Yoshua

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24

Yoshua 1


1 Ikawa baada ya kufa kwake Musa, mtumishi wa Bwana, Bwana akamwambia Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa, akasema,
2 Musa mtumishi wangu amekufa; haya basi, ondoka, vuka mto huu wa Yordani; wewe na watu hawa wote, mkaende hata nchi niwapayo wana wa Israeli.
3 Kila mahali zitakapopakanyaga nyayo za miguu yenu, nimewapa ninyi, kama nilivyomwapia Musa.
4 Tangu jangwa hili na mlima huu, Lebanoni, mpaka mto ule mkubwa, mto wa Frati, nchi yote ya Wahiti, tena mpaka bahari ile kubwa upande wa machweo ya jua, hapo ndipo patakapokuwa mpaka wenu.
5 Hapatakuwa mtu ye yote atakayeweza kusimama mbele yako siku zote za maisha yako; kama nilivyokuwa pamoja na Musa, ndivyo nitakavyokuwa pamoja na wewe; sitakupungukia wala sitakuacha.
6 Uwe hodari na moyo wa ushujaa, maana ni wewe utakayewarithisha watu hawa nchi hii niliyowaapia baba zao ya kwamba nitawapa.
7 Uwe hodari tu na ushujaa mwingi, uangalie kutenda sawasawa na sheria yote aliyokuamuru Musa mtumishi wangu; usiiache, kwenda mkono wa kuume, au wa kushoto, upate kufanikiwa sana kila uendako.
8 Kitabu hiki cha torati kisiondoke kinywani mwako, bali yatafakari maneno yake mchana na usiku, upate kuangalia kutenda sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa humo; maana ndipo utakapoifanikisha njia yako, kisha ndipo utakapositawi sana.
9 Je! Si mimi niliyekuamuru? Uwe hodari na moyo wa ushujaa; usiogope wala usifadhaike; kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yu pamoja nawe kila uendako.
10 Ndipo Yoshua akawaamuru maakida wa watu, akisema,
11 Piteni katikati ya matuo, mkawaamuru hao watu, mkisema, Fanyeni tayari vyakula; kwa maana baada ya siku tatu mtavuka mto huu wa Yordani, ili kuingia na kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wenu, mpate kuimiliki.
12 Tena Yoshua akawaambia Wareubeni, na Wagadi, na hao wa nusu ya kabila ya Manase, akasema,
13 Likumbukeni neno lile alilowaamuru Musa mtumishi wa Bwana, akisema, Bwana, Mungu wenu, anawapa ninyi raha, naye atawapa nchi hii.
14 Wake zenu, na watoto wenu, na makundi yenu, watakaa katika nchi aliyowapa Musa ng'ambo ya Yordani; bali ninyi mtavuka mbele ya ndugu zenu, hali mmevikwa silaha zenu, watu wote wenye nguvu, na ushujaa, ili mpate kuwasaidia;
15 hata Bwana atakapowapa ndugu zenu raha, kama alivyowapa ninyi, na wao pia wamepata kuimiliki nchi awapayo Bwana, Mungu wenu; ndipo mtakapoirudia nchi ya milki yenu na kuimiliki, ambayo Musa mtumishi wa Bwana aliwapeni ng'ambo ya Yordani upande wa maawio ya jua.
16 Wakamjibu Yoshua, wakasema, Hayo yote uliyotuamuru tutayafanya, na kila mahali utakakotutuma tutakwenda.
17 Kama vile tulivyomsikiliza Musa katika mambo yote, ndivyo tutakavyokusikiliza wewe; Bwana, Mungu wako, na awe pamoja nawe tu, kama alivyokuwa pamoja na Musa.
18 Kila mtu atakayeiasi amri yako, asiyasikilize maneno yako katika mambo yote utakayomwamuru, atauawa. Uwe hodari na moyo wa ushujaa, hilo tu.

Yoshua 2


1 Yoshua, mwana wa Nuni, akawatuma watu wawili kutoka Shitimu kwa siri, ili kupeleleza, akawaambia, Enendeni mkaitazame nchi hii, na Yeriko. Wakaenda wakafika nyumbani kwa kahaba mmoja jina lake aliitwa Rahabu, wakalala huko.
2 Mfalme wa Yeriko akaambiwa, kusema, Tazama, watu wawili wa wana wa Israeli wameingia humu leo usiku, ili kuipeleleza nchi.
3 Mfalme wa Yeriko akatuma watu kwa Rahabu, akasema, Watoe watu wale waliokuja kwako, walioingia ndani ya nyumba yako, maana wamekuja ili kuipeleleza nchi.
4 Yule mwanamke akawatwaa wale watu wawili, akawaficha, akasema, Naam, wale watu walikuja kwangu, lakini sikujua walikotoka;
5 ikawa kama wakati wa kufungwa lango la mji, kulipokuwa giza, watu wale wakatoka, wala sijui walikokwenda; wafuateni upesi, maana mtawapata.
6 Lakini yeye alikuwa amewapandisha darini, akawaficha kwa mabua ya kitani, aliyokuwa ameyatandika juu ya dari.
7 Basi hao watu wakawafuata kwa njia iendayo Yordani mpaka vivukoni; na mara wale watu waliowafuatia walipokwisha kutoka, wakalifunga lango.
8 Tena kabla hawajalala akawaendea juu darini,
9 akawaambia wale wanaume, Mimi najua ya kuwa Bwana amewapa ninyi nchi hii, na ya kuwa hofu imetuangukia mbele yenu, na ya kuwa wenyeji wote wa nchi wanayeyuka mbele yenu.
10 Maana tumesikia jinsi Bwana alivyoyakausha maji ya bahari ya Shamu mbele yenu, hapo mlipotoka Misri, tena mambo hayo mliyowatendea wafalme wawili wa Waamori waliokuwa huko ng'ambo ya Yordani, yaani, Sihoni na Ogu, mliowaangamiza kabisa.
11 Na mara tuliposikia hayo mioyo yetu iliyeyuka, wala haukusalia ujasiri wo wote katika mtu awaye yote, kwa sababu yenu; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, yeye ndiye Mungu, katika mbingu juu na katika nchi chini.
12 Basi sasa, nawasihi, niapieni kwa Bwana, kwa kuwa nimewatendea ihisani, ya kwamba ninyi nanyi mtaitendea ihisani nyumba ya baba yangu; tena nipeni alama ya uaminifu;
13 ya kwamba mtawaponya hai baba yangu na mama yangu, na ndugu zangu wanaume na wanawake, na vitu vyote walivyo navyo, na kutuokoa roho zetu na kufa.
14 Wale wanaume wakamwambia, Uhai wetu badala ya uhai wenu, ikiwa hamwitangazi habari ya shughuli yetu hii; kisha itakuwa, wakati Bwana atakapotupa nchi hii, tutakutendea kwa ihisani na uaminifu.
15 Ndipo akawashusha kwa kamba dirishani, maana nyumba yake ilikuwa katika ukuta wa mji; naye alikaa ukutani.
16 Akawaambia, Enendeni zenu mlimani, wale wanaowafuatia wasije wakawapata; mkajifiche huko siku tatu hata wao wanaowafuatia watakaporudi; kisha enendeni zenu.
17 Wale wanaume wakamwambia, Sisi tunataka tusiwe na hatia kwa ajili ya kiapo hiki ulichotuapisha.
18 Angalia, tutakapoingia katika nchi hii, funga kamba hii nyekundu katika dirisha hili ulilotutelemshia; nawe uwakusanye kwako nyumbani mwako, baba yako, na mama yako, na ndugu zako, na watu wote wa nyumba ya baba yako.
19 Itakuwa mtu awaye yote atakayetoka katika mlango wa nyumba yako kwenda njiani, damu yake itakuwa juu ya kichwa chake mwenyewe, na sisi tutakuwa hatuna hatia; na mtu atakayekuwa ndani ya nyumba yako damu yake itakuwa juu ya vichwa vyetu, mkono wa mtu ukimpata.
20 Lakini wewe ukitangaza habari yetu hii, ndipo tutakuwa hatuna hatia, katika kiapo hiki ulichotuapisha.
21 Naye akasema, Na iwe hivyo kama yalivyo maneno yenu. Akawatoa, nao wakaenda zao; naye akaifunga ile kamba nyekundu dirishani
22 Watu hao wakaenda, wakafika mlimani, wakakaa huko siku tatu, hata wale waliowafuatia walipokuwa wamerudi; na wale waliowafuatia wakawafuatia katika njia ile yote, lakini hawakuwaona.
23 Kisha wale watu wakarudi, wakatelemka mlimani, wakavuka, wakamwendea Yoshua, mwana wa Nuni, nao wakamwambia habari za mambo yote yaliyowapata.
24 Wakamwambia Yoshua, Hakika Bwana ameitia nchi yote katika mikono yetu; tena zaidi ya hayo wenyeji wa nchi wanayeyuka mbele yetu.

Yoshua 3


1 Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao wakatoka Shitimu, wakafika mto wa Yordani, yeye na wana wa Israeli wote, wakakaa hapo kabla ya kuvuka.
2 Ikawa baada ya siku tatu, maakida wakapita katikati ya marago,
3 wakawaamuru watu wote wakisema, Mtakapoliona sanduku la agano la Bwana, Mungu wenu, na makuhani Walawi wakilichukua, ndipo mtakapoondoka hapa mlipo na kulifuata.
4 Lakini, na iwe nafasi kati ya ninyi na lile sanduku, kama dhiraa elfu mbili kiasi chake; msilikaribie mpate kuijua njia ambayo hamna budi kuiendea; kwa maana hamjapita njia hii bado.
5 Yoshua akawaambia watu, Jitakaseni; maana kesho Bwana atatenda mambo ya ajabu kati yenu.
6 Kisha Yoshua akawaambia makuhani, akasema, Liinueni sanduku la agano, mkavuke mbele ya hao watu. Wakaliinua sanduku la agano, wakatangulia mbele ya watu.
7 Bwana akamwambia Yoshua, Hivi leo nitaanza kukutukuza mbele ya Israeli wote, wapate kujua ya kuwa mimi nitakuwa pamoja na wewe, kama nilivyokuwa pamoja na Musa.
8 Nawe uwaamuru hao makuhani walichukuao sanduku la agano, ukawaambie, Mtakapofika ukingo wa maji ya Yordani, simameni katika Yordani.
9 Basi Yoshua akawaambia wana wa Israeli, Njoni huku, mkayasikie maneno ya Bwana, Mungu wenu.
10 Yoshua akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kuwa Mungu aliye hai yu kati yenu, na ya kuwa hatakosa kuwatoa mbele yenu Mkanaani, na Mhiti, na Mhivi, na Mperizi, na Mgirgashi, na Mwamori, na Myebusi.
11 Tazama, sanduku la agano la Bwana wa dunia yote linavuka mbele yenu na kuingia Yordani.
12 Basi sasa twaeni watu kumi na wawili katika kabila za Israeli, kila kabila mtu mmoja.
13 Itakuwa, wakati nyayo za makuhani walichukuao sanduku la Bwana, Bwana wa dunia yote, zitakaposimama katika maji ya Yordani, hayo maji ya Yordani yatatindika, maji yale yashukayo kutoka juu; nayo yatasimama kama chuguu.
14 Hata ikawa, hao watu walipotoka katika hema zao, ili kuvuka Yordani, makuhani waliolichukua sanduku la agano wakatangulia mbele ya watu,
15 basi hao waliolichukua hilo sanduku walipofika Yordani, na nyayo za makuhani waliolichukua sanduku zilipotiwa katika maji ya ukingoni, (maana Yordani hujaa hata kingo zake na kufurika wakati wote wa mavuno),
16 ndipo hayo maji yaliyoshuka kutoka juu yakasimama, yakainuka, yakawa chuguu, mbali sana, huko Adamu, mji ule ulio karibu na Sarethani, na maji yale yaliyotelemkia bahari ya Araba, yaani Bahari ya Chumvi, yakatindika kabisa; watu wakavuka kukabili Yeriko.
17 Na hao makuhani waliolichukua sanduku la agano la Bwana wakasimama imara mahali pakavu katikati ya Yordani; Israeli wote wakavuka katika nchi kavu, hata taifa lile lote likaisha kuvuka Yordani.

Yoshua 4


1 Ikawa, hapo hilo taifa zima lilipokuwa limekwisha vuka Yordani, ndipo Bwana akanena na Yoshua, akamwambia,
2 Haya, twaeni watu waume kumi na wawili katika hao watu, kila kabila mtu mmoja,
3 kisha uwaamrishe, kusema, Twaeni mawe kumi na mawili, hapo katikati ya Yordani, mahali hapo miguu ya hao makuhani iliposimama imara, mwende nayo mawe hayo, mkayaweke nchi kambini, hapo mtakapolala usiku huu.
4 Basi Yoshua akawaita hao watu kumi na wawili, aliokuwa amewaweka tayari tangu hapo, katika wana wa Israeli, kila kabila mtu mmoja;
5 naye Yoshua akawaambia, Haya, piteni ninyi mtangulie mbele ya sanduku la Bwana, Mungu wenu, mwende pale katikati ya Yordani, mkatwae kila mtu wenu jiwe moja begani mwake, kwa kadiri ya hesabu ya kabila za wana wa Israeli;
6 ili kwamba jambo hili liwe ishara kati yenu, hapo watoto wenu watakapowauliza ninyi katika siku zijazo, wakisema, Ni nini maana yake mawe haya?
7 Ndipo mtakapowaambia, Ni kwa sababu maji ya Yordani yalitindika mbele ya sanduku la agano la Bwana; hapo lilipovuka Yordani, hayo maji ya Yordani yalitindika; na mawe haya yatakuwa ni ukumbusho kwa wana wa Israeli milele.
8 Basi wana wa Israeli walifanya vile vile kama Yoshua alivyowaamuru, nao wakatwaa mawe kumi na mawili pale katikati ya Yordani, kama Bwana alivyomwambia Yoshua, sawasawa na hesabu ya kabila za wana wa Israeli; wakayachukua wakavuka nayo hata mahali pale walipolala, nao wakayaweka nchi kuko huko.
9 Kisha Yoshua akapanga mawe kumi na mawili katikati ya Yordani, mahali pale miguu ya hao makuhani waliolichukua hilo sanduku la agano iliposimama; nayo yapo pale pale hata hivi leo.
10 Kwa kuwa makuhani waliolichukua hilo sanduku walisimama katikati ya Yordani, hata mambo yote Bwana aliyomwamuru Yoshua awambie hao watu yakaisha, sawasawa na hayo yote Musa aliyokuwa amemwamuru Yoshua; kisha hao watu wakafanya haraka wakavuka.
11 Ikawa watu wote walipokuwa wamekwisha vuka kabisa, hilo sanduku la Bwana likavuka, na hao makuhani, mbele ya macho ya hao watu.
12 Na wana wa Reubeni, na wana wa Gadi na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wakavuka, hali ya kuvaa silaha mbele ya wana wa Israeli, kama Musa alivyowaambia;
13 walipata kama watu arobaini elfu hesabu yao, wenye kuvaa silaha tayari kwa vita, waliovuka mbele ya Bwana, waende vitani, hata nchi tambarare za Yeriko.
14 Siku ile Bwana alimtukuza Yoshua mbele ya macho ya Israeli wote; nao wakamcha, kama walivyokuwa wakimcha Musa, siku zote za maisha yake.
15 Kisha Bwana akanena na Yoshua, akamwambia,
16 Haya, uwaamuru makuhani, hao waliolichukua sanduku la ushuhuda, kwamba wakwee juu kutoka mle katika Yordani.
17 Basi Yoshua akawaamuru hao makuhani, akawaambia, Haya, kweeni mtoke Yordani.
18 Ilikuwa, hapo hao makuhani waliolichukua sanduku la agano la Bwana walipokwea juu kutoka mle kati ya Yordani, na nyayo za miguu yao hao makuhani zilipoinuliwa na kutiwa katika nchi kavu, ndipo maji ya Yordani yaliporudi mahali pake, na kujaa na kuipita mipaka yake, kama yalivyokuwa hapo kwanza.
19 Na hao watu wakakwea kutoka Yordani siku ya kumi ya mwezi wa kwanza, wakapiga kambi Gilgali, katika mpaka wa mashariki wa Yeriko.
20 Na yale mawe kumi na mawili waliyoyatwaa katikati ya Yordani Yoshua akayasimamisha Gilgali.
21 Akawaambia wana wa Israeli, akasema, Watoto wenu watakapowauliza baba zao katika siku zijazo, wakisema, Mawe haya maana yake ni nini?
22 Ndipo mtakapowaarifu watoto wenu mkisema, Israeli walivuka mto huu wa Yordani, kwa njia ya nchi kavu.
23 Kwa sababu Bwana, Mungu wenu aliyakausha maji ya Yordani, mbele yenu, hata mlipokwisha kuvuka kama Bwana, Mungu wenu, alivyoitenda Bahari ya Shamu, aliyoikausha mbele yetu hata tulipokwisha kuvuka;
24 watu wote wa duniani wapate kujua mkono wa Bwana, ya kuwa ni mkono wenye uweza, ili wamche Bwana, Mungu wenu, milele.

