu mia tatu waliokuwa pamoja naye, walikuwa wamepungukiwa na nguvu, lakini wawafuatia vivyo.
5 Naye akawaambia watu wa Sukothi, Tafadhali wapeni mikate hao watu waniandamao; kwa maana wanapungukiwa na nguvu, nami ni katika kuwafuatia Zeba na Salmuna, wafalme wa Midiani.
6 Hao wakuu wa Sukothi wakasema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna i mkononi mwako sasa, hata sisi tukawape jeshi lako mikate?
7 Ndipo Gideoni akasema, Kwa sababu hii, hapo Bwana atakapokuwa amewatia Zeba na Salmuna mkononi mwangu, ndipo nitaipura nyama ya miili yenu kwa miiba ya nyikani, na kwa michongoma.
8 Basi kutoka hapo alikwea kwenda Penieli, akasema na watu wa mahali hapo maneno kama hayo; watu wa Penieli nao wakamjibu kama vile watu wa Sukothi walivyomjibu.
9 Naye akawaambia hao watu wa Penieli nao, akisema, Nitakapokuja tena kwa amani, nitauvunja mnara huu.
10 Basi hao kina Zebu na Salmuna walikuwa katika Karkori, na majeshi yao walikuwa pamoja nao, watu kama kumi na tano elfu hesabu yao, ni wote waliobaki wa hilo jeshi lote la hao wana wa mashariki; kwa sababu walianguka watu mia na ishirini elfu waliokuwa wenye kutumia upanga.
11 Basi Gideoni alikwea kwa njia ya hao waliokuwa wenye kukaa hemani upande wa mashariki wa Noba na Yogbeha, akalipiga hilo jeshi; kwa maana lile jeshi lilikuwa salama.
12 Zeba na Salmuna walikimbia; naye akawaandamia; akawakamata hao wafalme wawili wa Midiani Zeba na Salmuna, akalitapanya-tapanya hilo jeshi lote.
13 Kisha huyo Gideoni mwana wa Yoashi akarudi kutoka vitani, kutoka kwenye makweleo ya Heresi.
14 Ndipo akamshika mtu mmoja hirimu katika watu wa Sukothi, akamwuliza; naye akamwandikia majina ya hao wakuu wa Sukothi, na wazee wa mji, watu sabini na saba.
15 Kisha akawafikilia wale watu wa Sukothi, akawaambia, Tazama, Zeba na Salmuna, ambao ninyi mlinisimanga kwa ajili yao, mliposema, Je! Mikono ya Zeba na Salmuna iko sasa mikononi mwako wewe, hata tuwape watu wako waliochoka mikate?
16 Basi akawatwaa hao wazee wa mji, na miiba ya nyikani na michongoma, akawafunza hao watu wa Sukothi kwayo.
17 Kisha akaupomosha mnara wa Penieli, na kuwaua watu wa mji huo.
18 Ndipo akawaambia hao Zeba na Salmuna, Hao watu mliowaua huko Tabori walikuwa watu wa namna gani? Wakamjibu, Walikuwa kama wewe ulivyo; kila mmoja alikuwa anafanana na wana wa mfalme.
19 Naye akasema, Watu hao walikuwa ndugu zangu, wana wa mamaangu mimi; kama yeye Bwana alivyo hai, kwamba mliwaokoa hai watu hao, mimi nisingewaua ninyi.
20 Kisha akamwambia Yetheri mwanawe mzaliwa wa kwanza, Haya, simama, uwaue hawa. Lakini huyo kijana hakutoa upanga wake; maana, akacha, kwa sababu alikuwa ni kijana tu.
21 Ndipo hapo Zeba na Salmuna wakasema, Simama wewe ukatuangukie sisi; kwa maana kama mtu alivyo, ndivyo zilivyo nguvu zake. Basi Gideoni akasimama, akawaua Zeba na Salmuna, akazitwaa koja zilizokuwa katika shingo za ngamia zao.
22 Ndipo watu wa Israeli wakamwambia Gideoni, Tawala wewe juu yetu, wewe, na mwanao, na mjukuu wako pia; kwa kuwa wewe umetuokoa na mikono ya Midiani.
23 Gideoni akawaambia, Mimi sitatawala juu yenu wala mwanangu hatatawala juu yenu; yeye Bwana atatawala juu yenu.
24 Kisha Gideoni akawaambia, Mimi nina haja yangu niitakayo kwenu, ni ya kila mtu kunipa hizo pete za masikio ya mateka yake. (Kwa maana walikuwa na pete za masikio za dhahabu, kwa sababu walikuwa ni Waishmaeli.)
25 Wakajibu, Tutakupa kwa mioyo. Basi wakatandika nguo chini, wakatia humo kila mtu pete za masikio ya mateka yake.
26 Na uzani wa hizo pete za dhahabu alizozitaka ulipata shekeli za dhahabu elfu moja na mia saba; mbali na makoja na vidani, na mavazi ya rangi ya zambarau waliyokuwa wameyavaa hao wafalme wa Midiani, tena mbali na mikufu iliyokuwa katika shingo za ngamia zao.
27 Basi Gideoni akafanya naivera kwa vitu vile, akaiweka katika mji wake, mji huo wa Ofra; nao Israeli wote wakaenda na kuiandama kwa ukahaba huko; nayo ilikuwa ni tanzi kwa Gideoni na kwa nyumba yake.
28 Hivyo Midiani walishindwa mbele ya wana wa Israeli, wala hawakuinua vichwa vyao tena. Nayo nchi ilipata kuwa na amani muda wa miaka arobaini katika siku za Gideoni.
29 Kisha huyo Yerubaali, mwana wa Yoashi, akaenda kukaa katika nyumba yake mwenyewe.
30 Gideoni alikuwa na wana sabini waliozawa na mwili wake; kwa maana alikuwa na wake wengi.
31 Na suria yake aliyekuwako Shekemu, yeye naye akamzalia mwana, naye akamwita jina lake Abimeleki.
32 Basi Gideoni mwana wa Yoashi akafa mwenye umri wa uzee mwema, akazikwa katika kaburi la Yoashi baba yake, katika Ofra ya Waabiezeri.
33 Kisha ikawa, mara alipokufa Gideoni, wana wa Israeli wakakengeuka tena, wakawaandama Mabaali kwa ukahaba, wakamfanya Baal-berithi kuwa ni mungu wao.
34 Kwani wana wa Israeli hawakumkumbuka Bwana, Mungu wao, ambaye ndiye aliyewaokoa na mikono ya adui zao wote pande zote;
35 wala hawakuifanyia mema nyumba ya Yerubaali, yaani Gideoni, kwa kuyafuata hayo mema yote aliyowafanyia Israeli.

