Hesabu

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24, 25, 26, 27, 28, 29, 30, 31, 32, 33, 34, 35, 36

Hesabu 1


1 Bwana akanena na Musa katika bara ya Sinai, hemani mwa kukutania, siku ya kwanza ya mwezi wa pili, katika mwaka wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri, akamwambia,
2 Fanyeni hesabu ya mkutano wote wa wana wa Israeli, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina ilivyo, kila mtu mume kichwa kwa kichwa;
3 tangu mwenye miaka ishirini umri wake, na zaidi, wote wawezao kutoka kwenenda vitani katika Israeli; wewe na Haruni mtawahesabu kwa kuandama majeshi yao.
4 Tena mtu mume mmoja wa kila kabila atakuwa pamoja nanyi; kila mmoja aliye kichwa cha nyumba ya baba zake.
5 Na majina ya hao waume watakaosimama pamoja nanyi ni haya; Wa Reubeni; Elisuri mwana wa Shedeuri.
6 Wa Simeoni; Shelumieli mwana wa Suri-shadai.
7 Wa Yuda; Nashoni mwana wa Aminadabu.
8 Wa Isakari; Nethaneli mwana wa Suari.
9 Wa Zabuloni; Eliabu mwana wa Heloni.
10 Katika wana wa Yusufu; wa Efraimu, Elishama mwana wa Amihudi; na wa Manase; Gamalieli mwana wa Pedasuri.
11 Wa Benyamini Abidani mwana wa Gideoni.
12 Wa Dani; Ahiezeri mwana wa Amishadai.
13 Wa Asheri; Pagieli mwana wa Okirani.
14 Wa Gadi; Eliasafu mwana wa Deueli.
15 Wa Naftali; Ahira mwana wa Enani.
16 Hao ndio walioitwa wa mkutano, wakuu wa kabila za baba zao; nao ndio vichwa vya wale maelfu ya Israeli.
17 Basi Musa na Haruni wakawatwaa hao watu waume waliotajwa majina yao;
18 nao waliukutanisha mkutano mzima, siku ya kwanza ya mwezi wa pili, nao wakaonyesha ukoo wa vizazi vyao kwa kuandama jamaa zao, kwa nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, kichwa kwa kichwa.
19 Kama Bwana alivyomwagiza Musa, ndivyo alivyowahesabu huko katika bara ya Sinai.
20 Na wana wa Reubeni, mzaliwa wa kwanza wa Israeli, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, kichwa kwa kichwa, kila mtu mume tangu umri wa miaka ishirini na zaidi wote walioweza kwenda vitani;
21 wale waliohesabiwa katika kabila ya Reubeni, walikuwa watu arobaini na sita elfu na mia tano (46,500).
22 Katika wana wa Simeoni, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, wale waliohesabiwa kama hesabu ya majina, kichwa kwa kichwa, kila mume tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;
23 wale waliohesabiwa katika kabila ya Simeoni, walikuwa watu hamsini na kenda elfu na mia tatu (59,300).
24 Katika wana wa Gadi, kwa kuandama vizazi vyao, jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;
25 wale waliohesabiwa katika kabila ya Gadi, walikuwa watu arobaini na tano elfu na mia sita na hamsini (45,650).
26 Katika wana wa Yuda, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;
27 wale waliohesabiwa katika kabila ya Yuda, walikuwa watu sabini na nne elfu na mia sita (74,600).
28 Katika wana wa Isakari, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kwa hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;
29 wale waliohesabiwa katika kabila ya Isakari, walikuwa watu hamsini na nne elfu na mia nne (54,400).
30 Katika wana wa Zabuloni, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;
31 wale waliohesabiwa katika kabila ya Zabuloni, walikuwa watu hamsini na saba elfu na mia nne (57,400).
32 Katika wana wa Yusufu, maana katika wana wa Efraimu, vizazi vyao kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani,
33 wale waliohesabiwa katika kabila ya Efraimu, walikuwa watu arobaini elfu na mia tano (40,500).
34 Katika wana wa Manase, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;
35 wale waliohesabiwa katika kabila ya Manase, walikuwa watu thelathini na mbili elfu na mia mbili (32,200).
36 Katika wana wa Benyamini, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;
37 wale waliohesabiwa katika kabila ya Benyamini, walikuwa watu thelathini na tano elfu na mia nne (35,400).
38 Katika wana wa Dani, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;
39 wale waliohesabiwa katika kabila ya Dani, walikuwa watu sitini na mbili elfu na mia saba (62,700).
40 Katika wana wa Asheri, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;
41 wale waliohesabiwa katika kabila ya Asheri, walikuwa watu arobaini na moja elfu na mia tano (41,500).
42 Katika wana wa Naftali, vizazi vyao, kwa kuandama jamaa zao, na nyumba za baba zao, kama hesabu ya majina, tangu umri wa miaka ishirini na zaidi, wote walioweza kwenda vitani;
43 wale waliohesabiwa katika kabila ya Naftali, walikuwa watu hamsini na tatu elfu na mia nne (53,400).
44 Hao ndio waliohesabiwa, ambao Musa na Haruni na wale wakuu wa Israeli watu kumi na wawili waliwahesabu; walikuwa kila mmoja kwa ajili ya nyumba ya baba zake.
45 Basi hao wote waliohesabiwa katika wana wa israeli kwa kuandama nyumba za baba zao tangu umri wa miaka ishirini na zaidi; wote walioweza kwenda vitani katika Israeli;
46 hao wote waliohesabiwa walikuwa ni watu waume mia sita na tatu elfu na mia tano na hamsini (603,550).
47 Lakini Walawi kwa kuiandama kabila ya baba zao hawakuhesabiwa katika watu hao.
48 Kwa kuwa Bwana alinena na Musa, na kumwambia,
49 Hiyo kabila ya Lawi tu usiihesabu, wala usiitie hesabu yao katika wana wa Israeli;
50 lakini uwaweke Walawi wawe juu ya maskani ya ushahidi, na juu ya vyombo vyake vyote, na juu ya vitu vyake vyote; wao wataichukua hiyo maskani, na vyombo vyake vyote; nao wataitumikia, na kupanga hema zao kwa kuizunguka maskani pande zote.
51 Tena hapo maskani itakapokwenda mbele, Walawi wataishusha; tena hapo maskani itakaposimamishwa, Walawi wataisimamisha; na mgeni atakayekaribia atauawa.
52 Na wana wa Israeli watazipanga hema zao, kila mtu katika marago yake mwenyewe, kila mtu hapo ilipo beramu yake mwenyewe, kama majeshi yao yalivyo.
53 Lakini Walawi watapanga hema zao kuizunguka maskani ya ushahidi pande zote, ili zisiwe hasira juu ya mkutano wa wana wa Israeli; kisha Walawi wataulinda ulinzi wa hiyo maskani ya ushahidi.
54 Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli; kama yote Bwana aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya.

Hesabu 2


1 Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
2 Wana wa Israeli watapanga kila mtu penye beramu yake mwenyewe, na alama za nyumba za baba zao; kuikabili hema ya kukutania ndiko watakakopanga kwa kuizunguka pande zote.
3 Na hao watakaopanga upande wa mashariki, kwa kuelekea maawio ya jua, ndio wale wa beramu ya marago ya Yuda, kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Yuda atakuwa Nashoni mwana wa Aminadabu.
4 Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa sabini na nne elfu na mia sita.
5 Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila ya Isakari; na mkuu wa wana wa Isakari atakuwa Nethaneli mwana wa Suari;
6 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa hamsini na nne elfu na mia nne;
7 na kabila ya Zabuloni; na mkuu wa wana wa Zabuloni atakuwa Eliabu mwana wa Heloni;
8 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa hamsini na saba elfu na mia nne.
9 Hao wote waliohesabiwa katika marago ya Yuda walikuwa mia na themanini na sita elfu na mia nne, kwa majeshi yao. Hao ndio watakaosafiri mbele.
10 Upande wa kusini kutakuwa na beramu ya marago ya Reubeni kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Reubeni atakuwa Elisuri mwana wa Shedeuri.
11 Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa arobaini na sita elfu na mia tano.
12 Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila ya Simeoni; na mkuu wa wana wa Simeoni atakuwa Shelumieli mwana wa Suri-shadai;
13 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa hamsini na kenda elfu na mia tatu;
14 na kabila ya Gadi; na mkuu wa wana wa Gadi atakuwa Eliasafu mwana wa Deueli;
15 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa arobaini na tano elfu na mia sita na hamsini.
16 Wote waliohesabiwa katika marago ya Reubeni walikuwa mia na hamsini na moja elfu na mia nne na hamsini, kwa majeshi yao. Nao ndio watakaosafiri mahali pa pili.
17 Ndipo hema ya kukutania itasafiri, pamoja na marago ya Walawi katikati ya marago yote; kama wapangavyo marago, watasafiri vivyo, kila mtu mahali pake, penye beramu zao.
18 Upande wa magharibi kutakuwa na beramu ya marago ya Efraimu kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Efraimu atakuwa Elishama mwana wa Amihudi.
19 Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao walikuwa arobaini elfu na mia tano.
20 Na karibu naye itakuwa kabila ya Manase; na mkuu wa wana wa Manase atakuwa Gamalieli mwana wa Pedasuri;
21 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa thelathini na mbili elfu na mia mbili;
22 tena kabila ya Benyamini; na mkuu wa wana wa Benyamini atakuwa Abidani mwana wa Gideoni;
23 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa thelathini na tano elfu na mia nne.
24 Wote waliohesabiwa katika marago ya Efraimu walikuwa mia na nane elfu na mia moja, kwa majeshi yao. Nao ndio watakaosafiri katika mahali pa tatu.
25 Upande wa kaskazini kutakuwa na beramu ya marago ya Dani kwa majeshi yao; na mkuu wa wana wa Dani atakuwa Ahiezeri mwana wa Amishadai.
26 Na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa sitini na mbili elfu na mia saba.
27 Na hao watakaopanga karibu naye ni kabila ya Asheri; na mkuu wa wana wa Asheri atakuwa Pagieli mwana wa Okrani;
28 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa arobaini na moja elfu na mia tano;
29 kisha kabila ya Naftali; na mkuu wa wana wa Naftali atakuwa Ahira mwana wa Enani;
30 na jeshi lake, na wale waliohesabiwa kwao, walikuwa hamsini na tatu elfu na mia nne.
31 Wote waliohesabiwa katika marago ya Dani walikuwa mia na hamsini na saba elfu na mia sita. Hao ndio watakaosafiri mwisho kwa kuandama beramu zao.
32 Hao ndio waliohesabiwa katika wana wa Israeli kwa nyumba za baba zao; wote waliohesabiwa katika marago kwa majeshi yao, walikuwa mia sita na tatu elfu na mia tano na hamsini.
33 Lakini Walawi hawakuhesabiwa katika wana wa Israeli; kama Bwana alivyomwagiza Musa.
34 Ndivyo walivyofanya wana wa Israeli; kama yote Bwana aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyopanga penye beramu zao, na ndivyo walivyosafiri, kila mtu kwa jamaa zao, kwa nyumba za baba zao.

Hesabu 3


1 Basi vizazi vya Haruni na Musa, siku hiyo Bwana aliyosema na Musa katika mlima wa Sinai, ni hivi.
2 Tena majina ya hao wana wa Haruni ni haya; Nadabu mzaliwa wa kwanza, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari.
3 Hayo ndiyo majina ya wana wa Haruni, hao makuhani waliotiwa mafuta, ambao aliwaweka wakfu ili wafanye kazi ya ukuhani.
4 Kisha Nadabu na Abihu walikufa mbele za Bwana, waliposongeza moto wa kigeni mbele za Bwana, katika bara ya Sinai, nao walikuwa hawana wana; na Eleazari na Ithamari wakafanya kazi ya ukuhani mbele ya uso wa Haruni baba yao.
5 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
6 Ilete karibu kabila ya Lawi, ukawaweke mbele ya Haruni kuhani, ili wapate kumtumikia.
7 Nao wataulinda ulinzi wake, na ulinzi wa mkutano wote mbele ya hema ya kukutania, ili watumike utumishi wa maskani.
8 Nao watavitunza vyombo vyote vya hema ya kukutania, na kulinda ulinzi wa wana wa Israeli, ili watumike utumishi wa maskani.
9 Nawe utawapa Haruni na wanawe hao Walawi wawe nao; amepewa watu hao kabisa kwa ajili ya wana wa Israeli.
10 Nawe utawaweka Haruni na wanawe, nao wataushika ukuhani wao, na mgeni atakayekaribia atauawa.
11 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
12 Mimi, tazama, nimewatwaa Walawi na kuwatoa kati ya wana wa Israeli badala ya wazaliwa wa kwanza wote wafunguao tumbo katika wana wa Israeli; na hao Walawi watakuwa wangu;
13 kwa kuwa hao wazaliwa wa kwanza wote ni wangu; katika siku ile niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri nikajiwekea wakfu wazaliwa wa kwanza wote wa Israeli, wa wanadamu na wa wanyama; watakuwa wangu; mimi ndimi Bwana.
14 Kisha Bwana akanena na Musa huko katika bara ya Sinai, na kumwambia,
15 Uwahesabu wana wa Lawi kwa kuandama nyumba za baba zao na jamaa zao; kila mtu mume tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi utawahesabu.
16 Basi Musa akawahesabu kama neno la Bwana kama alivyoagizwa.
17 Na wana wa Lawi walikuwa ni hawa kwa majina yao; Gershoni, na Kohathi, na Merari.
18 Na majina ya wana wa Gershoni kwa jamaa zao ni Libni na Shimei.
19 Na wana wa Kohathi kwa jamaa zao ni Amramu, na Ishari, na Hebroni, na Uzieli.
20 Na wana wa Merari kwa jamaa zao ni Mahli, na Mushi. Hizi ndizo jamaa za Walawi kwa nyumba za baba zao.
21 Katika Gershoni walikuwa jamaa ya Walibni, na jamaa ya Washimei, hawa ndio jamaa za Wagershoni.
22 Hao waliohesabiwa kwao, kama hesabu ya waume wote, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, hao waliohesabiwa kwao walikuwa saba elfu na mia tano.
23 Jamaa za Wagershoni watapanga rago nyuma ya maskani, upande wa magharibi.
24 Na mkuu wa nyumba ya baba zao Wagershoni atakuwa Eliasafu mwana wa Laeli.
25 Na ulinzi wa Wagershoni katika hema ya kukutania ni hiyo maskani, na Hema, na kifuniko chake, na pazia la mlango wa hema ya kukutania,
26 na kuta za nguo za ua, na sitara ya mlango wa ua, iliyo karibu na maskani, na karibu na madhabahu pande zote, na kamba zake zitumiwazo kwa matumizi yake yote.
27 Na katika Kohathi ni jamaa ya Waamrami, na jamaa ya Waishari, na jamaa ya Wahebroni, na jamaa ya hao Wauzieli; hizo ni jamaa za Wakohathi.
28 Kama hesabu ya waume wote, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, walikuwa elfu nane na mia sita, wenye kuulinda ulinzi wa mahali patakatifu.
29 Jamaa za wana wa Kohathi watapanga rago upande wa kusini wa maskani.
30 Na mkuu wa nyumba ya baba za jamaa za Wakohathi atakuwa Elisafani mwana wa Uzieli.
31 Na vitu watakavyovitunza ni hilo sanduku, na meza, na kinara cha taa, na madhabahu, na vile vyombo vya mahali patakatifu wavitumiavyo katika kutumika kwao, na pazia, na utumishi wake wote.
32 Na Eleazari mwana wa Haruni kuhani atakuwa mkuu wa hao wakuu wa Walawi, naye atawasimamia hao walindao ulinzi wa mahali patakatifu.
33 Katika Merari ni jamaa ya hao Wamahli, na jamaa ya Wamushi; hizo ni jamaa za Merari.
34 Na hao waliohesabiwa kwao, kama hesabu ya waume wote, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, walikuwa sita elfu na mia mbili.
35 Na mkuu wa nyumba ya baba za jamaa za Merari alikuwa Surieli mwana wa Abihaili; hao watapanga rago upande wa maskani, wa kaskazini.
36 Na usimamizi walioamriwa wana wa Merari ulikuwa ni kutunza mbao za maskani, na mataruma yake, na nguzo zake, na matako yake, na vyombo vyake vyote, na utumishi wake wote;
37 na nguzo za ua zilizouzunguka, na matako yake, na vigingi vyake, na kamba zake.
38 Na hao watakaopanga mbele ya maskani upande wa mashariki, mbele ya hema ya kukutania upande wa kuelekea maawio ya jua, watakuwa hawa, Musa na Haruni na wanawe, wenye kulinda ulinzi wa mahali patakatifu, yaani, huo ulinzi wa wana wa Israeli; na mgeni atakayekaribia atauawa.
39 Hao wote waliohesabiwa katika Walawi, ambao Musa na Haruni waliwahesabu kwa amri ya Bwana, kwa jamaa zao, waume wote tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, walikuwa ishirini na mbili elfu.
40 Kisha Bwana akamwambia Musa, Uwahesabu waume wote wazaliwa wa kwanza katika wana wa Israeli tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi uyahesabu majina yao.
41 Nawe utawatwaa Walawi kwa ajili yangu mimi (Mimi ndimi Bwana) badala ya hao wazaliwa wa kwanza wote katika wana wa Israeli; na wanyama wa Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wa wanyama wa wana wa Israeli.
42 Musa akahesabu, kama Bwana alivyomwagiza, wazaliwa wa kwanza wote katika wana wa Israeli.
43 Wazaliwa wa kwanza wote walio waume kwa hesabu ya majina, tangu umri wa mwezi mmoja na zaidi, katika hao waliohesabiwa kwao, walikuwa ishirini na mbili elfu na mia mbili na sabini na watatu.
44 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
45 Uwatwae Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza katika wana wa Israeli, na wanyama wa Walawi badala ya wanyama wao; na hao Walawi watakuwa wangu mimi; mimi ndimi Bwana.
46 Tena kwa kuwakomboa hao watu mia mbili na sabini na watatu, wa hao wazaliwa wa kwanza wa Israeli, ambao wamezidi ile hesabu ya Walawi,
47 utatwaa shekeli tano kwa kichwa cha kila mtu kwa hiyo shekeli ya mahali patakatifu (shekeli ni gera ishirini);
48 na hizo fedha ambazo waliosalia wamekombolewa kwazo utampa Haruni na wanawe.
49 Basi Musa akawatoza fedha za ukombozi, hao waliozidi hesabu ya wale waliokombolewa na Walawi;
50 akatwaa hizo fedha kwa wazaliwa wa kwanza wa wana wa Israeli; shekeli elfu moja na mia tatu na sitini na tano kwa shekeli ya mahali patakatifu;
51 kisha hizo fedha za ukombozi Musa akampa Haruni na wanawe, kama neno la Bwana, kama Bwana alivyomwagiza Musa.

Hesabu 4


1 Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
2 Katika wana wa Lawi uitenge hesabu ya wana wa Kohathi, kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao,
3 tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi hata umri wa miaka hamsini, wote waingiao katika utumishi huo, ili kufanya kazi ya hema ya kukutania.
4 Huu ndio utumishi wa wana wa Kohathi katika hema ya kukutania, katika vile vyombo vitakatifu sana;
5 hapo watakapong'oa safari, Haruni ataingia ndani, na wanawe, nao watalishusha pazia la sitara, na kulifunika sanduku la ushahidi kwa hilo pazia;
6 kisha atatia juu yake ngozi za pomboo za kulifunikia, na kutandika juu yake nguo ya rangi ya samawi tupu, kisha watatia hiyo miti yake.
7 Tena juu ya meza ya mikate ya wonyesho watatandika nguo ya rangi ya samawi, na kuweka juu yake sahani, na miiko, na mabakuli, na vikombe vya kumiminia; na hiyo mikate ya daima itakuwa juu yake;
8 nao watatandika juu yake nguo ya rangi nyekundu, na kuifunika kwa ngozi za pomboo za kuifunikia, na kuitia ile miti yake.
9 Kisha watatwaa nguo ya rangi ya samawi, na kukifunika kinara cha taa ya nuru, na taa zake, na makasi yake, na sahani zake za kutilia makaa, na vyombo vyake vyote vya mafuta, watumiavyo kwa kazi yake;
10 nao watakitia, na vyombo vyake vyote, ndani ya ngozi ya pomboo, na kukitia juu ya miti ya kukichukulia
11 Tena watatandika nguo ya rangi ya samawi juu ya madhabahu ya dhahabu, na kuifunika kwa ngozi za pomboo, na kuitia ile miti yake;
12 kisha watavitwaa vile vyombo vyote vya utumishi wavitumiavyo katika mahali patakatifu, na kuvitia katika nguo ya rangi ya samawi, na kuvifunika kwa ngozi za pomboo, na kuvitia juu ya miti ya kuvichukulia.
13 Nao watayaondoa hayo majivu madhabahuni; na kutandika nguo ya rangi ya zambarau juu yake;
14 nao wataweka vyombo vyake vyote juu yake ambavyo wavitumia katika madhabahu, vyetezo, na nyuma, na miiko, na mabakuli, vyombo vyote vya hiyo madhabahu; nao watatandika juu yake ngozi za pomboo, na kutia miti yake mahali pake.
15 Na Haruni na wanawe watakapokwisha kupafunika mahali patakatifu, na vyombo vyote vya mahali patakatifu, hapo watakapong'oa kambi; baadaye, wana wa Kohathi watakuja kuvichukua; lakini wasiviguse vile vitu vitakatifu, wasife. Vyombo vile ni mzigo wa wana wa Kohathi katika hema ya kukutania.
16 Na ulinzi wake Eleazari mwana wa Haruni kuhani utakuwa ni kuyaangalia mafuta kwa nuru, na uvumba mzuri, na sadaka ya unga ya daima, na mafuta ya kupaka, tena ulinzi wa hiyo maskani yote, na wa vitu vyote vilivyo ndani yake, mahali patakatifu, na vyombo vyake.
17 Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
18 Msiitenge kabisa kabila ya jamaa za Wakohathi katika hao Walawi;
19 lakini wafanyieni neno hili, ili kwamba wawe hai, wasife, hapo watakapovikaribia vile vitu vilivyo vitakatifu sana; Haruni na wanawe wataingia ndani, na kuwawekea kila mtu utumishi wake, na kila mtu mzigo wake;
20 lakini wasiingie wao kupaona mahali pale patakatifu, hata kwa dakika moja, ili wasife.
21 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
22 Fanya jumla ya wana wa Gershoni nao, kwa nyumba za baba zao, na jamaa zao;
23 tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini utawahesabu; wote watakaoingia kutumika, ili kufanya kazi katika hema ya kukutania.
24 Huu ni utumishi wa jamaa za Wagershoni, katika kutumika na katika kuchukua mizigo;
25 wao watayachukua mapazia ya maskani, na hema ya kukutania, hizo nguo za kufunikia, na zile ngozi za pomboo za kufunikia zilizo juu yake, na pazia la mlango wa hema ya kukutania;
26 na kuta za nguo za ua, na sitara ya ile nafasi ya kuingilia ya lango la ua, ulio karibu na maskani na madhabahu, kuzunguka pande zote, na kamba zake, na vyombo vyote vya utumishi wao, na yote yatakayotendeka kwavyo, watatumika katika hayo.
27 Utumishi wote wa wana wa Wagershoni, katika mzigo wao wote, na utumishi wao wote, utakuwa kwa amri ya Haruni na wanawe; nanyi mtawaagizia mzigo wao wote kuulinda.
28 Huu ni utumishi wa jamaa za wana wa Wagershoni katika hema kukutania; na ulinzi utakuwa chini ya mkono wa Ithamari mwana wa Haruni kuhani.
29 Katika habari ya wana wa Merari, utawahesabu kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao;
30 tangu aliyepata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini, utawahesabu, kila atakayeingia katika huo utumishi, ili kufanya kazi ya hema ya kukutania.
31 Na mausia ya mzigo wao ni haya, kwa utumishi wao wote katika hema ya kukutania; mbao za maskani, na mataruma yake, na nguzo zake, na matako yake;
32 na viguzo vya ua vya kuuzunguka pande zote, na matako yake, na vigingi vyake, na kamba zake, na vyombo vyake vyote, pamoja na utumishi wake wote; nanyi mtawaagizia kila mtu kwa jina lake vile vyombo vya mzigo wao watakaoulinda.
33 Huu ni utumishi wa jamaa za wana wa Merari, kwa utumishi wao wote, katika hema ya kukutania, chini ya mkono wa Ithamari mwana wa Haruni kuhani.
34 Basi Musa na Haruni na hao wakuu wa mkutano wakawahesabu wana wa Kohathi kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao,
35 tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini, kila mtu aliyeingia katika utumishi kwa kazi katika hema ya kukutania,
36 na waliohesabiwa kwao kwa jamaa zao, walikuwa elfu mbili na mia saba hamsini.
37 Hao ndio waliohesabiwa katika jamaa za Wakohathi, wote waliotumika katika hema ya kukutania, ambao Musa na Haruni waliwahesabu kwa amri ya Bwana kwa mkono wa Musa.
38 Na hao waliohesabiwa katika wana wa Gershoni, kwa jamaa zao na nyumba zao baba zao,
39 tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini, kila mtu aliyeingia katika utumishi, kwa kazi katika hema ya kukutania,
40 hata wale waliohesabiwa kwao, kwa jamaa zao na nyumba za baba zao, walikuwa elfu mbili na mia sita na thelathini.
41 Hao ndio waliohesabiwa katika jamaa za wana wa Gershoni, wote waliotumika katika hema ya kukutania, ambao Musa na Haruni waliwahesabu kwa amri ya Bwana.
42 Na hao waliohesabiwa katika jamaa za wana wa Merari, kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao,
43 tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini, kila mtu aliyeingia katika utumishi kwa kazi katika hema ya kukutania,
44 wale waliohesabiwa kwao, kwa jamaa zao, walikuwa elfu tatu na mia mbili.
45 Hao ndio waliohesabiwa katika jamaa za wana wa Merari, ambao Musa na; Haruni waliwahesabu kwa amri ya Bwana, kwa mkono wa Musa.
46 Wote waliohesabiwa katika Walawi, ambao Musa na Haruni na hao wakuu wa Israeli waliwahesabu, kwa jamaa zao, na nyumba za baba zao,
47 tangu waliopata umri wa miaka thelathini na zaidi, hata umri wa miaka hamsini, kila aliyeingia kufanya kazi ya utumishi, na kazi ya kuchukua mizigo katika hema ya kukutania,
48 hao waliohesabiwa kwao, walikuwa elfu nane na mia tano themanini.
49 Kwa amri ya Bwana, walihesabiwa kwa mkono wa Musa, kila mtu kwa utumishi wake, na kama mzigo wake ulivyokuwa; ndivyo walivyohesabiwa na yeye, kama Bwana alivyomwagiza Musa.