Yoshua 5


1 Ikawa, wafalme wa Waamori, waliokaa ng'ambo ya Yordani pande za magharibi, na wafalme wote wa Wakanaani, waliokuwa karibu na bahari, waliposikia jinsi Bwana alivyoyakausha maji ya Yordani mbele ya wana wa Israeli, hata tulipokwisha kuvuka, basi mioyo yao iliyeyuka, wala haikuwamo roho ya nguvu ndani yao tena; kwa ajili ya wana wa Israeli.
2 Wakati huo Bwana akamwambia Yoshua, Haya, jifanyie visu vya mawe ya gumegume, watahiri tena wana wa Israeli mara ya pili.
3 Basi Yoshua akajifanyia visu vya mawe ya gumegume, akawatahiri wana wa Israeli huko Gibea-haaralothi.
4 Na sababu ya Yoshua kutahiri ni hii; watu wote waliotoka Misri, waliokuwa waume, hao watu waume wote waendao vitani walikufa katika bara njiani, baada ya wao kutoka Misri.
5 Kwa kuwa watu wote waliotoka walikuwa wamekwisha kutahiriwa; lakini watu wote waliozaliwa katika bara njiani walipokwisha kutoka Misri, hao hawakutahiriwa.
6 Kwa kuwa wana wa Israeli walitembea muda wa miaka arobaini barani, hata hilo taifa zima, yaani, watu waume waendao vitani, waliotoka Misri, walipokuwa wameangamia; kwa sababu hawakuisikiza sauti ya Bwana; nao ndio Bwana aliowaapia ya kwamba hatawaacha waione hiyo nchi, ambayo Bwana aliwaapia baba zao kwamba atatupa sisi; nchi ijaayo maziwa na asali.
7 Na watoto wao, aliowainua badala yao ndio hao aliowatahiri Yoshua; kwa kuwa wao walikuwa hawakutahiriwa, kwa maana walikuwa hawakuwatahiri njiani.
8 Ilikuwa walipokwisha kutahiriwa taifa zima, wakakaa kila mtu mahali pake maragoni, hata walipopoa.
9 Bwana akamwambia Yoshua, Siku hii ya leo nimeivingirisha hiyo aibu ya Misri iondoke juu yenu. Kwa hiyo jina la mahali pale likaitwa Gilgali, hata hivi leo.
10 Basi wana wa Israeli wakapanga hema zao huko Gilgali; nao wakala sikukuu ya pasaka siku ya kumi na nne ya mwezi, jioni, katika nchi tambarare za Yeriko.
11 Nao wakala katika mazao ya nchi siku ya pili ya kuiandama hiyo sikukuu ya pasaka, mikate isiyotiwa chachu, na bisi, siku iyo hiyo.
12 Ndipo ile mana ikakoma siku ya pili yake, baada ya wao kuyala hayo mazao ya nchi; na hao wana wa Israeli hawakuwa na mana tena; lakini wakala katika viliwa vya nchi ya Kanaani mwaka huo.
13 Ikawa hapo Yoshua alipokuwa karibu na mji wa Yeriko, akavua macho yake na kuangalia, na tazama, mtu mume akasimama kumkabili mbele yake, naye alikuwa na upanga wazi mkononi mwake; Yoshua akamwendea, na kumwambia, Je! Wewe u upande wetu, au upande wa adui zetu?
14 Akasema, La, lakini nimekuja sasa, nili amiri wa jeshi la Bwana. Yoshua akapomoka kiusouso hata nchi, naye akasujudu, akamwuliza, Bwana wangu aniambia nini mimi mtumishi wake?
15 Huyo amiri wa jeshi la Bwana akamwambia Yoshua, Vua viatu vyako miguuni mwako; kwa kuwa mahali hapo usimamapo ni patakatifu. Yoshua akafanya vivyo.

Yoshua 6


1 Basi Yeriko ulikuwa umefungwa kabisa kwa sababu ya wana wa Israeli; hapana mtu aliyetoka wala hapana mtu aliyeingia.
2 Bwana akamwambia Yoshua, Tazama, nimeutia Yeriko katika mkono wako, na mfalme wake, na mashujaa wake.
3 Nanyi mtauzunguka mji huu, watu wote wa vita, mkiuzunguka mji mara moja. Fanya hivi siku sita.
4 Na makuhani saba watachukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume, mbele ya hilo sanduku; na siku ya saba mtauzunguka mji mara saba, nao makuhani watapiga tarumbeta zao.
5 Kisha itakuwa watakapopiga hizo pembe za kondoo waume kwa nguvu, nanyi mtakaposikia sauti ya tarumbeta, watu wote watapiga kelele kwa sauti kuu; na ukuta wa mji utaanguka chini pale pale, na hao watu watapanda, kila mtu akiendelea mbele kukabili.
6 Bali Yoshua, mwana wa Nuni, akawaita makuhani, akawaambia, Lichukueni sanduku la agano, tena makuhani saba na wachukue tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele ya sanduku la Bwana.
7 Naye akawaambia watu, Piteni mbele, mkauzunguke mji, na hao watu wenye silaha na watangulie mbele ya sanduku la Bwana.
8 Basi ikawa Yoshua alipokwisha kusema na watu, wale makuhani saba, wenye kuzichukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele za Bwana, wakatangulia, wakazipiga hizo tarumbeta; nalo sanduku la agano la Bwana likawafuata.
9 Wale watu wenye silaha walikwenda mbele ya hao makuhani waliozipiga tarumbeta, na wale waliokuwa nyuma wakalifuata hilo sanduku; makuhani wakizipiga tarumbeta walipokuwa wakienda.
10 Yoshua akawaamuru watu, akasema Msipige kelele, wala sauti zenu zisisikiwe, wala neno lo lote lisitoke kinywani mwenu, hata siku ile nitakapowaamuru kupiga kelele, ndipo mtakapopiga kelele.
11 Basi akalipeleka sanduku la Bwana liuzunguke huo mji, likauzunguka mara moja, kisha wakaenda kambini wakakaa kambini.
12 Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, nao makuhani wakalichukua sanduku la Bwana.
13 Na wale makuhani saba wakazichukua tarumbeta saba za pembe za kondoo waume mbele ya sanduku la Bwana, wakaendelea wakazipiga tarumbeta; nao watu wenye silaha wakawatangulia, na hao waliokuwa nyuma wakalifuata sanduku la Bwana; makuhani wakizipiga tarumbeta walipokuwa wakienda.
14 Siku ya pili wakauzunguka mji mara moja, wakarejea kambini; ndivyo walivyofanya siku sita.
15 Ikawa siku ya saba wakaondoka asubuhi na mapema wakati wa mapambazuko, wakauzunguka mji vivyo hivyo mara saba; ila siku hiyo waliuzunguka huo mji mara saba.
16 Hata mara ya saba makuhani walipozipiga tarumbeta, Yoshua akawaambia watu, Pigeni kelele; kwa maana Bwana amewapeni mji huu.
17 Na mji huu utakuwa wakfu kwa Bwana, mji wenyewe na vitu vyote vilivyomo; isipokuwa Rahabu, yule kahaba, ataishi, yeye na watu wote walio pamoja naye nyumbani, kwa sababu aliwaficha hao wapelelezi tuliowatuma.
18 Na ninyi, msikose kujiepusha na kitu kilichowekwa wakfu; msije mkakitwaa kitu kilichowekwa wakfu, baada ya kukiweka wakfu; nanyi hivyo mtayafanya matuo ya Israeli kuwa yamelaaniwa na kuyafadhaisha.
19 Lakini fedha yote, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na chuma, ni vitakatifu kwa Bwana; vitaletwa katika hazina ya Bwana.
20 Basi watu wakapiga kelele, na makuhani wakazipiga tarumbeta; hata ikawa, hapo watu waliposikia sauti ya tarumbeta hao watu wakapiga kelele kwa sauti kuu sana, na ule ukuta wa mji ukaanguka nchi kabisa, hata watu wakapanda juu, wakaingia katika mji, kila mtu akiendelea kukabili mbele; wakautwaa huo mji.
21 Basi wakaangamiza kabisa vitu vyote vilivyokuwa ndani ya mji, wanaume na wanawake, watoto na wazee, na ng'ombe, na kondoo, na punda, kwa makali ya upanga.
22 Naye Yoshua akawaambia wale wanaume wawili walioipeleleza nchi, Ingieni katika nyumba ya yule kahaba, mkamtoe huyo mwanamke mwenyewe na vitu vyote alivyo navyo, kama mlivyomwapia.
23 Basi wale vijana wapelelezi wakaingia, wakamtoa Rahabu, na baba yake, na mama yake, na ndugu zake, na vitu vyote walivyokuwa navyo, wakawatoa na jamaa zake wote pia; wakawaweka nje ya matuo ya Israeli.
24 Kisha wakauteketeza mji kwa moto, na vitu vyote vilivyokuwa ndani yake; bali fedha, na dhahabu, na vyombo vya shaba, na vya chuma, wakavitia katika hazina ya nyumba ya Bwana.
25 Lakini Yoshua akamhifadhi Rahabu, yule kahaba, na watu wa nyumba ya baba yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo; naye akakaa kati ya Israeli hata leo; kwa sababu aliwaficha wale wajumbe aliowatuma Yoshua ili kuupeleleza mji wa Yeriko.
26 Naye Yoshua akawaapisha kiapo wakati ule, akasema, Na alaaniwe mbele za Bwana mtu yule atakayeinuka na kuujenga tena mji huu wa Yeriko; ataweka msingi wake kwa kufiliwa na mzaliwa wa kwanza wake, tena atayasimamisha malango yake kwa kufiliwa na mtoto wake mwanamume aliye mdogo.
27 Basi Bwana alikuwa pamoja na Yoshua; sifa zake zikaenea katika nchi ile yote.

Yoshua 7


1 Lakini wana wa Israeli walifanya dhambi katika kitu kilichowekwa wakfu; maana Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila ya Yuda, alitwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; hasira ya Bwana ikawaka juu ya wana wa Israeli.
2 Kisha Yoshua akatuma watu kutoka Yeriko mpaka mji wa Ai, ulio karibu na Bethaveni, upande wa mashariki wa Betheli, akawaambia, akisema, Pandeni juu mkaipeleleze nchi, basi wakapanda juu wakaupeleleza Ai.
3 Wakarejea kwa Yoshua wakamwambia, Wasiende watu wote, ila waende watu kama elfu mbili, tatu, wakaupige Ai; usiwataabishe watu wote kwa kuwaendesha huko; maana watu hao ni wachache tu.
4 Basi watu wakaenda huko wapata elfu tatu tu; nao wakakimbia mbele ya watu wa Ai.
5 Watu wa Ai wakawapiga watu kama thelathini na sita; wakawafuatia kutoka mbele ya mlango mpaka Shebarimu, wakawapiga huko kwenye matelemko; mioyo ya watu ikayeyuka, ikawa kama maji.
6 Yoshua akararua mavazi yake, akaanguka kifudifudi mbele ya sanduku la Bwana hata jioni, yeye na wazee wa Israeli; wakatia mavumbi vichwani mwao.
7 Yoshua akasema, Ee Bwana MUNGU, kwa nini umewavusha watu hawa mto wa Yordani, ili kututia katika mikono ya Waamori, na kutuangamiza? Laiti tungelikuwa radhi kukaa ng'ambo ya Yordani
8 Ee Bwana, niseme nini baada ya Israeli kuwapa visogo adui zao?
9 Maana Wakanaani na wenyeji wote wa nchi hii watasikia habari hii, nao watatuzingira, na kulifuta jina letu katika nchi. Nawe utafanya nini kwa ajili ya jina lako kuu?
10 Bwana akamwambia Yoshua, Haya! Inuka, mbona umeanguka kifudifudi hivi?
11 Israeli wamefanya dhambi, naam, wamelivunja agano langu nililowaagiza; naam, wametwaa baadhi ya vitu vilivyowekwa wakfu; tena wameiba, tena wameficha na kuvitia pamoja na vitu vyao wenyewe.
12 Ndiposa wana wa Israeli hawawezi kusimama mbele ya adui zao; wakawapa visogo adui zao, kwa sababu wamelaaniwa; mimi sitakuwa pamoja nanyi tena, msipokiharibu kitu kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu.
13 Haya! Inuka, uwatakase watu, ukaseme, Jitakaseni, mwe tayari kesho; maana Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi; Kitu kilichowekwa wakfu kiko katikati yako, Ee Israeli; huwezi kusimama mbele ya adui zako, hata mtakapokiondoa kile mlicho nacho kilichowekwa wakfu.
14 Basi asubuhi mtaletwa karibu nami kabila kwa kabila; kisha itakuwa ya kwamba kabila ile atakayoitwaa Bwana itakaribia jamaa kwa jamaa; na jamaa ile atakayoitwaa Bwana itakaribia nyumba kwa nyumba; na nyumba ile atakayoitwaa Bwana itakaribia mtu kwa mtu.
15 Tena itakuwa ya kwamba yeye atakayetwaliwa, naye anacho kitu kile kilichowekwa wakfu, atateketezwa kwa moto, yeye na vitu vyote alivyo navyo; kwa sababu amelivunja agano la Bwana, na kwa sababu ametenda upumbavu katika Israeli.
16 Basi Yoshua akaondoka asubuhi na mapema, akawasogeza Israeli kabila kwa kabila; kabila ya Yuda ikatwaliwa.
17 Akazisogeza jamaa za Yuda, akaitwaa jamaa ya Wazera; akaisogeza jamaa ya Wazera mtu kwa mtu; Zabdi akatwaliwa.
18 Akawasogeza watu wa nyumba yake mmoja mmoja; na Akani, mwana wa Karmi, mwana wa Zabdi, mwana wa Zera, wa kabila ya Yuda akatwaliwa.
19 Yoshua akamwambia Akani, Mwanangu, nakusihi, umtukuze Bwana, Mungu wa Israeli, ukaungame kwake; uniambie sasa ulilolitenda; usinifiche.
20 Akani akamjibu Yoshua, akasema, Kweli nimefanya dhambi juu ya Bwana, Mungu wa Israeli, nami nimefanya mambo haya na haya.
21 Nilipoona katika nyara joho nzuri ya Babeli, na shekeli mia mbili za fedha, na kabari ya dhahabu, uzani wake shekeli hamsini, basi nalivitamani nikavitwaa; tazama, vimefichwa mchangani katikati ya hema yangu, na ile fedha chini yake.
22 Basi Yoshua akatuma wajumbe wakapiga mbio mpaka hemani; na tazama, vile vitu vilikuwa vimefichwa hemani mwake, na ile fedha chini yake.
23 Wakavitoa kutoka hapo katikati ya hema, wakavileta kwa Yoshua, na kwa wana wa Israeli wote, nao wakaviweka chini mbele za Bwana.
24 Kisha Yoshua, na Israeli wote pamoja naye, wakamtwaa Akani, mwana wa Zera, na ile fedha, na Lile joho, na ile kabari ya dhahabu, na wanawe, na binti zake, na ng'ombe zake, na punda zake, na kondoo zake, na hema yake, na vitu vyote alivyokuwa navyo, wakavileta juu hata bonde la Akori.
25 Yoshua akasema, Mbona umetufadhaisha hivi? Bwana atakufadhaisha wewe leo. Ndipo Israeli wote wakampiga kwa mawe, kisha wakawateketeza kwa moto, na kuwapiga kwa mawe.
26 Kisha wakakusanya juu yake chungu kubwa ya mawe hata leo; naye Bwana akauacha ukali wa hasira yake. Kwa sababu hiyo jina la mahali pale likaitwa, Bonde la Akori, hata hivi leo.

