Walawi

Sura: 1, 2, 3, 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 12, 13, 14, 15, 16, 17, 18, 19, 20, 21, 22, 23, 24, 25, 26, 27

Walawi 1


1 Bwana akamwita Musa, na kusema naye kutoka katika hema ya kukutania, akamwambia,
2 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mtu wa kwenu atakapomtolea Bwana matoleo, mtatoa matoleo yenu katika wanyama wa mifugo, katika ng'ombe na katika kondoo.
3 Matoleo yake kwamba ni sadaka ya kuteketezwa ya ng'ombe, atatoa ng'ombe mume mkamilifu; ataleta mlangoni pa hema ya kukutania, ili akubaliwe mbele ya Bwana.
4 Kisha ataweka mkono wake juu ya kichwa cha hiyo sadaka ya kuteketezwa; nayo itakubaliwa kwa ajili yake, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake.
5 Naye atamchinja huyo ng'ombe mbele ya Bwana; kisha wana wa Haruni, hao makuhani, wataileta karibu hiyo damu, na kuinyunyiza damu yake kando-kando katika madhabahu iliyo hapo mlangoni pa hema ya kukutania
6 Kisha atachuna sadaka ya kuteketeza na kuikata vipande vyake.
7 Kisha wana wa Haruni, watatia moto juu ya madhabahu, na kuzipanga kuni juu ya moto,
8 kisha wana wa Haruni, makuhani, watazipanga kuni zilizo juu ya moto uliopo juu ya madhabahu;
9 lakini matumbo yake, na miguu yake, ataiosha kwa maji; na huyo kuhani ataviteketeza vyote juu ya madhabahu, ili iwe sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana.
10 Na matoleo yake kwamba ni katika kundi, katika kondoo, au katika mbuzi, kuwa sadaka ya kuteketezwa; atatoa mume mkamilifu.
11 Naye atamchinja hapo upande wa madhabahu ulioelekea kaskazini mbele za Bwana; na wana wa Haruni, hao makuhani, watainyunyiza damu yake juu ya madhabahu pande zote.
12 Kisha atamkata vipande vyake, pamoja na kichwa chake, na mafuta yake; kisha atavipanga vile vipande juu ya kuni zilizo juu ya madhabahu;
13 lakini matumbo yake, na miguu yake, ataosha kwa maji; na huyo kuhani atavisongeza vyote na kuviteketeza juu ya madhabahu; ni sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana.
14 Na matoleo yake atakayomtolea Bwana kuwa sadaka ya kuteketezwa, kwamba ni katika ndege, ndipo atakapoleta matoleo yake katika hua au katika makinda ya njiwa.
15 Kisha kuhani atamleta karibu na madhabahu, naye atamkongonyoa kichwa, na kumteketeza kwa moto juu ya madhabahu; na damu yake itachuruzishwa kando ya madhabahu;
16 kisha atakiondoa kile kibofu chake, pamoja na taka zake, na kukitupa kando ya madhabahu upande wa mashariki, mahali pa majivu;
17 kisha atampasua na mabawa yake, lakini asimkate vipande viwili; kisha kuhani atamteketeza juu ya madhabahu, juu ya kuni zilizo juu ya moto; ni sadaka ya kuteketezwa, dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana.

Walawi 2


1 Na mtu atakapomtolea Bwana matoleo ya sadaka ya unga, matoleo yake yatakuwa ya unga mwembamba; naye ataumiminia mafuta, na kutia na ubani juu yake;
2 kisha atauleta kwa wana wa Haruni, hao makuhani; naye atatwaa konzi moja katika huo unga mwembamba, na katika mafuta yake, na huo ubani wote; kisha kuhani atauteketeza kuwa ndio ukumbusho wake juu ya madhabahu, ni kafara ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana;
3 na huo uliosalia wa ile sadaka ya unga utakuwa ni wa Haruni na wanawe; ni kitu kitakatifu sana katika sadaka zilizosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.
4 Tena, utakapotoa matoleo ya sadaka ya unga uliookwa tanuuni, yatakuwa mikate isiyotiwa chachu, ya unga mwembamba uliokandwa na mafuta, au maandazi yasiyochachwa yaliyopakwa mafuta.
5 Tena matoleo yako kwamba ni sadaka ya unga wa kaangoni, yatakuwa ya unga mwembamba usiotiwa chachu, uliokandwa na mafuta.
6 Utaukata-kata vipande, na kutia mafuta juu yake; ni sadaka ya unga.
7 Tena matoleo yako kwamba ni sadaka ya unga ya chunguni, yataandaliwa kwa unga mwembamba pamoja na mafuta.
8 Nawe utamletea Bwana sadaka ya unga iliyofanywa ya vitu hivyo; nayo italetwa kwa kuhani, naye ndiye atakayeisongeza madhabahuni.
9 Kisha kuhani atatwaa humo huo ukumbusho wa sadaka ya unga, naye atauteketeza juu ya madhabahu; ni kafara ya kusongezwa kwa njia ya moto, ya harufu ya kupendeza kwa Bwana.
10 Na hicho kitakachosalia katika sadaka ya unga kitakuwa cha Haruni na wanawe; ni kitu kitakatifu sana katika sadaka zilizosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.
11 Sadaka ya unga iwayo yote itakayosongezwa kwa Bwana isitiwe chachu kabisa; kwa kuwa hamtateketeza chachu, wala asali iwayo yote, kuwa ni sadaka ya kusongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.
12 Vitu hivyo mtavisongeza kwa Bwana kuwa ni malimbuko; lakini visifike juu ya madhabahu kuwa ni harufu ya kupendeza.
13 Tena, kila toleo la sadaka yako ya unga utalitia chumvi; wala usiiache sadaka yako ya unga kupungukiwa na chumvi ya agano la Mungu wako; utatoa chumvi pamoja na matoleo yako yote.
14 Nawe kwamba wamtolea Bwana sadaka ya unga ya malimbuko, utatoa hiyo ngano katika masuke yake iliyochomwa motoni, ngano iliyopondwa ya masuke mabichi, ndiyo utakayoleta kuwa sadaka ya unga ya malimbuko yako.
15 Nawe utatia mafuta juu yake, na kuweka ubani juu yake; ni sadaka ya unga.
16 Huyo kuhani atauteketeza ukumbusho wake, yaani, sehemu ya ngano iliyopondwa ya hiyo sadaka, na sehemu ya mafuta yake, pamoja na ule ubani wake wote; ni kafara ya kusongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.

Walawi 3


1 Na matoleo yake kwamba ni sadaka za amani; kwamba asongeza katika ng'ombe, mume au mke, atamtoa huyo aliye mkamilifu mbele ya Bwana.
2 Naye ataweka mkono wake kichwani mwake huyo aliyemtoa, na kumchinja mlangoni pa hema ya kukutania; na wana wa Haruni, hao makuhani, watainyunyiza damu yake katika madhabahu pande zote.
3 Naye atasongeza katika sadaka hiyo ya amani, dhabihu kwa Bwana itakayofanywa kwa njia ya moto; yaani, mafuta yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo juu ya matumbo,
4 na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno, na hicho kitambi kilicho katika ini, pamoja na hizo figo; hayo yote atayaondoa.
5 Na wana wa Haruni watayateketeza kwa moto juu ya madhabahu, juu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyo katika kuni zilizo juu ya moto; ni dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, harufu ya kupendeza kwa Bwana.
6 Na matoleo yake kwa sadaka za amani atakayomchinjia Bwana, kwamba ni katika kundi la kondoo; mume au mke, atamtoa huyo aliye mkamilifu.
7 Kama akimtoa mwana-kondoo kuwa matoleo yake, ndipo atakapomtolea Bwana;
8 naye ataweka mkono wake kichwani mwake huyo aliyemsongeza, na kumchinja mlangoni pa hema ya kukutania; na wana wa Haruni watainyunyiza damu yake katika madhabahu pande zote.
9 Naye atasongeza katika sadaka hiyo ya amani dhabihu kwa Bwana, itakayofanywa kwa njia ya moto; yaani, mafuta yake, na mkia wenye mafuta mzima, atauondoa kwa kuukata hapo karibu na mfupa wa maungoni; na mafuta yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo katika matumbo,
10 na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini, pamoja na hizo figo; hayo yote atayaondoa.
11 Naye kuhani atayateketeza kwa moto juu ya madhabahu; ni chakula cha dhabihu ya kusongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.
12 Na matoleo yake, kwamba ni mbuzi, ndipo atakapomtoa mbele za Bwana;
13 naye ataweka mkono wake kichwani mwake, na kumchinja hapo mbele ya hema ya kukutania; na wana wa Haruni watainyunyiza damu yake katika madhabahu pande zote.
14 Naye atasongeza katika sadaka hiyo matoleo yake, dhabihu kwa Bwana kwa njia ya moto; yaani, mafuta yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo katika matumbo,
15 na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini pamoja na hizo figo mbili; hayo yote atayaondoa.
16 Naye kuhani atayateketeza kwa moto juu ya madhabahu; ni chakula cha dhabihu ya kusongezwa kwa njia ya moto, iwe harufu ya kupendeza; mafuta yote ni ya Bwana.
17 Neno hili litakuwa amri ya daima, katika vizazi vyenu vyote, ndani ya nyumba zenu zote, ya kwamba hamtakula mafuta wala damu kabisa.

Walawi 4


1 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Haya, nena na wana wa Israeli, uwaambie, Kama mtu ye yote akifanya dhambi pasipo kukusudia, katika neno lo lote ambalo Bwana amelizuilia lisifanywe, na kutenda neno lo lote la maneno hayo;
3 kama kuhani aliyetiwa mafuta akifanya dhambi, hata analeta hatia juu ya watu; ndipo na atoe kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya, na kumsongeza kwa Bwana ng'ombe mume mchanga mkamilifu, kuwa ni sadaka ya dhambi.
4 Naye atamleta huyo ng'ombe na kumweka mlangoni pa hiyo hema ya kukutania, mbele za Bwana; naye ataweka mkono wake kichwani mwake ng'ombe, na kumchinja huyo ng'ombe mbele za Bwana.
5 Kisha huyo kuhani aliyetiwa mafuta atatwaa baadhi ya damu ya huyo ng'ombe, na kuileta ndani ya hiyo hema ya kukutania;
6 kisha kuhani atatia kidole chake katika hiyo damu na kuinyunyiza damu mbele ya Bwana mara saba, mbele ya pazia la mahali patakatifu.
7 Kisha kuhani atatia baadhi ya hiyo damu juu ya pembe za madhabahu ya kufukizia uvumba mzuri mbele ya Bwana iliyo ndani ya hema ya kukutania; kisha damu yote ya huyo ng'ombe ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyoko mlangoni pa hema ya kukutania.
8 Kisha mafuta yote ya huyo ng'ombe wa sadaka ya dhambi atayaondoa; mafuta yote yafunikayo matumbo, na mafuta yote yaliyo katika matumbo,
9 na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini, pamoja na hizo figo, hayo yote atayaondoa,
10 vile vile kama yanavyoondolewa katika ng'ombe wa kuchinjwa kwa sadaka za amani; kisha huyo kuhani atayateketeza juu ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa.
11 Kisha ngozi yake ng'ombe, na nyama yake yote, pamoja na kichwa chake, na pamoja na miguu yake, na matumbo yake, na mavi yake,
12 maana, huyo ng'ombe mzima atamchukua nje ya marago hata mahali safi, hapo wamwagapo majivu, naye atamchoma moto juu ya kuni; atachomwa moto hapo majivu yamwagwapo.
13 Na kama mkutano mzima wa Israeli ukifanya dhambi, na jambo lenyewe likayafichamania macho ya huo mkutano, nao wamefanya mojawapo katika mambo yaliyozuiliwa na Bwana, kwamba wasiyafanye, nao wamepata hatia;
14 hapo itakapojulikana hiyo dhambi waliyoifanya, ndipo mkutano utatoa ng'ombe mume mchanga awe sadaka ya dhambi, na kumleta mbele ya hema ya kukutania.
15 Kisha wazee wa mkutano wataweka mikono yao kichwani mwake huyo ng'ombe mbele za Bwana;
16 kisha ng'ombe atachinjwa mbele za Bwana. Kisha kuhani aliyetiwa mafuta atatwaa katika damu ya huyo ng'ombe na kuileta ndani ya hema ya kukutania;
17 kisha kuhani atatia kidole chake katika hiyo damu, na kuinyunyiza mbele za Bwana, mbele ya pazia mara saba.
18 Kisha nyingine katika hiyo damu ataitia katika pembe za madhabahu iliyo mbele za Bwana, iliyoko ndani ya hema ya kukutania, kisha damu yote ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, iliyo mlangoni pa hema ya kukutania.
19 Kisha atayaondoa mafuta yake yote na kuyateketeza juu ya madhabahu.
20 Ndivyo atakavyomfanyia huyo ng'ombe; kama alivyomfanyia huyo ng'ombe wa sadaka ya dhambi, atamfanyia na huyu vivyo; naye kuhani atawafanyia upatanisho, nao watasamehewa.
21 Kisha atamchukua huyo ng'ombe nje ya marago, na kumchoma moto vile vile kama alivyomchoma moto ng'ombe wa kwanza; ni sadaka ya dhambi kwa ajili ya mkutano.
22 Mtawala atakapofanya dhambi, na kutenda pasipo kukusudia neno lo lote katika hayo ambayo Bwana, Mungu wake, aliyazuilia yasifanywe, naye amepata hatia;
23 akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ataleta mbuzi awe matoleo yake, mume, mkamilifu;
24 kisha ataweka mkono wake kichwani mwake huyo mbuzi, na kumchinja hapo wachinjapo sadaka ya kuteketezwa mbele za Bwana; ni sadaka ya dhambi.
25 Kisha kuhani atatwaa katika damu ya hiyo sadaka ya dhambi kwa kidole chake, na kuitia katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, nayo damu yake ataimwaga hapo chini ya madhabahu ya kuteketeza.
26 Na mafuta yake yote atayateketeza juu ya madhabahu, kama alivyoyateketeza mafuta ya hizo sadaka za amani; naye kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake, naye atasamehewa.
27 Na mtu awaye yote katika watu wa nchi akifanya dhambi pasipo kukusudia, kwa kufanya neno lo lote katika hayo ambayo Bwana alizuilia yasifanywe, naye akapata hatia;
28 akijulishwa hiyo dhambi yake aliyoifanya, ndipo atakapoleta mbuzi mke mkamilifu, awe matoleo yake kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya.
29 Naye ataweka mkono wake kichwani mwake hiyo sadaka ya dhambi, na kumchinja sadaka ya dhambi mahali hapo pa sadaka ya kuteketezwa.
30 Kisha kuhani atatwaa katika hiyo damu yake kwa kidole chake, na kuitia katika pembe za madhabahu ya kuteketeza na damu yake yote ataimwaga chini ya madhabahu.
31 Kisha atayaondoa mafuta yake yote, kama vile mafuta yanavyoondolewa katika hizo sadaka za amani; kisha kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, iwe harufu ya kupendeza kwa Bwana; na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atasamehewa.
32 Naye akileta mwana-kondoo kuwa sadaka ya dhambi, ataleta wa kike mkamilifu.
33 Naye ataweka mkono wake kichwani mwake sadaka ya dhambi, kisha atamchinja awe sadaka ya dhambi, mahali hapo wachinjapo sadaka ya kuteketezwa.
34 Kisha kuhani atatwaa katika hiyo damu ya sadaka ya kuteketezwa kwa kidole chake na kuitia katika pembe za madhabahu ya sadaka ya kuteketezwa, kisha damu yake yote ataimwaga hapo chini ya madhabahu;
35 kisha atayaondoa mafuta yake yote, kama mafuta ya mwana-kondoo yalivyoondolewa katika hizo sadaka za amani; kisha kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, kwa desturi ya hizo sadaka za Bwana zilizosongezwa kwa njia ya moto; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, naye atasamehewa.

Walawi 5


1 Na mtu awaye yote akifanya dhambi, kwa kuwa ameisikia sauti yenye kuapisha, naye akawa ni shahidi, kwamba aliona au kujua, asipolifunua neno lile, ndipo atakapochukua uovu wake mwenyewe;
2 au kama mtu akigusa kitu kilicho najisi, kama ni mzoga wa mnyama wa nyikani aliye najisi, au kama ni mzoga wa mnyama wa mfugo aliye najisi, au kama ni mzoga wa mdudu aliye najisi, naye jambo hilo linamfichamania, akapata kuwa najisi, ndipo atakapochukua uovu wake;
3 au kama akiugusa uchafu wa binadamu, uchafu uwao wote ambao kwa huo amepata unajisi, na jambo hilo linamfichamania, hapo apatapo kulijua, ndipo atakapokuwa na hatia;
4 au, kama mtu akijiapisha, kwa kutamka haraka kwa midomo yake, kutenda uovu, au kutenda mema, neno lo lote mtu atakalolitamka kwa kiapo pasipo kufikiri, na neno hilo likamfichamania; hapo atakapolijua, ndipo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo;
5 kisha itakuwa, hapo atakapokuwa na hatia katika mambo hayo mojawapo, ndipo atakapoliungama jambo hilo alilolikosa;
6 naye atamletea Bwana sadaka yake ya hatia kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, mwana-kondoo wa kike, au mbuzi mke, kutoka katika kundi lake, kuwa ni sadaka ya dhambi; kisha kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake.
7 Lakini asipomweza mwana-kondoo, ndipo atakapomletea Bwana hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, kuwa ni sadaka yake ya hatia ya jambo hilo alilolikosa; mmoja wa hao ndege kwa sadaka ya dhambi, na wa pili kwa sadaka ya kuteketezwa.
8 Naye atawaleta kwa kuhani, atakayemsongeza kwanza yule wa sadaka ya dhambi, naye atamkongonyoa kichwa shingoni mwake, lakini asimpasue vipande viwili;
9 kisha baadhi ya damu ya hiyo sadaka ya dhambi atainyunyiza katika ubavu wa madhabahu; na damu iliyosalia itachuruzishwa hapo chini ya madhabahu; ni sadaka ya dhambi.
10 Kisha huyo ndege wa pili atamsongeza kuwa sadaka ya kuteketezwa, sawasawa na sheria; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya hiyo dhambi yake aliyoifanya, naye atasamehewa.
11 Lakini asipowaweza hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, ndipo hapo atakapoleta matoleo yake kwa ajili ya neno hilo alilolikosa, sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba, kuwa sadaka yake ya dhambi; asitie mafuta juu yake, wala ubani usitiwe juu yake; maana, ni sadaka ya dhambi.
12 Naye atamletea kuhani, na kuhani atatwaa konzi yake ya huo unga kuwa ukumbusho wake, na kuuteketeza juu ya madhabahu, juu ya sadaka zilizosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto; ni sadaka ya dhambi.
13 Na huyo kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya dhambi yake ambayo katika mambo hayo mojawapo amefanya dhambi, naye atasamehewa; na unga uliosalia utakuwa wa kuhani, kama hiyo sadaka ya unga ilivyokuwa.
14 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
15 Mtu awaye yote akiasi na kufanya dhambi naye hakukusudia, katika mambo matakatifu ya Bwana; ndipo atakapomletea Bwana sadaka yake ya hatia, kondoo mume mkamilifu katika kundi lake; sawasawa na hesabu utakayomwandikia katika shekeli za fedha, kwa shekeli ya mahali patakatifu, kuwa sadaka ya hatia;
16 naye atalipa kwa ajili ya hilo alilolikosa katika kitu kile kitakatifu, kisha ataongeza na sehemu ya tano, na kumpa kuhani; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake kwa huyo kondoo mume wa sadaka ya hatia, naye atasamehewa.
17 Na kama mtu akifanya dhambi, na kutenda mambo hayo mojawapo ambayo Bwana alizuilia yasifanywe, ajapokuwa hakuyajua, ni mwenye hatia vivyo, naye atachukua uovu wake.
18 Naye ataleta kondoo mume wa kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, amsongeze kwa huyo kuhani; na kuhani atamfanyia upatanisho kwa ajili ya jambo hilo alilolikosa pasipo kukusudia, asilijue, naye atasamehewa.
19 Ni sadaka ya hatia; hakika yake ni mwenye hatia mbele za Bwana.