Hesabu 5


1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Waamrishe wana wa Israeli kwamba wamtoe kila mwenye ukoma maragoni, na kila mtu aliye na kisonono, na kila aliye najisi kwa ajili ya wafu;
3 mtawatoa nje wote, waume kwa wake, mtawaweka nje ya marago; ili wasiyatie unajisi marago yao, ambayo mimi naketi katikati yake.
4 Wana wa Israeli wakafanya vivyo, wakawatoa na kuwaweka nje ya marago; kama Bwana alivyonena na Musa, ndivyo walivyofanya wana wa Israeli.
5 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
6 Uwaambie wana wa Israeli, Mtu mume au mke atakapofanya dhambi yo yote, ifanywayo na binadamu, kumwasi Bwana, na mtu huyo akawa na hatia;
7 ndipo watakapoungama dhambi yao waliyoifanya; naye atarudisha kwa hatia yake, kwa utimilifu wake, tena ataongeza juu yake sehemu ya tano, na kumpa huyo aliyemkosa.
8 Lakini kwamba mtu huyo hana jamaa ya karibu ambaye inampasa kurudishiwa kwa ajili ya hiyo hatia, kile kitakachorudishwa kwa Bwana kwa hiyo hatia kitakuwa cha kuhani, pamoja na kondoo mume wa upatanisho, ambaye kwa huyo utafanywa upatanisho kwa ajili yake.
9 Tena kila sadaka ya kuinuliwa, ya vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, watakavyosongeza kwa kuhani, itakuwa ni yake.
10 Tena vitu vilivyowekwa wakfu na mtu awaye yote, vitakuwa ni vya kuhani; kitu cho chote mtu atakachompa kuhani, kitakuwa chake.
11 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
12 Nena na wana wa israeli, uwaambie, kama mke wa mtu ye yote akikengeuka, na kumkosa mumewe,
13 na mtu mume akalala naye kwa uasherati, na jambo hilo likamfichamania mumewe, likawa jambo lisilojulikana, na huyo mwanamke akawa najisi, wala hapana shahidi aliyeshuhudia juu yake, wala hakufumaniwa;
14 kisha mumewe akashikwa na roho ya wivu, akamwonea wivu mkewe, naye akawa najisi huyo mwanamke; au kama akiingiwa na roho ya wivu, akamwonea wivu mkewe, naye hakuwa na unajisi huyo mke;
15 ndipo huyo mume atamchukua mkewe, aende naye kwa kuhani, naye ataleta sadaka yake kwa ajili yake, yaani, sehemu ya kumi ya efa ya unga wa shayiri; asitie mafuta juu yake, wala asitie ubani juu yake; maana, ni sadaka ya unga ya wivu, ni sadaka ya unga ya ukumbusho ya kukumbukia uovu.
16 Basi kuhani atamleta mwanamke akaribie, na kumweka mbele za Bwana;
17 kisha kuhani atatwaa maji matakatifu katika chombo cha udongo; kisha kuhani atatwaa katika vumbi lililo pale chini ya maskani, na kulitia katika hayo maji;
18 kisha kuhani atamweka mwanamke mbele za Bwana, naye atazifungua nywele za kichwani mwa huyo mwanamke, kisha atampa hiyo sadaka ya unga ya ukumbusho mikononi mwake, ambayo ni sadaka ya unga ya wivu, naye kuhani atakuwa na hayo maji ya uchungu yaletayo laana mkononi mwake;
19 tena kuhani atamwapisha huyo mwanamke, naye atamwambia mwanamke, Kwamba hakulala mtu mume pamoja nawe, tena kwamba hukukengeuka kuandama uchafu, uli chini ya mumeo, maji haya ya uchungu yaletayo laana yasikudhuru;
20 lakini kwamba umekengeuka uli chini ya mumeo, na kwamba u hali ya unajisi, na mtu mume amelala nawe, asiyekuwa mumeo;
21 hapo ndipo kuhani atamwapisha mwanamke kwa kiapo cha kuapiza, kisha kuhani atamwambia huyo mwanamke maneno haya, Bwana na akufanye wewe uwe laana na kiapo kati ya watu wako, hapo Bwana akufanyapo paja lako kupooza, na tumbo lako kuvimba;
22 na maji yaletayo laana yatakuingia matumboni mwako, na kukuvimbisha tumbo, na kukupoozesha paja lako; na mwanamke ataitika, Amina, Amina.
23 Kisha kuhani ataziandika laana hizo ndani ya kitabu, na kuzifuta katika maji ya uchungu;
24 kisha atamnywesha mwanamke hayo maji ya uchungu yaletayo laana; nayo maji yaletayo laana yataingia ndani yake, nayo yatageuka kuwa uchungu.
25 Kisha kuhani ataitwaa hiyo sadaka ya unga ya wivu, kwa kuiondoa mkononi mwa huyo mwanamke, naye ataitikisa sadaka ya unga mbele ya Bwana, na kuisongeza pale madhabahuni;
26 kisha kuhani atatwaa konzi moja ya sadaka ya unga, kuwa ni ukumbusho wake, na kuuteketeza madhabahuni, baadaye atamnywesha mwanamke hayo maji.
27 Kisha hapo atakapokwisha kumnywesha maji, ndipo itakapokuwa, kama amekuwa hali ya unajisi na kumkosa mumewe, hayo maji yaletayo laana yatamwingia ndani yake, nayo yatakuwa uchungu, na tumbo lake litavimba, na paja lake litapooza; na huyo mwanamke atakuwa laana kati ya watu wake.
28 Na kama mwanamke hakuwa na unajisi lakini yu safi; ndipo ataachiliwa, naye atazaa wana.
29 Hii ndiyo sheria ya wivu, mwanamke, ambaye yu chini ya mumewe, akikengeuka, na kupata unajisi;
30 au, roho ya wivu ikimwingia mtu mume, naye akamwonea wivu mkewe; ndipo atakapomweka huyo mwanamke mbele za Bwana, na kuhani atatenda juu yake sheria hii yote.
31 Na huyo mume atakuwa hana uovu, na mwanamke atauchukua uovu wake.

Hesabu 6


1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena na watu wa Israeli, uwaambie, Mtu mume au mtu mke atakapoweka nadhiri kubwa, nadhiri ya Mnadhiri, ili ajiweke wakfu kwa Bwana;
3 atajitenga na divai na vileo; hatakunywa siki ya divai, wala siki ya kileo, wala asinywe maji yo yote ya zabibu, wala asile zabibu, mbichi wala zilizokauka.
4 Siku zote za kujitenga kwake asile kitu cho chote kilichoandaliwa kwa mzabibu, tangu kokwa hata maganda.
5 Siku zote za nadhiri yake ya kujitenga, wembe usimfikilie kichwani mwake; hata hizo siku zitakapotimia, ambazo alijiweka wakfu kwa Bwana, atakuwa mtakatifu, ataziacha nywele za kichwani mwake zikue ziwe ndefu.
6 Siku hizo zote ambazo alijiweka awe wa Bwana asikaribie maiti.
7 Hatajitia unajisi kwa ajili ya baba yake, wala kwa ajili ya mamaye, wala kwa nduguye mume, wala kwa umbu lake, wakifa wao; kwa sababu ya huku kujiweka kwa Mungu ni juu ya kichwa chake.
8 Siku zote za kujitenga kwake, yeye ni mtakatifu kwa Bwana
9 Na kama mtu ye yote akifa ghafla karibu naye, akajitia unajisi kichwa cha kutengwa kwake, ndipo atakinyoa kichwa siku hiyo ya kutakaswa kwake, atakinyoa siku ya saba.
10 Tena siku ya nane ataleta hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, aende nao kwa kuhani, hata mlangoni pa hema ya kukutania;
11 naye kuhani atasongeza mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa, naye atafanya upatanisho kwa ajili yake, kwa sababu aliingia kosani kwa ajili ya mfu, naye atatakasa kichwa chake siku iyo hiyo.
12 Kisha ataziweka kwa Bwana hizo siku za kujitenga kwake, naye ataleta mwana-kondoo mume wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya hatia; lakini hizo siku za kwanza hazitahesabiwa, kwa kuwa kule kujitenga kwake kulitiwa unajisi.
13 Na sheria ya Mnadhiri ni hii, zitakapotimia hizo siku za kujitenga kwake; ataletwa mlangoni pa hema ya kukutania;
14 naye atasongeza sadaka yake kwa Bwana, mwana-kondoo mmoja mume wa mwaka wa kwanza mkamilifu, kuwa sadaka ya kuteketezwa, na mwana-kondoo mmoja mke wa mwaka wa kwanza mkamilifu, kuwa sadaka ya dhambi, na kondoo mume mmoja mkamilifu kwa sadaka ya amani,
15 na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, mikate ya unga mwembamba iliyokandwa kwa mafuta, na mikate ya kaki isiyochachwa, iliyotiwa mafuta, pamoja na sadaka zake za unga, na sadaka zake za kinywaji.
16 Na kuhani atavisongeza mbele za Bwana, naye atasongeza sadaka yake ya dhambi, na sadaka yake ya kuteketezwa;
17 naye atamsongeza huyo kondoo mume kuwa dhabihu ya sadaka za amani kwa Bwana, pamoja na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu; kisha kuhani atasongeza sadaka ya unga nayo, na sadaka yake ya kinywaji.
18 Naye Mnadhiri atakinyoa kichwa cha kujitenga kwake, mlangoni pa hema ya kukutania, kisha atatwaa hizo nywele za kichwa cha kujitenga kwake, na kuzitia katika moto ulio chini ya dhabihu ya sadaka za amani.
19 Kisha kuhani atautwaa mkono wa huyo kondoo mume uliotokoswa, na mkate mmoja usio chachu atautwaa kikapuni, na mkate mmoja wa kaki, naye ataitia mikononi mwa yule Mnadhiri, baada ya kunyoa kichwa cha kujitenga kwake;
20 naye kuhani atavitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana; kitu hicho ni kitakatifu kwa kuhani, pamoja na kidari cha kutikiswa, na paja la kuinuliwa; kisha baadaye Mnadhiri ana ruhusa kunywa divai.
21 Sheria ya Mnadhiri awekaye nadhiri ni hiyo, tena ni sheria ya sadaka yake atakayomtolea Bwana kwa ajili ya kujitenga kwake, pamoja na vitu vile ambavyo aweza kuvipata zaidi; kama nadhiri yake awekayo ilivyo, ndivyo impasavyo kufanya kwa kuiandama sheria ya kujitenga kwake.
22 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
23 Nena na Haruni na wanawe, uwaambie, Hivi ndivyo mtakavyowabarikia wana wa Israeli; mtawaambia;
24 Bwana akubarikie, na kukulinda;
25 Bwana akuangazie nuru za uso wake, na kukufadhili;
26 Bwana akuinulie uso wake, na kukupa amani.
27 Ndivyo watakavyoweka jina langu juu ya wana wa Israeli; nami nitawabarikia.

Hesabu 7


1 Ilikuwa siku hiyo Musa alipokwisha kuisimamisha maskani, na kuitia mafuta, na kuitakasa, na vyombo vyake vyote, na hiyo madhabahu na vyombo vyake vyote, na kuvitia mafuta, na kuvitakasa;
2 ndipo wakuu wa Israeli, vichwa vya nyumba za baba zao, wakatoa matoleo; hao ndio wakuu wa kabila, hao ndio waliokuwa juu yao waliohesabiwa;
3 nao wakamletea Bwana matoleo yao, magari sita yenye mafuniko juu, na ng'ombe kumi na wawili; gari moja kwa wakuu wawili wawili, na ng'ombe mmoja kwa kila mkuu; nao wakayasongeza hapo mbele ya maskani.
4 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
5 Pokea mikononi mwao, ili kwamba viwe vya kutumiwa katika utumishi wa hema ya kukutania; nawe utawapa Walawi vitu hivyo, kila mtu utampa kama utumishi wake ulivyo.
6 Basi Musa akapokea hayo magari, na ng'ombe, akawapa Walawi.
7 Wana wa Gershoni akawapa magari mawili na ng'ombe wanne, kama utumishi wao ulivyokuwa;
8 na wana wa Merari akawapa magari manne na ng'ombe wanane kama utumishi wao ulivyokuwa, chini ya mkono wa Ithamari, mwana wa Haruni kuhani.
9 Lakini hakuwapa wana wa Kohathi; maana, utumishi wa vile vitu vitakatifu ulikuwa ni wao; nao wakavichukua mabegani mwao.
10 Kisha wale wakuu wakatoa matoleo kwa ajili ya kuiweka wakfu madhabahu, katika siku hiyo iliyotiwa mafuta, wakuu wakayatoa matoleo yao mbele ya madhabahu.
11 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia, Watasongeza matoleo yao, kila mkuu kwa siku yake, kwa ajili ya kuiweka wakfu madhabahu.
12 Basi aliyetoa matoleo yake siku ya kwanza ni Nashoni mwana wa Aminadabu, wa kabila ya Yuda;
13 na matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha uzani wake ni shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga;
14 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kimejaa uvumba;
15 ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mmoja mume, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa;
16 mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi;
17 na kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe waume wawili, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Nashoni mwana wa Aminadabu.
18 Siku ya pili Nethaneli mwana wa Suari, mkuu wa Isakari, alitoa;
19 yeye akasongeza matoleo yake, sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa ni sadaka ya unga;
20 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilikuwa kimejaa uvumba;
21 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa;
22 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi;
23 na kwa dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Nethaneli mwana wa Suari.
24 Siku ya tatu Eliabu mwana wa Heloni, mkuu wa wana wa Zabuloni;
25 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga;
26 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba;
27 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa;
28 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi;
29 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Eliabu mwana wa Heloni.
30 Siku ya nne Elisuri mwana wa Shedeuri, mkuu wa wana wa Reubeni;
31 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga;
32 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba;
33 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa;
34 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi;
35 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Elisuri mwana wa Shedeuri.
36 Siku ya tano Shelumieli mwana wa Suri-shadai, mkuu wa wana Simeoni;
37 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga;
38 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba;
39 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa;
40 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi;
41 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Shelumieli mwana wa Suri-shadai
42 Siku ya sita Eliasafu mwana wa Deueli, mkuu wa wana wa Gadi
43 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga;
44 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba;
45 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa;
46 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi;
47 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Eliasafu mwana wa Deueli.
48 Siku ya saba Elishama mwana wa Amihudi, mkuu wa wana wa Efraimu;
49 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga;
50 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba;
51 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa;
52 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi;
53 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Elishama mwana wa Amihudi.
54 Siku ya nane Gamalieli mwana wa Pedasuri, mkuu wa wana wa Manase;
55 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga;
56 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba;
57 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa;
58 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi;
59 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Gamalieli mwana wa Pedasuri.
60 Siku ya kenda Abidani mwana wa Gideoni, mkuu wa wana wa Benyamini;
61 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga;
62 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba;
63 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa;
64 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi;
65 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Abidani mwana wa Gideoni.
66 Siku ya kumi Ahiezeri mwana wa Amishadai, mkuu wa wana wa Dani;
67 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga;
68 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba;
69 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa;
70 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi;
71 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Ahiezeri mwana wa Amishadai.
72 Na siku ya kumi na moja Pagieli mwana wa Okrani, mkuu wa wana wa Asheri;
73 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga;
74 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba;
75 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa;
76 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi;
77 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Pagieli mwana wa Okrani.
78 Na siku ya kumi na mbili Ahira mwana wa Enani, mkuu wa wana wa Naftali;
79 matoleo yake yalikuwa sahani moja ya fedha, uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na bakuli moja ya fedha, uzani wake shekeli sabini, kwa shekeli ya mahali patakatifu; vyombo hivyo vyote viwili vilikuwa vimejaa unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, kuwa sadaka ya unga;
80 na kijiko kimoja cha dhahabu, uzani wake shekeli kumi, kilichojaa uvumba;
81 na ng'ombe mmoja mume mchanga, na kondoo mume mmoja, na mwana-kondoo mume mmoja wa mwaka wa kwanza, kuwa sadaka ya kuteketezwa;
82 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi;
83 tena kwa ajili ya dhabihu ya sadaka za amani, ng'ombe wawili waume, na kondoo waume watano, na mbuzi waume watano, na wana-kondoo watano waume wa mwaka wa kwanza; hayo ndiyo matoleo ya Ahira mwana wa Enani.
84 Hayo ndiyo matoleo yaliyotolewa na wakuu wa Israeli kwa ajili ya kuiweka wakfu madhabahu, siku hiyo ilipotiwa mafuta; sahani za fedha kumi na mbili, na bakuli za fedha kumi na mbili, na vijiko vya dhahabu kumi na viwili;
85 kila sahani ya fedha uzani wake ni shekeli mia na thelathini, na kila bakuli uzani wake ni shekeli sabini; fedha yote ya vile vyombo ilikuwa shekeli elfu mbili na mia nne, kwa shekeli ya mahali patakatifu;
86 na vijiko vya dhahabu vilivyojaa uvumba kumi na viwili, uzani wake kila kijiko shekeli kumi, kwa shekeli ya mahali patakatifu; dhahabu yote ya vile vijiko ilikuwa shekeli mia na ishirini;
87 ng'ombe wote waliokuwa wa sadaka ya kuteketezwa walikuwa ng'ombe waume kumi na wawili, na hao kondoo waume walikuwa kumi na wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza walikuwa kumi na wawili, pamoja na sadaka yao ya unga; na mbuzi waume wa sadaka ya dhambi ni kumi na wawili;
88 na ng'ombe wote waliokuwa wa dhabihu ya sadaka za amani ni ng'ombe waume ishirini na wanne, na hao kondoo waume walikuwa ni sitini, na hao mbuzi waume walikuwa ni sitini, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza walikuwa sitini. Hayo ndiyo matoleo yaliyotolewa kwa ajili ya kuiweka wakfu madhabahu, baada ya hiyo madhabahu kutiwa mafuta.
89 Kisha, Musa alipoingia ndani ya hema ya kukutania ili kunena na Mungu ndipo alipoisikia Sauti ikinena naye kutoka hapo juu ya kiti cha rehema, kilichokuwa juu ya sanduku la ushahidi, ikitoka kati ya yale makerubi mawili; naye akanena naye.

Hesabu 8


1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena na Haruni, ukamwambie, Utakapoziweka taa, hizo taa saba zitatoa nuru hapo mbele ya kinara cha taa.
3 Basi Haruni akafanya; akaziweka taa zake ili zitoe nuru hapo mbele ya kinara, kama Bwana alivyomwagiza Musa.
4 Na hii ndiyo kazi ya hicho kinara cha taa, ilikuwa ni kazi ya ufuzi wa dhahabu; tangu tako lake hata maua yake kilikuwa ni kazi ya ufuzi; vile vile kama ule mfano Bwana aliokuwa amemwonyesha Musa, ndivyo alivyokifanya kinara.
5 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
6 Watwae Walawi na kuwaondoa kati ya wana wa Israeli, kisha uwatakase.
7 Nawe utawafanyia mambo haya ili kuwatakasa; nyunyiza juu yao maji yatakasayo dhambi, nao wajinyoe kwa wembe mwili wote, kisha wazifue nguo zao, na kujitakasa.
8 Kisha na watwae ng'ombe mume mmoja mchanga, na sadaka yake ya unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, nawe utatwaa ng'ombe mume mchanga mwingine kuwa sadaka ya dhambi.
9 Nawe utawahudhurisha Walawi mbele ya hema ya kukutania; nawe utaukutanisha mkutano wote wa wana wa Israeli;
10 nawe utawahudhurisha Walawi mbele za Bwana; kisha wana wa Israeli wataweka mikono yao juu ya Walawi;
11 naye Haruni atawasongeza Walawi mbele za Bwana wawe sadaka ya kutikiswa, kwa ajili ya wana wa Israeli, ili wawe wenye kufanya utumishi wa Bwana.
12 Kisha Walawi wataweka mikono yao juu ya vichwa vya hao ng'ombe; nawe umtoe mmoja kuwa sadaka ya dhambi kwa Bwana, na huyo wa pili awe sadaka ya kuteketezwa, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya Walawi.
13 Kisha utawaweka Walawi mbele ya Haruni, na mbele ya wanawe na kuwasongeza kwa Bwana wawe sadaka ya kutikiswa.
14 Ndivyo utakavyowatenga Walawi na kuwatoa katika wana wa Israeli; na Walawi watakuwa wangu.
15 Kisha baadaye Walawi wataingia ndani, ili wafanye utumishi wa hema ya kukutania; nawe utawatakasa, na kuwasongeza wawe sadaka ya kutikiswa.
16 Kwa kuwa nimepewa kabisa mimi watu hawa kutoka katika wana wa Israeli; badala ya wote wafunguao mimba, maana, wazaliwa wa kwanza wa wana wa Israeli wote, nimewatwaa wawe wangu.
17 Kwa kuwa wazaliwa wa kwanza wote katika wana wa Israeli ni wangu, wa wanadamu na wa wanyama; siku hiyo niliyowapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri niliwatakasa kwa ajili yangu mwenyewe.
18 Nami nimewatwaa Walawi badala ya wazaliwa wa kwanza wote walio katika wana wa Israeli.
19 Nami nimempa Haruni hao Walawi wawe kipawa chake yeye na wanawe, kutoka kwa wana wa Israeli, ili watumike utumishi wa wana wa Israeli katika hema ya kukutania, kisha wafanye upatanisho kwa ajili ya wana wa Israeli; ili kusiwe na maradhi kati ya wana wa Israeli, hapo wana wa Israeli watakapopakaribia mahali patakatifu.
20 Basi Musa na Haruni, na mkutano wote wa wana wa Israeli, wakawafanyia Walawi mambo hayo; kama hayo yote Bwana aliyomwagiza Musa kwa habari za hao Walawi, ndivyo wana wa Israeli walivyowafanyia.
21 Walawi wakajitakasa na dhambi, nao wakafua nguo zao; kisha Haruni akawasongeza mbele za Bwana wawe sadaka ya kutikiswa; Haruni akafanya kwa ajili yao ili kuwatakasa.
22 Kisha baada ya hayo Walawi wakaingia ili wafanye utumishi wao ndani ya hema ya kukutania mbele ya Haruni na mbele ya wanawe; kama Bwana alivyomwagiza Musa kwa habari za hao Walawi, ndivyo walivyowafanyia.
23 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
24 Mambo yawapasayo hao Walawi ni haya; tangu waliopata umri wa miaka ishirini na mitano na zaidi wataingia ndani ili watumike utumishi katika kazi ya hema ya kukutania;
25 tena tangu waliopata umri wa miaka hamsini wataacha kutumika huo utumishi, wasitumike tena;
26 lakini watatumika pamoja na ndugu zao katika hema ya kukutania, kushika ulinzi, lakini wasitumike katika huo utumishi tena. Ndivyo utakavyowafanyia Walawi katika mambo ya ulinzi wao.