Waamuzi 9


1 Abimeleki, mwana wa Yerubaali, akaenda Shekemu kwa ndugu za mama yake, akanena nao, na wote waliokuwa wa nyumba ya baba ya mama yake, akasema,
2 Haya, neneni tafadhali masikioni mwa waume wote wa Shekemu, mkaulize, Je! Ni lipi lililo jema kwenu, kwamba hao wana wa Yerubaali wote, ambao ni watu sabini, watawale juu yenu, au kwamba mtu mmoja atawale juu yenu? Tena kumbukeni ya kwamba mimi ni mfupa na nyama yenu.
3 Hao ndugu za mama yake wakanena habari zake masikioni mwa hao watu wote wa Shekemu maneno hayo yote; na mioyo yao ikaelekea kumwandama Abimeleki; kwa kuwa walisema, Huyu ni ndugu yetu.
4 Wakampa vipande vya fedha sabini vilivyotoka katika nyumba ya Baal-berithi, na kwa fedha hizo Abimeleki akaajiri watu wapuuzi mabaradhuli, wafuatane naye.
5 Kisha akaenda nyumbani kwa babaye huko Ofra, akawaua nduguze, hao wana wa Yerubaali, watu sabini, akawaua juu ya jiwe moja; lakini Yothamu, mwana mdogo wa Yerubaali, alisalia; kwa maana alijificha.
6 Kisha hao watu wote wa Shekemu wakakusanyika pamoja, na jamaa yote ya Milo, wakaenda na kumtawaza Abimeleki awe mfalme, karibu na huo mgandi ulio karibu na ngome iliyo katika Shekemu.
7 Kisha walipomwambia huyo Yothamu, yeye akaenda, akasimama juu ya kilele cha kilima cha Gerizimu, akapaza sauti yake, akapiga kelele, na kuwaambia, Nisikieni mimi, enyi watu wa Shekemu, ili kwamba Mungu naye apate kuwasikia ninyi.
8 Siku moja miti ilitoka ili kuutia mmoja mafuta uwe mfalme juu yao; ikauambia mti mzeituni, Tawala wewe juu yetu.
9 Lakini huo mzeituni ukaiambia, Je! Niache mafuta yangu, ambayo kwangu mimi watu wamheshimu Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti?
10 Kisha miti ikauambia mtini, Njoo wewe, utawale juu yetu.
11 Lakini huo mtini ukaiambia, Je! Niuache utamu wangu, na matunda yangu mazuri, niende nikayonge-yonge juu ya miti?
12 Kisha miti ikauambia mzabibu, Njoo wewe, utawale juu yetu.
13 Huo mzabibu nao ukaiambia, Je! Niiache divai yangu, ambayo humfurahisha Mungu na wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti?
14 Ndipo hiyo miti yote ikauambia mti wa miiba, Njoo wewe, utawale juu yetu.
15 Huo mti wa miiba ukaiambia miti, Kwamba ninyi mwanitia mafuta niwe mfalme juu yenu kwelikweli, basi njoni mtumaini kivuli changu; na kwamba sivyo, na utoke moto katika mti wa miiba na kuiteketeza mierezi ya Lebanoni.
16 Basi sasa ikiwa mmetenda kwa uaminifu na uelekevu, katika kumtawaza Abimeleki awe mfalme, na ikiwa mmemtendea mema Yerubaali na nyumba yake, na kumtendea kama ilivyostahili mikono yake;
17 (kwa maana baba yangu aliwatetea ninyi, na kuhatirisha uhai wake, na kuwaokoa na mikono ya Midiani;
18 nanyi mmeinuka juu ya nyumba ya baba yangu hivi leo nanyi mmewaua wanawe, watu sabini, juu ya jiwe moja, nanyi mmemtawaza Abimeleki, mwana wa kijakazi chake, awe mfalme juu ya watu wa Shekemu kwa sababu yeye ni ndugu yenu;)
19 basi ikiwa mmemtendea kwa uaminifu na uelekevu Yerubaali na nyumba yake hivi leo, basi furahini ninyi katika huyo Abimeleki, yeye naye na afurahi kwenu ninyi;
20 lakini kwamba sivyo hivyo, basi, moto na utoke katika Abimeleki na kuwateketeza watu wa Shekemu, na jamaa ya Milo; kisha moto na utoke katika hao watu wa Shekemu, na katika jamaa ya Milo, na kumteketeza Abimeleki.
21 Kisha Yothamu akaenda zake na kukimbia, akaenda Beeri, na kukaa kuko, kwa kumwogopa Abimeleki nduguye.
22 Basi Abimeleki alitawala juu ya Israeli muda wa miaka mitatu.
23 Kisha Mungu akapeleka roho mbaya kati ya Abimeleki na watu wa Shekemu; nao watu wa Shekemu wakamtendea Abimeleki kwa udanganyifu;
24 ili kwamba huo udhalimu waliotendewa hao wana sabini wa Yerubaali uje, tena kwamba damu yao iandikwe juu ya Abimeleki ndugu yao, aliyewaua, na juu ya watu wa Shekemu, waliomtia nguvu mikono yake ili awaue hao nduguze.
25 Basi watu wa Shekemu wakaweka watu kumvizia juu ya vilele vya milima, ambao waliwanyang'anya vitu vyao watu wote waliopita njia hiyo karibu nao; naye Abimeleki aliambiwa.
26 Kisha Gaali, mwana wa Ebedi, akaenda pamoja na nduguze, wakavuka na kufika Shekemu; na watu wa Shekemu wakamtumaini yeye.
27 Nao wakatoka kwenda mashambani, wakavuna mashamba yao ya mizabibu, na kuzishindika hizo zabibu, na kufanya sikukuu, kisha wakaingia nyumbani mwa mungu wao, wakala na kunywa na kumlaani huyo Abimeleki.
28 Naye Gaali mwana wa Ebedi akasema, Abimeleki ni nani, na Shekemu ni nani, hata tukamtumikie yeye? Yeye, je! Si mwana wa Yerubaali? Na Zebuli siye akida wake? Haya, ninyi watumikieni hao watu wa Hamori, babaye Shekemu; Lakini sisi je! Tumtumikie kwa sababu gani?
29 Laiti watu hawa wangekuwa chini ya mkono wangu! Hapo basi mimi ningemwondoa huyo Abimeleki. Kisha akamwambia Abimeleki, Haya, ongeza askari zako, utoke nje.
30 Basi hapo Zebuli, aliyekuwa liwali wa mji, alipoyasikia hayo maneno ya Gaali mwana wa Ebedi, hasira zake zikamwaka.
31 Naye akatuma wajumbe waende kwa Abimeleki kwa siri, akasema, Tazama, Gaali, mwana wa Ebedi, na ndugu zake wamekuja Shekemu; na tazama waufitinisha mji huu kinyume chako.
32 Basi sasa, inuka wewe, usiku, wewe na watu walio pamoja nawe, mvizie mashambani;
33 kisha itakuwa, asubuhi, mara litakapokucha jua, wewe utaamka asubuhi na mapema, na kuushambulia mji huo; tena, angalia, hapo yeye na wale watu walio pamoja naye watakapokutokea nje kupigana nawe, ndipo utapata kuwatenda kama utakavyopata nafasi.
34 Basi Abimeleki akainuka na watu wote waliokuwa pamoja naye, usiku nao wakauvizia Shekemu kwa vikosi vinne.
35 Huyo Gaali mwana wa Ebedi akatoka nje, akasimama penye maingilio ya lango la mji; naye Abimeleki na hao watu waliokuwa pamoja naye wakainuka kutoka mahali pale walipokuwa wanavizia.
36 Basi Gaali alipowaona hao watu, akamwambia Zebuli, Tazama, watu washuka kutoka katika vilele vya milima. Zebuli akamwambia, Ni kivuli cha milima unachokiona kama ndio watu.
37 Kisha Gaali akasema mara ya pili, akanena, Angalia, watu washuka katikati ya nchi, na kikosi kimoja kinakuja kwa njia ya mwaloni wa Meonenimu.
38 Ndipo Zebuli akamwambia, Je! Kinywa chako sasa ki wapi, hata ukasema Huyo Abimeleki ni nani, hata inatupasa kumtumikia yeye? Je! Hawa sio watu hao uliowadharau wewe? Haya, toka nje sasa, tafadhali, upigane nao.
39 Basi Gaali akatoka nje mbele ya watu wa Shekemu, akapigana na Abimeleki.
40 Lakini Abimeleki akamkimbiza, naye akakimbia mbele yake, wengi wakaanguka waliojeruhiwa hata kufikilia maingilio ya hilo lango.
41 Abimeleki akakaa Aruma; naye Zebuli akawatoa Gaali na ndugu zake, wasikae katika Shekemu.
42 Ikawa siku ya pili yake, watu wakatoka waende mashambani; naye Abimeleki aliambiwa.
43 Naye akawatwaa watu wake, na kuwagawanya wawe vikosi vitatu, nao wakavizia mashambani; naye akaangalia, na tazama, watu walikuwa watoka humo mjini; basi akainuka na kupigana nao, akawapiga.
44 Abimeleki, na vile vikosi vilivyokuwa pamoja naye, wakafuliza kwenda mbele, wakasimama penye maingilio ya lango la mji, na vile vikosi viwili vikawarukia hao wote waliokuwa mashambani, na kuwapiga.
45 Abimeleki akapigana na huo mji mchana kutwa; akautwaa mji, akawaua watu waliokuwamo ndani yake; kisha akaupomosha mji, na kuutia chumvi.
46 Kisha watu wote waliokaa katika ile buruji ya Shekemu waliposikia habari hiyo wakaingia ndani ya ngome ya nyumba ya El-berithi.
47 Abimeleki aliambiwa ya kuwa watu hao wote wa buruji ya Shekemu wamekutana pamoja.
48 Basi Abimeleki akakwea kwenda kilima cha Salmoni, yeye na wote waliokuwa pamoja naye; naye Abimeleki akashika shoka mkononi mwake, akakata tawi moja katika miti, akalishika na kujitweka fuzini mwake; akawaambia hao watu waliokuwa pamoja naye, Haya, mliyoniona mimi kufanya, fanyeni upesi vivyo, kama nilivyofanya mimi.
49 Basi watu hao wote vivyo wakakata kila mtu tawi lake, wakamwandama Abimeleki, wakayaweka hayo matawi pale ngomeni, na kuiteketeza moto hiyo ngome juu yao; basi hivyo watu wote wa hiyo buruji ya Shekemu wakafa, walipata kama watu elfu, waume kwa wake.
50 Ndipo Abimeleki alipokwenda Thebesi, akapanga kinyume cha Thebesi na kuutwaa.
51 Lakini ndani ya huo mji palikuwa na buruji yenye nguvu, na watu wote waume na wake wakakimbilia huko, na watu wote wa mji, nao wakajifungia ndani, wakapanda paa la buruji.
52 Abimeleki akaiendea hiyo buruji na kupigana nayo; naye akaukaribia mlango wa buruji ili auteketeze kwa moto.
53 Na mwanamke mmoja akabwaga jiwe la kusagia la juu, nalo likampiga Abimeleki kichwani, na kulivunja fuvu la kichwa chake.
54 Ndipo akamwita kwa haraka huyo kijana aliyekuwa anamchukulia silaha zake, na kumwambia, Futa upanga wako, uniue, ili watu wasiseme juu yangu Aliuawa na mwanamke. Basi huyo kijana wake akamchoma upanga, naye akafa.
55 Basi hapo watu wa Israeli walipoona ya kuwa Abimeleki amekufa, wakaondoka wakaenda kila mtu mahali pake.
56 Basi hivyo Mungu akalipiza kisasi juu ya uovu wa Abimeleki aliomtenda baba yake, katika kuwaua hao nduguze watu sabini;
57 uovu wote wa watu wa Shekemu Mungu alilipiza juu ya vichwa vyao; na hiyo laana ya Yothamu mwana wa Yerubaali ikawajilia juu yao.

Waamuzi 10


1 Baada yake Abimeleki, akainuka Tola mwana wa Pua, mwana wa Dodo, mtu wa Isakari, kuwaokoa Israeli; naye alikuwa akikaa Shamiri, katika nchi ya vilima vilima ya Efraimu.
2 Huyo akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini na mitatu, akafa, akazikwa katika Shamiri.
3 Baada yake huyo akainuka Yairi, Mgileadi; naye akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini na miwili.
4 Huyo alikuwa na wana thelathini waliokuwa wakipanda wana-punda thelathini, nao walikuwa na miji thelathini, ambayo inaitwa Hawoth-yairi hata hivi leo, nayo iko katika nchi ya Gileadi.
5 Yairi akafa, akazikwa huko Kamoni.
6 Kisha wana wa Israeli walifanya tena yaliyo maovu mbele za macho ya Bwana, wakawatumikia Mabaali, na Maashtorethi, na miungu ya Shamu, na miungu ya Sidoni, na miungu ya Moabu, na miungu ya wana wa Amoni, na miungu ya Wafilisti; nao wakamwacha Bwana, wala hawakumtumikia yeye.
7 Hasira za Bwana ziliwaka juu ya Israeli, akawauza na kuwaua mikononi mwa Wafilisti, na mikononi mwa wana wa Amoni.
8 Nao wakawasumbua na kuwaonea wana wa Israeli mwaka huo; waliwaonea wana wa Israeli wote waliokuwa ng'ambo ya pili ya Yordani katika nchi ya Waamori, iliyoko huko Gileadi, muda wa miaka kumi na minane.
9 Wana wa Amoni nao wakavuka Yordani ili wapigane na Yuda, na kupigana na Benyamini, na nyumba ya Efraimu; basi hivyo Israeli walikuwa wanasumbuliwa sana.
10 Ndipo wana wa Israeli wakamlilia Bwana, wakisema, Sisi tumekufanyia dhambi, kwa sababu tumemwacha Mungu wetu, na kuyatumikia Mabaali.
11 Naye Bwana akawaambia wana wa Israeli, Je! Sikuwaokoa ninyi na hao Wamisri, na Waamori, na wana wa Amoni, na Wafilisti?
12 Hao Wasidoni nao, na Waamaleki, na Wamaoni, waliwaonea, nanyi mlinililia, nami niliwaokoa na mikono yao.
13 Lakini mmeniacha mimi, na kuitumikia miungu mingine; basi kwa ajili ya hayo mimi sitawaokoa tena.
14 Haya, endeni mkaililie hiyo miungu mliyoichagua; na hiyo iwaokoe wakati wa kusumbuka kwenu.
15 Wana wa Israeli wakamwambia Bwana Tumefanya dhambi; utufanyie yote uyaonayo kuwa ni mema; lakini tuokoe, twakusihi, siku hii ya leo, haya tu.
16 Nao wakaiondoa hiyo miungu ya kigeni iliyokuwa kati yao, nao wakamtumikia Bwana; na roho yake ilihuzunika kwa sababu ya msiba wa Israeli.
17 Wakati huo wana wa Amoni walikutana pamoja, wakapanga marago huko Gileadi. Wana wa Israeli nao wakajikusanya wakapanga marago Mispa.
18 Na hao watu, wakuu wa Gileadi, wakaambiana wao kwa wao, Je! Ni mtu yupi atakayeanza kupigana na wana wa Amoni? Yeye atakuwa ni kichwa juu ya wenyeji wote wa Gileadi.