Walawi 6


1 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Mtu awaye yote akifanya dhambi, na kuasi juu ya Bwana, akamdanganya mwenziwe katika jambo la amana, au la mapatano, au la kunyang'anya, au kumwonea mwenziwe;
3 au kuzumbua kitu kilichopotea na kutenda la uongo juu yake, na kuapa kwa uongo; katika mambo hayo yote mojawapo atakalolitenda mtu, na kufanya dhambi kwalo;
4 ndipo itakapokuwa, akiwa amefanya dhambi, na kupata hatia, atarudisha hicho alichokipata kwa kunyang'anya, au kitu kile alichokipata kwa kuonea, au ile amana aliyowekewa, au kitu kile kilichopotea alichokizumbua yeye,
5 au kitu cho chote ambacho amekiapia uongo; atakirudisha hata kwa utimilifu wake, kisha ataongeza na sehemu ya tano zaidi juu yake; naye atampa huyo mwenyewe, siku hiyo ambayo atakapohukumiwa kuwa mwenye hatia.
6 Kisha ataleta sadaka yake ya hatia kwa Bwana, ni kondoo mume wa katika kundi lake, mkamilifu, sawasawa na hesabu utakayomwandikia, kuwa sadaka ya hatia, na kumpa kuhani;
7 na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana, naye atasamehewa; katika jambo lo lote alifanyalo hata akapata kuwa mwenye hatia kwalo.
8 Bwana akanena na Musa na kumwambia,
9 Haya, mwagize Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya sadaka ya kuteketezwa ni hii; hiyo sadaka ya kuteketezwa itakuwa pale motoni juu ya madhabahu usiku wote hata asubuhi; na huo moto wa madhabahu utawaka juu yake usizimike.
10 Naye kuhani atavaa nguo yake ya kitani, na suruali zake za kitani atazivaa mwilini mwake; naye atayazoa majivu ambayo huo moto umeiteketezea sadaka juu ya madhabahu, kisha atayaweka kando ya madhabahu.
11 Kisha atayavua mavazi yake, na kuvaa mavazi mengine, kisha atayachukua yale majivu kwenda nayo nje ya marago hata mahali safi.
12 Na huo moto ulio madhabahuni atautunza uwake daima juu yake, usizimike; naye kuhani atateketeza kuni katika moto huo kila siku asubuhi; naye ataipanga sadaka ya kuteketezwa juu yake, naye atayateketeza mafuta ya sadaka za amani juu yake.
13 Moto utatunzwa uwake juu ya madhabahu daima; usizimike.
14 Na amri ya hiyo sadaka ya unga ni hii; wana wa Haruni wataisongeza mbele za Bwana, mbele ya madhabahu.
15 Naye atatwaa konzi yake katika huo unga, katika huo unga mwembamba wa sadaka ya unga, na katika mafuta yake, na ubani wote ulio juu ya sadaka ya unga, kisha atauteketeza juu ya madhabahu kuwa harufu ya kupendeza, kuwa ukumbusho wake kwa Bwana.
16 Na unga uliosalia Haruni na wanawe wataula; utaliwa pasipo kutiwa chachu, katika mahali patakatifu; katika ua wa hema ya kukutania ndipo watakapoula.
17 Hautaokwa na chachu. Nimewapa kuwa sehemu yao katika matoleo yangu yasongezwayo kwa njia ya moto; ni kitu kitakatifu sana, kama hiyo sadaka ya dhambi, na kama hiyo sadaka ya hatia.
18 Kila mwana mume miongoni mwa wana wa Haruni atakula katika huo, kuwa ni haki yao milele katika vizazi vyenu, katika matoleo ya Bwana yasongezwayo kwa njia ya moto; mtu awaye yote atakayevigusa atakuwa ni mtakatifu
19 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
20 Matoleo ya Haruni na wanawe watakayomtolea Bwana, katika siku atakayotiwa mafuta, ni haya; sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga daima, nusu yake asubuhi, na nusu yake jioni.
21 Utaandaliwa kaangoni pamoja na mafuta; ukisha kulowama utauleta ndani; utasongeza hiyo sadaka ya unga vipande vilivyookwa, iwe harufu ya kupendeza kwa Bwana.
22 Na huyo kuhani aliyetiwa mafuta badala yake katika hao wanawe ataisongeza; itateketezwa kabisa kwa Bwana kwa amri ya milele.
23 Tena kila sadaka ya unga ya kuhani itateketezwa kabisa; isiliwe.
24 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
25 Nena na Haruni na wanawe, uwaambie, Amri ya hiyo sadaka ya dhambi ni hii; mahali hapo pachinjwapo sadaka ya kuteketezwa ndipo itakapochinjwa sadaka ya dhambi, mbele za Bwana; ni takatifu sana.
26 Huyo kuhani atakayeisongeza kwa ajili ya dhambi ndiye atakayeila; italiwa katika mahali patakatifu, katika ua wa hema ya kukutania.
27 Kila kitu kitakachoigusa nyama ya sadaka hiyo kitakuwa kitakatifu; tena itakapomwagika damu yake yo yote katika nguo yo yote, utaifua nguo hiyo iliyomwagiwa, katika mahali patakatifu.
28 Lakini hicho chombo cha udongo ambacho hiyo nyama ilipikwa ndani yake kitavunjwa; na kama ikipikwa katika chombo cha shaba, kitasuguliwa, na kuoshwa kwa maji.
29 Kila mwana mume miongoni mwa makuhani atakula katika hiyo; ni takatifu sana.
30 Wala haitaliwa sadaka ya dhambi yo yote, ambayo damu yake yo yote ililetwa ndani ya hema ya kukutania, ili kufanya upatanisho katika mahali patakatifu; itachomwa moto.

Walawi 7


1 Na sheria ya hiyo sadaka ya hatia ni hii; ni takatifu sana.
2 Wataichinja sadaka ya hatia pale pale waichinjapo sadaka ya kuteketezwa; na damu yake atainyunyiza katika madhabahu pande zote.
3 Katika sadaka hiyo atasongeza mafuta yake yote; yaani, mkia wake wenye mafuta, na mafuta yafunikayo matumbo,
4 na figo zake mbili, na mafuta yaliyoshikamana nazo, yaliyo karibu na kiuno chake, na kitambi kilicho katika ini, pamoja na figo zake mbili, hayo yote atayaondoa;
5 na kuhani atayateketeza juu ya madhabahu, kuwa dhabihu kwa Bwana kwa njia ya moto; ni sadaka ya hatia.
6 Kila mtu mume miongoni mwa makuhani atakula katika sadaka hiyo; italiwa katika mahali patakatifu; ni takatifu sana.
7 Kama hiyo sadaka ya dhambi ilivyo, na sadaka ya hatia ni vivyo; sheria yake ni moja; huyo kuhani afanyaye upatanisho kwayo, ndiye atakayekuwa nayo.
8 Tena kuhani atakayesongeza sadaka ya kuteketezwa ya mtu awaye yote, huyo kuhani atatwaa awe nayo ngozi ya huyo mnyama wa sadaka ya kuteketezwa aliyemsongeza.
9 Na kila sadaka ya unga iliyookwa mekoni, na yote yaliyoandaliwa chunguni, au kaangoni, yote yatakuwa ya huyo kuhani aliyeyasongeza.
10 Na kila sadaka ya unga, kama umeandaliwa na mafuta, au kama ni mkavu, watautwaa wana wote wa Haruni kuutumia, kila mtu sawasawa.
11 Na sheria ya matoleo ya sadaka za amani, atakazosongeza mtu kwa Bwana, ni hii.
12 Kwamba aitoa kwa ajili ya shukrani, ndipo atakaposongeza pamoja na hiyo sadaka ya shukrani mikate isiyotiwa chachu, iliyoandaliwa na mafuta, na mikate ya kaki isiyochachwa iliyopakwa mafuta, na mikate ya unga mwembamba uliolowama mafuta.
13 Ataleta matoleo yake, pamoja na mikate iliyotiwa chachu, na pamoja na sadaka zake za amani, kwa ajili ya shukrani.
14 Na katika hayo atasongeza kimoja katika kila toleo kiwe sadaka ya kuinuliwa kwa Bwana; itakuwa ni ya kuhani atakayeinyunyiza hiyo damu ya sadaka za amani.
15 Na hiyo nyama ya sadaka zake za amani zilizochinjwa kwa ajili ya shukrani italiwa siku iyo hiyo ya matoleo yake; asisaze yo yote hata asubuhi.
16 Lakini kwamba hii sadaka ya matoleo yake ni nadhiri, au sadaka ya hiari, italiwa siku hiyo aliyoileta sadaka yake; kisha siku ya pili yake kitakachosalia kitaliwa;
17 lakini hicho kitakachosalia, katika hizo nyama za sadaka, hata siku ya tatu kitachomwa moto.
18 Tena kama nyama yo yote katika hiyo dhabihu yake ya sadaka za amani ikiliwa siku ya tatu, haitakubaliwa, wala haitahesabiwa kwake huyo mwenye kuisongeza; itakuwa ni machukizo, na mtu atakayeila atachukua uovu wake.
19 Tena nyama itakayogusa kitu kilicho najisi haitaliwa; itachomwa moto. Na katika hiyo nyama nyingine, kila mtu aliye safi ana ruhusa kuila;
20 lakini mtu huyo atakayekula katika nyama ya sadaka za amani, ambazo ni za Bwana, na unajisi wake akiwa nao juu yake, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.
21 Kisha mtu awaye yote atakapogusa kitu cho chote kilicho najisi, uchafu wa binadamu, au mnyama aliye najisi, au machukizo yo yote yaliyo najisi, kisha akala nyama ya dhabihu ya sadaka za amani, ambazo ni za Bwana, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.
22 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
23 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Msile mafuta yo yote, ya ng'ombe, wala ya kondoo, wala ya mbuzi.
24 Tena mafuta ya mnyama afaye mwenyewe, na mafuta ya mnyama aliyeraruliwa na wanyama, mna ruhusa kuyatumia kwa ajili ya matumizi mengine; lakini msiyale kabisa.
25 Kwani huyo mtu atakayekula mafuta ya mnyama, ambaye ni katika wanyama ambao watu husongeza sadaka kwa Bwana kwa moto, mtu huyo atakayekula mafuta hayo atakatiliwa mbali na watu wake.
26 Tena msiile damu yo yote, ama ya ndege, ama ya mnyama, katika nyumba zenu zote.
27 Mtu ye yote alaye damu, mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake.
28 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
29 Nena na wana wa Israeli uwaambie, Yeye asongezaye dhabihu yake ya sadaka za amani kwa Bwana, atamletea Bwana matoleo yake, kutoka katika ile dhabihu ya sadaka zake za amani;
30 mikono yake mwenyewe itamletea hizo sadaka za kusongezwa kwa moto; mafuta yake pamoja na kidari atayaleta, ili kwamba hicho kidari kitikiswe kuwa sadaka ya kutikiswa mbele ya Bwana.
31 Kuhani atayateketeza hayo mafuta juu ya madhabahu; lakini hicho kidari kitakuwa cha Haruni na cha wanawe.
32 Mguu wa nyuma wa upande wa kuume mtampa kuhani kuwa sadaka ya kuinuliwa kutoka katika hizo sadaka zenu za amani.
33 Katika wana wa Haruni, huyo atakayeisongeza damu ya sadaka za amani, na mafuta yake, yeye atapata mguu wa nyuma wa upande wa kuume kuwa sehemu yake.
34 Kwa maana, hicho kidari cha kutikiswa, na huo mguu wa kuinuliwa, nimevitwaa kwa wana wa Israeli, katika dhabihu zao za sadaka za amani, nami nimempa Haruni kuhani na wanawe, kuwa haki yao ya milele kutoka kwa wana wa Israeli.
35 Hii ndiyo sehemu ya Haruni, na sehemu ya wanawe, katika kutiwa mafuta kwao, katika hizo dhabihu zisongezwazo kwa Bwana kwa njia ya moto, siku hiyo aliyowaweka ili wamtumikie Bwana katika kazi ya ukuhani;
36 sehemu ambayo Bwana aliagiza wapewe na wana wa Israeli, siku hiyo aliyowatia mafuta. Ni haki yao ya milele katika vizazi vyao vyote.
37 Sheria ya sadaka ya kuteketezwa ni hii, na ya sadaka ya unga, na ya sadaka ya dhambi, na ya sadaka ya hatia, na ya kuwekwa wakfu, na ya sadaka za amani;
38 ambazo Bwana alimwagiza Musa katika mlima wa Sinai, siku hiyo aliyowaagiza wana wa Israeli wamtolee Bwana matoleo yao, huko katika jangwa la Sinai.

Walawi 8


1 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Mtwae Haruni, na wanawe pamoja naye, na yale mavazi, na mafuta ya kutia, na ng'ombe mume wa sadaka ya dhambi, na kondoo waume wawili, na kikapu cha mikate isiyotiwa chachu;
3 kisha ukutanishe mkutano wote hapo mlangoni pa hema ya kukutania.
4 Basi Musa akafanya kama alivyoambiwa na Bwana; na huo mkutano ulikutanishwa mlangoni pa hema ya kukutania.
5 Musa akawaambia mkutano, Neno aliloliagiza Bwana kwamba lifanywe, ni hili.
6 Basi Musa akawaleta Haruni na wanawe, akawaosha kwa maji.
7 Kisha akamvika Haruni ile kanzu, na kumfunga mshipi, na kumvika joho, na kumvika naivera, na kumfunga huo mshipi wa kazi ya mstadi wa naivera na kumfunga naivera kwa huo mshipi.
8 Kisha akamtia kile kifuko cha kifuani; akatia hizo Urimu na Thumimu katika hicho kifuko cha kifuani.
9 Akamvika na kile kilemba kichwani mwake; na juu ya kilemba, upande wa mbele, akakitia kile kipande cha dhahabu, hiyo taji takatifu; kama Bwana alivyomwagiza Musa.
10 Kisha Musa akatwaa hayo mafuta matakatifu ya kutia, akatia mafuta maskani, na vyote vilivyokuwamo, na kuvitakasa.
11 Kisha akanyunyiza hayo mafuta juu ya madhabahu mara saba, na kuitia mafuta madhabahu na vyombo vyake vyote, na birika na tako lake, ili kuvitakasa.
12 Kisha akamimina mafuta hayo ya kutia kichwani mwake Haruni, na kumtia mafuta, ili amtakase.
13 Kisha Musa akawaleta wana wa Haruni, na kuwavika kanzu, na kuwafunga mishipi, na kuwavika vilemba; kama Bwana alivyomwagiza Musa.
14 Kisha akamleta yule ng'ombe mume wa sadaka ya dhambi; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao katika kichwa cha huyo ng'ombe wa sadaka ya dhambi.
15 Kisha akamchinja; na Musa akaitwaa damu yake, akaitia katika pembe za madhabahu pande zote kwa kidole chake, akaitakasa madhabahu, kisha akaimwaga hiyo damu hapo chini ya madhabahu, na kuitakasa, ili afanye upatanisho kwa ajili yake.
16 Kisha akayatwaa mafuta yote yaliyokuwa katika matumbo yake, na kitambi kilichokuwa katika ini, na figo zake mbili, na mafuta yake, na Musa akayateketeza juu ya madhabahu.
17 Lakini huyo ng'ombe mwenyewe, na ngozi yake, na nyama yake, na mavi yake, akayachoma moto nje ya marago; vile vile kama Bwana alivyomwagiza Musa.
18 Kisha akamsongeza yule kondoo mume wa sadaka ya kuteketezwa; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao kichwani mwa huyo kondoo.
19 Kisha akamchinja; na Musa akainyunyiza damu yake katika madhabahu pande zote.
20 Kisha akamkata kondoo vipande vyake; na Musa akateketeza kichwa, na vile vipande, na mafuta.
21 Kisha akayaosha matumbo na miguu yake kwa maji; na Musa akamteketeza huyo kondoo wote juu ya madhabahu; ilikuwa ni sadaka ya kuteketezwa kuwa harufu ya kupendeza; ilikuwa ni sadaka iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto; kama Bwana alivyomwagiza Musa.
22 Kisha akamsongeza kondoo mume wa pili, huyo kondoo wa kuwaweka wakfu; na Haruni na wanawe wakaweka mikono yao kichwani mwa huyo kondoo.
23 Kisha akamchinja; na Musa akatwaa katika damu yake, na kuitia katika ncha ya sikio la kuume la Haruni, na katika chanda chake cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole cha gumba cha guu lake la kuume.
24 Kisha akawaleta wana wa Haruni, na Musa akaitia hiyo damu katika ncha za masikio ya kuume, na katika vyanda vya gumba vya mikono yao ya kuume, na katika vidole vya gumba vya maguu yao ya kuume; kisha Musa akainyunyiza hiyo damu katika madhabahu pande zote.
25 Kisha akayatwaa hayo mafuta, na mkia wenye mafuta, na mafuta yote yaliyokuwa katika matumbo, na kitambi cha ini, na figo mbili, na mafuta yake, na mguu wa nyuma wa upande wa kuume;
26 kisha katika kikapu cha mikate isiyotiwa chachu, kilichokuwa pale mbele za Bwana, akatwaa mkate mmoja usiochachwa, na mkate mmoja ulioandaliwa na mafuta na kaki moja nyembamba, akaiweka juu ya mafuta, na juu ya huo mguu wa nyuma wa upande wa kuume;
27 kisha akaweka vyote katika mikono ya Haruni, na katika mikono ya wanawe, na kuvitikisa huku na huku viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana.
28 Kisha Musa akavitwaa tena mikononi mwao, na kuviteketeza juu ya madhabahu, juu ya hiyo sadaka ya kuteketezwa vilikuwa vya kuwaweka wakfu, ni harufu nzuri; ilikuwa dhabihu iliyosongezwa kwa Bwana kwa moto.
29 Kisha Musa akakitwaa kile kidari, akakitikisa huku na huku, kiwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana; ni sehemu ya Musa katika huyo kondoo mume wa kuwaweka wakfu; kama Bwana alivyomwagiza Musa.
30 Kisha Musa akatwaa baadhi ya mafuta ya kutia, na ya damu iliyokuwa pale juu ya madhabahu, na kumnyunyizia Haruni, katika mavazi yake, na wanawe, katika mavazi yao, pamoja naye; akamtakasa Haruni, na mavazi yake, na wanawe, na mavazi ya wanawe, pamoja naye.
31 Kisha Musa akawaambia huyo Haruni na wanawe, Tokoseni hiyo nyama mlangoni pa hema ya kukutania; mkaile pale pale, na hiyo mikate iliyo katika kile kikapu cha kuwaweka wakfu, kama nilivyoagizwa kusema, Haruni na wanawe wataila.
32 Nacho kitakachosalia katika hiyo nyama na mikate mtakichoma moto.
33 Wala msitoke nje mlangoni pa hema ya kukutania muda wa siku saba, hata siku za kuwekwa wakfu kwenu zitakapotimia; kwa kuwa atawaweka muda wa siku saba.
34 Vile vile kama vilivyotendeka siku ya leo, ni vivyo Bwana alivyoagiza kufanywa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu.
35 Nanyi mtakaa mlangoni pa hema ya kukutania muda wa siku saba mchana na usiku, na kuulinda ulinzi wa Bwana ili kwamba msife; kwani ndivyo nilivyoagizwa.
36 Basi Haruni na wanawe wakafanya mambo hayo yote Bwana aliyoyaagiza kwa mkono wa Musa.