Yoshua 8


1 Kisha Bwana akamwambia Yoshua, Usiche, wala usifadhaike; wachukue watu wote wa vita waende pamoja nawe, nanyi inukeni, mwende Ai, angalia, mimi nimemtia mkononi mwako huyo mfalme wa Ai, na watu wake, na mji wake, na nchi yake;
2 nawe utautenda mji wa Ai na mfalme wake kama ulivyoutenda mji wa Yeriko na mfalme wake; lakini nyara zake na wanyama wake wa mji mtavitwaa kuwa mateka yenu wenyewe; huo mji uuwekee waoteaji upande wa nyuma.
3 Basi Yoshua akainuka, na watu wote wa vita pamoja naye, ili waende Ai; Yoshua akachagua watu thelathini elfu, watu mashujaa wenye uwezo, akawapeleka wakati wa usiku.
4 Akawaagiza, akasema, Angalieni, mtaotea kuuvizia ule mji, upande wa nyuma wa mji; msiende mbali sana na mji, lakini kaeni tayari nyote;
5 na mimi, na watu wote walio pamoja nami, tutaukaribia mji; kisha itakuwa, hapo watakapotoka nje kupigana nasi, kama walivyofanya hapo kwanza, sisi tutakimbia mbele yao;
6 nao watatoka nje watufuate, hata tuwavute waende mbali na mji wao; kwa kuwa watasema, Wakimbia mbele yetu, kama walivyofanya kwanza; nasi tutakimbia mbele yao;
7 basi ninyi mtainuka mtoke hapo mwoteapo, na kuushika mji; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, atautia mikononi mwenu.
8 Kisha itakuwa, mtakapoushika mji, ndipo mtauteketeza mji kwa moto; sawasawa na hilo neno la Bwana; angalieni, nimewaagiza.
9 Basi Yoshua akawatuma; nao wakaenda hata hapo watakapootea, wakakaa kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa Ai; lakini Yoshua akalala usiku huo kati ya watu.
10 Yoshua akaamka asubuhi na mapema, akawakutanisha watu, kisha akatangulia kukwea kwenda Ai mbele ya hao watu, yeye na wazee wa Israeli.
11 Watu wote, hao wa vita, waliokuwa pamoja naye, wakaenda wakakaribia, na kufikilia mbele ya mji, wakatua upande wa kaskazini wa Ai; napo palikuwa na bonde kati ya yeye na Ai.
12 Kisha akatwaa watu kama elfu tano, akawaweka kuotea kati ya Betheli na Ai, upande wa magharibi wa huo mji.
13 Basi wakawaweka hao watu, jeshi zima lililokuwa upande wa kaskazini wa mji, na wale waliokuwa waotea upande wa magharibi wa mji; naye Yoshua akaenda usiku huo katikati ya hilo bonde.
14 Kisha ikawa hapo huyo mfalme wa Ai alipoona jambo hilo, ndipo walipofanya haraka, na wakaamka asubuhi na mapema, na watu waume wa mji wakatoka nje waende kupigana na Israeli, yeye na watu wake wote, kwa wakati ulioamriwa, kuikabili Araba; lakini hakujua ya kwamba walikuwako waviziao kinyume chake kwa upande wa nyuma wa mji.
15 Kisha Yoshua na watu wa Israeli wote walifanya kana kwamba wameshindwa mbele yao, wakakimbia kwa njia ya nyika.
16 Watu wote waliokuwa ndani ya mji waliitwa wakusanyike pamoja ili kuwafuatia; nao wakamfuatia Yoshua, wakasongea mbele na kuuacha mji.
17 Hakusalia mtu ye yote ndani ya Ai, au katika Betheli, asiyetoka nje kuwafuatia Israeli; wakauacha mji wazi na kuwafuatia Israeli.
18 Kisha Bwana akamwambia Yoshua, Haya, unyoshe huo mkuki ulio nao mkononi mwako, uuelekeze upande wa Ai; kwa kuwa nitautia mkononi mwako. Basi Yoshua akaunyosha huo mkuki uliokuwa mkononi mwake kuuelekea huo mji.
19 Wale watu waliovizia wakainuka kwa upesi kutoka mahali pao, nao wakapiga mbio mara hapo alipokuwa amekwisha unyosha mkono wake, wakaingia ndani ya mji, na kuushika; nao wakafanya haraka kuuteketeza kwa moto huo mji.
20 Kisha hapo hao watu wa Ai walipotazama nyuma yao, wakaona, na tazama, moshi wa huo mji ulikuwa unapaa juu kwenda mawinguni, nao hawakuwa na nguvu za kukimbia huku wala huku; na wale watu waliokuwa wamekimbia kuenenda nyikani wakageuka na kuwarudia hao waliokuwa wakiwafuatia.
21 Basi hapo Yoshua na Israeli wote walipoona ya kwamba hao waliovizia wamekwisha kuushika huo mji, na ya kwamba moshi wa mji umepaa juu, ndipo wakageuka tena, na kuwaua watu wa Ai.
22 Tena hao; wengine wakatoka nje kuutoka huo mji kinyume chao; basi hivyo walikuwa wa katikati ya Israeli, wengine upande huu na wengine upande huu; nao wakawapiga, hata wasimwache hata mmoja miongoni mwao aliyesalia, wala kupona.
23 Kisha wakamshika mfalme wa Ai ali hai, nao wakamleta kwa Yoshua.
24 Kisha ikawa, hapo Israeli walipokuwa wamekwisha kuwaua wenyeji wote wa Ai katika bara, hapo katika nyika walipokuwamo wakiwafuatia, nao walikuwa wamekwisha anguka wote kwa makali ya upanga, hata walipokuwa wameangamizwa wote, ndipo Israeli wakarejea Ai, na kuupiga huo mji kwa makali ya upanga.
25 Wote walioanguka siku hiyo waume kwa wake, walikuwa ni kumi na mbili elfu, yaani, watu wote wa mji wa Ai.
26 Kwani huyo Yoshua hakuuzuia mkono wake, huo ulionyosha huo mkuki, hata hapo alipokuwa amewaangamiza kabisa wenyeji wote wa Ai.
27 Isipokuwa wanyama wa mji na nyara za mji Israeli wakatwaa wenyewe kuwa ni mapato yao, sawasawa na hilo neno la Bwana alilomwamuru Yoshua.
28 Basi Yoshua akaupiga moto mji wa Ai, na kuufanya kuwa ni chungu ya magofu hata milele, kuwa ni ukiwa hata siku hii ya leo.
29 Na huyo mfalme wa Ai akamtundika katika mti hata wakati wa jioni; kisha hapo jua lilipokuchwa Yoshua akaagiza, nao wakauondoa mzoga wake katika huo mti, na kuutupa hapo penye maingilio ya lango la mji, kisha wakaweka pale juu yake chungu kubwa ya mawe, hata hivi leo.
30 Ndipo Yoshua alijenga madhabahu kwa Bwana, Mungu wa Israeli katika mlima Ebali.
31 Kama Musa, mtumishi wa Bwana, alivyowaamuru wana wa Israeli, kama ilivyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, madhabahu ya mawe yasiyochongwa, ambayo mtu hakutumia juu yake chombo cha chuma; nao wakatoa juu yake sadaka za kuteketezwa kwa Bwana, na kuchinja sadaka za amani.
32 Akaandika huko juu ya mawe hayo nakala ya torati ya Musa, aliyoiandika mbele ya wana wa Israeli.
33 Na Israeli wote, na wazee wao, na maakida yao, na makadhi yao, wakasimama upande huu wa sanduku na upande huu, mbele ya makuhani Walawi, waliolichukua sanduku la agano la Bwana, huyo aliyekuwa mgeni pamoja na huyo mzalia; nusu yao mbele ya mlima Gerizimu, na nusu yao mbele ya mlima Ebali, kama Musa, mtumishi wa Bwana, alivyoamuru, ili wawabarikie watu wa Israeli kwanza.
34 Na baadaye alisoma maneno yote ya torati, baraka na laana, sawasawa na maneno yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati.
35 Hapakuwa na hata neno moja katika hayo aliyoamuru Musa, ambalo Yoshua hakulisoma mbele ya kusanyiko lote la Israeli, na mbele ya wanawake, na watoto, na wageni waliokaa nao.

Yoshua 9


1 Kisha ikawa hapo wafalme wote waliokaa ng'ambo ya pili ya Yordani, hapo penye nchi ya vilima, na katika Shefela, na katika upande wa pwani yote ya bahari kubwa kuikabili Lebanoni, yaani, huyo Mhiti, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi, waliposikia habari ya mambo hayo;
2 ndipo walipojikutanisha pamoja wenyewe kwa wenyewe, ili kupigana na Yoshua, na hao Israeli, kwa nia moja.
3 Lakini wenyeji wa Gibeoni waliposikia habari ya hayo yote Yoshua aliyokuwa amewatenda watu wa Yeriko, na wa Ai,
4 wao wakatenda kwa hila, nao wakaenda na kujifanya kama ndio wajumbe, wakaenda na magunia makuukuu juu ya punda zao, na viriba vya mvinyo vilivyokuwa vikuukuu vilivyoraruka-raruka, na kutiwa viraka;
5 na viatu vilivyotoboka na kushonwa-shonwa katika miguu yao, na mavao makuukuu waliyokuwa wanavaa; tena mkate wote wa chakula chao ulikuwa umekauka na kuingia koga.
6 Nao wakamwendea Yoshua hata maragoni huko Gilgali, nao wakamwambia yeye na watu wa Israeli, Sisi tumetoka nchi ya mbali sana; basi kwa hiyo fanyeni agano pamoja nasi.
7 Basi watu wa Israeli wakawaambia hao Wahivi, Labda mwakaa kati yetu; nasi tutawezaje kufanya agano nanyi?
8 Nao wakamwambia Yoshua, Sisi tu watumishi wako. Yoshua akawauliza, Ninyi ni nani? Nanyi mwatoka wapi?
9 Nao wakamwambia, Sisi watumishi wako twatoka nchi iliyo mbali sana, kwa sababu ya jina la Bwana, Mungu wako; kwa kuwa sisi tumesikia sifa zake, na habari ya hayo yote aliyofanya huko Misri,
10 na habari ya hayo yote aliyowatenda wale wafalme wawili wa Waamori, waliokuwa huko ng'ambo ya pili ya Yordani, maana huyo Sihoni, mfalme wa Heshboni, na Ogu, mfalme wa Bashani, aliyekuwa huko Ashtarothi.
11 Kisha wazee wetu, na wenyeji wote wa nchi yetu, walinena nasi na kutuambia, Chukueni vyakula mkononi mwenu kwa ajili ya safari, mwende mkawalaki watu hao, na kuwaambia, Sisi tu watumishi wenu; basi sasa fanyeni agano nasi.
12 Huu mkate wetu tuliutwaa ukali moto katika nyumba zetu, siku hiyo tuliyotoka kuja kwenu, uwe chakula chetu; lakini sasa, tazama, umekauka, na kuingia koga;
13 na viriba vyetu hivi, tulivyovitia divai, vilikuwa ni vipya; sasa, tazama, vimeraruka-raruka; na haya mavazi yetu na viatu vyetu vimekuwa vikuukuu kwa vile tulivyokuja safari ya mbali sana.
14 Basi hao watu wakatwaa katika vyakula vyao, wala wasitake shauri kinywani mwa Bwana.
15 Naye Yoshua akafanya amani pamoja nao, na kufanya agano nao, ili kwamba waachwe hai; na wakuu wa mkutano wakawaapia.
16 Kisha ikawa, mwisho wa siku ya tatu baada ya kufanya hilo agano nao, walisikia habari ya kuwa watu hao ni jirani zao, na ya kwamba waliketi kati yao.
17 Kisha wana wa Israeli walisafiri, wakaifikilia miji ya watu hao siku ya tatu. Basi miji ya watu hao ilikuwa ni hii, Gibeoni, na Kefira, na Beerothi, na Kiriath-yearimu.
18 Wana wa Israeli hawakuwapiga, kwa sababu wakuu wa mkutano walikuwa wamekwisha kuwaapia kwa Bwana, Mungu wa Israeli. Nao mkutano wote wakawanung'unikia hao wakuu.
19 Lakini wakuu wote waliwaambia mkutano wote, Sisi tumewaapia kwa Bwana, Mungu wa Israeli; basi sasa hatuwezi kuwagusa watu hawa.
20 Tutawafanyia neno hili, kisha tutawaacha wawe hai; hasira isije juu yetu, kwa ajili ya hicho kiapo tulichowaapia.
21 Wakuu waliwaambia, Waacheni wawe hai; basi wakawa wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya mkutano wote; vile vile kama hao wakuu walivyowaambia.
22 Basi Yoshua akawaita, akanena nao, na kuwaambia, Mbona ninyi mmetudanganya, huku mkisema, Sisi tu mbali sana na ninyi; nanyi kumbe! Mwakaa kati yetu?
23 Basi sasa mmelaaniwa kisha hatakosekana kuwapo mtu wa kwenu aliye mtumwa, wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya nyumba ya Mungu wangu.
24 Nao wakamjibu Yoshua, na kusema, Ni kwa sababu ya sisi watumishi wako kuambiwa hakika, jinsi huyo Bwana, Mungu wako alivyomwamuru mtumishi wake Musa kuwapa ninyi nchi hii yote, na kuwaangamiza wenyeji wote wa nchi hii watoke mbele zenu; kwa sababu hii tuliogopa mno kwa ajili ya uhai wetu kwa sababu yenu, nasi tumefanya neno hili.
25 Basi sasa, tazama, sisi tu mkononi mwako; basi kama uonavyo kuwa ni vyema na haki kwako wewe kututenda, tutende vivyo.
26 Naye akawafanyia hivyo, na kuwaokoa na mkono wa wana wa Israeli, ili wasiwaue.
27 Siku iyo hiyo Yoshua akawafanya kuwa ni wenye kupasua kuni, na wenye kuteka maji, kwa ajili ya mkutano, na kwa ajili ya madhabahu ya Bwana, hata siku hii ya leo, katika mahali hapo atakapopachagua.