Hesabu 9


1 Kisha Bwana akanena na Musa katika bara ya Sinai, mwezi wa kwanza wa mwaka wa pili baada ya kutoka kwao katika nchi ya Misri, akamwambia,
2 Tena, wana wa Israeli na washike sikukuu ya Pasaka kwa wakati wake ulioagizwa.
3 Siku ya kumi na nne ya mwezi huu, wakati wa jioni, mtaishika kwa wakati wake ulioagizwa; kwa amri zake zote, na kama hukumu zake zote zilivyo, ndivyo mtakavyoishika.
4 Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli kwamba waishike sikukuu hiyo ya Pasaka;
5 Nao wakaishika Pasaka katika mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, wakati wa jioni, katika bara ya Sinai vile vile kama hayo yote Bwana aliyomwagiza Musa, ndivyo walivyofanya wana wa Israeli.
6 Basi walikuwako watu waume kadha wa kadha waliokuwa na unajisi kwa ajili ya maiti wa mtu, hata wasiweze kuishika Pasaka siku hiyo; nao wakaenda mbele ya Musa na Haruni, siku hiyo hao watu wakamwambia,
7 Sisi tu hali ya unajisi kwa ajili ya maiti wa mtu; nasi tumezuiwa kwa nini hata tusipate kumtolea Bwana matoleo kwa wakati wake ulioagizwa, kati ya wana wa Israeli?
8 Musa akawaambia, Ngojeni hapo; hata nipate sikiza Bwana atakaloagiza juu yenu.
9 Bwana akanena na Musa, akamwambia,
10 Nena na wana wa Israeli, kuwaambia, Mtu wa kwenu, au wa vizazi vyenu, ye yote atakayekuwa na unajisi kwa ajili ya maiti, au akiwako mbali katika safari, na haya yote, ataishika Pasaka kwa Bwana;
11 mwezi wa pili, siku ya kumi na nne ya mwezi, wakati wa jioni, wataishika; watamla pamoja na mikate isiyotiwa chachu na mboga za uchungu;
12 wasisaze kitu chake cho chote hata asubuhi, wala wasimvunje mfupa wake; kama hiyo sheria yote ya Pasaka ilivyo ndivyo watakavyoishika.
13 Lakini mtu aliye safi, wala hakuwa katika safari, naye amekosa kuishika Pasaka, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake; kwa sababu hakumtolea Bwana matoleo kwa wakati wake ulioamriwa, mtu huyo atachukua dhambi yake.
14 Na kama mgeni akiketi kati yenu ugenini, naye ataka kuishika Pasaka kwa Bwana; kama hiyo sheria ya Pasaka ilivyo, na kama amri yake ilivyo, ndivyo atakavyofanya; mtakuwa na sheria moja, kwa huyo aliye mgeni, na kwa huyo aliyezaliwa katika nchi.
15 Na siku hiyo maskani iliposimamishwa, lile wingu likaifunika maskani, yaani, hema ya kukutania; wakati wa jioni likawa juu ya maskani, mfano wa moto, hata asubuhi.
16 Ndivyo ilivyokuwa sikuzote; lile wingu liliifunika kwa mfano wa moto usiku.
17 Na kila lilipoinuliwa lile wingu juu ya ile Hema ndipo wana wa Israeli waliposafiri; na mahali lilipokaa lile wingu, ndipo wana wa Israeli walipopiga kambi yao.
18 Kwa amri ya Bwana Wana wa Israeli walisafiri, na kwa amri ya Bwana walipiga kambi; wakati lile wingu ilipokaa juu ya maskani walikaa katika kambi yao.
19 Na lile wingu lilipokawia juu ya maskani siku nyingi, ndipo wana wa Israeli walipolinda malinzi ya Bwana, wala hawakusafiri.
20 Na pengine lile wingu lilikaa juu ya maskani siku chache; ndipo kwa amri ya Bwana walikaa katika kambi yao, tena kwa amri ya Bwana walisafiri.
21 Na pengine lile wingu lilikaa tangu jioni hata asubuhi; na lile wingu lilipoinuliwa asubuhi walisafiri, au kama likikaa usiku na mchana pia, lilipoinuliwa lile wingu, ndipo waliposafiri.
22 Ikiwa lile wingu lilikawia, likikaa juu ya maskani siku mbili, au mwezi, au mwaka, wana wa Israeli walikaa katika kambi yao, wasisafiri;
23 bali lilipoinuliwa walisafiri. Kwa amri ya Bwana walipiga kambi yao, na kwa amri ya Bwana walisafiri; wakayalinda malinzi ya Bwana, kwa mkono wa Musa.

Hesabu 10


1 Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia,
2 Jifanyie tarumbeta mbili za fedha; utazifanya za kazi ya ufuzi; nawe utazitumia kwa kuwaita mkutano wakutane, na kwa kusafiri kwao yale makambi.
3 Na hapo watakapozipiga hizo tarumbeta, mkutano wote utakukutanikia wewe, hapo mlangoni pa hema ya kukutania.
4 Nao wakipiga tarumbeta moja tu ndipo wakuu, walio vichwa vya maelfu ya Israeli, watakukutanikia wewe
5 Tena hapo mtakapopiga sauti ya kugutusha sana, marago yaliyoko upande wa mashariki yatasafiri. Tena hapo mtakapopiga sauti ya kugutusha ya pili, marago yaliyoko upande wa kusini watasafiri;
6 watapiga sauti ya kugutusha kwa ajili ya safari zao.
7 Lakini mkutano utakapokutanishwa pamoja mtapiga, lakini hamtapiga sauti ya kugutusha.
8 Wana wa Haruni, makuhani, ndio watakaopiga hizo tarumbeta; nazo zitakuwa kwenu ni amri ya milele katika vizazi vyenu vyote.
9 Tena hapo mtakapokwenda kupiga vita katika nchi yenu, kupigana na adui awaoneaye ninyi, ndipo mtakapopiga sauti ya kugutusha kwa tarumbeta; nanyi mtakumbukwa mbele za Bwana, Mungu wenu, nanyi mtaokolewa na adui zenu.
10 Tena katika siku ya furaha yenu, na katika sikukuu zenu zilizoamriwa, na katika kuandama miezi kwenu, mtapiga hizo tarumbeta juu ya sadaka zenu za kuteketezwa, na juu ya dhabihu za sadaka zenu za amani; nazo zitakuwa kwenu ni ukumbusho mbele za Mungu wenu; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
11 Ikawa mwaka wa pili, mwezi wa pili, siku ya ishirini ya mwezi, hilo wingu liliinuka kutoka pale juu ya maskani ya ushahidi.
12 Wana wa Israeli wakasafiri kwenda mbele, kwa safari zao kutoka jangwa la Sinai; na hilo wingu likakaa katika jangwa la Parani.
13 Nao wakasafiri kwanza kwa amri ya Bwana kwa mkono wa Musa.
14 Mahali pa mbele ilisafiri beramu ya marago ya wana wa Yuda, kwa majeshi yao; na Nashoni mwana wa Aminadabu ndiye aliyekuwa juu ya jeshi lake.
15 Na juu ya jeshi la kabila ya wana wa Isakari alikuwa Nethaneli mwana wa Suari.
16 Na juu ya jeshi la kabila ya wana wa Zabuloni ni Eliabu mwana wa Heloni.
17 Na maskani ilishushwa; na wana wa Gershoni, na wana wa Merari, walioichukua maskani, wakasafiri kwenda mbele.
18 Kisha beramu ya marago ya Reubeni ikasafiri kwenda mbele kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake alikuwa Elisuri mwana wa Shedeuri.
19 Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Simeoni ni Shelumieli mwana wa Suri-shadai.
20 Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Gadi ni Eliasafu mwana wa Deueli.
21 Ndipo wakasafiri Wakohathi wenye kuvichukua vile vitu vitakatifu; na hao wengine wakaisimamisha maskani kabla hawajaja wao.
22 Kisha beramu ya marago ya wana wa Efraimu ikasafiri kwenda mbele kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake ni Elishama mwana wa Amihudi.
23 Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Manase ni Gamalieli mwana wa Pedasuri.
24 Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Benyamini ni Abidani mwana wa Gideoni.
25 Kisha beramu ya marago ya wana wa Dani, ambayo yalikuwa ni nyuma ya marago yote, ikasafiri, kwa majeshi yao; na juu ya jeshi lake ni Ahiezeri mwana wa Amishadai.
26 Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Asheri ni Pagieli mwana wa Okrani;
27 Tena juu ya jeshi la kabila ya wana wa Naftali ni Ahira mwana wa Enani.
28 Ndivyo zilivyokuwa safari zao wana wa Israeli kwa majeshi: yao; nao wakasafiri kwenda mbele.
29 Kisha Musa akamwambia Hobabu, mwana wa Reueli Mmidiani, mkwewe Musa, Sisi twasafiri kwenenda mahali ambapo Bwana amenena habari zake hivi, Nitawapa ninyi mahali hapo; uje pamoja nasi, nasi tutakufanyia mema; kwa kuwa Bwana ametamka mema juu ya Israeli.
30 Naye akamwambia, Siendi mimi; ila nitairudia nchi yangu mwenyewe, na kwa jamaa zangu mwenyewe.
31 Naye akamwambia, Usituache, tafadhali; kwa kuwa wewe wajua jinsi tutakavyopanga nyikani, nawe utakuwa kwetu badala ya macho.
32 Itakuwa, ukienda pamoja nasi, naam, itakuwa mema yo yote Bwana atakayotutendea sisi, tutakutendea wewe vivyo.
33 Basi wakasafiri kutoka penye mlima wa Bwana safari ya siku tatu; na sanduku la agano la Bwana likatangulia mbele yao mwendo wa siku tatu, ili kuwatafutia mahali pa kupumzika.
34 Na wingu la Bwana lilikuwa juu yao mchana hapo waliposafiri kwenda mbele kutoka kambini.
35 Ilikuwa, hapo sanduku liliposafiri kwenda mbele, ndipo Musa akasema, Inuka, Ee Bwana, adui zako na watawanyike; na wakimbie mbele zako hao wakuchukiao.
36 Tena hapo liliposimama, akasema, Ee Bwana, uwarudie maelfu kumi ya maelfu ya Israeli.

Hesabu 11


1 Kisha hao watu walikuwa kama wanung'unikao, wakinena maovu masikioni mwa Bwana; Bwana aliposikia hayo, hasira zake zikawaka; na moto wa Bwana ukawaka kati yao, ukateketeza katika mipaka ya mwisho wa marago.
2 Ndipo watu wakamlilia Musa; naye Musa akamwomba Bwana, na ule moto ukakoma.
3 Jina la mahali hapo likaitwa Tabera; kwa sababu huo moto wa Bwana ukawaka kati yao.
4 Kisha mkutano wa wafuasi waliokuwa kati yao, wakashikwa na tamaa; wana wa Israeli nao wakalia tena, wakasema, N'nani atakayetupa nyama tule?
5 Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu;
6 lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hii mana tu.
7 Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtama na kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake bedola.
8 Watu wakazunguka-zunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa nyunguni, na kuandaa mikate; na tamu yake ilikuwa kama tamu ya mafuta mapya.
9 Umande ulipoyaangukia marago wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao.
10 Basi Musa akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za Bwana zikawaka sana; Musa naye akakasirika.
11 Musa akamwambia Bwana, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? Kwa nini sikupata neema machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu?
12 Je! Ni mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote je! Ni mimi niliyewazaa, hata ikawa wewe kuniambia, Haya, wachukue kifuani mwako, mfano wa baba mwenye kulea achukuavyo mtoto anyonyaye, uende nao mpaka nchi uliyowaapia baba zao?
13 Nipate wapi nyama ya kuwapa watu hawa wote? Kwani wanililia, wakisema Tupe nyama, tupate kula.
14 Mimi siwezi kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa kunishinda.
15 Na kama ukinitenda hivi, nakuomba uniulie mbali, kwamba nimepata fadhili mbele ya macho yako; nami nisiyaone haya mashaka yangu.
16 Kisha Bwana akamwambia Musa, Nikusanyie watu sabini, miongoni mwa wazee wa israeli, ambao wewe wawajua kuwa ndio wazee wa watu hawa, na maakida juu yao; ukawalete hata hema ya kukutania, wasimame huko pamoja nawe.
17 Nami nitashuka niseme nawe huko, nami nitatwaa sehemu ya roho iliyo juu yako na kuiweka juu yao; nao watachukua mzigo wa watu hawa pamoja nawe, ili usiuchukue wewe peke yako.
18 Kisha uwaambie watu hawa, Jitakaseni nafsi zenu kabla ya kesho, nanyi mtakula nyama; kwa maana mmelia masikioni mwa Bwana, mkisema, Ni nani atakayetupa nyama, tule? Maana huko Misri tulikuwa na uheri. Basi kwa sababu hiyo Bwana atawapa nyama, nanyi mtakula.
19 Hamtakula siku moja, wala siku mbili, wala siku tano, wala siku kumi, wala siku ishirini;
20 lakini mtakula muda wa mwezi mzima, hata hapo nyama hiyo itakapotoka katika mianzi ya pua zenu, nanyi mtaikinai, kwa sababu mmemkataa Bwana aliye kati yenu, na kulia mbele zake, mkisema, Tulitoka Misri kwa maana gani?
21 Musa akasema, Watu hawa ambao mimi ni kati yao, ni watu sita mia elfu waendao kwa miguu; nawe umesema, Nitawapa nyama, ili wale muda wa mwezi mzima.
22 Je! Makundi ya kondoo na ng'ombe yatachinjwa kwa ajili yao, ili kuwatosha? Au samaki wote wa baharini watakusanywa pamoja kwa ajili yao, ili kuwatosha?
23 Bwana akamwambia Musa, Je! Mkono wa Bwana umepungua urefu wake? Sasa utaona kwamba neno langu litatimizwa kwako, au sivyo.
24 Musa akatoka, akawaambia watu maneno ya Bwana; akawakutanisha watu sabini miongoni mwa wazee wa watu, akawaweka kuizunguka Hema.
25 Ndipo Bwana akashuka ndani ya wingu, akanena naye, akatwaa sehemu ya roho iliyokuwa juu ya Musa, akaitia juu ya wale wazee sabini; ikawa, roho hiyo ilipowashukia, wakatabiri, lakini hawakufanya hivyo tena.
26 Lakini watu wawili walisalia kambini, jina la mmoja aliitwa Eldadi, na jina la wa pili aliitwa Medadi; na roho ile ikawashukia; nao walikuwa miongoni mwao walioandikwa, lakini walikuwa hawakutoka kwenda hemani; nao wakatabiri kambini.
27 Mtu mmoja kijana akapiga mbio, akaenda akamwambia Musa, akasema, Eldadi na Medadi wanatoa unabii kambini.
28 Yoshua mwana wa Nuni, mtumishi wa Musa tangu ujana wake, akajibu akasema, Ee bwana wangu Musa, uwakataze.
29 Musa akamwambia, Je! Umekuwa na wivu kwa ajili yangu; ingekuwa heri kama watu wote wa Bwana wangekuwa manabii na kama Bwana angewatia roho yake.
30 Kisha Musa akaenda akaingia kambini, yeye na wale wazee wa Israeli.
31 Kisha upepo ukavuma kutoka kwa Bwana, nao ukaleta kware kutoka pande za baharini, nao ukawaacha wakaanguka karibu na kambi, kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, na kama kiasi cha mwendo wa siku moja upande huu, kuizunguka, nao wakafikilia kiasi cha dhiraa mbili juu ya uso wa nchi.
32 Watu wakaondoka mchana huo wote, na usiku huo wote, na siku ya pili yote, kuwakusanya hao kware; yeye aliyepata ya upungufu kuliko wenziwe alipata kiasi cha homeri kumi; nao wakawaanika wote kando-kando ya kambi kuizunguka pande zote.
33 Kisha hapo hiyo nyama ilipokuwa ikali kati ya meno yao, hawajaitafuna bado, hasira za Bwana ziliwaka juu ya watu, Bwana akawapiga watu kwa pigo kuu mno.
34 Jina la mahali pale likaitwa Kibroth-hataava; maana, ni hapo walipowazika hao watu waliotamani.
35 Kutoka hapo Kibroth-hataava watu wakasafiri kwenda Haserothi; wakakaa huko Haserothi.

Hesabu 12


1 Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi.
2 Wakasema, Je! Ni kweli Bwana amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? Bwana akasikia maneno yao.
3 Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi.
4 Bwana akanena ghafula na Musa, na Haruni na Miriamu, na kuwaambia, Tokeni nje ninyi watatu, mwende hemani mwa kukutania. Basi hao watatu wakatoka nje.
5 Bwana akashuka katika nguzo ya wingu akasimama pale mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka nje wote wawili.
6 Kisha akawaambia,Sikizeni basi maneno yangu;Akiwapo nabii kati yenu,Mimi,Bwana,nitajifunua kwake katika maono,Nitasema naye katika ndoto.
7 Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote;
8 Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la Bwana yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa?
9 Hasira za Bwana zikawaka juu yao; naye akaenda zake.
10 Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma.
11 Kisha Haruni akamwambia Musa, Ee bwana wangu nakusihi sana usituwekee dhambi juu yetu, kwa kuwa tumefanya ya upumbavu, na kufanya dhambi.
12 Nakusihi, asiwe kama mmoja aliyekufa, ambaye nyama ya mwili wake nusu imelika hapo atokapo tumbo la mama yake.
13 Musa akamlilia Bwana, akasema, Mpoze, Ee Mungu, nakusihi sana.
14 Bwana akamwambia Musa, Je! Kama baba yake angalimtemea mate usoni tu, hangaliona aibu muda wa siku saba? Na afungwe nje ya kambi muda wa siku saba, kisha baada ya hayo ataletwa ndani tena.
15 Basi Miriamu alifungwa nje ya kambi muda wa siku saba; wala watu hawakusafiri hata Miriamu alipoletwa ndani tena.
16 Baada ya hayo watu wakasafiri kutoka Haserothi, wakapanga kambi katika nyika ya Parani.

Hesabu 13


1 Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia,
2 Tuma watu, ili waende wakaipeleleze nchi ya Kanaani, niwapayo wana wa Israeli; katika kabila ya baba zao mtamtuma mtu mmoja, kila mtu na awe mkuu kati yao.
3 Basi Musa akawatuma kutoka nyika ya Parani kama alivyoagizwa na Bwana; wote walikuwa ni watu walio vichwa vya wana wa Israeli.
4 Na majina yao ni haya; katika kabila ya Reubeni, Shamua mwana Zakuri.
5 Katika kabila ya Simeoni, Shafati mwana wa Hori.
6 Katika kabila ya Yuda, Kalebu mwana wa Yefune.
7 Katika kabila ya Isakari, Igali mwana wa Yusufu.
8 Katika kabila ya Efraimu, Hoshea mwana wa Nuni
9 Katika kabila ya Benyamini, Palti mwana wa Rafu.
10 Katika kabila ya Zabuloni, Gadieli mwana wa Sodi.
11 Katika kabila ya Yusufu, yaani, katika kabila ya Manase, Gadi mwana wa Susi.
12 Katika kabila ya Dani, Amieli mwana wa Gemali.
13 Katika kabila ya Asheri, Sethuri mwana wa Mikaeli.
14 Katika kabila ya Naftali, Nabi mwana wa Wofsi.
15 Katika kabila ya Gadi, Geueli mwana wa Maki.
16 Hayo ndiyo majina ya hao watu waliotumwa na Musa waende kuipeleleza nchi. Na huyo Hoshea mwana wa Nuni, Musa akamwita jina lake Yoshua.
17 Musa akawapeleka ili waipeleleze nchi ya Kanaani, akawaambia, Pandeni sasa katika Negebu mkapande milimani,
18 mkaitazame nchi ni ya namna gani; na watu wanaokaa ndani yake, kwamba ni hodari au dhaifu, kwamba ni wachache au wengi;
19 na nchi wanayoikaa kwamba ni njema au mbaya; kwamba wanakaa katika matuo au katika ngome;
20 nayo nchi ni ya namna gani, kwamba ni nchi ya unono au ya njaa, kwamba ina msitu au sivyo. Iweni na moyo mkuu, mkayalete matunda ya nchi. Basi wakati ule ulikuwa wakati wa kuiva zabibu za kwanza.
21 Basi wakapanda wakaipeleleza nchi toka jangwa la Sini hata Rehobu, mpaka kuingia Hamathi.
22 Wakapanda katika Negebu, wakafika Hebroni; na Ahimani, na Sheshai, na Talmai, wana wa Anaki, walikuwako huko. Nao Hebroni ulijengwa miaka saba kabla ya Soani wa Misri.
23 Wakafika bonde la Eshkoli, na huko wakakata tawi lenye kishada kimoja cha zabibu, wakalichukua kwa mti kati ya watu wawili; wakaleta makomamanga pia, na tini.
24 Bonde lile liliitwa bonde la Eshkoli kwa sababu ya hicho kishada walichokata huko wana wa Israeli.
25 Wakarejea baada ya kuipeleleza nchi, mwisho wa siku arobaini.
26 Wakaenda wakafika kwa Musa, na kwa Haruni, na kwa mkutano wote wa wana wa Israeli, katika jangwa la Parani, huko Kadeshi; wakawaletea habari, wao na mkutano wote, wakawaonyesha matunda ya nchi.
27 Wakamwambia wakasema, Tulifika nchi ile uliyotutuma, na hakika yake, ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali, na haya ndiyo matunda yake.
28 Lakini watu wanaokaa katika nchi ile ni hodari, na miji yao ina maboma, nayo ni makubwa sana; na pamoja na hayo tuliwaona wana wa Anaki huko.
29 Amaleki anakaa katika nchi ya Negebu; na Mhiti, na Myebusi, na Mwamori wanakaa katika milima, na Mkanaani anakaa karibu na bahari; na kando ya ukingo wa Yordani.
30 Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka.
31 Bali wale watu waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi.
32 Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya ile nchi waliyoipeleleza, wakasema, Ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno.
33 Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.

Hesabu 14


1 Mkutano wote wakapaza sauti zao wakalia; watu wakatoka machozi usiku ule.
2 Kisha wana wa Israeli wote wakamnung'unikia Musa na Haruni; mkutano wote wakawaambia, Ingekuwa heri kama tungalikufa katika nchi ya Misri, au, ingekuwa heri kama tungalikufa katika jangwa hili.
3 Mbona Bwana anatuleta mpaka nchi hii ili tuanguke kwa upanga? Wake zetu na watoto wetu watakuwa mateka; je! Si afadhali turudi Misri?
4 Wakaambiana, Na tumweke mtu mmoja awe akida, tukarudi Misri.
5 Ndipo Musa na Haruni wakaanguka kifudifudi mbele ya mkutano wa kusanyiko la wana wa Israeli.
6 Na Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, waliokuwa miongoni mwao walioipeleleza nchi, wakararua nguo zao;
7 wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu.
8 Ikiwa Bwana anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali.
9 Lakini msimwasi Bwana, wala msiwaogope wale wenyeji wa nchi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye Bwana yu pamoja nasi; msiwaogope.
10 Lakini mkutano wote wakaamuru wapigwe kwa mawe. Ndipo utukufu wa Bwana ukaonekana katika hema ya kukutania, mbele ya wana wa Israeli wote.
11 Bwana akamwuliza Musa, Je! Watu hawa watanidharau hata lini? Wasiniamini hata lini? Nijapokuwa nimefanya ishara hizo zote kati yao.
12 Nitawapiga kwa tauni, na kuwaondolea urithi wao, nami nitakufanya wewe kuwa taifa kubwa, kisha yenye nguvu kuliko wao.
13 Basi Musa akamwambia Bwana, Ndipo Wamisri watasikia habari hiyo; kwa kuwa wewe uliwaleta watu hawa kwa uweza wako, kutoka kati yao;
14 kisha watawaambia wenyeji wa nchi hii; wamesikia wao ya kuwa wewe Bwana u kati ya watu hawa; maana, wewe Bwana waonekana uso kwa uso, na wingu lako lasimama juu yao, kisha wewe watangulia mbele yao, katika nguzo ya wingu mchana, na katika nguzo ya moto usiku.
15 Basi kama wewe ukiwaua watu hawa mfano wa mtu mmoja, ndipo mataifa yaliyosikia habari za sifa zako watakaponena na kusema,
16 Ni kwa sababu yeye Bwana hakuweza kuwaleta watu hao kuwatia katika nchi aliyowaapia, kwa ajili ya hayo amewaua nyikani.
17 Basi sasa nakusihi sana, uweza wa Bwana wangu na uwe mkuu, kama ulivyonena, uliposema,
18 Bwana ni mpole wa hasira, mwingi wa rehema, mwenye kusamehe uovu na makosa, naye hatamfanya mwenye hatia kuwa hana makosa kwa njia yo yote; mwenye kuwapatiliza wana kwa uovu wa baba zao, katika kizazi cha tatu na cha nne.
19 Nakusihi, usamehe uovu wa watu hawa, kama ukuu wa rehema yako ulivyo, kama ulivyowasamehe watu hawa, tangu huko Misri hata hivi sasa.
20 Bwana akasema, Mimi nimewasamehe kama neno lako lilivyokuwa;
21 lakini hakika yangu, kama niishivyo, tena kama dunia hii nzima itakavyojawa na utukufu wa Bwana;
22 kwa sababu watu hawa wote, ambao wameuona utukufu wangu na ishara zangu, nilizozitenda huko Misri, na huko jangwani, pamoja na haya wamenijaribu mara hizi kumi, wala hawakuisikiza sauti yangu;
23 hakika yangu hawataiona hiyo nchi niliyowaapia baba zao, wala katika hao wote walionidharau hapana atakayeiona;
24 lakini mtumishi wangu Kalebu, kwa kuwa alikuwa na roho nyingine ndani yake, naye ameniandama kwa moyo wote, nitamleta yeye mpaka nchi hiyo aliyoingia; na uzao wake wataimiliki.
25 Basi Mwamaleki na Mkanaani wakaa katika bonde; kesho geukeni, mkaende jangwani kwa njia iendayo Bahari ya Shamu.
26 Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
27 Je! Nichukuane na mkutano mwovu huu uninung'unikiao hata lini? Nimesikia manung'uniko ya wana wa Israeli, waninung'unikiayo.
28 Waambieni, Kama niishivyo, asema Bwana, hakika yangu kama ninyi mlivyonena masikioni mwangu, ndivyo nitakavyowafanyia ninyi;
29 mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili, na wote waliohesabiwa miongoni mwenu, kama jumla ya hesabu yenu, tangu waliopata umri wa miaka ishirini na zaidi, hao walioninung'unikia,
30 hakika yangu hamtaingia ninyi katika nchi, ambayo niliinua mkono wangu ya kwamba nitawaketisha humo, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni.
31 Lakini Watoto wenu, ambao mlisema watakuwa mateka, ndio nitakaowaleta na kuwatia ndani, nao wataijua nchi ninyi mliyoikataa.
32 Lakini katika habari zenu, mizoga yenu itaanguka katika jangwa hili.
33 Kisha watoto wenu watakuwa wachungaji jangwani muda wa miaka arobaini nao watauchukua mzigo wa uasherati wenu, hata mizoga yenu itakapoangamia jangwani.
34 Kwa hesabu ya hizo siku mlizoipeleleza ile nchi, yaani, siku arobaini kila siku kuhesabiwa mwaka, mtayachukua maovu yenu, ndiyo miaka arobaini, nanyi mtakujua kufarikana kwangu.
35 Mimi Bwana nimekwisha nena, hakika yangu ndilo nitakaloutenda mkutano mwovu huu wote, waliokusanyika juu yangu; wataangamia katika nyika hii, nako ndiko Watakakokufa.
36 Kisha hao watu, ambao Musa aliwatuma waipeleleze nchi, waliorudi, na kufanya mkutano wote kumnung'unikia, kwa walivyoleta habari mbaya juu ya nchi,
37 watu hao walioileta habari mbaya ya nchi wakafa kwa tauni mbele ya Bwana.
38 Lakini Yoshua mwana wa Nuni, na Kalebu mwana wa Yefune, wakabaki hai miongoni mwa wale watu waliokwenda kuipeleleza nchi.
39 Kisha Musa akawaambia wana wa Israeli wote maneno haya, na hao watu wakaombolea sana.
40 Wakainuka na mapema asubuhi, wakakwea juu ya mlima hata kileleni, wakisema, Tazameni, sisi tupo hapa, nasi tutakwea kwenda mahali Bwana alipotuahidi; kwani tumefanya dhambi.
41 Musa akawaambia, Kwa nini ninyi sasa kuyahalifu maagizo ya Bwana? Maana halitafanikiwa jambo hilo.
42 Msikwee, kwa kuwa Bwana hamo kati yenu; msipigwe na kuangushwa mbele ya adui zenu.
43 Kwa kuwa Mwamaleki na Mkanaani wako mbele yenu, nanyi mtaanguka kwa upanga, kwa sababu mmerudi nyuma msimwandame Bwana, kwa hiyo Bwana hatakuwa pamoja nanyi.
44 Lakini walithubutu kukwea mlimani hata kileleni; ila sanduku la agano la Bwana halikutoka humo maragoni, wala Musa hakutoka.
45 Ndipo Mwamaleki, na Mkanaani waliokaa huko mlimani, wakatelemka, wakawapiga na kuwaangusha, hata kufikilia Horma.