Walawi 9


1 Basi ilikuwa siku ya nane, Musa akawaita Haruni na wanawe, pamoja na wazee wa Israeli;
2 akamwambia Haruni, Twaa wewe mwana-ng'ombe mume awe sadaka ya dhambi, na kondoo mume wa sadaka ya kuteketezwa, wakamilifu, ukawasongeze mbele ya Bwana.
3 Nawe utawaambia wana wa Israeli, ukisema, Twaeni mbuzi mume awe sadaka ya dhambi; na mwana-ng'ombe, na mwana-kondoo, wote wa mwaka wa kwanza, wakamilifu, kwa sadaka ya kuteketezwa;
4 na ng'ombe mume, na kondoo mume, kwa sadaka za amani, ili kuwachinja mbele za Bwana; na sadaka ya unga uliochanganywa na mafuta; kwa maana, Bwana hivi leo atawatokea.
5 Nao wakayaleta hayo yaliyoagizwa na Musa wakayaweka mbele ya hema ya kukutania; kisha mkutano wote ukakaribia wakasimama mbele za Bwana.
6 Kisha Musa akasema, Neno aliloliagiza Bwana kwamba mlifanye ni hili; na huo utukufu wa Bwana utawatokea.
7 Musa akamwambia Haruni, Ikaribie madhabahu, uitoe sadaka yako ya dhambi, na sadaka yako ya kuteketezwa, ukafanye upatanisho kwa ajili ya nafsi yako, na kwa ajili ya watu; nawe uitoe hiyo dhabihu ya watu, ukafanye upatanisho kwa ajili yao; kama Bwana alivyoagiza.
8 Basi Haruni akakaribia madhabahuni, akamchinja huyo mwana-ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliyekuwa kwa ajili ya nafsi yake.
9 Kisha wana wa Haruni wakamsongezea Haruni ile damu; naye akatia kidole chake katika damu, na kuitia katika pembe za madhabahu, kisha akaimwaga hiyo damu hapo chini ya madhabahu;
10 lakini mafuta, na figo, na kitambi kilichotoka katika ini ya hiyo sadaka ya dhambi, akaviteketeza juu ya madhabahu, kama Bwana alivyomwagiza Musa.
11 Na nyama, na ngozi akazichoma moto nje ya marago.
12 Naye akaichinja sadaka ya kuteketezwa; na wanawe Haruni wakamsongezea ile damu, naye akainyunyiza katika madhabahu pande zote.
13 Nao wakamletea sadaka ya kuteketezwa kipande kwa kipande, na kichwa; naye akaviteketeza juu ya madhabahu.
14 Kisha akaosha matumbo, na miguu na kuiteketeza juu ya hiyo sadaka ya kuteketezwa madhabahuni.
15 Kisha akaisongeza dhabihu ya watu, akamtwaa mbuzi wa sadaka ya dhambi aliyekuwa kwa hao watu, na kumchinja, na kumtoa kwa ajili ya dhambi kama yule wa kwanza.
16 Kisha akaisongeza sadaka ya kuteketezwa, na kuitoa sawasawa na sheria.
17 Kisha akaisongeza sadaka ya unga, na kutwaa konzi humo, na kuiteketeza juu ya madhabahu, pamoja na sadaka ya kuteketezwa ya asubuhi.
18 Huyo ng'ombe mume naye akamchinja, na huyo kondoo mume pia, dhabihu ya sadaka za amani, zilizokuwa kwa ajili ya watu; na wanawe Haruni wakamsongezea ile damu, naye akainyunyiza katika madhabahu pande zote,
19 na mafuta ya ng'ombe; na ya kondoo, mkia wake wa mafuta, na hayo yafunikayo matumbo, na figo zake, na kitambi cha ini;
20 nao wakayaweka hayo mafuta juu ya vidari, naye akayateketeza mafuta juu ya madhabahu;
21 na vile vidari, na mguu wa nyuma wa upande wa kuume, Haruni akavitikisa huku na huku viwe sadaka ya kutikiswa mbele ya Bwana; kama Musa alivyoagiza.
22 Kisha Haruni akainua mikono yake na kuielekeza kwa hao watu, akawabariki; kisha akashuka akisha isongeza sadaka ya dhambi, na sadaka ya kuteketezwa, na sadaka za amani.
23 Kisha Musa na Haruni wakaingia ndani ya hema ya kukutania, kisha wakatoka nje, na kuwabarikia watu; na huo utukufu wa Bwana ukawatokea watu wote.
24 Kisha moto ukatoka hapo mbele za Bwana, na kuiteketeza sadaka ya kuteketezwa, na yale mafuta juu ya madhabahu; watu wote walipouona huo moto wakapiga kelele wakainama kifudifudi.

Walawi 10


1 Na Nadabu na Abihu, wana wa Haruni, wakatwaa kila mtu chetezo chake, wakatia moto ndani yake, wakatia na uvumba, nao wakatoa moto wa kigeni mbele ya Bwana, ambao yeye hakuwaagiza.
2 Kisha moto ukatoka hapo mbele za Bwana, nao ukawala, nao wakafa mbele za Bwana.
3 Ndipo Musa akamwambia Haruni, Jambo hili ni hilo Bwana alilolinena, akisema, Nitatakaswa mimi katika hao wanikaribiao, nami nitatukuzwa mbele ya watu hao wote. Haruni akanyamaza kimya.
4 Musa akawaita Mishaeli na Elisafani, wana wa Uzieli mjombaye Haruni, na kuwaambia, Njoni karibu, mwachukue hawa ndugu zenu, mkawaondoe hapa mbele ya maskani, mwende nao nje ya marago.
5 Basi wakaja karibu, na kuwachukua, hali wamevaa nguo zao, wakawachukua nje ya marago; kama Musa alivyosema.
6 Kisha Musa akamwambia Haruni na wanawe Eleazari na Ithamari, Msiache wazi nywele za vichwani mwenu, wala msiyararue mavao yenu; ili kwamba msife, tena asiukasirikie mkutano wote; lakini ndugu zenu, nyumba yote ya Israeli, na waomboleze kwa ajili ya hicho kichomo alichowasha Bwana.
7 Wala hamtatoka nje mlangoni mwa hema ya kukutania, msije mkafa; kwa sababu mafuta ya kutiwa ya Bwana ya juu yenu. Nao wakafanya kama hilo neno la Musa.
8 Kisha Bwana akanena na Haruni, na kumwambia,
9 Usinywe divai wala kileo cho chote, wewe, wala wanao pamoja nawe, hapo mwingiapo ndani ya hema ya kukutania, ili kwamba msife; amri hii itakuwa ni amri ya milele katika vizazi vyenu;
10 kisha, mpate kupambanua kati ya yaliyo matakatifu na hayo yaliyo ya siku zote, na kati ya yaliyo najisi na hayo yaliyo safi;
11 tena mpate kuwafundisha wana wa Israeli amri hizi zote ambazo Bwana amewaambia kwa mkono wa Musa.
12 Kisha Musa akanena na Haruni, na Eleazari, na Ithamari, hao wanawe waliobaki, Twaeni hiyo sadaka ya unga iliyosalia katika kafara za Bwana zilizotolewa kwa moto, mkaile pasipo kutiwa chachu, pale karibu na madhabahu; kwa kuwa ni takatifu sana;
13 nanyi mtaila katika mahali patakatifu, kwa sababu ni haki yako, na haki ya wanao, katika hizo kafara zisongezwazo kwa Bwana kwa moto; kwani ni hivyo nilivyoagizwa.
14 Na kidari cha kutikiswa, na mguu wa kuinuliwa, mtavila katika mahali palipo safi; wewe, na wanao, na binti zako pamoja nawe; kwa maana vimetolewa kuwa ni haki yako, na haki ya wanao, katika zile kafara za sadaka za amani za wana wa Israeli.
15 Mguu wa kuinuliwa, na kidari cha kutikiswa, Watavileta pamoja na dhabihu zisongezwazo kwa njia ya moto, za hayo mafuta ili kuvitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana; kisha vitakuwa ni vyako wewe, na vya wanao pamoja nawe, ni haki yenu milele, kama Bwana alivyoagiza.
16 Kisha Musa akamtafuta sana huyo mbuzi wa sadaka ya dhambi, naye, tazama, alikuwa amekwisha kuchomwa moto; naye akawakasirikia hao Eleazari na Ithamari, wana wa Haruni, hao waliobaki, akawaambia,
17 Kwa nini hamkula hiyo sadaka ya dhambi katika mahali patakatifu, kwa kuwa ni takatifu sana, naye amewapa ninyi ili kuuchukua uovu wa mkutano, na kuwafanyia upatanisho mbele za Bwana?
18 Angalieni, hiyo damu yake haikuletwa ndani ya mahali patakatifu; iliwapasa kuila ndani ya mahali patakatifu, kama nilivyowaagiza.
19 Haruni akamwambia Musa, Angalia, hivi leo wamesongeza sadaka yao ya dhambi, na sadaka yao ya kuteketezwa, mbele za Bwana; kisha mambo kama haya yamenipata; tena kama ningalikula hiyo sadaka ya dhambi hivi leo, je! Lingekuwa ni jambo la kupendeza mbele za macho ya Bwana?
20 Naye Musa aliposikia hayo, yakampendeza.

Walawi 11


1 Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
2 Neneni na wana wa Israeli, mkiwaambia, Wanyama hawa ndio wanyama wenye uhai mtakaowala, katika hayawani wote walio juu ya nchi.
3 Kila mnyama mwenye kwato katika miguu yake, mwenye miguu ya kupasuka kati, mwenye kucheua, katika hayawani, hao ndio mtakaowala.
4 Pamoja na hayo, wanyama hawa hamtawala katika wale wenye kucheua, na katika wale walio na kwato; ngamia, kwa sababu yuacheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu.
5 Na wibari, kwa sababu yeye hucheua lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu.
6 Na sungura, kwa sababu hucheua, lakini hana kwato, yeye ni najisi kwenu.
7 Na nguruwe, kwa sababu yeye anazo kwato, ni mwenye miguu iliyopasuka kati, lakini hacheui, yeye ni najisi kwenu.
8 Msiile nyama yao, wala msiiguse mizoga yao; hao ni najisi kwenu.
9 Katika hao wote walio ndani ya maji mtakula hawa; kila aliye na mapezi na magamba, ndani ya hayo maji, na ndani ya bahari, na ndani ya mito, mtakula hao.
10 Na hao wote wasio na mapezi na magamba, ndani ya bahari, na ndani ya mito, katika hao waendao majini, na katika wote wenye uhai, waliomo majini, hao ni machukizo kwenu,
11 watakuwa machukizo kwenu; msiile nyama yao, na mizoga yao itakuwa machukizo kwenu.
12 Kila asiye na mapezi wala magamba aliye ndani ya maji ni machukizo kwenu.
13 Kisha katika ndege hawa watakuwa ni machukizo kwenu; hawataliwa, ndio machukizo; tai, na furukombe, na kipungu;
14 na mwewe, na kozi kwa aina zake,
15 na kila kunguru kwa aina zake;
16 na mbuni, na kirukanjia, na dudumizi, na kipanga kwa aina zake;
17 na bundi, na mnandi, na bundi mkubwa;
18 na mumbi, na mwari, na mderi;
19 na korongo, na koikoi kwa aina zake, na hudihudi, na popo.
20 Tena vyote vitambaavyo vyenye mabawa viendavyo kwa miguu minne, hivi ni machukizo kwenu.
21 Pamoja na hayo, hivi vitambaavyo vyenye mabawa viendavyo kwa miguu minne ni halali kula, hao walio na miguu mirefu, ya kurukia juu ya nchi;
22 katika hao mna ruhusa kuwala; nzige kwa aina zake, na nzige kuu kwa aina zake, na panzi kwa aina zake, na parare kwa aina zake.
23 Lakini vyote vitambaavyo vyenye mabawa, vilivyo na miguu minne, ni machukizo kwenu.
24 Nanyi mtakuwa najisi kwa wanyama hao; kila atakayegusa mzoga wao atakuwa ni najisi hata jioni;
25 na mtu awaye yote atakayechukua cho chote cha mizoga yao atafua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni.
26 Kila mnyama aliyepasuliwa ukwato, naye hana kwato mbili, wala hacheui, huyo ni najisi kwenu; kila agusaye wanyama hao atakuwa ni najisi.
27 Tena kila mnyama aendaye kwa vitanga vyake, katika hao wanyama wote waendao kwa miguu minne, hao ni najisi kwenu; awaye yote atakayegusa mizoga yao, atakuwa ni najisi hata jioni.
28 Na huyo atakayechukua mzoga wa wanyama hao atafua nguo zake, naye atakuwa ni najisi hata jioni; hao ni najisi kwenu
29 Tena katika vitu vile vitambaavyo, vitambaavyo juu ya nchi, hivi ni najisi kwenu; kicheche, na panya, na mjombakaka, kwa aina zake,
30 na guruguru na kenge, na mjusi na goromoe, na lumbwi.
31 Wanyama hao ndio walio najisi kwenu katika hao watambaao; awaye yote atakayewagusa, wakiisha kufa, atakuwa ni najisi hata jioni.
32 Tena kitu cho chote, wanyama hao mmojawapo atakachokiangukia, wakiisha kufa, kitakuwa ni najisi; kwamba ni chombo cha mti, au nguo, au ngozi, au gunia, chombo cho chote kitakachoangukiwa, ambacho ni chombo cha kufanyia kazi yo yote, lazima kitiwe ndani ya maji, nacho kitakuwa ni najisi hata jioni; ndipo kitakapokuwa ni safi.
33 Na kila chombo cha udongo, wanyama hao mmojawapo atakachokiangukia, kila kilichomo ndani yake kitakuwa ni najisi, na hicho chombo kitavunjwa.
34 Kila chakula kilichomo, ambacho ni kuliwa, hicho ambacho maji hutumiwa juu yake, kitakuwa ni najisi; na kila kinyweo ambacho ni cha kunywewa, kilichomo katika chombo kama hicho, kitakuwa ni najisi.
35 Na kila kitu kitakachoangukiwa na kipande cho chote cha mizoga yao kitakuwa najisi; kwamba ni tanuru, au meko ya vyungu, kitavunjwa vipande vipande; ni najisi vitu hivyo, navyo vitakuwa najisi kwenu.
36 Pamoja na hayo, chemchemi, au shimo, ambamo maji yakusanyika, vitakuwa ni safi; lakini hicho kitakachogusa mizoga yao kitakuwa ni najisi.
37 Na kipande cho chote cha mzoga kikiwa kimeangukia mbegu za kupandwa zitakazopandwa, zitakuwa safi.
38 Lakini kwamba hizo mbegu zilitiwa maji na cho chote cha mizoga yao kuziangukia, ni najisi kwenu.
39 Kama akifa mnyama awaye yote, ambaye mna ruhusa kumla, yeye anayeugusa mzoga wake atakuwa najisi hata jioni.
40 Na yeye atakayekula nyama ya mzoga wake atafua nguo zake, naye atakuwa najisi hata jioni; yeye atakayeuchukua mzoga wake atafua nguo zake, naye atakuwa ni najisi hata jioni.
41 Na kila kitu kitambaacho juu ya nchi ni machukizo; hakitaliwa.
42 Kila aendaye kwa tumbo lake, na kila aendaye kwa miguu minne, na kila aendaye kwa miguu mingi, maana, ni vyote vyenye kutambaa vitambaavyo juu ya nchi, hamtavila, kwa kuwa ni machukizo.
43 Msifanye nafsi zenu kuwa ni chukizo kwa kitu cho chote chenye kutambaa, kitambaacho, wala msifanye nafsi zenu kuwa ni najisi kwa vitu hivyo, mkajipatia uchafu kwa hivyo.
44 Kwa kuwa mimi ni Bwana, Mungu wenu; takaseni nafsi zenu basi; iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu; wala msitie uchafu nafsi zenu kwa kitu kitambaacho cha aina yo yote, kiendacho juu ya nchi.
45 Kwa kuwa mimi ni Bwana niliyewaleta kutoka nchi ya Misri, ili kwamba niwe Mungu wenu; basi mtakuwa watakatifu, kwa kuwa mimi ni Mtakatifu.
46 Hii ndiyo sheria katika hao wanyama, na ndege, na kila kiumbe kilicho hai, kiendacho ndani ya maji, na kila kiumbe kitambaacho juu ya nchi;
47 ili kupambanua kati ya hao walio najisi na hao walio safi, na kati ya kiumbe kilicho hai ambacho chaliwa, na hicho kilicho hai ambacho hakiliwi.

Walawi 12


1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena na hao wana wa Israeli, uwaambie, Mwanamke akitunga mimba na kuzaa mtoto mume, ndipo atakuwa yu najisi siku saba; kama katika siku za kutengwa kwake kwa ajili ya hedhi, ndivyo atakavyokuwa najisi.
3 Siku nane mtoto atatahiriwa govi ya zunga lake.
4 Na huyo mwanamke atakaa katika damu ya kutakata kwake siku thelathini na tatu; asiguse kitu kilicho kitakatifu, wala asiingie mahali patakatifu, hata siku hizo za kutakata kwake zitakapotimia.
5 Lakini kwamba amezaa mtoto mke ndipo atakuwa najisi juma mbili, kama katika kutengwa kwake; naye atakaa katika damu ya kutakata kwake muda wa siku sitini na sita.
6 Kisha hizo siku za kutakaswa kwake zitakapotimia, kwa ajili ya mwana, au kwa ajili ya binti, ataleta mwana-kondoo wa mwaka mmoja kuwa sadaka ya kuteketezwa na kinda la njiwa, au hua, kuwa sadaka ya dhambi, awalete mlangoni pa hema ya kukutania, na kumpa kuhani;
7 na yeye atawasongeza mbele za Bwana, na kufanya upatanisho kwa ajili yake; naye atatakasika na jicho la damu yake. Hii ndiyo amri yake huyo azaaye, kwamba ni mtoto mume au mke.
8 Kama mali yake huyo mwanamke haimfikilii mwana-kondoo, hapo ndipo atakapochukua hua wawili, au makinda mawili ya njiwa; mmoja kuwa sadaka ya kuteketezwa, na wa pili kuwa sadaka ya dhambi; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi.