Yoshua 10


1 Basi ikawa hapo Adoni-sedeki, mfalme wa Yerusalemu, aliposikia jinsi Yoshua alivyoushika mji wa Ai na kuuharibu kabisa; kama alivyoufanyia mji wa Yeriko na mfalme wake, akaufanya vivyo Ai na mfalme wake; na jinsi wenyeji waliokaa Gibeoni walivyofanya amani na Israeli, na ya kwamba walikuwa kati yao;
2 ndipo wakacha mno, kwa sababu Gibeoni ulikuwa ni mji mkubwa, kama ilivyo miji ya kifalme mmojawapo, tena kwa sababu ulikuwa ni mji mkubwa kupita Ai, tena watu wake wote walikuwa ni mashujaa.
3 Basi kwa hiyo Adoni-sedeki, mfalme wa Yerusalemu, akatuma ujumbe kwa Hohamu, mfalme wa Hebroni, na kwa Piramu, mfalme wa Yarmuthi, na kwa Yafia, mfalme wa Lakishi, na kwa Debiri, mfalme wa Egloni, akiwaambia,
4 Haya, kweeni mje kwangu, mnisaidie, tuupige Gibeoni; kwa sababu umefanya mapatano ya amani pamoja na Yoshua na wana wa Israeli.
5 Ndipo hao wafalme watano wa Waamori, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni na mfalme wa Yarmuthi na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni, wakakutana pamoja, kisha wakakwea, wao na jeshi zao zote, na kupanga marago yao kinyume cha Gibeoni, na kuupiga vita.
6 Ndipo watu wa Gibeoni wakatuma wajumbe kwenda kwa Yoshua huko Gilgali maragoni, wakamwambia, Usiulegeze mkono wako hata ukatuacha sisi watumishi wako; uje kwetu kwa upesi, utuokoe, na kutusaidia; kwa sababu wafalme wote wa Waamori wakaao katika nchi ya vilima wamekutana pamoja juu yetu.
7 Basi Yoshua akakwea kutoka Gilgali, yeye, na watu wa vita wote pamoja naye, na mashujaa wenye uwezo pia wote.
8 Bwana akamwambia Yoshua, Usiwache watu hao; kwa kuwa mimi nimekwisha kuwatia mikononi mwako; hapana mtu awaye yote miongoni mwao atakayesimama mbele yako.
9 Basi Yoshua akawafikilia ghafula; kwani alikwea kutoka Gilgali kwenda usiku kucha.
10 Bwana naye akawatapanya mbele ya Israeli, naye Israeli akawaua uuaji ulio mkuu hapo Gibeoni, akawafukuza waikimbilie hiyo njia ya kukwelea kwenda Beth-horoni, na kuwapiga hata kufikilia Azeka, tena hata kufikilia Makeda.
11 Kisha ikawa, hapo walipokuwa wakimbia mbele ya Israeli, hapo walipokuwa katika kutelemkia Beth-horoni, ndipo Bwana alipowatupia mawe makubwa kutoka mbinguni juu yao hata kufikilia Azeka, nao wakafa; hao waliokufa kwa kuuawa na hayo mawe ya barafu walikuwa ni wengi kuliko hao waliouawa na wana wa Israeli kwa upanga.
12 Ndipo Yoshua akanena na Bwana katika siku hiyo ambayo Bwana aliwatoa Waamori mbele ya wana wa Israeli; akasema mbele ya macho ya Israeli, Wewe Jua, simama kimya juu ya Gibeoni; Na wewe Mwezi, simama katika bonde la Aiyaloni.
13 Ndipo jua likasimama, na mwezi ukatulia, Hata hilo taifa lilipokuwa limekwisha jipatiliza juu ya adui zao.
14 Haikuwapo siku nyingine mfano wa siku hiyo katika siku zilizotangulia mbele yake wala katika hizo zilizoandama baada yake, hata ikawa yeye Bwana kuisikia sauti ya binadamu; kwa kuwa Bwana alipiga vita kwa ajili ya Israeli.
15 Basi Yoshua akarudi, na Israeli wote wakarudi pamoja naye, mpaka maragoni hapo Gilgali.
16 Na hawa wafalme watano wakakimbia, wakajificha ndani ya pango la Makeda.
17 Kisha Yoshua aliambiwa habari hiyo, ya kwamba, Hao wafalme watano wameonekana, nao wa hali ya kujificha ndani ya pango la Makeda
18 Basi Yoshua akasema, Haya, vingirisheni mawe makubwa mdomoni mwa lile pango, kisha wekeni watu hapo ili kuwalinda;
19 lakini msikae ninyi; wafuatieni adui zenu, mwapige hao walio nyuma; msiwaache wakaingia ndani ya miji yao; kwa kuwa Bwana, Mungu wenu, amewatia mikononi mwenu.
20 Kisha ikawa, hapo Yoshua, na wana wa Israeli, walipokuwa wamekwisha kuwaua watu wengi mno, hata wakaangamizwa, na hayo mabaki yao yaliyowasalia walipokuwa wamekwisha ingia katika miji yao yenye boma,
21 ndipo hao watu wote wakamrudia Yoshua maragoni huko Makeda salama; hakuna mtu awaye yote aliyetoa ulimi kinyume cha hao wana wa Israeli hata mmojawapo.
22 Kisha Yoshua akasema, Haya, funua mdomo wa pango, mniletee hao wafalme watano hapa nje ya pango.
23 Nao wakafanya, wakamletea hao wafalme watano hapo nje ya pango, yaani, mfalme wa Yerusalemu, na mfalme wa Hebroni, na mfalme wa Yarmuthi, na mfalme wa Lakishi, na mfalme wa Egloni.
24 Kisha ikawa hapo walipomletea Yoshua hao wafalme watano hapo nje, Yoshua akawaita wanaume wote wa Israeli, akawaambia majemadari wa watu wa vita waliokwenda naye, Haya, jongeeni karibu, mweke nyayo za miguu yenu katika shingo za wafalme hawa. Nao wakajongea karibu, wakatia nyayo zao katika shingo zao.
25 Yoshua akawaambia, Msiche, wala msifadhaike; iweni hodari na wa mioyo ya ushujaa; kwa kuwa ndivyo Bwana atakavyowafanyia adui zenu wote ambao mwapigana nao.
26 Baadaye Yoshua akawapiga, na kuwaua, akawatundika katika miti mitano; nao wakawa wakitundikwa katika hiyo miti hata jioni.
27 Kisha wakati wa kuchwa jua, Yoshua akatoa amri, nao wakawatelemsha katika hiyo miti, na kuwatupa katika lile pango ambamo walikuwa walijificha kisha wakatia mawe makubwa mdomoni mwa pango, hata hivi leo.
28 Siku hiyo Yoshua akautwaa mji wa Makeda, akaupiga kwa makali ya upanga, na mfalme wake; akawaangamiza kabisa na wote pia waliokuwamo ndani yake, hakumwacha hata mmoja aliyesalia; naye akamfanyia huyo mfalme wa Makeda kama alivyomfanyia huyo mfalme wa Yeriko.
29 Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Makeda, mpaka Libna, na Israeli wote pamoja naye, nao wakapiga Libna;
30 Bwana akautia na mji huo pia pamoja na mfalme wake mkononi mwa Israeli; naye akaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake; hakumwacha hata mmoja aliyesalia ndani yake; naye akamtenda mfalme wake kama alivyomtenda huyo mfalme wa Yeriko.
31 Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Libna, na Israeli wote pamoja naye, wakafika Lakishi, wakapanga marago mbele yake na kupigana nao;
32 Bwana akautia huo mji wa Lakishi mkononi mwa Israeli, naye akautwaa siku ya pili, akaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake, sawasawa na hayo yote aliyoutenda Libna.
33 Wakati huo Horamu, mfalme wa Gezeri, akakwea ili kuusaidia Lakishi, lakini Yoshua akampiga yeye na watu wake, hata asimsazie hata mtu mmoja.
34 Kisha Yoshua akapita kutoka hapo Lakishi, na Israeli wote pamoja naye, hata wakafikilia Egloni; nao wakapanga marago mbele yake, na kupigana nao;
35 siku iyo hiyo wakautwaa, nao wakaupiga kwa makali ya upanga, na wote pia waliokuwamo ndani yake akawaangamiza kabisa siku hiyo, sawasawa na hayo yote aliyoufanyia mji wa Lakishi.
36 Kisha Yoshua akakwea kutoka hapo Egloni, na Israeli wote pamoja naye, hata wakafikilia Hebroni; nao wakapigana nao;
37 wakautwaa, na kuupiga kwa makali ya upanga, na mfalme wake, na miji yake yote, na wote waliokuwamo ndani yake; hakumwacha aliyesalia hata mtu mmoja, sawasawa na hayo yote aliyoufanyia huo mji wa Egloni; lakini akauangamiza kabisa, na wote pia waliokuwamo ndani yake.
38 Kisha Yoshua akarudi, na Israeli wote pamoja naye, hata Debiri; nao wakapigana nao;
39 kisha akautwaa, na mfalme wake, na miji yake yote; nao wakawapiga kwa makali ya upanga, wakawaangamiza kabisa wote pia waliokuwamo ndani yake; hakumwacha hata mmoja aliyesalia; kama alivyoufanyia Hebroni aliufanyia na Debiri vivyo, na mfalme wake; kama alivyoufanyia Libna, na mfalme wake.
40 Basi Yoshua akaipiga nchi hiyo yote, nchi ya vilima, na nchi ya Negebu, na nchi ya Shefela, na nchi ya matelemko, na wafalme wake wote; hakumwacha aliyesalia hata mmoja; lakini akawaharibu kabisa wote waliokuwa wavuta pumzi, kama Bwana, Mungu wa Israeli, alivyoamuru.
41 Yoshua akawapiga kutoka Kadesh-barnea mpaka Gaza, na nchi yote ya Gosheni, hata Gibeoni.
42 Na wafalme hao wote na nchi zao Yoshua akatwaa, wakati huo, kwa sababu yeye Bwana, Mungu wa Israeli, alipigana kwa ajili ya Israeli,
43 Kisha Yoshua akarudi, na Israeli wote pamoja naye, hata marago yao huko Gilgali.

Yoshua 11


1 Kisha ikawa, hapo huyo Yabini, mfalme wa Hazori, aliposikia habari ya mambo hayo, akatuma mjumbe aende kwa Yobabu, mfalme wa Madoni, na kwa mfalme wa Shimroni, na mfalme wa Akshafu,
2 na hao wafalme waliokuwa upande wa kaskazini, katika nchi ya vilima, na katika Araba upande wa kusini wa Kinerethi, na katika Shefela, na katika nchi zilizoinuka za Dori upande wa magharibi,
3 na kwa Mkanaani upande wa mashariki, na upande wa magharibi, na kwa Mwamori, na Mhiti, na Mperizi na Myebusi katika nchi ya vilima, na kwa Mhivi pale chini ya Hermoni katika nchi ya Mispa.
4 Nao wakatoka nje, wao na jeshi zao zote pamoja nao, watu wengi mno, kama mchanga ulio ufuoni mwa bahari kwa wingi, pamoja na farasi na magari mengi sana.
5 Wafalme hao wote wakakutana pamoja; wakaenda na kupanga mahema yao pamoja hapo penye maji ya Meromu, ili kupigana na Israeli.
6 Bwana akamwambia Yoshua, Usiche wewe kwa ajili ya hao; kwani kesho wakati kama huu nitawatoa hali wameuawa wote mbele ya Israeli; utawatema farasi zao, na magari yao utayapiga moto.
7 Basi Yoshua akaenda, na watu wote wa vita pamoja naye, ili kupigana nao hapo penye maji ya Meromu ghafula; wakawaangukia.
8 Bwana akawatia mkononi mwa Israeli, nao wakawapiga, na kuwafukuza hata kufikilia Sidoni ulio mkuu, na hata kufikilia Misrefoth-maimu, tena hata kufikilia bonde la Mispa upande wa mashariki; wakawapiga hata wasiwasaze hata mtu mmoja aliyesalia.
9 Yoshua akawafanyia vile vile kama Bwana alivyomwamuru; akawatema farasi zao, na magari yao akayapiga moto.
10 Yoshua akarudi wakati huo na kuutwaa Hazori, akampiga mfalme wa Hazori kwa upanga; kwa kuwa Hazori hapo kwanza ulikuwa ni kichwa cha falme hizo zote.
11 Nao wakawapiga wote pia waliokuwamo ndani ya Hazori kwa makali ya upanga, wakawaangamiza kabisa; hakusazwa hata mmoja aliyevuta pumzi; kisha akauteketeza Hazori kwa moto.
12 Tena miji yote ya wafalme hao, na wafalme wake wote, Yoshua akawatwaa, akawapiga kwa makali ya upanga, na kuwaangamiza kabisa; vile vile kama huyo Musa mtumishi wa Bwana alivyomwamuru.
13 Lakini katika habari ya miji hiyo iliyosimama katika vilima vyao, Israeli hawakuipiga moto miji hiyo, isipokuwa ni mji wa Hazori tu; mji huo Yoshua aliupiga moto.
14 Tena nyara zote za miji hiyo, na wanyama wa miji, wana wa Israeli walitwaa kuwa nyara zao wenyewe; lakini kila mtu wakampiga kwa makali ya upanga, hata walipokuwa wamewaangamiza wote, wala hawakumsaza mmoja mwenye kuvuta pumzi.
15 Vile vile kama Bwana alivyomwamuru Musa mtumishi wake, ndivyo Musa alivyomwamuru Yoshua; naye Yoshua akafanya vivyo; hakukosa kufanya neno lo lote katika hayo yote Bwana aliyomwamuru Musa.
16 Hivyo Yoshua akatwaa nchi hiyo yote, hiyo nchi ya vilima, na nchi yote ya Negebu, na nchi yote ya Gosheni, na hiyo Shefela, na hiyo Araba na nchi ya vilima vilima ya Israeli, na hiyo nchi tambarare;
17 tangu kilima cha Halaki, kiendeleacho upande wa Seiri, mpaka Baal-gadi katika bonde la Lebanoni chini ya kilima cha Hermoni; naye akawatwaa wafalme wao wote, akawapiga, na kuwaua.
18 Yoshua akapiga vita siku nyingi na wafalme hao wote.
19 Haukuwapo mji hata mmoja uliofanya amani na wana wa Israeli, isipokuwa ni wale Wahivi wenye kukaa Gibeoni; wakaitwaa yote vitani.
20 Kwa kuwa lilikuwa ni la Bwana kuifanya mioyo yao kuwa migumu, hata wakatoka kupigana na Israeli, ili apate kuwaangamiza kabisa, wasihurumiwe lakini apate kuwaangamiza, kama vile Bwana alivyomwamuru Musa.
21 Wakati huo Yoshua akaenda na kuwakatilia mbali hao Waanaki watoke nchi ya vilima, kutoka Hebroni, na kutoka Debiri, na kutoka Anabu, na kutoka katika nchi yote ya vilima vilima ya Yuda, na kutoka katika nchi yote ya vilima vilima ya Israeli; Yoshua akawaangamiza kabisa na miji yao.
22 Hawakusalia Waanaki hata mmoja katika nchi ya wana wa Israeli; isipokuwa katika Gaza, na katika Gathi, na katika Ashdodi walisalia.
23 Basi Yoshua akaitwaa hiyo nchi yote, sawasawa na hayo yote Bwana aliyokuwa amemwambia Musa; Yoshua naye akawapa Israeli kuwa ni urithi wao, sawasawa na walivyogawanyikana kwa kabila zao. Kisha nchi ikatulia isiwe na vita tena.

Yoshua 12


1 Basi hawa ndio wafalme wa nchi, ambao wana wa Israeli waliwapiga na kuimiliki nchi yao ng'ambo ya pili ya Yordani, upande wa maawio ya jua, kutoka bonde la Amoni mpaka mlima wa Hermoni, na nchi yote ya Araba upande wa mashariki;
2 Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekaa huko Heshboni, naye ndiye aliyetawala toka Aroeri, ulioko kando ya bonde la Arnoni, na toka huo mji ulio katikati ya bonde, na nusu ya Gileadi, hata kuufikilia mto wa Yaboki, mpaka wa hao wana wa Amoni;
3 na nchi ya Araba mpaka bahari ya Kinerethi, kuelekea mashariki, tena mpaka bahari ya Ataba, mpaka Bahari ya Chumvi, kwendea mashariki, njia ya kwendea Beth-yeshimothi; tena upande wa kusini, chini ya matelemko ya Pisga;
4 tena mpaka wa Ogu mfalme wa Bashani, aliyekuwa wa hayo mabaki ya hao Warefai, aliyekaa Ashtarothi na Edrei,
5 naye alitawala katika mlima wa Hermoni, na katika Saleka, na katika Bashani yote, hata mpaka wa Wageshuri, na Wamaaka, na nusu ya Gileadi, mpaka wa huyo Sihoni mfalme wa Heshboni.
6 Musa mtumishi wa Bwana na wana wa Israeli wakawapiga; naye Musa mtumishi wa Bwana akawapa Wareubeni, na Wagadi, na nusu ya kabila ya Manase iwe urithi wao.
7 Hawa ni wafalme wa hiyo nchi ambao Yoshua na wana wa Israeli waliwapiga ng'ambo ya pili ya Yordani upande wa magharibi, kutoka Baal-gadi katika bonde la Lebanoni mpaka kilima cha Halaki, kilichoelekea Seiri; Yoshua naye akawapa kabila za Israeli iwe milki yao sawasawa na magawanyo yao;
8 katika nchi ya vilima, na katika Shefela, na katika nchi ya Araba, na katika matelemko, na katika bara, na katika Negebu; nchi ya Mhiti, na Mwamori, na Mkanaani, na Mperizi, na Mhivi, na Myebusi;
9 mfalme wa Yeriko, mmoja; mfalme wa Ai, ulio karibu na Betheli, mmoja;
10 mfalme wa Yerusalemu, mmoja; mfalme wa Hebroni, mmoja;
11 mfalme wa Yarmuthi, mmoja; na mfalme wa Lakishi, mmoja;
12 mfalme wa Egloni, mmoja; na mfalme wa Gezeri, mmoja;
13 mfalme wa Debiri, mmoja; na mfalme wa Gederi, mmoja;
14 mfalme wa Horma, mmoja; na mfalme wa Aradi, mmoja;
15 mfalme wa Libna, mmoja; na mfalme wa Adulamu, mmoja;
16 mfalme wa Makeda, mmoja; na mfalme wa Betheli, mmoja;
17 mfalme wa Tapua, mmoja; na mfalme wa Heferi, mmoja;
18 mfalme wa Afeka, mmoja; na mfalme wa Lasharoni, mmoja;
19 mfalme wa Madoni, mmoja; na mfalme wa Hazori, mmoja;
20 mfalme wa Shimron-meroni, mmoja; na mfalme wa Akshafu, mmoja;
21 mfalme wa Taanaki, mmoja; na mfalme wa Megido, mmoja;
22 na mfalme wa Kedeshi, mmoja; mfalme wa Yokneamu wa Karmeli, mmoja;
23 mfalme wa Dori katika kilima cha Dori, mmoja; na mfalme wa makabila katika Gilgali, mmoja;
24 na mfalme wa Tirsa, mmoja; wafalme hao wote walikuwa ni thelathini na mmoja.