Waamuzi 11


1 Basi huyo Yeftha, Mgileadi, alikuwa mtu shujaa sana, naye alikuwa ni mwana wa mwanamke kahaba; Gileadi akamzaa Yeftha.
2 Mkewe huyo Gileadi akamzalia wana; na hao wana wa mkewe hapo walipokuwa wamekua wakubwa wakamtoa Yeftha, na kumwambia, Wewe hutarithi katika nyumba ya babaetu; kwa sababu wewe u mwana wa mwanamke mwingine.
3 Ndipo Yeftha akawakimbia hao nduguze, akakaa katika nchi ya Tobu; na watu mabaradhuli walikwenda na kutangamana na Yeftha, wakatoka kwenda pamoja naye.
4 Ikawa baadaye, wana wa Amoni wakapigana na Israeli.
5 Ikatukia, hapo wana wa Amoni walipopigana na Israeli, wazee wa Gileadi wakaenda kumtwaa huyo Yeftha katika ile nchi ya Tobu;
6 wakamwambia Yeftha, Njoo wewe uwe kichwa chetu, ili tupate kupigana na wana wa Amoni.
7 Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi, Je! Ninyi hamkunichukia mimi na kunifukuza nitoke katika nyumba ya baba yangu? Basi kwani kunijilia hivi sasa wakati mlio katika taabu?
8 Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Kwa ajili ya hayo sasa tumegeuka kukuelekea wewe tena, ili uende pamoja nasi na kupigana na wana wa Amoni, nawe utakuwa kichwa chetu juu ya wenyeji wote wa Gileadi.
9 Basi Yeftha akawaambia wazee wa Gileadi Kwamba mwanirejeza kwetu tena ili kupigana na wana wa Amoni, naye Bwana akiwatoa mbele yangu, je! Mimi nitakuwa kichwa chenu?
10 Wazee wa Gileadi wakamwambia Yeftha, Yeye Bwana atakuwa shahidi kati yetu; hakika yetu tutafanya sawasawa na neno lako.
11 Ndipo Yeftha akaenda pamoja na wazee wa Gileadi, na hao watu wakamfanya awe kichwa, tena mkuu, juu yao; naye Yeftha akanena maneno yake yote mbele ya Bwana huko Mispa.
12 Basi Yeftha akatuma wajumbe waende kwa mfalme wa wana wa Amoni akasema, Je! Wewe una nini nami, hata umenijilia kupigana juu ya nchi yangu?
13 Mfalme wa wana wa Amoni akawajibu hao wajumbe wa Yeftha Kwa sababu Israeli waliitwaa nchi yangu, hapo walipokwea kutoka katika nchi ya Misri, tokea Arnoni mpaka Yaboki, na hata Yordani; basi sasa rudisha hizo nchi tena pasipo matata.
14 Yeftha akatuma wajumbe mara ya pili waende kwa huyo mfalme wa wana wa Amoni;
15 akamwambia, Yeftha akuambia hivi; Israeli hakuitwaa nchi ya Moabu, wala nchi ya wana wa Amoni;
16 lakini hapo walipokwea kutoka Misri, na Israeli walienenda katika bara hata kuifikilia Bahari ya Shamu, na kufikilia Kadeshi;
17 ndipo Israeli wakatuma wajumbe waende kwa mfalme wa Edomu, wakisema, Nakuomba sana unipe ruhusa nipite katika nchi yako; lakini mfalme wa Edomu hakusikia. Ni vivyo wakampelekea wajumbe mfalme wa Moabu; wala yeye hakukubali; basi Israeli wakakaa katika Kadeshi.
18 Kisha akaenda nyikani na kuizunguka hiyo nchi ya Edomu, na nchi ya Moabu, nao wakapita upande wa mashariki wa nchi ya Moabu, wakapanga marago upande wa pili wa Arnoni; wala hawakuingia ndani ya mpaka wa Moabu, kwa maana Arnoni ilikuwa ni mpaka wa Moabu.
19 Kisha Israeli wakatuma wajumbe waende kwa Sihoni mfalme wa Waamori, mfalme wa Heshboni: Israeli wakamwambia, Twakuomba utupe ruhusa tupite katika nchi yako, mpaka mahali pangu.
20 Lakini huyo Sihoni hakuwaamini Israeli ili wapite ndani ya mpaka wake; bali Sihoni akawakutanisha watu wake wote, nao wakapanga kambi katika Yahasa, wakapigana na Israeli.
21 Bwana, Mungu wa Israeli, akamtia Sihoni na watu wake wote mikononi mwa Israeli, nao wakawapiga; basi Israeli wakaimiliki hiyo nchi ya Waamori, wenye kukaa nchi hiyo.
22 Nao wakaumiliki mpaka wote wa Waamori, tokea Arnoni hata Yaboki, tokea hiyo bara hata Yordani.
23 Basi sasa yeye Bwana, Mungu wa Israeli, amewapokonya Waamori watoke mbele ya watu wake Israeli, na wewe wataka kuwatamalaki?
24 Je! Wewe hutakitamalaki hicho ambacho huyo Kemoshi mungu wako akupa kukitamalaki? Kadhalika, awaye yote ambaye Bwana, Mungu wetu, amemfukuza atoke mbele yetu hao ndio tutakaowatamalaki.
25 Na wewe sasa, je! U mwema kuliko Balaki mwana wa Sipori, huyo mfalme wa Moabu, kwa lo lote? Je! Yeye alishindana na Israeli, au kupigana nao?
26 Wakati Israeli waliokuwa wakikaa Heshboni na miji yake, na katika Aroeri na miji yake, na katika miji hiyo yote iliyo huko kando ya Arnoni, muda wa miaka mia tatu; mbona ninyi hamkuipata tena katika majira hayo?
27 Basi mimi sikukufanyia wewe dhambi, lakini wewe unanitenda uovu kwa kupigana nami; yeye Bwana, yeye Mwamuzi, na awe mwamuzi hivi leo kati ya wana wa Israeli na wana wa Amoni.
28 Lakini mfalme wa wana wa Amoni hakuyasikiza hayo maneno ya Yeftha aliompelekea.
29 Ndipo roho ya Bwana ikamjilia juu yake Yeftha, naye akapita katika Gileadi na Manase, akapita na katika Mispa ya Gileadi, na kutoka hapo Mispa ya Gileadi akapita kuwaendea wana wa Amoni.
30 Naye Yeftha akamwekea Bwana nadhiri, akasema, Kwamba wewe utawatia wana wa Amoni mkononi mwangu kweli,
31 ndipo itakuwa ya kwamba, kile kitakachotoka katika milango ya nyumba yangu kunilaki, hapo nitakaporudi na amani kutoka kwa hao wana wa Amoni, kitu hicho kitakuwa ni cha Bwana, nami nitakisongeza kiwe sadaka ya kuteketezwa.
32 Basi Yeftha akavuka kuwaendea wana wa Amoni ili kupigana nao; naye Bwana akawaua mkononi mwake.
33 Akawapiga kutoka Aroeri hata kufikilia Minithi, miji ishirini, na mpaka Abel-keramimu, akawapiga kwa machinjo makuu mno. Basi hivyo wana wa Amoni walishindwa mbele ya wana wa Israeli.
34 Kisha Yeftha akafika Mispa nyumbani kwake, na tazama, binti yake akamtokea kumlaki, na matari na machezo; naye alikuwa ni mwanawe pekee; hakuwa na mwingine, mwana wala binti, ila yeye.
35 Ikawa alipomwona akayararua mavazi yake, akasema, Ole wangu! Mwanangu, umenitweza sana, nawe u mmoja miongoni mwa hao wanisumbuao; kwa kuwa mimi nimemfunulia Bwana kinywa changu, nami siwezi kurejea nyuma.
36 Binti yake akamwambia, Baba yangu, wewe umemfunulia Bwana kinywa chako; basi unifanyie sawasawa na hayo yaliyotoka kinywani mwako; kwa kuwa yeye Bwana amekulipia kisasi juu ya adui zako, hao wana wa Amoni.
37 Kisha akamwambia baba yake, Basi na nifanyiwe neno hili; niache peke yangu muda wa miezi miwili, ili nipate kwenenda milimani, na kuombolea uanawali wangu, mimi na wenzangu.
38 Akamwambia, Haya, enda. Akampeleka mbali muda wa miezi miwili; naye akaenda zake, yeye na wenziwe, akauombolea uanawali wake huko milimani.
39 Basi ikawa mwisho wa hiyo miezi miwili, akarudi kwa babaye, aliyemtenda sawasawa na ile nadhiri yake aliyokuwa ameiweka; naye alikuwa hajamjua mtu mume. Kisha ikawa desturi katika Israeli,
40 kwamba binti za Israeli waende mwaka baada ya mwaka ili kumkumbuka huyo mwana wa Yeftha, Mgileadi, siku nne katika mwaka.

Waamuzi 12


1 Kisha watu wa Efraimu walikutana pamoja na kupita kwenda upande wa kaskazini; wakamwambia Yeftha, Kwa nini wewe kuvuka kwenda kupigana na wana wa Amoni, nawe hukutuita sisi kwenda pamoja nawe? Tutaipiga moto nyumba yako juu yako.
2 Yeftha akawaambia, Mimi na watu wangu tulikuwa na matata makubwa na wana wa Amoni; nami hapo nilipowaita ninyi, hamkuniokoa na mikono yao.
3 Nami nilipoona ya kuwa ninyi hamniokoi, niliuhatirisha uhai wangu, na kuvuka ili nipigane na wana wa Amoni, Bwana naye akawatia mkononi mwangu; basi kwa nini ninyi kunijia hivi leo kutaka kupigana nami?
4 Ndipo Yeftha akawakutanisha watu wote wa Gileadi, na kupigana na Efraimu; na hao watu wa Gileadi wakawapiga Efraimu, kwa sababu walisema, Ninyi Wagileadi ni watoro mliotoroka Efraimu, mnaokaa kati ya Efraimu, na kati ya Manase.
5 Nao Wagileadi wakavishika vivuko vya Yordani kinyume cha hao Waefraimu; kisha ilikuwa, hapo watoro waliotoroka Efraimu mmojawapo aliposema Niache nivuke, hao watu wa Gileadi wakamwambia, Je! Wewe u Mwefraimu? Kwamba alisema, La;
6 ndipo wakamwambia, Haya, tamka sasa neno hili, Shibolethi; naye akasema, Sibolethi; kwa maana hakuweza kufanya midomo yake kutamka neno hilo sawasawa; ndipo wakamshika, na kumwua hapo penye vivuko vya Yordani; basi wakaanguka wakati huo watu arobaini na mbili elfu wa Efraimu.
7 Huyo Yeftha akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka sita. Ndipo akafa Yeftha, Mgileadi, akazikwa katika miji ya Gileadi mmojawapo.
8 Baada yake huyo, Ibzani wa Bethlehemu akawa mwamuzi wa Israeli.
9 Alikuwa na wana thelathini; na binti thelathini akawapeleka waende mahali pengine, kisha akaleta wanawake thelathini kutoka mahali pengine kwa ajili ya hao wanawe. Akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka saba.
10 Huyo Ibzani akafa, akazikwa huko Bethlehemu.
11 Baada yake huyo, Eloni, Mzabuloni, akawa mwamuzi wa Israeli akawaamua Israeli muda wa miaka kumi.
12 Huyo Eloni, Mzabuloni, akafa, akazikwa katika Aiyaloni katika nchi ya Zabuloni.
13 Baada yake huyo, Abdoni mwana wa Hileli, Mpirathoni, akawa mwamuzi wa Israeli.
14 Naye alikuwa na wana arobaini, na wajukuu thelathini, waliokuwa wakipanda wana-punda sabini; akawa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka minane.
15 Huyo Abdoni mwana wa Hileli, Mpirathoni, akafa, akazikwa huko Pirathoni katika nchi ya Efraimu, katika nchi ya vilima ya Waamaleki.