Hesabu 15


1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Mtakapoingia nchi yenu ya kukaa, niwapayo,
3 nanyi mwataka kumsongezea Bwana sadaka kwa moto, kwamba ni sadaka ya kuteketezwa, au dhabihu ya kuchinjwa, ili kuondoa nadhiri, au kuwa sadaka ya hiari, au katika sikukuu zenu zilizoamriwa, ili kumfanyia Bwana harufu ipendezayo, katika ng'ombe, au katika kondoo;
4 ndipo yeye atakayetoa matoleo yake na amtolee Bwana sadaka ya unga ya sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta;
5 na divai kwa sadaka ya kinywaji, robo ya hini, utaiandaa pamoja na sadaka ya kuteketezwa, au kwa dhabihu ya kuchinjwa, kwa ajili ya kila mwana-kondoo.
6 Au kwa ajili ya kondoo mume, utaiandaa sadaka ya unga ya sehemu za kumi mbili za efa ya unga mwembamba uliochanganywa na sehemu ya tatu ya hini ya mafuta;
7 na kwa sadaka ya kinywaji utasongeza sehemu ya tatu ya hini ya divai, kuwa harufu ya kupendeza kwa Bwana.
8 Tena hapo utakapomwandaa ng'ombe mume kwa sadaka ya kuteketezwa, au kwa dhabihu ya kuchinjwa, kwa kuondoa nadhiri, au kwa sadaka za amani kwa Bwana;
9 ndipo utakapotoa, pamoja na huyo ng'ombe, sadaka ya unga ya sehemu za kumi tatu za efa ya unga mwembamba uliochanganywa na nusu ya hini ya mafuta.
10 Tena utasongeza nusu ya hini ya divai kwa sadaka ya kinywaji, kwa sadaka iliyosongezwa kwa moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana.
11 Ndivyo itakavyofanywa kwa kila ng'ombe, au kwa kila kondoo mume, au kwa kila mwana-kondoo mume, au kila mwana-mbuzi.
12 Kama hesabu ilivyo ya hao mtakaowaandaa, ndivyo mtakavyofanya kwa kila mmoja, sawasawa na hesabu yao.
13 Wote ambao wamezaliwa kwenu watafanya hayo yote kwa kuandama mfano huo, katika kusongeza sadaka kwa moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana.
14 Tena kwamba mgeni amekaa kwenu, au mtu ye yote aliye kati yenu katika vizazi vyenu, naye yuataka kusongeza sadaka kwa moto, na harufu ya kupendeza kwa Bwana; kama ninyi mfanyavyo, na yeye atafanya vivyo.
15 Katika huo mkutano, kutakuwa na amri moja kwenu ninyi na kwa mgeni akaaye pamoja nanyi; ni amri ya milele katika vizazi vyenu; kama ninyi mlivyo, na mgeni atakuwa vivyo mbele za Bwana.
16 Itakuwa sheria moja na amri moja kwenu ninyi na kwa mgeni akaaye nanyi.
17 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
18 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapoingia nchi niwapelekayo,
19 ndipo itakapokuwa ya kwamba hapo mtakapokula katika chakula cha nchi hiyo, mtamsongezea Bwana sadaka ya kuinuliwa.
20 Katika unga wenu wa kwanza wa chenga-chenga mtasongeza mkate uwe sadaka ya kuinuliwa; vile vile kama mfanyavyo sadaka ya kuinuliwa ya sakafu ya kupuria nafaka, ndivyo mtakavyoiinua.
21 Malimbuko ya unga wenu mtampa Bwana sadaka ya kuinuliwa, katika vizazi vyenu.
22 Tena mtakapokosa, msiyashike maagizo hayo yote Bwana aliyomwambia Musa,
23 hayo yote Bwana aliyowaagiza kwa mkono wa Musa, tangu siku hiyo Bwana aliyoleta maagizo, na baadaye katika vizazi vyenu
24 ndipo itakapokuwa, kama ni kosa lililofanywa pasipo kujua, wala mkutano haukuwa na fahamu, ndipo mkutano wote utasongeza ng'ombe mume mmoja mdogo kuwa sadaka ya kuteketezwa, kuwa harufu ya kupendeza kwa Bwana, pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka yake ya kinywaji, kama amri ilivyo, na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi.
25 Naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya mkutano wote wa wana wa Israeli, nao watasamehewa; maana, lilikuwa ni kosa, nao wamekwisha leta matoleo yao, sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa moto, na sadaka yao ya dhambi pia wameileta mbele za Bwana kwa ajili ya kosa lao;
26 nao mkutano wote wa wana wa Israeli watasamehewa, na mgeni akaaye kati yao; maana, katika habari za hao wote jambo hilo lilitendeka pasipo kujua.
27 Tena kama mtu mmoja akifanya dhambi pasipo kujua, ndipo atasongeza mbuzi mmoja mke wa mwaka wa kwanza kuwa sadaka ya dhambi.
28 Naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili ya huyo mtu akosaye, atakapofanya dhambi pasipo kujua, mbele za Bwana, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake; naye atasemehewa.
29 Mtakuwa na sheria moja kwa huyo afanyaye neno lo lote pasipo kujua, kwa huyo aliyezaliwa kwenu kati ya wana wa Israeli, na kwa mgeni akaaye kati yao.
30 Lakini mtu afanyaye neno lo lote kwa kusudi, kama ni mzalia, kama ni mgeni, huyo amtukana Bwana; na mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.
31 Kwa sababu amelidharau neno la Bwana, na kuyavunja maagizo yake; mtu huyo atakatiliwa mbali, uovu wake utakuwa juu yake.
32 Kisha wakati huo wana wa Israeli walipokuwako jangwani, wakamwona mtu mmoja akikusanya kuni siku ya Sabato.
33 Hao waliomwona akikusanya kuni wakamleta kwa Musa na Haruni, na kwa mkutano wote.
34 Nao wakamweka kifungoni, maana, lilikuwa halijasemwa atakalotendwa.
35 Bwana akamwambia Musa, Mtu huyo lazima atauawa; mkutano wote watampiga kwa mawe huko nje ya marago.
36 Basi mkutano wote wakampeleka nje ya marago, nao wakampiga kwa mawe, akafa; kama Bwana alivyomwagiza Musa.
37 Kisha Bwana akasema na Musa, na kumwambia,
38 Nena na wana wa Israeli, na kuwaagiza ya kwamba wajifanyie vishada katika ncha za nguo zao, katika vizazi vyao, tena ya kwamba watie katika kila kishada cha kila ncha nyuzi za rangi ya samawi;
39 nacho kitakuwa kwenu ni kishada, ili mpate kukiangalia, na kuyakumbuka maagizo yote ya Bwana, na kuyafanya; tena kwamba msiende kutanga-tanga kuandama mioyo yenu wenyewe, na macho yenu wenyewe, ambayo mlikuwa mkiyaandama kwa uasherati hapo kwanza;
40 ili mpate kukumbuka na kuyafanya maagizo yangu yote, na kuwa watakatifu kwa Mungu wenu.
41 Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili kwamba niwe Mungu wenu; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.

Hesabu 16


1 Basi Kora, mwana wa Ishari, mwana wa Kohathi, mwana wa Lawi, akatwaa watu, pamoja na Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu, na Oni, mwana wa Pelethi, waliokuwa wana wa Reubeni;
2 nao, pamoja na watu kadha wa kadha wa wana wa Israeli, watu mia mbili na hamsini, Wakuu wa mkutano, waliokuwa wateule wa mkutano, watu wenye sifa, wakainuka mbele ya Musa;
3 nao wakakusanyika kinyume cha Musa na Haruni, na kuwaambia, Ninyi inawatosha, kwa kuwa mkutano wote ni mtakatifu, kila mmoja miongoni mwao, Bwana naye yu kati yao; n'nini basi kujitukuza juu ya mkutano wa Bwana?
4 Musa aliposikia maneno haya, akapomoka kifudifudi;
5 kisha akanena na Kora na mkutano wake wote, akawaambia, Asubuhi Bwana ataonyesha ni kina nani walio wake, kisha ni nani aliye mtakatifu, tena ni nani atakayemkaribisha kwake; maana, yeye atakayemchagua ndiye atakayemsongeza kwake.
6 Fanyeni neno hili; twaeni vyetezo, ninyi Kora na mkutano wake wote;
7 vitieni na moto, mkaweke na uvumba juu yake mbele za Bwana kesho; kisha itakuwa ya kwamba mtu Bwana atakayemchagua, yeye atakuwa mtakatifu; inawatosha ninyi, enyi wana wa Lawi.
8 Musa akamwambia Kora, Sikizeni basi, enyi Wana wa Lawi;
9 Je! Mwaona kuwa ni jambo dogo kwenu, kuwa Mungu wa Israeli amewatenga ninyi na mkutano wa Israeli, ili apate kuwakaribisha kwake; ili mfanye utumishi wa maskani ya Bwana, na kusimama mbele ya mkutano ili kuwatumikia;
10 tena ya kuwa amekuleta uwe karibu, na ndugu zako wote wana wa Lawi pamoja nawe? Nanyi, je! Mwataka na ukuhani pia?
11 Kwa sababu hii wewe na mkutano wako wote mmekusanyika kinyume cha Bwana; na Haruni, je! Yeye ni nani hata mkamnung'unikia?
12 Kisha Musa akatuma kuwaita Dathani na Abiramu, wana wa Eliabu; nao wakasema, Hatuji sisi;
13 je! Ni jambo dogo, wewe kutuleta kutoka nchi iliyojawa na maziwa na asali, ili kutuua jangwani, lakini pamoja na haya wajikuza mwenyewe uwe mkuu juu yetu kabisa?
14 Kisha, hukutuleta katika nchi iliyojawa na maziwa na asali, wala hukutupa urithi wa mashamba, na mashamba ya mizabibu; je! Unataka kuwatoboa macho watu hawa? Hatuji.
15 Musa akakasirika sana, akamwambia Bwana. Usiikubali sadaka yao; mimi sikutwaa hata punda mmoja kwao, wala sikumwumiza hata mtu mmoja miongoni mwao.
16 Kisha Musa akamwambia Kora, Wewe na mkutano wako wote iweni hapa mbele ya Bwana kesho, wewe, na wao, na Haruni;
17 mkatwae kila mtu chetezo chake, na kutia uvumba juu yake, mkavilete mbele za Bwana, vyetezo mia mbili na hamsini; wewe pia, na Haruni, kila mtu na awe na chetezo chake.
18 Basi wakavitwaa kila mtu chetezo chake, wakatia na moto ndani yake, wakatia na uvumba juu ya moto, na kusimama pale mlangoni pa hema ya kukutania, pamoja na Musa na Haruni.
19 Kisha Kora akakutanisha mkutano wote kinyume chao mlangoni pa hema ya kukutania; na utukufu wa Bwana ukatokea mbele ya mkutano wote.
20 Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
21 Jitengeni ninyi mkaondoke kati ya mkutano huu, ili nipate kuwaangamiza mara moja.
22 Nao wakapomoka kifudifudi, wakasema, Ee Mungu, Mungu wa roho za wenye mwili wote, je! Mtu mmoja atafanya dhambi, nawe utaukasirikia mkutano wote?
23 Bwana akasema na Musa, na kumwambia,
24 Nena na mkutano, na kuwaambia, Ondokeni ninyi hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani, na Abiramu.
25 Basi Musa akainuka na kuwaendea Dathani na Abiramu; na wazee wa Israeli wakaandamana naye.
26 Akasema na mkutano, na kuwaambia, Nawasihi, ondokeni penye hema za hawa watu waovu, wala msiguse kitu chao cho chote, msiangamizwe katika dhambi zao zote.
27 Basi wakaondoka hapo karibu na maskani ya Kora, na Dathani na Abiramu, pande zote; nao kina Dathani na Abiramu wakatoka nje wakasimama mlangoni mwa hema zao, pamoja na wake zao, na wana wao na watoto wao wadogo.
28 Musa akasema, Kwa jambo hili mtajua ya kwamba Bwana amenituma, ili nifanye kazi hizi zote; kwa kuwa mimi sikuzifanya kwa akili zangu mwenyewe.
29 Kama watu hawa wakifa kifo cha sikuzote, kama watu wote wafavyo, au kama wakipatilizwa kwa mapatilizo ya watu wote; hapo basi Bwana hakunituma mimi.
30 Lakini Bwana akiumba kitu kipya, na hiyo nchi ikifunua kinywa chake na kuwameza, pamoja na wote walio nao, nao washukia shimoni wali hai; ndipo mtatambua ya kwamba watu hawa wamemdharau Bwana
31 Basi ilikuwa, hapo alipokwisha kusema maneno haya yote, nchi iliyokuwa chini yao ikapasuka;
32 nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza, na watu wa nyumba zao na wote walioshikamana na Kora, na vyombo vyao vyote.
33 Basi wao, na wote waliokuwa nao, wakashukia shimoni wali hai; nayo nchi ikawafunika wakaangamia kutoka mle mkutanoni.
34 Nao Israeli wote waliokuwa kando-kando yao wakakimbia kwa ajili ya kilio chao; kwa kuwa walisema, Nchi isije kutumeza na sisi.
35 Kisha moto ukatoka kwa Bwana, ukawateketeza hao watu mia mbili hamsini waliofukiza uvumba.
36 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
37 Mwambie Eleazari mwana wa Haruni kuhani, avitoe vile vyetezo hapo penye moto ukaumwage huo moto kule; kwani ni vitakatifu;
38 vile vyetezo vya hao waliofanya dhambi na kuzihasiri nafsi zao wenyewe, na vifanywe mbao za kufuliwa kuwa kifuniko cha madhabahu; kwa kuwa walivisongeza mbele za Bwana, navyo ni vitakatifu; vitakuwa ishara kwa wana wa Israeli.
39 Basi Eleazari kuhani akavitwaa vile vyetezo vya shaba, vilivyosongezwa na hao walioteketezwa; nao wakavifua viwe kifuniko cha madhabahu;
40 viwe ukumbusho kwa wana wa Israeli, ili mgeni awaye yote asiye wa kizazi cha Haruni, asikaribie kufukiza uvumba mbele za Bwana; asiwe mfano wa Kora, na mkutano wake; kama Bwana alivyonena naye, kwa mkono wa Musa.
41 Lakini siku ya pili yake mkutano wote wa wana wa Israeli wakamnung'unikia Musa, na Haruni, wakasema, Ninyi mmewaua watu wa Bwana.
42 Basi ilikuwa, hapo huo mkutano ulipokuwa umekutanika kinyume cha Musa, na kinyume cha Haruni, wakaangalia upande wa hema ya kukutania; na tazama, hilo wingu likaifunika hema, na utukufu wa Bwana ukaonekana.
43 Na Musa na Haruni wakaenda hapo mbele ya hema ya kukutania.
44 Naye Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
45 Ondokeni kati ya mkutano, ili niwaangamize mara moja. Wao wakapomoka kifudifudi.
46 Musa akamwambia Haruni, Haya, shika chetezo chako, ukatie moto ndani yake, moto wa madhabahuni, kisha utie na uvumba juu ya moto, ukakichukue haraka, wende nacho katika huo mkutano, ukawafanyie upatanisho; kwa kuwa ghadhabu zimetoka kwa Bwana; hiyo tauni imeanza.
47 Basi Haruni akakishika chetezo kama Musa alivyonena, akapiga mbio akaenda katikati ya mkutano; na tazama, tauni ilikuwa imeanza kati ya watu; akatia uvumba juu ya moto na kufanya upatanisho kwa ajili ya hao watu.
48 Akasimama kati ya hao waliokufa na hao waliokuwa wakali hai; tauni ikazuiwa.
49 Basi waliokufa kwa tauni walikuwa kumi na nne elfu na mia saba, zaidi ya hao waliokufa katika jambo la Kora.
50 Haruni akamrudia Musa pale mlangoni pa hema ya kukutania; hiyo tauni ikazuiwa.

Hesabu 17


1 Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia,
2 Nena na wana wa Israeli, kisha upokee kwao fimbo, fimbo moja kwa ajili ya nyumba ya kila baba, katika wakuu wao wote, kama nyumba za baba zao zilivyo, fimbo kumi na mbili; kisha andika jina la kila mtu katika fimbo yake.
3 Na katika fimbo ya Lawi utaliandika jina la Haruni; maana, itakuwa fimbo moja kwa kila kichwa cha nyumba za baba zao.
4 Nawe utaziweka katika hema ya kukutania mbele ya huo ushahidi, hapo nikutanapo pamoja nanyi.
5 Kisha itakuwa, mtu huyo nitakayemchagua, fimbo yake itachipuka; nami nitayakomesha kwangu manung'uniko ya wana wa Israeli, wanung'unikiayo juu yenu.
6 Basi Musa akawaambia wana wa Israeli, ndipo wakuu wao wote wakampa fimbo, fimbo moja kwa kila mkuu, kama nyumba za baba zao zilivyokuwa, fimbo kumi na mbili; na fimbo ya Haruni ilikuwa kati ya fimbo zao.
7 Kisha Musa akaziweka hizo fimbo mbele za Bwana katika hema ya kukutania.
8 Ilikuwa siku ya pili yake, Musa akaingia ndani ya hema ya ushahidi; na tazama, ile fimbo ya Haruni iliyokuwa kwa nyumba ya Lawi ilikuwa imechipuka, imetoa michipukizi, na kuchanua maua; na kuzaa malozi mabivu.
9 Kisha Musa akazileta nje hizo fimbo zote kutoka hapo mbele za Bwana na kuziweka mbele ya wana wa Israeli wote; nao wakaangalia, na kila mtu akaitwaa fimbo yake.
10 Kisha Bwana akamwambia Musa, Irudishe fimbo ya Haruni mbele ya ushahidi, ili itunzwe iwe ishara juu ya hawa wana wa maasi; ili uyakomeshe manung'uniko yao waliyoninung'unikia, ili wasife.
11 Basi Musa akafanya vivyo; kama Bwana alivyomwagiza, ndivyo alivyofanya.
12 Kisha wana wa Israeli wakanena na Musa, na kumwambia, Angalia, sisi twafa, twaangamia, sote twaangamia.
13 Kila mtu akaribiaye, aikaribiaye maskani ya Bwana, hufa; je! Tutakufa pia sote?