Walawi 13


1 Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
2 Mtu atakapokuwa na kivimbe katika ngozi ya mwili wake, au kikoko, au kipaku king'aacho, nalo likawa pigo la ukoma katika ngozi ya mwili wake, ndipo atakapoletwa kwa Haruni kuhani, au kwa wanawe, makuhani mmojawapo;
3 na huyo kuhani ataliangalia hilo pigo lililo katika ngozi ya mwili; na kwamba malaika yaliyo katika hilo pigo yamegeuka kuwa meupe, na hilo pigo kuonekana kwake limeingia ndani kuliko ile ngozi ya mwili wake, ni pigo la ukoma hilo; na kuhani atamwangalia na kusema kuwa yu mwenye unajisi.
4 Na hicho kipaku king'aacho, kwamba ni cheupe katika ngozi ya mwili wake, na kuonekana kwake si shimo la kuingia ndani kuliko ngozi, na malaika hayakugeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba huyo aliye na hilo pigo;
5 kisha kuhani atamwangalia siku ya saba; naye akiona ya kuwa pigo limeshangaa, na pigo halikwendelea mbele katika ngozi yake, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba tena;
6 kisha siku ya saba kuhani atamwangalia tena; na tazama, ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, wala pigo halikwendelea mbele katika ngozi yake, ndipo kuhani atasema kuwa yu safi; ni kikoko; naye atazifua nguo zake, kisha atakuwa yu safi.
7 Lakini kwamba kikoko kimeenea katika ngozi yake baada ya kuonyesha nafsi yake kwa kuhani kwa kupata kutakaswa kwake ataonyesha nafsi yake tena kwa kuhani;
8 na kuhani ataangalia, na tazama ikiwa hicho kikoko kimeenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kuwa yu najisi; ni ukoma.
9 Pigo la ukoma litakapokuwa katika mtu, ndipo ataletwa kwa kuhani;
10 na kuhani ataangalia, na tazama, ikiwa pana kivimbe cheupe katika ngozi yake, na malaika yamegeuzwa kuwa meupe, tena ikiwa pana nyama mbichi iliyomea katika kile kivimbe,
11 ni ukoma wa zamani ulio katika ngozi ya mwili wake, na kuhani atasema kuwa yu najisi; hatamweka mahali, kwa kuwa yeye yuna unajisi.
12 Tena kwamba huo ukoma ukitokeza katika ngozi yake, na ukoma ukamwenea ngozi yote, tangu kichwa hata miguuni, kama aonavyo kuhani;
13 ndipo huyo kuhani ataangalia; na tazama, ikiwa ukoma umemwenea mwili wake wote, atasema kuwa yu safi huyo aliye na hilo pigo umegeuka kuwa mweupe wote; yeye ni safi.
14 Lakini po pote itakapoonekana nyama mbichi kwake mtu huyo, atakuwa yu najisi.
15 Kuhani ataiangalia hiyo nyama mbichi, naye atasema kuwa yu najisi; ile nyama mbichi ni najisi; ni ukoma.
16 Au kama hiyo nyama mbichi iligeuka tena, na kugeuzwa kuwa nyeupe, ndipo atamwendea kuhani,
17 na huyo kuhani atamwangalia; na tazama, ikiwa hilo pigo limegeuzwa kuwa jeupe, ndipo huyo kuhani atasema kuwa yu safi huyo aliyekuwa na pigo; yeye yu safi.
18 Tena mwili wa mtu utakapokuwa na jipu katika ngozi yake, nalo limepoa,
19 na mahali palipokuwa na lile jipu pana kivimbe cheupe, au kipaku king'aacho, cheupe lakini chekundu kidogo, ndipo atamwonyesha kuhani mahali hapo;
20 na kuhani ataangalia, na tazama, kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, na malaika yakiwa yamegeuka kuwa meupe, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi; ni pigo la ukoma limetokea katika hilo jipu.
21 Lakini kuhani akipaangalia, na tazama hamna malaika meupe ndani yake, wala hapana pa kuingia ndani kuliko ile ngozi, lakini paanza kufifia, ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba;
22 na kwamba pameenea katika ngozi, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo.
23 Lakini ikiwa kipaku hicho king'aacho kimeshangaa pale pale, wala hakienei, ni kovu ya jipu; na kuhani atasema kwamba yu safi.
24 Au mwili wa mtu ukiwa una mahali katika ngozi yake penye moto, na hiyo nyama iliyomea pale penye moto, kama kikiwa kipaku chekundu kidogo, au cheupe;
25 ndipo kuhani atapaangalia; na tazama, yakiwa malaika yaliyo katika kile kipaku yamegeuka kuwa meupe, na kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe; ni ukoma, umetokea katika mahali penye moto; na kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo la ukoma.
26 Lakini kuhani akipaangalia, na tazama, malaika meupe hamna katika hicho kipaku king'aacho, nacho hakikuingia ndani kuliko ngozi, lakini chafifia; ndipo kuhani atamweka mahali muda wa siku saba;
27 na kuhani atamwangalia siku ya saba; kama kimeenea katika ngozi, ndipo huyo kuhani atasema kwamba yu najisi; hili ni pigo la ukoma.
28 Na kama hicho kipaku kikishangaa pale pale, wala hakikuenea katika ngozi, lakini kimefifia; ni kufura kwake pale penye moto, na kuhani atasema kwamba yu safi; kwa kuwa ni kovu la kuwasha hili.
29 Tena mtu, mume au mke, akiwa na pigo juu ya kichwa, au katika ndevu zake,
30 ndipo kuhani ataliangalia hilo pigo; na tazama, kwamba kumeonekana kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, tena zikiwamo nywele za rangi ya manjano kisha nyembamba, ndipo kuhani atasema kwamba yu najisi, maana, ni kipwepwe, ni ukoma wa kichwa, au wa ndevu.
31 Tena kuhani akiliangalia lile pigo la kipwepwe, na tazama, kwamba kumeonekana si kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe, wala hamna nywele nyeusi ndani yake, ndipo kuhani atamweka mahali huyo aliye na pigo la kipwepwe muda wa siku saba;
32 na siku ya saba kuhani ataliangalia hilo pigo; na ikiwa hicho kipwepwe hakikuenea, wala hamna nywele za rangi ya manjano ndani yake, na kwamba kipwepwe hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi yenyewe,
33 ndipo huyo mtu atanyolewa, lakini hicho kipwepwe hatakinyoa; na kuhani atamweka mahali huyo aliye na kipwepwe muda wa siku saba tena;
34 na siku ya saba kuhani atakiangalia hicho kipwepwe, na tazama, ikiwa kipwepwe hakikuenea katika ngozi yake, wala hakionekani kuingia ndani kuliko ngozi; ndipo huyo kuhani atasema kwamba yu safi; naye atazifua nguo zake, naye atakuwa yu safi.
35 Lakini hicho kipwepwe kama kikienea katika ngozi yake baada ya kutakasika kwake;
36 ndipo kuhani atamwangalia; na ikiwa hicho kipwepwe kimeenea katika ngozi yake, kuhani hatatafuta hizo nywele za rangi ya manjano; yeye yu najisi.
37 Lakini akiona ya kuwa hicho kipwepwe kimeshangaa, na nywele nyeusi zimemea humo; hicho kipwepwe kimepoa, naye yu safi, na huyo kuhani atasema kwamba yu safi.
38 Mtu, mume au mke, atakapokuwa na vipaku ving'aavyo katika ngozi ya mwili, vipaku ving'aavyo vyeupe;
39 ndipo kuhani ataangalia; na tazama, ikiwa vile vipaku ving'aavyo vilivyo katika ngozi ya mwili wake ni vyeupe kidogo; ni mba hivyo, imetokea katika ngozi; yeye yu safi.
40 Kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani mwake, yeye ni mwenye upaa, yu safi.
41 Tena kwamba nywele za mtu zimemtoka kichwani upande wa mbele, yeye ni mwenye upaa wa kipaji; yu safi.
42 Lakini kwamba katika kile kichwa kilicho na upaa, au kile kipaji kilicho na upaa, laonekana pigo jeupe kisha jekundu kidogo; ni ukoma, unatokea katika kichwa chake cha upaa, au katika kipaji chake cha upaa.
43 Ndipo kuhani atamwangalia; na tazama, kivimbe cha pigo kikiwa cheupe na chekundu-chekundu, katika kichwa chake chenye upaa, au katika kipaji chake cha upaa, kama vile kuonekana kwa ukoma katika ngozi ya mwili;
44 yeye ni mtu mwenye ukoma, yu najisi; na kuhani hana budi atasema kuwa yu najisi; pigo lake li katika kichwa chake.
45 Kisha mwenye ukoma aliye na pigo ndani yake, nguo zake zitararuliwa, na nywele za kichwa chake zitaachwa wazi, naye atafunika mdomo wake wa juu, naye atapiga kelele, Ni najisi, ni najisi.
46 Siku zote ambazo pigo li ndani yake, yeye atakuwa mwenye unajisi; yeye yu najisi; atakaa peke yake; makazi yake yatakuwa nje ya marago.
47 Tena, vazi nalo ambalo pigo la ukoma li ndani yake, kwamba ni vazi la sufu, au kwamba ni la kitani;
48 likiwa limefumwa, au kusokotwa; likiwa ni la kitani au la sufu; kwamba ni katika ngozi, au kitu cho chote kilichofanywa cha ngozi;
49 hilo pigo likiwa la rangi ya majani au jekundu, katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi; ni pigo la ukoma, nalo ataonyeshwa kuhani;
50 na kuhani ataliangalia hilo pigo, naye atakiweka mahali kile kilicho na pigo muda wa siku saba;
51 kisha siku ya saba ataliangalia hilo pigo; kama pigo limeenea katika hilo lililofumwa, au katika hilo lililosokotwa, au katika ngozi, ijapokuwa hiyo ngozi ina matumizi yo yote; hilo pigo ni ukoma unaokula; vazi hilo ni najisi.
52 Naye atalichoma moto vazi hilo, kwamba ni lililofumwa au kwamba ni lililosokotwa, kama ni la sufu, au la kitani, au kitu cho chote cha ngozi, ambacho kina hilo pigo ndani yake; kwa maana, ni ukoma unaokula; vazi hilo litachomwa moto;
53 Na kama kuhani akitazama, na tazama, ikiwa hilo pigo halikuenea katika hilo vazi, wala katika hilo lililofumwa, wala katika hilo lililosokotwa, wala katika kitu cho chote cha ngozi;
54 ndipo kuhani ataamuru kwamba wakifue kitu kile kilicho na hilo pigo, naye atakiweka mahali muda wa siku saba tena;
55 kisha kuhani ataangalia, baada ya kuoshwa hilo pigo; na tazama, ikiwa hilo pigo halikugeuka rangi yake, wala halikuenea, li najisi; utakichoma moto; ni uharibifu likiwa lina upaa ndani au nje.
56 Huyo kuhani akiangalia, na tazama, ikiwa hilo pigo limeanza kufifia, baada ya kufuliwa kwake, ndipo atalirarua hilo pigo litoke katika vazi, au katika ngozi, au katika lililofumwa, au katika lililosokotwa;
57 kisha, likionekana li vivyo katika hilo vazi, katika lililofumwa, au katika lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi, ni pigo lenye kuenea; nawe vazi hilo lenye pigo utalichoma moto.
58 Na hilo vazi, lililofumwa, au lililosokotwa, au kitu cho chote cha ngozi, utakalolifua, kama hilo pigo limetoka na kuliacha, ndipo litafuliwa mara ya pili, nalo litakuwa safi.
59 Na katika pigo la ukoma katika vazi la sufu, au la kitani, kama ni katika lililofumwa, au lililosokotwa, au katika kitu cho chote cha ngozi, sheria yake ni hiyo, kusema kwamba ni safi, au kusema kwamba ni najisi.

Walawi 14


1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Hii ndiyo sheria ya mwenye ukoma, katika siku ya kutakaswa kwake; ataletwa kwa kuhani,
3 na huyo kuhani atatoka aende nje ya marago; na kuhani ataangalia, na tazama, ikiwa pigo la ukoma limepoa kwake huyo mwenye ukoma;
4 ndipo huyo kuhani ataagiza kwamba watwae kwa ajili yake atakayetakaswa ndege wawili walio hai, ambao ni safi, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo;
5 kisha kuhani ataagiza ndege mmoja achinjwe katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni;
6 kisha huyo ndege aliye hai atamshika, na huo mti wa mwerezi, na hiyo sufu nyekundu, na hisopo, naye atavichovya hivyo, pamoja na yule ndege aliye hai, katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa juu ya maji ya mtoni;
7 kisha atamnyunyizia huyo atakayetakaswa na ukoma mara saba, naye atasema kwamba yu safi, kisha atamwacha yule ndege aliye hai aende zake nyikani.
8 Naye huyo atakayetakaswa atazifua nguo zake, na kunyoa nywele zake zote, na kuoga katika maji, naye atakuwa safi; baada ya hayo ataingia ndani ya marago, lakini ataketi nje ya hema yake muda wa siku saba.
9 Kisha siku ya saba atanyoa nywele zote za kichwani mwake, na ndevu zake, na nyushi zake, nywele zake zote pia atazinyoa; kisha atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa safi.
10 Kisha siku ya nane atachukua wana-kondoo wawili waume wakamilifu, na mwana-kondoo mmoja wa kike wa mwaka wa kwanza mkamilifu, na sehemu tatu za kumi za efa moja ya unga mwembamba kuwa sadaka ya unga, kuchanganywa na mafuta, na logi moja ya mafuta.
11 Kisha kuhani atakayemtakasa atamsimamisha huyo mtu atakayetakaswa, pamoja na vitu vile vyote, mbele za Bwana, mlangoni pa hema ya kukutania;
12 kisha kuhani atamshika mmoja katika hao wana-kondoo waume, na kumsongeza awe sadaka ya hatia, pamoja na hiyo logi ya mafuta, kisha atavitikisa kuwa ni sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana;
13 kisha atamchinja huyo mwana-kondoo mahali hapo wachinjapo sadaka ya dhambi na sadaka ya kuteketezwa, ndani ya mahali patakatifu; kwa kuwa kama hiyo sadaka ya dhambi ilivyo ya kuhani, ni vivyo sadaka ya hatia; ni takatifu sana;
14 kisha huyo kuhani atatwaa katika hiyo damu ya sadaka ya hatia, naye kuhani ataitia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume;
15 kisha kuhani atatwaa katika hiyo logi ya mafuta, na kuyamimina katika kitanga cha mkono wake mwenyewe wa kushoto;
16 kisha kuhani atatia kidole cha mkono wa kuume katika hayo mafuta, yaliyo katika mkono wake wa kushoto, naye atayanyunyiza hayo mafuta kwa kidole chake mara saba mbele za Bwana;
17 na katika yale mafuta yaliyobaki mkononi mwake kuhani atayatia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume, juu ya damu ya sadaka ya hatia;
18 na mafuta yaliyobaki, yaliyo katika mkono wa kuhani, atayatia juu ya kichwa cha huyo atakayetakaswa; na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, mbele za Bwana.
19 Kisha kuhani atasongeza sadaka ya dhambi, na kufanya upatanisho kwa ajili yake huyo atakayetakaswa kwa sababu ya unajisi wake; kisha baadaye ataichinja sadaka ya kuteketezwa;
20 kisha kuhani ataisongeza hiyo sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, juu ya madhabahu na kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, naye atakuwa safi.
21 Tena kwamba ni maskini, naye hawezi kupata kiasi hicho, ndipo atatwaa mwana-kondoo mmoja wa kiume, awe sadaka ya hatia ya kutikiswa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake, na sehemu ya kumi ya efa ya unga mwembamba, uliochanganywa na mafuta kuwa sadaka ya unga, na logi ya mafuta;
22 na hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, kama awezavyo kuwapata; huyo mmoja atakuwa sadaka ya dhambi, na wa pili atakuwa sadaka ya kuteketezwa.
23 Hata siku ya nane atawaleta kwa kuhani, mlangoni pa hema ya kukutania mbele za Bwana, kwa ajili ya kutakaswa kwake.
24 Na kuhani atamtwaa huyo mwana-kondoo wa sadaka ya hatia, na hiyo logi ya mafuta, naye kuhani atavitikisa viwe sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana;
25 kisha atamchinja mwana-kondoo wa sadaka ya hatia, na kuhani atatwaa katika damu ya sadaka ya hatia, na kuitia katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume;
26 kisha kuhani atamimina sehemu ya hayo mafuta katika kitanga cha mkono wake mwenyewe wa kushoto;
27 kisha kuhani atanyunyiza baadhi ya hayo mafuta yaliyo katika mkono wake wa kushoto, kwa kidole chake cha mkono wa kuume mara saba mbele za Bwana;
28 kisha kuhani atatia mengine katika hayo mafuta yaliyo mkononi mwake katika ncha ya sikio la kuume la huyo atakayetakaswa, na katika chanda cha gumba cha mkono wake wa kuume, na katika kidole kikuu cha mguu wake wa kuume, juu ya mahali pale penye damu ya sadaka ya hatia;
29 na mafuta yaliyobaki katika mkono wa kuhani atayatia juu ya kichwa cha huyo atakayetakaswa, ili kufanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana.
30 Kisha atasongeza hao hua mmojawapo, au hao makinda ya njiwa mmojawapo, kadiri ya awezao kuwapata;
31 hata kadiri aliyoweza, mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa, pamoja na sadaka ya unga; na huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake huyo atakayetakaswa mbele za Bwana.
32 Huyo ambaye ndani yake mna pigo la ukoma, ambaye hawezi kukipata hicho kipasacho kutakaswa kwake, sheria yake ni hiyo.
33 Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
34 Hapo mtakapoingia nchi ya Kanaani, ambayo nawapa kuwa ni milki yenu, nami nitakapolitia pigo la ukoma katika nyumba ya nchi hiyo ya milki yenu;
35 ndipo mwenye nyumba hiyo atakwenda na kumwambia kuhani, akisema, Naona mimi ya kwamba pana kama pigo katika nyumba yangu;
36 ndipo kuhani ataagiza kwamba watoe vyote vilivyomo nyumbani, mbele ya kuhani hajaingia ndani kuliangalia hilo pigo, ili kwamba vyote vilivyomo nyumbani visiwekwe kuwa unajisi; kisha baadaye kuhani ataingia ndani ya nyumba hiyo aitazame;
37 naye ataliangalia hilo pigo, na tazama, likiwa pigo limo ndani ya kuta za nyumba, nalo lina mashimo-mashimo, rangi ya majani, au mekundu, na kuonekana kuingia ndani kuliko huo ukuta;
38 ndipo kuhani atatoka katika nyumba hiyo mpaka mlangoni pa nyumba, na kuifunga hiyo nyumba muda wa siku saba;
39 siku ya saba kuhani atakwenda tena, naye ataangalia; na tazama, likiwa pigo limeenea katika kuta za nyumba;
40 ndipo kuhani atawaambia wayatoe hayo mawe, yaliyo na pigo, na kuyatupa mahali penye uchafu nje ya mji;
41 naye atafanya kwamba hiyo nyumba ikwanguwe ndani pande zote, na chokaa watakayokwangua wataimwaga nje ya mji mahali palipo na uchafu;
42 kisha watatwaa mawe mengine, na kuyatia mahali pa mawe hayo; naye atatwaa chokaa nyingine, na kuipaka chokaa hiyo nyumba.
43 Na kama hilo pigo likirudi tena, na kutokea ndani ya nyumba, baada ya yeye kuyatoa hayo mawe, na baada ya kuikwangua nyumba, na baada ya kupakwa chokaa,
44 ndipo kuhani ataingia ndani na kuangalia, na tazama, likiwa pigo limeenea ndani ya hiyo nyumba, ni ukoma unaokula hiyo nyumba; ni katika unajisi.
45 Naye ataibomoa nyumba, mawe yake, na miti yake, na chokaa yote ya hiyo nyumba; naye atavichukua vyote nje ya mji hata mahali palipo na uchafu.
46 Tena mtu atakayeingia ndani ya hiyo nyumba wakati huo wote iliofungwa, atakuwa najisi hata jioni.
47 Na mtu alalaye ndani ya nyumba hiyo atazifua nguo zake, naye alaye chakula ndani ya nyumba hiyo atazifua nguo zake.
48 Tena kwamba kuhani akiingia ndani na kuangalia, na tazama, ikiwa pigo halikuenea katika hiyo nyumba, baada ya nyumba kupakwa chokaa; ndipo kuhani atasema kwamba hiyo nyumba i safi, maana, pigo limepoa.
49 Naye atatwaa ndege wawili, na mti wa mwerezi, na sufu nyekundu, na hisopo, kwa kuitakasa hiyo nyumba;
50 naye atamchinja mmojawapo wa ndege hao katika chombo cha udongo kilicho juu ya maji ya mtoni;
51 kisha atatwaa huo mti wa mwerezi, na hisopo, na sufu nyekundu, pamoja na huyo ndege aliye hai, na kuvichovya vyote katika damu ya huyo ndege aliyechinjwa, na katika hayo maji ya mtoni, na kuinyunyiza nyumba mara saba;
52 naye ataitakasa hiyo nyumba kwa damu ya ndege, na kwa maji ya mtoni, na kwa huyo ndege aliye hai, na kwa mti wa mwerezi, na kwa hisopo, na kwa sufu nyekundu;
53 lakini ndege aliye hai atamwacha atoke mle mjini aende nyikani; ndivyo atakavyofanya upatanisho kwa ajili ya hiyo nyumba; nayo itakuwa safi.
54 Hiyo ndiyo sheria ya pigo la ukoma ya kila aina, na ya kipwepwe;
55 na ya ukoma wa vazi, na ukoma wa nyumba;
56 na kivimbe, na kikoko na kipaku king'aacho;
57 ili kufunza itakapokuwa ni unajisi, na itakapokuwa ni safi; hiyo ndiyo sheria ya ukoma.