Waamuzi 13


1 Wana wa Israeli wakafanya tena yaliyo mabaya mbele za macho ya Bwana, Bwana akawatia katika mikono ya Wafilisti, muda wa miaka arobaini.
2 Palikuwa na mtu mmoja wa Sora, wa jamaa ya Wadani; jina lake akiitwa Manoa; na mkewe alikuwa tasa, hakuzaa watoto.
3 Malaika wa Bwana akamtokea yule mwanamke, akamwambia, Tazama, wewe sasa u tasa, huzai; lakini utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume.
4 Basi sasa, jihadhari, nakuomba, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi;
5 kwani tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; na wembe usipite juu ya kichwa chake; maana mtoto huyo atakuwa mnadhiri wa Mungu tangu tumboni; naye ataanza kuwaokoa Israeli na mikono ya Wafilisti.
6 Ndipo yule mwanamke akaenda akamwambia mume wake, akisema, Mtu wa Mungu alinijia, na uso wake ulikuwa kama uso wa malaika wa Mungu, wa kutisha sana; nami sikumwuliza, Umetoka wapi? Wala hakuniambia jina lake;
7 lakini aliniambia, Tazama, utachukua mimba, nawe utamzaa mtoto mwanamume; basi sasa, usinywe divai wala kileo, wala usile kitu kilicho najisi. Maana mtoto huyo atakuwa Mnadhiri wa Mungu tangu tumboni, hata siku ya kufa kwake.
8 Ndipo huyo Manoa akamwomba Bwana, akisema, Ee Bwana, nakuomba, yule mtu wa Mungu uliyemtuma na aje kwetu mara ya pili, atufundishe hayo yatupasayo kumfanyia huyo mtoto atakayezaliwa.
9 Mungu akasikiza sauti ya Manoa; naye malaika wa Mungu akamwendea yule mwanamke tena alipokuwa anaketi shambani; lakini mumewe, Manoa, hakuwapo pamoja naye.
10 Basi huyo mwanamke akaenda haraka, akapiga mbio, na kumwambia mumewe, akisema, Tazama, huyo mtu amenitokea, huyo aliyenijilia siku ile.
11 Basi Manoa akainuka, akamwandama mkewe, na kumfikilia mtu huyo, akamwuliza, Je! Wewe ndiwe mtu yule aliyenena na huyu mwanamke? Akasema, Naam, ni mimi.
12 Manoa akasema, Basi sasa hayo maneno yako yatakapotimia, je! Huyo mtoto atakuwa wa namna gani, na kazi yake itakuwa ni nini?
13 Malaika wa Mungu akamwambia Manoa, Katika hayo yote niliyomwambia huyo mwanamke na ajihadhari.
14 Asile kitu cho chote kitokacho katika mzabibu, wala asinywe divai, wala mvinyo, wala asile kitu cho chote kilicho najisi; hayo yote niliyomwamuru na ayatunze.
15 Kisha Manoa akamwambia huyo malaika wa Bwana, Nakuomba, tukuzuie, ili tupate kuandaa mwana-mbuzi kwa ajili yako.
16 Lakini malaika wa Bwana akamwambia Manoa, Ujapokuwa wanizuia, sitakula katika mkate wako; na kwamba wataka kufanya tayari sadaka ya kuteketezwa, inakupasa kumsongezea Bwana. Kwa kuwa Manoa hakujua ya kwamba yeye ni malaika wa Bwana.
17 Manoa akamwambia huyo malaika wa Bwana, Jina lako ni nani, ili kwamba hapo hayo maneno yako yatakapotimia nipate kukutukuza?
18 Huyo malaika wa Bwana akamwambia, Kwani wewe kuniuliza jina langu, kwa kuwa jina hilo ni la ajabu?
19 Basi Manoa akamtwaa yule mwana-mbuzi, pamoja na sadaka ya unga, akamtolea Bwana hapo juu ya mwamba; huyo malaika akatenda la ajabu; Manoa na mkewe wakaangalia.
20 Kwa maana, ikawa, mara huo mwali wa moto ulipopaa juu mbinguni kutoka pale madhabahuni, huyo malaika wa Bwana akapaa katika mwali wa moto wa madhabahu; nao Manoa na mkewe wakaangalia; wakainama kifudifudi.
21 Lakini malaika wa Bwana hakumtokea Manoa tena, wala mkewe. Ndipo Manoa alipojua ya kwamba ndiye malaika wa Bwana.
22 Manoa akamwambia mkewe, Hakika yetu tutakufa sisi, kwa sababu tumemwona Mungu.
23 Lakini mkewe akamwambia, Kama Bwana angetaka kutuua hangepokea sadaka ya kuteketezwa, wala sadaka ya unga, mikononi mwetu, wala hangetuonyesha mambo hayo yote, wala hangetuambia mambo kama hayo wakati huu.
24 Basi yule mwanamke akamzaa mtoto mwanamume akamwita jina lake Samsoni, mtoto huyu akakua, Bwana akambarikia.
25 Roho ya Bwana ikaanza kumtaharakisha katika Mahane-dani, katikati ya Sora na Eshtaoli.

Waamuzi 14


1 Samsoni akatelemkia Timna, akaona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti.
2 Kisha akapanda, akawaambia baba yake na mama yake, akasema, Nimemwona mwanamke huko Timna, mmojawapo wa binti za Wafilisti; basi mnipatie, nimwoe.
3 Ndipo baba yake na mama yake wakamwambia, Je! Hapana mwanamke hata mmoja katika ndugu zako, au katika jamaa zangu zote, hata uende kumwoa mwanamke kwa hawa Wafilisti wasiotahiriwa? Samsoni akamwambia baba yake; Mnipatie huyo, kwa maana ananipendeza sana.
4 Lakini baba yake na mama yake hawakujua ya kuwa jambo hili ni la Bwana; maana alitaka kisa juu ya Wafilisti. Basi wakati ule Wafilisti walikuwa wakiwatawala Israeli.
5 Ndipo Samsoni na baba yake na mama yake wakatelemkia Timna, wakafika mashamba ya mizabibu huko Timna; na tazama, mwana-simba akamngurumia.
6 Roho ya Bwana ikamjilia kwa nguvu, naye akampasua kana kwamba anampasua mwana-mbuzi, wala hakuwa na kitu cho chote mkononi mwake; lakini hakuwaambia baba yake na mama yake aliyoyafanya.
7 Basi akatelemka na kuzungumza na huyo mwanamke; naye akampendeza Samsoni sana.
8 Kisha baadaye akarudi ili kumtwaa, naye akageuka kando kuuangalia mzoga wa huyo simba; na tazama, nyuki wengi walikuwamo ndani ya mzoga wa simba, na asali.
9 Akatwaa asali mikononi mwake akaenda mbele, huku akila alipokuwa akienenda, akawafikilia babaye na mamaye, akawapa, nao wakala; lakini hakuwaambia ya kuwa ameitwaa hiyo asali katika mzoga wa simba.
10 Basi babaye akamtelemkia huyo mwanamke; Samsoni naye akafanya karamu huko; kwa kuwa vijana ndivyo walivyokuwa wakifanya.
11 Basi ikawa hapo walipomwona, wakamletea wenziwe thelathini, wawe pamoja naye.
12 Samsoni akawaambia, Mimi nitawategea ninyi kitendawili; kama mwaweza kunionyesha katika hizo siku saba za karamu, na kukitambua, ndipo hapo nitawapa mavazi thelathini ya kitani na mavao mengine thelathini;
13 lakini msipoweza kunionyesha ndipo hapo ninyi mtanipa mimi mavazi thelathini ya kitani na mavao mengine thelathini. Basi wakamwambia, Haya, tega kitendawili chako, ili tupate kukisikia.
14 Naye akawaambia, Katika huyo mwenye kula kikatoka chakula, Katika huyo mwenye nguvu ukatoka utamu.
15 Ikawa kwa siku ya saba, wakamwambia mkewe Samsoni, Mbembeleze mumeo, ili atuonyeshe hicho kitendawili, tusije tukakuteketeza moto wewe na nyumba ya baba yako; je! Mmetuita ili mpate kuichukua mali yetu? Je! Sivyo?
16 Basi mkewe Samsoni akalia mbele yake, akasema, Wewe wanichukia tu, wala hunipendi; wewe umewategea kitendawili hao wana wa watu wangu, nawe hukuniambia mimi. Naye akamwambia, Angalia, sikumwambia baba yangu wala mama yangu, nami nikuambie wewe?
17 Naye akalia mbele yake hizo siku saba, wakati ulioendelea karamu yao; basi ikawa siku ya saba akamwambia, kwa sababu alikuwa akimsisitiza sana; naye akawaambia wale wana wa watu wake hicho kitendawili.
18 Nao watu wa mji wakamwambia siku ya saba kabla ya jua kuchwa,Ni kitu gani kilicho tamu kuliko asali? Ni kitu gani kilicho na nguvu kuliko simba? Naye akawaambia, kwamba hamkulima na mtamba wangu,Hamngekitambua kitendawili changu.
19 Roho ya Bwana ikamjilia juu yake kwa nguvu, naye akatelemkia Ashkeloni, akapiga watu waume thelathini katika watu hao, na kuzitwaa nyara zao, na kuwapa hao waliokitambua kitendawili mavao hayo. Hasira zake zikamwaka, naye akakwea kwenda nyumbani kwa baba yake.
20 Lakini huyo mke wa Samsoni aliozwa mwenzake, ambaye alikuwa amemtendea kama rafikiye.