Hesabu 18


1 Bwana akamwambia Haruni, Wewe na wanao na nyumba ya baba zako pamoja nawe mtachukua uovu wa patakatifu; wewe na wanao pamoja nawe mtauchukua ukuhani wenu.
2 Na ndugu zako nao, kabila ya Lawi, kabila ya baba yako, uwalete karibu pamoja nawe, ili waungwe nawe, na kukuhudumia; bali wewe na wanao pamoja nawe mtakuwa mbele ya hema ya ushahidi.
3 Nao watashika ulinzi kwa amri yako, na ulinzi wa Hema yote; lakini wasikaribie vyombo vya patakatifu, wala madhabahu, wasife, wao pamoja na ninyi.
4 Nao wataungwa nawe, na kuushika ulinzi wa hema ya kukutania, kwa ajili ya utumishi wote wa hema; na mgeni asiwakaribie ninyi.
5 Nanyi mtashika ulinzi wa patakatifu, na ulinzi wa madhabahu, isiwe ghadhabu juu ya wana wa Israeli tena.
6 Nami, tazama, nimewatwaa ndugu zenu Walawi miongoni mwa wana wa Israeli; kwenu ninyi watu hao ni kipawa alichopewa Bwana, waufanye utumishi wa hema ya kukutania.
7 Nawe na wanao pamoja nawe mtautunza ukuhani wenu, kwa ajili ya kila kitu cha madhabahu, na kwa ajili ya vile vilivyomo ndani ya pazia, nanyi mtatumika. Nawapeni ukuhani kuwa utumishi wa kipawa; na mgeni akaribiaye atauawa.
8 Kisha Bwana akamwambia Haruni, Tazama, nimekupa wewe ulinzi wa sadaka zangu za kuinuliwa, maana, vitu vyote vya hao wana wa Israeli vilivyowekwa wakfu; nimekupa wewe na wanao vitu hivyo kwa ajili ya kule kutiwa mafuta kwenu, kuwa haki yenu milele.
9 Vitu hivi vitakuwa vyako katika vile vilivyo vitakatifu sana, visiteketezwe motoni; matoleo yao yote, maana, kila sadaka yao ya unga, na kila sadaka yao ya dhambi, na kila sadaka yao ya hatia watakayonitolea, vitakuwa vitakatifu sana kwa ajili yako wewe na kwa wanao.
10 Utakula vitu hivyo kuwa ni vitu vitakatifu sana; kila mume atakula vitu hivyo; vitakuwa vitakatifu kwako wewe.
11 Tena kitu hiki ni chako; ile sadaka ya kuinuliwa ya kipawa chao, maana, sadaka za kutikiswa zote za wana wa Israeli; hizi nimekupa wewe, na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu milele; kila mtu katika nyumba yako aliye safi atakula katika hizo.
12 Yaliyo mazuri katika mafuta, na yaliyo mazuri ya mavuno ya zabibu, na ya mavuno ya nafaka, malimbuko yake watakayompa Bwana, amekupa wewe hayo.
13 Matunda ya kwanza yaivayo katika yote yaliyo katika nchi yao, watakayomletea Bwana, yatakuwa yako, kila mtu aliye safi katika nyumba yako atakula katika vitu hivyo.
14 Kila kitu kilichowekwa wakfu katika Israeli kitakuwa chako.
15 Kila kifunguacho tumbo, cha wenye mwili wote watakachomsongezea Bwana cha wanadamu na cha wanyama, ni chako; lakini mzaliwa wa kwanza wa binadamu, huna budi utamkomboa, na mzaliwa wa kwanza wa wanyama wasio safi utamkomboa.
16 Na hao watakaokombolewa katika wanyama hao, tangu aliyepata umri wa mwezi mmoja utamkomboa, kama utakavyohesabu kima chake, kwa fedha ya shekeli tano, kwa shekeli ya mahali patakatifu (nayo ni gera ishirini).
17 Lakini mzaliwa wa kwanza wa ng'ombe, au mzaliwa wa kwanza wa kondoo, au mzaliwa wa kwanza wa mbuzi, hutawakomboa hao; maana, ni watakatifu hao; utanyunyiza damu yao katika madhabahu, na kuyateketeza mafuta yao kuwa sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa moto, iwe harufu ya kupendeza.
18 Tena nyama yao itakuwa ni yako wewe, kama kile kidari cha kutikiswa, na kama mguu wa nyuma wa upande wa kuume, itakuwa yako.
19 Sadaka zote za kuinuliwa za vitu vitakatifu, wana wa Israeli wavisongezavyo kwa Bwana, nimekupa wewe na wanao na binti zako pamoja nawe, ni haki yenu ya milele; ni agano la chumvi la milele mbele za Bwana kwa ajili yako, na kizazi chako pamoja nawe.
20 Kisha Bwana akamwambia Haruni, Wewe hutakuwa na urithi katika nchi yao, wala hutakuwa na fungu lo lote kati yao; mimi ni fungu lako, na urithi wako, katika wana wa Israeli.
21 Na wana wa Lawi, nimewapa zaka yote katika Israeli kuwa urithi wao, badala ya huo utumishi wautumikao, maana, ni huo utumishi wa hema ya kukutania.
22 Mwanzo wa sasa wana wa Israeli wasikaribie hema ya kukutania, wasije wakachukua dhambi, nao wakafa.
23 Lakini Walawi watatumika utumishi wa hema ya kukutania, nao watauchukua uovu wao; hii itakuwa amri ya milele katika vizazi vyenu vyote, na kati ya wana wa Israeli hawatakuwa na urithi.
24 Kwa kuwa zaka ya wana wa Israeli, waisongezayo kuwa sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana, nimewapa Walawi kuwa urithi wao; kwa hiyo nimewaambia, ya kwamba, katika wana wa Israeli hawatakuwa na urithi uwao wote.
25 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
26 Tena utanena na Walawi, na kuwaambia, Hapo mtakapoitwaa zaka mkononi mwa wana wa Israeli niliyowapa ninyi kutoka kwao kuwa urithi wenu, ndipo mtakaposongeza sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana katika hiyo, iwe zaka katika hiyo zaka.
27 Na sadaka yenu ya kuinuliwa itahesabiwa kwenu, kama ndiyo nafaka ya sakafu ya kupuria, na kama kujaa kwake kinu cha kushindikia zabibu.
28 Hivyo ninyi nanyi mtasongeza sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana katika zaka zenu zote, mpokeazo mikononi mwa wana wa Israeli; kwa hiyo mtampa Haruni kuhani hiyo sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana.
29 Katika vipawa vyenu vyote mtasongeza kila sadaka ya kuinuliwa ya Bwana, ya wema wake wote, hiyo sehemu yake iliyowekwa takatifu.
30 Kwa ajili ya hayo utawaambia, Mtakapoinua humo hayo yaliyo mema, ndipo yatahesabiwa kuwa ya Walawi, kama kuongea kwake sakafu ya kupuria nafaka, na kama maongeo ya kinu cha kushindikia zabibu.
31 Nanyi mtakula hayo kila mahali, ninyi na watu wa nyumbani mwenu; kwa kuwa ni thawabu yenu badala ya utumishi wenu katika hema ya kukutania.
32 Nanyi hamtachukua dhambi kwa ajili yake, hapo mtakapokwisha kuinua humo hayo mema yake; lakini msivitie unajisi vile vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, ili msife.

Hesabu 19


1 Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
2 Hii ndiyo amri ya sheria Bwana aliyoagiza, akisema, Waambie wana wa Israeli wakuletee ng'ombe mke mwekundu asiye na kipaku, mkamilifu, ambaye hajatiwa nira bado;
3 nanyi mtamleta kwa Eleazari kuhani, naye atakwenda naye nje ya kambi, na mtu mmoja atamchinja mbele yake;
4 kisha Eleazari kuhani atatwaa katika damu yake kwa kidole chake, na kuinyunyiza damu yake kuelekea upande wa mbele wa hema ya kukutania mara saba;
5 kisha mtu mmoja atamchoma moto huyo ng'ombe mbele yake; ngozi yake, na nyama yake, na damu yake, pamoja na mavi yake pia atachoma moto;
6 kisha kuhani atatwaa mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, na kuvitupa katika huo moto unaomchoma ng'ombe.
7 Ndipo kuhani atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, kisha baadaye ataingia kambini, naye kuhani atakuwa najisi hata jioni.
8 Na huyo aliyemchoma moto ng'ombe atazifua nguo zake majini, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
9 Kisha mtu mmoja aliye safi atayazoa majivu ya huyo ng'ombe, na kuyaweka yawe akiba katika mahali safi nje ya kambi, nayo yatatunzwa kwa ajili ya mkutano wa wana wa israeli, kuwa ndiyo maji ya farakano; ni sadaka ya dhambi.
10 Na yeye ayazoaye majivu ya huyo ng'ombe atazifua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni; na jambo hili litakuwa amri ya milele, kwa wana wa Israeli, na wa mgeni akaaye kati yao.
11 Mtu agusaye maiti ye yote atakuwa najisi muda wa siku saba;
12 naye atajitakasa kwa yale maji siku ya tatu, na siku ya saba atakuwa safi; lakini kama hajitakasi siku ya tatu, ndipo na siku ya saba hatakuwa safi.
13 Mtu awaye yote agusaye maiti wa mtu aliyekufa, asijitakase, yuatia unajisi maskani ya Bwana; na mtu huyo atakatiliwa mbali na Israeli; maana, hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake, atakuwa najisi; unajisi wake ukali juu yake bado.
14 Hii ndiyo amri, mtu afapo ndani ya hema; kila mtu aingiaye ndani ya hema hiyo, na kila mtu aliye humo hemani, atakuwa najisi muda wa siku saba.
15 Na kila chombo kilicho wazi, kisichofungwa na kifuniko, ni najisi.
16 Kisha mtu ye yote huko nje shambani atakayemgusa mtu aliyeuawa kwa upanga, au mzoga, au mfupa wa mtu, au kaburi, atakuwa najisi muda wa siku saba.
17 Na kwa huyo aliye najisi watatwaa katika majivu ya kuchomwa kwake hiyo sadaka ya dhambi, na maji ya mtoni yatachanganywa na majivu katika chombo;
18 kisha mtu mmoja aliye safi atatwaa hisopo, na kuitia katika hayo maji naye atayanyunyiza juu ya hema, na juu ya vyombo vyote, na juu ya watu waliokuwapo, na juu yake yeye aliyeugusa mfupa, au mtu aliyeuawa, au mzoga, au kaburi;
19 na yule aliye safi atamnyunyiza huyo aliye najisi siku ya tatu, na siku ya saba; na katika siku ya saba atamtakasa; naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa safi jioni.
20 Lakini mtu atakayekuwa najisi, naye hataki kujitakasa, mtu huyo atakatiliwa mbali katika mkutano, kwa sababu amepatia unajisi mahali patakatifu pa Bwana; hayo maji ya farakano hayakunyunyizwa juu yake; yeye yu najisi.
21 Nayo itakuwa amri ya sikuzote kwao; na yeye anyunyizaye maji ya farakano atazifua nguo zake; naye ayagusaye hayo maji ya farakano atakuwa najisi hata jioni.
22 Na kitu cho chote atakachokigusa mtu aliye najisi kitakuwa najisi; na mtu atakayekigusa kitu hicho atakuwa najisi hata jioni.

Hesabu 20


1 Kisha wana wa Israeli, mkutano wote, wakaingia bara ya Sini, katika mwezi wa kwanza, watu wakakaa Kadeshi; Miriamu akafa huko, akazikwa huko.
2 Na hapo hapakuwa na maji kwa ule mkutano; wakajikusanya juu ya Musa na juu ya Haruni.
3 Watu wakashindana na Musa, wakanena, wakisema, Ingalikuwa heri kama tungalikufa wakati ule ndugu zetu walipokufa mbele za Bwana!
4 Mbona mmewaleta kusanyiko la Bwana hata jangwa hili ili tufe huku, sisi na wanyama wetu?
5 Na mbona mmetupandisha kutoka Misri ili kutuleta hata mahali hapa pabaya? Si mahali pa mbegu, wala tini, wala mizabibu, wala makomamanga; wala hapana maji ya kunywa.
6 Musa na Haruni wakatoka pale palipokuwa mkutano, wakaenda hata mlangoni pa hema ya kukutania, wakaanguka kifudifudi; utukufu wa Bwana ukawatokea.
7 Bwana akasema na Musa, akinena,
8 Twaa ile fimbo, ukawakusanye mkutano, wewe na Haruni ndugu yako, ukauambie mwamba mbele ya macho yao utoe maji yake, nawe utawatokezea maji katika mwamba, na hivyo utawanywesha maji mkutano na wanyama wao.
9 Musa akaitwaa hiyo fimbo kutoka mbele za Bwana kama alivyomwamuru.
10 Musa na Haruni wakawakusanya kusanyiko mbele ya mwamba, akawaambia, Sikieni sasa, enyi waasi; je! Tuwatokezee maji katika mwamba huu?
11 Musa akainua mkono wake akaupiga ule mwamba kwa fimbo yake mara mbili; maji yakatoka mengi, mkutano wakanywa na wanyama wao pia.
12 Bwana akamwambia Musa na Haruni, Kwa kuwa hamkuniamini mimi, ili kunistahi mbele ya macho ya wana wa Israeli, basi kwa sababu hiyo, hamtawaingiza kusanyiko hili katika ile nchi niliyowapa.
13 Maji haya ni maji ya Meriba; kwa sababu wana wa Israeli waliteta na Bwana, naye alijionyesha kuwa mtakatifu kati yao.
14 Kisha Musa akatuma wajumbe kutoka Kadeshi wamwendee mfalme wa Edomu, na kusema, Ndugu yako Israeli asema, Wewe wazijua taabu zote zilizotupata;
15 jinsi baba zetu walivyotelemkia Misri, nasi tulikaa Misri muda mwingi, nao Wamisri walitutenda vibaya sana, na baba zetu pia;
16 tena tulipomlilia Bwana, akatusikiza sauti yetu, akamtuma malaika, na kututoa tutoke Misri; nasi tupo hapa Kadeshi, mji wa mpakani mwako mwa mwisho;
17 tafadhali utupe ruhusa tupite katika nchi yako; hatutapita katika mashamba, wala katika mashamba ya mizabibu, wala hatutakunywa maji ya visimani; tutaifuata njia kuu ya mfalme, tusigeuke kwenda upande wa kuume, wala upande wa kushoto, hata tutakapopita mpaka wako.
18 Edomu akamwambia, Hutapita katika nchi yangu, nisije nikakutokea kupigana nawe kwa upanga.
19 Wana wa Israeli wakamwambia, Tutakwea kwa njia kuu; tena kama tukinywa maji yako, mimi na wanyama wangu wa mifugo, ndipo nitakulipa thamani yake; nipe ruhusa nipite kwa miguu yangu wala sitaki neno lingine lo lote.
20 Akamwambia, Hutapita katika nchi yangu. Kisha Edomu akamtokea ili kupigana naye, na watu wengi, na kwa mkono wa nguvu.
21 Basi hivyo Edomu akakataa kumpa Israeli ruhusa kupita katika mipaka yake; kwa hivyo Israeli akageuka na kumwacha.
22 Kisha wakasafiri kutoka Kadeshi; wana wa Israeli, mkutano mzima, wakafikilia mlima wa Hori.
23 Bwana akanena na Musa na Haruni katika mlima wa Hori, karibu na mpaka wa nchi ya Edomu, akawaambia,
24 Haruni atakusanywa awe pamoja na watu wake; kwa kuwa hataingia katika nchi niliyowapa wana wa Israeli, kwa sababu mliasi kinyume cha neno langu hapo penye maji ya Meriba.
25 Uwatwae Haruni na mwanawe Eleazari uwalete juu ya mlima wa Hori;
26 umvue Haruni mavazi yake, ukamvike Eleazari mwanawe mavazi hayo; kisha Haruni atakusanywa kwa watu wake, naye atakufa huko.
27 Musa akafanya kama Bwana alivyomwagiza; wakakwea katika mlima wa Hori mbele ya macho ya mkutano wote.
28 Kisha Musa akamvua Haruni mavazi yake, akamvika mwanawe Eleazari mavazi hayo; Haruni akafa huko katika kilele cha mlima; Musa na Eleazari wakatelemka mlimani.
29 Na mkutano wote ulipoona ya kuwa Haruni amekufa, wakamwombolea Haruni muda wa siku thelathini, maana, nyumba yote ya Israeli ikamwombolea.

Hesabu 21


1 Na Mkanaani, mfalme wa Aradi, aliyeketi upande wa Negebu, alisikia habari ya kuwa Israeli alikuja kwa njia ya Atharimu; basi akapigana na Israeli, na watu kadha wa kadha miongoni mwao akawateka mateka.
2 Basi Israeli akaweka nadhiri kwa Bwana akasema, Kama wewe utawatia watu hawa mikononi mwangu kweli ndipo mimi nitaiharibu miji yao kabisa.
3 Bwana akasikiza sauti ya Israeli, akawatia Wakanaani mikononi mwao; nao wakawaharibu wao na miji yao kabisa; na jina la mahali hapo likaitwa Horma.
4 Wakasafiri kutoka mlima wa Hori kwa njia ya Bahari ya Shamu; ili kuizunguka nchi ya Edomu, watu wakafa moyo kwa sababu ya ile njia.
5 Watu wakamnung'unikia Mungu, na Musa, Mbona mmetupandisha huku kutoka nchi ya Misri, ili tufe jangwani? Maana hapana chakula, wala hapana maji, na roho zetu zinakinai chakula hiki dhaifu.
6 Bwana akatuma nyoka za moto kati ya watu, wakawauma, watu wengi wakafa.
7 Watu wakamwendea Musa, wakasema, Tumefanya dhambi kwa sababu tumemnung'unikia Mungu, na wewe; utuombee kwa Bwana, atuondolee nyoka hawa. Basi Musa akawaombea watu.
8 Bwana akamwambia Musa, Jifanyie nyoka ya shaba, ukaiweke juu ya mti, na itakuwa kila mtu aliyeumwa, aitazamapo ataishi.
9 Musa akafanya nyoka ya shaba, akaiweka juu ya mti, hata ikiwa nyoka amemwuma mtu, alipoitazama ile nyoka ya shaba, akaishi.
10 Kisha wana wa Israeli wakasafiri, wakapanga marago Obothi.
11 Wakasafiri kutoka Obothi, wakapanga Iye-abarimu, katika jangwa iliyoelekea Moabu, upande wa maawio ya jua.
12 Kutoka huko wakasafiri, wakapanga katika bonde la Zeredi.
13 Kutoka huko wakasafiri, wakapanga upande wa pili wa Arnoni, ulio jangwani, utokao katika mpaka wa Waamori; maana, Arnoni ndio mpaka wa Moabu, kati ya Moabu na Waamori.
14 Kwa hiyo imesemwa katika chuo cha Vita vya Bwana, Wahebu katika Sufa, Na bonde za Arnoni,
15 Na matelemko ya hizo bonde Kwenye kutelemkia maskani ya Ari, Na kutegemea mpaka wa Moabu.
16 Kutoka huko wakasafiri kwenda Beeri; ni kisima ambacho Bwana alimwambia Musa, Uwakutanishe watu, nami nitawapa maji.
17 Ndipo Israeli wakaimba wimbo huu; Bubujika Ee kisima; kiimbieni;
18 Kisima walichokichimba wakuu, Ambacho wakuu wa watu wakakifukua, Kwa fimbo za enzi, kwa fimbo zao.
19 na kutoka Matana wakaenda Nahalieli; na kutoka Nahalieli wakaenda Bamothi;
20 na kutoka Bamothi wakaenda bondeni kwenye konde la Moabu, hata kilele cha Pisga, kielekeacho chini jangwani.
21 Kisha Israeli akatuma wajumbe kumwendea Sihoni mfalme wa Waamori, na kusema,
22 Nipe ruhusa nipite katika nchi yako; hatutageuka kando kwenda mashambani, wala kuingia katika mashamba ya mizabibu hatutakunywa maji ya visimani; tutakwenda kwa njia kuu ya mfalme, hata tutakapokuwa tumepita mpaka wako.
23 Lakini Sihoni hakukubali kumwacha Israeli kupita katika mpaka wake; bali Sihoni akawakutanisha watu wake wote, akatoka aende kupigana na Israeli jangwani, akafika mpaka Yahasa; akapigana na Israeli.
24 Israeli wakampiga kwa makali ya upanga, na kuimiliki nchi yake, tangu mto wa Arnoni hata mto wa Yaboki, mpaka nchi ya wana wa Amoni; kwa kuwa mpaka wa wana wa Amoni ulikuwa una nguvu.
25 Basi Israeli wakaitwaa miji hiyo yote; Israeli wakakaa katika miji yote ya Waamori, katika Heshboni, na miji yake yote.
26 Kwa kuwa Heshboni ulikuwa ni mji wa Sihoni mfalme wa Waamori, aliyekuwa akipigana na mfalme wa Moabu wa mbele, na kumpokonya nchi yake yote mkononi mwake, mpaka mto wa Arnoni.
27 Kwa hiyo, hao wanenao kwa mithali wasema, Njoni Heshboni, Mji wa Sihoni na ujengwe na kuthibitishwa;
28 Maana, moto umetoka Heshboni, Umekuwa Ari ya Moabu, Mwali wa moto umetoka mji wa Sihoni; Wakuu wa mahali palipoinuka Arnoni
29 Ole wako Moabu! Umeangamia, enyi watu wa Kemoshi; Amewatoa wanawe kuwa wakimbizi, Na binti zake waende utumwani, Wamwendee Sihoni mfalme wa Waamori.
30 Tumewapigia mishale; Heshboni umepotea mpaka Diboni, Nasi tumeharibu mpaka Nofa, Ifikiliayo Medeba.
31 Basi hivyo Israeli akaketi katika nchi ya Waamori.
32 Kisha Musa akapeleka watu ili kupeleleza Yazeri, nao wakaitwaa miji yake, wakawafukuza Waamori waliokuwamo.
33 Kisha wakageuka na kukwea kwa njia ya Bashani; na Ogu mfalme wa Bashani akaondoka apigane nao huko Edrei, yeye na watu wake wote.
34 Bwana akamwambia Musa, Usimche; kwa kuwa nimekwisha mtia mkononi mwako, na watu wake wote, na nchi yake; nawe utamtenda kama ulivyomtenda Sihoni mfalme wa Waamori, aliyeketi Heshboni.
35 Basi wakampiga, na wanawe, na watu wake wote, hata wasisaze kwake mtu ye yote; nao wakaimiliki nchi yake.

Hesabu 22


1 Kisha wana wa Israeli wakasafiri na kupanga katika nchi tambarare za Moabu ng'ambo ya pili ya Yordani karibu ya Yeriko.
2 Na Balaki mwana wa Sipori akaona mambo yote ambayo Israeli wamewatendea Waamori.
3 Moabu akawaogopa hao watu sana, kwa kuwa walikuwa wengi; Moabu akafadhaika kwa sababu ya wana wa Israeli.
4 Moabu akawaambia wazee wa Midiani, Sasa jeshi hili la watu litaramba vitu vyote vinavyotuzunguka, kama vile ng'ombe arambavyo majani ya mashamba. Na Balaki, mwana wa Sipori, alikuwa mfalme wa Moabu zamani zile.
5 Basi akatuma wajumbe kwa Balaamu mwana wa Beori, hata Pethori, ulio kando ya Mto, mpaka nchi ya wana wa watu wake, kwenda kumwita, akisema, Tazama, kuna watu waliotoka Misri; tazama, wanaufunika uso wa nchi, tena wanakaa kunikabili mimi.
6 Basi, njoo wewe, nakusihi unilaanie watu hawa; maana wana nguvu kunishinda mimi. Labda nitawaweza, tupate kuwapiga, niwafukuze watoke katika nchi yangu, kwa maana najua ya kuwa yeye umbarikiye hubarikiwa, na yeye umlaaniye hulaaniwa.
7 Wazee wa Moabu, na wazee wa Midiani, wakaenda, wakichukua ujira wa uganga mikononi mwao; wakamfikilia Balaamu, wakamwambia maneno ya Balaki.
8 Akawaambia, Kaeni hapa usiku huu, nami nitawaletea jawabu kama Bwana atakavyoniambia; wakuu wa Moabu wakakaa na Balaamu.
9 Mungu akamjia Balaamu, akasema, Ni watu gani hawa ulio nao pamoja nawe?
10 Balaamu akamwambia Mungu, Balaki mwana wa Sipori, mfalme wa Moabu, amewatuma kwangu, akisema,
11 Tazama, kuna watu waliotoka Misri, wanaufunika uso wa nchi; basi njoo unilaanie watu hawa; labda nitaweza kupigana nao, na kuwafukuza.
12 Mungu akamwambia Balaamu, Usiende pamoja nao; wala usiwalaani watu hawa, maana wamebarikiwa.
13 Balaamu akaondoka asubuhi akawaambia wakuu wa Balaki, Enendeni zenu hata nchi yenu; kwa maana Bwana amekataa kunipa ruhusa niende pamoja nanyi.
14 Wakuu wakaondoka wakaenda kwa Balaki, wakasema, Balaamu, anakataa kuja pamoja nasi.
15 Basi Balaki akatuma wakuu mara ya pili, wengi zaidi, wenye cheo wakubwa kuliko wale wa kwanza.
16 Wakamfikilia Balaamu, wakamwambia, Balaki mwana wa Sipori asema hivi, Nakusihi, neno lo lote lisikuzuie usinijie;
17 maana nitakufanyizia heshima nyingi sana, na neno lo lote utakaloniomba nitalitenda; basi njoo, nakusihi, unilaanie watu hawa.
18 Balaamu akajibu akawaambia watumishi wa Balaki, Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la Bwana, Mungu wangu, kulipunguza au kuliongeza.
19 Basi sasa nawasihi, kaeni hapa tena usiku huu, nipate kujua Bwana atakaloniambia zaidi.
20 Mungu akamjia Balaamu usiku, akamwambia, Kwa kuwa watu hawa wamekuja kukuita, enenda pamoja nao; lakini neno lile nitakalokuambia ndilo utakalolitenda, basi.
21 Balaamu akaondoka asubuhi, akatandika punda wake, akaenda pamoja na wakuu wa Moabu.
22 Hasira ya Mungu ikawaka kwa sababu alikwenda; malaika wa Bwana akajiweka njiani, ili kumpinga. Basi alikuwa amepanda punda wake, na watumishi wake wawili walikuwa pamoja naye.
23 Na yule punda akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, na upanga wake mkononi mwake amekwisha kuufuta; punda akageuka upande ili kuiacha njia, akaingia shambani. Balaamu akampiga punda ili kumrejeza njiani.
24 Kisha malaika wa Bwana akasimama mahali penye bonde, katikati ya mashamba ya mizabibu, tena penye kitalu upande huu na kitalu upande huu.
25 Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajisonga ukutani, akamseta Balaamu mguu wake, basi akampiga mara ya pili.
26 Malaika wa Bwana akaendelea mbele akasimama mahali pembamba sana, hapakuwa na nafasi ya kugeukia mkono wa kuume, wala mkono wa kushoto.
27 Yule punda akamwona malaika wa Bwana, akajilaza chini ya Balaamu; hasira yake Balaamu ikawaka, akampiga punda kwa fimbo yake.
28 Bwana akakifunua kinywa cha yule punda, naye akamwambia Balaamu, Nimekutenda nini, hata ukanipiga mara tatu hizi?
29 Balaamu akamwambia punda; Kwa sababu umenidhihaki; laiti ningekuwa na upanga mkononi mwangu ningekuua sasa hivi.
30 Yule punda akamwambia Balaamu, Je! Mimi si punda wako, nawe umenipanda maisha yako yote hata leo? Nimezoea kukutenda hayo? Akasema, La!
31 Ndipo Bwana akafunua macho ya Balaamu akamwona malaika wa Bwana amesimama njiani, ana upanga mkononi mwake, umekwisha kufutwa naye akainama kichwa, akaanguka kifudifudi.
32 Malaika wa Bwana akamwambia, Mbona umempiga punda wako mara tatu hizi? Tazama mimi nimekuja ili kukupinga, kwa sababu njia yako imepotoka mbele zangu,
33 punda akaniona, akageuka upande mbele zangu mara tatu hizi; kama asingejiepusha nami, bila shaka ningalikuua wewe, nikamwacha yeye hai.
34 Balaamu akamwambia malaika wa Bwana, Nimefanya dhambi; maana sikujua ya kuwa wewe umesimama njiani ili kunipinga; basi sasa, ikiwa umechukizwa, nitarudi tena.
35 Malaika wa Bwana akamwambia Balaamu Enenda pamoja na watu hawa, lakini neno lile nitakalokuambia, ndilo utakalosema. Basi Balaamu akaenda pamoja na wakuu wa Balaki.
36 Balaki aliposikia ya kuwa Balaamu amefika, akatoka kwenda kumlaki, mpaka Mji wa Moabu, ulioko katika mpaka wa Arnoni, ulioko katika upande wa mwisho wa mpaka huo.
37 Balaki akamwambia Balaamu, Je! Mimi sikutuma watu kwako kwa bidii ili kukuita? Mbona hukunijia? Je! Siwezi mimi kukufanyizia heshima nyingi?
38 Balaamu akamwambia Balaki, Tazama, nimekujia. Je! Mimi sasa nina uwezo wo wote kusema neno lo lote? Neno lile Mungu atakalolitia kinywani mwangu, ndilo nitakalolisema.
39 Balaamu akaenda pamoja na Balaki wakafika Kiriath-husothi.
40 Balaki akachinja ng'ombe, na kondoo, akampelekea Balaamu na wale wakuu waliokuwa pamoja naye.
41 Ikawa asubuhi Balaki akamchukua Balaamu, akampandisha hata mahali pa juu pa Baali; na kutoka huko akawaona watu, hata pande zao za mwisho.