Walawi 15


1 Kisha Bwana akanena na Musa na Haruni, na kuwaambia,
2 Haya, semeni na wana wa Israeli, mkawaambie, Mtu ye yote atakapokuwa na kisonono kimtokacho mwilini mwake, atakuwa najisi kwa ajili ya kisonono chake.
3 Na unajisi wake katika kisonono chake ni huu; kama mwili wake unachuruzika kisonono chake, au kama kisonono chake kimezuiwa mwilini mwake, ni unajisi wake.
4 Kitanda cho chote akilaliacho mwenye kisonono kitakuwa najisi; na kitu cho chote ambacho akiketia kitakuwa najisi.
5 Mtu ye yote atakayekigusa kitanda chake huyo, atazifua nguo zake, na kuoga mwili wake majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
6 Na mtu atakayeketi katika kitu cho chote alichokiketia mwenye kisonono, atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
7 Na mtu atakayegusa mwili wake mwenye kisonono atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
8 Tena kama mwenye kisonono akimtemea mate mtu aliye safi; ndipo atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa yu najisi hata jioni.
9 Na tandiko lo lote atakalolipanda mwenye kisonono litakuwa najisi.
10 Mtu awaye yote atakayegusa kitu cho chote kilichokuwa chini yake huyo atakuwa najisi hata jioni; na mtu atakayevichukua vitu vile atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
11 Na mtu ye yote atakayeguswa na mwenye kisonono, asipokuwa amenawa mikono yake majini, atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
12 Na chombo cha udongo ambacho amekigusa mwenye kisonono, kitavunjwa-vunjwa; na kila chombo cha mti kitaoshwa majini.
13 Na huyo aliye na kisonono atakapotakaswa na kisonono chake, atajihesabia siku saba kwa kutakaswa kwake, naye atazifua nguo zake; naye ataoga mwili wake katika maji ya mtoni, naye atakuwa safi.
14 Na siku ya nane atajipatia hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, naye atakwenda mbele za Bwana mlangoni pa hema ya kukutania, naye atampa kuhani hao ndege;
15 na kuhani atawasongeza, mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atafanya upatanisho mbele za Bwana kwa ajili ya kisonono chake.
16 Na mtu ye yote akitokwa na shahawa yake, ndipo ataoga mwili wake wote majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
17 Na kila nguo, na kila ngozi, ambayo ina shahawa, itafuliwa kwa maji, nayo itakuwa najisi hata jioni.
18 Huyo mwanamke naye ambaye mtu mume amelala naye kwa shahawa, wote wawili wataoga majini, nao watakuwa najisi hata jioni.
19 Mwanamke ye yote, kama anatokwa na kitu, na kitu chake alichokuwa nacho mwilini mwake ni damu, ataketi katika kutengwa kwake muda wa siku saba; na mtu ye yote atakayemgusa atakuwa najisi hata jioni.
20 Na kitu cho chote akilaliacho katika kutengwa kwake kitakuwa najisi; na kila kitu ambacho akiketia kitakuwa najisi.
21 Mtu ye yote atakayekigusa kitanda chake huyo mwanamke atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
22 Mtu ye yote atakayekigusa cho chote ambacho huyo mwanamke amekiketia atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
23 Kwamba ni katika kitanda, au cho chote alichokikalia huyo mwanamke, atakapokigusa kitu hicho, atakuwa najisi hata jioni.
24 Na mtu ye yote atakayelala na mwanamke na unajisi ukawa juu yake, atakuwa najisi muda wa siku saba; na kila kitanda alichokilalia kitakuwa najisi.
25 Na mwanamke kama akitokwa na damu yake siku nyingi, nayo si katika majira ya kutengwa kwake, au kama anatoka damu kuzidi majira ya kutengwa kwake; siku hizo zote za kutoka damu ya unajisi wake, atakuwa kama alivyokuwa katika siku za kutengwa kwake; yeye yu najisi.
26 Kila kitanda akilaliacho katika siku zote za kutoka damu kitakuwa kama kitanda cha kutengwa kwake; na kila kitu atakachokilalia kitakuwa najisi, kama unajisi wa kutengwa kwake.
27 Na mtu ye yote atakayevigusa vitu vile atakuwa najisi, naye atazifua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni.
28 Lakini huyo mwanamke kwamba ametakaswa na kule kutoka damu kwake, ndipo atakapojihesabia siku saba, na baadaye atakuwa safi.
29 Siku ya nane atajipatia hua wawili, au makinda mawili ya njiwa, na kumletea kuhani, mlangoni pa hema ya kukutania.
30 Kuhani atamsongeza mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wa pili kuwa sadaka ya kuteketezwa; naye kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake mbele za Bwana, kwa ajili ya kutoka damu ya unajisi kwake.
31 Ni hivi mtakavyowatenga wana wa Israeli na unajisi wao; ili wasife katika unajisi wao, hapo watakapoitia unajisi maskani yangu iliyo katikati yao.
32 Hii ndiyo sheria ya mwenye kisonono, na ya mtu ambaye shahawa yake yamtoka, akawa na unajisi kwa hiyo;
33 na ya mwanamke ambaye yu katika kutengwa kwake, na ya mtu ambaye ana kisonono, kama ni mtu mume, kama ni mtu mke, na ya huyo alalaye na mwanamke mwenye unajisi.

Walawi 16


1 Bwana akasema na Musa, baada ya kufa kwa hao wana wawili wa Haruni, walipokaribia mbele za Bwana, wakafa;
2 Bwana akamwambia Musa, Sema na Haruni ndugu yako, kwamba asiingie wakati wo wote katika mahali patakatifu ndani ya pazia, mbele ya kiti cha rehema, kilicho juu ya sanduku, asije akafa; maana, mimi nitaonekana katika lile wingu juu ya kiti cha rehema.
3 Haruni ataingia katika patakatifu na vitu hivi; ng'ombe mume mchanga kwa sadaka ya dhambi, na kondoo mume kwa sadaka ya kuteketezwa.
4 Ataivaa ile kanzu takatifu ya kitani, atakuwa na zile suruali za kitani mwilini mwake, atafungwa ule mshipi wa kitani, naye atavaa ile kofia ya kitani; hayo ndiyo mavazi matakatifu, naye ataoga mwili wake majini, na kuyavaa.
5 Kisha atatwaa mikononi mwa mkutano wa Waisraeli mbuzi waume wawili, kwa sadaka ya dhambi; na kondoo mume kwa sadaka ya kuteketezwa.
6 Na Haruni atamtoa yule ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake, na kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake.
7 Kisha atawatwaa wale mbuzi wawili na kuwaweka mbele za Bwana mlangoni pa hema ya kukutania.
8 Na Haruni atapiga kura juu ya wale mbuzi wawili; kura moja kwa ajili ya Bwana; na kura ya pili kwa ajili ya Azazeli.
9 Na Haruni atamleta yule mbuzi aliyeangukiwa na kura kwa ajili ya Bwana, na kumtoa awe sadaka ya dhambi.
10 Bali yule mbuzi aliyeangukiwa na kura kwa ajili ya Azazeli atawekwa hai mbele za Bwana ili kumfanyia upatanisho, ili kumpeleka jangwani kwa ajili ya Azazeli.
11 Na Haruni atamsongeza ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake, na kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake; naye atamchinja yule ng'ombe wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya nafsi yake.
12 Kisha atatwaa chetezo kilichojaa makaa ya moto yatokayo katika madhabahu iliyo mbele za Bwana, na konzi mbili za uvumba mzuri uliopondwa sana, mikononi mwake, naye atauleta ndani ya pazia.
13 Kisha atatia ule uvumba juu ya moto mbele za Bwana, ili moshi wa ule uvumba ukisitiri kiti cha rehema kilicho juu ya ushuhuda, asije akafa.
14 Kisha atatwaa baadhi ya damu ya yule ng'ombe, na kuinyunyiza kwa kidole chake juu ya kiti cha rehema upande wa mashariki; na mbele ya kiti cha rehema atainyunyiza ile damu kwa kidole chake mara saba.
15 Kisha atamchinja yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, aliye kwa ajili ya watu, na kuileta damu yake ndani ya pazia, na kwa damu hiyo atafanya vile vile kama alivyofanya kwa damu ya ng'ombe, na kuinyunyiza juu ya kiti cha rehema, na mbele ya kiti cha rehema,
16 naye atafanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, kwa sababu ya mambo machafu ya wana wa Israeli, na kwa sababu ya makosa yao, naam, kwa ajili ya dhambi zao zote; naye atafanya vile vile kwa ajili ya hema ya kukutania, ikaayo pamoja nao katikati ya machafu yao.
17 Wala hapatakuwa na mtu katika hema ya kukutania, wakati aingiapo ili kufanya upatanisho katika patakatifu, hata atakapotoka nje, baada ya kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake mwenyewe, na kwa ajili ya nyumba yake, na kwa ajili ya mkutano wote wa Israeli.
18 Kisha atatoka na kuiendea madhabahu iliyo mbele za Bwana na kufanya upatanisho kwa ajili yake; atatwaa baadhi ya damu ya yule ng'ombe, na ya damu ya yule mbuzi, na kuitia juu ya pembe za madhabahu pande zote.
19 Tena atanyunyiza baadhi ya damu juu ya madhabahu kwa kidole chake mara saba, na kuitakasa, ili machafu yote ya wana wa Israeli yaitoke.
20 Naye akiisha kufanya upatanisho kwa ajili ya mahali patakatifu, na hema ya kukutania, na madhabahu, atamleta yule mbuzi aliye hai.
21 Na Haruni ataweka mikono yake miwili juu ya kichwa cha yule mbuzi aliye hai, na kuungama juu yake uovu wote wa wana wa Israeli, na makosa yao, naam, dhambi zao zote; naye ataziweka juu ya kichwa chake yule mbuzi, kisha atampeleka aende jangwani kwa mkono wa mtu aliye tayari.
22 Na yule mbuzi atachukua juu yake uovu wao wote, mpaka nchi isiyo watu; naye atamwacha mbuzi jangwani.
23 Na Haruni ataingia katika hema ya kukutania, naye atavua mavazi yake ya kitani, aliyoyavaa alipoingia katika patakatifu, atayaacha humo;
24 naye ataosha mwili wake kwa maji mahali patakatifu, na kuvaa nguo zake, na kutoka, na kusongeza sadaka ya kuteketezwa yake mwenyewe, na sadaka ya kuteketezwa ya watu, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya nafsi yake, na kwa ajili ya watu.
25 Na mafuta ya sadaka ya dhambi atayateketeza juu ya madhabahu.
26 Na mtu yule amwachaye mbuzi wa Azazeli aende zake, ataosha nguo zake, na kuosha mwili wake kwa maji, na baadaye ataingia katika marago.
27 Na yule ng'ombe wa sadaka ya dhambi, na yule mbuzi wa sadaka ya dhambi, ambao damu yao ililetwa ndani ifanye ukumbusho katika patakatifu, watachukuliwa nje ya marago; nao watachoma moto ngozi zao, na nyama yao, na mavi yao.
28 Na yeye awachomaye moto atafua nguo zake, na kuosha mwili wake kwa maji, na baadaye ataingia maragoni.
29 Amri hii itakuwa amri ya milele kwenu; katika mwezi wa saba, siku ya kumi ya mwezi, mtajitaabisha roho zenu, msifanye kazi ya namna yo yote, mzalia na mgeni akaaye kati yenu.
30 Kwa maana siku hiyo upatanisho utafanywa kwa ajili yenu, ili kuwatakasa; nanyi mtatakaswa na dhambi zenu zote mbele za Bwana.
31 Ni Sabato ya raha ya makini kwenu nanyi mtajitaabisha roho zenu; ni amri ya milele.
32 Na kuhani atakayetiwa mafuta na kuwekwa wakfu badala ya baba yake, ataufanya huo upatanisho, naye atayavaa mavazi ya kitani, yaani, yale mavazi matakatifu.
33 Naye atafanya upatanisho kwa ajili ya patakatifu, naye atafanya upatanisho kwa ajili ya hema ya kukutania, na kwa ajili ya madhabahu; naye atafanya upatanisho kwa ajili ya makuhani, na kwa ajili ya watu wote wa kusanyiko.
34 Na amri hii itakuwa amri ya milele kwenu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya wana wa Israeli kwa sababu ya dhambi zao zote, mara moja kila mwaka. Naye akafanya vile vile kama Bwana alivyomwamuru Musa.

Walawi 17


1 Bwana akamwambia Musa, akisema,
2 Sema na Haruni, na wanawe, na wana wote wa Israeli, ukawaambie; Neno hili ndilo aliloliamuru Bwana, akisema,
3 Mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli atakayechinja ng'ombe, au mwana-kondoo, au mbuzi, ndani ya marago, au atakayemchinja nje ya marago,
4 wala hamleti mlangoni pa hema ya kukutania, ili amtoe kuwa matoleo kwa Bwana mbele ya hema ya Bwana; mtu huyo atahesabiwa kuwa ana hatia ya damu; amemwaga damu; na mtu huyo atakatiliwa mbali na watu wake;
5 ili kusudi wana wa Israeli walete sadaka zao, wazichinjazo mashambani, naam, wazilete kwa Bwana, mpaka mlango wa hema ya kukutania, kwa huyo kuhani, ili wazichinje ziwe sadaka za amani kwa Bwana.
6 Naye kuhani atainyunyiza damu yake juu ya madhabahu ya Bwana, mlangoni pa hema ya kukutania, na kuyateketeza mafuta yake, yawe harufu njema mbele za Bwana.
7 Wala hawatatoa tena sadaka zao kwa wale majini, ambao huwafuata ili wafanye uasherati nao. Sheria hii itakuwa sheria ya milele kwao, kizazi baada ya kizazi.
8 Nawe utawaambia, Mtu awaye yote katika nyumba ya Israeli, au miongoni mwa wageni, wanaokaa nao, atoaye sadaka ya kuteketezwa au dhabihu,
9 wala haileti mlangoni pa hema ya kukutania, ili aisongeze kwa Bwana basi mtu huyo atatengwa na watu wake.
10 Kisha mtu awaye yote wa nyumba ya Israeli, au miongoni mwa hao wageni wakaao kati yao, atakayekula damu, ya aina yo yote, nitakunja uso wangu juu ya mtu huyo alaye damu, nami nitamkatilia mbali na watu wake.
11 Kwa kuwa uhai wa mwili u katika hiyo damu; nami nimewapa ninyi hiyo damu juu ya madhabahu, ili kufanya upatanisho kwa ajili ya nafsi zenu; kwani ni hiyo damu ifanyayo upatanisho kwa sababu ya nafsi.
12 Kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Hapana mtu miongoni mwenu aliye na ruhusa kula damu, wala mgeni aketiye kati yenu asile damu.
13 Mtu ye yote aliye wa wana wa Israeli, au wa hao wageni wakaao kati yenu, ambaye amemshika mnyama, au ndege ambaye huliwa, katika kuwinda kwake; atamwaga damu yake, na kuifunika mchanga.
14 Kwa maana kuliko huo uhai wa mnyama, hiyo damu yake ni moja na uhai wake; kwa hiyo naliwaambia wana wa Israeli, Msile damu ya mnyama wa aina yo yote; kwa kuwa uhai wa wanyama wote ni katika hiyo damu yake; atakayeila awaye yote atakatiliwa mbali.
15 Tena kila mtu atakayekula nyamafu, au nyama aliyeraruliwa na wanyama, kama ni mzalia, kama ni mgeni, atafua nguo zake, na kuoga majini, naye atakuwa najisi hata jioni; ndipo atakapokuwa safi.
16 Lakini kwamba hazifui, wala haogi mwili, ndipo atakapochukua uovu wake.

Walawi 18


1 Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena wewe na wana wa Israeli, uwaambie, Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
3 Nanyi msifanye matendo kama yale ya nchi ya Misri mliyokaa; wala msifanye matendo kama yale ya nchi ya Kanaani, nitakayowapeleka; wala msiende katika amri zao hao.
4 Mtazifanya hukumu zangu, nanyi mtazishika amri zangu, ili mwenende katika hizo; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
5 Kwa ajili ya hayo mtazishika amri zangu na hukumu zangu; ambazo mtu akizitumia ataishi kwa hizo; mimi ndimi Bwana.
6 Mtu ye yote aliye wa kwenu asimkaribie mwenziwe aliye wa jamaa yake ya karibu ili kumfunua utupu; mimi ndimi Bwana.
7 Utupu wa baba yako, wala utupu wa mama yako, usifunue, maana ndiye mama yako; usifunue utupu wake.
8 Utupu wa mke wa baba yako, usifunue; maana, ni utupu wa baba yako.
9 Utupu wa umbu lako, binti ya baba yako, au binti ya mama yako, kwamba alizaliwa nyumbani mwenu au kwamba alizaliwa kwengine, utupu wa hao usifunue.
10 Utupu wa binti ya mwanao mume, au wa binti ya binti yako, utupu wao hao usifunue; kwa kuwa ndio utupu wako mwenyewe.
11 Utupu wa binti ya mkewe baba yako, aliyezaliwa na baba yako, yeye ni umbu lako, usifunue utupu wake.
12 Usifunue utupu wa umbu lake baba yako; maana, yeye ni jamaa aliye karibu.
13 Usifunue utupu wa umbu la mama yako; maana, yeye ni jamaa ya mama yako ya karibu.
14 Usifunue utupu wa ndugu ya baba yako, usimkaribie mkewe huyo; yeye ni shangazi lako.
15 Usifunue utupu wa mkweo mwanamke; yeye ni mke wa mwanao; usifunue utupu wake huyo.
16 Usifunue utupu wa mke wa nduguyo; maana, ni utupu wa nduguyo.
17 Usifunue utupu wa mwanamke na binti yake; usimtwae binti ya mwanawe mume, au binti ya binti yake, ili kufunua utupu wake; hao ni jamaa ya karibu; ni uovu mkuu.
18 Wala usitwae mwanamke pamoja na nduguye, awe mtesi wake, na kufunua utupu wake, huyo wa pili atakapokuwa yu hai.
19 Nawe usimkaribie mwanamke kufunua utupu wake wakati wa kutengwa kwa ajili ya unajisi wake.
20 Usilale na mke wa mwenzio, ukajitia unajisi naye.
21 Nawe usitoe kizazi chako cho chote na kuwapisha kwa Moleki, wala usilinajisi jina la Mungu wako; mimi ndimi Bwana.
22 Usilale na mwanamume mfano wa kulala na mwanamke; ni machukizo.
23 Wala usilale na mnyama ye yote, ili kujitia unajisi kwake; wala mwanamke asisimame mbele ya mnyama ili kulala naye; ni uchafuko.
24 Msijitie unajisi katika mambo hayo hata mojawapo; kwa maana hizo taifa nitakazozitoa mbele zenu zimekuwa najisi kwa mambo hayo yote;
25 na hiyo nchi imekuwa najisi; kwa ajili ya hayo naipatiliza uovu wake juu yake, na hiyo nchi yatapika wenyeji wake na kuwatoa.
26 Kwa hiyo mtazishika amri zangu na hukumu zangu, wala msifanye machukizo hayo mojawapo; yeye aliye mzalia, wala mgeni aketiye kati yenu;
27 (kwa kuwa hao watu wa nchi wameyafanya machukizo haya yote, hao waliotangulia mbele zenu, na hiyo nchi imekuwa najisi;)
28 ili kwamba hiyo nchi isiwatapike na ninyi pia, hapo mtakapoitia unajisi, kama ilivyoitapika hiyo taifa iliyotangulia mbele yenu.
29 Kwani mtu awaye yote atakayefanya machukizo hayo mojawapo, nafsi hizo zitakazoyafanya zitakatiliwa mbali na watu wao.
30 Kwa ajili ya hayo yashikeni mausia yangu, ili kwamba msifanye kabisa desturi hizi zichukizazo mojawapo, zilizotangulia kufanywa mbele zenu, wala msijitie unajisi katika mambo hayo; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.