Waamuzi 15


1 Lakini ikawa baadaye, wakati wa mavuno ya ngano Samsoni akaenda kumtazama mkewe, akamchukulia mwana-mbuzi; akasema, Nitaingia chumbani kwa mke wangu. Lakini baba yake mwanamke hakumwacha kuingia.
2 Baba yake akasema, Hakika mimi nalidhani ya kuwa umemchukia kabisa; basi nalimpa rafiki yako. Je! Ndugu yake mdogo mzuri kuliko yeye? Tafadhali, mtwae huyo badala yake.
3 Samsoni akasema, Safari hii nitakuwa sina hatia katika habari za hawa Wafilisti, hapo nitakapowadhuru.
4 Samsoni akaenda akakamata mbweha mia tatu; kisha akatwaa vienge vya moto akawafunga mbweha mkia kwa mkia, akatia kienge kati ya kila mikia miwili.
5 Alipokwisha kuviwasha moto vile vienge, akawaachia mbweha kati ya ngano ya Wafilisti, akayateketeza matita, na ngano, hata na mashamba ya mizeituni.
6 Ndipo Wafilisti wakasema, Ni nani aliyetenda hivi? Wakasema, Ni huyo Samsoni, mkwewe yule Mtimna, kwa sababu alimchukua mkewe akampa mwenzake. Wafilisti wakaenda wakamteketeza yeye na baba yake kwa moto.
7 Samsoni akawaambia, Ikiwa ninyi mnafanya mambo kama hayo, hakika nitajilipiza kisasi juu yenu, na baadaye nitakoma.
8 Akawapiga upeo, mapigo makuu sana, kisha akatelemka akakaa katika ufa wa jabali la Etamu.
9 Basi Wafilisti wakapanda wakapiga kambi yao katika Yuda, wakajieneza katika Lehi.
10 Watu wa Yuda wakasema, Mbona mmekuja kupigana nasi? Wakasema, Tumepanda ili kumfunga Samsoni, kumtenda yeye kama alivyotutenda sisi.
11 Ndipo watu elfu tatu wa Yuda wakatelemka hata ule ufa wa jabali la Etamu, wakamwambia Samsoni, Je! Hujui ya kuwa Wafilisti wanatutawala? Ni nini hii, basi, uliyotutenda? Akawaambia, Kadiri ile walivyonitenda mimi, ndivyo nilivyowatenda wao.
12 Wakamwambia, Tumeshuka ili kukufunga, tupate kukutia katika mikono ya Wafilisti. Samsoni akawaambia, Niapieni ya kwamba ninyi wenyewe hamtaniangukia.
13 Wakamwambia, wakisema, Vema, lakini tutakufunga sana, na kukutia katika mikono yao; lakini hakika hatutakuua. Basi wakamfunga kwa kamba mbili mpya, wakamchukua kutoka huko jabalini.
14 Alipofika Lehi, Wafilisti wakapiga kelele walipokutana naye; ndipo roho ya Bwana ikamjia kwa nguvu, na zile kamba zilizokuwa juu ya mikono yake zikawa kama kitani iliyoteketezwa kwa moto, na vile vifungo vyake vikaanguka mikononi mwake.
15 Naye akaona mfupa mbichi wa taya ya punda, akautwaa, akapiga watu elfu kwa mfupa huo;
16 Samsoni akasema, Kwa taya ya punda chungu juu ya chungu, Kwa taya ya punda nimepiga watu elfu.
17 Ikawa, alipokuwa amekwisha kunena akautupa ule mfupa wa taya mkononi mwake; na mahali pale pakaitwa Ramath-lehi.
18 Kisha akaona kiu sana, akamwita Bwana akasema, Wewe umetupa wokovu huu kwa mkono wa mtumishi wako; na sasa nitakufa kwa kiu, na kuanguka katika mikono ya watu wasiotahiriwa.
19 Lakini Mungu akapasua mahali penye shimo palipo katika Lehi, pakatoka maji; naye alipokwisha kunywa, roho yake ikamrudia, akaburudika; kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Enhakore, napo pa katika Lehi hata hivi leo.
20 Naye akawa mwamuzi wa Israeli: katika siku za Wafilisti muda wa miaka ishirini.

Waamuzi 16


1 Samsoni akaenda Gaza, akaona huko mwanamke kahaba, akaingia kwake.
2 Watu wa Gaza wakaambiwa, ya kwamba, huyo Samsoni amekuja huku. Wakamzingira, wakamvizia usiku kucha, penye lango la mji, wakanyamaza kimya usiku kucha, wakisema, Na tungoje mpaka mapambazuko, ndipo tutamwua.
3 Basi Samsoni akalala hata usiku wa manane, akaondoka katikati ya usiku, akaishika milango ya lango la mji, na miimo yake miwili, akaing'oa pamoja na komeo lake, akajitwika mabegani, akavichukua hata kilele cha mlima ule unaokabili Hebroni.
4 Ikawa baada ya hayo akampenda mwanamke mmoja katika bonde la Soreki, jina lake akiitwa Delila.
5 Nao wakuu wa Wafilisti wakamwendea, wakamwambia, Mbembeleze, upate kujua asili ya nguvu zake nyingi, na jinsi tutakavyoweza kumshinda, tupate kumfunga na kumtesa; nasi tutakupa kila mtu fedha elfu na mia moja.
6 Delila akamwambia Samsoni, Tafadhali uniambie asili ya nguvu zako nyingi, na jinsi uwezavyo kufungwa, ili uteswe.
7 Samsoni akamwambia, Wakinifunga kwa kamba mbichi saba ambazo hazijakauka bado, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu.
8 Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamletea kamba mbichi saba zisizokauka, naye akamfunga nazo.
9 Na yule mwanamke alikuwa na watu katika chumba cha ndani, wakimwotea. Basi akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Ndipo akazikata zile kamba kama vile uzi wa pamba ukatwavyo ukiguswa na moto. Basi hiyo asili ya nguvu zake haikujulikana.
10 Delila akamwambia Samsoni, Tazama, umenidhihaki, na kuniambia uongo; sasa tafadhali, niambie, waweza kufungwa kwa kitu gani?
11 Akamwambia Wakinifunga tu kwa kamba mpya ambazo mtu hakufanya kazi nazo, hapo ndipo nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu.
12 Basi Delila akatwaa kamba mpya akamfunga nazo, akamwambia, Wafilisti wanakujia, Samsoni. Na wale wenye kuotea walikuwa katika chumba cha ndani. Naye akazikata, akazitupa kutoka mikononi mwake kama uzi.
13 Delila akamwambia Samsoni, Hata sasa umenidhihaki, umeniambia maneno ya uongo; niambie sasa, waweza kufungwa kwa kitu gani? Akamwambia, Ukivifuma hivi vishungi saba vya nywele za kichwa changu katika mtande wa nguo.
14 Basi akazifunga kwa msumari, akamwambia Samsoni, Wafilisti wanakujia. Naye akaamka usingizini, akaung'oa ule msumari, na ule mtande.
15 Mwanamke akamwambia, Wawezaje kusema, Nakupenda; na moyo wako haupo pamoja nami? Umenidhihaki mara hizi tatu, wala hukuniambia asili ya nguvu zako nyingi.
16 Ikawa, kwa vile alivyomsumbua kwa maneno yake kila siku, na kumwudhi, roho yake ikadhikika hata kufa.
17 Ndipo alipomwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akamwambia, Wembe haukupita juu ya kichwa changu kamwe; maana mimi nimekuwa Mnadhiri wa Mungu, tangu tumboni mwa mama yangu; nikinyolewa, ndipo nguvu zangu zitanitoka, nami nitakuwa dhaifu, nitakuwa kama wanadamu wenzangu.
18 Delila alipoona ya kuwa amemwambia yote yaliyokuwa moyoni mwake, akatuma mtu akawaita wakuu wa Wafilisti, akisema, Njoni huku mara hii tu, maana ameniambia yote aliyo nayo moyoni mwake. Ndipo wakuu wa Wafilisti wakamwendea wakachukua ile fedha mikononi mwao.
19 Naye akamlaza usingizi magotini pake. Kisha akamwita mtu akavinyoa vile vishungi saba vya nywele za kichwa chake; akaanza kumsumbua, nguvu zake zikamtoka.
20 Kisha akasema, Samsoni, Wafilisti wanakujia. Akaamka katika usingizi wake, akasema, Nitakwenda nje kama siku nyingine, na kujinyosha. Lakini hakujua ya kuwa Bwana amemwacha.
21 Wafilisti wakamkamata, wakamng'oa macho; wakatelemka naye mpaka Gaza, wakamfunga kwa vifungo vya shaba; naye alikuwa akisaga ngano katika gereza.
22 Lakini zile nywele za kichwa chake zikaanza kukua tena baada ya kunyolewa kwake.
23 Kisha wakuu wa Wafilisti wakakusanyika ili kumtolea sadaka Dagoni mungu wao, na kufurahi; maana walisema, Mungu wetu amemtia Samsoni adui wetu mikononi mwetu.
24 Na hao watu walipomwona wakamhimidi mungu wao, maana walisema, Mungu wetu amemtia mikononi mwetu huyu adui wetu, aliyeiharibu nchi yetu na kuwaua watu wengi miongoni mwetu.
25 Ikawa mioyo yao iliposhangilia, wakasema, Mwiteni Samsoni, ili atufanyie michezo. Basi wakamwita Samsoni atoke gerezani, akacheze mbele yao wakamweka katikati ya nguzo mbili.
26 Samsoni akamwambia yule kijana aliyemshika mkono, Niache nizipapase nguzo ambazo nyumba hii inazikalia, nipate kuzitegemea.
27 Basi nyumba ile ilikuwa imejaa watu waume kwa wake; na wakuu wote wa Wafilisti walikuwamo humo, na juu ya dari palikuwa na watu elfu tatu waume kwa wake waliokuwa wakitazama, wakati Samsoni alipocheza.
28 Samsoni akamwita Bwana, akasema, Ee Bwana MUNGU, unikumbuke, nakuomba, ukanitie nguvu, nakuomba, mara hii tu, Ee Mungu, ili nipate kujilipiza kisasi juu ya Wafilisti kwa ajili ya macho yangu mawili.
29 Kisha Samsoni akazishika nguzo mbili za katikati ambazo nyumba ile ilikaa juu yake, akazitegemea, moja kwa mkono wake wa kuume na moja kwa mkono wake wa kushoto.
30 Samsoni akasema; Na nife pamoja na hawa Wafilisti. Akainama kwa nguvu zake zote; ile nyumba ikawaangukia hao wakuu, na watu wote waliokuwa ndani yake. Basi wale watu aliowaua wakati wa kufa kwake walikuwa wengi kuliko wale aliowaua wakati wa uhai wake.
31 Ndipo ndugu zake, na watu wote wa nyumba ya baba yake wakatelemka, wakamtwaa wakamchukua, wakamzika kati ya Sora na Eshtaoli, katika kiwanja cha kuzikia cha Manoa baba yake. Naye alikuwa mwamuzi wa Israeli muda wa miaka ishirini.