Hesabu 23


1 Balaamu akamwambia Balaki, Nijengee hapa madhabahu saba, ukaniandalie hapa ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba.
2 Balaki akafanya kama Balaamu alivyonena. Balaki na Balaamu wakatoa sadaka, ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.
3 Balaamu akamwambia Balaki, Simama karibu na sadaka yako, nami nitakwenda, labda Bwana atakuja kuonana nami; na lo lote atakalonionyesha nitakuambia. Akaenda hata mahali peupe juu ya kilima.
4 Mungu akakutana na Balaamu; naye Balaamu akamwambia, Nimetengeneza madhabahu saba, nami nimetoa sadaka ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.
5 Bwana akatia neno katika kinywa chake Balaamu, akasema, Umrudie Balaki; ukaseme maneno haya.
6 Akarudi kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, yeye na wakuu wote wa Moabu pamoja naye.
7 Akatunga mithali yake, akasema, Balaki amenileta kutoka Aramu, Mfalme wa Moabu kutoka milima ya mashariki, Njoo! Unilaanie Yakobo, Njoo! Unishutumie Israeli.
8 Nimlaanije, yeye ambaye Mungu hakumlaani? Nimshutumuje, yeye ambaye Bwana hakumshutumu?
9 Kutoka kilele cha majabali namwona; Na kutoka milimani namtazama; Angalia, ni watu wakaao peke yao, Wala hawatahesabiwa pamoja na mataifa.
10 Ni nani awezaye kufanya idadi ya mavumbi ya Yakobo, Au kuhesabu robo ya Israeli? Na nife kifo chake mwenye haki, Na mwisho wangu uwe mfano wa mwisho wake.
11 Balaki akamwambia Balaamu, Umenitendea nini? Nimekuleta ili Uwalaani adui zangu, na tazama, umewabariki kabisa kabisa.
12 Naye akajibu, akasema, Je! Hainipasi kuangalia, niseme neno lile Bwana atialo kinywani mwangu?
13 Balaki akamwambia, Haya! Njoo, tafadhali, hata mahali pengine, na kutoka huko utaweza kuwaona; utaona upande wa mwisho wao tu, wala hutawaona wote, ukanilaanie hao kutoka huko.
14 Akamchukua mpaka shamba la Sofimu, hata kilele cha Pisga, akajenga madhabahu saba, akatoa sadaka ng'ombe mume mmoja na kondoo mume mmoja juu ya kila madhabahu.
15 Akamwambia Balaki, Simama hapa karibu na sadaka yako ya kuteketezwa, nami nitaonana na Bwana kule.
16 Bwana akaonana na Balaamu akatia neno kinywani mwake, akasema, Umrudie Balaki, ukaseme hivi.
17 Akafika kwake, na tazama, amesimama karibu na sadaka yake ya kuteketezwa, na wakuu wa Moabu pamoja naye. Balaki akamwambia, Bwana amenena nini?
18 Naye akatunga mithali yake, akasema, Ondoka Balaki, ukasikilize; Nisikilize, Ee mwana wa Sipori;
19 Mungu si mtu, aseme uongo; Wala si mwanadamu, ajute; Iwapo amesema, hatalitenda? Iwapo amenena, hatalifikiliza?
20 Tazama, nimepewa amri kubariki, Yeye amebariki, nami siwezi kulitangua.
21 Hakutazama uovu katika Yakobo, Wala hakuona ukaidi katika Israeli. Bwana, Mungu wake, yu pamoja naye, Na sauti kuu ya mfalme i katikati yao.
22 Mungu amewaleta kutoka Misri, Naye ana nguvu kama nguvu za nyati.
23 Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli. Sasa habari za Yakobo na Israeli zitasemwa, Ni mambo gani aliyoyatenda Mungu!
24 Tazama, watu hawa wanaondoka kama simba mke, Na kama simba anajiinua nafsi yake, Hatalala hata atakapokula mawindo, Na kunywa damu yao waliouawa.
25 Balaki akamwambia Balaamu, Basi usiwalaani kabisa, wala usiwabariki kabisa.
26 Lakini Balaamu akajibu akamwambia Balaki, Je! Sikukuambia ya kwamba, Kila neno Bwana atakalolisema sina budi kulitenda?
27 Kisha Balaki akamwambia Balaamu, Haya, njoo sasa, nikupeleke mahali pengine; labda Mungu ataridhia kwamba unilaanie watu hao huko.
28 Basi Balaki akamchukua Balaamu akaenda naye mpaka kilele cha mlima Peori, mahali paelekeapo upande wa nyika iliyo chini yake.
29 Balaamu akamwambia Balaki, Haya, unijengee hapa madhabahu saba, kisha uniandalie ng'ombe waume saba, na kondoo waume saba.
30 Basi Balaki akafanya kama Balaamu alivyosema, akasongeza sadaka ng'ombe mume na kondoo mume juu ya kila madhabahu.

Hesabu 24


1 Basi Balaamu alipoona ya kuwa ilimpendeza Bwana kuwabariki Israeli, hakwenda, kama hapo kwanza, ili kutafuta uchawi, bali alielekeza uso wake jangwani.
2 Balaamu akainua macho yake akawaona Israeli wamekaa kabila kabila; roho ya Mungu ikamjia.
3 Akatunga mithali yake, akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema;
4 Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho;
5 Mahema yako ni mazuri namna gani, Ee Yakobo, Maskani zako, Ee Israeli!
6 Mfano wa bonde zimetandwa, Mfano wa bustani kando ya mto, Mfano wa mishubiri aliyoipanda Bwana, Mfano wa mierezi kando ya maji.
7 Maji yatafurika katika ndoo zake, Na mbegu zake zitakuwa katika maji mengi. Na mfalme wake ataadhimishwa kuliko Agagi, Na ufalme wake utatukuzwa.
8 Mungu amemleta kutoka Misri, Ana nguvu mfano wa nguvu za nyati; Atawameza mataifa walio adui zake, Ataivunja mifupa yao vipande vipande. Atawachoma kwa mishale yake.
9 Aliinama, akalala mfano wa simba, Na kama simba mke; ni nani atakayemstusha? Na abarikiwe kila akubarikiye, Na alaaniwe kila akulaaniye.
10 Hasira ya Balaki ikawaka juu ya Balaamu akayapiga makofi; Balaki akamwambia Balaamu, Nalikuita ili unilaanie adui zangu, na tazama, umewabariki kabisa mara tatu hizi.
11 Basi sasa kimbilia mahali pako; naliazimu kukuheshimu sana; lakini, tazama, Bwana amekuzuilia heshima.
12 Balaamu akamwambia Balaki, Je! Sikuwaambia wajumbe wako ulionipelekea, nikisema,
13 Kama Balaki angenipa nyumba yake imejaa fedha na dhahabu, siwezi kupita mpaka wa neno la Bwana, kutenda neno jema, wala neno baya, kwa nia yangu mwenyewe; Bwana atakalolinena ndilo nitakalolinena mimi.
14 Basi sasa, tazama, ninakwenda kwa watu wangu; haya, nitakuarifu mambo ambayo watu hawa watakayowatenda watu wako siku za mwisho.
15 Akatunga mithali yake akasema, Balaamu mwana wa Beori asema, Yule mtu aliyefumbwa macho asema,
16 Asema, yeye asikiaye maneno ya Mungu, Na kuyajua maarifa yake Aliye Juu. Yeye aonaye maono ya Mwenyezi, Akianguka kifudifudi, amefumbuliwa macho,
17 Namwona, lakini si sasa; Namtazama, lakini si karibu; Nyota itatokea katika Yakobo Na fimbo ya enzi itainuka katika Israeli; Nayo itazipiga-piga pembe za Moabu, Na kuwavunja-vunja wana wote wa ghasia.
18 Na Edomu itakuwa milki Seiri pia itakuwa milki, waliokuwa adui zake; Israeli watakapotenda kwa ushujaa.
19 Mwenye kutawala atakuja toka Yakobo, Atawaangamiza watakaobaki mjini.
20 Kisha akamwangalia Amaleki, akatunga mithali yake, akasema, Amaleki alikuwa ni wa kwanza wa mataifa; Lakini mwisho wake atafikilia uharibifu.
21 Kisha akamwangalia Mkeni, akatunga mithali yake, akasema, Makao yako yana nguvu, Na kitundu chako kimewekwa katika jabali.
22 Pamoja na haya Wakeni wataangamizwa, Hata Ashuru atakapokuchukua mateka.
23 Akatunga mithali yake akasema, Ole wao! Ni nani atakayepona, Mungu atakapofanya haya?
24 Lakini merikebu zitakuja kutoka pwani kwa Kitimu, Nazo zitamtaabisha Ashuru, na Eberi zitamtaabisha, Yeye naye atafikilia uharibifu.
25 Basi Balaamu akainuka, akaondoka na kurudi mahali pake; Balaki naye akaenda zake.

Hesabu 25


1 Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu;
2 kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao.
3 Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli.
4 Kisha Bwana akamwambia Musa, Watwae wakuu wote wa hao watu, ukamtungikie Bwana watu hao mbele ya jua, ili kwamba hizo hasira kali za Bwana ziwaondokee Israeli.
5 Basi Musa akawaambia waamuzi wa Israeli, Waueni kila mtu watu wake waliojiungamanisha na Baal-peori.
6 Na tazama, mtu mmoja miongoni mwa wana wa Israeli akaja na kuwaletea nduguze mwanamke Mmidiani mbele ya macho ya Musa, na mbele ya macho ya mkutano wote wa wana wa Israeli, hapo walipokuwa walia mbele ya mlango wa hema ya kukutania.
7 Naye Finehasi mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, alipoona jambo hilo, akaondoka hapo katikati ya mkutano, akashika fumo mkononi mwake;
8 akamwandama huyo mtu wa Israeli na kuingia ndani ya hema nyuma yake, naye akawachoma wote wawili kwa fumo lake, yule mume wa Israeli na huyo mwanamke kati ya tumbo lake. Basi pigo likazuiwa kwao wana wa Israeli.
9 Nao waliokufa kwa hilo pigo walikuwa watu elfu ishirini na nne hesabu yao.
10 Kisha Bwana akanena na Musa, akamwambia,
11 Finehasi, mwana wa Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, amezigeuza hasira zangu zisiwe juu ya wana Wa Israeli, kwa kuwa alikuwa na wivu kati yao kwa wivu wangu mimi, hata nisiwaangamize wana wa Israeli katika wivu wangu.
12 Basi kwa hiyo, sema, Tazama, nampa yeye agano langu la amani;
13 tena kwake yeye, na kizazi chake baada yake, litakuwa agano la ukuhani wa milele; kwa sababu alikuwa na wivu kwa ajili ya Mungu wake, na kuwafanyia upatanisho wana wa Israeli.
14 Basi jina la Mwisraeli huyo aliyeuawa pamoja na yule mwanamke Mmidiani, aliitwa Zimri, mwana wa Salu, mkuu wa nyumba ya baba zake, katika kabila la Simeoni.
15 Na jina la huyo mwanamke Mmidiani aliyeuawa, aliitwa Kozbi, binti Suri; naye alikuwa kichwa cha watu wa nyumba ya baba zake huko Midiani
16 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
17 Wasumbue Wamidiani, na kuwapiga;
18 kwa sababu wao wawasumbua ninyi kwa hila zao, ambazo kwa hizo wamewadanganya ninyi katika jambo la Peori, na katika jambo la huyo Kozbi, binti wa mkuu wa Midiani, umbu lao, huyo aliyeuawa siku hiyo ya pigo katika jambo la Peori.

Hesabu 26


1 Ikawa baada ya hilo pigo, Bwana akanena na Musa na Eleazari, mwana wa Haruni kuhani, na kuwaambia,
2 Fanya jumla ya mkutano wote wa wana wa Israeli, tangu umri wa miaka ishirini, na zaidi, kwa nyumba za baba zao, hao wote katika Israeli wawezao kutoka kuenenda vitani.
3 Kisha Musa na Eleazari kuhani wakanena nao katika nchi tambarare za Moabu karibu na mto wa Yordani, huko Yeriko, wakawaambia,
4 Fanyeni jumla ya watu, tangu umri wa miaka ishirini, na zaidi; kama Bwana alivyomwagiza Musa na wana wa Israeli, hao waliotoka nchi ya Misri.
5 Reubeni mzaliwa wa kwanza wa Israeli, wana wa Reubeni; wa Hanoki, jamaa ya Wahanoki; na wa Palu, jamaa ya Wapalu;
6 na wa Hesroni, jamaa ya Wahesroni; na wa Karmi, jamaa ya Wakarmi.
7 Hizi ndizo jamaa za Wareubeni; na hao waliohesabiwa kwao walikuwa arobaini na tatu elfu na mia saba na thelathini.
8 Na wana wa Palu; Eliabu.
9 Na wana wa Eliabu; Nemueli, na Dathani, na Abiramu. Hawa ndio Dathani na Abiramu waliochaguliwa na mkutano, ambao walishindana na Musa na Haruni katika mkutano wa Kora, hapo waliposhindana na Bwana;
10 nchi ikafunua kinywa chake, na kuwameza pamoja na Kora, mkutano huo ulipokufa; wakati moto ulipowateketeza watu mia mbili na hamsini, nao wakawa ishara.
11 Pamoja na hayo, hao wana wa Kora hawakufa.
12 Na wana wa Simeoni kwa jamaa zao; wa Yemueli, jamaa ya Wayemueli; wa Yamini, jamaa ya Wayamini; na Yakini, jamaa ya Wayakini;
13 wa Sohari, jamaa ya Wasohari; wa Shauli, jamaa ya Washauli.
14 Hizi ndizo jamaa za Wasimeoni, watu ishirini na mbili elfu na mia mbili.
15 Na wana wa Gadi kwa jamaa zao; wa Sifoni, jamaa ya Wasifoni; wa Hagi, jamaa ya Wahagi; wa Shuni, jamaa ya Washuni;
16 wa Ezboni, jamaa ya Waezboni; wa Eri, jamaa ya Waeri;
17 wa Arodi, jamaa ya Waarodi; wa Areli, jamaa ya Waareli.
18 Hizi ndizo jamaa za wana wa Gadi kama waliohesabiwa kwao, arobaini elfu na mia tano.
19 Na wana wa Yuda, Eri na Onani; na hao Eri na Onani wakafa katika nchi ya Kanaani.
20 Na wana wa Yuda kwa jamaa zao; wa Shela, jamaa ya Washela; wa Peresi, jamaa ya Waperesi; wa Zera, jamaa ya Wazera.
21 Na wana wa Peresi walikuwa; wa Hesroni, jamaa ya Wahesroni; wa Hamuli, jamaa ya Wahamuli.
22 Hizi ndizo jamaa za Yuda kama waliohesabiwa kwao, sabini na sita elfu na mia tano.
23 Na wana wa Isakari kwa jamaa zao; wa Tola, jamaa ya Watola; wa Puva, jamaa ya Wapuva;
24 wa Yashubu, jamaa ya Wayashubu; wa Shimroni, jamaa ya Washimroni.
25 Hizi ndizo jamaa za Isakari kama waliohesabiwa kwao, sitini na nne elfu na mia tatu.
26 Na wana wa Zabuloni kwa jamaa zao; wa Seredi, jamaa ya Waseredi; wa Eloni, jamaa ya Waeloni; wa Yaleeli, jamaa ya Wayaleeli.
27 Hizi ndizo jamaa za Wazabuloni kama waliohesabiwa kwao, sitini elfu na mia tano.
28 Na wana wa Yusufu kwa jamaa zao; Manase na Efraimu.
29 Wana wa Manase; wa Makiri, jamaa ya Wamakiri; na Makiri akamzaa Gileadi; wa Gileadi, jamaa ya Wagileadi.
30 Hawa ndio wana wa Gileadi; wa Abiezeri, jamaa ya Waabiezeri; wa Heleki, jamaa ya Waheleki;
31 na wa Asrieli, jamaa ya Waasrieli; na wa Shekemu, jamaa ya Washekemu;
32 na wa Shemida, jamaa ya Washemida; na wa Heferi, jamaa ya Waheferi.
33 Na Selofehadi mwana wa Heferi hakuwa na wana waume, isipokuwa wa kike; na majina ya hao binti za Selofehadi ni haya, Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa.
34 Hizi ndizo jamaa za Manase; na waliohesabiwa kwao walikuwa ni hamsini na mbili elfu na mia saba.
35 Na wana wa Efraimu kwa jamaa zao; wa Shuthela, jamaa ya Washuthela; wa Beredi, jamaa ya Waberedi; wa Tahathi, jamaa ya Watahathi.
36 Na wana wa Shuthela ni hawa; wa Erani, jamaa ya Waerani.
37 Hizi ndizo jamaa za wana wa Efraimu kama waliohesabiwa kwao, thelathini na mbili elfu na mia tano. Hao ndio wana wa Yusufu kwa jamaa zao.
38 Na wana wa Benyamini kwa jamaa zao; wa Bela, jamaa ya Wabela; na wa Ashbeli, jamaa ya Waashbeli; wa Ahiramu, jamaa ya Waahiramu;
39 wa Shufamu, jamaa ya Washufamu; wa Hufamu, jamaa ya Wahufamu.
40 Na wana wa Bela walikuwa Ardi na Naamani; wa Ardi, jamaa ya Waardi; wa Naamani, jamaa ya Wanaamani.
41 Hao ndio wana wa Benyamini kwa jamaa zao; na waliohesabiwa kwao walikuwa arobaini na tano elfu na mia sita.
42 Na wana wa Dani ni hawa kwa jamaa zao; wa Shuhamu, jamaa ya Washuhamu. Hizi ndizo jamaa za Dani kwa jamaa zao.
43 Jamaa zote za Washuhamu, kama waliohesabiwa kwao, walikuwa sitini na nne elfu na mia nne.
44 Na wana wa Asheri kwa jamaa zao; wa Imna, jamaa ya Waimna; wa Ishvi jamaa ya Waishvi; wa Beria, jamaa ya Waberia.
45 Wa wana wa Beria; wa Heberi, jamaa ya Waheberi; wa Malkieli, jamaa ya Wamalkieli.
46 Na jina la binti wa Asheri aliitwa Sera.
47 Hizi ndizo jamaa za wana wa Asheri kama waliohesabiwa kwao, hamsini na tatu elfu na mia nne.
48 Na wana wa Naftali kwa jamaa zake; wa Yaseeli, jamaa ya Wayaseeli; na wa Guni, jamaa ya Waguni;
49 wa Yeseri, jamaa ya Wayeseri, wa Shilemu jamaa ya Washilemu.
50 Hizi ndizo jamaa za Naftali kwa jamaa zao; na waliohesabiwa kwao walikuwa arobaini na tano elfu na mia nne.
51 Hao ndio waliohesabiwa katika wana wa Israeli, mia sita na moja elfu, na mia saba na thelathini (601,730).
52 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
53 Watu hawa watagawanyiwa nchi hiyo iwe urithi wao, vile vile kama hesabu ya majina yao ilivyo.
54 Hao waliozidi hesabu yao utawapa urithi zaidi, na hao waliopunguka hesabu yao, utawapa urithi kama upungufu wao; kila mtu kama watu wake walivyohesabiwa, ndivyo atakavyopewa urithi wake.
55 Lakini nchi itagawanywa kwa kura; kwa majina ya kabila za baba zao, ndivyo watakavyopata urithi.
56 Kama kura itakavyokuwa, ndivyo urithi wao utakavyogawanywa kati yao, hao wengi na hao wachache.
57 Na hao waliohesabiwa katika Walawi kwa jamaa zao ni hawa; wa Gershoni, jamaa ya Wagershoni; na wa Kohathi, jamaa ya Wakohathi; na wa Merari, jamaa ya Wamerari.
58 Hizi ndizo jamaa za Lawi; jamaa ya Walibni, na jamaa ya Wahebroni, na jamaa ya Wamala, na jamaa ya Wamushi jamaa ya Wakora. Na Kohathi alimzaa Amramu.
59 Na jina la mke wa Amramu aliitwa Yokebedi, binti wa Lawi, ambaye alizaliwa kwake Lawi huko Misri; na huyo Yokebedi akamzalia Amramu Haruni, na Musa, na Miriamu umbu lao.
60 Tena kwake Haruni walizaliwa hawa, Nadabu, na Abihu, na Eleazari, na Ithamari.
61 Tena Nadabu na Abihu wakafa, hapo waliposongeza moto wa kigeni mbele za Bwana.
62 Na hao waliohesabiwa kwao walikuwa ishirini na tatu elfu, kila mwanamume tangu huyo aliyepata umri wa mwezi mmoja, na zaidi; kwa kuwa hawakuhesabiwa katika wana wa Israeli, kwa sababu hawakupewa urithi katika wana wa Israeli.
63 Hao ndio waliohesabiwa na Musa na Eleazari kuhani; ambao waliwahesabu wana wa Israeli katika nchi tambarare za Moabu, karibu na Yordani, hapo Yeriko.
64 Lakini katika watu hao hapakuwa na mtu hata mmoja wa wale waliohesabiwa na Musa na Haruni kuhani; waliowahesabu wana wa Israeli katika bara ya Sinai.
65 Kwa kuwa Bwana alisema juu yao, Hapana budi watakufa nyikani. Napo hapakusalia mtu mmoja miongoni mwao, isipokuwa Kalebu mwana wa Yefune, na Yoshua mwana wa Nuni.

Hesabu 27


1 Wakati huo wakakaribia hao binti za Selofehadi, mwana wa Heferi, mwana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, wa jamaa za Manase mwana wa Yusufu; na majina ya hao binti za Selofehadi ni haya; Mala, na Noa, na Hogla, na Milka, na Tirsa.
2 Nao wakasimama mbele ya Musa, na mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya wakuu, na mkutano wote, mlangoni pa hema ya kukutania, wakasema,
3 Babaetu alikufa nyikani, naye hakuwamo katika mkutano wa hao waliojikutanisha kinyume cha Bwana katika mkutano wa Kora; lakini akafa katika dhambi zake mwenyewe; naye alikuwa hana wana wa kiume.
4 Kwa nini basi jina la babaetu kufutwa katika jamaa zake kwa sababu alikuwa hana mwana wa kiume? Tupe sisi urithi pamoja na ndugu zake babaetu.
5 Basi Musa akaleta neno lao mbele ya Bwana
6 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
7 Hao binti za Selofehadi wananena lililo haki; kweli utawapa milki ya urithi pamoja na ndugu za baba yao; nawe utawapa urithi wa baba yao.
8 Kisha utanena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Mtu akifa, naye hana mwana wa kiume, ndipo utampa binti yake urithi wake.
9 Tena ikiwa hana binti, mtawapa nduguze urithi wake.
10 Na ikiwa hana ndugu, mtawapa ndugu za babaye huo urithi wake.
11 Tena ikiwa babaye hana ndugu, utampa huyo aliye karibu naye katika jamaa zake huo urithi wake, naye atakuwa nao; na neno hili litakuwa ni amri ya hukumu kwa wana wa Israeli, kama Bwana alivyomwagiza Musa.
12 Bwana akamwambia Musa, Panda wewe juu ya mlima huu wa Abarimu, uitazame nchi niliyowapa wana wa Israeli.
13 Na ukiisha kuiona, wewe nawe utakusanyika pamoja na baba zako, kama Haruni ndugu yako alivyokusanyika;
14 kwa sababu mliasi juu ya neno langu katika jangwa la Sini wakati wa mateto ya mkutano, wala hamkunistahi, hapo majini, mbele ya macho yao. (Maji hayo ndiyo maji ya Meriba ya Kadeshi katika jangwa la Sini.)
15 Musa akanena na Bwana akisema,
16 Bwana, Mungu wa roho za wenye mwili wote, na aweke mtu juu ya mkutano,
17 atakayetoka mbele yao, na kuingia mbele yao; atakayewaongoza watokapo, na kuwaleta ndani; ili mkutano wa Bwana wasiwe kama kondoo wasio na mchungaji.
18 Bwana akamwambia Musa, Mtwae Yoshua, mwana wa Nuni, mtu mwenye roho ndani yake, ukamwekee mkono wako;
19 kisha ukamweke mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote; ukampe mausia mbele ya macho yao.
20 Nawe utaweka juu yake sehemu ya heshima yako, ili mkutano wote wa wana wa Israeli wapate kutii.
21 Naye atasimama mbele ya Eleazari kuhani, naye atamwulizia kwa hukumu ya ile Urimu mbele za Bwana; kwa neno lake watatoka, na kwa neno lake wataingia; yeye na wana wa Israeli wote pamoja naye, mkutano wote pia.
22 Musa akafanya kama Bwana alivyomwamuru; akamtwaa Yoshua, akamweka mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wote;
23 kisha akaweka mikono yake juu yake, akampa mausia, kama Bwana alivyosema kwa mkono wa Musa.