Walawi 19


1 Bwana akanena na Musa, akamwambia,
2 Nena na mkutano wote wa wana wa Israeli, uwaambie, Mtakuwa watakatifu; kwa kuwa mimi Bwana, Mungu wenu, ni mtakatifu.
3 Kila mtu na amche mama yake, na baba yake, nanyi mtazitunza Sabato zangu; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
4 Msigeuke kuandama sanamu, wala msijifanyizie miungu ya kusubu mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
5 Nanyi hapo mtakapomchinjia Bwana sadaka ya amani mtaisongeza ili kwamba mpate kukubaliwa.
6 Italiwa siku iyo hiyo mliyoichinja, na siku ya pili yake; na kama kitu cho chote katika sadaka hiyo kilisalia hata siku ya tatu kitachomwa moto.
7 Kwamba sadaka hiyo yaliwa hata kidogo siku ya tatu ni machukizo; haitakubaliwa;
8 lakini kila mtu atakayekula atauchukua uovu wake mwenyewe, kwa sababu amekinajisi kitu hicho kitakatifu cha Bwana; na nafsi hiyo itakatiliwa mbali na watu wake.
9 Na mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala usiyakusanye masazo ya mavuno yako;
10 wala usiyakusanye masazo ya mizabibu yako, wala usiyaokote matunda ya mizabibu yako yaliyopukutika; uyaache kwa ajili ya maskini na mgeni; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
11 Msiibe, wala msidanganye, wala msiambiane uongo.
12 Msiape uongo kwa jina langu, hata ukalinajisi jina la Mungu wako; Mimi ndimi Bwana.
13 Usimdhulumu jirani yako, wala kumnyang'anya mali yake; ijara yake aliyeajiriwa isikae kwako usiku kucha hata asubuhi.
14 Usimlaani kiziwi, wala usitie kwazo mbele ya kipofu, bali umche Mungu wako; Mimi ndimi Bwana.
15 Msitende yasiyo haki katika hukumu, usimpendelee mtu maskini, wala kumstahi mwenye nguvu; bali utamhukumu jirani yako kwa haki.
16 Usiende huko na huko katikati ya watu wako, kama mchongezi; wala usisimame kinyume cha damu ya jirani yako; mimi ndimi Bwana.
17 Usimchukie ndugu yako moyoni mwako; ni lazima kumkemea jirani yako, wala usichukue dhambi kwa ajili yake.
18 Usifanye kisasi, wala kuwa na kinyongo juu ya wana wa watu wako; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi Bwana.
19 Mtazishika amri zangu. Usiwaache wanyama wako wa mfugo wakazaana kwa namna mbalimbali; usipande shamba lako mbegu za namna mbili pamoja; wala usivae mwilini mwako nguo ya namna mbili zilizochanganywa pamoja.
20 Tena mtu ye yote alalaye na mwanamke aliye mjakazi, naye ameposwa na mume, wala hakukombolewa kwa lo lote, wala hakupewa uhuru; wataadhibiwa; hawatauawa, kwa sababu huyo mwanamke hakuwa huru.
21 Na huyo mume ataleta sadaka yake ya hatia aitoe kwa Bwana, hata mlangoni pa hema ya kukutania; kondoo mume kwa hiyo sadaka ya hatia.
22 Kisha huyo kuhani atafanya upatanisho kwa ajili yake, kwa huyo kondoo mume wa sadaka ya hatia mbele za Bwana, kwa ajili ya dhambi yake aliyoifanya; naye atasamehewa hiyo dhambi yake aliyoifanya.
23 Nanyi hapo mtakapoingia nchi ile, mkiwa mmepanda miti ya namna zote kwa ajili ya chakula, ndipo mtayahesabu matunda yake kama ni kutotahiriwa; muda wa miaka mitatu miti hiyo itakuwa kwenu kama kutotahiriwa; matunda yake hayataliwa.
24 Lakini mwaka wa nne matunda yake yote yatakuwa ni matakatifu, kwa ajili ya kumpa Bwana shukrani.
25 Na katika mwaka wa tano mtakula katika matunda yake, ili ipate kuwapa maongeo yake; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
26 Msile kitu cho chote pamoja na damu yake; wala msifanye kuloga, wala kutumia utambuzi.
27 Msinyoe denge pembe za vichwani, wala msiharibu pembe za ndevu zenu.
28 Msichanje chale yo yote katika nyama ya miili yenu kwa ajili ya wafu, wala msiandike alama miilini mwenu; mimi ndimi Bwana.
29 Usimnajisi binti yako, ili kumfanya awe kahaba; isiwe hiyo nchi kuuandama ukahaba, na nchi kujawa na uovu mkuu.
30 Zishikeni Sabato zangu, mpaheshimu patakatifu pangu; mimi ndimi Bwana.
31 Msiwaendee wenye pepo, wala wachawi; msiwatafute; ili kutiwa unajisi na wao; Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
32 Mwondokeeni mtu mwenye mvi; heshimuni uso wa mtu mzee; nawe mche Mungu wako, Mimi ndimi Bwana.
33 Na mgeni akikaa pamoja nawe katika nchi yako, usimdhulumu.
34 Mgeni akaaye pamoja nawe atakuwa kama mzalia kwenu; mpende kama nafsi yako; kwa maana ninyi mlikuwa wageni katika nchi ya Misri; Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
35 Msifanye yasiyo haki katika hukumu, wala katika kupima, wala katika mizani, wala katika cheo.
36 Mizani ya haki, vipimo vya haki, efa ya haki, hini ya haki, ndivyo mtakavyokuwa navyo. Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, niliyewatoa katika nchi ya Misri.
37 Zishikeni sheria zangu, na hukumu zangu, na kuzitenda. Mimi ndimi Bwana.

Walawi 20


1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Tena uwaambie wana wa Israeli, Mtu awaye yote miongoni mwa wana wa Israeli, au miongoni mwa wageni waketio katika Israeli, atakayetoa katika kizazi chake na kumpa Moleki, sharti atauawa; wenyeji wa nchi watampiga kwa mawe.
3 Mimi nami nitamkazia uso wangu mtu huyo, nami nitamkatilia mbali na watu wake; kwa kuwa ametoa katika kizazi chake na kumpa Moleki, ili kupatia unajisi patakatifu pangu, na kulinajisi jina langu takatifu.
4 Tena kama wenyeji wa nchi wakimfumbia macho mtu huyo kwa njia yo yote, hapo atoapo katika kizazi chake na kumpa Moleki, wasimwue;
5 ndipo mimi nitamkazia uso wangu mtu huyo, na jamaa zake, nami nitamkatilia mbali, na hao wote wamwandamao katika uzinifu, ili kufanya uzinifu pamoja na Moleki, watengwe mbali na watu wao.
6 Na mtu yule atakayewaendea wenye pepo, na wachawi, ili kuzini pamoja nao, nitakaza uso wangu juu ya mtu yule, nitamtenga na watu wake.
7 Jitakaseni basi, iweni watakatifu, kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
8 Nanyi zishikeni sheria zangu, na kuzitenda; Mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi.
9 Kwa maana kila mtu amlaaniye baba yake au mama yake hakika atauawa, amemlaani baba yake na mama yake; damu yake itakuwa juu yake.
10 Na mtu aziniye na mke wa mtu mwingine, naam, yeye aziniye na mke wa jirani yake, mtu mume aziniye, na mwanamke aziniye, hakika watauawa.
11 Na mtu mume atakayelala pamoja na mke wa baba yake amefunua utupu wa baba yake; wote wawili hakika watauawa; damu yao itakuwa juu yao.
12 Na mtu mume akilala na mkwewe mwanamke wote wawili hakika watauawa; wamefanya yaliyo uchafuko; damu yao itakuwa juu yao.
13 Tena mtu mume akilala pamoja na mtu mume, kama alalavyo na mtu mke, wote wawili wamefanya machukizo; hakika watauawa; damu yao itakuwa juu yao.
14 Tena mtu mume akimwoa mke pamoja na mama yake, ni uovu mkuu; watachomwa moto, yeye mume na hao wanawake pia; ili kwamba usiwe uovu kati yenu.
15 Tena mtu mume akilala na mnyama, hakika atauawa; nanyi mtamwua huyo mnyama.
16 Tena mwanamke akimkaribia mnyama ye yote, na kulala pamoja naye, mtamwua huyo mwanamke, na mnyama pia; hakika watauawa; damu yao itakuwa ni juu yao.
17 Tena mtu mume akimwoa umbu lake, binti ya baba yake, au binti ya mama yake, na kuuona utupu wake, na huyo mwanamke kauona utupu wake huyo mume; ni jambo la aibu; watakatiliwa mbali mbele ya macho ya wana wa watu wao; amefunua utupu wa umbu lake; naye atauchukua uovu wake.
18 Tena mtu mume akilala na mwanamke aliye na ugonjwa wake, na kufunua utupu wake; amelifunua jito la damu yake, naye mwanamke amefunua jito la damu yake; wote wawili watakatiliwa mbali na watu wao.
19 Usifunue utupu wa umbu la mama yako, wala umbu la baba yako; kwa kuwa huyo amefunua utupu wa jamaa yake ya karibu; watauchukua uovu wao.
20 Tena mtu mume akilala na mke wa mjomba wake, ameufunua utupu wa mjomba wake; watauchukua uovu wao; watakufa bila kuzaa mwana.
21 Tena mtu mume akimtwaa mke wa nduguye, ni uchafu; ameufunua utupu wa nduguye; hao watakuwa hawana wana.
22 Basi zishikeni amri zangu zote, na hukumu zangu zote, na kuzifanya; ili kwamba hiyo nchi, ambayo nawapeleka ninyi kukaa, isiwatapike.
23 Nanyi msiende kwa kuziandama desturi za taifa, niitoayo mbele yenu; kwa kuwa wao waliyafanya mambo hayo yote, na kwa ajili ya hayo niliwachukia.
24 Lakini mimi nimewaambia ninyi, Mtairithi nchi yao, nami nitawapa ninyi kuimiliki; nchi iliyojaa maziwa na asali; mimi ni Bwana, Mungu wenu, niliyewatenga ninyi na mataifa.
25 Kwa ajili ya hayo mtapambanua kati ya mnyama aliye safi na mnyama aliye najisi, na kati ya ndege aliye tohara na ndege aliye najisi; nanyi msizifanye nafsi zenu kuwa machukizo kwa njia ya mnyama, au kwa njia ya ndege, au kwa njia ya kitu cho chote ambacho nchi imejaa nacho, niliowatenga nanyi kuwa ni najisi.
26 Nanyi mtakuwa watakatifu kwangu mimi; kwa kuwa mimi Bwana ni mtakatifu nami nimewatenga ninyi na mataifa, ili kwamba mwe wangu.
27 Tena mtu mume au mtu mke aliye na pepo, au aliye mchawi, hakika atauawa; watawapiga kwa mawe; damu yao itakuwa juu yao.

Walawi 21


1 Kisha Bwana akamwambia Musa, Nena na hao makuhani, wana wa Haruni, uwaambie, Mtu asijinajisi kwa ajili ya wafu katika watu wake;
2 isipokuwa ni kwa ajili ya jamaa yake wa karibu, kwa ajili ya mama yake, na kwa ajili baba yake, na kwa ajili ya mwanawe, na kwa ajili ya binti yake, na kwa ajili ya nduguye mwanamume;
3 na kwa ajili ya umbu lake aliye mwanamwali, aliye wa udugu kwake, ambaye hajaolewa na mume; ana ruhusa kujitia unajisi kwa ajili yake huyo.
4 Asijitie unajisi, ijapokuwa ni mkubwa katika watu wake, hata akajinajisi.
5 Wasijifanyie upaa kichwani, wala wasinyoe pembe za ndevu zao, wala wasichanje chale katika miili yao.
6 Watakuwa watakatifu kwa Mungu wao, wala wasilinajisi jina la Mungu wao; kwa kuwa wao ndio wasongezao sadaka za Bwana kwa njia ya moto, chakula cha Mungu wao; kwa ajili ya hayo watakuwa watakatifu.
7 Wasimwoe mwanamke aliye kahaba, au huyo aliye mwenye unajisi; wala wasimwoe mwanamke aliyeachwa na mumewe; kwa kuwa yeye kuhani ni mtakatifu kwa Mungu wake.
8 Kwa hiyo basi utamtakasa; kwa kuwa yeye husongeza chakula cha Mungu wako; atakuwa mtakatifu kwako wewe; kwa kuwa mimi Bwana niwatakasaye ninyi ni mtakatifu.
9 Na binti ya kuhani ye yote atakapojitia unajisi kwa ukahaba, amemtia unajisi baba yake; atachomwa moto.
10 Na yeye aliye kuhani mkuu katika nduguze, ambaye mafuta ya kutiwa yamemiminwa kichwani mwake, naye akawekwa wakfu ili ayavae hayo mavazi, yeye hataziacha wazi nywele za kichwa chake, wala hatazirarua nguo zake;
11 wala hataingia penye maiti, wala asijitie unajisi kwa ajili ya baba yake wala mama yake;
12 wala asitoke katika mahali patakatifu, wala asipatie unajisi mahali patakatifu pa Mungu wake; kwa kuwa utakaso wa hayo mafuta ya kutiwa ya Mungu wake u juu yake; mimi ndimi Bwana.
13 Naye atamwoa mwanamke katika ubikira wake.
14 Asitwae mjane, wala mwanamke aliyeachwa na mumewe, wala mwanamke mwenye unajisi, wala kahaba; lakini atamwoa mwanamwali katika watu wake mwenyewe.
15 Naye asiwatie unajisi kizazi chake katika watu wake; kwa kuwa mimi ndimi Bwana nimtakasaye.
16 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
17 Nena na Haruni, umwambie, Mtu awaye yote wa kizazi chako wewe katika vizazi vyao, aliye na kilema, asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake.
18 Kwa kuwa mtu awaye yote aliye na kilema hatakaribia; mtu kipofu, au kiwete, au mtu aliye na pua iliyoharibika, au aliye na kitu kilichozidi vimpasavyo mwili,
19 au mtu aliyevunjika mguu, au aliyevunjika mkono,
20 au aliye na kijongo, au aliye kibeti, au aliye na kilema cha jichoni, au aliye na upele, au mwenye buba, au aliyevunjika mapumbu;
21 mtu awaye yote wa kizazi cha Haruni kuhani aliye na kilema asikaribie kuzisongeza sadaka za Bwana kwa njia ya moto; ana kilema huyo asikaribie kusongeza chakula cha Mungu wake.
22 Atakula chakula cha Mungu wake, katika hicho kilicho kitakatifu sana, na hicho kilicho kitakatifu.
23 Lakini hataingia ndani ya pazia, wala asikaribie madhabahu, kwa sababu ana kilema; ili kwamba asipanajisi patakatifu pangu; kwa kuwa mimi ndimi Bwana niwatakasaye.
24 Basi Musa akanena na Haruni na wanawe, na wana wa Israeli wote.

Walawi 22


1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena na Haruni na wanawe, ili wajitenge wenyewe na vitu vitakatifu vya wana wa Israeli ambavyo wanitakasia mimi, tena kwamba wasilinajisi jina langu takatifu; mimi ndimi Bwana.
3 Waambie, Mtu ye yote wa kizazi chenu chote katika vizazi vyenu, atakayevikaribia vile vitu vitakatifu, ambavyo wana wa Israeli wamtakasia Bwana, naye ana unajisi, mtu huyo atakatiliwa mbali asiwe mbele zangu; mimi ndimi Bwana.
4 Mtu ye yote wa kizazi cha Haruni aliye mwenye ukoma, au mwenye kisonono; yeye asile katika vitu vitakatifu, hata atakapokuwa safi. Tena mtu awaye yote atakayekinusa kitu kilicho na unajisi kwa sababu ya wafu, au mtu ambaye shahawa humtoka;
5 au mtu amgusaye mnyama atambaaye, wa kumpatia unajisi, au kwamba amgusa mtu wa kumpatia unajisi, kwa unajisi wo wote alio nao;
6 huyo mtu atakayegusa kitu cho chote namna hiyo atakuwa najisi hata jioni, naye hatakula katika vitu vitakatifu, asipooga mwili wake majini.
7 Jua likiisha kuchwa atakuwa safi; kisha baadaye atakula katika vitu vitakatifu, maana ni chakula chake.
8 Nyamafu au mnyama aliyeraruliwa na wanyama asile, asijitie unajisi kwa hiyo nyama; mimi ndimi Bwana.
9 Basi kwa hiyo watayashika mausia yangu, wasije wakachukua dhambi kwa hayo, nao wakafa humo, wakiyanajisi; mimi ndimi Bwana niwatakasaye.
10 Mgeni awaye yote asile katika kitu kitakatifu; mgeni wa kuhani akaaye kwake, au mtumishi aliyeajiriwa, asile katika kitu kitakatifu.
11 Lakini kwamba kuhani akinunua mtu ye yote, kwa kumnunua kwa fedha zake, yeye atakula katika hicho; na hao waliozaliwa nyumbani mwake watakula katika chakula chake.
12 Na binti ya kuhani kwamba ameolewa na mgeni, asile katika sadaka ya kuinuliwa katika vitu vile vitakatifu.
13 Lakini kwamba binti ya kuhani ni mjane, au kwamba ameachwa na mumewe, wala hana mtoto, kisha amerudi na kuketi katika nyumba ya baba yake, kama vile katika ujana wake, yeye atakula katika chakula cha baba yake; lakini mgeni awaye yote asile katika chakula hicho.
14 Tena kama mtu ye yote akila katika kitu kilicho kitakatifu pasipo kukijua, ndipo ataongeza sehemu ya tano juu ya kitu hicho, na kumpa kuhani kitu hicho kitakatifu.
15 Wala wasivinajisi vitu vitakatifu vya wana wa Israeli, wavisongezavyo kwa Bwana;
16 hata wakawatwika ule uovu uletao hatia, hapo walapo vitu vyao vitakatifu; kwa kuwa mimi ndimi Bwana niwatakasaye.
17 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
18 Nena na Haruni na wanawe, na wana wa israeli wote, uwaambie, Mtu ye yote wa nyumba ya Israeli, au wa wageni walio katika Israeli, atakayetoa matoleo yake, kama ni nadhiri zao mojawapo, au kama ni sadaka yo yote ya hiari, watakayomtolea Bwana kuwa sadaka ya kuteketezwa;
19 ili mpate kukubaliwa, mtaleta mume mkamilifu, katika ng'ombe, au katika kondoo, au katika mbuzi.
20 Lakini mnyama ye yote aliye na kilema msimtoe; kwa kuwa hatakubaliwa kwa ajili yenu.
21 Na mtu awaye yote atakayemtolea Bwana dhabihu katika sadaka za amani, ili kuondoa nadhiri, au sadaka ya moyo wa kupenda, katika ng'ombe, au katika kondoo, atakuwa mkamilifu, apate kukubaliwa; pasiwe na kilema ndani yake cho chote.
22 Kipofu, au aliyevunjika mahali, au kiwete au aliye na vidonda, au aliye na upele, au aliye na kikoko, hamtamtolea Bwana wanyama hao, wala msiwasongeze kwa Bwana kwa njia ya moto juu ya madhabahu.
23 Ng'ombe, au mwana-kondoo aliye na kitu kilichozidi, au aliyepungukiwa na kitu katika vitu vya mwilini mwake, mna ruhusa kutoa kuwa sadaka ya moyo wa kupenda; lakini kwa ajili ya nadhiri hatakubaliwa.
24 Mnyama aliyeumia mapumbu yake, au kusetwa, au kuvunjwa, au kukatwa, msimtolee Bwana; wala msifanye hivi katika nchi yenu.
25 Wala msisongeze chakula cha Mungu wenu katika wanyama hao mmojawapo kitokacho mkononi mwa mgeni; kwa sababu uharibifu wao u ndani yao, wana kilema ndani yao; hawatakubaliwa kwa ajili yenu.
26 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
27 Hapo ng'ombe, au kondoo, au mbuzi, akizaliwa, atakuwa pamoja na mamaye muda wa siku saba; na siku ya nane na baadaye atakubaliwa kuwa ni sadaka ya kutolewa kwa Bwana kwa njia ya moto.
28 Tena kama ni ng'ombe, au kama ni kondoo, msimchinje huyo na mwanawe wote wawili kwa siku moja.
29 Tena mtakapomchinjia Bwana dhabihu ya shukrani, mtamchinja ili mpate kukubaliwa.
30 Italiwa siku iyo hiyo; msisaze kitu chake hata asubuhi; mimi ndimi Bwana.
31 Kwa hiyo mtayashika maagizo yangu, na kuyafanya; mimi ndimi Bwana.
32 Wala msilinajisi jina langu takatifu; lakini nitatakaswa mimi katika wana wa Israeli; mimi ndimi Bwana niwatakasaye ninyi,
33 niliyewaleta mtoke nchi ya Misri, ili niwe Mungu wenu; mimi ndimi Bwana.