Yoshua 13


1 Basi Yoshua alipokuwa mzee, na kwendelea sana miaka yake, Bwana akamwambia, Wewe umekuwa mzee na kwendelea sana miaka yako, kisha inasalia nchi nyingi sana bado kumilikiwa.
2 Nchi iliyosalia ni hii; nchi zote za Wafilisti, na Wageshuri wote;
3 kutoka Shihori, hicho kijito kilichokabili Misri, hata mpaka wa Ekroni upande wa kaskazini, nchi inayohesabiwa kuwa ni ya hao Wakanaani; mashehe matano wa hao Wafilisti; Wagaza, na Waashdodi, na Waashkeloni, na Wagiti, na Waekroni; tena Waavi,
4 upande wa kusini; nchi yote ya Wakanaani na Meara iliyo ya Wasidoni, mpaka Afeka, hata mpaka wa Waamori;
5 na nchi ya Wagebali na Lebanoni yote, upande wa kuelekea maawio ya jua, kutoka Baal-gadi ulio chini ya mlima wa Hermoni mpaka kufikilia maingilio ya Hamathi;
6 na watu wote wenye kuikaa nchi ya vilima kutoka Lebanoni hata Misrefoth-maimu, maana, hao Wasidoni wote; hao wote nitawafukuza watoke mbele ya wana wa Israeli; lakini wewe uwape Israeli kuwa ni urithi wao, kama nilivyokuamuru.
7 Basi sasa gawanya nchi hii, iwe urithi wa hizi kabila kenda, na nusu ya kabila ya Manase.
8 Pamoja na yeye, Wareubeni na Wagadi walipata urithi wao, waliopewa na Musa, huko ng'ambo ya Yordani upande wa mashariki, vile vile kama huyo Musa mtumishi wa Bwana alivyowapa;
9 kutoka huko Aroeri, iliyo pale ukingoni mwa bonde la Amoni, na huo mji ulio pale katikati ya bonde, na nchi tambarare yote ya Medeba mpaka Diboni;
10 na miji yote ya Sihoni mfalme wa Waamori, aliyetawala katika Heshboni, hata mpaka wa wana wa Amoni;
11 na Gileadi na mpaka wa Wageshuri, na Wamaaka, na mlima wa Hermoni wote, na Bashani yote mpaka Saleka;
12 ufalme wote wa Ogu uliokuwa katika Bashani, huyo aliyekuwa akitawala katika Ashtarothi na katika Edrei (huyo alisalia katika mabaki ya wale Warefai); kwa kuwa Musa aliwapiga hao na kuwafukuza.
13 Pamoja na hayo wana wa Israeli hawakuwafukuza Wageshuri, wala Wamaaka; lakini Wageshuri na Wamaaka wamekaa kati ya Israeli, hata siku hii ya leo.
14 Lakini hakuwapa watu wa kabila ya Lawi urithi uwao wote; maana sadaka za Bwana, Mungu wa Israeli, zisongezwazo kwa njia ya moto ndizo urithi wake huyo, kama alivyomwambia.
15 Musa akawapa kabila ya wana wa Reubeni kwa kadiri ya jamaa zao.
16 Mpaka wao ulikuwa kutoka hapo Aroeri, iliyo pale ukingoni mwa bonde la Arnoni, na huo mji ulio katikati ya bonde, na nchi tambarare yote iliyo karibu na Medeba;
17 na Heshboni na miji yake yote iliyoko katika bonde; na Diboni, na Bamoth-baali, na Beth-baal-meoni;
18 na Yahasa, na Kedemothi, na Mefaathi;
19 na Kiriathaimu, na Sibma, na Sereth-shahari katika kilima cha hilo bonde;
20 na Beth-peori, na nchi za matelemko ya Pisga, na Beth-yeshimothi;
21 na miji yote ya nchi tambarare, na ufalme wote wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akitawala katika Heshboni, aliyepigwa na Musa pamoja na hao wakubwa wa Midiani, nao ni Evi, na Rekemu, na Suri, na Huri, na Reba, hao mashehe wa Sihoni, waliokuwa katika nchi hiyo.
22 Balaamu naye, huyo mwana wa Beori, huyo mchawi, wana wa Israeli walimwua kwa upanga kati ya hao wengine waliowaua.
23 Na mpaka wa wana wa Reubeni ulikuwa ni mto wa Yordani, na mpaka wake. Huo ndio urithi wa wana wa Reubeni sawasawa na jamaa zao, miji yake na vijiji vyake.
24 Musa akawapa kabila ya Gadi, hao wana wa Gadi, kwa kadiri ya jamaa zao.
25 Mpaka wao ulikuwa ni Yazeri, na miji hiyo ya Gileadi, na nusu ya nchi ya wana wa Amoni, mpaka Aroeri uliokabili Raba;
26 tena kutoka Heshboni mpaka Ramath-Mizpe, na Betonimu; tena kutoka Mahanaimu hata mpaka wa Debiri;
27 tena katika bonde, Beth-haramu, na Bethnimira, na Sukothi, na Safoni, hiyo iliyosalia ya ufalme wa Sihoni mfalme wa Heshboni, yaani mto wa Yordani na mpaka wake, mpaka mwisho wa bahari ya Kinerethi ng'ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki.
28 Huo ndio urithi wa wana wa Gadi sawasawa na jamaa zao, miji yake na vijiji vyake.
29 Kisha Musa akawapa hao wa nusu ya kabila ya Manase urithi wao; ulikuwa ni wa hiyo nusu ya kabila ya wana wa Manase sawasawa na jamaa zao.
30 Na mpaka wao ulikuwa kutoka huko Mahanaimu, Bashani yote, na ufalme wote wa Ogu mfalme wa Bashani, na miji yote ya Yairi, iliyo katika Bashani, miji sitini;
31 na nusu ya Gileadi, na Ashtarothi, na Edrei, hiyo miji ya ufalme wa Ogu katika Bashani, ilikuwa ni ya wana wa Makiri mwana wa Manase maana, kwa hiyo nusu ya wana wa Makiri sawasawa na jamaa zao.
32 Hizi ndizo mirathi ambazo Musa alizigawanya katika nchi tambarare za Moabu, ng'ambo ya pili ya Yordani, kukabili Yeriko, upande wa mashariki.
33 Lakini Musa hakuwapa kabila ya Lawi urithi uwao wote; yeye Bwana, Mungu wa Israeli, ndiye urithi wao, kama alivyowaambia.

Yoshua 14


1 Kisha hizi ndizo nchi ambazo wana wa Israeli walizitwaa katika nchi ya Kanaani, ambazo Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni, na vichwa vya nyumba za mababa wa kabila za Israeli, waliwagawanyia,
2 kwa kuandama hiyo kura ya urithi wao, vile vile kama Bwana alivyoamuru kwa mkono wa Musa, kwa ajili ya hizo kabila kenda, na hiyo nusu ya kabila.
3 Kwa kuwa Musa alikuwa amekwisha kuwapa urithi hizo kabila mbili na nusu, ng'ambo ya pili ya Yordani; lakini hakuwapa Walawi urithi uwao wote kati yao.
4 Kwa kuwa wana wa Yusufu walikuwa kabila mbili, Manase na Efraimu; nao hawakuwapa Walawi sehemu katika hiyo nchi, isipokuwa waliwapa miji wapate kuikaa, pamoja na viunga vyake kwa ajili ya wanyama wao wa mifugo, na kwa ajili ya riziki zao.
5 Vile vile kama Bwana alivyomwamuru Musa, hao wana wa Israeli walifanya vivyo, nao wakaigawanya hiyo nchi.
6 Wakati huo wana wa Yuda walimkaribia Yoshua hapo Gilgali; na Kalebu, mwana wa Yefune, huyo Mkenizi, akamwambia, Wewe wajua hilo neno Bwana alilomwambia Musa, huyo mtu wa Mungu, katika habari zangu, na katika habari zako wewe, tulipokuwa katika Kadesh-barnea.
7 Mimi nilikuwa mtu wa miaka arobaini umri wangu, hapo Musa mtumishi wa Bwana aliponituma niende kutoka Kadesh-barnea ili kuipeleleza hiyo nchi; nami nilimletea habari tena, kama ilivyokuwa ndani ya moyo wangu.
8 Lakini wale ndugu zangu waliokwea kwenda pamoja nami waliiyeyusha mioyo ya watu; ila mimi nilimfuata Bwana, Mungu wangu, kwa utimilifu.
9 Kisha Musa akaniapia siku hiyo, akasema, Hakika hiyo nchi ambayo miguu yako imekanyaga itakuwa ni urithi kwako wewe, na kwa watoto wako milele, kwa sababu wewe umemfuata Bwana, Mungu wako, kwa utimilifu.
10 Sasa basi, angalia, yeye Bwana ameniweka hai, kama alivyosema, miaka hii arobaini na mitano, tangu wakati huo Bwana alipomwambia Musa neno hilo, wakati Israeli waliokuwa wakienenda barani; na sasa tazama, hivi leo nimepata miaka themanini na mitano umri wangu.
11 Hata sasa mimi nina nguvu zangu hivi leo kama nilivyokuwa siku hiyo Musa aliyonituma; kama nguvu zangu zilivyokuwa wakati huo, na nguvu zangu ndivyo zilivyo sasa, kwa vita na kwa kutoka nje na kuingia ndani.
12 Basi sasa unipe mlima huu, ambao Bwana alinena habari zake siku hiyo; kwani wewe ulisikia siku hiyo jinsi Waanaki walivyokuwa huko, na miji ilivyokuwa mikubwa yenye boma; yumkini yeye Bwana atakuwa pamoja nami, nami nitawafukuza watoke nje, kama Bwana alivyonena.
13 Yoshua akambarikia, akampa Kalebu, huyo mwana wa Yefune, Hebroni kuwa urithi wake.
14 Kwa hiyo Hebroni ukawa urithi wa Kalebu, mwana wa Yefune, Mkenizi, hata leo; kwa sababu alimwandama Bwana, Mungu wa Israeli, kwa utimilifu.
15 Basi jina la Hebroni hapo kwanza uliitwa Kiriath-arba; huyo Arba alikuwa ni mtu mkubwa kupita wenziwe wote katika hao Waanaki. Hiyo nchi nayo ikatulia, vita vikakoma.

Yoshua 15


1 Kura ya kabila ya wana wa Yuda kwa kuandama jamaa zao ilikuwa kufikilia hata mpaka wa Edomu, hata bara ya Sini upande wa kusini, huko mwisho upande wa kusini.
2 Mpaka wao wa kusini ulikuwa kutoka mwisho wa Bahari ya Chumvi, kutoka ile hori ielekeayo kusini;
3 nao ukaendelea upande wa kusini wa kukwea kwenda Akrabimu, kisha ukaendelea hata Sini, kisha ukaenda upande wa kusini wa Kadesh-barnea, kisha ukaendelea karibu na Hesroni, kisha ukafikilia Adari, na kuzunguka kwendea Karka;
4 kisha ukaendelea hata Azmoni, na kutokea hapo penye kijito cha Misri; na matokeo ya huo mpaka yalikuwa baharini; huu ndio mpaka wenu wa upande wa kusini.
5 Na mpaka wa upande wa mashariki ulikuwa Bahari ya Chumvi, hata mwisho wa mto wa Yordani. Na mpaka wa upande wa kaskazini ulikuwa kutoka pale penye hori ya baharini mwisho wa mto wa Yordani;
6 na huo mpaka ukaendelea hata Beth-hogla, kisha ukaendelea upande wa kaskazini wa Beth-araba; kisha mpaka ukaendelea hata jiwe la Bohani mwana wa Reubeni;
7 kisha mpaka ukaendelea hata Debiri kutoka bonde la Akori, vivyo ukaendelea upande wa kaskazini, kwa kuelekea Gilgali, iliyo mkabala wa kukwelea kwenda Adumimu, ulio upande wa kusini wa mto; kisha huo mpaka ukaendelea hata ukafikilia maji ya Enshemeshi, na matokeo yake yalikuwa hapo Enrogeli;
8 kisha mpaka ukaendelea karibu na bonde la mwana wa Hinomu, na kufikilia ubavuni mwa huyu Myebusi upande wa kusini (ndio Yerusalemu); kisha mpaka ukaendelea hata kilele cha mlima ulio pale mkabala wa bonde la Hinomu upande wa magharibi, lililo pale mwisho wa bonde la Warefai upande wa kaskazini;
9 kisha mpaka ulipigwa kutoka juu ya mlima huo hata kufikilia chemchemi ya maji ya Neftoa kisha ukatokea hata miji ya kilima cha Efroni; kisha mpaka ulipigwa hata kufikilia Baala (ndio Kiriath-yearimu);
10 kisha mpaka ukazunguka kutoka Baala kwendelea upande wa magharibi hata kilima Seiri, kisha ukaendelea hata upande wa mlima wa Yearimu upande wa kaskazini (huo ndio Kesaloni), kisha ukatelemkia Beth-shemeshi, na kwendelea karibu na Timna;
11 kisha mpaka ukatokea hata kufikilia upande wa Ekroni upande wa kaskazini; tena mpaka ulipigwa hata Shikroni, na kwendelea hata kilima cha Baala, kisha ukatokea hapo Yabneeli; na matokeo ya mpaka yalikuwa baharini.
12 Na mpaka wa upande wa magharibi ulifikilia hata bahari kubwa, na mpaka wake. Huo ndio mpaka wa wana wa Yuda kwa kuzunguka kote kote sawasawa na jamaa zao.
13 Kisha alimpa huyo Kalebu mwana wa Yefune sehemu kati ya wana wa Yuda, kama Bwana alivyomwamuru Yoshua, maana ni Kiriath-arba, ni huyo Arba aliyekuwa babaye Anaki (huo ndio Hebroni).
14 Huyo Kalebu aliwafukuza watoke hapo hao wana watatu wa Anaki, nao ni Sheshai, na Ahimani, na Talmai, wana wa Anaki.
15 Kisha akakwea kutoka huko ili kuwaendea wenyeji wa Debiri; jina la Debiri hapo kwanza lilikuwa Kiriath-seferi.
16 Kalebu akasema, Yeye atakayeupiga Kiriath-seferi na kuutwaa, mimi nitampa Aksa binti yangu awe mkewe.
17 Naye Othnieli mwana wa Kenazi, nduguye Kalebu, aliutwaa; basi akampa Aksa binti yake awe mkewe.
18 Kisha ikawa, hapo huyo mwanamke alipokwenda kwa mumewe, akamtaka aombe shamba kwa baba yake; akashuka katika punda wake; Kalebu akamwuliza, Wataka nini?
19 Huyo mwanamke akasema, Nipe baraka; kwa kuwa umeniweka katika nchi ya kusini, unipe na chemchemi za maji pia. Ndipo akampa chemchemi za maji ya juu, na chemchemi za maji ya chini.
20 Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Yuda sawasawa na jamaa zao.
21 Miji ya mwisho ya kabila ya wana wa Yuda upande wa kuelekea mpaka wa Edomu katika nchi ya Negebu ilikuwa ni Kabseeli, na Ederi, na Yaguri;
22 na Kina, na Dimona, na Adada;
23 na Kedeshi, na Hazori, na Ithnani;
24 na Zifu, na Telemu, na Bealothi;
25 na Hazor-hadata, na Kerioth-hezroni (ndio Hazori);
26 na Amamu, na Shema, na Molada;
27 na Hasar-gada, na Heshmoni, na Bethpeleti;
28 na Hasarshuali, na Beer-sheba, na Biziothia;
29 na Baala, na Iyimu, na Esemu;
30 na Eltoladi, na Kesili, na Horma;
31 na Siklagi, na Madmana, na Sansana;
32 na Lebaothi, na Shilhimu, na Aini, na Rimoni; miji hiyo yote ni miji ishirini na kenda, pamoja na vijiji vyake.
33 Katika nchi ya Shefela, Eshtaoli, na Sora, na Ashna,
34 na Zanoa, na Enganimu, na Tapua, na Enamu;
35 na Yarmuthi, na Adulamu, na Soko, na Azeka;
36 na Shaarimu, na Adithaimu, na Gedera, na Gederothaimu miji kumi na minne, pamoja na vijiji vyake.
37 Senani, na Hadasha, na Migdal-gadi;
38 na Dilani, na Mispe, na Yoktheeli;
39 na Lakishi, na Boskathi, na Egloni;
40 na Kaboni, na Lamasi, na Kithilishi;
41 na Gederothi, na Beth-dagoni, na Naama, na Makeda; miji kumi na sita, pamoja na vijiji vyake.
42 Libna, na Etheri, na Ashani;
43 na Yifta, na Ashna, na Nesibu;
44 na Keila, na Akizibu, na Maresha; miji kenda, pamoja na vijiji vyake.
45 Ekroni, pamoja na miji yake na vijiji vyake;
46 kutoka huko Ekroni mpaka baharini, yote iliyokuwa upande wa Ashdodi, pamoja na vijiji vyake.
47 Ashdodi, na miji yake na vijiji vyake; na Gaza, na miji yake na vijiji vyake; mpaka kijito cha Misri, na bahari kubwa, na mpaka wake.
48 Na katika nchi ya vilima, Shamiri, na Yatiri, na Soko;
49 na Dana, na Kiriath-sana (ambao ni Debiri);
50 na Anabu, na Eshtemoa, na Animu;
51 na Gosheni, na Holoni, na Gilo; miji kumi na mmoja, pamoja na vijiji vyake.
52 Arabu, na Duma, na Eshani;
53 na Yanumu, na Beth-tapua, na Afeka;
54 na Humta, na Kiriath-arba (ndio Hebroni), na Siori; miji kenda, pamoja na vijiji vyake.
55 Maoni, na Karmeli, na Zifu, na Yuta;
56 na Yezreeli, na Yokdeamu, na Zanoa;
57 na Kaini, na Gibea, na Timna; miji kumi, pamoja na vijiji vyake.
58 Halhuli, na Bethsuri, na Gedori;
59 na Maarathi, na Bethanothi, Eltekoni; miji sita, pamoja na vijiji vyake.
60 Kiriath-baali (ndio Kiriath-yearimu), na Raba; miji miwili, pamoja vijiji vyake.
61 Huko nyikani, Betharaba, na Midini, na Sekaka;
62 na Nibshani, na huo Mji wa Chumvi, na Engedi; miji sita, pamoja na vijiji vyake.
63 Tena katika habari ya Wayebusi, hao wenye kukaa Yerusalemu, wana wa Yuda hawakuweza kuwatoa; lakini hao Wayebusi walikaa pamoja na wana wa Yuda huko Yerusalemu hata hivi leo.