Hesabu 28


1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Waagize hao wana wa Israeli, uwaambie, Matoleo yangu, chakula changu cha sadaka zangu zisongezwazo kwa moto, za harufu ya kupendeza kwangu mimi, mtaangalia kuzisongeza kwangu wakati wake upasao.
3 Nawe utawaambia, Hii ndiyo sadaka isongezwayo kwa moto mtakayomsongezea Bwana; wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu, wawili kila siku, wawe sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote.
4 Mwana-kondoo mmoja utamsongeza asubuhi, na mwana-kondoo wa pili utamsongeza jioni;
5 pamoja na sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na robo ya hini ya mafuta ya kupondwa.
6 Ni sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, iliyoamriwa huko katika mlima wa Sinai iwe harufu ya kupendeza, sadaka ya kusongezwa kwa Bwana kwa moto.
7 Na sadaka yake ya kinywaji itakuwa robo ya hini kwa mwana-kondoo mmoja; hiyo sadaka ya kinywaji, ya kileo, utammiminia Bwana katika mahali hapo patakatifu.
8 Na mwana-kondoo wa pili utamsongeza wakati wa jioni; kama ile sadaka ya unga iliyosongezwa asubuhi, na kama sadaka yake ya kinywaji, ndivyo utakavyoisongeza, ni sadaka ya kusongezwa kwa moto, ni harufu ya kupendeza kwa Bwana.
9 Tena katika siku ya Sabato watasongezwa wana-kondoo wawili, waume wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, pamoja na sehemu ya kumi mbili za efa za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, pamoja na sadaka yake ya kinywaji;
10 hii ndiyo sadaka ya kuteketezwa ya kila Sabato, zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.
11 Tena katika mianzo ya miezi yenu mtamsongezea Bwana sadaka ya kuteketezwa; nayo ni ng'ombe waume wadogo wawili, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, saba;
12 pamoja na sehemu ya kumi tatu za efa za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, kwa kila ng'ombe; na sehemu ya kumi mbili za unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, uliochanganywa na mafuta, kwa huyo kondoo mume mmoja;
13 na sehemu ya kumi moja ya unga mwembamba uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga kwa kila mwana-kondoo; kuwa sadaka ya kuteketezwa ya harufu ya kupendeza, ni sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.
14 Tena sadaka zake za vinywaji zitakuwa nusu ya hini ya divai kwa ng'ombe, na sehemu ya tatu ya hini kwa kondoo mume, na robo ya hini kwa mwana-kondoo; hii ndiyo sadaka ya kuteketezwa ya kila mwezi katika miezi yote ya mwaka.
15 Tena mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi kwa Bwana itasongezwa zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.
16 Tena, mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi, ni pasaka ya Bwana.
17 Siku ya kumi na tano ya mwezi huo patakuwa na sikukuu; mkate usiotiwa chachu utaliwa muda wa siku saba.
18 Siku ya kwanza patakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi;
19 lakini mtaisongeza sadaka kwa njia ya moto, sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana; ng'ombe waume wadogo wawili, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza saba; watakuwa wakamilifu kwenu;
20 pamoja na sadaka zake za unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta; mtasongeza sehemu ya kumi tatu kwa ng'ombe mmoja, na sehemu ya kumi mbili kwa kondoo mume;
21 na sehemu ya kumi moja utasongeza kwa kila mwana-kondoo, wale wana-kondoo saba;
22 tena mtasongeza mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.
23 Mtasongeza wanyama hao zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi, iliyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote.
24 Mtasongeza sadaka kwa mfano huu kila siku muda wa siku saba, chakula cha sadaka iliyosongezwa kwa moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana; itasongezwa zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, pamoja na sadaka yake ya kinywaji.
25 Na siku ya saba mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi.
26 Tena katika siku ya malimbuko, hapo mtakapomsongezea Bwana sadaka ya unga mpya katika sikukuu yenu ya majuma mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi;
27 lakini mtasongeza sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu ya kupendeza kwa Bwana; ng'ombe waume wadogo wawili, kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza saba;
28 pamoja na sadaka zake za unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, sehemu ya kumi tatu kwa kila ng'ombe, na sehemu ya kumi mbili kwa kondoo mume,
29 na sehemu ya kumi moja kwa kila mwana-kondoo, wa wale wana-kondoo saba;
30 na mbuzi mume mmoja, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.
31 Zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, mtasongeza wanyama hao (watakuwa wakamilifu kwenu), pamoja na sadaka zake za vinywaji.

Hesabu 29


1 Tena mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi, mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi; ni siku ya kupiga tarumbeta kwenu.
2 Nanyi mtasongeza sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu ya kupendeza kwa Bwana; ng'ombe mume mdogo mmoja, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu saba;
3 pamoja na sadaka yake ya unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, sehemu ya kumi tatu kwa ng'ombe, sehemu ya kumi mbili kwa kondoo mume,
4 na sehemu ya kumi moja kwa kila mwana-kondoo katika wale wana-kondoo saba;
5 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu;
6 zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya kuandama mwezi, na sadaka yake ya unga, na hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kama ilivyo amri yake, kuwa harufu ya kupendeza, ni sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa moto.
7 Tena siku ya kumi ya huo mwezi wa saba mtakuwa na kusanyiko takatifu; nanyi mtazitesa nafsi zenu, msifanye kazi yo yote ya utumishi
8 lakini mtamsongezea Bwana sadaka ya kuteketezwa, kuwa harufu ya kupendeza; ng'ombe mume mdogo mmoja, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza saba; watakuwa wakamilifu kwenu;
9 pamoja na sadaka zake za unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, sehemu ya kumi tatu kwa huyo ng'ombe, na sehemu ya kumi mbili kwa huyo kondoo,
10 na sehemu ya kumi moja kwa kila mwana-kondoo katika wale wana-kondoo saba;
11 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya dhambi ya upatanisho, na hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji.
12 Tena siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba mtakuwa na kusanyiko takatifu; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi, nanyi mtamfanyia Bwana sikukuu muda wa siku saba;
13 nanyi mtasongeza sadaka ya kuteketezwa, sadaka isongezwayo kwa moto, harufu ya kupendeza kwa Bwana; ng'ombe waume wadogo kumi na watatu, na kondoo waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza kumi na wanne; wote watakuwa wakamilifu;
14 pamoja na sadaka zake za unga, unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, sehemu ya kumi tatu kwa kila ng'ombe katika wale kumi na watatu na sehemu ya kumi mbili kwa kila kondoo katika hao kondoo waume wawili;
15 na sehemu ya kumi moja kwa kila mwana-kondoo katika wale wana-kondoo kumi na wanne;
16 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka yake ya kinywaji.
17 Tena siku ya pili mtasongeza ng'ombe waume wadogo kumi na wawili, na kondoo waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza kumi na wanne wakamilifu;
18 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama hesabu yao ilivyo, kwa kuandama hiyo amri;
19 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji.
20 Tena siku ya tatu mtasongeza ng'ombe waume kumi na mmoja, na kondoo waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu kumi na wanne;
21 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama hesabu yao ilivyo, kwa kuiandama amri;
22 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka yake ya kinywaji.
23 Tena siku ya nne mtasongeza ng'ombe waume kumi, na kondoo waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu kumi na wanne;
24 na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama hesabu yao ilivyo, kwa kuiandama amri;
25 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya sikuzote, na sadaka yake ya unga, na sadaka yake ya kinywaji.
26 Tena siku ya tano mtasongeza ng'ombe waume kenda, na kondoo Waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu kumi na wanne;
27 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama hesabu yao ilivyo, kwa kuiandama amri;
28 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya siku zote, na hiyo sadaka yake ya unga na sadaka yake ya kinywaji.
29 Tena siku ya sita mtasongeza ng'ombe waume wanane, na kondoo waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu kumi na wanne;
30 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama hesabu yao ilivyo, kwa kuiandama amri;
31 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya siku zote, na hiyo sadaka yake ya unga na sadaka yake ya kinywaji.
32 Tena siku ya saba mtasongeza ng'ombe waume saba, na kondoo waume wawili, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu kumi na wanne;
33 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa hao ng'ombe, na kwa hao kondoo, na kwa wale wana-kondoo, kama hesabu yao ilivyo, kwa kuiandama amri;
34 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya siku zote, na hiyo sadaka yake ya unga na sadaka yake ya kinywaji.
35 Tena siku ya nane mtakuwa na kusanyiko la makini sana; hamtafanya kazi yo yote ya utumishi;
36 lakini mtasongeza sadaka ya kuteketezwa, sadaka ya kusongezwa kwa moto, harufu ya kupendeza kwa Bwana; ng'ombe mume mmoja, na kondoo mume mmoja, na wana-kondoo waume wa mwaka wa kwanza wakamilifu saba;
37 pamoja na sadaka yake ya unga, na sadaka zake za vinywaji, kwa huyo ng'ombe, na kwa huyo kondoo mume, na kwa wale wana-kondoo, kama hesabu yao ilivyo, kwa kuiandama amri;
38 na mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi; zaidi ya hiyo sadaka ya kuteketezwa ya siku zote, na hiyo sadaka yake ya unga na sadaka yake ya kinywaji.
39 Sadaka hizo mtamsongezea Bwana katika sikukuu zenu zilizoamriwa, zaidi ya nadhiri zenu, na sadaka zenu za hiari, kuwa sadaka zenu za kuteketezwa, na sadaka zenu za unga, na sadaka zenu za vinywaji, na sadaka zenu za amani.
40 Naye Musa akawaambia wana wa Israeli vile vile kama hayo yote Bwana alivyomwagiza Musa.

Hesabu 30


1 Kisha Musa akanena na wale vichwa vya kabila za wana wa Israeli, na kuwaambia, Neno hili ndilo aliloliagiza Bwana.
2 Mtu atakapomwekea Bwana nadhiri, au, atakapoapa kiapo ili kufunga nafsi yake kwa kifungo, asilitangue neno lake; atafanya sawasawa na hayo yote yamtokayo kinywani mwake.
3 Tena mtu mke atakapomwekea Bwana nadhiri, na kufunga nafsi yake kwa kifungo, naye aketi katika nyumba ya babaye, katika ujana wake;
4 babaye naye akasikia nadhiri yake, na kile kifungo chake alichofungia nafsi yake, na babaye akamnyamazia; ndipo nadhiri zake zote zitathibitika, na kila kifungo alichofungia nafsi yake kitathibitika.
5 Lakini kama huyo babaye akimkataza siku hiyo aliyosikia; nadhiri zake ziwazo zote, wala vifungo vyake alivyoifungia nafsi yake havitathibitika; na Bwana atamsamehe, kwa kuwa babaye alimkataza.
6 Tena kama amekwisha kuolewa na mume, wakati huo wa nadhiri zake, au wa neno hilo alilolitamka kwa midomo yake pasipo kufikiri, alilojifungia;
7 na mumewe akasikia, naye akamnyamazia siku hiyo aliyosikia neno hilo; ndipo nadhiri zake zitathibitika, na vile vifungo ambavyo ameifunga nafsi yake vitathibitika.
8 Lakini kama mumewe akimkataza siku hiyo aliyolisikia; ndipo ataitangua nadhiri yake iliyo juu yake na neno alilolitamka kwa midomo yake pasipo kufikiri, alilojifungia; na Bwana atamsamehe
9 Lakini nadhiri ya mjane, au ya mwanamke aliyeachishwa mume, kila neno ambalo ameifunga nafsi yake kwalo, litathibitika juu yake.
10 Tena kama aliweka nadhiri nyumbani mwa mumewe, au kama aliifunga nafsi yake kwa kifungo pamoja na kiapo,
11 na mumewe alisikia akamnyamazia, wala hakumkataza; ndipo nadhiri zake zote zitathibitika, na kila kifungo alichojifungia kitathibitika.
12 Lakini kama mumewe alizibatilisha na kuzitangua siku hiyo aliyozisikia, ndipo kila neno lililotoka midomoni mwake katika hizo nadhiri zake, au katika kile kifungo cha nafsi yake, halitathibitika; huyo mumewe amezitangua; na Bwana atamsamehe.
13 Kila nadhiri, na kila kiapo kifungacho, ili kuitaabisha nafsi ya mwanamke mumewe aweza kuthibitisha, au mumewe aweza kutangua.
14 Lakini mumewe akimnyamazia mkewe kabisa siku hata siku ndipo azithibitisha nadhiri zote za mkewe, au vifungo vyake vyote vilivyo juu yake; yeye amezithibitisha, kwa kuwa alimnyamazia mkewe siku hiyo aliyozisikia nadhiri zake.
15 Lakini akizibatilisha na kuzitangua baada ya kuzisikia; ndipo yeye atachukua uovu wa mkewe.
16 Hizi ndizo amri, ambazo Bwana alimwagiza Musa, kati ya mtu mume na mkewe, kati ya baba na binti yake, katika ujana wake, ali nyumbani mwa babaye.

Hesabu 31


1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Walipize kisasi wana wa Israeli juu ya Wamidiani; kisha baadaye utakusanywa uwe pamoja na watu wako.
3 Basi Musa akanena na watu, na kuwaambia, Wavikeni silaha watu miongoni mwenu waende vitani, ili waende kupigana na Midiani, wapate kumlipiza kisasi Bwana, juu ya Midiani.
4 Katika kila kabila mtatoa watu elfu, katika kabila zote za Israeli, nanyi mtawapeleka waende vitani.
5 Basi walitolewa katika maelfu ya Israeli, elfu moja ya kila kabila, watu waume kumi na mbili elfu walioandaliwa kwa vita.
6 Basi Musa akawapeleka, watu elfu wa kila kabila waende vitani, wao na Finehasi mwana wa Eleazari kuhani, waende vitani, na vile vyombo vya mahali patakatifu, na hizo tarumbeta za kupiga sauti za kugutusha mkononi mwake.
7 Nao wakapigana na Midiani kama Bwana alivyomwagiza Musa; nao wakamwua kila mume.
8 Nao wafalme wa Midiani wakawaua pamoja na watu wengine waliouawa; Evi, na Rekemu, na Suri, na Huri, na Reba, hao wafalme watano wa Midiani; Balaamu mwana wa Beori naye wakamwua kwa upanga.
9 Wana wa Israeli wakawachukua mateka wanawake wa Midiani na watoto wao; na ng'ombe zao wote, na kondoo zao wote, na mali zao zote, wakachukua nyara.
10 Na miji yao yote, kila mahali walipokuwa wakikaa, na marago yao yote wakayateketeza kwa moto.
11 Nao wakatwaa hizo nyara zote, na mateka yote, ya wanadamu na ya wanyama.
12 Nao wakawaleta mateka ya wanadamu, na mateka ya wanyama, na hizo nyara, na kuyaweka mbele ya Musa, na mbele ya Eleazari kuhani, na mbele ya mkutano wa wana wa Israeli, hapo maragoni katika nchi tambarare za Moabu, zilizo karibu na Yordani hapo Yeriko.
13 Basi Musa, na Eleazari kuhani, na wakuu wote wa huo mkutano, wakatoka nje kwenda kuwalaki nje ya marago.
14 Musa akawakasirikia majemadari wa jeshi, na hao maakida wa elfu elfu, na wakuu wa mia mia, hao waliorudi kutoka katika kupiga vita.
15 Musa akawauliza, Je! Mmewaponya wanawake wote hai?
16 Tazama, hawa ndio waliowakosesha wana wa Israeli, kwa shauri la Balaamu, wamfanyie Bwana dhambi katika hilo jambo la Peori, na kwa hivyo pigo lilikuwa katika mkutano wa Bwana.
17 Basi kwa ajili hiyo mwueni kila mume katika hao watoto, na kila mwanamke aliyemjua mume kwa kulala pamoja naye.
18 Lakini hao watoto wote wa kike ambao hawakumjua mume kwa kulala pamoja naye, mtawaweka hai kwa ajili yenu.
19 Nanyi fanyeni matuo yenu nje ya marago muda wa siku saba; mtu awaye yote aliyemwua mtu, na awaye yote aliyemgusa mtu aliyeuawa, jitakaseni nafsi zenu siku ya tatu, na siku ya saba, ninyi na mateka yenu.
20 Na katika habari ya kila nguo, na kila kitu kilichofanywa cha ngozi, na kazi yote ya singa za mbuzi, na vyombo vyote vilivyofanywa vya mti, mtajitakasa wenyewe;
21 Kisha Eleazari kuhani akawaambia waume wa vita wote waliokwenda vitani, Hii ndiyo amri ya sheria Bwana aliyomwagiza Musa;
22 lakini dhahabu, na fedha, na shaba, na chuma, na bati, na risasi,
23 kila kitu kiwezacho kuuhimili moto, mtakipitisha katika moto, nacho kitakuwa safi, pamoja na haya kitatakaswa kwa hayo maji ya farakano; na kila kitu kisichouhimili moto mtakipitisha katika hayo maji.
24 Nanyi mtazifua nguo zenu siku ya saba, nanyi mtakuwa safi, kisha baadaye mtaingia maragoni.
25 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
26 Fanya jumla ya hayo mateka ya wanadamu, na ya wanyama pia, wewe, na Eleazari kuhani, na wakuu wa nyumba za baba za mkutano;
27 ukagawanye nyara mafungu mawili; kati ya watu waliozoea vita, waliotoka nje waende vitani, na huo mkutano wote;
28 kisha uwatoze hao watu wa vita waliotoka kwenda vitani sehemu kwa ajili ya Bwana; mmoja katika mia tano, katika wanadamu, na katika ng'ombe, na katika punda, na katika kondoo;
29 twaa katika nusu yao, ukampe Eleazari kuhani, kuwa sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana.
30 Na katika hiyo nusu ya wana wa Israeli utatwaa mmoja atakayetolewa katika kila hamsini, katika wanadamu, na katika ng'ombe, na katika punda, na katika kondoo, maana, katika wanyama wote, ukawape Walawi, hao walindao ulinzi wa maskani ya Bwana.
31 Musa na Eleazari kuhani wakafanya kama Bwana alivyomwagiza Musa.
32 Basi masazo ya hizo nyara walizotwaa watu wa vita, zilikuwa ni kondoo mia sita na sabini na tano elfu,
33 na ng'ombe sabini na mbili elfu,
34 na punda sitini na moja elfu,
35 tena wanadamu jumla yao ilikuwa thelathini na mbili elfu, katika hao wanawake ambao hawakumjua mume kwa kulala pamoja naye.
36 Na hiyo nusu ambayo ilikuwa ni sehemu ya hao waliotoka kwenda vitani, hesabu yake ilikuwa kondoo mia tatu na thelathini na saba elfu na mia tano;
37 na kodi ya Bwana katika hao kondoo ilikuwa kondoo mia sita na sabini na watano.
38 Tena, ng'ombe walikuwa thelathini na sita elfu; na katika hao kodi ya Bwana ilikuwa ng'ombe sabini na wawili.
39 Na punda walikuwa thelathini elfuna mia tano, katika hao kodi ya Bwana ilikuwa punda sitini na mmoja.
40 Na wanadamu walikuwa watu kumi na sita elfu; katika hao sehemu ya Bwana ilikuwa ni watu thelathini na wawili.
41 Basi Musa akampa Eleazari kuhani hiyo sehemu, iliyokuwa sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana, kama Bwana alivyomwagiza Musa.
42 Tena katika hiyo nusu iliyokuwa ya wana wa Israeli, ambayo Musa aliitenga na watu waliokwenda vitani,
43 (basi hiyo nusu ya mkutano ilikuwa ni kondoo mia tatu na thelathini na saba elfu na mia tano,
44 na ng'ombe thelathini na sita elfu,
45 na punda thelathini elfu, na mia tano,
46 na wanadamu kumi na sita elfu;)
47 na katika hiyo nusu iliyokuwa ya wana wa Israeli, Musa akatwaa mmoja aliyetolewa katika kila hamsini, wa binadamu na wa wanyama, akawapa Walawi, waliolinda ulinzi wa maskani ya Bwana; kama Bwana alivyomwagiza Musa.
48 Na majemadari waliokuwa juu ya elfu elfu za hiyo jeshi, na maakida wa elfu elfu, na maakida wa mia mia, wakamkaribia Musa;
49 wakamwambia Musa wakisema, Sisi watumishi wako tumefanya jumla ya hesabu ya watu wa vita walio chini ya mikono yetu, na hapana hata mmoja aliyetupungukia.
50 Nasi tumeleta matoleo ya Bwana, aliyopata kila mtu, ya vyombo vya dhahabu, na mitali, na timbi, na pete za muhuri, na vipini, na vikuku, ili kuzifanyia upatanisho nafsi zetu mbele ya Bwana.
51 Musa na Eleazari kuhani wakapokea kwao hiyo dhahabu, maana, vile vyombo vyote vilivyofanyizwa.
52 Na dhahabu yote ya sadaka ya kuinuliwa waliyosongeza kwa Bwana, ya maakida wa elfu elfu, na maakida wa mia mia, ilikuwa shekeli kumi na sita elfu na mia saba na hamsini.
53 (Kwa kuwa hao watu wa vita walikuwa wametwaa nyara, kila mtu nafsi yake.)
54 Basi Musa na Eleazari kuhani wakapokea hiyo dhahabu mikononi mwa hao maakida wa elfu elfu na wa mia mia, na kuileta ndani ya hema ya kukutania, ili iwe ukumbusho kwa ajili ya wana wa Israeli mbele za Bwana.