Walawi 23


1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena na wana wa Israeli, na kuwaambia, Sikukuu za Bwana, ambazo mtazipigia mbiu kuwa ni makusanyiko matakatifu; hizi ni sikukuu zangu.
3 Mtafanya kazi siku sita; lakini siku ya saba ni Sabato ya kustarehe kabisa, kusanyiko takatifu; msifanye kazi ya namna yo yote; ni Sabato kwa Bwana katika makao yenu yote.
4 Sikukuu za Bwana ni hizi, ni makusanyiko matakatifu, ambayo mtayapigia mbiu kwa nyakati zake.
5 Mwezi wa kwanza, siku ya kumi na nne ya mwezi wakati wa jioni, ni pasaka ya Bwana.
6 Na siku ya kumi na tano ya mwezi ule ule ni sikukuu kwa Bwana ya mkate usiotiwa chachu; mtaila mikate isiyochachwa muda wa siku saba.
7 Siku ya kwanza mtakuwa na kusanyiko takatifu msifanye kazi yo yote ya utumishi.
8 Lakini mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto siku saba; siku ya saba ni kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.
9 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
10 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapokuwa mmekwisha ingia hiyo nchi niwapayo, na kuyavuna mavuno yake, ndipo mtakapomletea kuhani mganda wa malimbuko ya mavuno yenu;
11 naye atautikisa mganda mbele za Bwana ili kwamba ukubaliwe kwa ajili yenu; siku ya pili baada ya Sabato kuhani atautikisa.
12 Na siku hiyo mtakayoutikisa mganda, mtamsongeza mwana-kondoo wa kiume mkamilifu wa mwaka wa kwanza awe sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana.
13 Na sadaka yake ya unga itakuwa sehemu za kumi mbili za efa za unga mwembamba uliochanganywa na mafuta, ni kafara iliyosongezwa kwa Bwana kwa moto kuwa harufu ya kupendeza; na sadaka yake ya kinywaji itakuwa ni divai, robo ya hini.
14 Nanyi msile mkate, wala bisi, wala masuke machanga, hata siku iyo hiyo, hata mtakapokuwa mmekwisha kuleta sadaka ya Mungu wenu; hii ni amri ya milele katika vizazi vyenu katika makao yenu yote.
15 Nanyi mtajihesabia tangu siku ya pili baada ya Sabato, tangu siku hiyo mliyouleta mganda wa sadaka ya kutikiswa; zitatimia Sabato saba;
16 hata siku ya pili ya hiyo Sabato ya saba mtahesabu siku hamsini; nanyi mtamsongezea Bwana sadaka ya unga mpya.
17 Mtatoa katika makao yenu mikate miwili ya kutikiswa, itakuwa ya sehemu za kumi mbili za efa; itakuwa ya unga mwembamba, itaokwa na chachu, iwe malimbuko kwa Bwana.
18 Nanyi, pamoja na hiyo mikate, mtasongeza wana-kondoo saba, walio wakamilifu, wa mwaka wa kwanza, na ng'ombe mume mmoja, na kondoo waume wawili; watakuwa sadaka ya kuteketezwa kwa Bwana, pamoja na sadaka yao ya unga, na sadaka zao za kinywaji, sadaka ya harufu ya kupendeza iliyosongezwa kwa Bwana kwa njia ya moto.
19 Nanyi mtasongeza mbuzi mume mmoja kuwa sadaka ya dhambi, na wana-kondoo wawili waume wa mwaka wa kwanza kuwa dhabihu ya sadaka za amani.
20 Kisha kuhani atawatikisa pamoja na hiyo mikate ya malimbuko kuwa sadaka ya kutikiswa mbele za Bwana, pamoja na wale wana-kondoo wawili; watakuwa watakatifu kwa Bwana, wawe wa huyo kuhani.
21 Nanyi mtapiga mbiu siku iyo hiyo; kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; msifanye kazi yo yote ya utumishi; ni amri ya milele katika makao yenu yote, katika vizazi vyenu.
22 Nanyi hapo mtakapovuna mavuno ya nchi yenu, usivune kabisa kabisa pembe za shamba lako, wala msiyakusanye masazo ya mavuno yako; utayaacha kwa ajili ya huyo maskini, na mgeni; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
23 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
24 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Mwezi wa saba, siku ya kwanza ya mwezi, kutakuwa na kustarehe kabisa kwenu, ni ukumbusho wa kuzipiga baragumu, ni kusanyiko takatifu.
25 Msifanye kazi yo yote ya utumishi; nanyi mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto.
26 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
27 Lakini siku ya kumi ya mwezi huo wa saba ni siku ya upatanisho; itakuwa kusanyiko takatifu kwenu, nanyi mtazitesa nafsi zenu; nanyi mtasongeza sadaka kwa Bwana kwa njia ya moto.
28 Nanyi msifanye kazi yo yote siku hiyo; kwa kuwa ni siku ya upatanisho, ili kufanya upatanisho kwa ajili yenu mbele za Bwana, Mungu wenu.
29 Kwa kuwa mtu awaye yote asiyejitesa mwenyewe siku iyo hiyo, atakatiliwa mbali na watu wake.
30 Na mtu ye yote afanyaye kazi ya namna yo yote siku hiyo, mtu huyo nitamwangamiza atoke katika watu wake.
31 Msifanye kazi ya namna yo yote; ni amri ya milele katika vizazi vyenu, katika makao yenu yote.
32 Itakuwa kwenu sabato ya kustarehe kabisa, nanyi mtazitesa nafsi zenu; siku ya kenda ya mwezi wakati wa jioni, tangu jioni hata jioni, mtaishika hiyo Sabato yenu.
33 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
34 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Siku ya kumi na tano ya mwezi huo wa saba ni sikukuu ya vibanda muda wa siku saba kwa Bwana.
35 Siku ya kwanza kutakuwa na kusanyiko takatifu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.
36 Mtamsongezea Bwana sadaka kwa moto siku saba; siku ya nane kutakuwa na kusanyiko takatifu kwenu; nanyi mtamsongezea Bwana sadaka kwa moto; ni mkutano wa makini huu; msifanye kazi yo yote ya utumishi.
37 Sikukuu za Bwana ni hizi, ambazo mtazipigia mbiu ya kuwa ni makusanyiko matakatifu, ili mmsongezee Bwana sadaka kwa moto, sadaka ya kuteketezwa, na sadaka ya unga, na dhabihu, na sadaka za kinywaji, kila sadaka kwa siku yake;
38 zaidi ya hizo Sabato za Bwana, na zaidi ya matoleo yenu, na zaidi ya hizo nadhiri zenu zote, na zaidi ya sadaka zenu za hiari, ambazo mwampa Bwana.
39 Lakini siku ya kumi na tano ya mwezi wa saba, hapo mtakapokuwa mmekwisha kuyachuma mavuno ya nchi, mtaweka sikukuu ya Bwana muda wa siku saba; siku ya kwanza kutakuwa na kustarehe kabisa, na siku ya nane kutakuwa na kustarehe kabisa.
40 Nanyi siku ya kwanza mtajipatia matunda ya miti mizuri, na makuti ya mitende, na matawi ya miti minene, na mierebi ya vijitoni; nanyi mtafurahi mbele za Bwana, Mungu wenu, muda wa siku saba.
41 Nanyi mtaishika kuwa sikukuu kwa Bwana muda wa siku saba katika mwaka; ni amri ya milele katika vizazi vyenu; mtaishika katika mwezi wa saba.
42 Mtakaa katika vibanda muda wa siku saba; wazalia wote wa Israeli watakaa katika vibanda;
43 ili vizazi vyenu vipate kujua ya kuwa niliwaketisha wana wa Israeli katika vibanda, hapo nilipowaleta kutoka nchi ya Misri; mimi ndimi Bwana Mungu wenu.
44 Naye Musa akawaambia wana wa Israeli hizo sikukuu za Bwana.

Walawi 24


1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Waagize wana wa Israeli kwamba wakuletee mafuta ya zeituni safi ya kupondwa kwa ajili ya ile nuru, ili hiyo taa iwake daima.
3 Hapo nje ya pazia la ushahidi, ndani ya hema ya kukutania, Haruni ataitengeza tangu jioni hata asubuhi mbele za Bwana daima; ni amri ya milele katika vizazi vyenu.
4 Atazitengeza hizo taa katika kile kinara kilicho safi mbele za Bwana daima.
5 Nawe utatwaa unga mwembamba, na kuoka mikate kumi na miwili ya huo unga; sehemu za kumi mbili za efa, zitakuwa katika mkate mmoja.
6 Nawe iweke mistari miwili, mikate sita kwa kila mstari, juu ya hiyo meza safi, mbele za Bwana.
7 Nawe utatia ubani safi juu ya kila mstari, ili uwe ukumbusho kwa hiyo mikate, sadaka ya kusongezwa kwa Bwana kwa moto.
8 Kila siku ya Sabato ataipanga mbele za Bwana daima; ni kwa ajili ya wana wa Israeli, agano la milele.
9 Nayo itakuwa ya Haruni na wanawe; nao wataila katika mahali patakatifu; kwa sababu kwake ni takatifu sana katika sadaka zisongezwazo kwa Bwana kwa moto, kwa amri ya milele.
10 Ikawa mwana wa mwanamke wa Kiisraeli, ambaye babaye alikuwa Mmisri, akatokea kati ya wana wa Israeli; na huyo mwana wa mwanamke wa Kiisraeli, na Mwisraeli mmoja, wakapigana pamoja ndani ya marago;
11 kisha huyo mwana wa mwanamke wa Kiisraeli akalikufuru hilo Jina, na kuapiza; nao wakamleta kwa Musa. Na jina la mamaye alikuwa akiitwa Shelomithi, binti ya Dibri, wa kabila ya Dani.
12 Nao wakamtia kifungoni, ili wapate kuambiwa neno litakalotoka kinywani pa Bwana.
13 Na Bwana akasema na Musa, na kumwambia,
14 Mtoe huyo aliyeapiza nje ya marago; na wale wote waliomsikia na waweke mikono yao kichwani mwake, kisha mkutano wote na wamwue kwa kumpiga kwa mawe.
15 Nawe nena na wana wa Israeli na kuwaambia, Mtu awaye yote atakayemlaani Mungu wake atachukua dhambi yake.
16 Na yeye atakayelikufuru jina la Bwana hakika atauawa; mkutano wote watamwua kwa kumpiga kwa mawe; kama ni mgeni, kama ni mzalia, hapo atakapolikufuru jina la Bwana atauawa.
17 Na mtu ampigaye mtu hata akafa, lazima atauawa;
18 na atakayempiga mnyama hata akafa atalipa; uhai kwa uhai.
19 Na mtu akimtia mwenziwe kilema; vile vile kama alivyofanya, naye atafanyiwa vivyo;
20 jeraha kwa jeraha, jicho kwa jicho, jino kwa jino; vile vile kama alivyomtia mtu kilema, naye atalipwa vivyo.
21 Na mtu amwuaye mnyama atalipa; na yeye atakayemwua binadamu atauawa.
22 Mtakuwa na sheria moja tu, kwa huyo aliye mgeni, na kwa mzalia; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
23 Musa akanena na wana wa Israeli, nao wakamtoa huyo aliyeapiza nje ya marago, wakamwua kwa kumpiga kwa mawe. Wana wa Israeli wakafanya kama Bwana alivyomwagiza Musa.

Walawi 25


1 Kisha Bwana akanena na Musa katika mlima wa Sinai, na kumwambia,
2 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtakapoingia katika nchi niwapayo, ndipo hiyo nchi itashika Sabato kwa ajili ya Bwana.
3 Panda shamba lako miaka sita, na miaka sita lipelee shamba lako la mizabibu, na kuyachuma matunda yake;
4 lakini katika mwaka wa saba itakuwa ni Sabato ya kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi, ni Sabato kwa Bwana; usipande shamba lako, wala usipelee shamba lako la mizabibu.
5 Hicho kimeacho chenyewe katika mavuno yako, usikivune, wala zabibu za mizabibu isiyopelewa usizitunde; utakuwa mwaka wa kustarehe kabisa kwa ajili ya hiyo nchi.
6 Na hiyo Sabato ya nchi itakuwa chakula kwenu; kwako wewe, na kwa mtumwa wako, na kwa mjakazi wako, na kwa mtumishi aliyeajiriwa, na kwa mgeni wako akaaye pamoja nawe;
7 na kwa hayawani wako, na kwa wanyama walio katika nchi yako; maongeo yote yatakuwa ni chakula chao.
8 Nawe utajihesabia Sabato saba za miaka, maana, miaka saba mara saba; zitakuwa ni siku za Sabato saba za miaka kwenu, maana miaka arobaini na kenda.
9 Ndipo utakapoipeleka pande zote hiyo baragumu yenye sauti kuu, siku ya kumi ya mwezi wa saba; katika siku hiyo ya upatanisho mtaipeleka baragumu katika nchi yenu yote.
10 Na mwaka wa hamsini mtautakasa, na kupiga mbiu ya kuachwa mahuru katika nchi yote kwa watu wote wanayokaa; itakuwa ni yubile kwenu, nanyi kila mtu atairudia milki yake mwenyewe, nanyi mtarejea kila mtu kwa jamaa yake.
11 Mwaka huo wa hamsini utakuwa ni yubile kwenu; msipande mbegu, wala msivune kitu hicho kimeacho chenyewe, wala msizitunde zabibu za mizabibu isiyopelewa.
12 Kwa kuwa ni yubile; utakuwa mwaka mtakatifu kwenu; mtakula maongeo yake yatokayo shambani.
13 Mwaka huo wa yubile mtairudia kila mtu milki yake.
14 Tena kama ukimwuzia jirani yako cho chote, au kununua cho chote mkononi mwa jirani yako, msidanganyane wenyewe kwa wenyewe;
15 kwa hesabu ya miaka iliyo baada ya yubile, ndivyo utakavyonunua kwa jirani yako, na kama hesabu ya miaka ya mavuno ndivyo atakavyokuuzia wewe.
16 Kama hesabu ya miaka ilivyo ni nyingi ndivyo utakavyoongeza bei yake, na kama hesabu ya miaka ilivyo ni chache ndivyo utakavyopunguza bei yake; kwani yeye akuuzia mavuno kama hesabu yake ilivyo.
17 Wala msidanganyane; lakini utamcha Mungu wako; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
18 Kwa sababu hii zitendeni amri zangu, mkazishike hukumu zangu, na kuzifanya; nanyi mtakaa katika hiyo nchi salama.
19 Nayo nchi itazaa matunda yake, nanyi mtakula na kushiba, na kuketi humo salama.
20 Na kama mkisema, Je! Mwaka wa saba tutakula nini? Angalieni hatutapanda mbegu, wala kukusanya maongeo yetu;
21 ndipo nitawaamria baraka yangu iwe juu yenu mwaka wa sita, nayo utazaa matunda hesabu ya miaka mitatu.
22 Na mwaka wa nane mtapanda mbegu, na kuyala yale matunda, akiba hiyo ya zamani, hata mwaka wa kenda, hata matunda yake yatakapoletwa ndani, mtakula hiyo akiba ya zamani.
23 Nayo nchi haitauzwa kabisa kabisa; kwani nchi ni yangu mimi; maana ninyi ni wageni na wasafiri wangu.
24 Nanyi mtatoa ukombozi kwa ajili ya nchi, katika nchi yote ya milki yenu.
25 Kwamba nduguyo amekuwa maskini, na kuuza sehemu ya milki yake, ndipo jamaa yake aliye karibu naye atakuja, naye ataikomboa ile aliyoiuza nduguye.
26 Na kama mtu hana atakayeikomboa, naye mwenyewe amepata mali na kujiona kuwa anayo ya kutosha kuikomboa;
27 ndipo na aihesabu hiyo miaka ya kuuzwa kwake, na kilichozidi kumrudishia huyo mtu aliyeinunua; naye atairejea milki yake.
28 Lakini asipoweza kujipatia mwenyewe, ndipo hiyo iliyouzwa itakaa mkononi mwake huyo aliyeinunua, hata mwaka wa yubile; na katika yubile itatoka, naye atairejea milki yake.
29 Tena kwamba mtu anauza nyumba ya kukaa, iliyo ndani ya mji wenye kuta, ndipo ana ruhusa kuikomboa katika mwaka mmoja mzima baada ya kuiuza; atakuwa na amri ya kuikomboa muda wa mwaka mzima.
30 Na kama haikukombolewa katika muda wa mwaka mzima, ndipo hiyo nyumba iliyo ndani ya mji wenye kuta itathibitishwa milele kuwa ya huyo aliyeinunua, katika vizazi vyake; nayo haitatoka katika yubile.
31 Lakini nyumba za vijiji, ambavyo havikuzingirwa na kuta, zitahesabiwa pamoja na mashamba ya nchi; nazo zina ruhusa ya kukombolewa, nazo zitatoka katika yubile.
32 Pamoja na hayo, miji ya Walawi, nyumba za miji ya milki yao, Walawi wana ruhusa ya kuzikomboa majira yo yote.
33 Tena kama mtu mmoja wa hao Walawi akikomboa, ndipo nyumba iliyouzwa, na mji wa milki yake, itatoka katika yubile; maana, hizo nyumba za miji ya Walawi ni milki yao kati ya wana wa Israeli.
34 Lakini konde la malisho ya miji yao lisiuzwe kwa kuwa ni milki yao ya daima.
35 Na ikiwa ndugu yako amekuwa maskini, na mkono wake umelegea kwako, ndipo utamsaidia, atakaa nawe kama mgeni, na msafiri.
36 Usitake riba kwake wala faida, bali mche Mungu wako, ili ndugu yako akae nawe.
37 Usimpe fedha yako upate riba, wala usimpe vyakula vyako kwa kujitakia faida.
38 Mimi ndimi Bwana, Mungu wako, niliyewatoa katika nchi ya Misri ili niwape nchi ya Kanaani, nipate kuwa Mungu wenu.
39 Tena kwamba nduguyo amekuwa maskini pamoja nawe, akajiuza kwako; usimtumikishe mfano wa mtumwa;
40 kwako wewe atakuwa mfano wa mtumishi aliyeajiriwa, au mfano wa msafiri; naye atatumika kwako hata mwaka wa yubile;
41 ndipo atakapotoka kwako aende zake, yeye na wanawe pamoja naye, naye atairejea jamaa yake mwenyewe, tena atairejea milki ya baba zake.
42 Kwa kuwa hao ni watumishi wangu, niliowaleta watoke nchi ya Misri; wasiuzwe mfano wa watumwa.
43 Usitawale juu yake kwa nguvu; ila umche Mungu wako.
44 Tena katika habari za watumwa wako na wajakazi wako, utakaokuwa nao; mataifa walio kando-kando yenu, katika hao mtanunua watumwa na wajakazi.
45 Tena katika wana wa wageni wakaao kati yenu mtajinunulia, na katika jamaa zao walio pamoja nanyi, waliowazaa katika nchi yenu; wao watakuwa milki yenu.
46 Nanyi mtawafanya kuwa urithi kwa watoto wenu baada yenu, wawe milki yao; siku zote mtatwaa watumwa wenu katika hao; lakini msitawale kwa nguvu juu ya ndugu zenu, hao wana wa Israeli, wenyewe kwa wenyewe.
47 Tena kama mgeni au mtu akaaye nawe akitajirika, na nduguyo amekuwa maskini karibu naye, akajiuza kwa huyo mgeni, au kwa huyo akaaye kwako, au kwa ukoo wa jamaa ya huyo mgeni;
48 baada ya kuuzwa aweza kukombolewa; mtu mmoja miongoni mwa ndugu zake ana ruhusa kumkomboa;
49 au mjomba wake, au mwana wa mjomba wake, ana ruhusa ya kumkomboa, au mtu awaye yote aliye karibu naye wa jamaa yake, ana ruhusa ya kumkomboa; au kwamba yeye mwenyewe amepata mali, ana ruhusa ya kujikomboa mwenyewe.
50 Naye atafanya hesabu na huyo aliyemnunua, tangu mwaka huo aliojiuza hata mwaka wa yubile; na ile bei ya kuuzwa kwake itakuwa kama hesabu ya hiyo miaka ilivyo; atakuwa pamoja naye kama majira ya mtumishi aliyeajiriwa yalivyo.
51 Kwamba ikali imesalia miaka mingi, kama hesabu yake ilivyo ndivyo atakavyolipa bei ya ukombozi wake, katika hiyo fedha ambayo alinunuliwa kwayo.
52 Tena kwamba imesalia miaka michache tu hata mwaka wa yubile, ndipo atafanya hesabu naye, kama hesabu ya miaka yake ilivyo, ndivyo atakavyolipa tena bei ya ukombozi wake.
53 Kama mtumishi aliyeajiriwa mwaka hata mwaka, ndivyo atakavyokuwa pamoja naye; asitawale juu yake kwa nguvu mbele ya macho yako.
54 Tena kwamba hakukombolewa kwa njia hizi mojawapo, ndipo atatoka katika mwaka wa yubile, yeye, na watoto wake pamoja naye.
55 Kwa kuwa wana wa Israeli ni watumishi; ni watumishi wangu niliowaleta watoke katika nchi ya Misri; mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.