Yoshua 16


1 Kura ya wana wa Yusufu ilianza kutoka mto wa Yordani hapo Yeriko, hapo penye maji ya Yeriko upande wa mashariki, maana, ni hiyo nyika, kukwea kutoka Yeriko kati ya hiyo nchi ya vilima mpaka Betheli;
2 kisha ikatoka huko Betheli kwendelea Luzu, kisha ikaendelea hata kuufikilia mpaka wa Waarki mpaka Atarothi;
3 kisha ikatelemkia upande wa magharibi hata kuufikilia mpaka wa Wayafleti, hata mpaka wa Beth-horoni ya chini, hata kufikilia Gezeri; na matokeo yake yalikuwa hapo baharini.
4 Na wana wa Yusufu, Manase na Efraimu, walitwaa urithi wao.
5 Na mpaka wa wana wa Efraimu kwa kuandama jamaa zao ulikuwa hivi; mpaka na urithi wao upande wa mashariki ulikuwa ni Ataroth-adari, hata Beth-horoni wa juu;
6 kisha mpaka ukatokea kwendelea upande wa magharibi huko Mikmeta upande wa kaskazini; kisha mpaka ukazunguka kwendea upande wa mashariki hata Taanath-shilo, kisha ukaendelea upande wa mashariki wa Yanoa;
7 kisha ulitelemka kutoka Yanoa hata Atarothi, na Naara, kisha ukafikilia Yeriko, na kutokea hapo penye mto wa Yordani.
8 Kutoka hapo Tapua mpaka ukaendelea upande wa magharibi hata kijito cha Kana; na matokeo yake yalikuwa baharini. Huo ndio urithi wa hao wana wa Efraimu kwa kuandama jamaa zao;
9 pamoja na ile miji iliyotengwa kwa ajili ya wana wa Efraimu katikati ya urithi wa hao wana wa Manase, miji yote pamoja na vijiji vyake.
10 Nao hawakuwatoa Wakanaani waliokuwa Wakikaa Gezeri; lakini hao Wakanaani waliketi kati ya Efraimu, hata hivi leo, wakawa watumishi wa kufanya kazi za shokoa.

Yoshua 17


1 Kisha hii ndiyo kura iliyoiangukia kabila ya Manase; maana, yeye alikuwa ni mzaliwa wa kwanza, wa Yusufu. Katika habari za Makiri, mzaliwa wa kwanza wa Manase, babaye Gileadi, kwa sababu alikuwa mtu wa vita, basi alikuwa na Gileadi na Bashani.
2 Na kura ilikuwa ni ya hao wana wa Manase waliosalia kwa kuandama jamaa zao; kwa wana wa Abiezeri, na kwa wana wa Heleki, na kwa wana wa Asrieli, na kwa wana wa Shekemu, na kwa wana wa Heferi, na kwa wana wa Shemida; hao ndio wana waume wa Manase, mwana wa Yusufu, kwa kuandama jamaa zao.
3 Lakini Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, hakuwa na wana waume ila binti; na majina ya hao binti zake walikuwa wakiitwa Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa.
4 Nao wakakaribia mbele ya Eleazari, kuhani, na mbele ya Yoshua, mwana wa Nuni, na mbele ya mashehe, wakasema, Bwana alimwamuru Musa kutupa sisi urithi kati ya ndugu zetu; basi kwa kuiandama hiyo amri ya Bwana akawapa urithi kati ya ndugu za baba yao.
5 Kisha kura zilizomwangukia Manase zilikuwa ni sehemu kumi, mbali na nchi ya Gileadi na Bashani, iliyo ng'ambo ya Yordani;
6 kwa sababu hao binti za Manase walikuwa na urithi katika wanawe waume; na nchi ya Gileadi ilikuwa ni mali ya hao wana waume wa Manase waliosalia.
7 Mpaka wa Manase ulikuwa kutoka Asheri hata Mikmeta, ulioelekea Shekemu; tena mpaka ukaendelea upande wa kuume, hata kuwafikilia wenyeji wa Entapua.
8 Hiyo nchi ya Tapua ilikuwa ni mali ya Manase; lakini ule mji wa Tapua uliokuwa katika mpaka wa Manase ulikuwa ni mali ya wana wa Efraimu.
9 Tena mpaka ulitelemkia mpaka kijito cha Kana, upande wa kusini wa hicho kijito; miji hiyo ilikuwa ya Efraimu kati ya miji ya Manase; na mpaka wa Manase ulikuwa upande wa kaskazini wa hicho kijito, na matokeo yake yalikuwa baharini;
10 upande wa kusini ilikuwa ni mali ya Efraimu, na upande wa kaskazini ilikuwa ni mali ya Manase, na bahari ilikuwa mpaka wake; nao wakafikilia hata Asheri upande wa kaskazini, na kufikilia hata Isakari upande wa mashariki.
11 Tena Manase alikuwa na miji katika Isakari na katika Asheri, nayo ni hii, Bethsheani na vijiji vyake, na Ibleamu na miji yake, na wenyeji wa Dori na miji yake, na wenyeji wa Endori na miji yake, na wenyeji wa Taanaki na miji yake, na wenyeji wa Megido na miji yake, hata mahali patatu palipoinuka.
12 Lakini wana wa Manase hawakuweza kuwafukuza wenyeji wa miji hiyo; bali hao Wakanaani walijikaza ili wakae katika nchi hiyo.
13 Kisha ikawa, hapo hao wana wa Israeli walipokuwa wamepata nguvu zaidi, ndipo wakawatenza nguvu hao Wakanaani wafanye kazi ya shokoa, wala hawakuwafukuza kabisa.
14 Kisha wana wa Yusufu wakanena na Yoshua, wakasema, Kwa nini umenipa mimi kura moja tu na fungu moja kuwa ni urithi wangu, kwa kuwa mimi ni taifa kubwa la watu, kwa sababu Bwana amenibarikia hata hivi sasa?
15 Yoshua akawaambia, Kwamba wewe u taifa kubwa la watu, haya, kwea uende mwituni, ujikatie mahali hapo kwa ajili ya nafsi yako katika nchi ya Waperizi, na ya hao Warefai; ikiwa hiyo nchi ya vilima ya Efraimu ni nyembamba, haikutoshi.
16 Wana wa Yusufu wakasema, Hiyo nchi ya vilima haitutoshi sisi; lakini Wakanaani wote wakaao katika nchi ya bondeni wana magari ya chuma, hao walio katika Bethsheani na miji yake, na hao walio katika bonde la Yezreeli pia.
17 Kisha Yoshua alinena na nyumba ya Yusufu, maana, ni Efraimu na Manase, akawaambia, Wewe u taifa kubwa la watu, nawe una uwezo mwingi; hutapata kura moja tu;
18 lakini hiyo nchi ya vilima itakuwa ni yako; maana, ijapokuwa ni mwitu, wewe utaukata, na matokeo yake yatakuwa ni yako; kwa kuwa wewe utawafukuza hao Wakanaani, wajapokuwa wana magari ya chuma, wajapokuwa ni wenye uwezo.

Yoshua 18


1 Kisha mkutano mzima wa wana wa Israeli walikutana pamoja hapo Shilo, wakasimamisha hema ya kukutania kuko; nayo nchi ilikuwa imeshindwa mbele zao.
2 Zilisalia katika wana wa Israeli kabila saba ambazo hazijagawanyiwa bado urithi wao.
3 Yoshua akawauliza wana wa Israeli, akasema, Je! Hata lini mtakuwa walegevu katika kuingia kwenu na kuimiliki hiyo nchi, ambayo yeye Bwana, Mungu wa baba zenu, amewapa?
4 Haya, jichagulieni watu watatu kwa ajili ya kila kabila; nami nitawatuma, nao watainuka waende kati ya hiyo nchi, na kuiandika kama urithi wao ulivyo; kisha watanijilia mimi.
5 Watu hao wataigawanya nchi iwe mafungu saba; Yuda atakaa katika mpaka wake huko upande wa kusini, na nyumba ya Yusufu watakaa katika mpaka wao upande wa kaskazini.
6 Nanyi mtaiandika nchi iwe mafungu saba, kisha hayo maandiko yake mtaniletea mimi hapa; nami nitawapigia kura hapa mbele ya Bwana, Mungu wetu.
7 Kwa maana Walawi hawana fungu kati yenu; Kwa kuwa huo ukuhani wa Bwana ndio urithi wao; tena Gadi, na Reubeni, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wamekwisha pata urithi wao ng'ambo ya pili ya Yordani upande wa mashariki, ambao walipewa na Musa, mtumishi wa Bwana.
8 Basi watu hao wakainuka wakaenda; kisha Yoshua aliwaagiza wale waliokwenda kuiandika nchi, akawaambia, Endeni, mkapite katikati ya nchi, na kuiandika habari zake, kisha mnijie tena hapa, nami nitawapigia kura kwa ajili yenu hapo mbele za Bwana huko Shilo.
9 Basi watu hao wakaenda, wakapita katikati ya nchi, wakaandika habari zake katika chuo, na kuigawanya kwa miji yake, hata iwe mafungu saba, kisha wakamrejea Yoshua maragoni huko Shilo.
10 Kisha Yoshua akapiga kura kwa ajili yao hapo mbele za Bwana katika Shilo; huko Yoshua akawagawanyia wana wa Israeli hiyo nchi sawasawa na mafungu yao.
11 Kisha ilizuka kura ya kabila ya wana wa Benyamini kwa kuandama jamaa zao; na mpaka wa hiyo kura yao ukatokea kati ya wana wa Yuda na wana wa Yusufu.
12 Mpaka wao upande wa kaskazini ulikuwa kutoka mto wa Yordani; kisha mpaka ukaendelea kufikilia ubavuni mwa mji wa Yeriko upande wa kaskazini, kisha ukaendelea kati ya nchi ya vilima kwa kuelekea upande wa magharibi; na matokeo yake yalikuwa hapo penye nyika ya Bethaveni.
13 Kisha mpaka ukaendelea kutoka hapo na kufikilia mji wa Luzu, ubavuni mwa Luzu (ndio Betheli), kwa upande wa kusini; kisha mpaka ukatelemkia Ataroth-adari, karibu na mlima ulio upande wa kusini wa Beth-horoni wa chini.
14 Kisha mpaka uliendelea na kuzunguka upande wa magharibi wa kuelekea kusini, kutoka huo mlima ulio mkabala wa Beth-horoni upande wa kusini; na matokeo yake yalikuwa hapo Kiriath-baali (ndio Kiriath-yearimu), ni mji wa wana wa Yuda; huo ndio upande wa magharibi.
15 Na upande wa kusini ulikuwa ukitoka upande wa mwisho wa Kiriath-yearimu, na mpaka ukatokea upande wa magharibi, ukaendelea hata chemchemi ya maji, pale Neftoa;
16 kisha mpaka ulitelemka hata mwisho wa mlima ulio pale mkabala wa bonde la mwana wa Hinomu, lililo pale katika bonde la Warefai, upande wa kaskazini; nao ukatelemkia mpaka bonde la Hinomu, hata ubavuni mwa Myebusi upande wa kusini, kisha ukatelemka hata Enrogeli,
17 kisha ulipigwa upande wa kaskazini, nao ukatokea hapo Enshemeshi, ukatokea hata kufikilia Gelilothi, ambao ni mkabala wa makweleo ya Adumimu; kisha ulitelemka hata jiwe la Bohani mwana wa Reubeni;
18 kisha ukaendelea mbele ubavuni kuikabili Araba, upande wa kuelekea kaskazini, nao ukatelemka hata hiyo Araba;
19 kisha mpaka ukaendelea mbele ubavuni mwa Beth-hogla upande wa kaskazini; na matokeo ya mpaka yalikuwa katika ile hori ya kaskazini ya Bahari ya Chumvi, mwisho wa kusini wa mto wa Yordani; huo ndio mpaka wa upande wa kusini.
20 Na mto wa Yordani ulikuwa ndio mpaka wake upande wa mashariki. Huo ndio urithi wa wana wa Benyamini, kwa kuandama mipaka yake kwa kuuzunguka kote kote, sawasawa na jamaa zao.
21 Basi miji ya kabila ya wana wa Benyamini kwa kuandama jamaa zao ilikuwa ni Yeriko, na Beth-hogla, na Emek-kesisi,
22 na Bethiaraba, na Semaraimu, na Betheli;
23 na Avimu, na Para, na Ofra;
24 na Kefar-amoni, na Ofni, na Geba; miji kumi na miwili, pamoja na vijiji vyake;
25 na Gibeoni, na Rama, na Beerothi;
26 na Mispa, na Kefira, na Moza;
27 na Rekemu, na Irpeeli, na Tarala;
28 na Zela, na Elefu, na huyo Myebusi (ndio Yerusalemu), na Gibeathi, na Kiriathi; miji kumi na minne, pamoja na vijiji vyake. Huo ndio urithi wa wana wa Benyamini kwa kuandama jamaa zao.