Hesabu 32


1 Basi wana wa Reubeni, na hao wana wa Gadi, walikuwa na wanyama wa mifugo wengi sana; nao walipoona nchi ya Yazeri, na nchi ya Gileadi, ya kuwa mahali hapo palikuwa ni mahali pa kuwafaa wanyama;
2 hao wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, wakamwendea Musa na Eleazari kuhani, na wakuu wa mkutano, wakanena nao, wakisema,
3 Atarothi, na Diboni, na Yazeri, na Nimra, na Heshboni, na Eleale, na Sebamu, na Nebo na Beoni,
4 nchi hiyo ambayo Bwana aliipiga mbele ya mkutano wa Israeli, ni nchi ifaayo kwa mfugo wa wanyama, nasi watumishi wako tuna wanyama.
5 Wakasema, Kama tumepata kibali mbele ya macho yako, sisi watumishi wako na tupewe nchi hii iwe milki yetu; usituvushe mto wa Yordani.
6 Musa akawaambia wana wa Gadi na wana wa Reubeni, Je! Ndugu zenu waende vitani nanyi mtaketi hapa?
7 Mbona mwawavunja mioyo yao wana wa Israeli, wasivuke na kuingia nchi hiyo ambayo Bwana amewapa?
8 Ndivyo walivyofanya baba zenu, hapo nilipowatuma kutoka Kadesh-barnea ili waende kuiangalia hiyo nchi.
9 Kwa kuwa walipokwea na kuingia bonde la Eshkoli, na kuiona nchi, wakawavunja mioyo wana wa Israeli, ili wasikwee kuingia nchi Bwana aliyowapa.
10 Na siku ile hasira za Bwana ziliwaka, naye akaapa, akisema,
11 Hakika yangu hapana mtu mmoja katika wale watu waliotoka Misri, tangu huyo aliyepata umri wa miaka ishirini, na zaidi, atakayeiona hiyo nchi niliyomwapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo; kwa sababu hawakuniandama kwa moyo wote;
12 ila Kalebu mwana wa Yefune, Mkenizi, na Yoshua mwana wa Nuni; kwa kuwa wao wamemwandama Bwana kwa moyo wote.
13 Na hasira za Bwana ziliwaka juu ya Israeli, naye akawatembeza huku na huku jangwani muda wa miaka arobaini, hata kizazi hicho kizima kilichokuwa kimefanya uovu machoni pa Bwana kikaisha angamia.
14 Na tazama, ninyi mmeinuka badala ya baba zenu, maongeo ya watu wenye dhambi, ili kuongeza tena hizo hasira kali za Bwana juu ya Israeli.
15 Kwa kuwa mkigeuka msimwandame, yeye atawaacha tena nyikani; nanyi mtawaangamiza watu hawa wote.
16 Basi wakamwendea karibu, na kusema, Sisi tutafanya mazizi hapa kwa ajili ya wanyama wetu wa mifugo, na kujenga miji kwa ajili ya watoto wetu;
17 lakini sisi wenyewe tutakuwa tayari na silaha zetu kutangulia mbele ya wana wa Israeli, hata tutakapowafikisha mahali pao; na watoto wetu watakaa katika hiyo miji yenye maboma, kwa sababu ya wenyeji wa nchi.
18 Sisi hatutarudia nyumba zetu, hata wana wa Israeli watakapokuwa wamekwisha kurithi kila mtu urithi wake.
19 Kwa kuwa sisi hatutarithi pamoja nao huko ng'ambo ya pili ya Yordani, huko mbele; kwa sababu urithi wetu umetuangukia upande huu wa Yordani kwa mashariki.
20 Basi Musa akawaambia, Kama mtafanya jambo hili; kama mtajivika silaha, ili kutangulia mbele ya Bwana mwende vitani,
21 tena kama kila mume wa kwenu mwenye kuchukua silaha atavuka Yordani mbele ya Bwana, hata atakapokuwa amekwisha watoa adui zake mbele yake,
22 na hiyo nchi kushindwa mbele za Bwana; ndipo baadaye mtarudi, nanyi mtakuwa hamna hatia mbele za Bwana, wala kwa Israeli; na nchi hii itakuwa milki yenu mbele za Bwana.
23 Lakini kama hamtaki kufanya neno hilo, ninyi mmefanya dhambi mbele za Bwana, nanyi jueni ya kwamba hiyo dhambi yenu itawapata hapana budi.
24 Basi, jengeni miji kwa ajili ya watoto wenu, na mazizi kwa ajili ya kondoo zenu; mkayafanye hayo mliotamka kwa vinywa vyenu.
25 Ndipo wana wa Gadi na wana wa Reubeni wakanena na Musa, na kumwambia, Sisi watumishi wako tutafanya kama wewe bwana wangu utuagizavyo.
26 Watoto wetu, na wake wetu, na kondoo zetu, na ng'ombe zetu wote, watakuwa hapo katika miji ya Gileadi;
27 lakini sisi watumishi wako tutavuka, kila mume aliyevaa silaha za vita, mbele za Bwana, tuende vitani, kama wewe bwana wangu usemavyo.
28 Basi Musa akamwagiza Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni, na wakuu wa nyumba za mababa za kabila za wana wa Israeli, katika habari za watu hao.
29 Musa akawaambia, Kwamba wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, watavuka Yordani pamoja nanyi, kila mtu aliyevaa silaha kwa vita, mbele za Bwana, nayo nchi itashindwa mbele yenu; ndipo mtawapa nchi ya Gileadi kuwa milki yao;
30 lakini ikiwa hawataki kuvuka pamoja nanyi, hali wamevaa silaha zao, ndipo watakuwa na milki zao kati yenu katika nchi ya Kanaani.
31 Wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, wakajibu na kusema, Kama Bwana alivyotuambia sisi watumishi wako, ndivyo tutakavyofanya.
32 Tutavuka, hali tumevaa silaha zetu, mbele za Bwana, kuingia nchi ya Kanaani, nayo milki ya urithi wetu itakuwa ng'ambo ya pili ya Yordani.
33 Basi Musa akawapa wao, maana, wana wa Gadi, na wana wa Reubeni, na hiyo nusu ya kabila ya Manase, mwana wa Yusufu, ufalme wa Sihoni mfalme wa Waamori, na ufalme wa Ogu mfalme wa Bashani, hiyo nchi, kama miji yao ilivyokuwa, pamoja na mipaka yake, maana, miji ya hiyo nchi iliyozunguka kotekote.
34 Kisha wana wa Gadi wakajenga Diboni, na Atarothi, na Aroeri;
35 na Atrothi-shofani, na Yazeri, na Yogbeha;
36 na, Beth-nimra, na Beth-harani; miji yenye maboma, na mazizi ya kondoo.
37 Na wana wa Reubeni wakajenga Heshboni, na Eleale, na Kiriathaimu;
38 na Nebo, na Baal-meoni, (majina yake yalikuwa yamegeuzwa) na Sibma; nao wakaiita miji waliyoijenga majina mengine.
39 Na wana wa Makiri mwana wa Manase wakaenda Gileadi, na kuitwaa, na kuwapokonya Waamori waliokuwamo humo.
40 Basi Musa akampa Makiri, mwana wa Manase, Gileadi, naye akakaa humo.
41 Kisha Yairi mwana wa Manase akaenda na kuvitwaa vijiji vya Gileadi. Akaviita jina lake Hawoth-yairi.
42 Kisha Noba akaenda na kutwaa Kenathi na vijiji vyake, na kuita jina lake Noba, kwa kuandama jina lake mwenyewe.

Hesabu 33


1 Hizi ndizo safari za wana wa Israeli, hapo walipotoka nchi ya Misri kwa jeshi zao chini ya mkono wa Musa na Haruni.
2 Musa akaandika jinsi walivyotoka katika safari zao, kwa amri ya Bwana; na hizi ndizo safari zao kama kutoka kwao kulivyokuwa.
3 Wakasafiri kutoka Ramesesi mwezi wa kwanza, siku ya kumi na tano ya mwezi wa kwanza; siku ya pili baada ya Pasaka, wana wa Israeli wakatoka kwa mkono wa nguvu mbele ya macho ya Wamisri wote,
4 hapo Wamisri walipokuwa wanazika wazaliwa wa kwanza wao wote, Bwana aliokuwa amewapiga kati yao; Bwana akafanya hukumu juu ya miungu yao nayo.
5 Wana wa Israeli wakasafiri kutoka Ramesesi, wakapanga katika Sukothi.
6 Kisha wakasafiri kutoka Sukothi, wakapanga Ethamu, palipo katika mwisho wa nyika.
7 Wakasafiri kutoka Ethamu, na kurudi nyuma hata Pi-hahirothi palipokabili Baal-sefoni; wakapanga mbele ya Migdoli.
8 Wakasafiri kutoka hapo mbele ya Hahirothi, wakapita katikati ya bahari na kuingia jangwani; kisha wakaenda safari ya siku tatu katika nyika ya Ethamu, wakapanga Mara.
9 Wakasafiri kutoka Mara, wakafikilia Elimu; huko Elimu palikuwa na chemchemi za maji kumi na mbili, na mitende sabini; nao wakapanga hapo.
10 Wakasafiri kutoka Elimu wakapanga karibu na Bahari ya Shamu.
11 Wakasafiri kutoka Bahari ya Shamu, wakapanga katika nyika ya Sini.
12 Wakasafiri kutoka nyika ya Sini, wakapanga Dofka.
13 Wakasafiri kutoka Dofka, wakapanga Alushi.
14 Wakasafiri kutoka Alushi, wakapanga Refidimu, ambapo hapakuwa na maji ya watu kunywa.
15 Wakasafiri kutoka Refidimu, wakapanga katika nyika ya Sinai.
16 Wakasafiri kutoka nyika ya Sinai, wakapanga Kibroth-hataava.
17 Wakasafiri kutoka Kibroth-hataava, wakapanga Haserothi.
18 Wakasafiri kutoka Haserothi, wakapanga Rithma.
19 Wakasafiri kutoka Rithma, wakapanga Rimon-peresi.
20 Wakasafiri kutoka Rimon-peresi, wakapanga Libna.
21 Wakasafiri kutoka Libna, wakapanga Risa.
22 Wakasafiri kutoka Risa, wakapanga Keheletha.
23 Wakasafiri kutoka Keheletha, wakapanga katika mlima wa Sheferi
24 Wakasafiri kutoka huo mlima wa Sheferi, wakapanga Harada.
25 Wakasafiri kutoka Harada, wakapanga Makelothi.
26 Wakasafiri kutoka Makelothi, wakapanga Tahathi.
27 Wakasafiri kutoka Tahathi wakapanga Tera.
28 Wakasafiri kutoka Tera, wakapanga Mithka.
29 Wakasafiri kutoka Mithka, wakapanga Hashmona.
30 Wakasafiri kutoka Hashmona, wakapanga Moserothi.
31 Wakasafiri kutoka Moserothi, wakapanga Bene-yakani.
32 Wakasafiri kutoka Bene-yakani, wakapanga Hor-hagidgadi.
33 Wakasafiri kutoka Hor-hagidgadi, wakapanga Yotbatha.
34 Wakasafiri kutoka Yotbatha, wakapanga Abrona.
35 Wakasafiri kutoka Abrona, wakapanga Esion-geberi.
36 Wakasafiri kutoka Esion-geberi, wakapanga katika nyika ya Sini (ni Kadeshi).
37 Wakasafiri kutoka Kadeshi wakapanga katika mlima wa Hori, katika mpaka wa nchi ya Edomu,
38 Haruni akakwea mlima wa Hori, kwa amri ya Bwana, akafa hapo, katika mwaka wa arobaini baada ya wana wa Israeli kutoka katika nchi ya Misri, mwezi wa tano, siku ya kwanza ya mwezi.
39 Naye Haruni alikuwa mtu wa umri wa miaka mia na ishirini na mitatu hapo alipokufa katika mlima wa Hori.
40 Ndipo Mkanaani, mfalme wa Aradi, aliyekaa pande za Negebu katika nchi ya Kanaani akasikia habari za kuja kwao wana wa Israeli.
41 Nao wakasafiri kutoka mlima wa Hori, wakapanga Salmona.
42 Wakasafiri kutoka Salmona, wakapanga Punoni.
43 Wakasafiri kutoka Punoni, wakapanga Obothi.
44 Wakasafiri kutoka Obothi, wakapanga Iye-abarimu, katika mpaka wa Moabu.
45 Wakasafiri kutoka Iye-abarimu, wakapanga Dibon-gadi.
46 Wakasafiri kutoka Dibon-gadi, wakapanga Almon-diblathaimu.
47 Wakasafiri kutoka Almon-diblathaimu, wakapanga katika milima ya Abarimu, kukabili Nebo.
48 Wakasafiri kutoka hiyo milima ya Abarimu, wakapanga katika nchi tambarare za Moabu, karibu na mto wa Yordani, hapo Yeriko.
49 Wakapanga karibu na Yordani, tangu Beth-yeshimothi hata kufikilia Abel-shitimu katika nchi tambarare za Moabu.
50 Kisha Bwana akanena na Musa hapo katika nchi tambarare za Moabu, karibu na Yordani, hapo Yeriko, na kumwambia,
51 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa Yordani na kuingia nchi ya Kanaani,
52 ndipo mtakapowafukuza wenyeji wote wa hiyo nchi mbele yenu, nanyi mtayaharibu mawe yao yote yenye kuchorwa sanamu, na kuziharibu sanamu zao zote za kusubu, kuvunja-vunja mahali pao pote palipoinuka;
53 nanyi mtaishika hiyo nchi kuimiliki na kuketi humo; kwa kuwa mimi nimewapa ninyi hiyo nchi ili mwimiliki.
54 Nanyi mtairithi nchi kwa kufanya kura, kama jamaa zenu zilivyo; hao walio wengi mtawapa urithi zaidi, na hao waliopunguka utawapa kama kupunguka kwao; mahali po pote kura itakapomwangukia mtu ye yote, mahali hapo ni pake; mtarithi kama kabila za baba zenu zilivyo.
55 Lakini kama hamtaki kuwafukuza wenyeji wa nchi watoke mbele yenu; ndipo hao ambao mtakaowasaza watakuwa kama sindano machoni mwenu, na kama miiba ubavuni mwenu, nao watawasumbua katika hiyo nchi ambayo mwakaa.
56 Kisha itakuwa, kama nilivyoazimia kuwatenda wao, ndivyo nitakavyowatenda ninyi.

Hesabu 34


1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Waagize wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapoingia nchi ya Kanaani, (hii ndiyo nchi itakayowaangukia kuwa urithi, maana, hiyo nchi ya Kanaani kama mipaka yake ilivyo,)
3 ndipo upande wenu wa kusini utakuwa tangu bara ya Sini kupita kando ya Edomu, na mpaka wenu wa kusini utakuwa tangu mwisho wa Bahari ya Chumvi kuelekea mashariki;
4 kisha mpaka wenu utageuka kwenda upande wa kusini wa kukwelea kwake Akrabimu, kisha kupita kwendelea Sini; na kutokea kwake kutakuwa kuelekea upande wa kusini wa Kadesh-barnea; kisha utaendelea mpaka Hasar-adari, na kufikilia Azmoni;
5 kisha mpaka utageuka kutoka Azmoni kwendelea kijito cha Misri, na kutokea kwake kutakuwa hapo baharini.
6 Kisha mpaka wenu wa upande wa magharibi mtakuwa na bahari kubwa na mpaka wake; hii ndiyo mpaka wenu upande wa magharibi.
7 Kisha mpaka wenu wa upande wa kaskazini utakuwa ni huu; kutoka bahari kubwa mtajiandikia mlima wa Hori;
8 na kutoka mlima wa Hori mtaandika mpaka kuingilia kwake Hamathi; na kutokea kwake mpaka kutakuwa hapo Sedada;
9 tena mpaka utatokea hata Zifroni, na kutokea kwake kutakuwa hapo Hasarenani; huo ndio mpaka wenu wa upande wa kaskazini.
10 Kisha mtaandika mpaka wenu wa upande wa mashariki kutoka Hasarenani hata Shefamu;
11 kisha mpaka utatelemka kutoka Shefamu mpaka Ribla, upande wa mashariki wa Aini; kisha mpaka utatelemka na kufikilia upande wa bahari ya Kinerethi upande wa mashariki;
12 kisha mpaka utatelemkia Yordani, na kutokea kwake kutakuwa hapo katika Bahari ya Chumvi; hii ndiyo nchi yenu kama mipaka yake ilivyo kuizunguka pande zote.
13 Kisha Musa akawaagiza wana wa Israeli, akisema, Hii ndiyo nchi mtakayoirithi kwa kupiga kura, ambayo Bwana ameagiza wapewe watu wa zile kabila kenda, na nusu ya kabila;
14 kwa kuwa kabila ya wana wa Reubeni kwa nyumba za baba zao, na kabila ya wana wa Gadi kwa nyumba za baba zao, wamekwisha pata, na hiyo nusu ya kabila ya Manase wamekwisha pata urithi wao;
15 hizo kabila mbili na nusu ya kabila wamekwisha pata urithi wao huko ng'ambo ya pili ya Yordani, hapo Yeriko, upande wa mashariki, kuelekea maawio ya jua.
16 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
17 Haya ndiyo majina ya watu watakaowagawanyia nchi iwe urithi wenu; Eleazari kuhani, na Yoshua mwana wa Nuni.
18 Kisha mtamtwaa mkuu mmoja wa kila kabila, ili waigawanye nchi iwe urithi wenu.
19 Na majina ya watu hao ni haya; katika kabila ya Yuda, ni Kalebu mwana wa Yefune.
20 Na katika kabila ya wana wa Simeoni, Shemueli mwana wa Amihudi.
21 Katika kabila ya Benyamini, ni Elidadi mwana wa Kisloni.
22 Na katika kabila ya wana wa Dani, mkuu, Buki mwana wa Yogli.
23 Katika wana wa Yusufu; katika kabila ya wana wa Manase, mkuu, Hanieli mwana wa Efodi;
24 na katika kabila ya wana wa Efraimu, mkuu, Kemueli mwana wa Shiftani.
25 Na katika kabila ya wana wa Zabuloni, mkuu, Elisafani mwana wa Parnaki.
26 Na katika kabila ya wana wa Isakari, mkuu, Paltieli mwana wa Azani.
27 Na katika kabila ya wana wa Asheri, mkuu, Ahihudi mwana wa Shelomi.
28 Na katika kabila ya wana wa Naftali, mkuu, Pedaheli mwana wa Amihudi.
29 Hao ndio Bwana aliowaagiza wawagawanyie urithi wana wa Israeli katika nchi ya Kanaani.

Hesabu 35


1 Kisha Bwana akanena na Musa katika nchi tambarare za Moabu, karibu na mto wa Yordani, hapo Yeriko, akamwambia,
2 Uwaagize wana wa Israeli wawape Walawi miji wapate mahali pa kukaa, katika milki yao; pamoja na malisho yaliyoizunguka hiyo miji kotekote mtawapa Walawi.
3 Hiyo miji watakuwa nayo ili wakae humo, na malisho watakuwa nayo kwa wanyama wao wa mifugo, na kwa mali zao, na kwa wanyama wao wote.
4 Na yale malisho ya miji mtakayowapa Walawi, ukubwa wake utakuwa tangu ukuta wa mji kupima kiasi cha dhiraa elfu pande zote.
5 Nanyi mtapima hapo nje ya mji upande wa mashariki dhiraa elfu mbili, na upande wa kusini dhiraa elfu mbili, na upande wa magharibi dhiraa elfu mbili, na upande wa kaskazini dhiraa elfu mbili, huo mji ulio katikati. Hayo ndiyo yatakayokuwa kwao malisho ya miji.
6 Na hiyo miji mtakayowapa Walawi, itakuwa miji sita ya makimbilio, mtakayoweka kwa ajili ya mwenye kumwua mtu, ili akimbilie huko; pamoja na hiyo mtawapa miji arobaini na miwili zaidi.
7 Miji yote mtakayowapa hao Walawi jumla yake itakuwa miji arobaini na minane; mtawapa miji hiyo pamoja na malisho yake.
8 Tena katika miji mtakayotoa ya hiyo milki ya wana wa Israeli, katika hao walio wengi mtatwaa miji mingi; na katika hao walio wachache mtatwaa miji michache; kila mtu kama ulivyo urithi wake atakaourithi, atawapa Walawi katika miji yake.
9 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
10 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtakapovuka mto wa Yordani na kuingia nchi ya Kanaani,
11 Ndipo mtajiwekea miji iwe miji ya makimbilio kwa ajili yenu; ili kwamba mwenye kumwua mtu, pasipo kukusudia kumwua, apate kukimbilia huko.
12 Na hiyo miji itakuwa kwenu kuwa makimbilio, kumkimbia mwenye kutwaa kisasi, ili asiuawe mwenye kumwua mtu, hata atakaposimama mbele ya mkutano ahukumiwe.
13 Na hiyo miji mtakayowapa itakuwa kwenu ni miji sita ya makimbilio.
14 Mtawapa miji mitatu ng'ambo ya pili ya Yordani, na miji mitatu mtawapa katika nchi ya Kanaani; miji hiyo itakuwa ni miji ya makimbilio.
15 Miji hiyo sita itakuwa miji ya makimbilio kwa ajili ya wana wa Israeli, na kwa ajili ya mgeni, na kwa ajili ya huyo aketiye kati yao hali ya ugeni; ili kila amwuaye mtu, naye hakukusudia kumwua, apate kukimbilia huko.
16 Lakini kama alimpiga kwa chombo cha chuma, akafa, ni mwuaji huyo; mwuaji hakika yake atauawa.
17 Na kama alimpiga kwa jiwe lililokuwa mkononi mwake, ambalo kwa hilo humkini mtu kufa, naye akafa, yeye ni mwuaji; huyo mwuaji lazima atauawa.
18 Au kama alimpiga kwa chombo cha mti kilichokuwa mkononi mwake ambacho kwa hicho humkini mtu kufa, naye akafa, ni mwuaji huyo, mwuaji lazima atauawa.
19 Mwenye kutwaa kisasi cha damu ndiye atakayemwua mwuaji; hapo atakapokutana naye, atamwua.
20 Tena kwamba alimsukuma kwa kumchukia, au kwamba alimtupia kitu kwa kumvizia, hata akafa;
21 au akampiga kwa mkono wake kwa kuwa ni adui, naye akafa; yeye aliyempiga lazima atauawa; yeye ni mwuaji; mwenye kutwaa kisasi cha damu atamwua mwuaji, hapo atakapokutana naye.
22 Lakini ikiwa alimsukuma ghafula pasipo kumchukia; au akamtupia kitu cho chote pasipo kumvizia,
23 au kwa jiwe liwalo lote, ambalo kwa kupigwa kwalo humkini mtu kufa, asipomwona, akamtupia hata akafa, naye hakuwa adui yake, wala hakumtakia madhara;
24 ndipo mkutano utaamua kati ya huyo aliyempiga mtu na huyo atakayetwaa kisasi cha damu, kama hukumu hizi zilivyo;
25 nao mkutano utamwokoa yule aliyemwua mtu na mkono wa mwenye kutwaa kisasi cha damu; tena mkutano utamrejeza katika mji wake wa makimbilio, aliokuwa anaukimbilia; naye atakaa humo hata kifo chake kuhani mkuu, aliyepakwa mafuta kwa mafuta matakatifu.
26 Lakini kama mwenye kumwua mtu akienda wakati wo wote kupita mpaka wa huo mji wa makimbilio, alioukimbilia;
27 na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwona, naye yu nje ya mpaka wa mji wake wa makimbilio, na mwenye kutwaa kisasi cha damu akamwua huyo mwuaji, hatakuwa na hatia ya damu;
28 kwa sababu ilimpasa kukaa ndani ya mji wake wa makimbilio hata kifo chake kuhani mkuu lakini kuhani mkuu atakapokwisha kufa huyo mwuaji atarudi aende nchi ya urithi wake.
29 Mambo haya yatakuwa ni amri ya hukumu kwenu, katika vizazi vyenu vyote, katika makazi yenu yote.
30 Mtu awaye yote atakayemwua mtu, huyo mwuaji atauawa kwa vinywa vya mashahidi; lakini shahidi mmoja hatashuhudia juu ya mtu hata akafa.
31 Tena, msipokee fidia kwa ajili ya uhai wa mwuaji, ambaye amekuwa na hatia ya mauti; Lakini lazima atauawa.
32 Tena hamtapokea fidia kwa ajili ya huyo aliyeukimbilia mji wake wa makimbilio, apate kwenda tena kuketi katika nchi, hata kifo cha kuhani mkuu.
33 Hivi hamtaitia unajisi nchi ambayo mwakaa; kwa kuwa damu huitia nchi unajisi; wala hapana sadaka itoshayo kwa ajili ya nchi, kwa ajili ya damu iliyomwagwa ndani yake, isipokuwa ni damu ya huyo aliyeimwaga.
34 Kwa hiyo msiitie unajisi nchi muiketiyo, ambayo naketi nami kati yake; kwa kuwa mimi Bwana nakaa kati ya wana wa Israeli.

Hesabu 36


1 Kisha wale wakuu wa nyumba za mababa ya jamaa ya wana wa Gileadi, mwana wa Makiri, mwana wa Manase, katika jamaa za wana wa Yusufu, wakakaribia, na kunena mbele ya Musa, na mbele ya wakuu walio juu ya nyumba za mababa ya wana wa Israeli;
2 wakasema, Bwana alimwagiza bwana wangu awape wana wa Israeli nchi kwa kupiga kura iwe urithi wao; tena bwana wangu aliagizwa na Bwana awape binti za Selofehadi ndugu yetu huo urithi wa baba yao.
3 Wakiolewa na watu wa wana wa hizo kabila nyingine za wana wa Israeli, ndipo urithi wao utatwaliwa na kuondolewa katika urithi wa baba zetu, na hiyo kabila watakayotiwa ndani yake itaongezewa urithi wao; basi urithi huo utaondolewa katika kura ya urithi wetu.
4 Tena itakapokuwapo hiyo yubile ya wana wa Israeli, ndipo urithi wa hiyo kabila ambayo wamekuwa ndani yake utaongezewa huo urithi wao; hivyo urithi wao utaondolewa katika urithi wa kabila ya baba zetu.
5 Basi Musa akawaagiza wana wa Israeli kama neno la Bwana lilivyokuwa, akasema, Kabila ya wana wa Yusufu imenena yaliyo haki.
6 Bwana ameagiza neno hili katika habari ya binti za Selofehadi, akasema, Na waolewe na waume wawapendao; lakini na waolewe katika jamaa ya kabila ya baba zao.
7 Hivyo hapana urithi wo wote wa wana wa Israeli utakaotoka kabila hii kwenda kabila hii; kwa kuwa wana wa Israeli watashikamana kila mtu na urithi wa kabila ya baba zake.
8 Na kila binti atakayemiliki urithi katika kabila yo yote katika wana wa Israeli, ataolewa katika jamaa moja ya kabila ya baba yake, ili wana wa Israeli wapate kumiliki kila mtu urithi wa baba zake.
9 Hivyo hapatakuwa na urithi uwao wote utakaotoka kabila hii kwenda kabila hii; kwa kuwa kabila za wana wa Israeli zitashikamana kila mmoja na urithi wake mwenyewe.
10 Basi hao binti za Selofehadi wakafanya kama Bwana alivyomwagiza Musa;
11 kwa kuwa Mala, na Tirsa, na Hogla, na Milka, na Noa, binti za Selofehadi waliolewa na waume, wana wa ndugu za baba yao.
12 Waliolewa katika jamaa za wana wa Manase, mwana wa Yusufu, na urithi wao ukakaa katika kabila ya jamaa ya baba yao.
13 Haya ndiyo maagizo na hukumu, ambayo Bwana aliwaagiza wana wa Israeli, kwa mkono wa Musa, hapo katika nchi tambarare za Moabu, karibu na Yordani, hapo Yeriko