Walawi 26


1 Msifanye sanamu yo yote, wala msijisimamishie sanamu ya kuchonga, wala mnara, wala msiweke jiwe lo lote lililochorwa katika nchi yenu ili kulisujudia; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
2 Zishikeni Sabato zangu, na kupastahi patakatifu pangu; mimi ndimi Bwana.
3 Kama mkienda katika amri zangu, na kuyashika maagizo yangu, na kuyafanya;
4 ndipo nitazinyesha mvua zenu kwa nyakati zake, na nchi itazaa maongeo yake, na miti ya mashambani itazaa matunda yake.
5 Tena kupura nafaka kwenu kutaendelea hata wakati wa kuvuna zabibu, na kuvuna zabibu kutaendelea hata wakati wa kupanda mbegu; nanyi mtakula chakula chenu na kushiba, na kuketi katika nchi yenu salama.
6 Nami nitawapa amani katika nchi, tena mtalala wala hapana atakayewatia hofu; nami nitawakomesha wanyama wabaya katika nchi yenu, wala hautapita upanga katika nchi yenu.
7 Nanyi mtawafukuza adui zenu, nao wataanguka mbele zenu kwa upanga.
8 Na watu watano wa kwenu watawafukuza watu mia, na watu mia wa kwenu watawafukuza watu elfu kumi; na adui zenu wataanguka mbele yenu kwa upanga.
9 Nami nitawaelekezea uso wangu, na kuwapa uzazi mwingi, na kuwaongeza; nami nitalithibitisha agano langu pamoja nanyi.
10 Nanyi mtakula akiba ya zamani mliyoiweka siku nyingi, tena hayo ya zamani mtayatoa, ili myaweke yaliyo mapya.
11 Nami nitaiweka maskani yangu kati yenu; wala roho yangu haitawachukia.
12 Nami nitakwenda kati yenu, nami nitakuwa Mungu wenu, nanyi mtakuwa watu wangu.
13 Mimi ndimi Bwana, Mungu wenu, niliyewaleta mtoke katika nchi ya Misri, ili msiwe watumwa wao; nami nimeivunja miti ya kongwa lenu, nikawaendesha mwende sawasawa.
14 Lakini msiponisikiza, wala hamtaki kuyafanya maagizo hayo yote;
15 nanyi mkizikataa amri zangu, na roho yenu ikichukia hukumu zangu, hata ikawa hamtaki kuyafanya maagizo yangu yote, bali mwalivunja agano langu;
16 mimi nami nitawatenda jambo hili; nitaamrisha uje juu yenu utisho, hata kifua kikuu na homa, zitakazoharibu macho yenu, na kuidhoofisha roho; nanyi mtapanda mbegu yenu bure, kwa kuwa adui zenu wataila.
17 Nami nitauelekeza uso wangu kinyume chenu, nanyi mtapigwa mbele ya adui zenu; hao wawachukiao watatawala juu yenu; nanyi mtakimbia wakati ambao hapana awafukuzaye.
18 Tena ikiwa baada ya hayo hamtaki kunisikiza, ndipo nitawaadhibu zaidi mara saba kwa ajili ya dhambi zenu.
19 Nami nitakivunja kiburi cha uwezo wenu; nami nitazifanya mbingu zenu kuwa kama chuma, na nchi yenu kuwa kama shaba;
20 na nguvu zenu mtazitumia bure; kwa kuwa nchi yenu haitazaa mazao yake, wala miti ya nchi haitazaa matunda yake.
21 Nanyi ikiwa mwaenenda kinyume changu, wala hamtaki kunisikiza; nitaleta mapigo mara saba zaidi juu yenu, kama dhambi zenu zilivyo.
22 Nami nitaleta wanyama wakali kati yenu, ambao watawanyang'anya watoto wenu, na kuwaharibu wanyama wenu wa kufugwa, na kuwapunguza muwe wachache hesabu yenu; na njia zenu zitakuwa ni ukiwa.
23 Tena kama hamtaki kurejezwa upya kwangu mimi kwa mambo haya, bali mwaendelea kunishikia kinyume; ndipo mimi nami nitaendelea kuwashikia ninyi kinyume;
24 nami nitawapiga, naam mimi, mara saba kwa ajili ya dhambi zenu.
25 Nami nitaleta upanga juu yenu, utakaopatiliza kisasi cha hilo agano; nanyi mtakutanishwa ndani ya miji yenu; nami nitaleta tauni kati yenu; nanyi mtatiwa mkononi mwa adui.
26 Hapo nitakapovunja tegemeo lenu la mkate, wanawake kumi wataoka mikate yenu katika tanuu moja, nao watawapa mikate yenu tena kwa kupima kwa mizani; nanyi mtakula, lakini hamtashiba.
27 Tena ikiwa baada ya hayo yote hamtaki kunisikiza, bali mwaenenda kwa kunishikia kinyume;
28 ndipo nami nitakwenda kwa kuwashikia ninyi kinyume katika ghadhabu yangu; nami nitawaadhibu mara saba kwa dhambi zenu.
29 Nanyi mtakula nyama ya miili ya wana wenu, na nyama ya miili ya binti zenu mtaila.
30 Nami nitapaharibu mahali penu palipoinuka, na kuziangusha sanamu zenu za jua, nami nitaitupa mizoga yenu juu ya mizoga ya sanamu zenu; na roho yangu itawachukia.
31 Nami nitaifanya miji yenu iwe maganjo, na mahali penu patakatifu nitapatia ukiwa; wala sitasikia harufu ya manukato yenu yapendezayo.
32 Nami nitaitia hiyo nchi ukiwa; na adui zenu watakaokaa huko wataistaajabia.
33 Nanyi nitawatapanya-tapanya katika mataifa, nami nitaufuta upanga nyuma yenu; na nchi yenu itakuwa ni ukiwa, na miji yenu maganjo.
34 Hapo ndipo nchi itakapozifurahia Sabato zake, wakati itakapokuwa hali ya ukiwa, nanyi mtakapokuwa katika nchi ya adui zenu; ndipo nchi itakapopumzika, na kuzifurahia Sabato zake.
35 Wakati wote itakapokuwa na ukiwa, itapumzika; ni hayo mapumziko ambayo haikuwa nayo katika Sabato zenu, hapo mlipokaa katika nchi hiyo.
36 Tena hao wa kwenu watakaobaki, nitawatilia woga mioyoni mwao, katika hizo nchi za adui zao; na sauti ya jani lililopeperushwa itawakimbiza; nao watakimbia, kama mtu akimbiavyo upanga; nao wataanguka hapo ambapo hapana afukuzaye.
37 Nao wataangukiana wenyewe kwa wenyewe, kama mbele ya upanga, hapo ambapo hapana afukuzaye; wala hamtakuwa na nguvu za kusimama mbele ya adui zenu.
38 Nanyi mtaangamia kati ya mataifa, na nchi ya adui zenu itawameza.
39 Na watu wa kwenu watakaobaki watafifia kwa ajili ya uovu wao, katika hizo nchi za adui zenu; tena watafifia kwa ajili ya uovu wa baba zao, pamoja nao.
40 Nao wataukiri uovu wao, na uovu wa baba zao, katika maasi yao waliyoasi juu yangu, tena ya kuwa kwa sababu wameendelea kunishikia kinyume,
41 mimi nami nimeendelea kuwashikia kinyume wao, na kuwatia katika nchi ya adui zao; lakini hapo, kama mioyo yao isiyokuwa tohara ikinyenyekea, nao wakubali adhabu ya uovu wao;
42 ndipo nitakapokumbuka agano langu pamoja na Yakobo, tena agano langu na Isaka, tena agano langu na Ibrahimu nitalikumbuka; nami nitaikumbuka nchi hiyo.
43 Nchi nayo itaachwa na wao, nayo itazifurahia Sabato zake, itakapokuwa ukiwa pasipokuwa na wao; nao wataikubali adhabu ya uovu wao; kwa sababu, naam, ni kwa sababu wamezikataa hukumu zangu, na roho zao zimezichukia amri zangu.
44 Lakini pamoja na hayo yote, watakapokuwa katika nchi ya adui zao, mimi, sitawatupa, wala sitawachukia, niwaangamize kabisa, na kulivunja agano langu pamoja nao; kwa kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wao;
45 lakini kwa ajili yao nitalikumbuka agano la baba zao, niliowaleta watoke katika nchi ya Misri mbele ya macho ya mataifa, ili kwamba niwe Mungu wao; mimi ndimi Bwana.
46 Hizi ni amri na hukumu na sheria, Bwana alizozifanya kati ya yeye na hao wana wa Israeli katika huo mlima wa Sinai kwa mkono wa Musa.

Walawi 27


1 Kisha Bwana akanena na Musa, na kumwambia,
2 Nena na wana wa Israeli, uwaambie, Hapo mtu atakapoondoa nadhiri, hizo nafsi za watu zitakuwa kwa Bwana, kama utakavyowahesabia wewe.
3 Na hesabu yako itakuwa kwa mtu mume, tokea aliye na umri wa miaka ishirini hata umri wa miaka sitini, hesabu yako itakuwa shekeli hamsini za fedha, kwa shekeli ya mahali patakatifu.
4 Kama ni mwanamke, hesabu yako itakuwa shekeli thelathini.
5 Tena akiwa mwenye umri wa miaka mitano hata umri wa miaka ishirini, ndipo hesabu yako itakuwa shekeli ishirini kwa mwanamume, na shekeli kumi kwa mwanamke.
6 Tena akiwa mwenye umri wa mwezi mmoja hata umri wa miaka mitano, ndipo hesabu yako itakuwa shekeli tano za fedha kwa mwanamume, na hesabu yako itakuwa shekeli tatu za fedha kwa mwanamke.
7 Tena akiwa mwenye umri wa miaka sitini na kuzidi; kama ni mwanamume, hesabu yako itakuwa shekeli kumi na tano, na kwa mwanamke shekeli kumi.
8 Lakini kwamba ni maskini zaidi ya kuhesabu kwako, ndipo atawekwa mbele ya kuhani, na huyo kuhani atamtia kima; kama uwezo wake huyo aliyeweka nadhiri ulivyo, ndivyo kuhani atakavyomtia kima.
9 Tena kama ni mnyama wa namna ambayo watu husongeza kuwa sadaka kwa Bwana, kila mmoja katika wanyama hao atakayetolewa kwa Bwana, na mtu ye yote, atakuwa ni mtakatifu.
10 Yeye hatamgeuza, wala kumbadili mwema kwa mbaya, au mbaya kwa mwema; kwamba atabadili mnyama kwa mnyama ye yote, ndipo mnyama huyo na yule waliobadiliwa wote wawili watakuwa watakatifu.
11 Na kama ni mnyama ye yote asiye safi, wa namna ambayo hawamsongezi kwa Bwana, basi atamweka huyo mnyama mbele ya kuhani;
12 na kuhani atamtia kima, akiwa mwema akiwa mbaya; kama wewe kuhani utakavyomtia kima, ndivyo itakavyokuwa.
13 Lakini kwamba ataka kumkomboa kweli, ndipo atakapoongeza sehemu ya tano juu ya hesabu yako.
14 Na mtu atakapoiweka nyumba yake iwe wakfu kwa Bwana ndipo kuhani ataihesabu kima chake hiyo nyumba, ikiwa njema ikiwa mbaya; kama kuhani atakavyoihesabu kima chake ndivyo itakavyokuwa.
15 Tena mtu huyo aliyeweka nyumba yake iwe wakfu kama akitaka kuikomboa, ndipo atakapoongeza sehemu ya tano ya hiyo fedha ya hesabu yako, nayo itakuwa mali yake.
16 Tena kama mtu akiweka wakfu kwa Bwana sehemu ya shamba la milki yake, ndipo hesabu yako itakuwa kama kule kupanda kwake kulivyo; kupanda kwake homeri moja ya mbegu ya shayiri, kutahesabiwa kuwa ni shekeli hamsini za fedha.
17 Kwamba anaweka shamba lake liwe wakfu tangu mwaka wa yubile, litasimama vivyo kama hesabu yako ilivyo.
18 Lakini akiliweka shamba lake wakfu baada ya yubile, ndipo kuhani atamhesabia hiyo fedha kama hesabu ya miaka iliyobaki hata mwaka wa yubile, na kuhesabiwa kwako kutapunguzwa.
19 Na kama yeye aliyeliweka shamba wakfu akitaka kulikomboa kweli, ndipo atakapoongeza sehemu ya tano ya hiyo fedha ya hesabu yako, nalo litathibitishwa kwake.
20 Lakini asipotaka kulikomboa shamba, au kama amemwuzia mtu mwingine hilo shamba, halitakombolewa tena kabisa;
21 ila hilo shamba litakuwa takatifu kwa Bwana litakapotoka katika yubile, kama ni shamba lililowekwa wakfu; litakuwa mali ya kuhani.
22 Tena kama akiweka wakfu kwa Bwana shamba ambalo amelinunua, ambalo si shamba la milki yake;
23 ndipo kuhani atamhesabia kima cha kuhesabu kwako hata mwaka wa yubile: naye atatoa siku hiyo kama hesabu yako, kuwa ni kitu kitakatifu kwa Bwana.
24 Mwaka wa yubile shamba hilo litarejea kwake huyo ambaye lilinunuliwa kwake, yaani, huyo ambaye nchi hiyo ni milki yake.
25 Na hesabu zako zote zitaandamana shekeli ya mahali patakatifu; gera ishirini zitakuwa shekeli moja.
26 Mzaliwa wa kwanza tu katika wanyama, aliyewekwa kuwa mzaliwa wa kwanza kwa Bwana, mtu awaye yote hatamweka kuwa mtakatifu; kama ni ng'ombe, kama ni kondoo, huyo ni wa Bwana.
27 Na kama ni wa mnyama asiye safi, ndipo atamkomboa kama hesabu yako ilivyo, naye ataongeza sehemu ya tano ya bei yake; au asipokombolewa, ndipo atauzwa kama hesabu yako ilivyo.
28 Pamoja na hayo, hakitauzwa wala kukombolewa kitu cho chote kilichowekwa wakfu, ambacho mtu amekiweka wakfu kwa Bwana, katika vitu vyote alivyo navyo, kama ni mtu, au mnyama, au kama ni shamba la milki yake; kila kitu kilichowekwa wakfu ni kitakatifu sana kwa Bwana.
29 Kila aliyewekwa wakfu, aliyewekwa wakfu na binadamu, hatakombolewa; sharti atauawa.
30 Tena zaka yote ya nchi, kama ni mbegu ya nchi, au kama ni matunda ya nchi, ni ya Bwana; ni takatifu kwa Bwana.
31 Na kama mtu akitaka kukomboa cho chote cha zaka yake, ataongeza sehemu yake ya tano juu yake.
32 Tena zaka yote ya ng'ombe, au ya kondoo, kila apitaye chini ya fimbo; sehemu ya kumi watakuwa ni watakatifu kwa Bwana.
33 Hataangalia kwamba ni mwema au kwamba ni mbaya, wala hatambadili; na kama akimbadili na yo yote, ndipo wote wawili, huyo na huyo waliobadiliwa watakuwa ni watakatifu; hatakombolewa.
34 Haya ndiyo maagizo, Bwana aliyomwagiza Musa kwa ajili ya wana wa Israeli katika mlima wa Sinai.