Yoshua 19


1 Kisha kura ya pili ilitokea kwa ajili ya Simeoni, maana, kwa ajili ya hiyo kabila ya wana wa Simeoni, kwa kuandama jamaa zao; na urithi wao ulikuwa katikati ya urithi wa wana wa Yuda.
2 Miji waliyokuwa nayo katika urithi wao ni Beer-sheba, na Sheba, na Molada;
3 na Hasarshuali, na Bala, na Esemu;
4 na Eltoladi, na Bethuli, na Horma;
5 na Siklagi, na Bethmarkabothi, na Hasarsusa;
6 na Bethlebaothi, na Sharuheni; miji kumi na mitatu, pamoja na vijiji vyake;
7 na Aini, na Rimoni, na Etheri, na Ashani; miji minne, pamoja na vijiji vyake;
8 tena vijiji vyote vilivyozunguka miji hiyo kote kote mpaka Baalath-beeri, Rama wa Kusini. Huo ndio urithi wa kabila ya wana wa Simeoni kwa kuandama jamaa zao.
9 Huo urithi wa hao wana wa Simeoni ulitoka katika fungu la wana wa Yuda; kwa maana hilo fungu la wana wa Yuda lilikuwa ni kubwa mno kwao; kwa hiyo wana wa Simeoni walikuwa na urithi katikati ya urithi wao.
10 Kisha kura ya tatu ilitokea kwa ajili ya wana wa Zabuloni kwa kuandama jamaa zao; na mpaka wa urithi wao ulifikilia hata Saridi;
11 kisha mpaka wao ukakwea kwendelea upande wa magharibi, hata kufikilia Marala, nao ukafikilia hata Dabeshethi; nao ukafikilia kijito cha maji kilicho mkabala wa Yokneamu;
12 kisha ukazunguka kutoka Saridi kwendelea upande wa mashariki kwa kuelekea maawio ya jua hata kufikilia mpaka wa Kisiloth-ubori; kisha ukatokea hata Daberathi, kisha ukakwea kwendelea Yafia;
13 kutoka hapo ukaendelea kuelekea mashariki mpaka Gath-heferi, hata kufikilia Ethkasini; kisha ukatokea huko Rimoni ufikiliao hata Nea;
14 kisha mpaka uliizunguka nchi hiyo kwa upande wa kaskazini hata Hanathoni; kisha matokeo yake yalikuwa katika bonde la Iftaeli;
15 na Katathi, na Nahalali, na Shimroni, na Idala, na Bethlehemu; miji kumi na miwili, pamoja na vijiji vyake.
16 Huu ndio urithi wa wana wa Zabuloni kwa kuandama jamaa zao; miji hii pamoja na vijiji vyake.
17 Kisha kura ya nne ilitokea kwa ajili ya Isakari, maana, ni kwa ajili ya wana wa Isakari kwa kuandama jamaa zao.
18 Na mpaka wao ulifikilia Yezreeli, na Kesulothi, na Shunemu;
19 na Hafaraimu, na Shioni, na Anaharathi;
20 na Rabithu, na Kishioni, na Ebesi;
21 na Remethi, na Enganimu, na Enhada, na Bethpasesi;
22 na mpaka ukafikilia hata Tabori, na Shahasuma na Bethshemeshi; na matokeo ya mpaka wao yalikuwa katika mto wa Yordani; miji kumi na sita, pamoja na vijiji vyake.
23 Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Isakari kwa kuandama jamaa zao; miji hiyo pamoja na vijiji vyake.
24 Kisha kura ya tano ilitokea kwa ajili ya kabila ya wana wa Asheri kwa kuandama jamaa zao.
25 Na mpaka wao ulikuwa ni Helkathi, na Hali, na Beteni, na Akishafu;
26 na Alameleki, na Amadi, na Mishali; nao ukafikilia hata Karmeli upande wa magharibi, tena ulifikilia hata Shihor-libnathi;
27 kisha ukazunguka kuelekea maawio ya jua mpaka Beth-dagoni, nao ukafikilia hata Zabuloni, tena mpaka bonde la Iftaeli upande wa kaskazini hata Bethemeki na Neyeli; kisha ukatokea hata Kabuli upande wa kushoto;
28 na Ebroni, na Rehobu, na Hamoni, na Kana, hata kufikilia Sidoni mkuu;
29 kisha mpaka ulizunguka kuelekea Rama, na mji wa Tiro ulio na boma; kisha mpaka ulizunguka kuelekea Hosa; na matokeo yake yalikuwa baharini katika nchi ya Akzibu;
30 na Uma pia, na Afeka, na Rehobu; miji ishirini na miwili, pamoja na vijiji vyake.
31 Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Asheri kwa kuandama jamaa zao; miji hii pamoja na vijiji vyake.
32 Kisha kura ya sita ikatokea kwa ajili ya wana wa Naftali, maana, ni kwa ajili ya wana wa Naftali kwa kuandama jamaa zao.
33 Na mpaka wao ulikuwa kutoka Helefu, tokea ule mwaloni ulio katika Saananimu, na Adami-nekebu, na Yabineeli, hata kufikilia Lakumu; na matokeo yake yalikuwa katika mto wa Yordani;
34 tena mpaka ulizunguka kwendelea upande wa magharibi hata Aznoth-tabori, tena kutoka hapo ukaendelea mpaka Hukoki; kisha ukafikilia hata Zabuloni upande wa kusini, tena ulifikilia hata Asheri upande wa magharibi, tena ulifikilia hata Yuda hapo katika mto wa Yordani kwa upande wa kuelekea maawio ya jua.
35 Na miji yenye boma ilikuwa ni hii, Sidimu, na Seri, na Hamathi, na Rakathi, na Kinerethi;
36 na Adama, na Rama, na Hazori;
37 na Kedeshi, na Edrei, na Enhasori;
38 na Ironi, na Migdal-eli, na Horemu, na Bethanathi, na Bethshemeshi; miji kumi na kenda, pamoja na vijiji vyake.
39 Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Naftali kwa kuandama jamaa zao; miji hiyo pamoja na vijiji vyake.
40 Kisha kura ya saba ilitokea kwa ajili ya kabila ya wana wa Dani kwa kuandama jamaa zao.
41 Na mpaka wa urithi wao ulikuwa ni Sora, na Eshtaoli, na Irishemeshi;
42 na Shaalabini, na Aiyaloni, na Ithla;
43 na Eloni, na Timna, na Ekroni;
44 na Elteka, na Gibethoni, na Baalathi;
45 na Yehudi, na Bene-beraki, na Gathrimoni;
46 na Meyarkoni, na Rakoni, pamoja na huo mpaka uliokuwa mkabala wa Yafa.
47 Kisha mpaka wa wana wa Dani ulitokea kuwapita wao; kwa kuwa hao wana wa Dani wakakwea na kupigana na Leshemu, na kuutwaa, na kuupiga kwa makali ya upanga, na kuumiliki, nao wakakaa humo, wakauita Dani, kwa kuliandama jina la huyo Dani mzee wao.
48 Huu ndio urithi wa kabila ya wana wa Dani kwa kuandama jamaa zao; miji hii pamoja na vijiji vyake.
49 Basi wakamaliza hiyo kazi yao ya kuigawanya nchi iwe urithi kwa kuandama mipaka yake; kisha wana wa Israeli wakampa Yoshua, mwana wa Nuni, urithi katikati yao;
50 sawasawa na ile amri ya Bwana wakampa mji alioutaka, maana, ni Timnath-sera katika nchi ya vilima ya Efraimu; naye akaujenga huo mji na kukaa mumo.
51 Hizi ndizo nchi, ambazo Eleazari kuhani, na Yoshua huyo mwana wa Nuni, pamoja na hao vichwa vya nyumba za mababa ya kabila za wana wa Israeli, walizigawanya kwa njia ya kupiga kura, ziwe urithi, huko Shilo mbele ya Bwana, hapo mlangoni mwa hema ya kukutania. Basi hivyo wakamaliza kazi ya kuigawanya hiyo nchi.

Yoshua 20


1 Kisha Bwana akanena na Yoshua, na kumwambia,
2 Nena wewe na wana wa Israeli, uwaambie, Haya, toeni hiyo miji ya makimbilio, ambayo niliwaambia habari zake kwa mkono wa Musa;
3 ili kwamba mwenye kuua mtu, aliyemwua mtu awaye yote pasipo kukusudia, na pasipo kujua, apate kukimbilia kuko; nayo itakuwa ni mahali pa kukimbilia kwenu, kumkimbia huyo ajilipizaye kisasi cha damu.
4 Naye ataikimbilia miji hiyo mmojawapo, naye atasimama hapo penye maingilio ya lango la huo mji, kisha atanena neno lake masikioni mwa wazee wa mji; nao watamtia kwao ndani ya mji, na kumpa mahali, ili apate kukaa kati yao.
5 Na kama huyo mwenye kujilipiza kisasi cha damu akimwandamia, ndipo hawatamtoa huyo mwuaji kumtia mkononi mwake huyo; kwa sababu alimpiga mwenziwe naye hakujua, wala hakumchukia tangu hapo.
6 Naye atakaa katika mji huo, hata hapo atakaposimama mbele ya mkutano kuhukumiwa, hata kifo chake kuhani mkuu mwenye kuwapo siku hizo; ndipo yule mwuaji atarudi, na kuuendea mji wake mwenyewe, na nyumba yake mwenyewe, hata mji huo alioutoka hapo alipokimbia.
7 Nao wakaweka Kedeshi katika Galilaya katika nchi ya vilima ya Naftali, na Shekemu katika nchi ya vilima ya Efraimu, na Kiriath-arba (ndio Hebroni) katika nchi ya vilima ya Yuda.
8 Tena ng'ambo ya pili ya Yordani pande za Yeriko upande wa kuelekea mashariki wakaweka Bezeri ulioko nyikani, katika nchi tambarare ya kabila ya Reubeni, na Ramothi katika Gileadi katika kabila ya Gadi, na Golani katika Bashani katika kabila ya Manase.
9 Miji hiyo ndiyo miji iliyoamriwa kwa ajili ya wana wa Israeli wote, na kwa ajili ya mgeni akaaye kati yao ugenini, ili kwamba mtu awaye yote atakayemwua mtu pasipo kukusudia apate kimbilia huko, asife kwa mkono wa mwenye kujilipiza kisasi cha damu, hata hapo atakapokuwa amekwisha simama mbele ya mkutano.

Yoshua 21


1 Wakati huo hao vichwa vya nyumba za mababa ya Walawi wakamwendea Eleazari, kuhani, na Yoshua, mwana wa Nuni, na hao waliokuwa vichwa vya nyumba za mababa ya kabila za wana wa Israeli;
2 wakanena nao hapo Shilo katika nchi ya Kanaani, wakisema, Yeye Bwana aliamuru kwa mkono wa Musa kwamba sisi tupewe miji tupate kukaa humo, pamoja na malisho yake kwa ajili ya wanyama wetu wa mifugo.
3 Basi wana wa Israeli wakawapa Walawi miji hii, pamoja na malisho yake, katika urithi wao, sawasawa na hiyo amri ya Bwana.
4 Kura ikatokea kwa ajili ya jamaa za Wakohathi; na wana wa Haruni kuhani, waliokuwa katika Walawi, walipata miji kumi na mitatu kwa kura katika kabila ya Yuda, na katika kabila ya Simeoni, na katika kabila ya Benyamini.
5 Kisha Wakohathi wengine waliosalia walipata kwa kura katika jamaa za kabila ya Efraimu, na katika kabila ya Dani, na katika hiyo nusu ya kabila ya Manase, miji kumi.
6 Tena wana wa Gershoni walipata kwa kura katika jamaa za kabila ya Isakari, na katika kabila ya Asheri, na katika kabila ya Naftali, na katika hiyo nusu ya kabila ya Manase huko Bashani, miji kumi na mitatu.
7 Na wana wa Merari kwa kuandama jamaa zao walipata katika kabila ya Reubeni, na katika kabila ya Gadi, na katika kabila ya Zabuloni, miji kumi na miwili.
8 Kisha wana wa Israeli waliwapa Walawi kwa kura miji hiyo pamoja na malisho yake, kama Bwana alivyoamuru kwa mkono wa Musa.
9 Kisha wakawapa katika kabila ya wana wa Yuda, na katika kabila ya wana wa Simeoni, miji hii iliyotajwa hapa kwa majina;
10 nayo ilikuwa kwa ajili ya wana wa Haruni, wa jamaa ya Wakohathi, waliokuwa wa wana wa Lawi; kwa kuwa kura ya kwanza ilikuwa ni yao.
11 Nao wakawapa Kiriath-arba, huyo Arba alikuwa baba yake Anaki, (ndio Hebroni), katika nchi ya vilima ya Yuda, pamoja na malisho yake yaliyouzunguka pande zote.
12 Lakini mashamba ya mji, na vile vijiji vyake, wakampa Kalebu mwana wa Yefune kuwa milki yake.
13 Kisha wakawapa wana wa Haruni kuhani Hebroni pamoja na malisho yake, huo mji wa kukimbilia kwa ajili ya mwuaji, na Libna pamoja na malisho yake;
14 na Yatiri pamoja na malisho yake, na Eshtemoa pamoja na malisho yake;
15 na Holoni pamoja na malisho yake, na Debiri pamoja na malisho yake;
16 na Aini pamoja na malisho yake, na Yuta pamoja na malisho yake, na Bethshemeshi pamoja na malisho yake; miji kenda katika kabila hizo mbili.
17 Tena katika kabila ya Benyamini, Gibeoni pamoja na malisho yake, na Geba pamoja na malisho yake;
18 na Anathothi pamoja na malisho yake, na Almoni pamoja na malisho yake; miji minne.
19 Miji yote ya wana wa Haruni, makuhani, ilikuwa ni miji kumi na mitatu, pamoja na malisho yake.
20 Na jamaa za wana wa Kohathi, Walawi, hao wana wengine wa Kohathi waliosalia, wao walikuwa na miji ya kura yao katika kabila ya Efraimu.
21 Nao wakawapa Shekemu pamoja na malisho yake, katika nchi ya vilima ya Efraimu, huo mji wa makimbilio kwa ajili ya mwuaji; na Gezeri pamoja na malisho yake;
22 na Kibisaumu pamoja na malisho yake, na Beth-horoni pamoja na malisho yake, miji minne.
23 Tena katika kabila ya Dani Elteke pamoja na malisho yake, na Gibethoni pamoja na malisho yake;
24 na Aiyaloni pamoja na malisho yake, na Gath-rimoni pamoja na malisho yake; miji minne.
25 Tena katika hiyo nusu ya kabila ya Manase, Taanaki pamoja na malisho yake, na Gath-rimoni pamoja na malisho yake; miji miwili.
26 Miji yote ya jamaa za wana wa Kohathi waliosalia ilikuwa ni miji kumi, pamoja na malisho yake.
27 Tena wana wa Gershoni, katika jamaa za Walawi, waliwapa, katika hiyo nusu ya kabila ya Manase, Golani katika Bashani pamoja na malisho yake, huo mji wa makimbilio kwa ajili ya mwuaji; na Beeshtera pamoja na malisho yake; miji miwili.
28 Tena katika kabila ya Isakari, Kishioni pamoja na malisho yake, na Daberathi pamoja na malisho yake;
29 na Yarmuthi pamoja na malisho yake, na Enganimu pamoja na malisho yake; miji minne.
30 Tena katika kabila ya Asheri, Mishali pamoja na malisho yake, na Abdoni pamoja na malisho yake;
31 na Helkathi pamoja na malisho yake, na Rehobu pamoja na malisho yake; miji minne.
32 Tena katika kabila ya Naftali, Kedeshi katika Galilaya pamoja na malisho yake, huo mji wa makimbilio kwa ajili ya mwuaji, na Hamoth-dori pamoja na malisho yake, na Kartani pamoja na malisho yake; miji mitatu.
33 Miji yote ya Wagershoni kwa kuandama jamaa zao ilikuwa ni miji kumi na mitatu, pamoja na malisho yake.
34 Tena jamaa za wana wa Merari, hao Walawi waliosalia, katika kabila ya Zabuloni, Yokneamu pamoja na malisho yake, na Karta pamoja na malisho yake,
35 na Dimna pamoja na malisho yake, na Nahalali pamoja na malisho yake; miji minne.
36 Tena katika kabila ya Reubeni, Bezeri pamoja na malisho yake, na Yahasa pamoja na malisho yake,
37 na Kedemothi pamoja na malisho yake, na Mefaathi pamoja na malisho yake; miji minne.
38 Tena katika kabila ya Gadi Ramothi katika Gileadi pamoja na malisho yake, huo mji wa makimbilio kwa ajili ya mwuaji, na Mahanaimu pamoja na malisho yake;
39 na Heshboni pamoja na malisho yake, na Yazeri pamoja na malisho yake; jumla yake miji minne.
40 Miji hiyo yote ilikuwa ni miji ya wana wa Merari kwa kuandama jamaa zao, ni hizo jamaa za Walawi zilizosalia; na kura yao ilikuwa ni miji kumi na miwili.
41 Miji yote ya Walawi iliyokuwa kati ya milki ya wana wa Israeli ilikuwa ni miji arobaini na minane, pamoja na malisho yake.
42 Miji hiyo kila mmoja ulikuwa pamoja na malisho yake, yaliyouzunguka pande zote; ndivyo ilivyokuwa katika miji hiyo yote.
43 Basi Bwana aliwapa Israeli nchi hiyo yote, ambayo aliapa kwamba atawapa baba zao; nao wakaimiliki, na kukaa mumo.
44 Kisha Bwana akawapa raha pande zote, sawasawa na hayo yote aliyokuwa amewaapia baba zao; wala katika adui zao wote hakusimama hata mtu mmoja miongoni mwao mbele zao; yeye Bwana akawatia adui zao wote mikononi mwao.
45 Halikuanguka neno lo lote katika jambo lo lote lililokuwa ni jema ambalo Bwana alikuwa amelinena katika habari ya nyumba ya Israeli; yalitimia mambo yote.