Waamuzi 17


1 Wakati huo alikuwako mtu mmoja wa nchi ya vilima ya Efraimu, ambaye jina lake alikuwa akiitwa Mika.
2 Naye akamwambia mama yake, Hizo fedha elfu na mia moja ulizonyang'anywa, ambazo uliweka kiapo kwa ajili yake na kusema masikioni mwangu, tazama, ninazo mimi hizo fedha; ni mimi niliyezitwaa. Mama yake akasema, mwanangu na abarikiwe na Bwana.
3 Basi akamrudishia mama yake hizo fedha elfu na mia moja. Mama yake akasema, Mimi naziweka fedha hizi kabisa ziwe wakfu kwa Bwana, zitoke mkononi mwangu kwa ajili ya mwanangu, ili kufanya sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu; basi kwa hiyo nakurudishia wewe.
4 Basi hapo alipomrudishia mama yake hizo fedha, mama yake akatwaa fedha mia mbili, akampa fundi mwenye kusubu fedha, naye akafanya sanamu ya kuchonga kwazo, na sanamu ya kusubu; ambazo zilikuwa ndani ya nyumba ya Mika.
5 Basi mtu huyo Mika alikuwa na nyumba ya miungu, naye akafanya naivera, na kinyago, akamweka wakfu mmoja miongoni mwa wanawe, akawa kuhani wake.
6 Siku hizo hapakuwa na mfalme katika israeli; kila mtu alifanya hayo aliyoyaona kuwa ni mema machoni pake mwenyewe.
7 Alikuwako mtu mmoja hirimu aliyetoka Bethlehemu-yuda, wa jamaa ya Yuda, aliyekuwa ni Mlawi, naye akakaa huko hali ya ugeni.
8 Mtu huyo akatoka katika huo mji, katika Bethlehemu-yuda, ili aende kukaa hali ya ugeni hapo atakapoona mahali; akafikilia nchi ya vilima vilima ya Efraimu katika safari yake, hata nyumba ya huyo Mika.
9 Mika akamwuliza, Watoka wapi wewe? Akamwambia, Mimi ni Mlawi wa Bethlehemu-yuda, nami naenda kukaa hali ya ugeni po pote nitakapoona mahali.
10 Mika akamwambia, kaa pamoja nami, uwe kwangu baba, tena kuhani, nami nitakupa fedha kumi mwaka kwa mwaka, na nguo ya kuvaa, na vyakula. Basi huyo Mlawi akaingia ndani.
11 Huyo Mlawi aliridhika kukaa na mtu huyo; kisha huyo hirimu akawa kwake kama wanawe mmojawapo.
12 Basi Mika akamweka wakfu huyo Mlawi, huyo hirimu, naye akawa kuhani wake, akakaa nyumbani mwa Mika.
13 Ndipo Mika akasema, Sasa najua ya kwamba Bwana atanitendea mema, kwa kuwa nina Mlawi kuwa kuhani wangu.

Waamuzi 18


1 Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; tena katika siku hizo kabila ya Wadani wakajitafutia urithi wapate mahali pa kukaa; maana hata siku hiyo urithi wao haujawaangukia kati ya kabila za Israeli.
2 Basi wana wa Dani wakatuma watu wa jamaa zao, watu watano katika hesabu yao yote, watu mashujaa, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli, ili kuipeleleza hiyo nchi, kuiaua; wakawaambia, Haya, endeni mkaikague nchi hii; basi wakaifikilia nchi ya vilima vilima ya Efraimu, hata nyumba ya huyo Mika, Wakalala huko.
3 Basi hapo walipokuwa karibu na nyumba ya Mika, wakatambua sauti yake huyo hirimu, huyo Mlawi; ndipo wakageuka wakaenda kuko, na kumwuliza, Je! Ni nani aliyekuleta wewe huku? Nawe wafanya nini mahali hapa? Una kazi gani hapa?
4 Naye akawaambia, Hivi na hivi ndivyo alivyonifanyia Mika, ameniajiri, nami nimekuwa kuhani wake.
5 Nao wakamwambia, Tafadhali tutakie shauri la Mungu, ili tupate kujua kwamba njia yetu tuiendeayo itafanikiwa.
6 Kuhani akawaambia, Haya endeni na amani; njia mnayoiendea i mbele za Bwana.
7 Ndipo hao watu watano wakaenda zao, wakafika Laisha, wakawaona wale watu waliokuwamo ndani yake, jinsi walivyokaa salama salimini kwa mfano wa walivyokaa hao Wasidoni, wenye starehe na hifadhi, kwa maana hapakuwa na mtu katika nchi hiyo aliyekuwa na amri, aliyeweza kuwatweza katika neno lo lote, nao walikuwa wa mbali na hao Wasidoni, wala hawakuwa na shughuli na mtu ye yote.
8 Kisha wakawarudia ndugu zao huko Sora na Eshtaoli; ndugu zao wakawauliza; Haya, mna habari gani?
9 Wakasema, Haya, inukeni, twende tukapigane nao; kwa maana tumeiona hiyo nchi nayo ni nchi nzuri sana; nanyi, je! Mwanyamaa tu? Msiwe wavivu kwenda, na kuingia, ili mpate kuimiliki nchi hiyo.
10 Hapo mtakapokwenda mtawafikilia watu wakaao salama salimini, na hiyo nchi nayo ni kubwa; kwa kuwa Mungu ameitia mikononi mwenu; ni mahali ambapo hapana kupungukiwa na kitu cho chote kilicho duniani.
11 Basi wakatoka hapo watu mia sita waliovaa silaha za vita, wa jamaa ya Wadani, kutoka Sora, na kutoka Eshtaoli.
12 Wakakwea juu na kupiga kambi huko Kiriath-yearimu, katika Yuda; kwa sababu hiyo wakapaita mahali pale jina lake Mahane-dani hata hivi leo; tazama, ni hapo nyuma ya Kiriath-yearimu.
13 Nao wakapita huko hata hiyo nchi ya vilima vilima ya Efraimu, wakafikilia nyumba ya huyo Mika.
14 Ndipo hao watu watano waliokwenda kuipeleleza nchi ya Laisha wakajibu, na kuwaambia ndugu zao Je! Ninyi mwajua ya kwamba mna naivera ndani ya nyumba hizi, na kinyago na sanamu ya kuchonga, na sanamu ya kusubu? Basi sasa fikirini iwapasayo kufanya.
15 Basi wakageuka wakaenda kuko, wakafikilia nyumba ya huyo hirimu, Mlawi, hata hiyo nyumba ya Mika, nao wakamwuliza habari za hali yake.
16 Hao watu mia sita wenye kuvaa silaha zao za vita, waliokuwa ni wana wa Dani, wakasimama penye maingilio ya lango.
17 Na hao watu watano waliokwenda kuipeleleza hiyo nchi wakakwea juu, wakaingia ndani, na kuitwaa hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu; na huyo kuhani akasimama penye maingilio ya lango pamoja na hao watu waume sita mia wenye kuvaa silaha za vita.
18 Nao hapo walipoingia ndani ya nyumba ya Mika, na kuileta hiyo sanamu ya kuchonga, na hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kusubu, huyo kuhani akawauliza, Je! Mwafanya nini ninyi?
19 Wao wakamwambia, Nyamaza wewe, weka mkono wako kinywani mwako, uende pamoja nasi, uwe kwetu baba, tena kuhani; je! Ni vema kwako kuwa kuhani kwa ajili ya nyumba ya mtu mmoja, au kuwa kuhani kwa ajili ya kabila na jamaa katika Israeli?
20 Huyo kuhani moyo wake ukafurahi, naye akaitwaa hiyo naivera, na kile kinyago, na hiyo sanamu ya kuchonga, akaenda katikati ya hao watu.
21 Basi wakageuka wakaenda zao, lakini watoto wadogo na wanyama wao wa mifugo, na vyombo vyao, wakawatanguliza mbele yao.
22 Walipokuwa wamekwenda kitambo kizima kutoka nyumba ya Mika, wale watu waliokuwa katika nyumba zilizokuwa karibu na nyumba ya Mika walikutana, wakawaandama na kuwapata hao wana wa Dani.
23 Wakawapigia kelele wana wa Dani. Nao wakageuza nyuso zao na kumwambia Mika, Una nini wewe, hata ukaja na mkutano namna hii?
24 Akasema, Ninyi mmeichukua miungu niliyoifanya, na huyo kuhani, nanyi mmekwenda zenu, nami nina nini tena? Basi imekuwaje ninyi kuniuliza, Una nini wewe?
25 Hao wana wa Dani wakamwambia, Hiyo sauti yako isisikiwe kati yetu, wasije walio na hasira wakakuangukia, nawe ukapotewa na uhai wako, pamoja na uhai wa watu wa nyumbani mwako.
26 Basi wana wa Dani wakaenda zao; naye Mika alipoona ya kuwa ni wenye nguvu kumshinda yeye, akageuka akarudi nyumbani kwake.
27 Nao wakakitwaa hicho alichokuwa amekifanya Mika, na kuhani aliyekuwa naye nao wakafikilia Laisha, kwenye watu waliokuwa wenye starehe na hifadhi, wakawapiga kwa makali ya upanga; wakaupiga moto mji wao.
28 Wala hakuwako mwokozi, kwa sababu huo mji ulikuwa ni mbali sana na Sidoni, nao hawakuwa na shughuli na mtu awaye yote; na mji huo ulikuwa katika hilo bonde lililo karibu na Bethrehobu. Nao wakaujenga huo mji na kukaa humo.
29 Wakauita mji jina lake Dani, kwa kuliandama jina la baba yao Dani, aliyezaliwa kwake Israeli; lakini jina la mji huo hapo kwanza ulikuwa ukiitwa Laisha.
30 Kisha wana wa Dani wakajisimamishia hiyo sanamu ya kuchonga; na Yonathani mwana wa Gershomu, mwana wa Musa, yeye na wanawe walikuwa ni makuhani katika kabila ya Wadani hata siku ya kuchukuliwa mateka hiyo nchi.
31 Basi wakajisimamishia hiyo sanamu ya kuchonga aliyoifanya Mika, wakati wote ile nyumba ya Mungu ilipokuwako huko Shilo.