Yoshua 22


1 Wakati huo Yoshua akawaita Wareubeni, na Wagadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase,
2 naye akawaambia, Ninyi mmeyaandama hayo yote mliyoamriwa na Musa, mtumishi wa Bwana, nanyi mmeisikia sauti yangu katika yote niliyowaamuru mimi;
3 hamkuwaacha hao ndugu zenu siku hizi nyingi hata hivi leo, lakini mmeyashika mausia ya amri ya Bwana, Mungu wenu.
4 Na sasa yeye Bwana, Mungu wenu, amewapa ndugu zenu kustarehe, kama alivyowaambia; basi sasa rudini ninyi mwende mahemani kwenu, hata nchi ya milki yenu, ambayo huyo Musa, mtumishi wa Bwana, aliwapa ng'ambo ya pili ya Yordani.
5 Lakini mjibidiishe sana kuzifanya amri na sheria, ambazo Musa, mtumishi wa Bwana, aliwaamuru, kumpenda Bwana, Mungu wenu, na kwenenda katika njia zake zote, na kuzishika amri zake, na kushikamana na yeye, na kumtumikia kwa moyo wenu wote na nafsi yenu yote.
6 Basi Yoshua akawabarikia, na kuwapa ruhusa waende zao; nao wakaenda mahemani kwao.
7 Basi Musa alikuwa amewapa hiyo nusu moja ya kabila ya Manase urithi katika Bashani; lakini hiyo nusu ya pili Yoshua aliwapa urithi kati ya ndugu zao, ng'ambo ya Yordani upande wa kuelekea magharibi. Zaidi ya hayo Yoshua, hapo alipowapeleka waende zao mahemani kwao, akawabarikia,
8 kisha akanena nao, na kuwaambia, Rudini na mali mengi mahemani kwenu, na ng'ombe wengi sana, na fedha, na dhahabu, na shaba, na chuma, na mavao mengi sana; mzigawanye na ndugu zenu hizo nyara za adui zenu.
9 Basi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase wakarudi, wakatoka kwa wana wa Israeli katika Shilo, ulioko nchi ya Kanaani, ili waende nchi ya Gileadi, hiyo nchi ya milki yao, waliyokuwa wanaimiliki, sawasawa na amri ya Bwana kwa mkono wa Musa.
10 Nao walipofika pande za Yordani, zilizo katika nchi ya Kanaani, hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na nusu ya kabila ya Manase, wakajenga madhabahu huko karibu na Yordani, iliyoonekana kuwa ni madhabahu kubwa.
11 Wana wa Israeli walisikia ikinenwa, Tazama, wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wamejenga madhabahu huko upande wa mbele wa nchi ya Kanaani, katika nchi iliyo karibu na Yordani, kwa upande huo ulio milki ya wana wa Israeli.
12 Basi, wana wa Israeli waliposikia habari hiyo, mkutano wote wa wana wa Israeli wakakutanika pamoja huko Shilo, ili waende kupigana nao.
13 Kisha wana wa Israeli wakatuma wajumbe waende kwa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, hata nchi ya Gileadi; nao ni hawa, Finehasi mwana wa Eleazari kuhani;
14 na pamoja naye wakuu kumi, mkuu mmoja wa nyumba ya mababa kwa ajili ya kila kabila ya Israeli; nao kila mmoja alikuwa ni kichwa cha nyumba ya mababa katika maelfu ya Israeli.
15 Nao wakawafikilia hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, katika nchi ya Gileadi, na wakasema nao, wakinena,
16 Mkutano wote wa Bwana wanena, Ni kosa gani hili mlilolikosa juu ya Mungu wa Israeli, hata mkakengeuka hivi leo na kuacha kumwandama Bwana, katika kujijengea madhabahu, na kuasi hivi leo juu ya Bwana?
17 Je! Ule uovu wa Peori haututoshi, ambao hamjajitakasa nafsi zenu katika huo hata hivi leo, ijapokuwa ilikuja tauni juu ya mkutano wa Bwana,
18 hata ikawa hamna budi hivi leo kugeuka na kuacha kumwandama Bwana? Kisha itakuwa, kwa kuwa ninyi mwamwasi Bwana hivi leo, kwamba kesho yeye atakasirika na mkutano wote wa Israeli.
19 Basi kwamba hiyo nchi ya milki yenu si tohara, ndipo ninyi vukeni na kuingia nchi ya milki yake Bwana, ambayo maskani ya Bwana inakaa ndani yake, nanyi twaeni milki kati yetu; lakini msimwasi Bwana, wala msituasi sisi, kwa kujijengea madhabahu zaidi ya hiyo madhabahu ya Bwana, Mungu wetu.
20 Je! Huyo Akani mwana wa Zera hakukosa katika vile vitu vilivyowekwa wakfu, na hasira ikauangukia mkutano wote wa Israeli? Kisha mtu huyo hakuangamia peke yake katika uovu wake?
21 Ndipo hapo wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, wakajibu, na kuwaambia hao waliokuwa ni vichwa vya maelfu ya Israeli, wakasema,
22 Mungu, Mungu Bwana, naam, Mungu, Mungu Bwana, yeye yuajua, na Israeli naye atajua; kama ni katika uasi, au kama ni katika kosa juu ya Bwana, (usituokoe hivi leo);
23 sisi kujijengea madhabahu ili kukengeuka na kuacha kumwandama Bwana; au kama ni kusongeza juu yake sadaka ya kuteketezwa, au sadaka ya unga, au kama ni kusongeza sadaka za amani juu yake, yeye Bwana mwenyewe na alitake jambo hili;
24 au kama sisi tumefanya jambo hili kwa hadhari sana, tena makusudi, huku tukisema, Katika siku zijazo wana wenu yamkini wakanena na wana wetu, na kusema, Ninyi mna nini na Bwana, yeye Mungu wa Israeli?
25 Kwa kuwa yeye Bwana ameufanya huu mto wa Yordani uwe mpaka katikati ya sisi na ninyi, enyi wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, hamna fungu katika Bwana; basi hivyo wana wenu wangewakomesha wana wetu wasimche Bwana.
26 Kwa ajili ya hayo tulisema, Na tufanye tayari ili kujijengea madhabahu, si kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, wala kwa sadaka yo yote;
27 bali itakuwa ni ushahidi kati ya sisi na ninyi, tena kati ya vizazi vyetu baada yetu, ili kwamba tufanye huo utumishi wa Bwana mbele yake kwa njia ya sadaka zetu za kuteketezwa, na kwa dhabihu zetu, na kwa sadaka zetu za amani; ili kwamba wana wenu wasiwaambie wana wetu katika zamani zijazo, Ninyi hamna fungu katika Bwana.
28 Kwa hiyo tulisema, Itakuwa, hapo watakapotuambia neno kama hilo, au kuwaambia watu wa vizazi vyetu katika zamani zijazo neno kama hilo, ndipo sisi tutawaambia, Angalieni huu mfano wa madhabahu ya Bwana, walioufanya baba zetu, si kwa ajili ya sadaka ya kuteketezwa, wala kwa ajili ya dhabihu; lakini ni ushahidi kati ya sisi na ninyi.
29 Mungu na atuzuie msimwasi Bwana, na kukengeuka hivi leo na kuacha kumwandama Bwana, hata mkajenga madhabahu kwa ajili ya sadaka za kuteketezwa, au sadaka za unga, au dhabihu, mbali na ile madhabahu ya Bwana, Mungu wetu, iliyo huko mbele ya maskani yake.
30 Basi Finehasi kuhani, na wakuu wa mkutano, maana, ni hao waliokuwa vichwa vya maelfu ya Israeli waliokuwa pamoja naye, hapo walipoyasikia hayo maneno waliyoyasema hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, maneno hayo yaliwaridhia sana.
31 Naye Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, akawaambia wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, na wana wa Manase, akasema, Siku hii ya leo twajua ya kwamba Bwana yu kati yetu, kwa sababu hamkukosa katika jambo hili mbele ya Bwana; sasa ninyi mmewaokoa wana wa Israeli na mkono wa Bwana.
32 Kisha Finehasi, mwana wa Eleazari, kuhani, na hao wakuu, wakarudi na kuwaacha wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, wakatoka katika nchi ya Gileadi, na kuingia nchi ya Kanaani; wakawarudia wana wa Israeli, wakawapa habari.
33 Wana wa Israeli nao wakaliridhia jambo hilo; nao wana wa Israeli wakamhimidi Mungu, wala hawakusema tena habari ya kuwaendea juu yao kupigana nao, wala kuiharibu nchi waliyoikaa wana wa Reubeni, na wana wa Gadi.
34 Basi hao wana wa Reubeni, na wana wa Gadi, wakaiita madhabahu hiyo Edi; wakasema, Kwa kuwa ni ushahidi kati yetu ya kwamba yeye Bwana ndiye Mungu.

Yoshua 23


1 Hata ikawa baada ya siku nyingi, Bwana alipokuwa amekwisha kuwapa Israeli raha mbele ya adui zao pande zote, naye Yoshua alipokuwa mzee, mwenye miaka mingi sana,
2 Yoshua akawaita Israeli wote, wazee wao, na wakuu wao, na makadhi yao, na maakida yao, akawaambia, Mimi ni mzee, nami nimekwendelea sana katika miaka yangu;
3 nanyi mmeona mambo yote ambayo Bwana, Mungu wenu, amewatenda mataifa haya yote kwa ajili yenu; kwa maana Bwana, Mungu wenu, ndiye aliyewapigania ninyi.
4 Tazama, nimewagawieni kwa kura mataifa haya yaliyobaki, yawe urithi kwa kabila zenu, toka mto wa Yordani, pamoja na mataifa yote niliyowakatilia mbali, mpaka bahari kubwa upande wa machweo ya jua.
5 Yeye Bwana, Mungu wenu, atawatoa kwa nguvu mbele yenu, atawafukuza wasiwe mbele ya macho yenu tena; nanyi mtaimiliki nchi yao, kama Bwana Mungu wenu, alivyowaambia.
6 Basi, iweni mashujaa sana kuyashika yote yaliyoandikwa katika kitabu cha torati ya Musa, na kuyatenda, msiyaache kwa kugeukia upande wa kuume wala upande wa kushoto.
7 Msiingie kati ya mataifa haya, yaani, haya yaliyobaki kati yenu; wala msitaje majina ya miungu yao, wala kuwaapisha watu kwa majina hayo, wala kuitumikia, wala kujiinamisha mbele yao;
8 bali shikamaneni na Bwana, Mungu wenu, kama mlivyotenda hata hivi leo.
9 Maana Bwana amefukuza mbele yenu mataifa walio hodari, kisha wenye nguvu, lakini kwenu ninyi hapana mtu aliyesimama mbele yenu hata leo.
10 Mtu mmoja miongoni mwenu atafukuza watu elfu; maana Bwana, Mungu wenu, ndiye anayewapigania, kama alivyowaambia.
11 Jihadharini nafsi zenu, basi, ili mmpende Bwana, Mungu wenu.
12 Lakini mkirudi nyuma kwa njia yo yote na kushikamana na mabaki ya mataifa, yaani, mataifa haya yaliyobaki kati yenu, na kuoana nao, na kuingia kwao, nao kuingia kwenu;
13 jueni hakika ya kuwa Bwana, Mungu wenu, hatawafukuza tena mataifa haya mbele ya macho yenu, bali watakuwa mtego kwenu na tanzi, na mjeledi mbavuni mwenu, na miiba machoni mwenu, hata mtakapoangamia na kutoka katika nchi hii njema, ambayo Bwana, Mungu wenu, amewapa ninyi.
14 Angalieni, mimi leo ninakwenda njia ile waendayo watu wote wa ulimwengu; nanyi nyote mnajua mioyoni mwenu, na rohoni mwenu, ya kuwa halikuwapungukia ninyi hata neno moja katika mambo hayo mema yote aliyoyanena Bwana, Mungu wenu, katika habari zenu; yote yametimia kwenu hapana neno lo lote mlilopungukiwa.
15 Kisha itakuwa, kama yalivyowafikilia yale mambo mema yote, Bwana, Mungu wenu, aliyowaahidia ninyi, kadhalika Bwana atawafikilizia mabaya yote, hata atakapokuwa amewaangamiza katika nchi hii njema, Bwana Mungu wenu, aliyowapa.
16 Hapo mtakapolivunja agano la Bwana, Mungu wenu, alilowaamuru, na kwenda kuitumikia miungu mingine, na kujiinamisha mbele yao, ndipo hasira ya Bwana itakapowaka juu yenu, nanyi mtaangamia upesi katika nchi hii njema aliyowapa.

Yoshua 24


1 Yoshua akawakusanya kabila zote za Israeli huko Shekemu, akawaita wazee wa Israeli, na wakuu wao, na waamuzi wao, na maakida wao nao wakahudhuria mbele za Mungu.
2 Yoshua akawaambia watu wote, Bwana, Mungu wa Israeli, asema hivi, Baba zenu hapo zamani walikaa ng'ambo ya Mto, maana Tera, baba yake Ibrahimu, naye ni baba yake Nahori; wakaitumikia miungu mingine.
3 Nami nikamtwaa Ibrahimu baba yenu toka ng'ambo ya Mto, nikamwongoza katika nchi yote ya Kanaani; nikaongeza uzao wake, nikampa Isaka.
4 Kisha nikampa huyo Isaka, Yakobo na Esau; nami nikampa Esau mlima Seiri aumiliki; Yakobo na watoto wake wakashuka Misri.
5 Kisha nikawatuma Musa na Haruni nikaipiga nchi ya Misri, kwa hayo yote niliyoyatenda kati yake; hatimaye nikawatoa ninyi.
6 Nikawatoa baba zenu watoke Misri; nanyi mkaifikilia bahari; Wamisri wakawafuatia baba zenu kwa magari na wapanda farasi mpaka bahari ya Shamu.
7 Nao walipomlilia Bwana, akaweka giza kati ya ninyi na Wamisri, akaileta bahari juu yao, akawafunikiza; nayo macho yenu yaliyaona mambo niliyoyatenda huko Misri; kisha mkakaa jangwani siku nyingi.
8 Kisha nikawaleta na kuwaingiza katika nchi ya Waamori waliokaa ng'ambo ya pili ya Yordani; nao wakapigana nanyi; nikawatia mikononi mwenu, mkaimiliki nchi yao; nami nikawaangamiza mbele yenu.
9 Ndipo Balaki, mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, akainuka, akapigana na Israeli; tena akatuma watu akamwita Balaamu, mwana wa Beori, aje awalaani;
10 lakini sikukubali kumsikiliza Balaamu; kwa hiyo akafuliza kuwabarikia ninyi; basi nikawatoa katika mkono wake.
11 Nanyi mliuvuka Yordani, mkafika Yeriko; nao watu wa Yeriko wakapigana nanyi, Mwamori, na Mperizi, na Mkanaani, na Mhiti, na Mgirgashi, na Mhivi, na Myebusi; nami nikawatia mikononi mwenu.
12 Nikatuma mavu mbele yenu, waliowafukuza mbele yenu hao wafalme wawili wa Waamori, si kwa upanga wako, wala kwa upinde wako.
13 Nami nimewapa ninyi nchi msiyoitendea kazi, na miji msiyoijenga, nanyi mmekaa humo; mnakula matunda ya mashamba ya mizabibu na mizeituni msiyoipanda.
14 Basi sasa mcheni Bwana, mkamtumikie kwa unyofu wa moyo na kwa kweli; na kuiweka mbali miungu ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, na huko Misri; mkamtumikie yeye Bwana.
15 Nanyi kama mkiona ni vibaya kumtumikia Bwana, chagueni hivi leo mtakayemtumikia; kwamba ni miungu ile ambayo baba zenu waliitumikia ng'ambo ya Mto, au kwamba ni miungu ya wale Waamori ambao mnakaa katika nchi yao; lakini mimi na nyumba yangu tutamtumikia Bwana.
16 Hao watu wakajibu wakasema, Hasha! Tusimwache Bwana, ili kuitumikia miungu mingine;
17 kwa maana Bwana, Mungu wetu, yeye ndiye aliyetupandisha sisi na baba zetu kutoka nchi ya Misri; kutoka nyumba ya utumwa; naye ndiye aliyezifanya ishara zile kubwa mbele ya macho yetu, na kutulinda katika njia ile yote tuliyoiendea, na kati ya watu wa mataifa yote tuliopita katikati yao.
18 Bwana ndiye aliyewafukuza watu wa mataifa yote watoke mbele yetu, naam, Waamori waliokaa katika nchi hii; basi, kwa sababu hiyo sisi nasi tutamtumikia Bwana, maana yeye ndiye Mungu wetu.
19 Yoshua akawaambia watu, Hamwezi kumtumikia Bwana; kwa kuwa yeye ni Mungu mtakatifu; yeye ni Mungu mwenye wivu; hatawasamehe makosa yenu, wala dhambi zenu.
20 Kama mkimwacha Bwana na kuitumikia miungu migeni, ndipo atageuka na kuwatenda mabaya na kuwaangamiza, baada ya kuwatendea mema.
21 Lakini hao watu wakamwambia Yoshua, La! Lakini tutamtumikia Bwana.
22 Yoshua akawaambia watu, Ninyi mmekuwa mashahidi juu ya nafsi zenu, ya kuwa mmemchagua Bwana, ili kumtumikia yeye. Wakasema, Sisi tu mashahidi.
23 Akasema, Basi sasa, iondoeni miungu migeni iliyo kati yenu, mkaielekeze mioyo yenu kwa Bwana, Mungu wa Israeli.
24 Ndipo hao watu wakamwambia Yoshua, Bwana, Mungu wetu, ndiye tutakayemtumikia; na sauti yake ndiyo tutakayoitii.
25 Basi Yoshua akafanya agano na wale watu siku ile, akawapa amri na agizo huko Shekemu.
26 Yoshua akayaandika maneno haya katika kitabu cha torati ya Mungu; kisha akatwaa jiwe kubwa, akalisimamisha huko, chini ya ule mwaloni uliokuwa karibu na patakatifu pa Bwana.
27 Yoshua akawaambia watu wote, Tazama, jiwe hili litakuwa shahidi juu yetu; kwa maana limesikia maneno yote ya Bwana aliyotuambia, basi litakuwa shahidi juu yenu, msije mkamkana Mungu wenu.
28 Basi Yoshua akawaruhusu watu, wakaenda zao, kila mtu kwenye urithi wake.
29 Ikawa, baada ya hayo, Yoshua, mwana wa Nuni, mtumishi wa Bwana, akafa, mwenye umri wa miaka mia na kumi.
30 Wakamzika katika mpaka wa urithi wake, huko Timnath-sera; ulio katika nchi ya vilima ya Efraimu, upande wa kaskazini wa mlima wa Gaashi.
31 Nao Israeli wakamtumikia Bwana siku zote za Yoshua, na siku zote za hao wazee walioishi baada ya kufa kwake Yoshua, hao walioijua kazi yote ya Bwana, aliyowatendea Israeli.
32 Na hiyo mifupa ya Yusufu, ambayo wana wa Israeli walikuwa wameileta kutoka Misri, wakaizika huko Shekemu katika ile sehemu ya nchi, Yakobo aliyoinunua kwa wana wa Hamori, babaye Shekemu, kwa vipande mia vya fedha; nayo ikawa ni urithi wa wana wa Yusufu.
33 Huyo Eleazari mwana wa Haruni naye akafa; wakamzika katika kilima cha Finehasi mwanawe, ambacho alipewa yeye katika nchi ya vilima ya Efraimu.