Waamuzi 19


1 Ikawa katika siku hizo, hapo kulipokuwa hapana mfalme katika Israeli, alikuwapo Mlawi mmoja aliyekuwa akikaa hali ya ugeni upande wa mbele wa nchi ya vilima vilima ya Efraimu, aliyejitwalia suria katika Bethlehemu-yuda.
2 Kisha huyo suria yake akaandama ukahaba kinyume chake, kumwacha kwenda nyumbani kwa baba yake huko Bethlehemu-yuda, akakaa kuko muda wa miezi minne.
3 Kisha mumewe akainuka akamfuata, aseme naye kwa upendo, ili apate kumrudisha tena, naye alikuwa na mtumishi wake pamoja naye na punda wawili; huyo mwanamke akamkaribisha katika nyumba ya baba yake; naye baba yake alipomwona akafurahi kuonana naye.
4 Kisha mkwewe, babaye huyo mwanamke, akamzuia; akakaa naye siku tatu; basi wakala na kunywa na kulala kuko.
5 Kisha ilikuwa siku ya nne, wakaamka asubuhi na mapema, naye akaondoka ili aende zake; baba yake huyo mwanamke akamwambia mkwewe, Tuza moyo wako, ule chakula kidogo, kisha baadaye mtakwenda zenu.
6 Basi wakaketi, wakala na kunywa wote wawili pamoja; kisha baba yake mwanamke akamwambia huyo mtu, Uwe radhi, tafadhali, ukae usiku kucha, na moyo wako na ufurahi.
7 Yule mtu akainuka ili aondoke; lakini mkwewe akamsihi-sihi, naye akalala kuko tena.
8 Basi akaamka asubuhi na mapema siku ya tano ili aende zake; na baba yake mwanamke akasema, Tuza moyo wako, tafadhali, ukae hata jua lipinduke; nao wakala chakula wote wawili.
9 Kisha hapo mtu huyo alipoinuka ili aende zake, yeye na suria yake, na mtumishi wake, huyo mkwewe, baba yake mwanamke, akamwambia, Tazama mchana wakaribia jioni, tafadhali kaa usiku kucha; tazama mchana wakaribia mwisho wake, lala hapa, ili moyo wako ufurahi; hata kesho uende zako asubuhi na mapema, ili upate kwenda kwenu.
10 Lakini huyo mtu hakukubali kukaa usiku huo, ila akainuka, akaenda zake, akafika mkabala wa Yebusi (huo ndio Yerusalemu); nao walikuwako pamoja naye punda wawili waliotandikwa; suria yake naye alikuwa pamoja naye.
11 Basi hapo walipokuwa karibu na Yebusi, mchana ulikuwa umeendelea mno; yule mtumishi akamwambia bwana wake, Haya, tafadhali, tugeuke kando na kuingia mji huu wa Wayebusi, tulale humu.
12 Bwana wake akamwambia, Hatutageuka sisi kuingia mji wa wageni, ambao si wa wana wa Israeli; lakini tutapita mpaka Gibea.
13 Kisha akamwambia mtumishi wake, Haya, tuifikilie miji hii mmojawapo nasi tutalala katika Gibea au katika Rama.
14 Basi wakashika njia kwenda zao mbele; jua likawachwea walipokuwa karibu na Gibea, ambao ni mji wa Benyamini.
15 Wakageuka huko, wapate kuingia na kulala katika Gibea; akaingia ndani, akaketi katika njia kuu ya mji; kwa kuwa hapakuwa na mtu awaye yote aliyewakaribisha nyumbani kwake kulala.
16 Kisha, tazama, akatokea mtu mume mzee, atoka kazini kwake shambani, wakati wa jioni; mtu huyo alikuwa ni wa ile nchi ya vilima vilima ya Efraimu, naye alikuwa anakaa katika Gibea hali ya ugeni lakini wenyeji wa mahali hapo walikuwa Wabenyamini.
17 Naye alipovua macho yake, akamwona huyo mtu msafiri katika njia kuu ya mji; huyo mzee akamwuliza, Waenda wapi wewe? Nawe watoka wapi?
18 Akamwambia, Sisi twapita hapa kutoka Bethlehemu-yuda, twaenda huko upande wa mbali wa nchi ya vilima vilima ya Efraimu; ndiko nilikotoka nami nilikwenda Bethlehemu-yuda; nami sasa naiendea nyumba ya Bwana wala hapana mtu anikaribishaye nyumbani mwake.
19 Walakini nyasi tunazo, na chakula cha hawa punda zetu; mkate pia tunao na divai kwa mimi na huyu kijakazi wako, na kwa huyu kijana aliye pamoja nasi watumishi wako; hapana uhitaji wa kitu cho chote.
20 Kisha huyo mzee alisema, Na iwe amani kwako; lakini na haya yaliyokupungukia na yawe juu yangu mimi lakini usilale njiani.
21 Basi akamtia ndani ya nyumba yake, akawapa punda chakula; nao wakaosha miguu, wakala na kunywa.
22 Hapo walipokuwa wakifurahisha mioyo yao, tazama, watu wa mji huo, watu mabaradhuli wakaizingira hiyo nyumba pande zote, wakagonga mlango; wakasema na huyo mwenye nyumba, huyo mzee, na kumwambia, Mlete nje mtu yule aliyefika nyumbani kwako, ili tupate kumjua.
23 Naye mtu mwenye nyumba akawatokea hapo nje, na kuwaambia, La, sivyo, ndugu zangu nawasihi msifanye uovu jinsi hii; kwa kuwa mtu huyu ameingia ndani ya nyumba yangu, msifanye upumbavu huu.
24 Tazama, binti yangu yupo hapa, ni mwanamwali, na suria wake huyo mtu; nitawaleta hapa nje sasa nanyi watwezeni, na kuwatenda hayo myaonayo kuwa ni mema; lakini mtu huyu msimtende jambo la upumbavu namna hii.
25 Lakini hao watu hawakukubali kumsikia; basi mtu huyo akamshika suria wake, na kumleta nje kwao; nao wakamjua, na kumtenda uovu usiku kucha hata asubuhi kisha kulipoanza kupambauka wakamwacha aende zake.
26 Ndipo huyo mwanamke akaja alfajiri, akaanguka chini mlangoni pa nyumba ya mtu yule alimokuwamo bwana wake, hata kulipokucha.
27 Bwana wake akaondoka asubuhi, akaifungua milango ya nyumba, akatoka nje ili aende zake, na tazama, huyo mwanamke suria yake alikuwa ameanguka pale mlangoni pa nyumba, na mikono yake ilikuwa i pale kizingitini.
28 Akamwambia, Haya ondoka, twende zetu; lakini hakuna aliyemjibu; ndipo akamwinua akamweka juu ya punda; mtu huyo akaondoka, akaenda mahali pake mwenyewe.
29 Naye alipokwisha kuingia nyumbani mwake, akatwaa kisu, kisha akamshika huyo suria yake, akampasua kiungo kwa kiungo, vipande kumi na viwili akampeleka katika mipaka yote ya Israeli.
30 Basi ikawa, wote walioliona jambo hilo wakasema, Jambo kama hili halijatendeka wala kuonekana tangu siku hiyo wana wa Israeli walipokwea kutoka katika nchi ya Misri hata leo; haya, lifikirini, fanyeni shauri, mkanene.

Waamuzi 20


1 Ndipo wana wa Israeli walipotoka; na mkutano ukakutanika kama mtu mmoja, kutoka Dani hata Beer-sheba, pamoja na nchi ya Gileadi wakamkutanikia Bwana huko Mispa.
2 Hao wakuu wa watu, maana wakuu wa kabila zote za Israeli, wakajihudhurisha katika huo mkutano wa watu wa Mungu, watu waume mia nne elfu waendao kwa miguu, wenye kutumia upanga.
3 Basi wana wa Benyamini walipata habari ya kuwa wana wa Israeli wamekwea kwenda Mispa. Wana wa Israeli wakasema, Tuambieni huo uovu ulikuwaje kutendeka?
4 Huyo Mlawi, huyo mume wa mwanamke aliyeuawa, akajibu na kusema, Mimi nilifikilia Gibea ulio wa Benyamini mimi na suria yangu, ili tulale.
5 Nao watu waume wa Gibea wakaniondokea, na kuizingira hiyo nyumba pande zote juu yangu wakati wa usiku; walidhani kuniua, na suria wangu wakamtenza nguvu, hata amekufa.
6 Basi nikamtwaa huyo suria yangu, na kumkata vipande, na kumpeleka katika nchi yote ya urithi wa Israeli; kwa sababu wametenda maovu makuu na upumbavu katika Israeli.
7 Angalieni, ninyi wana wa Israeli nyote, sasa toeni maneno na mashauri yenu.
8 Basi watu hao wote waliinuka kama mtu mmoja, wakisema, Hatutakwenda, hata mmoja, hemani kwake, wala hatutaondoka, hata mmoja, kwenda nyumbani kwake.
9 Lakini jambo tutakalowatenda watu wa Gibea ni hili; tutakwea kwa kura kwenda kuupiga;
10 nasi tutatwaa watu kumi katika mia katika kabila zote za Israeli, na watu mia katika elfu, na watu elfu katika elfu kumi, ili waende kuwatwalia watu vyakula, ili kwamba, hapo watakapofika Gibea ya Benyamini wapate kutenda mfano wa upumbavu huo wote walioutenda wao katika Israeli.
11 Basi waume wote wa Israeli walikutana pamoja juu ya mji huo, walikuwa wanashikamana pamoja kama mtu mmoja.
12 Kisha kabila za Israeli wakatuma watu waende katika kabila yote ya Benyamini, wakasema, Je! Ni uovu gani huu uliokuwa kati yenu?
13 Basi sasa watoeni watu hao, hao mabaradhuli walio katika Gibea, ili kwamba tupate kuwaua, na kuuondoa uovu katika Israeli. Lakini Benyamini hawakukubali kuisikia sauti ya ndugu zao wana wa Israeli.
14 Lakini wana wa Benyamini wakakutanika huko Gibea kutoka katika miji yao, ili watoke kwenda kupiga vita juu ya wana wa Israeli.
15 Hao wana wa Benyamini walihesabiwa siku ile kutoka hiyo miji, watu waume ishirini na sita elfu waliotumia upanga, zaidi ya hao waliokaa Gibea, ambao walihesabiwa watu wateule mia saba.
16 Katika watu hao wote walikuwako watu waume mia saba waliochaguliwa, wenye shoto; kila mmoja alikuwa anaweza kuutupia unywele mawe kwa teo, wala asikose.
17 Nao watu wa Israeli, mbali na hao wa Benyamini, walihesabiwa kuwa ni watu waume mia nne elfu, wenye kutumia upanga; hao wote walikuwa ni watu wa vita.
18 Basi wana wa Israeli wakainuka, wakakwea kwenda Betheli, nao wakataka shauri kwa Mungu; wakasema, Ni nani atakayekwea kwenda vitani kwanza kwa ajili yetu juu ya wana wa Benyamini? Bwana akawaambia, Yuda atakwea kwanza.
19 Basi wana wa Israeli waliondoka asubuhi, wakapanga hema zao juu ya Gibea.
20 Watu wa Israeli walitoka ili wapigane na Benyamini; nao watu wa Israeli wakaviandaa vita juu yao huko Gibea.
21 Wana wa Benyamini wakatoka Gibea, wakaangamiza hata nchi watu ishirini na mbili elfu katika Israeli siku hiyo.
22 Lakini watu hao, watu wa Israeli, walijitia nguvu, wakaviandaa vile vita mara ya pili mahali pale walipojiandaa siku ya kwanza.
23 Wana wa Israeli wakakwea juu na kulia mbele za Bwana hata jioni; wakamwuliza Bwana, wakisema, Je! Niende nikaribie tena kupiga vita juu ya wana wa Benyamini ndugu yangu? Bwana akasema, Haya, kweeni, mwende kupigana naye.
24 Basi wana wa Israeli wakakaribia juu ya wana wa Benyamini siku ya pili.
25 Benyamini alitoka kupigana nao kutoka Gibea siku ya pili, wakaangamiza hata nchi watu kumi na nane elfu tena katika watu wa Israeli; hao wote walikuwa wenye kutumia upanga.
26 Ndipo wana Israeli wote, na hao watu wote, wakakwea, wakaenda Betheli, na kulia, wakaketi hapo mbele za Bwana, wakafunga siku hiyo hata jioni; nao wakasongeza sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani mbele za Bwana.
27 Kisha wana wa Israeli wakauliza kwa Bwana (kwa sababu sanduku la agano la Mungu lilikuwako huko siku hizo,
28 na Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni, alikuwa anasimama mbele ya hilo sanduku siku hizo), wakasema, Je! Nitoke tena niende kupigana na wana wa Benyamini ndugu yangu, au niache? Bwana akawaambia, Haya, kweeni; kwa kuwa kesho nitamtoa na kumtia mkononi mwako.
29 Basi Israeli akaweka watu wavizie kinyume cha Gibea kuuzunguka pande zote.
30 Basi wana wa Israeli wakakwea kwenda kupigana na wana wa Benyamini siku ya tatu, wakajipanga ili kupigana na Gibea, kama walivyofanya nyakati nyingine.
31 Nao wana wa Benyamini wakatoka waende kupigana nao, wakavutwa waende mbali na huo mji; kisha wakaanza kupiga na kuua katika hao watu, wapata kama watu thelathini wa Israeli, kama walivyofanya nyakati nyingine, katika hizo njia kuu, ambazo njia mojawapo huendelea Betheli, na njia ya pili huendelea Gibea, katika shamba.
32 Wana wa Benyamini wakasema, Wamepigwa mbele yetu kama kwanza. Lakini wana wa Israeli wakasema, Haya, na tukimbie, na kuwavuta wauache mji waende katika njia kuu.
33 Basi hao watu wote wa Israeli wakaondoka mahali pao wakajipanga huko Baal-tamari; na hao wenye kuvizia wa Israeli wakatoka mahali hapo walipokuwa, hata Maare-geba.
34 Kisha watu elfu kumi waliochaguliwa katika Israeli wote wakaja juu ya Gibea, na vile vita vilikuwa vikali sana; lakini hawakujua ya kuwa uovu ulikuwa karibu nao.
35 Bwana akampiga Benyamini mbele ya Israeli; na wana wa Israeli waliangamiza watu waume ishirini na tano elfu na mia moja, wa Benyamini siku hiyo; wote hao waliokuwa wenye kutumia upanga.
36 Basi wana wa Benyamini waliona kuwa wamepigwa; kwa kuwa watu wa Israeli wakaondoka mbele ya Benyamini, kwa sababu walikuwa wanawatumaini hao wenye kuvizia waliokuwa wamewaweka kinyume cha Gibea.
37 Hao wenye kuvizia wakafanya haraka, wakaurukia Gibea; na hao wenye kuvizia wakaenda wakaupiga huo mji wote kwa makali ya upanga.
38 Basi hiyo ishara iliyoaganwa kati ya watu wa Israeli na hao wenye kuvizia ilikuwa ni hii, kwamba wafanye lipande wingu kubwa la moshi kutoka katika huo mji.
39 Nao watu wa Israeli walipogeuka katika vile vita, Benyamini naye akaanza kupiga na kuwaua watu wa Israeli kama watu thelathini; kwani walisema, Hakika yetu wamepigwa mbele yetu, vile vile kama katika vile vita vya kwanza.
40 Lakini hapo hilo wingu lilipoanza kupanda kutoka katika mji, kama nguzo ya moshi, ndipo Wabenyamini wakaangalia nyuma, na tazama, huo mji mzima ulikuwa wapaa juu katika moshi kwenda mbinguni.
41 Ndipo watu wa Israeli wakageuka, na watu wa Benyamini walisitushwa; kwa kuwa waliona ya kwamba wamefikiliwa na uovu.
42 Kwa hiyo wakageuza maungo yao mbele ya wana wa Israeli kuelekea njia ya kwenda nyikani; lakini vile vita vikawaandamia kwa kasi; na hao waliotoka katika ile miji wakawaangamiza katikati yake.
43 Waliwazingira Wabenyamini pande zote na kuwafukuza, na kuwakanyaga-kanyaga hapo walipopumzika, hata kufikilia Gibea upande wa maawio ya jua.
44 Wakaanguka watu wa Benyamini watu kumi na nane elfu, hao wote walikuwa ni watu waume mashujaa.
45 Kisha wakageuka na kukimbia upande wa nyika hata kulifikilia jabali la Rimoni; nao wakaokota katika watu hao katika njia kuu watu waume elfu tano; wakawaandamia kwa kasi mpaka Gidomu, nako wakawapiga wengine wao watu elfu mbili.
46 Basi jumla ya watu wa Benyamini walioanguka siku ile walikuwa ni watu ishirini na tano elfu waliokuwa wanatumia upanga; wote hao walikuwa ni watu mashujaa.
47 Lakini watu waume mia sita wakageuka, wakakimbia upande wa nyikani mpaka jabali la Rimoni, wakakaa kwenye hilo jabali la Rimoni muda wa miezi minne.
48 Kisha watu wa Israeli wakageuka tena kuwaendea wana wa Benyamini, wakawapiga kwa makali ya upanga, huo mji mzima, na hao wanyama wa mji, na kila kitu walichokiona; tena miji yote waliyoiona wakaitia moto.

Waamuzi 21


1 Basi watu wa Israeli walikuwa wameapa huko katika Mispa, wakisema, Hapana mtu awaye yote kwetu sisi atakayemwoza binti yake kumpa Benyamini.
2 Basi hao watu wakafikilia Betheli, wakaketi kuko mbele ya Mungu hata jioni, nao wakainua sauti zao na kulia sana.
3 Wakasema, Ee Bwana, Mungu wa Israeli, kwani jambo hili kuwa katika Israeli, ya kwamba hivi leo ni kabila moja limepunguka katika Israeli?
4 Kisha ikawa siku ya pili yake, hao watu wakaamka asubuhi na mapema, wakajenga madhabahu huko, wakasongeza sadaka za kuteketezwa na sadaka za amani.
5 Wana wa Israeli wakasema, Katika hizi kabila zote za Israeli ni ipi isiyofika katika mkutano kumkaribia Bwana? Kwa maana walikuwa wameweka kiapo kikuu katika habari za huyo asiyefika kumkaribia Bwana huko Mispa, huku wakisema, Hakika yake atauawa huyo.
6 Nao wana wa Israeli wakaghairi kwa ajili ya ndugu yao Benyamini, wakasema, Kabila moja imekatiliwa mbali na Israeli hivi leo.
7 Tufanyeje sisi ili tuwapatie wake hao waliosalia, kwa kuwa tumeapa kwa Bwana ya kwamba hatutawapa binti zetu ili wawaoe?
8 Basi wakasema, Ni ipi katika kabila za Israeli ambayo haikufika mbele ya Bwana huko Mispa? Na tazama, hakuja mmoja maragoni aliyetoka Yabeshi gileadi aufikilie huo mkutano.
9 Kwa maana hapo watu walipohesabiwa, hakuwapo hata mtu mmoja katika wenyeji wa Yabesh-gileadi.
10 Basi mkutano walipeleka huko watu kumi na mbili elfu wa hao waliokuwa mashujaa sana, kisha wakawaamuru, wakisema, Endeni mkawapige wenyeji wa Yabesh-gileadi kwa makali ya upanga, na hata wanawake na watoto wadogo.
11 Na jambo mtakalotenda ni hili; mtamwangamiza kila mume kabisa, na kila mwanamke ambaye amelala na mume.
12 Nao wakapata katika wenyeji wa Yabesh-gileadi wanawali mia nne, ambao hawajamjua mtu mume kwa kulala naye; basi wakawaleta maragoni huko Shilo, ulioko katika nchi ya Kanaani.
13 Basi mkutano ukatuma watu na kunena na wana wa Benyamini waliokuwako huko katika jabali la Rimoni, wakawatangazia amani.
14 Basi Benyamini wakarudi wakati huo; nao wakawapa wale wanawake waliowaponya wali hai katika hao wanawake wa Yabesh-gileadi; lakini hawakuwatosha.
15 Nao watu wakaghairi kwa ajili ya Benyamini, kwa sababu Bwana alikuwa amefanya pengo katika hizo kabila za Israeli.
16 Ndipo hao wazee wa huo mkutano walisema, Je! Tufanyeje ili tuwapatie wake hao waliosalia, kwa kuwa wanawake wameangamizwa katika Benyamini?
17 Wakasema, Lazima kuwa urithi kwa hao wa Benyamini waliopona, isiwe kabila kufutika katika Israeli.
18 Lakini sisi hatuwezi kuwaoza binti zetu kwa maana wana wa Israeli walikuwa wameapa, wakisema, Na alaaniwe huyo atakayempa Benyamini mke.
19 Kisha wakasema, Angalieni, iko sikukuu ya Bwana mwaka baada ya mwaka katika Shilo, ulioko upande kaskazini wa Betheli, upande wa mashariki wa hiyo njia kuu iendeayo kutoka Betheli kwenda Shekemu, nao ni upande wa kusini wa Lebona.
20 Basi wakawaagiza hao wana wa Benyamini wakisema, Haya, endeni, mkaotee katika mashamba ya mizabibu,
21 mkaangalie, kisha tazameni, kwamba hao binti za Shilo watoka ili wacheze katika hiyo michezo, basi tokeni ninyi mizabibuni, nanyi kila mtu na amshike mkewe katika hao binti za Shilo, kisha rudini nchi ya Benyamini.
22 Kisha itakuwa, hapo baba zao au ndugu zao, watakapokuja kushitaki, sisi tutawaambia, Kwa ihisani yenu tupeni sisi; kwa kuwa hatukumtwalia kila mtu mkewe katika vita; wala ninyi hamkuwapa wao, au kama sivyo ninyi sasa mngekuwa na hatia.
23 Wana wa Benyamini wakafanya vivyo, wakajitwalia wake, sawasawa na hesabu yao, katika hao waliocheza, wakawachukua wakaenda nao; kisha wakaenda kuurudia urithi wao, na kuijenga miji na kuikaa.
24 Nao wana wa Israeli wakati huo wakaenda zao, kila mtu akaenda kwa kabila yake na kwa jamaa yake; nao wakatoka huko, waende kila mtu kuuendea urithi wake.
25 Siku hizo hapakuwa na mfalme katika Israeli; kila mtu alifanya yaliyokuwa ni mema machoni pake mwenyewe.